Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Charles Stephen Kimei (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi siku hii ya leo nina afya tele. Pia nishukuru chama changu cha CCM kwa kunipa fursa ya kugombea kwenye Jimbo lile la Vunjo ambapo wananchi wake walitupa kura kwa wingi na CCM ikashinda kwa kishindo, kwa hiyo, CCM oyee.

WABUNGE FULANI: Oyee.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, niseme hivi, mimi niliyesoma hivi vitabu vitatu nasema ni kitabu kimoja ambacho bado kinaandikwa bado hakijaisha na naamini kwamba itakapofika mwezi Juni, 2025 tutaona chapter ya nne na pengine ikimpendeza Mheshimiwa Rais tutaona na chapter ya tano itakayokuwa inatuonesha kwamba dira ya 2025 kwenda 2050 itakuwaje lakini ni kitabu kitamu na utamu wake ni kwa sababu una happy ending, unaishia pazuri.

Mheshimiwa Spika, niliposoma nimeona kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyotoa Novemba 2015 anaanza na mambo magumu sana ya kuunda utawala bora na kutafuta uongozi ambao ungeweza ukapigana na mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali, kurudisha nidhamu na kuhakikisha kwamba mapato ya Serikali yanakusanywa vizuri na yanatumiwa vizuri. Naamini kwamba kwa kile alichokifanya kuunda uongozi ambao aliweza kufanya nao kazi lakini pia akawa anatumbuatumbua mpaka tukaona mambo yamesimama vizuri ndiyo sababu tunasema kwamba kusema kweli ni fundisho kubwa linalosema kwamba maendeleo ya Afrika, maendeleo ya Tanzania yanatokana na uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini uongozi bora siyo viongozi bora ni kiongozi mmoja ambaye anajitokeza, the leader, ana make a big difference katika mambo yote yanayofanyika kwenye nchi au kwenye kampuni inakuwa hivyo hivyo, kama ukiwa na kiongozi bora utaona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru na nasema kwamba kusema kweli ukisoma kitabu hiki ambacho kinaandikwa hakijaisha natumaini utaona wazi kwamba tumempata kiongozi ambaye anastahili sifa kwa kila Mtanzania. Hata mtiririko wa namna anavyoelezea dira na mkakati wake na malengo yake na milestone za kufikia na namna ya kutathmini utaona wazi kwamba ni kitu ambacho kinaeleweka kwa kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaona kitu kama hicho hata ukimuuliza bibi yangu pale mgombani kule Moshi wewe ni nani? Anakwambia mimi ni Mtanzania naenda kwenye uchumi wa kati, kipato cha kati na baadaye tutafika kwenye kipato cha juu. Kwa hiyo, kila mtu anaelewa ni kitu gani. Lengo kuu la nchi ni kuinua kipato cha Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake aliyotupa kwenye ufunguzi anasema wazi kwamba sasa amejua kutakuwa na miundombinu lakini hailiwi, lazima sasa tuweze kuwezesha wananchi wetu na wale tunaowaongoza kuongeza kipato chao, wajasiriamali kwa kuwawezesha kupata mikopo na kadhalika ili waweze kuinua kipato chao. Kwa hiyo, nasema kwamba kwa logic ya hiki kitabu kiko vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, nimsifu kwa kitu kimoja, katika nchi ambayo inaenda kwa kasi tunayoona, kasi ya ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia saba kwa wastani, lakini miradi mikubwa inatekelezwa. Utakuta kwamba mataifa mengi yanashangaa kwamba bado tumeweza kuendelea na utulivu wa uchumi mkubwa. Utulivu huo umetokana na umakini wa Mheshimiwa Rais, lakini pia tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wetu wa Fedha na Mipango pamoja na Gavana wa Benki Kuu kwa ushauri mzuri waliotoa. Kwa sababu wangeweza wakachukua njia rahisi ya kufanya inflation finance maana ku-print pesa na kukuza mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wao hawakufanya hivyo, wametumia njia ngumu ya kukusanya mapato kutoka kwa Watanzania, hiyo njia ngumu kuliko ku-print pesa au kukopa tu na ni kweli kwamba hii miradi mikubwa ungekuta kwamba inashawishi watu sana kuchukua mikopo ya ziada, lakini nashukuru kwamba hawakufanya vile wamefanya kitu ambacho ni kigumu, lakini tunaona matunda yake ni mazuri na ndio hapa unasema hapa tunaona kuna happy early.