Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Innocent Sebba Bilakwate (22 total)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri lakini sijaridhika na majibu yake. Niliuliza ni lini masoko haya yatafufuliwa kwa sababu haya masoko ni muhimu kwa ajili ya wananchi wa Kyerwa na Waziri mwenyewe anajua wananchi wa Kyerwa wanapata shida hawana mahali pa kupeleka mazao yao. Naomba anieleze ni lini masoko haya yatafufuliwa yaanze kujengwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba Naibu Waziri awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa na Watanzania ambao wananufaika na masoko haya, je, Serikali imetenga pesa kwenye Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya masoko haya kukamilika?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Innocent Bilakwate ameuliza nijibu ni lini? Nimemweleza, DASIP I ilikoma, nimewasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwamba Mpango wa DASIP II haujaanza, utakapoanza tuwaweke watu wa Karagwe na Kyerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina maslahi na sehemu hizi, napenda niseme ukweli, msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Katika bajeti sijaweka lolote kwa ajili ya masoko haya ya Nkwenda na Murongo, lakini kwa ajili ya Nkwenda na Murongo tumeandaa utaratibu ambapo wakulima wa mazao wa Karagwe, hasa maharage tutawaunganisha moja kwa moja na wanunuzi wa Oman na Innocent Bashungwa nimemteua aratibu shughuli hiyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati yupo kwenye kampeni aliahidi kuondoa tozo mbalimbali ambazo zinamdidimiza mkulima wa kahawa. Mpaka sasa Serikali bado haijaondoa hizo tozo. Je, Serikali ipo tayari kuwaruhusu wananchi wale wanaolima kahawa waweze kuuza kahawa sehemu nyingine ambapo watapata bei nzuri?
shimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba huu msururu wa kodi utatafutiwa utaratibu wa kuziondoa zile ambazo hazistahili kutozwa au zenye kuleta kero kwa wananchi. Pamoja na nia hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais bado mazao haya tunayahitaji hapa nchini. Serikali hii imeweka kipaumbele cha kuwa nchi ya viwanda na hivi viwanda vitahitaji malighafi ipatikane hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, halitakuwa jambo la busara leo tukisema kwa sababu tuna tatizo hili la kodi ndogo ndogo zenye kero, basi tuachie malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu ianze kuuzwa nje. Utaratibu tunaoufanya ni kuchukua hatua za dharura kuhakikisha kwamba bei zinakuwa nzuri na masoko yanakuwa mazuri ili kutowapa shida wananchi wakati wa kuuza mazao yao.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hizi pesa ni za wananchi ambao ni maskini na zimekaa muda mrefu bila kupata hiyo mikopo. Je, Serikali iko tayari kurejesha hizo pesa au kuongeza riba kwa sababu hizi pesa zimekaa muda mrefu na hawa wananchi hawajapata jibu na hili tatizo limekuwepo Karagwe pamoja na Kyerwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, dhana nzima ya kwanza kabisa ya makusudio ilikuwa ni kuwafanya wakulima hawa kuingia katika Hifadhi ya Jamii lakini mkulima aliingia katika mfumo huu baada ya kuchangia kipindi cha miezi sita mfululizo alikuwa anapata sifa ya kuweza kukopesheka kupitia SACCOS katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii tu kumwomba Mheshimiwa Mbunge kama bado kuna matatizo haya katika maeneo yao na kwamba wako wakulima ambao walikwisha kutoa fedha hizi wametimiza masharti na hawajapata mikopo mpaka leo, basi wawasiliane na ofisi yetu ili tuweze kuwasaidia katika upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya wakulima hawa. Vilevile nimtoe hofu tu ya kwamba fedha ile ambayo ilikuwa inachangiwa ni fedha ambayo ilikuwa ni ya mkulima mwenyewe kujiwekea kinga ya kijamii na ambayo ingemsaidia katika mafao tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama bado wana mawazo tofauti, Ofisi yetu iko wazi kwa ajili ya mashauriano na kuweza kuwasaidia katika kutatua changamoto hii ambayo inawakabili wananchi hawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza sijaridhika na majibu ambayo amenipa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu kusema hii barabara inapitika kila wakati si kweli! Barabara hii mwaka wa jana mzima ilikuwa ni barabara mbovu imejaa mashimo, magari yote yanayopita barabara ile yanaharibika sana. Kwa hiyo, kuna taarifa ambazo wamekuwa wakiletewa ambazo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza; je, yuko tayari yeye mwenyewe binafsi kwenda kuitembelea barabara ile na kuiona ili aone umuhimu wake kwa sababu taarifa ambazo wamekuwa wanaletewa sio za kweli?