Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya (59 total)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Ahadi hii ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami imeahidiwa kwa awamu mbili za Marais wetu, akiwemo Rais Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2010 alikuja Jimboni kwenye kampeni na akaahidi barabara hiyo kwa ujenzi wa kiwango cha lami. Pia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli naye alikuja 2015 naye aliahidi hivyo hivyo ujenzi wa barabara hyo kwa kiwango cha lami.

Swali ni lini fedha hizi zitapatikana kwasababu sasa hivi ni miaka 10 tunaahidiwa utafutaji wa hizo fedha, ni lini fedha hizo zitapatikana kwa ajili ya upembuzi yakinifu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili,kwa kuwa barabara hiyo inafungua mikoa mitatu na sasa hivi Wilaya ya Nyang’hwale inakimbia kiuchumi, barabara hayo yanaharibika na vumbi jingi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale, hususan pale Karumwa wananchi wanapata adha kubwa kwa vumbi kwasababu magari ni mengi.Je, ni lini Serikali itakomesha vumbi hilo na kuweza kuwanusuru wananchi wa Jimbo hilo na kuweza kuwanusuru wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale hususan Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale Karumwa kupata maradhi mbalimbali yakiwemo TB?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nassor Mbunge wa Nyang’hwale. Ni kweli barabara hii imeahidiwa na Mheshimiwa kama alivyosema Mheshimiwa wa Awamu ya Nne na Mheshimiwa wa Awamu ya Tano, lakini ni azma ya Serikali na ndiyo mpango wa Serikali kwamba katika Awamu hii ya Tano, kipindi cha pili, barabara zote zinazounganisha mikoa na wilaya lazima zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwahiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaamini katika kipindi hiki Serikali itapata fedha na barabara hii itajengwa. Barabara hii pia hata ukienda kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ipo imeahidiwa,kwahiyo ninahakika Serikali itatekeleza.Kwa maana hiyo tutakapokuwa tumejenga kwa kiwango cha lami maana yake hata lile vumbi linaloonekana Karumwa litakuwa limeondoka ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza. Kama alivyojibu Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni barabara ya kitaifa yaani National Road na ni barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Morogoro. Kutoka hapo Ifakara sehemu moja mpakani mwa Njombe na Morogoro, Mto Mfuji kuna kilomita takribani 225 na kwa kuwa barabara hii ni muhimu na ni barabara ya kitaifa, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Ifakara ng’ambo ya mto Lumemo kwenda kupita Mlimba, kwenda Mfuji, Madeke Njombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna haja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…

