Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Jafari Chaurembo (3 total)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo cha VETA katika Kata ya Chamazi eneo ambalo limetolewa bure na UVIKYUTA zaidi ya ekari 30 ili kuwawezesha vijana wengi wa Kitanzania kuweza kujiajiri na kuweza kupata ajira katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi Serikali ina mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba katika kila mkoa na katika kila wilaya tunakuwa na Chuo cha VETA. Katika awamu ya kwanza tumefanya ujenzi ambao mpaka hivi ssa unaendelea katika wilaya 29, lakini katika awamu ijayo tunatarajia katika kila wilaya kupeleka vyuo hivyo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kila wilaya tutafikia kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni nini kauli ya Serikali kwa kumalizia kipande cha Mbande – Kisewe ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Kata ya Chamazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, barabara ya Zakhem – Mbagala Kuu imepata fedha za Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar-Es-Salaam na imeshindwa kujengwa kwa sababu ya uwepo wa bomba la mafuta la TAZAMA. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia walao corridor ya mita saba ili barabara hiyo ambayo tayari inayo fedha iweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tunavyoongea sasa hivi, Mheshimiwa Chaurembo ni shahidi, tulikuwa na kilometa 6.05; kilometa moja imeshakamilika zimebaki kilometa 5.06. Nimhakikishie Mheshimiwa Chaurembo katika mwaka huu wa bajeti, kupitia fedha ya matengenezo, sasa tutaanza barabara ya kutoka Mbande kuja Msongola ambapo tunajenga kilometa 1.5 kwa kiwango cha lami. Pia kwa fedha ya maendeleo tutaendelea kutoka Msongola kwenda Mbande kilometa 1. Kwa hiyo, tutabakiwa kama na kilometa 2.5 ambazo zitakuwa bado hazijakamilika na fedha itakapopatikana tutaendelea kukamilisha barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuhamisha bomba ama barabara Serikali imelipokea na itakwenda kulifanyia kazi tuone kama tutahamisha kwa sababu inapita karibu na bomba. Tutaangalia namna ya kufanya ili barabara ile muhimu sana iweze kuanza kujengwa. Pia kwa sababu suala hili siyo la Idara yangu pekee kwa maana ya Wizara ya Ujenzi ni Wizara nyingi, kwa hiyo, tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kuona ni namna gani tufanye kuhamisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umeme unaozalishwa katika Sub-station ya Mbagala ni chini ya asilimia 20 tu unaotumika Mbagala na asilimia zaidi ya 80 unaenda kutumika Mkuranga. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga sub-station kule Mkuranga ili kuwapoza watu wa Mbagala waendelee kutumia umeme wao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Mbagala ndiyo Jimbo ambalo lina watumiaji wengi wa umeme ukilinganisha na mikoa mingine ya Ki-TANESCO, je, Serikali ina mpango gani wa kulifanya Jimbo la Mbagala kuwa mkoa wa Ki-TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mbagala tunayo Sub- station inayozalisha Megawatts 48 na Megawatts 40 zinakwenda Mkuranga kama alivyosema kwa sababu kuna viwanda vingi sana pale zinabaki Megawatts 8 tu. Tunapata umeme wa Mbagala kutoka Ubungo kupitia Gongolamboto lakini tunapata umeme mwingine kutoka Kurasini. Pale Kurasini tunapata Megawatts kama 26 hivi, zinazoenda kujazia pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba umeme unapungua katika eneo la Mbagala kwa sababu mahitaji yamekuwa makubwa. Hata hivyo, kama tulivyosema kwenye swali la msingi, tunaongeza uwezo wa kituo hicho cha Mbagala kwa kuweka MVA 50 lakini pia cha Kinyerezi ambacho pia kitaleta umeme pale Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali hilohilo ni kwamba tayari Serikali inafanya feasibility study ya kujenga sub-station nyingine kumi na kuziboresha nyingine kadhaa katika maeneo yetu ya Tanzania. Mkuranga kwa sababu ya umuhimu wake wa kuwa na viwanda vingi sana ni eneo mojawapo ambalo litapelekewa sub-station katika siku za hivi karibuni ili kupunguza mzigo mkubwa ambao vituo vyetu vya Mbagala na Kinyerezi vinaupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mkoa wa Dar es Salaam mpaka sasa unayo mikoa ya ki-TANESCO minne na hivi karibuni yamekuja maombi ya Kigamboni kuwa ni Mkoa wa ki-TANESCO na bado yanafanyiwa kazi. Niombe kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amelisema, tutaenda kuangalia vigezo kwa sababu kuna kuangalia idadi ya wateja, makusanyo, line ya umeme mkubwa na mdogo katika eneo husika, vigezo vikikidhi basi, mamlaka husika zitaamua na huduma zitapelekwa karibu zaidi na wananchi.