Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haji Amour Haji (2 total)

MHE. HAJI AMOUR HAJI Aliuliza:-

Kwa kuwa Serikali imeruhusu uwepo wa Mawakala wa Ajira nchini:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya ajira za nje ya nchi kwa Vijana wetu?

(b) Je, ni upi mchango wa Mawakala wa ajira hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasadia vijana wetu kupata ajira za nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kubaini nchi za kimkakati zenye fursa za ajira za staha na kuingia makubaliano (bilateral agreement) na nchi husika; kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kuwa na ujuzi utakaowawezesha kushindania fursa za ajira ndani na nje ya nchi; na kujenga mfumo wa huduma za ajira ambao pamoja na mambo mengine utarahisisha utafutaji wa kazi nje ya nchi; kuweka mwongozo wa kuratibu shughuli za wakala binafsi wa huduma za ajira wanaopeleka watu nje ya nchi; na kufanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2014 ili kuweza kuendana na mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Juni, 2021 Mawakala wa ajira nchini wamechangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya vijana 39,273 wamepewa huduma ya ushauri nasaha (employment and career counseling). Aidha, vijana 19,509 wamepewa mafunzo ya watafutakazi, vijana 11,371 wameunganishwa na fursa za mafunzo ya utarajali na vijana 10,554 wameunganishwa na fursa za kazi ndani na nje ya nchi. Ahsante sana.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Chombo Maalum (Agency) kitakachosimamia shughuli zote za kampuni binafsi za ulinzi ili kuongeza wigo wa kiutendaji pamoja na kuwepo kwa sheria itakayosimamia kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni sababu ya kuanzisha chombo maalumu (Agency) cha kusimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Jeshi la Polisi linatosha kusimamia shughuli za makampuni hayo kama ilivyo sasa kwa sababu ndiyo taasisi iliyopewa mamlaka kisheria ya kutoa leseni na hati za umiliki wa silaha hapa nchini ambazo pia humilikiwa na makampuni hayo. Utaratibu huo hutoa urahisi wa kufuatilia mwenendo wa makampuni katika utunzaji na matumizi ya silaha hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria itakayosimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Tayari mapendekezo ya kutungwa kwa sheria hiyo yapo kwenye hatua zaa awali za mawasiliano baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Baada ya maridhiano kati ya Serikali zetu mbili kufikiwa, maandalizi ya sheria hiyo yataendelea kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.