Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (2 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu na takwimu zilizotolewa na Serikali, ukweli ni kwamba kutoka ngazi ya Mkaguzi Msaidizi kwenda Mkaguzi kamili inapaswa kufanyika ndani ya mwaka mmoja mpaka miaka miwili. Je, Mheshimiwa Waziri anayo taarifa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka muda huu ambapo nimesimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuna Wakaguzi Wasaidizi ambao hawajapandishwa madaraja?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri atueleze hapa ikiwa anazo hizo taarifa ni kwa nini basi hao Wakaguzi hawajapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, si kweli kwamba tangu 2015 mpaka hapa tulipo watu hawajapandishwa madaraja. Kama ataangalia kwenye jibu langu la msingi nilitoa takwimu ambazo zinaonyesha kwamba kuna watu walipandishwa madaraja.

Mheshimiwa Spika, kingine nimfahamishe tu Mheshimiwa kwamba ni vizuri wakapata nafasi wakaipitia hii PGO (Police General Order) itawasaidia kujua baadhi ya taratibu ambazo zinatumika kupandisha madaraja. Kuna mambo ya msingi huwa yanaangaliwa, siyo kwamba watu wanapandishwa tu kwa sababu hawajapandishwa muda mrefu. Kwanza, lazima kipatikane kibali cha kupandisha majaraja. Pili, tunaangalia pia uwezo wa kiuongozi wa yule ambaye anatakiwa kupandishwa daraja. Tatu, tunazingatia zaidi vigezo vya kimaadili kwamba tunayekwenda kumpandisha cheo ana maadili gani katika kutumikia Taifa hili. Nne, tunaangalia kama hana mashtaka mengine. Tano, huwa tunaangalia na bajeti maana tukimpandisha cheo lazima tumpandishie na mshahara wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa afahamu kwamba utaratibu ndiyo huo lakini tumeanza na tumepandisha madaraja mbalimbali kwa watumishi wa Jeshi la Polisi kama ambavyo taratibu zimeeleza.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa ajili ya nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri kwamba, hayaleti matumaini ya moja kwa moja kwa wakazi wa Butiama naomba nijielekeze kwenye maswali kama ifuatavyo; Swali la kwanza; kwa kuwa, miradi hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja hapa utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua sana kwa lugha nyingine umekuwa na mwendo wa kinyonga. Je, nini kauli ya Serikali basi kuhusiana na bili zinazotolewa kwa wakazi wa Butiama bila kupatiwa huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua mwanamke ndoo kichwani. Swali langu ni kwamba, ni lini basi Serikali itatekeleza kauli mbiu hii kwa matendo kukamilisha miradi yote ya Serikali nchi nzima ambayo imeonekana kusuasua mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya bills, maeneo mengi yalikuwa na tatizo hili, lakini tayari Wizara tunashughulikia kwa karibu kuona kwamba, mtu anakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake. Tunaendelea kuweka mbinu mbalimbali kama kumhusisha moja kwa moja mtumiaji maji kwa kushirikiana na msomaji mita wataangalia kwa Pamoja, watasaini kadi na hapo sasa yule mlipaji atakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kumtua mwanamke ndoo kichwani; hili suala sasa hivi ni tayari linatekelezeka. Maeneo mengi ya Tanzania sasa hivi akinamama wameshakiri hawabebi tena maji vichwani na tayari Wizara tunaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maeneo yote ya pembezoni mwa miji kwa maana ya vijijini nao wanakwenda kukamilika katika mpango huu na kazi zinaendelea. Tayari tuna ari kubwa sana kama Wizara na watendaji wetu wametuelewa mwendo wetu ni mwendo wa kasi ya mwanga. Ahsante sana. (Makofi)