Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Innocent Sebba Bilakwate (16 total)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Ujenzi wa masoko ya Kimataifa yaliyokuwa yakijengwa huko Nkwenda na Murongo yamesimama kwa muda mrefu sana na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa walitegemea masoko hayo kwa ajili ya kuuzia mazao yao mbalimbali:-
Je, ni nini kimesababisha kusitishwa kwa ujenzi wa masoko hayo? Na ni lini sasa ujenzi utafufuliwa na kukamilishwa ili kutoa fursa za kufanya biashara na kwa majirani zetu pia?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Omwanawumkazi, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya masoko nchini hususan masoko ya mipakani, yakiwemo masoko ya Nkwenda na Murongo ni moja ya maeneo ya kipaumbele cha Serikali yetu. Masoko hayo yakikamilika yatakuwa ni kichocheo kwa wakulima kuzalisha zaidi na wafanyabiashara kuuza kwa uhakika, kutokana na kunufaika na soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo ni kati ya masoko matano ambayo yalikuwa yanajengwa kwa kutumia fedha za mradi wa wawekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project - DASIP).
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko mengine yaliyonufaika na mradi huo ni Kabanga - Ngara, Lemagwe - Tarime na Busoka - Kahama. Ujenzi wa Masoko hayo ulifikia kiwango cha kati ya asilimia 45 mpaka 65 kwa ujenzi na kusimama baada ya mradi wa DASIP I kufikia ukomo wake mwaka 2013 na Benki ya Maendeleo ya Afrika iliyokuwa ikifadhili ujenzi huo kusitisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo jitihada zinafanyika ili kuendelea na mradi wa DASIP awamu ya pili ili pamoja na mambo mengine tuweze kukamilisha ujenzi wa masoko yote yaliyokusudiwa yakiwemo masoko ya Nkwenda na Murongo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo vya ndani na wahisani wengine ili kumalizia ujenzi wa masoko hayo muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Kazi ya kuendeleza ujenzi na kukamilisha masoko hayo itaanza pindi Serikali itakapopata pesa hizo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Barabara ya Murushaka ni kiungo muhimu kwa Karagwe na Kyerwa na ni barabara muhimu sana kiuchumi, lakini barabara hiyo ni mbovu sana wala haipitiki kabisa:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutengeneza barabara hiyo ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Kyerwa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa lami barabara hiyo kwa sababu zaidi ya magari asilimia 90 yanayotoka Uganda na Kyerwa hutumia barabara hiyo iliyosahaulika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayozungumziwa ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Kagera inayoitwa Bugene au Omurushaka hadi Kaisho hadi Murongo, na ni ya changarawe, yenye jumla ya kilometa 112 na inapitika wakati wote licha ya sehemu chache korofi wakati wa mvua nyingi. Barabara hii inaunganisha Wilaya za Karagwe na Kyerwa na nchi jirani ya Uganda eneo la Murongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii imekuwa ikitenga fedha kila mwaka ili kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali pamoja na kuimarisha mlima mkali wa Rwabunuka ili uweze kupitika wakati wote, ambapo hadi sasa jumla ya kilometa 10 zimeshawekwa lami na kupunguza usumbufu kwa magari ya mizigo na abiria yanayopita katika mlima huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2015/2016, matengenezo ya barabara yanayojumuisha kuchonga barabara, kuweka changarawe sehemu korofi na kuimarisha mifereji yamefanyika ambapo tayari kilometa 40 zimeshawekwa katika hali nzuri na kilometa moja zaidi ya lami itajengwa katika mlima Rwabunuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna magari mengi katika barabara hii ya Bugene – Kaisho hadi Murongo. Serikali kulingana na vipaumbele vyake na umuhimu wa kila barabara inaendelea kutafuta fedha ili kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hii ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, Barabara Kuu ya Omugakorongo – Kigarama – Murongo yenye urefu wa kilometa 105 nayo imepewa kipaumbele, kwani hivi sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii utarahisisha usafiri wa bidhaa, mazao na abiria kati ya nchi ya Uganda na Wilaya za Kyerwa, Karagwe na pia kupunguza wingi wa magari katika barabara ya Bugene yaani Omurushaka – Kaisho hadi Murongo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Wananchi wengi katika Jimbo la Kyerwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama, jambo linalorudisha nyuma shughuli za maendeleo:-
