Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Agnesta Lambert Kaiza (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii adimu ambayo umenipatia ili niweze kusema machache kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuchangia nitumie fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima, lakini pia kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kujadili masuala mazima yanayohusiana na hotuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo mengi ambayo Mheshimiwa Rais alizungumza katika hotuba yake ni pamoja na nchi yetu kuingia katika uchumi wa kipato cha kati. Hii ni habari njema kwa Taifa na ni jambo la kujisifia kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni kweli Serikali yetu imetuingiza katika uchumi wa kipato cha kati, kuna mambo ya msingi sana ambayo yanapaswa au yalipaswa ku-reflect moja kwa moja kwamba sasa Tanzania tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mbele ya Bunge lako tukufu nijikite katika masuala makuu manne ambayo yanaashiria moja kwa moja kwamba ni ama tumedanganywa kama nchi kwamba tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati au Serikali imedanganya kwamba sasa hivi imekuwa ikikusanya mapato makubwa sana ambacho ni kiashiria cha ukuaji wa uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mosi, wewe ni shahidi kwamba Serikali imekopa pesa nyingi kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mfano NSSF; Serikali imechukua, au imekopa fedha ambazo Serikali ilitarajiwa irudishe ile mikopo ndani ya ule muda ambao masharti yanasema ili mwisho wa siku sasa wastaafu, mama zetu, mashangazi zetu, wajomba zetu ambao walitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana na baadaye wakastaafu sasa waweze kupewa…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza. Anataka kujenga hoja kwamba Serikali bado haijalipa fedha ambazo ilikuwa inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshafanya kazi hiyo na mpaka sasa zaidi ya trilioni 1.2 ambazo Mfuko wa PSSSF ulikuwa unaidai Serikali, fedha hizo zimekwisha kurudishwa na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi wakati tulipokuwa kwenye kikao cha Kamati, mimi mwenyewe na watendaji wa Mfuko tulishatoa taarifa hiyo kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengine ambayo Serikali bado inaendelea kufanya uhakiki. Utaratibu wa Serikali sasa hivi katika madeni yaliyobakia haiwezi kulipa bila kufanya uhakiki, kwa hiyo kila baada ya uhakiki Serikali imeendelea kuwa inalipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, labda nitakapokuja jioni ama wakati wa kuchangia Mpango tutatoa taarifa ya wastaafu wangapi wamekwishalipwa mafao yao na kwa nini labda kumekuwa na kuendelea kuwalipa wastaafu mafao kwa utaratibu mmoja na mwingine. Kwa hiyo maeneo haya tutayatolea maelezo lakini justification ya malipo ya Serikali tunayo na Serikali imelipa na tunaendelea kuhakiki na tunaendelea kulipa yale yaliyokwisha kuhakikiwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nikiri kwamba mama yangu, dada yangu, rafiki yangu mpenzi, anafanya kazi nzuri sana, lakini itoshe kusema kwamba hayo aliyoyasema kwamba Serikali haijalipa ndiyo hayo ambayo nayaongelea mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasema tayari imetuingiza kwenye kipato cha kati. Kama tumeingia kwenye kipato cha kati na tayari kuna wastaafu ambao waliitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana hawajalipwa, itoshe kusema kuna tatizo. Sasa nimshauri dada yangu na rafiki yangu achukue ushauri wangu huu, kwamba pamoja na kazi nzuri anayoifanya, hili linaitia doa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika ajenda yangu ya pili inayohusiana na Serikali kuchelewesha malipo kwa makandarasi. Ikiwa kweli Serikali hii imetuingiza katika kipato hiki cha kati, ilipaswa moja kwa moja kitu cha kwanza kabisa iwe inalipa on time fedha za makandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umesikia jana, leo, juzi, wachangiaji wengi katika Bunge hili wamekuwa wakilalamika kuhusiana na ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, unaposikia kuwa…

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa.

Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa taarifa ya mwisho kwa sababu muda wetu ni mfupi. Mheshimiwa Charles Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleweshe msemaji kwamba hivyo vitu anavyovizungumza haviendani na hoja anayotaka kutoa ya kusema kwamba tuko kwenye kipato cha kati. Kipato cha kati hakiendani na mambo ya Serikali kukopa au Serikali kutokulipa, hayo ni mambo tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika ni wastani wa pato la mtu mmoja. Unachukua pato la Taifa unaligawanya kwa idadi ya watu, unapata huo wastani. Kwa hiyo, hiyo haihusiani na mambo ya Serikali kutokulipa au kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwelekeza kwamba hilo analozungumza ana hoja nyingine pengine lakini siyo hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa hiyo siipokei, lakini nakuomba wewe na Kiti chako unilindie muda wangu wa dakika tano vizuri sana, nakuomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anadai kwamba ninachokiongelea hapa siyo sehemu ya hiyo dhana nzima ambayo nimetoka kuisema. Hata hivyo, ikiwa pato la Taifa hali-reflect maisha ya wananchi ya kila siku, tusijidanganye kwamba tumeingia katika uchumi wa kati. Mfano, wakandarasi wanashindwa kwenda kulipa fedha kwenye…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, nilikupa sekunde 30 kwa sababu kengele ilishagonga. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Niseme kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa hiyo nimeshiriki kwa asilimia 100 kupitia Muswada huu ambao uliletwa kwetu na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba Muswada huu haukuwa ni Muswada ambao ulikuwa una taswira ya maslahi mapana ya Taifa. Nasema hivyo kwa sababu ndiyo maana ukiangalia ripoti yetu Kamati unaona jinsi ambavyo tumeweza kufumua sheria nyingi ambazo zilipendekezwa na Serikali kwamba ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipongeze kwa namna ambavyo Serikali imeweza kuyachukua mapendekezo yetu kama Kamati na kuyafanyia kazi na kukubali kutembea katika ushauri ambao tumeweza kuutoa. Kwa sababu nasema hivyo, nakumbuka wakati Serikali inawasilisha mswada huu nilikuwepo na kutokana na Sheria hizi ambazo zilikuwa ni sheria kumi na tatu kabla hatujaondoa ile Tafsiri ya Sheria Sura ya kwanza, mimi mwenyewe nilisimama nikasema ikiwa Serikali haitokubaliana na mapendekezo ambayo binafsi mwenyewe niliyatoa, nilisema nitakuja kusimama juu meza hapa.

Mwenyekiti wangu nishahidi na Wajumbe, nikasema nitasismama juu meza kusema kabisa kwamba hizi Sheria hazina maslahi kabisa, lakini nawashukuru kwamba wameyachukua na wamekubali kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, haitoshi kabisa kusema kwamba nawapongeza kwa kuchukua mawazo yetu na ushauri wetu na kuufanyia kazi. Hiyo haitoshi, nasema haitoshi kwa sababu gani najaribu ku-imagine ikiwa Kamati hii ya Katiba na Sheria siku hiyo wakati tumekuwa tukipitia huu Muswada tungekuwa tumeamka vibaya, nikisema kuamka vibaya nafiri yaani tumeamka vibaya kama Kamati, halafu tukawa hatujaona haya ambayo tumeyaona na tukaleta mapendekezo na tukapitisha kama the way ambavyo Serikali ilikuwa inataka, ni wazi kabisa kwamba yangekuja tukukuta kama yale ya tozo.

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naushauri, niushauri, Serikali kabla haijaleta Muswada Bungeni, haijaleta Muswada kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, wawe wanakaa kwanza wanakuwa makini, watafute wataalam, watafute wabobezi, wakae nao chini, wawashirikishe namna na jinsi ambavyo wamepanga kuleta Muswada na wapate ushauri kwamba je, huu Muswada, hii Sheria mnayotaka kuipeleka imebeba maslahi mapana ya Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu haitoshi tu, haitoshi tu kusema kwamba tutarekebisha tayari tutakuwa tumeshatengeneza damage kubwa sana. Tupo hapa tunajadili mambo mbalimbali mfano, umesema kwamba siyo busara, siyo busara kuanza kuongelea yale mambo ambayo Serikali imekubali kuyafanyia kazi na mengine kuyaondoa.