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Rais akiwa pale Nkwenda kwenye kampeni aliiona barabara ile ikiwa na umuhimu kwa kuwa barabara hii inapita katikati ya Wilaya. Aliahidi kutupa kilometa 20 akiingia tu madarakani. Hizo kilometa 20 zinaanza kujengwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikiri kwamba miongoni mwa Wabunge ambao wanakuja ofisini kila wakati kufuatilia ni pamoja na Mheshimiwa Bilakwate. Mheshimiwa Bilakwate ameifuatilia barabara hii na tumekuwa tukijaribu kuangalia katika hizi barabara mbili zote zinaanzia karibu sehemu moja kuishia karibu sehemu moja. Suala ni ipi kati ya hizi mbili ni muhimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kilichopita kama ambavyo tumeongea ofisini, ni kwamba uongozi wa Mkoa pamoja na Mbunge aliyepita waliona kwamba hii barabara ya kupitia Kigarama ndiyo ipewe umuhimu wa kwanza na hii ya kupitia Omurushaka nayo wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa kule aliipa kipaumbele. Kwa hiyo, barabara zote mbili sisi kama Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tumezichukua kwa umuhimu wake. Tutaanza na hii ambayo tumeshaanza kufanya kazi, tukiimaliza hii tutakuja kukamilisha hii nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tunasubiri kuanza hii ya pili ambayo ndiyo anayoifuatilia kwa umakini sana Mheshimiwa, tunamwomba sana akubali kwamba ile kazi tunayoifanya kwanza ya kuimarisha ule mlima maana tatizo kubwa liko pale mlimani hasa. Ombi lake la kwanza nalikubali, nitakuwepo naye huko, tukaongee na wananchi kuthibitisha ahadi ya kiongozi wetu mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo afahamu mazingira tuliyonayo kutokana na hizi barabara mbili ambazo zote zinaonekana zina kipaumbele lakini viongozi wa Mkoa na Mbunge aliyepita inaonekana hiyo nyingine ndiyo waliitanguliza zaidi. Sasa ni suala la kutafuta namna gani zote mbili twende nazo kwa sababu zote zina umuhimu wa pekee na zinatoa huduma kubwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mheshimiwa Waziri naomba nikuulize swali; barabara ya Mgakolongo kwenda Kigarama mpaka Mlongo upembuzi ulishafanyika muda mrefu na wananchi wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwasababu walishawekewa “X”. Barabara hii ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Bilakwate kwa namna anavyofuatilia ujenzi wa barabara zote mbili zinazopita katika Jimbo lake; moja upande wa Kaskazini na nyingine Kusini n nikubaliane na yeye kwamba hii ya Kusini inapita katika maeneo makubwa, ingawa hapa hajayasema lakini ameyaongea katika Ofisi yangu. Naomba nimhakikishie kwamba fedha zimetengwa kwenye mwaka huu wa fedha wa mwaka 2016/2017; nimuhakikishie tutajenga kabla ya tarehe 30 Juni, 2017.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la maji katika Jimbo la Kyerwa ni kubwa sana na wananchi wake hawapati maji, hata asilimia 20 haifiki: Je, Serikali inawaahidi wananchi wa Jimbo la Kyerwa kama alivyojibu, “upembuzi yakinifu unaoendelea utakapokamilika mwaka 2017/2018;” Serikali inaahidi kutenga pesa ya kutosha kwa ajili ya kukamilisha mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ili miradi hii iweze kusimamiwa vizuri, ni vizuri tukawa na wataalam. Wilaya yangu ya Kyerwa hatuna wataalam wa kutosha, lakini wataalam wenyewe hao waliopo hawana vitendea kazi kama gari na vifaa vingine. Je, Serikali ipo tayari kutuletea wataalam wa kutosha na vitendea kazi ili kazi isimamiwe vizuri?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza alitaka kujua kama katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tungeweza kuweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambao unaendelea kufanyiwa usanifu. Namwahidi kwamba kazi hiyo tutaifanya ili wananchi wetu kule waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la pili, kwamba Wilaya yake ina wataalam wachache; ni kweli wilaya nyingi hazina Wahandisi wala vifaa. Katika Program ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili, tumeweka bajeti kwa ajili ya kununua magari na vifaa muhimu, lakini pia tumeomba vibali kwa ajili ya kuajiri Wahandisi wa kutosha ili tuweze kuwapeleka kwenye wilaya mbalimbali.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lilivyo swali la msingi, kwa zao la kahawa na migomba kuna ugonjwa uitwao mnyauko kwa jina lingine unaitwa ugonjwa wa manjano. Ugonjwa huu umeshambulia migomba pamoja na kahawa. Je, Serikali imefanya utafiti upi ili kulipatia ufumbuzi zao hili lisije likapotea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kati ya magonjwa ambayo yameleta changamoto katika zao la migomba na kahawa ni ugonjwa wa mnyauko na kwa kipindi fulani umeleta matatizo makubwa sana katika Mkoa wa Kagera. Serikali ilichukua hatua mahsusi za kutafuta namna ya kuzuia ugonjwa huo na tayari kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kampeni kubwa iliyofanyika kuudhibiti, Serikali ilishaudhibiti na sasa hali siyo mbaya sana.