Je, ni lini Serikali itatumia maji ya Mto Kagera kuwapatia wananchi maji safi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mfupi, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 200 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Miji ya Rubwera na Rwenkorongo ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kyerwa. Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ununuzi wa mabomba, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba za kusambaza maji pamoja na viungo vyake; kukarabati tanki moja na ununuzi wa pampu mbili za kuvuta na kusukuma maji toka kwenye visima virefu viwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu, kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga kukamilisha mradi mkubwa wa maji kwa ajili ya Mji wa Kyerwa pamoja na vijiji vinavyozunguka. Taarifa ya upembuzi yakinifu itakapokamilika, ndipo tutawezesha kufanya maamuzi iwapo Mto Kagera ndiyo utumike kama chanzo au kama kuna vyanzo mbadala ambavyo vinaweza kutumika ambapo uzalishaji wa maji utakuwa wa gharama nafuu zaidi na endelevu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Serikali imeahidi kujenga mabwawa ya maji katika Kata za Kanoni, Igarwa, Ihanda na Chenyoyo ili kuwapatia wananchi wa kata hizo maji.
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza kazi hiyo?
(b) Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa vijiji vya Kafunjo, Kijumbura na Bweranyange kwamba mradi wa maji wa Lyakajunju utakapotekelezwa utawaachia wananchi miundombinu ya maji ili kuwanusuru kuliwa na mamba wanapofuata maji ziwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Jimbo la Karagwe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza ujenzi wa mabwawa, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeziagiza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo yanayoweza kujengwa mabwawa na kutenga fedha kwenye bajeti zao za kujenga angalau bwawa moja kila mwaka. Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeweza kuainisha maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa kama ifuatavyo:-
Kata ya Kanoni eneo la Kabare na Omukigongo, Kata ya Igurwa eneo la Omukalinzi (Kabulala A) na Kata ya Nyakahanga eneo la Kashanda (Karazi). Mabwawa katika maeneo hayo yatajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha baada ya kazi za usanifu, kuandaa michoro, kuainisha gharama na nyaraka za zabuni kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo katika hatua za usanifu wa kina wa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Bwawa la Lwakajunju ambao kutekelezwa kwake kutavipatia huduma ya maji vijiji vyote vitakavyopitiwa na bomba kuu la maji katika umbali usiozidi kilometa 12 kutoka eneo la bomba kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya usanifu kukamilika itaainisha iwapo vijiji vya Kafunjo, Kijumbura na Bweranyange vitakuwa ndani ya kilometa 12 kutoka eneo la Bomba Kuu. Mradi huo utavipatia maji na endapo havitakuwepo basi Halmashauri iweke kwenye vipaumbele vijiji hivyo katika bajeti inayotengwa na Wizara kila mwaka.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mgakorongo, Kigarama mpaka Murongo iliwekwa kwenye ilani kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi waliokuwa ndani ya mradi waliowekewa alama ya ‘X’ wanashindwa kuendeleza maeneo yao wakisubiri fidia zaidi ya miaka mitano sasa:-
(a) Je, ni lini wananchi hawa watapewa fidia ili waendelee na mambo ya kimaendeleo?