Mheshimiwa Spika, lakini tujiulize kama wangekaa chini Serikali ikakaa chini na Wataalam wakaona namna gani wanakwenda kuleta Muswada wenye mantiki sisi tukafanya kuboresha boresha tu kidogo, tuboreshe tu kidogo siyo mnaleta Muswada, siyo tu unafumuliwa lakini mwingine tunautupa nje kabisa. mfano hii hapa ya Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya Kwanza…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ngoja upokee taarifa halafu utaendelea Mheshimiwa Agnesta.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru mchangiaji anachangia vizuri na tunashukuru Kamati kwa kupokea maoni na mawazo ya Wanakamati. Kazi ya Bunge ni kutunga Sheria na Serikali inapoleta Muswada hapa inatarajia maoni na ushauri kutoka kwa watunga Sheria. Sasa hawezi akasema kwamba yeye hawezi kupongeza sijui, ni kazi yake, anapongeza nini? Kwa hiyo, asilaumu chochote imeletwa mahala husika kwa watunga sheria, waitunge Serikali ifanyie kazi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, unapokea taarifa hiyo kwamba usilaumu chochote. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli sipokei hiyo taarifa na niseme, ukiangalia katika ushauri wa jumla wa Kamati pamoja nashauri zingine Kamati imeishauri Serikali kwamba kabla haijaleta, haijaleta huo Muswada iwe inakaa chini, inatathmini, inajiridhisha that’s why tuna wataalam, sasa kama tumeweka watu ambao wanapaswa kufanya uchambuzi kabla ya mambo hajafika Bungeni then why tumewaka watu kama hao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siipokei lakini niseme pia ni nafasi yangu kama Mbunge lakini pia kama Mjumbe Kamati kuishauri Serikali kwamba iwe inakaa, inatulia, inajipanga vizuri kuleta Miswada kuanzia sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiniambia kwamba kazi yangu ni kutunga Sheria, yaani kwamba Serikali upo kwa kajili ya kuleta Miswada halafu mimi naifumua tu, naifumua tu, naifumua, what is it them!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee na mchango wangu kuendelea kuishauri Serikali kama jinsi ambavyo Kamati imeshauri, kwamba siku nyingine mkae chini, muwaweke wataalam, mpate ushauri mbalimbali, mtafuta wadau kama jinsi ambavyo sisi kama Kamati tunaita wadau. Tuliwaita, wakaja wakapitia Muswada wenu huo huo, wakagundua vitu mbalimbali ambavyo haviko sawa that’s why tumewaletea Taarifa ambayo ipo sahihi na ninyi mmekwenda mmeifanyia kazi mmekubali kuifanyia marekebisho. Siyo tu kukubali mkanyofoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu umesema kwamba tusiongelee yale ambayo Serikali imeshayatoa kwa sababu tungesema yaliyojiri kwenye Kamati ni hatari tupu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapoendelea na mchango wangu ninapokuwa namalizana na suala zima la kuishauri Serikali katika marekebisho ya Kifungu cha 54 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria Sura ya Kwanza, pamoja na kwamba Kifungu hiki au Sheria hii tumeiondoa kabisa lazima ifike sehemu Serikali tuweze kujitathmini sana, kwamba sheria kama hii ambayo ilikuwa inapendekeza kwamba ile Bodi inapovunjwa yaani Bodi inapokuwa imeisha wakati wake mfano kwamba Katibu Mkuu akiwa peke yake…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Chief Whip!

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba tu niweke vizuri jambo hili kwa sababu Watanzania wanaweza kuwa pia wakapata fursa ya kusikiliza huu mjadala wetu kwa hiyo, ni lazima tuliweke sawa.

