Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Alexander Pastory Mnyeti (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Wanamisungwi kwa kunipitisha bila kupingwa na Madiwani wangu wote 27 na hatimaye sasa tupo humu kwa ajili ya kuwatumikia Wanamisungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, mchango wangu nitajikita kwenye mambo matatu, jambo la kwanza ni kweli kwamba Taifa letu msingi wake mkubwa ni kilimo na kwa sababu hiyo tuna kila sababu ya kuelekeza nguvu kubwa kwenye kilimo tuwasaidie wakulima wetu hawa ili waweze kuleta tija kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mashamba makubwa ambayo Serikali iliwapa wawekezaji ili wayaendeleze, lakini kwa masikitiko makubwa mashamba hayo mengi yametelekezwa na hao wawekezaji na hakuna kinachoendelea. Sasa niombe Wizara ya Ardhi, kama kuna namna yoyote ya kufanya mashamba hayo ama yarudi kwa wawekezaji wengine ama yarudi kwa wananchi ili wananchi waweze kuzalisha. Mashamba hayo wawekezaji unakuta mwekezaji mmoja anamiliki mashamba ekari 20,000, wengine ekari 50,000, wengine hivi, lakini ukiangalia uendelezaji wa mashamba hayo ni asilimia nne hadi 10, eneo lingine lililobaki lote liko wazi halilimwi na wananchi wanashangaa Serikali inashangaa na mwekezaji anashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama kweli lengo letu ni kuzuia kuagiza vitu nje ya nchi, hebu basi tutengeneze mazingira ya kuzalisha hayo mashamba yafanye kazi ili basi tuongeze pato la Taifa kwa namna hiyo, vinginevyo tutaendelea kuagiza choroko, ngono, nyanya, vitunguu, kila kitu tunaagiza kutoka nje lakini mashamba tunayo hayafanyiwi kazi. Ukienda kule Bassutu kuna mashamba ngano, tunasema tunaagiza ngano, wakati mashamba tunayo lakini hakuna anayeyalima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuko serious na hii mipango, otherwise mipango ya kwenye karatasi kama kweli tunataka tutoke hapa tulipo, yako mambo makubwa ambayo tunatakiwa tuchukue hatua ili basi tuweze kutoka hapa tulipokwama. Mashamba yametekelezwa, nenda Lotiana mashamba makubwa yametekelezwa. Leo Tanzania bado tunaagiza nyama kutoka nje ya nchi. Hii mipango, ni kweli ni mipango mizuri lakini utekelezaji wake mbona tunakwama, mashamba yametekelezwa, hatuendi kwenye kugota kwenye pointi ya kwamba tunatokaje kwenye hili tatizo lililokwamisha, haya makaratasi ni mazuri kwa sababu yameandikwa na Professors, ma-PhD holder lakini utekelezaji wake. Nazungumza utekelezaji wa namna gani tunakwama hapo tulipokwamia. Kwa hiyo, naomba hili niishauri sana Serikali kama kweli tuko serious hebu mtoke hapa tulipokwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumeanzisha viwanda vingi sana kwenye Taifa letu kwa muda mfupi, hongera sana Serikali kwa kazi hii nzuri. Hata hivyo, nasikitika kukujulisha kwamba viwanda hivi baada ya muda vitakufa vyote, kwa sababu hatuna malighafi yakuendesha hivyo viwanda, tunazalisha wapi? Unaniambia tunaanzisha viwanda ni kweli kule Iringa viwanda vya kuchakata mbao, lakini viwanda hivi miti iko wapi? Miti iko wapi, viwanda vinaanzishwa kule Misungwi, vinaanzishwa Kahama, vinaanzishwa wapi vya kuchakata pamba, pamba iko wapi? Tuwahamasishe wakulima wetu walime, tuwawezeshe pembejeo za kilimo walime. Hii Habari ya kumfurahisha mkuu wa nchi kwamba tunaanzisha viwanda, halafu baada ya miaka sita vimekufa, hii nataka niseme tutashindwa na tunashindwa very soon kwa sababu hatuwahamasishi wananchi kulima, hatuwatengenezei