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi tumeona kuna utulivu wa uchumi wa ujumla ndio, exchange rate imekuwa stable, mfumuko wa bei uko chini, riba zimetulia lakini hazijatulia mahali pake kwa sababu ziko juu bado watu wanalalamika riba asilimia 15 inflation asilimia tatu, really interest rate ni kubwa sana. Kwa hiyo, kinachohitajika sasa ni pengine tuhakikishe kwamba tunaendeleza sera hizo za kuhakikisha kwamba riba nazo zinashuka kwenye mabenki yetu. Utaona mabenki yanarekodi faida kubwa sana, mwaka huu kwa mfano, faida za mabenki ni kubwa sana kwa sababu wanatoza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoke hapo niseme hivi, kwa kuona kwamba miundombinu inaboreshwa vizuri, sasa njia ya peke ni kuongeza uwekezaji na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusema kwamba ameunda Wizara ndani ya ofisi yake ambayo inashughulika na uwekezaji. Niseme hivi kwamba private sekta haitaweza kunufaika sana kama blue print aliyoizungumza Mheshimiwa Mwijage haitatekelezwa kwa umakini na kwa haraka zaidi. Inatekelezwa kwa speed tofauti tofauti kwenye kila Wizara, lakini ingetekelezwa kwa speed ile wanayotekeleza kwa mfano Wizara ya Viwanda naamini ungekuta vitu vinabadilika na pengine private sector ingeweza ikaanza kushika hatamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba tatizo kubwa katika sekta binafsi ni kusema kwamba uwekezaji lazima uwe mkubwa sana, kumbe sasa hivi uwekezaji hata kwenye nyumba yako unaweza kwa sababu kuna umeme. Ukishakuwa na umeme unaweza ukawa na kiwanda kidogo cha kuchakata hata ndizi na hiyo ndio njia peke kusema kweli ya kuinua kipato kule kwetu mashambani kwa kuunda viwanda vidogo kwa vikundi au kwa mtu mmoja mmoja ambaye ataweza kuchakata mazao akayaongezea thamani na yale mazao yakauzwa sehemu nyingine ambapo hayapatikani au ambapo yanahitajika kwa wakati ule.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba pengine tuangalie namna gani ya kuwawezesha vijana wetu au wajasiriamali wanawake na wengine na hata akinababa kwa kuwapa exposure. Nikasema exposure haiwezi kutolewa kwa kumpeleka mtu China kuangalia maonesho China hapana, exposure ni kwamba pengine Shirika letu la SIDO lingekuwa karibu zaidi kule kwenye vijiji sasa linashughulika kwa kuona kwamba kweli linaonesha watu kwamba kuna kiwanda kidogo cha shilingi milioni moja au laki tano na hiki kiwanda unaweza ukakitumia mkiwa vijana watano, mkakitumia mkaongeza thamani mkapeleka mkauza. Naamini kwamba hicho lazima kifanyike na naamini kwamba Wizara inayohusika itafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunazungumza mambo ya mikopo, kupeleka watu vyuo vikuu, hii nataka kusema katika uchumi tunaojenga sasa hivi uchumi wa kati, tatizo kubwa ni skills study zile za watu kufanya vitu kwa mkono sio kuwa na degree sio kuwa na ma-Ph.D hayatasaidia sana. Utakuta kwamba unemployment kati ya watu waliomaliza chuo kikuu ni kubwa sana lakini mtu anayetengeneza simu, simu hizi tunazotembea nazo hizi mfukoni ukimtafuta mtaani humpati na wana kazi, mechanic wote wana kazi lakini tatizo moja tunasema tu kwamba elimu yetu inalenga chuo kikuu, hapana! Huko ni kwa zamani, elimu ilenge daraja…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …baada ya kumaliza form six watu wengi waende kujifunza kazi za mikono, study za mikono. Kwa hiyo, vyuo vya ufundi viongezeke…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Lakini na vyenyewe vibadilishe mwelekeo sio kuangalia zile study zilizokuwa zinahitajika zamani tuangalie study za kisasa, electronic base na ambazo…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei pokea taarifa, jitambulishe Mheshimiwa nani.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naitwa Mheshimiwa Musukuma, ningependa kumpa taarifa tu Mheshimiwa Dkt. Kimei kwamba anavyochangia anasema tuache kuamini ma-degree na ma-PhD. Nampa taarifa tu kwamba duniani kote matajiri wengi hawana degree. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa!