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika utendaji wao wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Lwakajunju, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana zaidi ya miaka 15. Kwa maana hiyo tumewaahidi sana akina mama wa Karagwe na wananchi kuwatua ndoo kichwani kwa muda mrefu sana. Kama unavyojua akina mama ule muda ambao wanautumia kwenda kuchota maji umbali mrefu ndio muda huo huo ungeutumia kufanya kazi za maendeleo. Sasa swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri naomba unipe comfort, je,huu mradi wa Lwakajunju utatekelezwa lini? Ni lini wananchi wa Karagwe watapata hii huduma ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kibajeti za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, je, Wizara ipo tayari kushirikianan na Halmashauri kuhakikisha fedha ambapo tunahitaji kwa ajili ya kuchimba mabwawa katika Kata za Kanoni, Igulwa Ihanda, Chonyonyo na Nyakahanga zinapatikana ili wananchi wapate huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na Mradi wa Lwakajunju, ameomba apate confort na wananchi wake pia. Comfort ya kwanza ni kwamba mradi huu umetengewa dola milioni 30 kutokana na mkopo wa India, ni mkopo wenye uhakika na sasa hivi tupo kwenye taratibu za kukamilisha usanifu ili tutangaze tender. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba mradi huu unatekelezwa kwasababu tayari una fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili linalohusiana na ushirikiano na Halmashauri, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba tutaendelea kushiriakana na Halmashauri zote kuhakikisha kwamba miradi ya maji inatekelezwa, mabwawa, mserereko, visima na mingine ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Kuhusu suala la fedha upungufu wa fedha tutaenda nalo sabamba, lakini suala la msingi ni kuhakikishe kwamba wananchi wanapata maji.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kweli nasikitika sana kuona majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri. Hii ni mara yangu ya pili namwuliza hili swali. Mara ya kwanza alinijibu hapahapa Bungeni, akasema kabla ya mwezi wa Sita barabara hii itakuwa imeanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, anapotujibu siyo kuwajibu Wabunge kuwafurahisha, haya ni majibu ambayo tunakuja kuuliza kwa ajili ya wananchi wetu. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu ambayo ni ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; ni lini barabara hii ujenzi utaanza? Kwa sababu hii barabara ni ya muda mrefu tangu kipindi cha Mheshimiwa Rais Mkapa amestaafu; amekuja Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, sasa anakuja Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, je, imetengwa pesa kwa ajili ya ujenzi huu kuanza na wananchi wapewe fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie, tunapojibu hapa kwanza tunaonesha dhamira lakini pili, tunaonesha mipango ambayo ipo mbioni. Hatuwezi kuanza ujenzi wa barabara hii kabla ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika. Hakuna aina hiyo ya ujenzi ya barabara kuu na muhimu kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge atupe fursa tukamilishe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa mwaka huu tunakamilisha kazi hizo mbili. Kwa hiyo, hatujatenga fedha za kuweza kujenga, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi hizo mbili. Nimhakikishie kwamba mara baada ya kazi hizo mbili kukamilika, ujenzi utaanza, Serikali hii ya Awamu ya Tano inachosema inakusudia kukitekeleza na huwa inakitekeleza.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ya mwaka huu hakutupatia pesa kwa ajili ya mradi mkubwa ambao uko kwenye usanifu. Naomba awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa, mradi huu utakapokuwa umekamilika kwa ajili ya usanifu.
Je, yuko tayari kuhakikisha anawapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji safi na salama kwa sababu maji ni tatizo Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mheshimiwa Bilakwate ilipata shilingi milioni 200 na fedha hizo tayari zimeshatumika kuboresha chanzo cha maji kwenye kijiji kimoja eneo la mjini na tayari maji yanapatikana. Pia, kupitia vyanzo vingine vya Wizara yetu ya Maji na Umwagiliaji, tayari tumesaini mkataba wa usanifu ambao ukikamilika, umelenga kuvipatia vijiji zaidi 57 maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kesho tunawasilisha bajeti kwenye Bunge hili na katika bajeti hiyo tayari utaona wewe mwenyewe ni nini tumetenga ambacho kitahakikisha kwamba baada ya kukamilisha mradi wa usanifu, basi ujenzi utaanza bila wasiwasi wa aina yoyote.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa Redio ya Taifa haisikiki katika Wilaya ya Kyerwa na wananchi hao wanapofungua redio wanapata Redio ya Rwanda na Uganda kitu ambacho kimewafanya wananchi hawa kuonekana kama wametengwa kwa sababu hawawezi kupata taarifa ambazo ni muhimu zinazohusu Taifa lao.