(b) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba, Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Omugakorongo – Kigarama hadi Murongo ni barabara kuu inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Kagera na ina jumla ya kilometa 111. Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii ndiyo maana imeiweka kwenye mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami. Hivi sasa upembuzi yakinifu wa barabara hii umekamilika, kazi inayoendelea ni usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea na uhakiki wa fidia ya mali zitakazoathiriwa na mradi kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 watalipa fidia mara zoezi la uhakiki litakapokamilika na Wizara yangu itahakikisha kuwa taratibu zote za malipo ya fidia na sheria zinafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kazi za ujenzi wa barabara ya Omugakorongo – Kigarama hadi Murongo zitaanza mara baada ya usanifu wa kina kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio ya Taifa (TBC Taifa) ili kujua yanayoendelea katika nchi yao kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kubadilisha teknolojia ya habari, badala yake sasa wanasikiliza redio za Rwanda na Uganda.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kyerwa iko katika Mkoa wa Kagera ambapo matangazo ya redio yanapatikana kupitia mtambo wa TBC ulioko katika Manispaa ya Bukoba. Mtambo huu unasafirisha mawimbi ya redio katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huu wa Kagera ikiwemo wananchi wa Jimbo la Kyerwa. Usikivu wa TBC katika eneo hili umeshuka na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa matangazo ya redio ikiwemo Jimbo la Kyerwa. Ili kuimarisha usikivu katika maeneo ya mipakani ikiwemo Wilaya ya Kyerwa, mpango wa TBC ni kujenga mitambo ya FM katika maeneo haya ili wananchi wake waweze kupata matangazo kutoka redio yao ya Taifa TBC.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa na kama ilivyobainishwa katika hotuba ya Bajeti ya Wizara ya mwaka 2017/2018 TBC imeanza kutekeleza mpango huu katika Wilaya na maeneo ya Kibondo, Nyasa, Longido, Tarime na Rombo na itaendelea katika wilaya nyingine ikiwemo Wilaya ya Kyerwa kadri bajeti inavyoendelea kuimarika.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kukamilisha ujenzi wa masoko ya kimataifa ya Nkwenda na Murongo ambayo yamekaa miaka mingi bila kukamilishwa wakati yangekamilishwa yangewapatia soko la uhakika wananchi wa Kyerwa na Mkoa mzima wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Masoko ya Kimkakati ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo ni miongoni mwa masoko matano yaliyokuwa yanajengwa kama sehemu ya utekelezaji wa Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) kupitia mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo ngazi ya Wilaya (District Agriculture Sector Investment Project – DASIP).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa masoko hayo mpaka sasa umekamilika kwa hatua za awali. Katika soko la Nkwenda ujenzi umekamilika kwa asilimia 25 hadi 30 na soko la Murongo ujenzi umekamilika kwa asilimia 40 hadi 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa masoko haya ulisimama baada ya mradi wa DASIP kufikia ukomo wake mwaka 2013 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iliyokuwa ikifadhili ujenzi huo kusitisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa masoko hayo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inayoratibu Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo katika bajeti ya mwaka wa 2017/2018, imetenga Sh. 385,914,778 kwa soko la Nkwenda na Sh.561,232,364 kwa soko la Murongo. Ujenzi wa masoko hayo utaendelea pindi fedha hizo zitakapotolewa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Serikali imezuia biashara ya BUTURA na wanunuzi wa kahawa kwa watu binafsi (moja kwa moja kwa wakulima) na kuagiza yote iuzwe kwa Vyama vya Msingi wakati vyama kama KDCU vilishindwa kuwapa bei nzuri wakulima:-
• Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inakuja na mbinu mpya ya kuwapa bei nzuri wakulima wa kahawa?
• Je, ni hatua zipi zimechukuliwa haraka ili kuhakikisha wale walioua Vyama vya Ushirika wanashtakiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imejipanga kuhakikisha kuwa biashara ya zao la kahawa itaendeshwa na kusimamiwa na Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali chini ya mfumo wa stakabadhi za ghala. Aidha, kupitia mfumo huu, kahawa ya mkulima itakusanywa na kukobolewa na kisha kuuzwa mnadani chini ya usimamizi wa Vyama Vikuu vya Ushirika, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bodi ya Kahawa na Bodi ya Stabadhi za Ghala ambapo kahawa itanunuliwa kwa bei ya ushindani na yenye tija itakayowezesha mkulima kulipwa malipo ya pili na ziada.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), imeendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara na kaguzi za kiuchunguzi katika vyama vya ushirika na kuchukua hatua mbalimbali za kisheria pindi inapobainika kuwepo kwa ubadhirifu. Aidha, wahusika wa ubadhirifu wamekuwa wakichukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na Bodi za Uongozi na Menejimenti zake kuondolewa madarakani na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ambapo baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hushtakiwa Mahakamani na kuwataka kurejesha fedha walizoiba.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafungua Ofisi za TANESCO Wilayani Kyerwa ili kuwafikishia karibu wananchi huduma zitolewazo na TANESCO, kama vile kununua umeme, kubadilisha mita na huduma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kuboresha huduma kwa wateja Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupitia bajeti ya mwaka 2018/2019 inajenga Ofisi ya TANESCO Wilaya ya Kyerwa katika Kiwanja Na. 210 C, kilichopo eneo la Rwenkorongo. Kazi ya ujenzi wa ofisi hiyo inaendelea vizuri na inatarajia kukamika mwezi Januari, 2019.
