Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Deogratius John Ndejembi (7 total)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri na ya kina. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kanzidata kwa kutumia TEHAMA ili kuhakikisha kwamba wanaonufaika ni wale ambao wanakidhi vigezo vilivyowekwa na pia kuondoa mianya ya watu wanaonufaika kusajiliwa mara mbili kwenye maeneo tofauti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni je, sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba kaya ambazo hazikunufaika awali sasa zitanufaika katika hii Awamu ya TASAF III, hususan wazee siyo tu wa Bukoba Manispaa, Mkoa wa Kagera bali wa Taifa kwa ujumla? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mpango huu wa kuanzisha kanzidata ya walengwa wote wanaopokea fedha za TASAF imeanza. Mwanzo ilianza katika halmashauri 19 nchini lakini hadi hivi ninavyoongea tayari imekwenda katika halmashauri 39 na tayari tunaanza kuweka mfumo kwa ajili ya kuunganisha na NIDA, kuunganisha na mitandao yetu ya simu ili walengwa hawa badala ya kupokea fedha hizi dirishani kwa wale wanaokwenda kugawa, fedha hizi ziende moja kwa moja kwenye simu zao. Tutafanya hivi ili kuhakikisha kwamba hakuna kwanza double payment katika suala hili, kwa sababu kuna maeneo ambayo watu huwa wanalalamika mtu anapokea mara mbili au mtu akiwa hayupo watu wengine wanachukua zile fedha. Sasa ili kudhibiti hilo ndiyo maana tunakwenda sasa katika ku-roll out hii katika halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na tuta- roll out katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili, kwamba ni lini Serikali sasa itatanua mpango huu kwa wazee ambao hawakuingia na kaya ambazo hazikuingia. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge yeye wa Viti Maalum anafahamu anatoka Kagera, lakini hata wa Jimbo la Bukoba Mjini Mheshimiwa Byabato anafahamu kwamba sasa kaya zote katika Awamu hii ya Pili ya TASAF zinakwenda kuingia kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwatoe mashaka Wabunge wote wa Majimbo humu ndani na wa Viti Maalum kwamba mpango huu unakwenda kwenye kaya 1,400,000 ambayo ni sawasawa na watu milioni saba wanakwenda kunufaika na Mpango huu wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge kutoka Kibaha Vijijini. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, najua TASAF ilianza awamu ya kwanza kwa kuwapatia walengwa miradi ya uwekezaji kama majengo mbalimbali zikiwemo kumbi za maonyesho. Katika Jimbo la Kibaha Vijijini, wazee walipewa mradi huu awamu ya kwanza; je, TASAF wana mkakati gani juu ya kuwafanyia ukarabati jengo ambalo walipewa katika awamu ya kwanza ambalo sasa limechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia nafasi hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge, awamu ya kwanza ilijikita zaidi katika ujenzi wa miundombinu na si Kibaha Vijijini tu bali katika halmashauri nyingi sana katika nchi yetu ambazo majengo haya au miradi hii ilifanyika. Sasa baada ya awamu ya kwanza kuisha na kwenda awamu ya pili na sasa tuko awamu ya tatu phase II, ni kwamba majengo haya na miradi hii yote ilikabidhiwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika. Na ni wajibu wa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatunza majengo haya na wasiwaachie tu wale walengwa peke yao; ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha sustainability ya miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kuelekea katika halmashauri yake na kuhakikisha tunakwenda kuangalia miradi hiyo na kuwaagiza Wakurugenzi ili kuhakikisha kunakuwa na sustainability.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo kimsingi yatapunguza maumivu makubwa waliyopata wananchi wa Hai tarehe mbili kutokana na majibu ya swali lao kuhusu suala la ushirika. Niwaambie wananchi wa Hai watulie Serikali yao inawapenda sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize swali la nyongeza la kwanza; kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa wananchi wa Hai tarehe 28 walifanya jambo lao kwa asilimia kubwa sana na kuleta utulivu humu Bungeni na huko nje; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza kwa kiwango angalau cha asilimia 50 ya ahadi ya Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali italipa madeni ya watumishi wa afya na Walimu ambao ni wastaafu, deni ambalo mimi mwenyewe nimeshaliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri la milioni 171 ili watumishi wa afya waendelee kufanya kazi yao kwa uaminifu? Ikizingatiwa miongoni...