Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Innocent Sebba Bilakwate (1 total)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga mazao ya kimkakati na miongoni mwa mazao haya kahawa ni mojawapo. Hata hivyo, zao hili ambalo ni muhimu limekuwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika, wananchi kucheleweshewa malipo pale wanapouza kahawa lakini pia wananchi kukosa pesa ya kuwasaidia pale wanapokuwa wanaelekea kuvuna. Nini kauli ya Serikali juu ya changamoto hizi ambazo zinamfanya mwananchi kukata tamaa juu ya zao hili muhimu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imedhamiria kusimamia kilimo kwa ujumla wake kwa mazao ya chakula pamoja na ya biashara. Haya mazao ya kibiashara usimamizi wake ni kuhakikisha kwamba kuanzia kilimo hiki kinapoanza kwa kuandaa shamba mpaka mavuno na hatimaye masoko yanaratibiwa vizuri. Tumejitahidi sana kufanya hivyo wakati wote ili kuhakikisha tunaleta tija kwa mkulima anayeshiriki kilimo kila siku kwenye zao ambalo linalimwa kwenye eneo lake kulingana na jiografia yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kahawa ni miongoni mwa mazao tena ni mazao ya kimkakati ambayo yanalimwa na jamii pana. Kwa hiyo, Serikali tumehakikisha kwamba zao hili nalo tunalisimamia.

Mheshimiwa Spika, zao hili kwenye masoko tunaliuza kwenye mfumo wa mnada kupitia Ushirika. Zao hili pia kwenye maeneo yote yanayolima ikiwemo na kule Kyerwa, Karagwe na maeneo mengine ya Mkoa wa Kagera lakini pia kule Ruvuma maeneo ya Mbinga, Kilimanjaro, Arusha tunaona Tarime kule Mkoani Mara zao hili linaleta manufaa sana kwa wakulima. Tunaendelea kuratibu masoko yake na kama ambavyo Wizara ya Kilimo ilivyomaliza bajeti yake juzi na kutoa maelezo bayana ya kuimarisha masoko, bado nataka niwahakikishie wakulima wa kahawa tunaendelea kusimamia Ushirika, tutaendelea kusimamia masoko yake na pale ambapo masoko haya yanaleta tija tutahakikisha mkulima analipwa kwa wakati ili aweze kupata fedha ajipange tena kwa kilimo msimu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Bilakwate kwa sababu hata wakati wa Bajeti ya Kilimo hapa alisimama kueleza haya na Wizara ikamjibu. Wizara ilipokuwa inamjibu yeye maana yake ilikuwa inajibu wananchi wanaolima kahawa wakiwemo wale wa kule Kyerwa. Kwa hiyo, niwahakikishie wakulima wote kwa mazao yote ikiwemo kahawa kwamba Serikali itaendelea kusimamia bei nzuri ya mazao haya lakini pia tutahakikisha baada ya kuuzwa fedha za mkulima zinalipwa katika kipindi kifupi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuhuisha sheria na mifumo na zile Kanuni za kutoka siku ya mnada na kipindi cha kulipwa na hatimaye fedha kumfikia mkulima. Tukishafanikiwa hapo kila mmoja atafarijika kuendelea na kilimo hiki wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nataka nisisitize tu kwamba pamoja na kuleta masoko yaliyo bora, malengo yetu hasa ni kuanzisha viwanda vya ndani ili zao hili liweze kuongezwa ubora na ubora ule ndio utakaoleta masoko. Pia zao hili mnada wake ulikuwa Moshi pekee kwa hiyo utamuona mwananchi wa kule Kyerwa, Mbinga hata waliopo kule Mbozi wanapeleka kahawa Moshi. Tumeamua sasa kuweka vituo vya karibu na wakulima hukohuko walipo ili minada hii ifanywe huko walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumefungua kituo cha mnada wa kahawa Kagera, Makambako pamoja na Mbozi ili wale wanaolima mikoa ya jirani kwenye maeneo haya waende kwenye minada ile. Minada hii itakuwa ya wazi, mtu yeyote aliyepo ndani na nje ya nchi anakaribishwa kuja kununua. Kahawa ya Tanzania ni nzuri sana na ina thamani kubwa, kwa hiyo, tunawashawishi wanunuzi wote wa kahawa kuitumia kahawa ya Tanzania ikiwemo kahawa inayolimwa kule Mkoani Kagera kwenye Wilaya ya Kyerwa na Karagwe kwa ujirani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)