Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (2 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshaji wa kupandisha vyeo kwa Askari wa Jeshi la Polisi katika ngazi ya Wakaguzi Wasaidizi na kwa Wakaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi ni Taasisi ya Serikali ambayo mfumo wake wa upandishwaji wa vyeo huzingatia sheria na kanuni za utumishi. Askari, Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi hupandishwa vyeo pamoja na watendaji wengine wa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia ikama na bajeti ya mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 mpaka 2018 jumla ya askari 2,354 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi Wasaidizi na kwa kipindi cha kuanzia 2015 mpaka 2020 jumla ya Wakaguzi Wasaidizi 1,163 walipandishwa vyeo kuwa Wakaguzi wa Polisi. Serikali itaendelea kuwapandisha vyeo Askari Wakaguzi na Maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kulingana na taratibu zilizoelezwa hapo awali. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama Butiama ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa Baba wa Taifa katika Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambart Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Butiama ni 61.18%. Katika kuhakikisha wananchi wa Butiama wanapata huduma ya maji safi Serikali kupitia RUWASA imekamilisha miradi ya maji katika Vijiji vya Nyabanje, Magunga, Kongoto, Bukwaba, Kamgendi na Masurura, vinavyohudumia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutatua tatizo la maji katika muda mrefu Butiama, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama mwezi Disemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022. Kazi zilizoanza kutekelezwa ni upimaji wa maeneo ya ujenzi wa matenki, mtambo wa kusafisha maji, njia kuu ya bomba na uletaji wa vifaa katika eneo la mradi. Mradi huu unatarajiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 katika eneo la mradi pamoja na vijiji vilivyoko ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for Development – SFD) kwa gharama ya dola za Marekani milioni 30.69 sawa na takribani shilingi bilioni 70.