Je Serikali haioni kuwa wananchi hawa wamekosa haki yao ya msingi ya kupata habari za Serikali hasa hasa kutoka kwa viongozi wao kama Mheshimiwa Rais anapokuwa anaongea na viongozi wengine? Hata mimi Mheshimiwa Mbunge ninapokuwa Bungeni nawawakilisha, hawa wananchi hawapati taarifa yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za dharura ili wananchi hawa waweze kupata taarifa ya Redio ya Taifa kwa sababu wanakosa hii haki ya msingi? Laini hata Televisheni ya Taifa haisikiki wala haionekani vizuri. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Innocent kwa maswali yake mawili mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba unipe ridhaa ya kuelezea suala hili kwa kirefu kidogo kwa sababu tuna Wilaya karibu 84 ambazo hazina usikivu wa redio katika nchi hii na suala hili limesababisha Wabunge wengi mara kwa mara kuuliza maswali yanayohusiana na usikivu wa redio yao ya Taifa. Kwa hiyo, naomba nitoe ufafanuzi kidogo ili kusudi tuweze kusaidiana kwa pamoja na kuhakikisha kwamba tatizo hili linapata ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwanza ametaka kujua kwamba Serikali haioni kwamba wananchi wanakosa haki yao ya msingi ya kusikiliza redio yao ya Taifa. Nitoe tu maelezo kwa kifupi kwamba kuna matatizo ambayo yanasababisha au tuseme kuna factors ambazo zinasababisha kuathiri usikivu wa redio katika maeneo mbali mbali. Kwanza, ukirudi nyuma tulikuwa tunatumia mitambo ya medium wave ambayo ilikuwa inaenea katika nchi nzima lakini kutokana na uchakavu wa mitambo hii na gharama kubwa ya kuinunua au kuikarabati imebidi sasa tuweke mitambo ya FM katika kila mkoa. Kwa hiyo, kila mkoa una mtambo wa FM.
Mheshimiwa Spika, sasa masuala ambayo yanaathiri usikivu kwanza ni capacity ya ule mtambo wenyewe lakini pia uwepo wa milima katika maeneo husika kwa mfano kama eneo la Mheshimiwa Innocent kuna milima mirefu ambayo mitambo hii inashindwa kuufikia. Suala lingine ambalo linaathiri usikivu ni ule uharibifu wa baadhi ya vifaa kama power amplifier ambao unatokana na matatizo mbalimbali kama vile radi au kukatika kwa umeme. Katika eneo la Mheshimiwa Innocent, kule Bukoba upo mtambo ambao kuna kifaa kimeharibika – MOSFET imeharibika na imekufa kabisa, kwa hiyo, usikivu umeathirika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo tumeamua kufanya, kwanza nimeshatoa maagizo ili kusudi wataalam waende katika maeneo yake, katika Wilaya ya Kyerwa ili kuweza kuona jinsi gani ya kutatua tatizo hili kwa sababu kwanza uwezekano upo wa kuweka booster, lakini pia waone kama wanaweza wakanunua kifaa kile ambacho kimeharibika.
Vilevile kuna utaratibu ambao sasa hivi TBC inafanya kuubadilisha mfumo wa satellite uplink ambayo iko Mikocheni, tunaamini kabisa kwamba hii satellite uplink ikirekebishwa ikawa ya kisasa zaidi tutaboresha usikivu kwa asilimia takribani 15 hivi.
Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao hayana usikivu, kufikia mwisho wa mwaka huu tunaamini kabisa hii satellite uplink inaweza ikawa imerekebishwa, kwa hiyo, usikivu utakapokuwa umeboreka katika maeneo yao watupe taarifa. Vilevile, kutokana na uharibifu wa vifaa katika vile vituo vyenyewe, yale maeneo ambayo yana usikivu wakati wowote watakapoona usikivu umesita katika maeneo yale watupe taarifa mapema ili kusudi wataalam wetu waweze kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tunafanya kwa sasa hivi ni huu utaratibu wa kuweka mitambo ya FM yaani kuongeza transmitter katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, nimetoa maagizo tayari kwamba wataalam wapite katika maeneo ya mipakani waone ni wapi panapostahili kuwekwa boosters lakini ni wapi pia ambao panastahili kuwekwa transmitters mpya. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu miradi hii ni ya muda mrefu na miundombinu yake inazidi kuharibika kama vile vifaa ambayo viko pale kuna kama nondo na vifaa vingine vinazidi kuharibika, kwa sababu Serikali imeshatenga pesa kwenye bajeti ya 2017/2018, kwa nini Serikali isichukue hatua za dharura kupeleka pesa hii ili iweze kukamilisha miradi hii kwa sababu ya umuhimu wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale kwenye miradi ile kuna walinzi ambao walikuwa wamewekwa pale, walinzi hao wametelekezwa muda mrefu na imefikia wakati hao walinzi wameondoka, pale hakuna walinzi. Serikali haioni pasipokuwa na walinzi inaweza ikasababisha vifaa vingine kuibiwa na kuharibu miundombinu ya mahali pale?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amezungumza kwamba miradi hii ni ya muda mrefu, lakini ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, nimuahidi tu kwamba nitafuatilia kuona kwamba kama tunaweza tukapata fedha hizo zilizotengwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na walinzi, niiombe Halmashauri ya Kyerwa kuhakikisha kwamba hata kwa kutumia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ni vema kuendelea kulinda miundombinu hii ambayo tayari ipo wakati tukiendelea kupata fedha kwa ajli ya kukamilisha miradi hiyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kama lilivyo swali la msingi, kwenye Jimbo langu la Kyerwa, wananchi wameanzisha vituo ambavyo wameshaanza ujenzi, wamefika kwenye kumalizia boma. Kwa mfano, kama Kata yangu ya Kimuri, kuna wananchi ambao wamejenga boma limefikia kwenye lenta na wameweza kujenga maboma zaidi ya kumi. Maboma haya yamekaa karibu miaka saba. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha maboma haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nikupe taarifa, Mheshimiwa Bilakwate anapoishi kwake pale wakati mwingine ninapofika pale hata mtandao wa simu anapata nchi ya Rwanda. Bahati mbaya hana Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya suala hili la maboma, kutokana na ombi lake tumeamua kujenga theater sasa na sehemu ya kupasulia wagonjwa pamoja na kupata huduma nyingine katika Kituo chake cha Afya cha Mulongo. Tumefanya hivi ili eneo lake liweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumefanya assessment ya maboma yote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jinsi gani tutayamalizia, yale ya Vituo vya Afya na Zahanati, takriban shilingi bilioni 950 zinahitajika. Katika mwaka huu wa bajeti tumeshatenga karibu shilingi bilioni takriban 95. Lengo kubwa ni kuhakikisha tunamalizia hivi viporo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Local Government Capital Development Grant, tumetenga karibu shilingi bilioni 251, karibu one third ya fedha hizo zinakwenda katika suala zima la umaliziaji wa maboma. Kwa hiyo, nawaagiza Wakurugenzi wote wakiwemo na wa Halmashauri yake; inapofika ile fedha, naomba tuweke mgawanyo mzuri wa jinsi gani tutakavyomalizia maboma haya na siyo ya afya peke yake, hata katika Sekta ya Elimu. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake kuhakikisha inaboresha zao la kahawa.
Mheshimiwa Spika, kwenye zao la kahawa kulikuwa na kodi nyingi na Serikali imejitahidi kuondoa kodi 17, lakini hizi kodi hazimnufaishi mkulima moja kwa moja zinawalenga wafanyabiasha. Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa hizi kodi ambazo zinamgusa moja kwa moja mkulima ili aweze kupata bei nzuri ya kahawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi mkulima anapoanza kulima, kupalilia mpaka kuvuna hasaidiwi kitu chochote, mwisho anaanza kukatwa kodi na mambo mengine. Je, Serikali imejipanga vipi kumsaidia huyu mkulima ili iweke miundombinu mizuri kuanzia anapolima akiwa shambani mpaka kwenye mnada? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana zao hili la kahawa ambalo linalimwa pia kwa wingi katika Jimbo lake lile la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, katika swali lake la kwanza, ni kweli kwamba Serikali tumeliona hili na ndiyo maana tumeanzisha ule utaratibu wa kuuza kahawa mnadani moja kwa moja kupitia Vyama vyetu vya Ushirika. Vilevile Serikali tumepunguza tozo ya mauzo ya mazao kupitia cess au farm gate price kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.
Mheshimiwa Spika, swali lake lile la pili ni kwamba zao la kahawa linategemea sana na muonjo ule wa kahawa. Kwa maana hiyo, katika kuweka ubora wa miundombinu pia na ubora wa zao lenyewe, ni kwamba kulekule shambani wakulima wanapaswa kutumia zile CPU kwa ajili ya kuchakata zile kahawa kwa sababu kahawa mbichi hairuhusiwi, hivyo iweze kuanikwa na kusafishwa vizuri, kabla haijapelekwa kukobolewa kule kwenye curing.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Sasa hivi ni kipindi cha msimu wa kahawa. Vyama vya Ushirika vimeshindwa kuwahudumia wananchi kupata maturubai ya kuvunia Kahawa na hii kahawa inaendelea kukaukia Mashambani, wananchi wamekosa msaada. Hata hivyo, hata wale ambao wamepata maturubai, maturubai haya hayana viwango yanachanika hovyo. Ni hatua zipi za dharura ambazo zitachukuliwa ili kunusuru zao hili na mkulima aweze kulifaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na matatizo sana katika suala zima la Vyama vyetu vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika na ndiyo maana kama Serikali tunasema kwamba, tuko katika mikakati ya kuhakikisha tunafufua, tunaimarisha na kuboresha Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kutokana na swali lake hili la msingi katika Jimbo lake la Kyerwa, kwamba mpaka sasa hivi kunasuasua, naomba nichukue fursa hii kuagiza Chama Kikuu cha Ushirika cha Kyerwa kuanzia leo wahakikishe kabisa kwamba, zoezi zima la mazao ya kahawa katika Jimbo la Kyerwa wanafanya kazi yao kwa ubunifu, wanafanya kazi yao kwa utii, wanafanyakazi yao kwa weledi, wanafanyakazi yao kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, lakini na mimi kama Naibu Waziri nikitoka hapa Bungeni ninaahidi kuwapigia Vyama Vikuu vya Ushirika vile AMCOS pale Kyerwa nikishirikiana na Mrajisi wangu kuhakikisha kwamba jambo hili halijirudii na linaweza kufanikiwa kwa uhakika. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya umeme kwa Kyerwa ni makubwa sana, yako maeneo mengi ambayo hayafikiwa kabisa kama Kata ya Bugomola, Kibale, Businde na Bugara na maeneo mengine mengi hayajafikiwa. Ni kwa nini Wizara isiruhusu TANESCO, REA wanapomaliza kupitisha line kuu, Wizara isiruhusu TANESCO wakaanza kuwafungia umeme wananchi ambao wanahitaji umeme?