mazingira mazuri wananchi wetu waweze kulima, waweze kupatiwa pembejeo za kilimo, matrekta na kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kiwanda chetu cha mbolea; leo mbolea tunanunua 60,000 mpaka 55,000 kwa mfuko wa kilo 25 mpaka 50. Sasa tuna Kiwanda chetu kule Minjingu, kiwanda peke kwenye Taifa letu, lakini Serikali ni kama wamekipuuza, bado wanaagiza mbolea nje ya nchi, inafika mbolea hapa kwa 50,000 mpaka 60,000, lakini kile kiwanda kipo, Serikali ikikiwezesha kidogo tunaweza tukanunua mbolea 20,000 mpaka 15,000 kwa sababu tuna uwezo wa kutengeneza mbolea yetu wenyewe kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka niwaambie….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nitazungumzia mambo matatu. Jambo la Kwanza, mwaka 2010 wananchi waliokuwa wanaishi karibu na ile Barabara ya kutoka Geita kwenda Usagara walilipwa fidia zao, lakini wananchi kama tisa hivi wakasalia wakidai jumla ya shilingi milioni 30. Tangu mwaka 2010 mpaka leo wananchi hao wanadai milioni 30, wanaidai Serikali, haya ni mambo ya aibu, milioni 30 kudaiwa na wananchi maskini, waliowanyang’anya maeneo yao wakapitisha barabara. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hilo alichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule Misungwi tuna hili Daraja la Kigongo kwenda Sengerema, daraja hili wale wakandarasi walipewa tender hiyo na sasa wanaendelea vizuri na ujenzi, lakini cha kusikitisha wamevamia milima ya wananchi wanaponda kokoto wanachukua bila utaratibu bila malipo ya aina yoyote. Mheshimiwa Rais alivyopita pale jambo hili liliibuliwa na wananchi na Mheshimiwa Rais akaagiza twende tukalishughulike. Tumekwenda kushughulika na jambo hilo tukaonyeshwa dharau ya juu, akaja Mheshimiwa Waziri tukamweleza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kumjulisha kwamba tangu ameondoka hakuna kilichofanywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri, yeye ndiye Waziri wa Ujenzi, anakuja pale anatoa maelekezo kwa wakandarasi aliowapa tender mwenyewe lakini bado watu hao hawafuati alichowaagiza. Hii nayo ni aibu kubwa. Nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, tupunguze sana kutoa tender hizi za ujenzi kwa wakandarasi wa Kichina wana dharau sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunashindwa kutengeneza wakandarasi wetu wenye nguvu ndani ya nchi yetu, tunashindwa nini kuwawezesha watu wetu wa ndani ili waweze kujenga barabara zetu na miradi mingine. Pale kwenye ule Mradi wa Kigongo – Busisi wale Wachina wanatengeneza, lakini hakuna mkandarasi mwenza wa Tanzania anayeangalia nini kinajengwa ili keshokutwa tujenge na sisi wenyewe madaraja yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewaacha wale Wachina, wanajenga wanavyotaka wenyewe, wakijenga chini ya kiwango hakuna anayejua, wakiweka mawe badala ya cement hakuna anayejua, mwisho wa siku tunakabidhiwa vitu hivi vikija kuanza kuharibika hakuna anayeweza kuvikarabati mpaka tuwatafute Wachina wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kweli tupo serious, otherwise nataka nitoe mfano mmoja, waulizeni Wazambia walifanywa nini na Wachina. Waliamua kukabidhi nchi yao kwa Wachina, leo tunavyozungumza kila kitu kimekamatwa na Wachina. Sasa na sisi tunarudi kulekule, madaraja yote Wachina, barabara zote Wachina, makalvati Wachina, majengo yote Wachina, kila kona Wachina, kila mtu Mchina sasa tunafanya nini? Hivi kweli hatuna, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu pale, hivi hajafundishwa mainjia vijana wetu wa Kitanzania wanaoweza kujenga madaraja. Sasa kama hajafundisha maana yake tunapotezeana muda sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hilo Waziri aliangalie, lakini hapo hapo kwenye hilo daraja kuna vijana wetu wameomba kazi, wanaozunguka maeneo hayo, wanaoishi katika maeneo hayo, mpaka kesho hakuna hata mmoja anayepewa kazi pale. Wale Wachina wana watu wao, tunaambiwa kwamba ile kampuni ya Kichina imeingia hapo miaka ya 70 au 60 kwa hiyo wana watu wao sijui wanawatoa wapi kuja kufanya kazi pale Misungwi, lakini wale watu wa Kigongo Ferry pale hawapati kazi, hata ndogo ndogo zile hawapewi. Mheshimiwa Waziri alikuja Misungwi nikamwambia jambo hili, lakini tangu ameondoka hakuna kilichofanyika. Sasa kama ni mambo ya porojo, basi tuendelee kupiga porojo, mwisho wa siku hakuna kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, nizungumzie kuhusu Shirika la Ndege. Sisi kule Mwanza unaingia kwenye mtandao unafanya booking, tunaipongeza Serikali kwa kununua ndege nyingi za kutosha, lakini unaingia unafanya booking unaambiwa ndege imejaa. Wakala anakwambia hebu subiri nikufanyie sarakasi upate tiketi ya kwenda Dar es Salaam, anafanya sarakasi yaani wakala wa tiketi naye amekuwa bosi sasa hivi, anafanya sarakasi unapata tiketi ya bahati nasibu, ukiingia kwenye ndege hakuna watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani tunahujumiana sisi wenyewe kwa wenyewe na huu mchezo Mheshimiwa Waziri nataka nimwambie, huu mchezo upo kwenye Wizara yake. Unafanya booking hakuna nafasi, ukiingia kwenye ndege ukibahatisha hukuti watu kwenye ndege bombardier ile inasafiri na watu 15 watu 20, lakini kwenye kutafuta unaambiwa tiketi zimejaa, tafuta usafiri mwingine. Hapa tunamkomesha nani? Ni nani tunamkomesha, tunajikaanga kwa mafuta yetu wenyewe Watanzania, ndege hizi mwisho wa siku zitakuwa ni za kupigia picha, watu wanatafuta tiketi, tiketi hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo hilo, ukifanya booking kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam unaambiwa tiketi laki tano. Ukiangalia kwenye ile ndege nyingine sitaki kuitaja jina hapa unakutana na tiketi ya laki mbili, halafu ukilipa hiyo laki tano ukiingia kwenye ndege hakuna watu, kwa nini Waziri asiweke bei reasonable ili watu wengi wa kawaida wapande ndege na ndege zetu zijae. Tunamhujumu nani? Tunahujumiana sisi wenyewe Watanzania, mwisho wa siku hizi ndege zitakuwa ni ya kupigia picha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS Mwanza unaweza ukazunguka nchi nzima ukitoka Dodoma hapa utaenda vizuri, utaenda vizuri ukishaona kibao kinasema, sasa unaingia Mkoa wa Mwanza unaanza kukutana na sarakasi za mabonde, viraka, mabarabara yasiyoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, maeneo mengine wanataka lami na sisi tunataka hayo hayo mabonde yadhibitiwe TANROADS Mwanza kuna shida gani? Kwa nini ukifika Mwanza tu ndio unakutana na mabonde kuinama unaingia kwenye majaluba mule mule kwenye lami kuna majaluba mule mule kuna matuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hebu iangalie vizuri Mwanza kuna shida gani Mwanza ni mkoa mkubwa huo ndio ukweli, haya mabonde mabonde ni aibu tunatiana aibu. Kama hatuwezi kutengeneza barabara basi tuseme hatuwezi kutengeneza barabara, lakini sio kila siku tunaziba viraka mara kiraka hiki kimepasuka hapa, mara kinazibwa hapa. Hizo gharama mara mia tano