NAIBU SPIKA: Hilo ni swali la pili? Au hilo hilo la kwanza?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahi kufanya ziara Jimbo la Mlimba na katika ziara yake aliahidi ujenzi wa kilomita 60. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii walau kwa kilomita hizo 60?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Asenga kwa juhudi ambazo anazifanya katika kufuatilia barabara hii ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Kilombero wanafaidika na barabara hii ya lami ambayo wanaifuatilia. Baada ya maneno hayo, nitoe tu jibu la jumla, kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa kuzindua Bunge hili la Kumi na Mbili, ukurasa wa 26 na 27, Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba barabara zenye urefu kilomita 2500 ambazo zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami zitakamilishwa katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ameenda mbali zaidi kwenye hotuba kwamba pia barabara zingine ambazo zitaanza kujengwa zenye urefu wa kilomita 6006 ikiwepo barabara hii pia zitakamilishwa ambazo ni zile ambazo ziko kwenye ilani lakini na ahadi zake mwenyewe. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi barabara Serikali itazikamilisha kama ilivyoahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JACQEULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa niaba ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Rukwa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni mkoa wenye vivutio vya utalii, lakini pia Mkoa wa Rukwa unajishughulisha na masuala ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika. Mkoa wa Rukwa ni mkoa ambao umeshika nafasi ya tatu kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya nafaka. Pamoja na hivyo Serikali bado haijajenga uwanja huo. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kama ucheleweshaji wa ujenzi wa uwanja huu unasababisha udumavu wa ukuaji kiuchumi wa Mkoa wa Rukwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamekaa muda mrefu sana hawajapata uwanja wa ndege; je, ni lini Serikali itaanza kujenga uwanja wa ndege wa Mkoa wa Rukwa ili kuwafanya wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanufaike na matunda mazuri ya Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kuhakikisha kwamba uwanja huu unajengwa. Katika swali la kwanza la nyongeza ameeleza kwamba kuna vivutio vya utalii tunakubali uvuvi, lakini pia ni kati ya mkoa unaozalisha. Serikali tayari imeshapata fedha, sasa hivi kilichopo tu ni kuanza ujenzi. Kwa hiyo, kwa sababu hiyo Serikali imelitambua hili, hivyo, hakutakuwa na sababu ya kuwa na udumavu kwa sababu tayari uwanja huo utaanza haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaanza kujenga uwanja huo? Katika jibu langu la msingi nimesema kila kitu kimeshakamilika, ni taratibu tu za mwisho za kibenki ambazo lazima zifanyike ili uwanja huo uanze. Kama mkandarasi tayari ameshapatikana kwa hiyo, tuna hakika ujenzi utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba barabara hii ina umuhimu na sasa kwa miaka miwili imekuwa ikiwekwa kwenye bajeti na haikujengwa na amesema imetegwa shilingi bilioni 5, je, atuambie ni lini atatangaza tenda ili barabara hii ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa anajua wazi kwamba bilioni 5 haiwezi kujenga barabara na barabara hii iko kwenye Ilani ya uchaguzi mwaka 2015-2020 na 2020-2025 na Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni juzi hapa, je, yupo tayari kuweka fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ili kumaliza kilomita zingine 20 kufika 70 kufikia eneo la Haydom?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini jana pia aliuliza swali la nyongeza lakini leo pia ameleta swali la msingi, kwa hivyo, natambua jinsi anavyofuatilia barabara hii kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu. Nimhakikishie kwamba kwa kuwa tayari fedha za awali zimeshatengwa hizo shilingi bilioni 5, kwa hiyo, taratibu za awali zitaanza ikiwa ni pamoja na kutangaza tenda na kufanya shughuli za awali za kuanza ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu swali namba 28 kwamba Serikali imeahidi barabara zote ambazo imezitolea ahadi katika Ilani lakini pia ni ahadi za Rais katika kipindi cha miaka hii mitano zitatekelezwa ikiwa ni pamoja na barabara hii ya Karatu – Dongobesh - Haydom ambayo Mheshimiwa Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini anaiulizia. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufanya marekebisho, Naibu Waziri amesema Mbunge wa Mbinga Mjini mimi ni Mbunge wa Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Pia nashukuru katika bajeti inayokuja ametutengea kilometa 5. Hofu yangu ni kwamba ikiwa mpango utakuwa ni wa kilometa tano tano barabara hii tunaweza kuikamilisha kwa muda wa miaka kumi na sita na kidogo. Je, Serikali ipo tayari kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hii ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Jimbo la Nyasa na wananchi wa Mkoa wa jirani wa Njombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hali ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS kwa jimbo la Mbinga Vijijini sasa hivi hazipitiki ama zinapitika kwa shida sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzifanya barabara hizi zipitike msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimuombe radhi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba huyu ni Mbunge wa Mbinga Vijijini na si Mbinga Mjini. Kwa hiyo, hata wananchi huko wanajua kwamba Mheshimiwa wao wa Mbinga Vijijini yupo anatetea barabara zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, sasa nijibu maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge anafahamu mara baada ya kuteuliwa hii barabara ni kati ya barabara ambazo mimi nimebahatika kwenda kuzitembelea, kwa hiyo, ninaifahamu vizuri sana. Hata hivyo, tukubali tu kwamba ni jitihada za Serikali kwamba fedha inapopatikana hata kama ni kiasi kidogo zile barabara ziendelee kutengenezwa. Hata hizi kilometa 5 zilizotengenezwa zimesaidia sana kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe, kwa hiyo, magari makubwa yanayopita pale hayawezi kukwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tutatenga fedha zote, Serikali inafanya jitihada fedha zitakazopatikana naamini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha barabara hii. Kwa sasa kadri tunavyopata fedha tutaendelea kutengeneza barabara kwa awamu na ndiyo maana hata hizi kilometa tano zilizotengenezwa zimetoa msaada mkubwa sana. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka niulize swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo inawezekana nikayapokea au nisiyapokee.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Mtwara ambayo tulipokea takribani bilioni 153 kwa ajili ya matengenezo makubwa sana. Lakini cha kushangaza bandari hii kwa nini isitumike kwa meli kubwa ambazo zinaweza zikabeba mizigo? Kwa sasa hivi kuna kampuni moja ya meli ambayo kampuni hii inaitwa Sibatanza hawa watu ndiyo ambao wanaleta meli pale peke yao na kuja kufanya kazi ya uchukuzi.

