Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maimuna Salum Mtanda (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa ridhaa yako kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa ridhaa ya kupeperusha bendera katika Jimbo la Newala Vijijini. Pia nipongeze na kuishukuru familia yangu kwa support wakati wote wa uchaguzi hadi sasa. Kipekee pia niwashukuru wapigakura wa Jimbo la Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Novemba, 2020 pamoja na ile ya 2015. Ni hotuba ambazo nimepitia zote, hotuba ambazo zina maono, hotuba ambazo kwa namna ya kipekee, hasa ile ya 2015, ilipotekelezwa pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilikifanya Chama Cha Mapinduzi kutembea kifua mbele wakati wa Uchaguzi wa Mwaka 2020. Nina imani hotuba hii ambayo ameitoa 2020 tukiitekeleza hivi inavyotakiwa 2025 itakuwa ni kuteleza kama kwenye ganda la ndizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi, tumeyaona. Amesimamia vizuri miundombinu katika nchi hii kuanzia afya, barabara, elimu na sekta nyingine zote. Tunampongeza sana kwa kile ambacho amekifanya kwa kusaidiana na wasaidizi wake ambao ni Mawaziri wetu. Hata hivyo, zipo changamoto kadhaa ambazo zikisimamiwa na kutekelezwa ipasavyo nadhani nchi hii itasonga mbele sana zaidi ya hapa ambapo tupo sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanazalisha kwa kiasi kikubwa zao la korosho, zao ambalo linaipatia nchi hii uchumi na fedha nyingi za kigeni, lakini kuna changamoto ya barabara yetu ya kiuchumi, barabara ambayo inatumika kupitisha zao la korosho kutoka kwenye maeneo ya wakulima kuelekea bandarini. Barabara ile imeshaombewa muda mrefu lakini haikamiliki. Ni barabara ya kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi hadi Nachingwea. Barabara ile hadi sasa imekamilishwa kwa kiwango cha lami kwa kilometa 50 tu. Niombe wenzetu wa Ujenzi kuharakisha ukamilishaji wa barabara ile ili mazao ya wakulima yapate kusafirishwa kwa urahisi kuelekea bandarini, lakini pia kuvinusuru vyombo ambavyo vinasafirisha mazao hayo kuelekea bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ambayo ipo Jimbo la Newala Vijijini imehamia mwaka jana katika eneo lake jipya la utawala. Eneo lile halina jengo la utawala na kwenye hotuba tumeelezwa na kusisitizwa suala la utawala bora. Utawala Bora ni pamoja na kuwepo na maeneo ya watumishi kutendea kazi, lakini Halmashauri ya Wilaya ya Newala haina jengo la Utawala. Niombe wahusika na wasimamizi wa masuala ya utawala kwa maana ya TAMISEMI watuangalie kwa jicho la pekee ili watumishi wale wapatiwe jengo la utawala nao wafanye kazi katika mazingira yaliyoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Newala Vijijini kuna changamoto ya maeneo ya kutolea huduma ya afya. Zipo kata 22 lakini ni kata tatu tu ndizo ambazo zina vituo vya afya. Naomba Mheshimiwa anayesimamia afya atuangalie kwa jicho la kipekee tupate vituo vya afya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia naishukuru Wizara ya Fedha kwa uwasilishaji mzuri wa Mpango wa Miaka Mitano inayokuja kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Mpango huu, tuna maana kwamba ni mwelekezo wa Serikali kwa miaka mitano ijayo. Sasa ili kuutendea haki Mpango huu na yale matarajio tunayoyatarajia yaweze kupatikana vizuri, kuna mambo lazima yaboreshwe ikiwemo rasilimali watu, lazima iwepo, miundombinu iboreke na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza wenzetu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa sababu wametuwezesha na kutuelewa sisi Wananewala kwa kuwaendeleza na kuchukua majengo ambayo yalikuwa ya NDF ili kuwa VETA. Sisi Wananewala tuna kiu kubwa ya kupata ajira kwa vijana wetu, kwa hiyo, tukawakabidhi wenzetu wa Wizara ya Elimu majengo ili yatumike kama VETA na vijana wetu wakapate ujuzi, waweze kujiajiri wenyewe na kisha maendeleo ya watu yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema, lakini majengo yale yatatumiwa na Wilaya zaidi ya moja kwa maana ya Tandahimba, hakuna VETA, ni majirani zetu, watatumia pale; Masasi kwa maana ya Lulindi, hawana VETA, watatumia pale na Wananewala. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ituongezee au itujengee mabweni ili wanafunzi watakaoenda kusoma pale wapate elimu na ujuzi unaotosheleza bila kuhangaika, mwisho wa siku wakapate wao wenyewe kujiajiri na maendeleo ya nchi yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili maendeleo yaweze kupatikana, lazima miundombinu iboreshwe hasa barabara. Wananewala Vijijini wana barabara yao ambayo inaunganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa maana ya Wilaya ya Lindi Vijijini na Newala; barabara ya kutoka Mkwiti – Kitangali hadi Amkeni. Barabara ile ni ya vumbi, lakini ikiboreshwa kwa kiwango cha lami, tuna uhakika kabisa kwamba mawasiliano yatakuwa rahisi, watu watafanya biashara, watakuwa wanasafiri kutoka eneo moja na kwenda eneo lingine na kujipatia fedha ambazo wataenda kuendeleza maisha yao na kuachana na hali ambayo wanayo kwa sasa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ambayo inasimamia ujenzi, kwa sababu tunataka kuboresha au kuleta maendeleo ya watu, basi itujengee barabara ile kwa kiwango cha lami ili nasi maendeleo yetu yaweze kupatikana kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchangiaji ambaye amezungumzia suala la utafiti kwa vyuo vyetu vya kilimo, ni muhimu sana. Utafiti wa mazao ni muhimu sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze fedha kwenye vyuo vya utafiti ili waweze kufanya utafiti wa mara kwa mara ambapo watakuwa up to date na hali ya mabadiliko ya mazao yetu kwa kadri inavyojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanamtwara tunalima korosho ambazo zina magonjwa mbalimbali; ni kama binadamu, magonjwa yanabadilika kila leo. Kwa hiyo, tusipowekeza kwenye utafiti wakulima wetu wakapata kujua aina ya magonjwa ambayo yanajitokeza kwa wakati huo kupitia watafiti wale wa TARI Naliendele, nadhani tutakuwa hatufanyi chochote na uzalishaji wa zao la korosho utakuwa unapungua kadri ya siku zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niunganishe na Maafisa Ugani. Tunaomba Maafisa hawa wawepo kwenye vijiji vyetu, kwa sababu sasa hivi tunavuna lakini kiholela…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja, lakini tunaomba tupatiwe Maafisa Ugani ili wakawasimamie wakulima wetu ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa mara nyingine naunga mkono hoja. (Makofi)