Mheshimiwa Spika, katika hatua za muda mfupi TANESCO imefungua ofisi katika Mji wa Nkwenda, kwa ajili ya kuwahudumia wateja wakati kazi ya ujenzi wa ofisi mpya inaendelea. Kwa sasa Meneja wa TANESCO Wilaya ya Misenyi pamoja watumishi wengine watatu, wanaendelea kutoa huduma kwa wateja wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kyerwa kupitia ofisi hiyo. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Wilaya ya Kyerwa ina Vituo vitatu vya Afya, lakini kituo kimoja ndicho kina uhakika wa kutoa huduma, vilevile kuna uhaba wa watumishi ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na nyumba za watumishi ili kutekeleza Ilani ya CCM na kuondoa adha wanayoipata akina mama, watoto na wananchi wengine kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ina jumla ya Vituo vya Huduma za Afya 32 vinavyohudumua watu takribani 394,375. Kati ya vituo hivyo, kuna Vituo vya Afya vitatu, vyote vikiwa vya Serikali, Zahanati ziko 28; 23 za Serikali na tano ni za watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ni miongoni mwa Halmashauri 67 nchini zilizopatiwa shilingi bilioni 1.5 kila moja kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Mpaka sasa hatua za awali za ujenzi zinaendelea na ujenzi wa awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019. Vilevile Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Vituo vya Afya Murongo na Kamuli katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ambapo mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 98.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Baada ya Serikali kukamilisha usanifu wa mradi wa maji wa vijiji 57 kwenye kata 15 Wilayani Kyerwa:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwenye Bajeti ya 2019/2020 ili miradi hiyo ianze kutekeleza Ilani ya CCM ya kumtua mama ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa vijiji 57 kwenye kata 15, Wilayani Kyerwa ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maji ambayo Serikali ina mpango wa kuitekeleza ili kuhudumia wananchi wengi. Mradi huu unalenga kuhudumia watu takriban 282,000 waishio kwenye vijiji hivyo utakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, usanifu wa mradi huu umekamilika na imeonekana kuhitaji kiasi kikubwa cha fedha. Hivyo, Serikali inafanya jitihada za kutafuta fedha za kutekeleza mradi huu wa kimkakati (Strategic Water Project).