Swali la pili kwa kuwa tumepoteza rasilimali nguvu kazi za watu takribani wachukuzi 6200 wamepoteza ajira kwenye Bandari ya Mtwara ni lini Naibu Waziri tutaongozana kwenda kuzungumza na wale wachukuzi ili waelewe hatma yao ya kazi zao za kila siku walizokuwa wanazifanya kwenye bandari ya Mtwara? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imewekeza shilingi bilioni si 153 lakini bilioni 157 kuboresha Bandari ya Mtwara kwa kujenga gati na kuwekeza fedha nyingi hizi ni ili kuhakikisha kwamba Bandari ya Mtwara inatumika kwa meli kubwa.

Sasa juhudi zinazofanyika mpaka sasa hivi kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, moja ni kwamba Serikali tayari imeshafanya usanifu kujenga chelezo kwa ajili ya kujenga meli yetu chini ya MSCL ambayo itakuwa na uwezo wa kufanya biashara kati ya bandari ya Mtwara na bandari zingine. Lakini tayari Serikali imeshamshawishi mfanyabiashara Dangote aweze kutumia Bandari ya Mtwara kuleta bidhaa zake lakini pia na kusafirisha bidhaa zake.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ushoroba wa Mtwara kuanzia Mtwara, Tunduru, Songea, Mbinga mpaka Mbambabay barabara hii imekamilika tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na upande wa wafanyabiashara wa Malawi kwamba waweze kutumia Bandari hii ya Mtwara, lakini pia mazungumzo yapo na upande wa Msumbiji Kaskazini Magharibi ili waweze kutumia bandari hiyo. Kwa maana hiyo tuna uhakika kwamba bandari hii itaendelea kufanyakazi kama ilivyokuwa imekusudiwa ndiyo maana Serikali imewekeza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongozana na Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga kwenda Mtwara mimi nasema hili halina shida naomba baada ya hapa tukubaliane lini tunakwenda lakini pia tunampongeza Mheshimiwa Mtenga kwa kuhakikisha kwamba bandari hii inafanyakazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE.ZUBERI M.KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye Bandari ya Mtwara, lakini commitment ya Serikali katika matumizi ya bandari ile bado haijaonekana. Mfano leo hii kule kuna kitengo cha mafuta (kuna pump ya mafuta ambayo inatakiwa wananchi wa Kanda ya Kusini wote wachukulie mafuta kwenye bandari ya Mtwara lakini ukienda kwa wafanyabiashara bado wanalalamika kwamba mafuta ya Mtwara yako bei juu kuliko Dar es Salaam, matokeo yake watu wanatoka Songea, wanatoka Lindi, wanatoka Tunduru wanafuata mafuta Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali namna bandari hii inaweza kutumika efficiently na sisi watu wa Kanda ya Kusini tukanufaika kwa kuwepo kwa bandari hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nini commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa ya Serikali ni kutengeneza miundombinu na tayari commitment ya Serikali imeonekana kuiboresha Bandari ya Mtwara ili iweze kufanya kazi kama ilivyopangwa na ndiyo maana katika jibu langu la msingi sasa tunatangaza na kuitangaza Bandari ya Mtwara ili iweze kutumika kwa sababu sasa inauwezo wa kupokea meli zote kubwa na tungeshauri wafanyabiashara wote waweze kutumia bandari ya Mtwara na hasa wale wa Ukanda wa Kusini. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba matumizi ya bandari ya Dar es Salaam yalisababisha uharibifu wa barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi kwenda Mtwara na hali ya barabara hiyo kwa sasa kwa kweli ni mbaya pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais aliagiza ikarabatiwe, lakini hali ni mbaya tunasafiri mpaka masaa saba badala ya masaa manne.