Mheshimiwa Spika, ninakubali ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge, lakini Mbunge anaposema kwamba Kamati imeiondoa Sheria ya Serikali siyo sahihi. Muswada huu ulioletwa ni Muswada mmoja wenye sheria ndogo mbalimbali. Kwa hiyo, ndani ya Muswada huu mmoja, yaani sheria hii iliyoletwa kipengele fulani ndicho kilichoondolewa.

Kwa hiyo, nilikuwa nataka twende kwa muktadha huo. Isipeleke picha kwenye public kwamba ule Muswada au sheria iliyoletwa na Serikali Bunge imeiondoa, lakini sehemu ya sheria iliyoletwa kwenye Muswada huu Namba hii ambao ndiyo unaendelea ndani ya Bunge basi katika hatua ya Kamati Serikali ilishauriwa jambo hili liondolewe.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kutoa hiyo taarifa ili kusudi tuchangie huku tukielewana kwa muktadha wa uelewa wa public na wenyewe humu ndani.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza ‘nshomile’ unakubali ushauri huu? (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Labda nimuulize Mheshimiwa Jenista ni kweli kuna sheria zimefutwa au hazipo?

Mheshimiwa Spika, mfano hatutaki kusema, ipo sheria mbovu nafikiri itajadiliwa kesho, imefutwa inahusiana na Posta ambayo walitengeneza mazingira ya ku-hold kwamba vifurushi kusafirisha vifurushi huku na kule kwa maana ya Posta peke yao ndiyo waweze kufanya shughuli katika utandawazi wa sasa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, hapo unawahisha shughuli, kama unajua ni ya kwesho basi iweke mpaka kesho. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, unajua ukichokozwa wakati mwingine na wewe unachokonoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimechokonoa lakini itoshe tu kusema Mheshimiwa Jenista pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba nia yangu ni njema sana tusitumie muda mwingi wa kufumua fumua hii Miswada mnayoileta ikiwa…

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta kuna Taarifa nadhani inahusu kuchokonoa.. (Kicheko)

Mheshimiwa Abdallah Mwinyi tafadhali.

T A A R I F A

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Agnesta kwamba hiyo sheria anayoizungumzia kesho siyo kwamba ni sheria nzima ni kipengele ndani ya sheria kama Mheshimiwa Jenista Mhagama alivyosema. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge na hilo nalo usiendelee nalo kwa sababu ni la kesho, Mheshimiwa malizia bado dakika moja tu kama unalo la kusema.(Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nimalize kwa kuendelea kuipongeza Kamati ya Katiba na Sheria chini ya Mwenyekiti wetu mahiri hakika tumeweza kufanya kazi kubwa kubwa isiyokuwa ya kifani na Mwenyekiti wetu anastahili pongezi kwa sababu Mheshimiwa Spika utakuwa shahidi, sheria 12 ambazo tulikuwa tunazifanyia marekebisho hakuna sheria hata moja ambayo tulisema kwamba Serikali walipoileta ilikuwa sawa kwamba sasa ipite kama ilivyo.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Ahsante sana. Muda umekwisha ni kengele ya pili.
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja katika Sehemu ya Nne ya Muswada huu inayoongelea Bohari ya Madawa, katika Muswada huu bohari wanahitaji au wanataka kufanya production ya madawa pamoja na vifaatiba. Sasa natambua kwamba, siku ya leo…

SPIKA: Uko kipengele gani? Ukurasa wa ngapi?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, niko katika Sehemu ya Nne ya Muswada. Naomba niendelee.

SPIKA: Part four.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba, bohari ya dawa inahitaji kuanza production ya madawa…

SPIKA: Yaani wapi?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne ya Muswada huu.

