Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Aloyce John Kamamba (5 total)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA Aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini vijiji vyote vya Wilaya ya Kakonko havijapata umeme?

(b) Je, ni lini vijiji hivyo vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Buyungu lina jumla ya vijiji 44, vijiji 40 tayari vinapatiwa umeme kupitia awamu ya pili na ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini. Kazi inayoendelea sasa ni kuunganisha umeme katika vijiji 22 kwa wateja ambavyo vilipata umeme tayari ili kukamilisha mpango kazi aliyopewa mkandarasi katika eneo hilo. Kazi hiyo, inatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2021.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa usambazaji wa umeme vijijini umekuwa unafanyika kwa awamu, vijiji vinne vilivyobaki ambavyo ni Kijiji vya Rumashi, Nyamtukuza, Nyabibuye na Kinyinya viko katika mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili utakaoanza mwezi Februari 2021 na kukamilika Septemba, 2022.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

Mwaka 2015 wakati wa Kampeni, Mhe. Rais aliahidi kujenga barabara ya kilometa tatu katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya.

Je, kwa nini ahadi hiyo haijatekelezwa na ni lini sasa itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa awamu. Katika mwaka wa fedha 2020, Serikali imeanza ujenzi wa barabara yenye urefu wa mita 630 kwa kiwango cha lami katika Mji wa Kakonko itakayogharimu shilingi milioni 500. Ujenzi huu umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barababara nchini ikiwemo Wilaya ya Kakonko kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini miradi ya maji katika Mji wa Kakonko kwa muda mrefu haijakamilika?

(b) Je, ni lini Mji wa Kakonko na vitongoji vyake vitapata maji safi na salama ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi Desemba, 2020 miradi 15 ilikuwa inatekelezwa katika Wilaya ya Kakonko ambapo miradi 14 imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi, mradi mmoja uliobaki ni mradi wa Kakonko ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kuhudumia Mji wa Kakonko pamoja na kijiji cha Kasuga.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Kakonko unatekelezwa na RUWASA kwa kutumia Wataalam wake wa ndani kwa ajili ya kuukamilisha. Utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ambayo inahusisha ulazaji wa bomba kilometa 35 na ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 500 kila moja utakamilika mwezi Desemba mwaka 2021 na kunufaisha Mji wa Kakonko pamoja na vijiji jirani vya Kasuga, Mbizi, Kanyonza pamoja na Kata ya Kiziguzigu yenye Vijiji vya Kiziguzigu, Kibingo, Kiyobera na Ruyenzi.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itahusu kufanya upanuzi kwa kulaza mabomba urefu wa kilometa 78 kuelekea vijiji vya Njoomlole, Muganza, Kihomoka na Nyakayenzi ambapo itakamilika mwezi Juni, mwaka 2022.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali pia imepanga kujenga miradi mipya katika Vijiji vya Chilambo na Kinonko, ukarabati na utanuzi wa mradi wa Muhange kwenda Muhange Juu na Shule ya Sekondari Ndalichako pamoja na kuchimba visima virefu viwili katika Vijiji vya Chilambo na Nyakiyobe.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Zahanati na Vituo vya Afya katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati na Vituo vya vya Afya vya kimkakati nchini, ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 38.15 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 758 kote nchini. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imetengewa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha za makato ya tozo za miamala ya simu shilingi bilioni 55.25 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 221 kwenye Tarafa zisizo na Vituo vya Afya vyenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imepokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Tarafa ya Nyaronga kata ya Gwalama.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kujenga zahanati na vituo vya afya katika Wilaya ya Kakonko na nchini kote katika maeneo ya kimkakati kulingana na vigezo vilivyowekwa badala ya kila Kijiji na kila Kata. Ahsante.