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza swali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kuajiri watumishi wa afya japo kwa asilimia 50. Bunge lako Tukufu na Wabunge wote humu ni mashuhuda wa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kujenga Hospitali za Wilaya, kuongeza vituo vya afya na zahanati. Hivyo basi, pale ambapo bajeti itaruhusu, tutaendelea kuajiri watumishi katika Idara ya Afya; na hawa 75 wanaokwenda Hai, ni sawa na asilimia 18.6 ya watumishi wote ambao wameajiriwa hivi sasa. Kwa hiyo, kadri uwezo utakavyoruhusu, tutaendelea kuleta watumishi katika Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juu ya madeni ya watumishi, Mheshimiwa Mbunge kwanza amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za hawa watumishi na ili jambo amenieleza mimi mwenyewe zaidi ya mara mbili. Tayari tunashughulikia, ukiacha deni ambalo alikuwa analizungumzia la shilingi milioni 171, tayari yalikuja maombi 137 katika Ofisi ya Rais Utumishi yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 246 ili yaweze kushughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa madeni yaliyolipwa ni Sh.50,690,000/= na madeni yenye thamani ya shilingi milioni 148 ambayo ni sawa na watu 88, yamerudishwa kwa mwajiri ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai kwa sababu yalikuwa na dosari mbalimbali. Pale ambapo Mkurugenzi wa Hai atarekebisha dosari zile na kuzileta katika Ofisi ya Rais Utumishi, basi nasi tutazifanyia uhakiki tuweze kulipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna madeni ya watu 27, sawa na shilingi milioni 33 na kitu hivi, tayari yameshafanyiwa uhakiki na yametolewa katika Ofisi ya Rais, Utumishi na sasa yapo Wizara ya Fedha, tayari kwa malipo muda wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Lushoto ina uhaba mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya elimu na afya. Katika sekta ya elimu, msingi peke yake ambapo tuna shule 168, tuna uhaba wa watumishi 1,274. Tuna vituo 63 vya kutoa huduma za afya lakini tuna uhaba wa watumishi 1,218. Ni lini Wizara hii itaiangalia Halmashauri ya Lushoto kwa jicho la huruma na kutuondoa katika kadhia hii ambayo wananchi wanaendelea kupata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri walimu kadri bajeti itakavyoruhusu. Katika bajeti ya mwaka 2021, Serikali ilitenga bajeti ya ajira 9,500 kwa walimu na watumishi katika kada ya afya 10,467. Hivyo basi, pale Serikali itakapoanza kuajiri hawa, tutaangalia pia na Mlalo kule ili aweze kupata watumishi hawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa msamaha ulitolewa kwa wale wote ambao waliondolewa kazini kwa kukosa sifa ya kidato cha nne na baadaye wakajiendeleza kupata sifa hizo; na kuna maeneo ambayo watu hawana mawasiliano ya simu kama Ulingombe, Vidunda, Malolo na Kisanga.

Je, Serikali inatoa tamko gani kwa waajiri kuhakikisha kwamba watu wote ambao wame-qualify kurudishwa na hawana taarifa wanapata taarifa hizi kwa wakati na wanarudishwa kazini bila masharti ya ziada?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watumishi hawa ambao walishindwa kujiendeleza kidato cha nne lakini walikuwa na sifa stahiki wakati wanaajiriwa waliondolewa kazini walitumikia hii nchi kwa uadilifu na uzalendo lakini hawakuwa na kosa mahali zaidi ya maelekezo ya Serikali.

Je, ni lini Serikali inaenda kuhakikisha kwamba malipo yao na stahiki zao zinalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, msamaha uliotolewa kwa watumishi hawa ambao waliajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004 ambapo tangazo la Serikali lilitoka mpaka ifikapo Mei, 2004 watumishi wote wanaoajiriwa Serikalini ni lazima wawe na sifa ya kidato cha nne. Hata hivyo kuna waajiri ambao waliajiri watumishi baada ya tangazo lile la Serikali. Tunatambua kwamba haikuwa kosa la wale watumishi walioajiriwa.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ilitoa maelekezo kupitia Katibu Mkuu Kiongozi kwamba hawa watumishi wote walioajiriwa baada ya tarehe hiyo wawe wamejiendeleza na kupata sifa ya kuajiriwa Serikalini, yaani cheti cha kidato cha nne mpaka ifikapo Desemba, 2020. Na waliorejeshwa kazini mpaka kufikia Desemba 2020 ni zaidi ya watumishi 4,335 ambao walirudi kwa sababu walikuwa wamejiendeleza.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa wale ambao kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kwamba hawakupata taarifa popote ya kwamba wajiendeleza na walijiendeleza kabla ya ile deadline iliyowekwa basi niwaelekeze waajiri wote nchini kuweza kuliangalia hili kuwachukua watumishi hawa kama walijiendeleza tu kabla ya kufikia Desemba, 2020 lakini hawakupata tangazo la kurejea kazini basi waajiri waweze kuliangalia hilo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili aliulizia wale ambao hawakujiendeleza lakini waliajiriwa baada ya Mei 2004. Hawa siku ya Mei Mosi Mheshimiwa Rais wetu mama yetu Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo, kwamba watumishi wote waliokuwa na sifa ya elimu ya darasa la saba walipwe stahiki zao kwa sababu hawa hawakughushi wao waliajiriwa siyo makosa yao basi stahiki zao kama hawakurejeshwa kazini na kama hawakujiendeleza walipwe. Tayari ofisi yetu ilishatoa waraka kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi kwa waajiri wote nchini kuanza kushughulikia hawa wenye elimu ya darasa la saba ambao hawakurejeshwa kazini, na tayari linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, na nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutupandisha daraja kutuita kidato cha saba.

