Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Robert Chacha Maboto (7 total)

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ahadi ambazo Hayati Dkt. Magufuli aliahidi wakati wa kampeni ilikuwa ni pamoja na kujenga soko kuu la Mji wa Bunda pamoja na stendi mpya.

Je, kati ya stendi na soko kuu, ahadi hii yenyewe itatekelezwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKO ANA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hapa nimeelezea kwa chini kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC, uendelezwaji wa miundombinu katika miji yetu. Na ule uendelezaji wa miundombinu kwenye TACTIC haihusu barabara peke yake, ni pamoja na masoko, stendi, madampo ya taka yaani tunatengeneza mji kuwa wa kisasa. Kwa hiyo, hata hiki anachokizungumza kuhusu soko kuu pamoja na stendi mpya katika Mji wa Bunda nafikiri itakuwa ndani ya package katika mradi huu wa TACTIC ambao mara utakapotekelezeka ni sehemu ya huo mradi, ahsante sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makao Makuu ya TANAPA Kanda ya Magharibi yako Bunda; na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ilitoa eneo kwa ajili ya kujenga ofisi zao za Kanda ya Magharibi. Je, ni lini TANAPA wataanza kujenga ofisi hizo? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimshukuru Mheshimiwa Robert Maboto kwa swali lake hilo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, TANAPA ina kanda nyingi nchi nzima na kila kanda inahitaji fedha ili tuweze kujenga miundombinu husika. Katika bajeti ambayo tutaileta mwaka huu tumeomba fedha kutoka Hazina ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo Ofisi ya Kanda ya TANAPA pale Bunda.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina Kata 14 na wakulima wake mazao yao yameathirika sana na wanyamapori, hasa tembo; Kata ya Nyatwali, Bunda Store, Mcharo na Sazila:-

Je, ni lini Waziri atatembelea Halmashauri hii ili aweze kujionea uharibifu huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wabunge wote ambao wanazungukwa maeneo ya uhifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria ambayo tulishapitisha kwamba wananchi wanapokutana na kadhia hii ya tembo na wanyama wengine tunatoa kifuta machozi. Nampongeza Mheshimiwa Robert Chacha kwamba ameendelea kulizungumzia suala hili la wananchi wake kuhakikisha wanapata kifuta machozi, lakini pia nimwahidi kwamba, nitafika kwenye eneo hilo ili tuweze kuzungumza na wananchi. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Bunda ni makutano kati ya barabara itokayo Ukerewe – Mwanza – Simiyu kwenda Sirari – Tarime – Musoma kuja Mwanza na Serengeti kuja Mwanza:-

Je, ni lini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaweka taa za barabarani za kuongoza magari ili kupunguza ajali zinazotokea eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, kwa sasa barabara zote zinazojengwa na zinazopita kwenye miji, katika mikataba lazima watengeneze barabara katika miji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpango upo sasa wa TANROADS kuhakikisha kwamba sehemu zote za miji ambazo zilikuwa hazina barabara za kuongozea magari kama alivyosema, wafanye usanifu ili tupate gharama yake na tuweze kuweka taa za kuongozea magari, hasa maeneo ambayo yana magari mengi. Kwa hiyo, study hiyo inaendelea. Naamini Bunda itakuwa ni sehemu ya wanufaika. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimu wa zao la pamba umefunguliwa tarehe 10 Mei na mategemeo ya wakulima ni kwamba wanapokwenda kuuza zao lao waweze kulipwa fedha zao.

Je, Wizara ya Kilimo imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inawasimamia wenye viwanda wasiende kukopa zao la wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magoto, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumetoa waraka kupitia Bodi ya Pamba, nunuzi yoyote anapochukua pama katika chama cha msingi ni lazima mkulima awe amelipwa ndani ya muda usiozidi saa 48 na mnunuzi yeyote atakayekwenda kinyume na hili tutamfutia leseni na kumuondoa kwenye database ya ununuzi wa pamba, hakuna kukopa pamba ya mkulima, hili ni la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili tumetoa bei dira ambayo wakulima ni lazima walipwe kiwango kisicho pungua bei hiyo, lakini wakati huo huo ushindani unaendelea, bei dira tuliosema Wizara ya Kilimo haitakiwi kupungua shilingi 1,050 bei ya chini ingawa bei inayoendelea sasa hivi ushindani umefika mpaka shilingi 1,100/1,150 na kila mnunuzi aweke pango la bei yake kwenye AMCOS ili mkulima anapopima pamba yake ajuwe bei ya siku hiyo ni shilingi ngapi na viongozi wa AMCOS wahakikishe wanamlipa bei iliyoko sokoni siku hiyo.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini, Alhamisi ya wiki iliyopita tembo wamekula mazao yao, hasa Kata za Bunda Stoo, Balili na Kunzugu. Wapo baadhi ambao wamefanyiwa tathmini ya mazao yao, je, ni lini Serikali itawalipa fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Robert Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kulipa malipo haya ya kifuta jasho na kifuta machozi na kulikuwa kuna malipo ya kipindi cha nyuma ambayo walikuwa wanadai na niliahidi hata kwa Mbunge mwenzie Mheshimiwa Esther Bulaya, kwamba nitafunga safari niende kwenye maeneo husika tukaangalie ni madai gani ambayo wanadai kisha Serikali iweze kuyalipa. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa maji Bunda Mjini ulikuwa wa thamani ya shilingi 10,600,000,000 fedha zilizokwisha kutolewa mpaka sasa ni shilingi 2,600,000,000 bado shilingi bilioni nane. Je, ni lini Serikali itamalizia fedha hizi ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maboto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi ule umeweza kupelekewa fedha hizi shilingi bilioni 2.6 na bado hizo shilingi bilioni 8 na fedha hizi tayari zipo kwenye mpango wa Wizara kuona kwamba tunaendelea kupeleka fedha. Ili kuweza kukamilisha mradi ule na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifanikisha Wizara ya Maji, kwa kuongeza fedha tofauti na namna ambavyo tulipitisha kwenye bajeti yetu. Hivyo, mradi kama huu na wenyewe pia tunaupa jicho la kipekee kabisa kuhakikisha kwamba unakwenda kukamilika. (Makofi)