SPIKA: Kabla Mheshimiwa Dkt. Kimei hujapokea taarifa hiyo, nisisitize tu Waheshimiwa Wabunge mumsikilize Mheshimiwa Dkt. Kimei hoja yake, ni hoja ya msingi sana. Hii habari kila mwanafunzi anaenda chuo kikuu anasoma vitu vya ajabu ambavyo tumezoea traditionally, sitaki kuyataja masomo, yako masomo yaani ni kama kumpotezea mtoto tu direction. Yalikuwa na maana enzi hizo, lakini leo hii dunia ya sasa, dunia ya uchumi wa kati, ndio hii anayopendekeza Mheshimiwa Dkt. Kimei. Skills na kwa hiyo hata mfuko wa mikopo uelekeze zaidi mikopo yake huko. Mheshimiwa Dkt. Kimei hebu rudia hiyo hoja yako bwana, nakupa dakika tatu. Katibu hebu iweke vizuri. (Makofi)

Waziri wa Elimu amekaa vizuri anakusikiliza sasa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ndio nasema hivyo kwamba, kusema kweli mahitaji ya uchumi wetu wa sasa hivi ni watu wanaoweza kutenda na mahitaji ni kwamba watu wana magari lakini hawawezi kutengeneza, ukitafuta fundi hakuna kwa sababu hakuna mtu anayefundisha vitu hivyo na siyo tena kutengeneza magari ambayo ni ya ajabu, sasa hivi tengenezeni magari ambayo lazima zile shule zetu za ufundi na zenyewe zi-adopt mahitaji ya sasa hivi. Ukienda uka-register wanafunzi utapata wanafunzi utapata wengi sana ukitafuta kwenye electronic base industry na nini utapata, lakini ukienda kwa ile ya zamani kwamba sijui unataka mtu wa kuranda. Tuna chuo cha ufundi pale kwetu Mamba pale lakini hakuna mtu anaenda kwa sababu wana mashine za kuranda wanafundisha kuranda au cherehani za kushona lakini ni zile za zamani sasa hivi kuna cherehani za kisasa.

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema hivi kwa kule kwetu kama anavyosema Mheshimiwa Saashisha, kusema kweli zao la kahawa limedorola sana na nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais aliweka hilo pia katika zao la kimkakati. Hata hivyo, niseme hivi kule Kilimanjaro ile ardhi imeshadidimia haifai tena hata kulima kahawa, utatumia madawa mengi na watu hawajui kutengeneza composite, kwa hiyo unakuta kwamba ile kahawa ukiipeleka kuuza nje tena hupati hata wanunuzi. Halafu bahati mbaya pia vile vihamba vyetu, yale mashamba yetu yamekuwa tragmented mtu mmoja ana robo heka, atalima wapi.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi, sisi Wachaga wengine tunataka tuhamie mahali ambapo kuna ardhi, tukalime huko, mambo ya kusongamana kule haifai na wameniomba wananchi wangu wa Vunjo kwamba jamani ukienda tafuta mahali utakakoweza kutupeleka tukalime tupate eneo tulime na sisi tuwe na tija, tuwe na mabilionea na sisi, lakini kusema kweli kule Uchagani huwezi kuwa bilionea kwa sababu hakuna ardhi. Watu wa kule Vunjo tuna shida hiyo na nitakuja kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, atusaidie.