Swali la pili, REA Awamu ya Pili ambayo kwetu Kyerwa ni REA Awamu ya Kwanza kwa sababu ndipo umeme ulipopelekwa huyu Mkandarasi amesuasua sana mpaka sasa ameshindwa maeneo mengi, wako wananchi wengi ambao wamelipia mpaka sasa hawajafungiwa miaka miwili.
Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kwa Mkandarasi huyu ambaye inaonekana ameshindwa kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate naye pia nimpongeze kwa namna ambavyo amefuatilia masuala la nishati katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza lilijielekeza kwenye mahitaji ya umeme, kwa nini TANESCO isiendelee kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo wanaopenda umeme. Napenda nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli katika Mkoa wa Kagera, Mkoa ambao pia ulikuwa haujaunganishwa kwenye gridi ya Taifa tumeunganisha Wilaya za Ngara mpaka Muleba na tunatarajia kukamilisha mpaka Bukoba Mjini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uunganishwaji wa gridi ya Taifa katika maeneo hayo kumejitokeza mahitaji na tumeendelea kuwapa maelekezo TANESCO kwamba inapotokea fursa siyo lazima kusubiri miradi ya REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, kama kweli wapo wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wanahitaji umeme na wao hoja siyo kusubiri umeme wa REA ambapo una bei nafuu wako tayari kulipia hata gharama za kuunganishwa umeme na TANESCO, naielekeza TANESCO ifanye upembuzi yakinifu na iwapelekee umeme wananchi hao kwasababu wao kwao umeme hawaangalii hoja kwamba ni wa REA au ni umeme kupitia TANESCO.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, natambua Kata alizozitaja Mheshimiwa na ni kweli mpaka sasa hivi hazijasambaziwa umeme. Natambua uwepo wa Mkandarasi Makuroi katika Mkoa wa Kagera, lakini ni ukweli nakiri kwamba katika Wilaya zingine mkandarasi yule hajafanya vizuri, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulimuita Makuroi kwa sababu anafanya pia na Mkoa wa Rukwa, na mimi nilipata fursa ya kutembelea Mkoa wa Rukwa nikaona ni namna gani anavyolegalega lakini kwa sasa ameshaagiza magari na nimeyathibitisha ana magari mengi tu ya kusambaza nguzo na tulithibisha order ambazo amezitoa katika viwanda mbalimbali vya nguzo vya Mkoa wa Iringa, kwa sasa hivi kwa kweli tumemuelekeza na wakandarasi wote wa miradi hii kwamba lazima kila Wilaya kuwe na genge lake na wasijielekeze sehemu moja.
Kwa hiyo, naomba nimthibitishe Mheshimiwa Mbunge baada ya jibu au baada ya kikao hiki tukutane ili tuendelee na mikakati yakuwasimamia wakandarasi wote. Ahsante.