zikatengeneze mabarabara mapya huko Kusini kama hamuwezi, kwa sababu imeonekana kama ni deal. Kila mwaka mnatengeneza mabarabara hii ni deal ya watu kila siku mnaziba viraka, kwa sababu ya deal kila siku deal. Pale Wilayani kwangu Misungwi kuna kilometa karibia 20 kila mwaka TANROADS wanatengeneza barabara kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu naona huu ni usanii na tunaiba pesa za watu. Jambo la mwisho limesemwa hapa kwamba, daraja la Busisi lisiendelee kujengwa mpaka ipatikane certificate ya mazingira. Yaani unaaga kwa mumeo kwamba nakwenda kazini kuja kusema kitu kama hicho kwamba, daraja lisijengwe eti kwa sababu hakuna certificate ya mazingira! Sisi tunasema hivi mazingira ni ya kwetu, daraja ni la kwetu, ziwa ni la kwetu, kila kitu ni cha kwetu tunahitaji daraja lijengwe na kwa wakati na likamilike na tunahitaji kwa muda mfupi. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kupongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya chini ya Waziri Bashungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mchango mfupi sana kwenye Wizara hii ya Michezo, jambo la kwanza ni makato yanayofanywa na Serikali baada ya mechi. Tunafahamu wote kwamba kuandaa timu au kuandaa mchezo ama mchezo ni gharama kubwa, lakini inasikitisha sana baada ya mechi, Serikali mmekuwa mkivamia hayo mapato na kuanza kuyakatakata vipande vipande. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapoandaa mechi tatizo la Serikali wanakwenda kuangalia nini kimepatikana siku ya mechi. Hawaangalii umetumia shilingi ngapi kuandaa hiyo mechi. Tafsiri yake ni kwamba wanakuja wanakatakata mpaka wanakula mtaji halafu kesho timu zinashindwa kuandaa mechi. Serikali haijui mchezaji ili ahudhurie mechi moja anahitaji kula, kuvaa, kutibiwa, kunywa maji, kwenda mazoezi na kufundishwa na mwalimu aliyebobea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote hayo Serikali hawayajui na hawataki kuyasikia. Siku ya mechi utawaona wako getini TRA wanakata asilimia 18, Halmashauri wanakata asilimia 10, BMT wanakata asilimia tatu, pasipo kujua umewekeza shilingi ngapi mpaka kufika siku ya mechi. Sasa kwa mfano, unatumia shilingi milioni nane kuandaa mechi moja, halafu getini unapata shilingi 2,100,000. Lakini fedha zote hizo Serikali inaziangalia na inakwenda kuzikata pasipo kujua umetumia shilingi ngapi kwenye kuandaa hiyo mechi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona huu ni uonevu na kwa stahili hii hatuwezi kuendeleza mpira wa miguu kwa namna yoyote ile, vinginevyo kama tunapiga story ili muda uende hakuna, haitawezekana. Hii kuandaa timu imekuwa ni kama watu wanapiga story sio jambo rahisi kama tunavyofikiria. Wachezaji hawa wanakula, wanatibiwa, wanaumwa, ankle, magoti, sijui visigino vimefanya nini. Ukimtibu mpaka kumpeleka kwenye mechi ni gharama kubwa, lakini inasikitisha sana wakati unafanya hayo yote Serikali haipo. Unawatibu wachezaji Serikali haipo, unalipa kocha Serikali haipo, Serikali inakuja kuonekana siku ya mechi inataka asilimia 18. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akaliangalie hili vizuri akae na wenzake muone mnawezaje kusaidia hivi vilabu ambavyo vinasuasua havina hata shilingi ya kuendesha huu mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tunampongeza sana Azam kwa udhamini mkubwa wa mwakani ambao ameufanya, lakini si tu mwakani, Azam hata mwaka huu, mwaka jana, mwaka juzi walau chochote ameweka kwenye mpira huu wa miguu na tayari ameanza kwenye michezo mingine kama ngumi, netball na michezo mingine. Tunampongeza sana huyu mwekezaji, mwekezaji mzawa tunaomba aendelee kufanya hivi kwa sababu ndio njia pekee ya kuinua soka la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuombe Mheshimiwa Waziri kuna mdhamini mwingine anaitwa Vodacom ambayo ligi inayokwisha sasa ambayo bado mechi tatu, nne kuisha. mdhamini huyu ndio mdhamini mkuu kwenye ligi ya Vodacom. Nasikitika kukujulisha mpaka sasa hajawahi kuweka hata shilingi 10 pamoja na udhamini huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila vilabu vinapouliza jambo hili limekuwa likipigwa chenga. Mheshimiwa Waziri ingilia kati, saidia hivi vilabu vipate haki yao hata kama anaacha, lakini haki ya vilabu vimepatikana ili waendelee na mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, najua hili linaweza likachelewa sana kueleweka lakini ndio ukweli, tukizungumza siasa ya mpira katika nchi hii tunazungumza siasa ya Simba na Yanga, lakini Simba na Yanga hawana msaada wowote kwenye kuunda timu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusisubiri matokeo ya timu ya Taifa ifanye vizuri halafu akili zetu na nguvu zetu zote tumeelekeza kwenye Simba na Yanga. Simba na Yanga hapa wote tunajua ina nguvu kubwa, ina political mileage kila mtu anashabikia na wengine tuko humu tunashabikia ni sawa kabisa. Lakini tusiulize kwa nini timu yetu ya Taifa haifanyi vizuri, ni kwa sababu akili zetu na nguvu zetu zote tumeelekeza kwenye Simba na Yanga, tumesahau vilabu vidogo ambavyo ndivyo vyenye mchango kwenye timu yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikutolee mfano mmoja, ukiongelea habari ya Simba, juzi Simba wamecheza robo fainali ya Kombe la Afrika tunawapongeza sana. Lakini nikutolee mfano mmoja kule, lineup ya Simba wachezaji watatu tu ndio Watanzania golikipa, namba mbili na namba tatu basi. Namba nne Mkenya, namba tano Ghana, namba sita Mganda, namba saba Mozambique, namba nane Zambia, namba tisa Congo, namba 10 Zambia, 11 Rwanda. Huwezi kupata timu ya Taifa kama wachezaji wa Simba na Yanga wote lineup wanatoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule Yanga, mara sijui Tusiletusinde, mara Tunombetunombe, mara Mandama, sijui vitu gani. (Kicheko)

Nataka nikuambie tunajenga Simba na Yanga kwa nguvu kubwa lakini hatujengi timu ya Taifa kwa sababu tunapoita wachezaji wa timu ya Taifa hatuwaiti wale kwa sababu wanatoka nje ya Taifa letu. (Makofi)

Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri kama kweli tunataka tujenge msingi wa mpira katika nchi hii, haya mambo ya Simba na Yanga tungeweka baadaye ikawa ni second option. Kipaumbele ikawa ni wachezaji wetu wa kitanzania wazawa, ambao tunaweza tukawatumia kwenye timu yetu ya Taifa na wakaleta tija kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwenye Taifa letu kila mtu ni Simba ama ni Yanga; anayejua mpira yuko Simba ama Yanga. Simba Yanga, Simba Yanga, Simba Yanga nonsense, hatuwezi kila saa hapa tunaongelea mambo ya Simba Yanga, Simba Yanga, which is Simba and Yanga. Kama tunazungumza habari ya maendeleo ya mpira ya miguu kwenye Taifa letu, Simba na Yanga ziwe second option.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, tuunde wachezaji wetu wa kizawa wanaoweza kuleta tija kwenye Taifa letu, tofauti na hapo tukiendelea kupiga hizi story tutapoteza muda na hakuna tutakachopata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)