Mheshimiwa Spika, mwisho, niseme hivi katika rasilimali tuliyonayo sisi kule Kilimanjaro, ni mlima Kilimanjaro na ni kweli wana Vunjo na wengine wote wanaozunguka ule mlima wanapata shida sana. Shida kubwa ni kwamba ajira haipatikani, vijana wengine wanaokuja kupata ajira kule ni kutoka maeneo mengine, lakini hata wale wanavijiji wanaozunguka ule mlima, ile nusu maili hawaruhusiwi kutumia, siku hizi wanapigwa, walikuwa wanasema ni wanawake tu waende huko, sasa wanawake wakaenda wenyewe, baadaye na wenyewe wakanyimwa kwenda huko kutafuta kuni, kutafuta majani ya ng’ombe na mbuzi na kadhalika. Sasa tunamwomba Waziri wa hifadhi naye atuangalizie hilo na ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Spika, mambo ya barabara yameshazungumza sana. Naunga mkono hoja ya kuongeza Mfuko wa TARURA, kusema kweli barabara zetu zina matatizo japokuwa hata zile ambazo zinatakiwa ziwekwe lami zimeahidiwa lami tunazo hizo kama tatu hivi ambazo Mheshimiwa Rais naye alituruhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Naona kengele imelia.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kimei, tunakushuru sana…

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa moyo moja na sisi tutatekeleza kila jambo ambalo liko kwenye hotuba hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa muda huu uliniopa nizungumze. Ninayo mengi kidogo,kwahiyo nitaenda moja kwa moja kwenye mjadala huu. Pia nikupongeze wewe kwa namna ambavyo unatuongoza, kusema kweli inatupa hamasa kubwa sana kuwa Bungeni hapa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba naunga mkono kwa asilimia mia moja Mpango ambao umewasilishwa hasa kwasababu nafikiria kwamba mpango huu una uhalisia kwa kiasi kikubwa. Uhalisia kwamba assumptions zilizotumika kwa mfano ya kusema kwamba tunaweza tukaongeza pato la Taifa mwaka ujao kwa 6.3%,wangeweza wakasema 7%, lakini wamesema 6.3%, naamini ni achievable kwasababu ya misingi ambayo tumeijenga. Naamini kwamba kuna mambo mengi ambayo yanaweza yakatuteteresha kwasababu hatujajua dunia ina kwenda wapi kwasababu ya wingu ambalo bado lipo kuhusiana na corona kwenye nchi za nje, lakini naamini endapo hali itabadilika kidogo tunaweza tukafikia hiyo 6.3% kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana pia wastani wa 8% utafikiwa mwishoni mwaawamu, lakini inawezekana pia hata 7%, ni nzuri sana kwasababu wale wanaojua kanuni ya ukuaji cumulative(limbikizo la ukuaji)wanaita ni the low ofcumulative growth. Kama unaongeza pato lako kwa asilimia 6.0 kwa mwaka unaweza uka-triple hiyo kwa miaka siyo zaidi ya miaka 10. Kwahiyo naamini kwamba tunaweza tukafikia hiyo nanihi yetu ambayo ni pato la uchumi wa kati, kiwango cha juu.Kwahiyo naamini tupo sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nakosa tu kwenye huuMpango, nilikuwa natamani sana nione mipango ambayo imekaa fungamanishi kama kwa mfano ulivyokuwa mpango wa SAGCOT ambao unaeleza vitu vingi ambavyo vinasaidianaili kuhakikisha kwamba ile corridor inatoa kitu. Sasa kuna mipango kama huo wa SAGGOTambao naamini kwamba bado uko unatekelezwa. Nilikuwa nataka tuone kamalogisticsmapaulogistics plan za kufanya Tanzania hususan Dar es Salaam kuwa ni logistichub ya nchi hizi ambazo zinapakana na sisi, lakini sijauona vizuri. Ndiyo tunajenga vizuri infrastructure ile ya kutufungulia mipaka na kupeleka vitu kwenye mipaka na tuweze kupata a lot of value additions, lakini bado naona haijafungamanishwa sawasawa,ili kuona zile corridor tulizonazo zote zitatusaidia namna gani kuongeza kipato chetu bila kutegemea sana vitu vingine ambavyo ni more primary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba wengi wanasema kilimo, kusema ukweli ni kizuri, lakini nataka kuwatahadharisha kwamba Mheshimiwa yuko sahihi anaposema kilimo hakilipi kama hatuna viwanda. Bado