SPIKA: Yaani kwa hiyo, unajadili zote kuanzia 11 mpaka 21 kwa ujumla wake?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kama ni zote haya endelea.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesema Bohari ya Madawa inahitaji kufanya production ya madawa plus vifaatiba. Siku ya leo kwanza tuko hapa kwa ajili ya kujadili ili tuweze kupitisha sheria hii, lakini mpaka naongea hapa mbele ya Bunge lako Tukufu MSD tayari kwa tetesi zilizopo kwamba…

SPIKA: Aah, ngoja. Yaani hapa tunatunga sheria, ndio maana jana Wanasheria walijiita wasomi, tofauti iko hapo. Tunapotunga sheria habari ya tetesi, sijui nini, yaani hapa tunaenda moja kwa moja wapi? Panasemaje? Sentensi gani ifutwe? Koma ihame kutoka wapi iende wapi? Isisomeke hivi ila isomeke namna hii, katika hatua hii hatuchangii hoja tena ya ile, hapa tunatunga sheria. Kwa hiyo, tuambie kabisa wapi pakibaki palivyo itakuwa hivi, lakini ukituambia tetesi hapa haiingii.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimeshaelewa naomba niendelee. Nimesema kwamba, bohari ya madawa inahitaji kufanya production…

SPIKA: Huendelei mpaka uniambie ni wapi? (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, Section 12 ya Muswada huu inaongeza neno production kwa maana ya uzalishaji.

SPIKA: Enhee.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sasa nimesema bohari inahitaji itoke kwenye usambazaji, I mean, iwe na usambazaji at the Same time inafanya production. Wote tunatambua na tunafahamu na nilisema wakati tuko kwenye Bunge la Bajeti, MSD ime-fail big time katika suala zima la usambazaji wa madawa, lakini leo hii inahitaji ijiongezee tena kazi nyingine ya kufanya production.

Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu sioni kama MSD ina capacity ya kufanya production at the Same time ikafanya usambazaji, lakini natambua kwamba, hata nikisema namna gani, nikipinga hii sheria namna gani, sheria hii itakwenda kupita. Sasa niseme jambo moja…

SPIKA: Kwa sababu hujaelewa tu, lakini ukieleweshwa vizuri utaelewa jinsi ambavyo MSD kwa kwenda kuzalisha baadhi ya madawa ambayo tunayaagiza nje na mahali pengine kwa bei kubwa itaokoa billions of shillings. Endelea tu. (Makofi)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakuelewa na kwa upande mwingine uko sahihi kwamba, MSD kama ingekuwa na capacity kwa sababu, tuna sehemu ya kuwaangalia kwanza walikuwa wanafanya usambazaji, wame-fail. Wewe ni shahidi na uliwahi kusema katika Bunge hili kwamba mdawa ni shida…

SPIKA: Hawatazalisha kila dawa. Kuna baadhi ya dawa ambazo wana capacity ndio wataenda kuzalisha.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sasa naomba niseme hivi kwa kuwa, inaonekana kwamba, MSD wanaweza kufanya production at the Same time wakafanya…

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

Mhe. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Iko Msekwa au iko wapi?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa iko hapa. Niko hapa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, Taarifa, Msekwa. Niko hapa Msekwa.

SPIKA: Ndio mwenye Taarifa? Msekwa, endelea Taarifa, hapa ndani subiri Ukumbi wa Msekwa kwanza.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, MSD isingeweza kuanza production kabla hatujaitungia sheria. Tunaitungia sheria ili iweze kuanza kufanya hiyo kazi kabla ya hapo ingafanya production bila sheria ingekuwa inafanya kitu cha ajabu, ingewekwa hata ndani. Ahsante.

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Tadayo. Kwamba tusiwahukumu kabla hatujawapa uwezo wa kufanya. Mheshimiwa Agnesta taarifa hiyo ni kwako, hapana siyo kwenu ninyi wawili. Taarifa hiyo inakwenda kwa Mheshimiwa Agnesta Lambert.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba, Taarifa hii siipokei.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Bahati mbaya muda umeisha.