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Kahawa ni miongoni mwa zao la Mkakati na Biashara lakini bei ya zao hilo imekuwa ya kusuasua:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha zao hilo linaongeza kipato cha Taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Seba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuhakikisha zao la kahawa linapata soko la uhakika na lenye tija kwa wakulima. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya pembejeo; Kuongeza uzalishaji kwa upanuzi wa mashamba ya wakulima; Kuzalisha miche bora ya kahawa yenye kuhimili ukame, magonjwa na wadudu ili kuongeza tija kwa wakulima; na Kuhamasisha matumizi ya kanuni bora za kilimo kupitia Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mikakati hiyo, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la kahawa kwa kufanya utafiti wa mahitaji ya soko, kuimarisha Vyama vya Ushirika, kusimamia mikataba baina ya wanunuzi na wakulima na kuhamasisha uzalishaji wa ufanisi wenye tija ili kuweza kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa mwaka 2019/2020, mfumo wa mauzo ya kahawa moja kwa moja (direct export) umetumika katika mauzo ya kahawa katika Mkoa wa Kagera ikiwemo Jimbo la Kyerwa ambapo asilimia 72.92 ya kilo 22,000,000 ya kahawa yote iliyozalishwa katika Mkoa wa Kagera imeuzwa kwa mfumo huo. Aidha, mfumo wa minada katika kanda pia umetumika ikiwa ni pamoja na kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuuza kahawa kwa mikataba mapema kabla ya mauzo halisi kufanyika. Hadi kufikia mwisho wa msimu wa 2018/2019 kiasi cha tani 66,646 za kahawa kiliuzwa ikiwa ni asilimia 102.86 ya makisio ya uzalishaji ya tani 65,000 na kuingizia Taifa Dola za Marekani milioni 123. Kati ya tani hizo zilizouzwa, tani 41,971 zimeuzwa kupitia minada ya kahawa na tani 24,575 zimeuzwa katika soko la moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawahakikishia wakulima wa kahawa nchini kuwa mifumo ya mauzo ya kahawa moja kwa moja na minada ya kahawa katika Kanda za Mbeya na Songwe; Ruvuma na Njombe; Kagera na Moshi iliyotumika msimu wa 2019/2020, itaendelea kutumika nchini. Kutumika kwa mifumo hiyo kutasaidia kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Serikali inavihimiza Vyama vya Ushirika na wakulima wa kahawa nchini kuzalisha kahawa kwa wingi yenye ubora kwa kuzingatia ubora unaokubalika sokoni ili wapate bei nzuri.
INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Usanifu na upembuzi wa kina wa mradi wa maji wa vijiji 57 Wilayani Kyerwa umekamilika muda mrefu. Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza ili wananchi wa Kyerwa waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nitoe pole kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa kuondokewa na kipenzi chetu aliyekuwa Mbunge Mheshimiwa Omary Nundu Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema roho yake peponi.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wialya ya Kyerwa ni mojawapo ya wilaya zinazounda Mkoa wa Kagera na kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imefika asilimia 45.6 kutokana na asilimia ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kuwa Serikali iliamua kubuni mradi mkubwa utakaoweza kuhudumia wananchi zaidi ya 232,000 walioko kwenye vijiji 57 kutoka kwenye chanzo kimoja ambacho ni Ziwa Rushwa kando na Mto Kagera. Kazi hii alipewa mtaalam mshauri Don Consult na aliweza kukamilisha kazi hiyo mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya usanifu pamoja na makisio ua utekelezaji wa mradi huo ni shilingi bilioni 144.

Baada ya kupitia gharama hizo, Serikali imeamua kupitia upya usanifu huo ili kujiridhisha na mfumo wa ujenzi uliopendekezwa na gharama za ujenzi wa mradi huo. Serikali imeamua kuchukua hatua na uamuzi huo kutokana na uzoefu ulipatikana kuwa baadhi ya miradi mikubwa imekuwa na gharama kubwa bila kuzingatia uhalisia wa teknolojia inayopendekezwa na pia uwezo wa uendeshaji wa jamii husika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wakati taratibu hizo zinaendelea, Serikali kwa upande wake inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kadri mapitio ya usanifu yatakavyoonesha na utatekelezwa kwa awamu. Kwa kuanza, mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga shilingi bilioni moja zitakazoanza kutekeleza mradi huo kwa awamu kwenye vijiji vya Mkiyonza, Nshunga, Milambi, Mkombozi, Rukuraijo, Nyabikurungo na Nyaruzumbura. Hivyo, Serikali inamuomba Mheshimiwa Mbunge kuwa mvumilivu wakati Serikali inaendelea kukamilisha mapitio ya usanifu kwa lengo la kuanza kutekeleza mradi huo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Eneo la Rubwera Kata ya Kyerwa ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na maeneo mengi yalikuwa ya wananchi, kuna eneo lilichukuliwa na Jeshi la Magereza na wananchi walizuiliwa kufanya shughuli yoyote kwenye eneo hilo.