watakaoweka bei kama tutawauzia primary product watakuwa bado ni walaji wa kule nje, ni walaji wa Ulaya na wanapoona kwamba tunataka kufanikiwa watazidi kutubana, watasema bei ziko hivi bei zitaanza kutuvuruga, kwahiyo njia tu pekee ya kuweza kuhakikisha kwamba beiya mazao yetu inaimarika ni kuhakikisha kwamba tuna-process, tunauza kitu ambacho kinaweza kikahifadhiwa, kikafika kwenye masoko tofauti tofauti kwa bei ambayo siyo ile inakuwa dictated by the consumers. Kama consumers ata- dictate bado utapata matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kama ninavyosema kilimo lazima tunapokizungumzia tuseme tutafanyaje tukiunganishe na viwanda ili kiweze ku-process. Niseme kwamba tumezungumza mambo mengi kuhusiana naukuaji nakadhalika, lakini ni lazima tuzungumzie strength. Watu wanapotengeneza plan yoyote unaangalia strength zako ni nini na ni sawa tukasema ni uongozi bora, amani, utulivu, mshikamano na vitu vyote hivyo na siasa safi, lakini kitu ambacho hatujakiona ni ile strength tuliyojenga kwa kutuliza uchumi wetu ukawa tulivu ambao mfumuko wa bei upo chini, wenye exchange rate ambayo ni nzuri nakadhalika ambayo inatufungulia milango ya kuweza kuisaidia Serikali yetu kuweza kukopa kwa bei nafuu kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa MWENYEKITI,tunapoangalia mipango hii mara nyingi tunajua tunatumia cash budget, sasa tukianza kuzungumza mpango kwa kuanzia kwenye matumizi kwa kuorodhesha vitu gani tunataka vifanywe, kwanza niseme naomba Mungu ajaalie kwamba pamoja na mafanikio tuliopata kwenye miundombinu, kule Vunjo wamesahau. Naomba wasisahau zile barabara zetu kule Vunjo,lakini kama tutaorodhesha kila mtu aorodheshe vitu, the shopping distance is huge,TARURA inataka pesa,TANROADs inataka pesa, halafu bado wengine wanasema Serikali ijenge viwanda, hili hapana, Serikali haiwezi kujenga viwanda, zaidi Serikali iwezeshe kwenye viwanda vya kimkakati ambavyo tunatakiwa Serikali kama tunavijua kwenye maelekezo ya hotuba za Rais. Hiyo ya kuwezesha viwanda vya kimkakati hata kama ikiingia ubia lakini kuhamasisha, sera ziwe safi,blue print iwepo, mambo yawe sawasawa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,kusema kweli hatuwezi kusema Serikali ikajenge viwanda vya alizeti nakadhalika hatutaweza hiyo, tuwezeshe watu na ndiyo kazi yetu kwenye zile kamati ambazo zinahusika. Kwahiyo nataka kusema hiyo tuwe makini,kwasababu hatuwezi kuorodhesha. Nimejifunza kitu cha msingi sana na nimefurahia sana Wabunge fulani wameanza kusema kwanini tusipate fedha namna hii. Kwasababu cha kwanza ni mapato, je, yanatoka wapi? Kuna Mheshimiwa Shabiby alisema pengine mapato tuongeze tozo kwenye matumizi ya mafuta na tena akatoa pia mawazo ya namna hii, yale ndiyo mambo tunataka tujue kwasababu ukishapata zile fedha ukimpa Rais wetu anazitumia vizuri, anajua kuzisimamia kwa ufanisi,zitazaa vyovyote tunavyotaka, lakini tuangalie na nashukuru wale wanaozungumzia kwamba tuzibe mianya ya pesa kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tax effort yetu we mention kwenye hizi documentis 13%,12.9% ndiyo revenue effort tuliyofanya mpaka mwaka jana na tunaendelea kusema mwaka unaokuja 13.3% ndiyo tax effort, nchi nyingine hata hapo Kenya 23% ya GDP, uwiano kati ya mapato ya Serikali na GDP, pato la Taifa ni 20%, sisi tunasema 13% ni ndogo sana, ina maana kwamba njia tunazotumia kutoza kodi na njia tunazokusanya mapato yetu ni finyu. Aidha, vile vyombo vyetu vinavyoshughulika na ukusanyaji wa mapato vijiunde upya vi-think out of the box, what is happening?Effort yoyote Mheshimiwa Rais aliyofanya kupata hela kwenye madini na nini lakini bado eti revenue effort 13% ofGDP isnothing, tunataka tupate 20% whichmeans tunapata 28 trilioni, tunge- finance vitu gani? TARURA ingepatapesa mpaka tushindwe kuzungumza, lakini