MHE. INNOCENT L. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa kuleta maji kwenye Mji wa Lubwera pale Makao Makuu ya Wilaya, lakini maji yale yaliyoletwa hayawatoshelezi wananchi. Naiuliza Serikali,ni lini itapanua ule mradi ili uweze kuwatosheleza wananchi kwa sababu ule mji unapanuka sana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi anavyofuatilia matatizo ya maji katika jimbo lake, jimbo ambalo lina vyanzo vingi vya maji, lakini lilikuwa halina maji ambayo yalikuwa yamewafikia wananchi; na jana alikuja ofisini kwangu kuendelea kufuatilia huo mradi wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo Lubwela tulichimba visima viwili, lakini mtandao umekuwa mkubwa, maji hayatoshi. Namwongezea kisima kimoja, tutaanza kuchimba mwezi huu pamoja na kujenga tenki, lakini hiyo ni sambamba na kupitia sasa huo mradi mkubwa ambao tayari usanifu wake unakamilika ambao utapeleka maji kwenye vijiji 57 katika jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tu wananchi wa Mheshimiwa Mbunge kwamba, yeye yuko makini, atahakikisha kwamba, wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, barabara inayotoka Mgakorongo – Kigalama – Bugomola - Mlongo ni barabara muhimu na inaunganisha nchi jirani pamoja na Wilaya jirani ya Karagwe. Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne, lakini na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi itajengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini barabara hii itajengwa na wananchi wakalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, maarufu kama Mchungaji, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mgakorongo – Kigalama – Mlongo ni barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na Uganda na inahudumiwa na Wakala wetu wa Barabara TANROADS. Katika sera ni kati ya barabara ambazo zina kipaumbele katika kutengenezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo tumeongelea hizi barabara, sijafika Kagera kwa ziara lakini nazitambua kwa sababu tumekuwa tukibadilishana mawazo. Niwapongeze sana wananchi wa Kyerwa kwa kweli hawakukosea kumchagua Mheshimiwa Bilakwate kwa sababu kazi nzuri anaifanya. Jukumu ambalo wamempa analifanya kisawasawa na sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba hatuwaangushi wananchi wa Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu barabara hii urefu wake ni takribani kilometa 79 hivi, ambapo itakwenda kuungana na barabara kubwa ambayo inakwenda kuunganisha nchi yetu pia na upande ule wa Mtukula. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa barabara hii, inapita maeneo yenye uzalishaji mkubwa na itakuwa na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ipo kwenye mpango kwa kweli, labda Mheshimiwa Bilakwate baada ya hapa tukae tuzungumze ili tuangalie kwa upana kwenye strategic plan tumepanga namna gani hatua kwa hatua kuikamilisha barabara hii. Pia tumetenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inaimarishwa ili dhana nzima ya kuhakikisha tunatekeleza sera yetu ya kuunganisha mikoa yetu na nchi za jirani inakamilika na wananchi wanapata huduma na kwa kweli inachangia pia katika uchumi wa nchi yetu.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wamekuwa wakishiriki huduma za afya kwa kujenga maboma. Kwenye Kata yangu ya Kimuri, wananchi wameweza kujenga vyumba zaidi ya 20 lakini vyumba hivi vimekaa zaidi ya miaka 10 Serikali haijaweza kukamilisha. Je, Mheshimiwa Waziri wako tayari kukamilisha hivyo vyumba ili wananchi waweze kupatiwa huduma bora ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo Serikali tunaenda kujenga vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya ni pamoja na Mkoa wa Kagera. Naamini Mheshimiwa Mbunge naye ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge wanufaika katika Serikali ya Awamu ya Tano ambao wanaenda kupata huduma hii ambayo haikuwepo kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la kukamilisha hivyo vyumba 20 ambavyo anavisema, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, wanasema kuona ni kusadiki. Ni vizuri pale ambapo tutapata nafasi ya kwenda kutazama ili tujue uhalisia na bajeti kiasi gani itahitajika kumalizia huo ujenzi ili nguvu ya wananchi isije ikapotea, kama Serikali tutakuwa tupo tayari.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana kwenye msimu wa kahawa, Serikali ilitangaza bei elekezi Sh.1,400 lakini wakulima wamelipwa Sh.1,106. Ni kwa nini wamelipwa hiyo badala ya bei elekezi iliyoelekezwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafsi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kupitia Bodi ya Kahawa, mwezi Julai mwaka jana ilitangaza bei elekezi ya Sh.1,400 ya kahawa. Bei elekezi ni bei ya chini anayotakiwa kulipa mkulima maana yake kama tungeruhusu wafanyabiashara binafsi kununua, lakini kahawa hii haikununuliwa na wafanyabiashara binafsi, ni wakulima wenyewe kupitia Vyama vyao vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika waliamua kwenda kuuza kahawa yao kule mnadani Moshi. Kwa hiyo kama wakulima wenyewe kupitia vyama vyao ndiyo waliamua kwenda kuuza kule baada ya kukusanya kahawa yao, kwa hiyo wanakwenda kulipwa kutokana na bei waliyouza kwenye mnada, siyo bei iliyotangazwa ile elekezi kwa sababu hakuna mfanyabiashara binafsi aliyenunua kwa wakulima