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hawa kama walivyoahidiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wakati wa uanzishwaji wa Wilaya mpya ya Kyerwa, eneo la wananchi wa Kijiji cha Rubwera Kitongoji cha Rwekorongo lilitolewa kwa ajili ya uanzishaji wa Gereza la Wilaya. Aidha, kwa mujibu wa tathmini ya Halmashauri ya Wilaya, jumla ya shilingi 661,928,640/= zinahitajika kuwafidia wananchi waliojitolea maeneo yao mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kuwalipa fidia wananchi wote nchini waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi na au uanzishaji wa magereza ikiwemo wananchi wa Rubwera. Aidha, Serikali itaendelea kulipa fidia hizo kwa wananchi kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha kutoka kwenye bajeti ya Serikali.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE Aliuliza:-

Je, lini utekelezaji wa mradi wa maji kwa vijiji 57 vya Wilaya ya Kyerwa utaanza kwa kuwa usanifu wa kina wa mradi huo umeshakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebba Innonent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Kyerwa, Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia Programu ya PforR na Programu ya Malipo kwa Matokeo (PBR) imetekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Nkwenda, Rugasha, Kitwechenkura, Kaikoti, Rwensinga, Kagenyi pamoja na sehemu ya Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya Kyerwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa mwaka huo, ukarabati wa visima virefu na vifupi umefanyika katika vijiji vya Kibale, Nyamiaga, Magoma, Rutunguru, Kihinda, Rwenkende, Kyerwa, Mirambi na Nyakakonyi ambapo wananchi wapatao 51,025 wananufaika na huduma ya maji safi. Utekelezaji wa miradi katika vijiji tajwa hapo juu ni sehemu ya utekelezaji wa miradi katika vijiji 57.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha vijiji vilivyobaki kati ya 57 vya Wilaya ya Kyerwa vinapata huduma ya maji, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.56 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 12 vya Runyinya, Nkwenda, Nyamweza, Rwabwere, Karongo, Iteera, Muleba, Chanya, Muhurile, Kimuli, Rwanyango na Chakalisa. Pia vijiji hivi viko ndani ya mradi wa vijiji 57.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022, Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 35 vilivyobaki ili kukamilisha utekelezaji wa mradi wa vijiji 57. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka miundombinu mizuri ya barabara katika Mbuga ya Ibanda na Rumanyika ili kuvutia watalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kwa kuendelea kuniamini kuhudumia Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe zilianzishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 509 na 510 la tarehe 05/07/2019. Hifadhi hizo zilitokana na kupandishwa hadhi kwa yaliyokuwa Mapori ya Akiba Ibanda na Rumanyika Orugundu.

Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha kufikika kwa hifadhi hizo, Serikali kupitia Taasisi za TANROADS na TARURA imekuwa ikitengeneza barabara mbalimbali zinazorahisisha kufika kwa watalii katika hifadhi hizo. Barabara hizo ni pamoja na Mgakorongo (Karagwe) hadi Murongo (Kyerwa) yenye urefu wa kilometa 112, ambayo inafanyiwa matengezo na TANROADS kila mwaka na imewekwa katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Mwaka wa Fedha 2020/2021. Vilevile barabara ya Omushaka – Kaisho – Murongo yenye urefu wa kilometa 120 imekuwa ikifanyiwa matengenezo kila mwaka na TANROADS.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha uwepo wa miundombinu mizuri ya barabara ndani ya hifadhi, Serikali imetenga shilingi milioni 311.9 kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 kwa ajili ya kuchonga barabara yenye urefu wa kilometa 20 katika Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe. Vilevile, kwa mwaka 2021/2022, Serikali ina mpango wa kutengeneza barabara yenye urefu wa kilometa 51 katika Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa; na barabara ya kilometa 20 katika Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe.

Mheshimiwa Spika, ni imani yetu kwamba jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Taifa Ibanda- Kyerwa na Rumanyika-Karagwe na maeneo mengine yote ya hifadhi zitasaidia kuweka mazingira mazuri ambayo yataziwezesha hifadhi hizo kutembelewa na watalii wengi waliopo katika maeneo ya karibu pamoja na wageni kutoka nchi jirani. Naomba kuwasilisha.