ninavyoona ni kwamba kuna kitu kiko hafifu hapo katikati kwenye ukusanyaji, sijui zinaenda wapi hizo hela. Kwanini iwe 13% au sisi tuna overstateGDP yetu pengine I do not know, lakini kama kweli takwimu ziko sahihi 13% ni ndogo toka tukiwa kule sisi miaka ya 1996, kwahiyo tunazungumza kwamba effort yetu lazima ifikie 20%, sasa mpaka leo hii 13%, tuna matatizo lazima tuanzie hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tuna-demand barabara na vitu vingine, je, mapato yanatoka wapi? Kwasababu hutapata kule kwenye Wizara ya Viwanda wanapata 6%, kilimo wanapata 6% of approved budget, it willnever work. Kwasababu hiyo tuna over state hizi revenue ndiyo sababu tunapanga vitu ambavyo ni hewa,havitatekelezeka,where is the money?The money is the cash budget, sasa niseme hivi kwanini nimeanza kusema kwamba tuna strength moja ya kukopesha. Revenue ya Serikali ya matumizi inatokana na vitu viwili taxrevenueyaani mambo ya kodi na tozo; pili, mikopo. Sasa mikopo inaweza ikatokana kwenye mabenki ya ndani napensionfunds nakadhalika yaani vianzio vya ndani, lakini pia zinaweza zikatoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nje na tunaambiwa kwamba nanii yetu iko chini sana, yaani uhimilivu wetu wa ukopaji bado tunaweza tuka-affordhata mara tano, sasa kwanini tusikope zaidi, tunaogopa nini kukopa kwasababu tunajenga rasilimali, tunajenga mtaji, nchi hii ina balance sheet yake,liabilities and assets. Watu wanaposema sijui deni hili siyo himilivu, deni walikuwa wanapiga ile gross hawaondoi ile rasilimali tuliyotengeneza,assetskwahiyo lazima uchukue asset - liabilities unapata net liability au netasset.

Sasa sisi ukiangalia kwa mfano vitu ambavyo vimejengwa Awamu hii ya Tano thamani yake na deni letu, ni kama hatuna deni yaani ukiangalia kwa uhimilivu watu wa Taifa letu,uhimilivu wa balance sheet ya kwetu,network yetu ni nzuri kwasababu tumekopa tumeweka kule, hata kama tungekuwa tumekopa mara ngap,i tutaingiza kwenye asset inazaa vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie…

MWENYEKITI: Tayari ni kengele ya pili.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Sasa nina mengi sana, lakini...

MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI:Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.(Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na napenda kwanza nimshukuru sana na nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake pamoja na Kamati ya Bajeti kwa namna ambavyo wamewasilisha Mpango huu. Natumaini wote imetufurahisha. Nataka nianze kwa kusema kwamba naunga hoja yake mkono, japokuwa nitakuwa na maoni mawili au matatu ili kuweza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hivi kwamba kusema ukweli kwanza tunawapongeza pia Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kutuwekea uchumi wetu kwenye hali ya utulivu. Tunajua kwamba ukuaji umekuwa mzuri sana, hata wakati huu wa covid, lakini pia mfumuko wa bei uko chini, uko vizuri, japokuwa namuunga mwenzangu mkono aliyezungumza kwamba pengine asilimia tatu ni ndogo sana, inatunyima fursa fulani ya kuweza kukuza zaidi kwa kuipa Sekta Binafsi na wale wanaouza, nafasi ya kuona faida watakayopata wakiendelea kuzalisha Zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona kwamba hali ya deni la Taifa ni himilivu. Pili, tunaona pia kwamba thamani ya shilingi yetu iko vizuri na pia tuna International Reserves ambazo ni nzuri. Hiyo ina maana kwamba ni strength kubwa sana ambayo tunaweza tukaitumia tukafanya assessment ya nchi yetu kwa athari ya wawekezaji na hivyo tukaanza kukopa kwa riba ya chini sana. Riba ya asilimia tano au sita unaweza ukapata kwa mfumo huo wa infrastructure bond au pia kwa kukopa moja kwa moja kwa direct placement ya bond yetu kwa wale wanaotaka kuwekeza Tanzania kwa sababu Tanzania imekaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwamba hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi elekezi. Hii miradi tunasema ya vielelezo kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza tukakopa, tukahamasisha na tukafanya haraka haraka tukaanza kuona matunda kutokana na miradi hii mikubwa ambayo itatoa chachu katika ukuaji wa Taifa letu. Nataka niseme kwamba tutumie hiyo kama fursa, kama ni strength na hiyo strength tuweze kuitumia kuweza kufanya mchakato huo wa kuweza kwenda kwenye soko la Kimataifa na kukopa na tusizingatie sana kukopa ndani kwa sababu tukikopa ndani maana yake tunai-crowd out private sector. Watu binafsi hawawezi kwenda nje kwa sababu hawajulikani, lakini Serikali inajulikana kwa sababu ni Serikali na Serikali is as good as gold.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukihamasika sisi Serikali tukakopa nje, tukaacha resources za ndani zinakopwa zaidi na watu binafsi, kwanza riba zitakuwa chini. Sasa hivi tuliambiwa kwamba riba nashangaa kwamba licha ya vigezo hivi vizuri vya uchumi, riba bado ziko kwenye asilimia 15. Nimekutana na watu wa BOT walituambia kwamba kwa sababu tunakopesha Serikali kwa asilimia 15, sio kweli! Serikali inalipa asilimia 15 kwa bond ya muda kati ya miaka 15 na 20, lakini Benki zinakopesha mikopo ya mwaka mmoja mpaka miwili sanasana pengine ni michache sana kwa miaka zaidi ya hapo. Sasa wakikopesha kwa asilimia 15 ni kubwa sana ambapo Serikali ikikopa kwa kipindi hicho kifupi riba inakuwa ni kwenye asilimia chini ya 10. Kwa hiyo unaona kwamba kuna uwezekano wa kushusha hizi riba kwa kuwezesha Sekta Binafsi kukopa zaidi na hivyo kuwezesha Sekta Binafsi kuwekeza na tukaona matokeo ya Mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kitu kimoja ambacho nimekisikiliza hapa. Tunafanya mambo kimazoea mazoea sana, yaani tatizo la sisi Waafrika pengine ni kwamba tunaanza kuzalisha halafu ndiyo tunatafuta soko. Kumbe uzalishaji unatakiwa uanze sokoni, unatafuta soko liko wapi. Ukishaona soko liko wapi na bei zake zikoje, ndiyo unasema sasa niki-incur au nikitumia gharama hizi kuzalisha nitapata faida, lakini mtu anazalisha ndizi heka 20 halafu zimeshaiva, anasema anatafuta soko liko wapi, hamna soko lolote namna hilo, huwezi kupata na mtu akijua unazo ndizi zinaoza anakupa bei ya chee! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze kufanya biashara kitofauti kwanza tufanye utafiti tujue kwamba ni kitu gani kinauzika wapi. Tunapoendelea kulima, tunazungumzia mazao haya ya asili siku zote, pamba, kahawa, tumbaku. Hivi tumeshajiuliza ni wapi masoko haya yakoje duniani kwa sasa hivi? Bei za huko mbele za kahawa zinaenda wapi, bei za tumbaku zinadidimia na tunaendelea kusema tumbaku na kadhalika. Ukweli tukifanya tathmini sahihi tukajua kwamba ni kitu gani cha kuzalisha hapa kwetu, sio lazima iwe ni mazao haya tunayoona, tumeona kwamba tulivyowaambia Wachaga kule kwamba hawa jamaa wenzetu wa Kyela wanalima avocado halafu wanapata kilo moja shilingi 1,500; kila mtu anatafuta mbegu ya avocado, huna haja ya kumtafutia mbolea, anatafuta mwenyewe kwa sababu anajua kwamba ina faida kulima avocado.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa na taarifa hizo lakini ukweli ni kwamba taarifa hizi hazimfikii mkulima, tunakaa na hizo taarifa, hujui kwamba unaweza sasa badala ya kulima kahawa ukalima avocado, kwa nini? Ukiendelea kulima kahawa kwenye ule udongo wa kule kwetu umeshakwisha kabisa kwa sababu umelima kahawa miaka 40 au 50, kwa hiyo hauna tena rutuba na hauna tija. Kwa sababu hauna tija badilisha uzalishe linguine, baada ya muda mwingine unaweza ukarudia tena kahawa na ndiyo mambo ya crop rotation, wale wanaojua mambo ya kilimo. Kwa hiyo naweza kusema kwamba pengine kuna haja ya kusema kwamba ni eneo lipi nibadilishe zao