kule Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hivi Vyama vya Ushirika siyo wafanyabiashara bali wanakusanya kwa niaba ya wanachama wenzao, kwa niaba ya wakulima wenzao baadaye wanakwenda kuuza kwa pamoja kule Moshi na ndiyo maana kwamba sasa hivi kutokana na myumbo wa bei mwaka jana, bei ilishuka kwenye soko la dunia na ikaathiri mnadani pale Moshi na ndiyo maana sasa bei hiyo wanakwenda kulipwa kwa kuzingatia bei iliyouzwa hiyo kahawa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kututengea hizi pesa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, lakini kipekee nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Jafo kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikimsumbua kuhusiana na Vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, kulingana na jiografia ya Wilaya yangu, ninaomba kuuliza swali. Kwa kuwa tuna vituo vitatu kwenye Tarafa nne na kwenye Kata 24: Serikali iko tayari kututengea kituo kingine kimoja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kyerwa tuna upungufu mkubwa wa watumishi. Kwenye kituo kingine unakuta kuna watumishi wawili kwenye Zahanati moja: Je, Serikali iko tayari kututengea watumishi wa kutosha ili wananchi waweze kupata huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Katika hali ya kawaida, mtu anayeshukuru tafsiri yake ni kwamba anaomba kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga Vituo vya Afya kwa kadiri nafasi ya kibajeti itakavyoruhusu. Jiografia ya Kyerwa hakika ni jiografia ambayo ina utata mkubwa, Jimbo ni kubwa. Naomba aendelee kuiamini Serikali, kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu na tutakavyokuwa tunaendelea kujenga Vituo vya Afya, naye tutamkumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna swali lake la pili; anaomba kuongeza idadi ya watumishi ili waweze kutoa huduma ambayo inastahili kwa wananchi wake. Sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba kibali cha kuweza kupata nafasi za kuajiri. Kwa kadiri nafasi zitakavyokuwa zimepatikana, hakika katika usambazaji tutahakikisha maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa yanazingatiwa. Naamini na eneo lake ni miongoni mwa maeneo hayo. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ninaomba kutoa maelezo ya nyongeza kuhusu uhaba wa watumishi, hasa afya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali inafanya jitihada za kujenga Vituo vya Afya na Zahanati nchi nzima. Tunakiri kwamba watumishi hawatoshi, ndiyo maana kwa kushirikiana na TAMISEMI tunafanya utaratibu wa kuongeza. Nimesimama hapa kueleza kwamba, sisi upande wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora tutaweka kwanza kipaumbele katika Zahanati na Vituo vya Afya vipya ambavyo havijaanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Viongozi wa Mikoa, Waheshimiwa Wabunge mkiwasimamia, kuhakikisha wanapoleta maombi watuletee kwamba Zahanati mpya inahitaji watumishi kadhaa, Kituo cha Afya kipya kinahitaji watumishi kadhaa. Pamoja na uhaba uliopo, lengo ni kwamba Vituo vyote vya Afya na Zahanati zote mpya zifunguliwe mara moja, ndiyo tutawapa kipaumbele, kwa sababu sehemu nyingine huduma bado zitaendelea kutolewa japo kwa upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda kwa ruhusa yako pia, nijibu suala la uhaba wa Walimu. Sasa hivi baada ya kufungua mwaka mpya huu wa masomo, Walimu wengi wamestaafu mwaka 2018, wengine wamefariki. Sisi upande wa Utumishi tutaanza kwanza kujaza idadi ya Walimu waliostaafu mwaka 2018, ili tuwe na kiwango cha Walimu kama waliokuwepo mwaka 2018, baada ya hapo tutaendelea na zoezi la kuajiri Walimu wapya.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa hatua ambayo imefikia kwenye usanifu, lakini niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sababu ya hali ngumu kwa wananchi wa Jimbo la Kyerwa hasa hasa kwenye vijiji ambavyo vinaguswa na mradi huu, je, Serikali iko tayari kwenye bajeti ya 2019/2020 kutenga angalau kiasi kidogo ili mradi huu uweze kuanza wakati Serikali inaendelea kutafuta hela kubwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna miradi ambayo iko katika Kata ya Mabira, Lukulaijo na kwenye Kijiji cha Kageni miradi hii imeshaanza lakini wakandarasi wamekuwa wakienda kwa kusuasua kwa sababu bado certificate zao hazijalipwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa wakandarasi hawa ili waweze kukamilisha hii miradi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Bilakwate, mimi binafsi nilipata nafasi ya kwenda katika jimbo lake, nimeona kazi kubwa anayoifanya katika jimbo lake pamoja na wananchi wake. Sasa nataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kwa wananchi wa Kyerwa kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Spika, tumefanya tathmini ule mradi ni fedha nyingi sana, lakini tunatambua maji ni uhai na hayana mbadala. Sasa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ukikosa ziwa la mama, la ngombe unanyonya, sisi tupo tayari kufanya njia mbadala katika kuhakikisha wananchi wake wa Kyerwa wanapata maji safi na salama ili waweze kuishi katika eneo lake. Kikubwa na cha msingi kabisa nimwombe kutokana na kuna miradi ambayo inaendelea katika jimbo lake, tukutane baada ya saa saba ili tuangalie ni namna gani tunamsaidia katika kuhakikisha fedha zile tunazilipa wananchi wake waweze kupata maji safi.