Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eric James Shigongo (9 total)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba na mimi niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Sengerema ina halmashauri mbili, Halmashauri ya Sengerema na Halmashauri ya Buchosa. Mimi ni Mbunge wa Buchosa, wakati wa kampeni nilimuomba Mheshimiwa Rais Halmashauri ya Buchosa nayo iwe Wilaya. Kwa hiyo, naomba kujua ni lini sasa Buchosa nao watakumbukwa kuwa Wilaya? Halmashauri hii ina mapato makubwa, ni halmashauri inayojitosheleza na inafaa kabisa kuwa wilaya ili huduma ziweze kuwasogelea wananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Erick Shigongo, Mbunge wa Buchosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kusogeza huduma za jamii karibu zaidi na wananchi na kuanzisha maeneo mapya ya utalawa. Ni sehemu ya kusogeza huduma kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Buchosa ambayo Mheshimiwa Shigongo anaielezea, naomba nimshauri kwamba utaratibu wa kuomba maeneo mapya ya utawala unafahamika na Ofisi ya Rais, TAMISEMI bado haijapata taarifa rasmi kutoka Mkoa wa Mwanza, ukihitaji kuomba Halmashauri ya Buchosa kuwa Wilaya. Kwa hiyo, naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge, wafuate utaratibu huo na Serikali itaona namna gani ya kulifanyia kazi suala hili. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa suala hili limekuwa la muda mrefu sana, lina jumla ya miaka kama minne au mitano, wananchi wanaendelea kupata mateso ya kulipa 600 wakati wa kuingia na 600 wakati wa kutoka, wananchi hawa maskini. Mimi binafsi nimeshasumbuka sana suala hili nimezungumza na Mheshimiwa Kakoko, nimezungumza na Mheshimiwa Abood, nimezungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu amenijibu na barua ninayo hapa ya kwamba amewaagiza TPA washughulikie suala hili mara moja. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa kwamba tozo hizo zitapunguzwa mara moja ili wananchi waweze kuondoka kwenye mateso? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ilivyojibiwa katika swali la msingi tozo hizo zinatolewa kwa mujibu wa sheria na zinafuata tariff book ambayo ni ya TPA. kama ambavyo imejibiwa katika jibu la msingi, sasa hivi tunafanya majadiliano ili tuweze kupunguza tozo hizo kulingana na malalamiko ya wananchi ili tuweze kwenda kisheria. Hatuwezi kupunguza sasa hivi kwani ndiyo mambo haya haya ambayo yatazuka tena katika Ripoti ya CAG kwamba tumetoza kinyume na Tariff Book. Kwa hiyo, tunafanya marejeo hayo na tutakapoyakamilisha, tutawasiliana na vijiji vyote kama vilivyotajwa pale katika Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela watashirikishwa katika kikao cha wadau ili tuweze kupata tozo muafaka ambazo zitakubalika kwa wananchi wote. Ahsante. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Matatizo yanayowapata wananchi wa Igunga ni sawasawa kabisa na matatizo yanayowapata wananchi wa Jimbo la Buchosa hasa katika Visiwa vya Kome na Maisome. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze kwamba ni lini watajenga minara katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Buchosa yameshaingizwa tayari kwenye mpango wa utekelezaji katika zabuni itakayotangazwa ya awamu ya sita ili eneo hilo sasa lipate mawasiliano kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Buchosa. Ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa ninalo swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Buyagu sasa linaelekea kufikia hatma, lakini bado wananchi wa Kata ya Ilunda Wilayani Sengerema wana adha ya namna hiyo ya kuwa na kivuko kidogo: Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kivuko kikubwa katika eneo hili la Ilunda? (Makofi)

Mheshmiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa Wilaya ya Sengerema inayo majimbo mawili; lipo Jimbo la Buchosa na Mheshimiwa anafahamu kwamba watu wa Kome, Nyakalilo, Nyakasasa, Mtama wana matatizo makubwa ya usafiri: Je, Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka kivuko kikubwa katika maeneo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shigongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika eneo la Sengerema – Buchosa wana bahati kwamba tunajenga daraja kubwa pale Kigongo – Busisi na kuna vivuko kadhaa vinafanya kazi katika Ziwa Victoria. Baada ya barabara hiyo na daraja kukamilika, maana yake vivuko vile vitahamishwa kwenda maeneo mengine; na maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anataja ndiyo sehemu mojawapo tunaenda kumaliza changamoto hii ili kuweza kutoa huduma katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumza sasa tunajenga kivuko kipya ambacho kitafanyakazi Kata Nyakarilo na Kome kitaenda katika eneo hilo. Vile vile tunafanya ukarabati wa kivuko cha MV. SabaSaba ili kiende kusaidia MV2 Kome kuweka huduma katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ipo makini sana kupeleka vivuko kwa sababu mbili; moja, ni sehemu ya biashara na pili, ni sehemu ya kutoa huduma. Watupe subira kazi zitakamilika na shida ya usafiri katika eneo hili kwenye visiwa mbalimbali Ziwa Victoria itakuwa imekamilika. Ahsante. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa yanayomkuta Mheshimiwa Sangu huko Kwela yanafanana kabisa na yanayotokea huko Jimboni Buchosa; na kwa kuwa kilimo sasa kimeshathibitika kwamba ni uti wa mgongo na unategemewa na Taifa letu: -

Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea skimu ya Uchiri iliyopo Buchosa ambayo imetelekezwa kwa muda mrefu, akiwa katika utaratibu wa kuifufua iweze kuwasaidia wananchi wa Buchosa na Taifa kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari kwenda kutembelea Jimbo la Buchosa na niko tayari kwenda kutembelea Jimbo la Sengerema kuangalia mabwawa, ambayo fedha zake zilitolewa na hayajafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, tutashirikiana Waheshimiwa Wabunge, tutakwenda pamoja. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Nianze kwanza kwa kutoa pongeza nyingi sana kwa Serikali kwa namna ilivyoshughulikia matatizo ya wananchi wa Jimbo la Buchosa. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa juhudi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa Lumea, Nyakariro, Karebezo hadi Nyehunge wa shilingi bilioni 1.6. Mradi huu ni kichefuchefu, ulijengwa chini ya kiwango, mabomba yanapasuka, maji yanamwagika chini na wananchi hawapati maji: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini atatembelea mradi huu ili kuweza kuwa na utaratibu wa kufanya maboresho na wananchi waweze kupata maji?

Pili, ni lini Serikali itapeleka watalaam kuchunguza na kugundua watu waliohusika na ubadhirifu kwenye mradi huu ili waweze kuchukuliwa hatua kuepusha kuharibu sifa ya Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kwenda kutembelea Mheshimiwa Mbunge mantahofu, mara baada ya Mkutano huu tutakwenda kutembelea na kujionea na kuona kwamba kazi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Watalaam kwenda kuchunguza, Mheshimiwa Waziri ameshatengeneza task force ya kufuatilia miradi yote kichefuchefu na kuona kwamba inafanyiwa kazi na inakamilika na huduma ya maji inapatikana bombani na tunamtua ndoo mwanamke kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, napenda kusema kwamba, ile task force naamini wamesikia na ninasisitiza maagizo ya Mheshimiwa Waziri mara wasikiapo maagizo haya waweze kwenda mara moja ili kuchunguza na miradi ile iweze kukamilika na lengo la kutoa maji na kumtua mama ndoo kichwani liweze kutimilika. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Kwa sababu mahitaji ya wananchi wa Mchinga ni kufanya biashara na kuongeza kipato, na kivuko hiki ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa jimbo hili. Ningependa kupata tamko rasmi la Serikali kwamba ni lini hasa watarajie kwamba ahadi hii ya Serikali itatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshi mi wa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Shigongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ni lini hasa. Nimemueleza hapa kwamba tulishafanya tathmini, na daraja hilo linahitaji shilingi milioni 147, na imetengwa katika bajeti ambayo tutapitisha katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika mwaka wa fedha unaokuja daraja hili litajengwa, na hiyo nina uhakika kwa asilimia 100. Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa changamoto wanayoipata wananchi wa maeneo ya Tanga na Pangani ni sawa sawa na matatizo waliyonayo wananchi wa Buchosa ambao ahadi ya Serikali ilikuwa ni kujenga barabara kutoka Sengerema, Nyehunge mpaka Kahunda, lakini wananchi wale wamesimamisha shughuli zao wakisubiri fidia na ujenzi uanze: -

Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwaambia wananchi wa Buchosa ni lini fidia zitalipwa na lini barabara itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara anayoitaja ya Sengerema – Nyehunge hadi Kahunda yenye kilomita zisizopungua 82 ipo kwenye maandalizi. Kama nilivyosema kwa barabara iliyopita, ni kati ya barabara ambazo zinategemea kuanzwa kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka huu wa fedha. Kabla ya kuanza ujenzi sheria inatuambia tuwalipe kwanza fidia. Kwa hiyo, mara tutakapoanza kutangaza ujenzi huo, basi na wananchi watapatiwa fidia kwanza. Ahsante. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali. Nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana Serikali kutuletea barabara ya lami, lakini ilishafanyika tathmini lakini wananchi wanasubiri malipo. Kwa sababu mchakato unaendelea, je tathmini italipwa lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu barabara hii inahusisha Majimbo mawili, Jimbo la Sengerema na Jimbo la Buchosa, je Serikali iko tayari kuchukua ushauri wa wananchi wa Buchosa, kwamba ujenzi wa barabara hii uanzie Buchosa kuelekea
Sengerema badala ya Sengerema kuelekea Buchosa?
(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eric Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilimuelewa kuhusu tathmini, nadhani ni fidia, italipwa lini? Kama nilimuelewa ni kwamba fedha ambazo tumetenga, kitu cha kwanza itakuwa ni kulipa fidia ya wananchi ambao watapisha ujenzi huo, halafu barabara itaanza kujengwa. Kwa hiyo, itakuwa ni hatua ya kwanza ya kufanywa kabla ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ushauri alioutoa, kwa mujibu wa barabara ilivyo ni Sengerema-Nyamazugo- Nyehunge; hili suala ambalo tayari hata zabuni kama zimeshatangazwa, maana yake zinataja kuanzia wapi kwenda wapi. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kwamba majimbo ni hayo mawili lakini barabara itaanzia huku tulikoitaja na kwenda pale inapokwisha kwa sasa. Ahsante sana.