Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aloyce John Kamamba (8 total)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kupeleka huduma kwa wananchi. Tatizo lililojitokeza hapa ni baadhi ya vitongoji hasa katika Mji wa Kakonko kurukwa. Mfano, vitongoji vya Itumbiko, Mbizi, Kizinda, Cheraburo zikiwemo taasisi kama shule za makanisa. Kwa nini taasisi na vitongoji hivi vinarukwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lini sasa haya maeneo ambayo yamerukwa yatapewa huduma hiyo ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji vya Jimbo la Kakonko havijarukwa isipokuwa Serikali inaendelea kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vyetu kwa awamu. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha vitongoji vimekuwa vikipatiwa umeme kulingana na mazingira yalivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeme umepelekwa katika vijiji 40 vya Jimbo la Kakonko na wakati tunapeleka umeme katika vijiji hivyo baadhi ya vitongoji vilifikiwa katika awamu ya pili ya REA na awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Sasa awamu ya tatu mzunguko wa pili itapeleka umeme katika vijiji lakini na baadhi ya vitongoji pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kakonko lipo katika awamu ya pili (b) ya mraji jazilizi wa umeme katika vitongoji. Jumla ya vitongoji 49 vitapatiwa umeme katika Jimbo la Kakonko na mradi huu wa jazilizi unaanza kuanzia mwezi Aprili. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha, vitongoji vya Jimbo la Kakonko lakini na vitongoji vingine vingi nchini vitaendelea kupelekewa umeme taratibu ikiwa ni pamoja na taasisi za umma. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Uhitaji wa viwanda kwa ajili ya kuchakata muhogo katika Jimbo la Vunjo unafanana sana na uhitaji wa huduma hiyo katika Jimbo la Buyungu. Jimbo la Buyungu na Wilaya ya Kakonko kwa ujumla ni wakulima wazuri sana wa zao la Muhogo. Tatizo letu ni upatikanaji wa mashine hizo za kuchakata na kuweza kupata unga na kuboresha thamani ya zao hilo, lakini pia ni bei…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali, je, ni lini tutapata mashine hizo za kuchakata unga wa Muhogo katika Wilaya yetu ya Buyungu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba kupitia shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO tayari tuna teknolojia mbalimbali na hasa za kuchakata mazao mbalimbali ikiwemo kuchakata muhogo. SIDO tayari kupitia ofisi za mikoa na hasa katika Mkoa wa Kigoma tayari tuna mashine hizo za kuchakata muhogo katika ofisi za Kibondo DC, Kakonko, Kasulu na Uvinza. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kupitia Ofisi zetu za SIDO, Mkoa wa Kigoma aweze kuwasiliana nao ili kuona kama atapata mashine kulingana na mahitaji yake ambayo yeye anaomba katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kama katika mashine hizo ambazo zipo katika Mkoa wa Kigoma itakuwa kwamba hazitoshelezi mahitaji yake basi nimhakikishie SIDO tupo tayari kuwasiliana nae ili tuweze kutengeneza mashine zinazokidhi mahitaji ya Mheshimiwa Mbunge na wajasiriamali katika Jimbo lake la Buyungu. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ujenzi huu ni ahadi ya muda mrefu, ni miaka sita sasa lakini kama ambavyo ameweza kutoa majibu utekelezaji wake umeanza kwa kuweka kifusi katika Mji ule wa Kakonko. Ni miezi minne sasa shughuli za biashara katika Mji ule hazifanyiki, je, Serikali iko tayari angalau kifusi kiweze kusawazishwa katika maeneo yale ili wananchi waendelee na shughuli zao wakati taratibu hizo nyingine zikifanyika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kakonko – Kinonko – Nyakayenze - Muhange na Kasanda - Gwanumpu - Mgunzu ni barabara ambayo iko chini ya TARURA. Barabara hii imeharibika sana pamoja na kwamba ni maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa, wananchi hawawezi kusafirisha mazao yao. Je, nini jibu la Serikali kuhusiana na suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaiuliza Serikali kwamba ni kwa nini sasa tusisambaze kile kifusi ili shughuli zingine ziendelee. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi ni kwamba barabara ile inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa hiyo, kile kifusi ni sehemu tu ya process za kukamilisha barabara ile. Kama tulivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba kufikia mwezi Mei, yaani mwezi ujao ile barabara itakuwa imekamilika kwa kiwango cha lami kwa sababu TARURA wako kazini. Hapa napozungumza wanasikia, nina hakika hilo zoezi litakuwa linaendelea na kazi inafanyika.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameainisha barabara ambazo zimeharibika sana na kuiomba Serikali iweze kuzifanyia kazi. Nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini na baada ya hapo nafikiri sisi na TARURA katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko tutakaa pamoja kuhakikisha barabara hiyo inajengwa ili kuondoa hiyo adha ambayo wananchi wanaipata. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kwenda eneo lenyewe la mgogoro ili aweze kujionea hali halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ikidhihirika kwamba katika utaratibu huo wa kugawa mipaka kuna makosa ambayo yatakuwa yamejitokeza wakati huo: Serikali iko tayari kuchukua hatua kwa wale ambao watakuwa wamekiuka taratibu za utoaji mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Kamamba ni: Je, nipo tayari kwenda katika eneo hilo ili nikajionee mwenyewe huo mgogoro? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya kipindi hiki cha Bunge la Bajeti nikipata nafasi ambayo itaniruhusu kuweza kwenda kwa sababu ni sehemu ya wajibu wangu kuyajua, kuyaona na kusikiliza changamoto za wananchi, nimhakikishie tu kwamba naenda kupanga ratiba na nitajitahidi nimjulishe tuweko pamoja ili kwa kushirikiana na maafisa kutoka hiyo Idara ya Wakimbizi, tuone namna ambavyo tunaenda kutatua hiyo changamoto ambayo kwa sasa wananchi inawakabili. Kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba, nipo tayari kufuatana naye kwenda katika eneo.