Mheshimiwa Spika, watumishi wa darasa la saba ambao waliondolewa kazini walifanya kazi zao kwa uaminifu, wengine walikuwa watendaji na watu wengine; lakini tamko hili lilitoka na waraka ukatoka mpaka leo asilimia 95 hawajawahi kulipwa wala kuitwa wala kupokelewa tu na waajiri. Sasa ningemwomba Mheshimiwa Waziri kama anaweza kutoa commitment angalau akatupa kopi ya zile nyaraka sisi Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kwenda kutetea wale waliondolewa na hawajapata stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, watumishi ambao hawakujiendeleza mpaka kufika Desemba, 2020 walikuwa kama 1,491, ambao hawakujiendeleza, na hivyo walikosa sifa ya kurejeshwa katika utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali wakati najibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Londo, kwamba Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan alitoa agizo lake siku ya Mei Mosi pale Mwanza. Kwamba hawa 1491 stahiki zao zilipwe; na tayari ofisi yetu ya Utumishi ilishatoa waraka tarehe 21 Mei, 2021 kwa waajiri wote kuanza kuhakiki madeni haya na kuangalia stahiki walizotakiwa kulipwa hawa wa darasa la saba. Naamini baada ya muda mfupi hawa 1491 wataanza kulipwa, kwa sababu ilikuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na hivyo tutalitekeleza kama aliyoelekeza yeye Mheshiwa Rais. Ahsante sana.
MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa kwa sasa hivi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuboresha maisha ya watumishi lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hivi Serikali haioni kumshusha mtumishi mshahara ni mojawapo ya adhabu apewazo anapokuwa na utovu wa nidhamu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali mtatoa tamko la kwamba hawa watumishi wanaofanyiwa recategorization mishahara yao ikiwa chini ya vyeo vile wanavyoenda kuanzia watabaki na mishahara yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze kusema siyo adhabu kumshusha mshahara mtumishi ambaye ametaka kubadilishiwa kada yaani recategorization kwa job satisfaction kwa sababu bila kufanya hivyo utakuta mwalimu tayari alikuwa ameshapanda daraja juu na sasa ameomba kuwa Afisa Sheria, natolea mfano, ni lazima aende kuwa Afisa Sheria Daraja la II, entry point ili kutengeneza seniority katika eneo la kazi. Bila ya kufanya hivyo, tunaweza tukawa tunawabadili kada watumishi anakwenda katika idara husika anakuta tayari kuna watumishi wengine waliotumikia kada hiyo miaka mingi yeye akaenda kuwa senior zaidi yao kwa sababu tu alishatumikia cheo kingine na kada nyingine. Kwa hiyo, kwa ajili ya kulinda hiyo seniority ni lazima aende katika entry point ya kazi ile aliyoiomba.

Mheshimiwa Spika, lakini akiwa ametumikia cheo kikubwa zaidi kwingine atahamia kule na mshahara binafsi ataombewa na mwajiri. Akiombewa mshahara binafsi atabaki nao kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba baada ya kufikia cheo sasa tuchukulie Afisa Sheria labda kafika kuwa Principal basi atalipwa mshahara ule wa Principal na ataacha mshahara wake wa mwanzo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, utumishi wa umma unaongozwa kwa sheria, taratibu na kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa. Kwa wale wote ambao wanastahili kufanyiwa recategorization ni wajibu wa waajiri kwanza kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya recategorization. Mbili, ni wajibu wa mwajiri kumfanyia recategorization huyo mtumishi na kumwacha na mshahara binafsi endapo kada yake ni ileile ambayo amejiendeleza nayo. Hili si ombi ni kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge kama kuna mifano maeneo mengine Waziri wangu pamoja na mimi mwenyewe tuko tayari kwenda kuweza kuwashughulikia hawa Maafisa Utumishi na waajiri ambao hawatekelezi sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nihitimishe kwa kusema hivyo, nashukuru sana. (Makofi)