lile, kama kule Uchagani kahawa haiendi tena, pengine twende upande wa avocado na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine pia unaona kwamba unatumia gharama nyingi kwa sababu ule udongo unatakiwa ufanye rotation, uzalishe kitu kingine. Naamini kwamba tunaposema tutafutiane masoko, cha kwanza ni hizo taarifa na hizo taarifa sasa hivi ni kielektroniki, tufungamanishe masoko yetu. Mtu hajui kwamba kama nina ndizi, Mbeya wananunua namna gani ndizi, Moshi wananunua namna gani, Nairobi wananunua namna gani kwa kutumia hizi gadgets zetu za mawasiliano hizi ambazo zinatupa bei kila mahali duniani virtually unaweza ukajua kila kitu kinauzwa namna gani. Kwa hiyo watu watajua bei zake na sio lazima ukutanishe mtu physically, unaweza ukakutanisha watu kwa mawasiliano haya tuliyonayo na hiyo ni bei nafuu ya kukutanisha watu, ni bei nafuu ya kumpa mtu tija ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, mimi nafikiri kwamba katika huu Mpango wetu, suala zima la ushirikishi, kujenga uchumi shirikishi na uchumi shindani. Issue iliyopo ni kwamba tutafanyaje vijana hawa wapate ajira na hawawezi kupata ajira bila kujiajiri wenyewe sasa hivi kwa sababu watu ni wengi ambao hawana ajira na hawataki kuingia kwenye kilimo kwa sababu kilimo hakina tija na kwa sababu hawajafundishwa namna ya kulima kwa tija au kwa faida. Kwa hiyo naomba hivi, kwamba pengine umefika muda sasa tujaribu kutengeneza mfumo wa kuwa-organize vijana kwenye vikundi na kuwaonesha namna gani ya kutengeneza mashamba yenye tija, kutengeneza viwanda vidogo vidogo vyenye tija na mtu asifikirie kwamba kiwanda ni kiwanda cha Mchuchuma, hapana. Tena sasa hivi hata kuzungumza mambo ya chuma ni kitu tofauti kidogo kwa sababu dunia haiendi kwenye mambo haya, inaenda kwenye software zaidi sasa hivi, kwa hiyo Sekta ya Huduma ndiyo itakuja kuwa ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Huduma maana yake ni sekta ya kuhudumia viwanda, kwa sababu ukiwa na kiwanda lazima kihudumiwe, maintenance na kadhalika. Sasa kama wewe unakimbizana tu hiki unasahau kule, haitawezekana, lazima tuingize fedha, lakini ili vijana waweze kufanya hivyo wanahitaji mtaji, mtaji unatokana na nini? Tunasema tutawapa vimikopo vidogo dogo kwenye halmashauri, haina kitu hiyo! Tuunde ile Mifuko ya Serikali ambayo imetawanyika kila mahali, tuunde National Credit Guarantee Scheme or Fund au kuwe na misingi ya kibiashara lakini nafuu ambayo itakuwa imewekwa na Serikali ili watu wanaotaka mikopo wanajua tunaenda pale ambapo kutakuwa na kitengo cha wakulima, vijana, vinakaa mahali Pamoja. Pia unaweza uka-leverage ile guarantee scheme ikazalisha maradufu kwa sababu kama default rate kwa mkopo, hiyo iliyotoka kwa vijana pengine ni only ten percent ina maana kwamba ukiwa na mkopo wa ku-guarantee watu 100 unazidisha mara 10, uta-guarantee watu mara 10 yaani kiasi cha fedha mara 10. Sasa hivi unatumia kile unam- guarantee mtu mmoja ambapo tunaweza tukapeleka kwenye guarantee fund tukawapa watu wakaendesha kibiashara, tukaweza kuwezesha watu kupata mikopo kwa wingi na mitaji kwa wingi kwa muda mrefu na muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, mimi ni muumini wa masuala ya kwamba, kilimo cha sasa hivi ni lazima kibadilike na kubadilika kwa kilimo hicho ni lazima tusifanye mambo ya mazoea, tujaribu kuona ni kitu gani kitaoteshwa wapi na wakulima wapewe taarifa za masoko ambayo ni sahihi. Kwa kumalizia niseme hivi, ili tuweze kuongeza lile fungu la kukopesha au kuwezesha watu kupata mitaji, lazima tuunde National Credit Guarantee Fund or Corporation ambayo itashughulika na Mifuko yote na ile fedha inakaa mahali pamoja na inatumika kwa faida ya wengi. Hapa nataka kukuhakikishia kwamba inaweza ikawa ni kubwa kuliko Benki zote hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)