Mheshimiwa Spika, swali lingine ni: Je, ikidhihirika kama kuna makosa kuna watu wamefanya mambo mengine, mengine, Serikali ipo tayari kuchukua hatua? Serikali ipo kwa ajili ya kuwatetea, kuwasemea na kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi. Tumegundua kuna baadhi ya mambo yanafanywa na baadhi ya maafisa au baadhi ya watu ambayo yanavunja utaratibu na sheria katika maeneo haya. Kama Serikali tuko tayari kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wengine wawe ni funzo na wasiendelee kufanya makosa hayo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakimbizi hawa tuliamua kuwapokea kwa sababu ya Mkataba wa Kimataifa ambao tuliukubali sisi wenyewe, kwamba ikitokea machafuko katika nchi fulani, basi kama wakija na tuki-prove kwamba kweli kuna tatizo, sisi tunawapokea.

Mheshimiwa Spika, pia tulikubaliana kwamba migogoro ikimalizika katika maeneo yao, sisi tupo tayari kuwarejesha katika maeneo yao kwa kushirikiana na mashirika na kwa kushirikiana na nchi zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu kwamba eneo hili ikitokea wakimbizi hawa wameondoka na ikawa hakuna machafuko, maana yake ni kwamba eneo hili tutalirejesha kwa Serikali, halafu Serikali itaona namna ya kufanya. Unless ikitokea fujo nyingine huko kwenye nchi za wenzetu ikawafanya wakimbizi waje, tutawapokea na kuwahifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo ameyatoa ametaja mradi wa maji katika Kijiji cha Muhange ambao unapata maji kutoka Mto Mgendezi kwenda Muhange Centre na kwenda Muhange ya Juu. Hata hivyo mradi huu sasa maji yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwasababu ni machafu. Lakini vilevile mradi huu haukukamilika kama ilivyokusudiwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huu?

Pili, kutokana na mradi wa maji na changamoto hizi ambazo nimezitaja, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili akazione hizo changamoto na hatimaye kutoa suluhu ya miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kusema nimesikitika kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge anasema maji ni machafu na mradi haujakamilika vizuri kwa sababu swali lake la pili ni ombi la kuambatana na mimi nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja na nitakwenda kujihakikishia na wakati tunaendelea kukamilisha session hii ya Bunge ninatoa maagizo kwa Meneja wa eneo lile aweze kuwajibika haya maji yaweze kufanyiwa treatment kadri ya utaalamu wetu wa Wizara ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo ameyatoa ametaja mradi wa maji katika Kijiji cha Muhange ambao unapata maji kutoka Mto Mgendezi kwenda Muhange Centre na kwenda Muhange ya Juu. Hata hivyo mradi huu sasa maji yanayotoka hayafai kwa matumizi ya binadamu kwasababu ni machafu. Lakini vilevile mradi huu haukukamilika kama ilivyokusudiwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na mradi huu?

Pili, kutokana na mradi wa maji na changamoto hizi ambazo nimezitaja, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili akazione hizo changamoto na hatimaye kutoa suluhu ya miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kusema nimesikitika kuona kwamba Mheshimiwa Mbunge anasema maji ni machafu na mradi haujakamilika vizuri kwa sababu swali lake la pili ni ombi la kuambatana na mimi nipende kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja na nitakwenda kujihakikishia na wakati tunaendelea kukamilisha session hii ya Bunge ninatoa maagizo kwa Meneja wa eneo lile aweze kuwajibika haya maji yaweze kufanyiwa treatment kadri ya utaalamu wetu wa Wizara ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa Chuo cha Ufundi VETA ambao unawakabili wananchi wa Wilaya ya Igunga unafanana sana na uhitaji wa chuo hicho katika Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lini Serikali itajenga chuo cha ufundi VETA katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamamba Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuwa na Chuo cha VETA katika kila Wilaya hapa nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko makini, kwa hivi sasa tunakamilisha ujenzi wa vyuo hivi 29 katika Wilaya hizi 29 nchini.

Baada ya awamu hii kukamilika Serikali tutajipanga vema kulingana na upatikanaji wa fedha tutahakikisha kwamba tunakwenda kujenga chuo katika kila Wilaya hapa nchini. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Serikali ambayo yametolewa na Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, zimetengwa milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu.

Je, Serikali lini itapeleka hizo fedha milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ukamilishaji wa zahanati hizo tatu utasababisha uhitaji mkubwa wa wataalam katika kada ya afya ambapo bado mpaka muda huu tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika kada hiyo ya afya.

Je, lini sasa Serikali itapeleka watumishi wa kutosheleza mahitaji ya watumishi wa kada ya afya katika wilaya ya Kakonko? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ambazo zimetengwa kwenye mwaka huu wa fedha 2021/2022 zitaendelea kupelekwa kwenye majimbo yetu, kwenye kata zetu kadiri zinavyopatikana. Kwa hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka huu wa fedha fedha hizi zitapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hizi tatu katika Jimbo hili la Kakonko.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la watumishi; ujenzi wa zahanati na vituo vya afya unaenda sambamba na mipango ya ajira kwa ajili ya watumishi wetu kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma katika vituo hivyo. Kwa hivyo, pamoja na ujenzi, lakini pia mipango ya ajira inaendelea kufanywa na vibali katika mwaka huu wa fedha vinaandaliwa kwa ajili ya kuajiri watumishi kwenda kutoa huduma za afya katika vituo hivyo. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba, suala hilo pia litakwenda sambamba na ujenzi wa vituo katika maeneo hayo. Ahsante.