Je, Serikali iko tayari sasa kutenga fedha ya kutosha kuikarabati barabara hii kwa kiwango kinachotakiwa ili turudie hali yetu ya zamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la msingi ilikuwa ni bandari lakini ilikuwa linahusianisha na uharibifu wa barabara kwa sababu magari mengi yanaendelea kutumika. Naomba tu niseme baada ya hapa kwa sababu halikuwa swali la msingi, nitaomba nionane na Mheshimiwa Nape ili niweze kuona namna ambavyo Serikali imetenga fedha kwa sababu ni utaratibu wa Serikali kutenga fedha kufanya matengenezo kwenye barabara zote na hasa barabara muhimu kama hizo.

Lakini figure kamili sina, ila fedha inatengwa kwa kila barabara kuhakikisha kwamba hiyo barabara inatumika. Ahsante. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niishukuru Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini pia naomba nimuulize swali kwamba eneo lile ni eneo ambalo lina watu wengi kwa maana kata sita katika ukanda ya maji na wakati mwingine kivuko kilichopo huwa kinasombwa na maji kupelekea wananchi wale wanaathirika kwa muda mrefu zaidi na eneo lile lina vituo viwili vya afya ambavyo vina ambulance mbili.

Kwa hiyo, naomba Serikali ione namna ya kufanya haraka katika kuhakikisha kwamba wananchi wale wa Jimbo la Kigoma Kusini katika maeneo yale ya kata sita wanapata ufumbuzi wa jambo hili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Nashon kwa kufuatilia jambo hili la barabara hii ya Ilagala. Niseme tu mimi Mkoa wa Kigoma nimefanyakazi na barabara hii naifahamu sana, ni kweli anachosema na ndiyo maana Serikali imeamua kutengeneza hili daraja ili kuondokana na adha hii.

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea tayari Serikali iko kwenye hatua ya manunuzi ya kufuata Mhandisi Mshauri ambayo inasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kusombwa na vivuko ni kweli kwamba kwenye daraja hili huu mto Maragalasi ni mto wenye zaidi ya kilometa 300 kwahiyo inawezekana kivuko hiki kinapata changamoto kwasababu ya magogo ambayo yanasombwa na mito na ndiyo maana usiku kivuko hiki huwa hakifanyikazi ila tu kinafanyakazi kunapotokea emergency.

Kwa hiyo tutaendelea na utaratibu huo huo lakini tutahakikisha kwamba hiyo barabara hilo daraja linakamilika mara mara fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza samahani, kwa kuwa leo ni siku yangu ya kwanza na mara yangu ya kwanza kuongea, napenda niwashukuru ndugu zangu wa Morogoro Kusini Mashariki. Pia nishukuru familia yangu, mama yangu mzazi na marehemu mke wangu popote alipo, Mungu amlaze mahali pema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa majibu ya Serikali na kwa kutambua ufinyu wa bajeti na kuzingatia umuhimu wa barabara hii, je, Serikali iko tayari kushirikiana nami kutafuta mkandarasi wa building and finance? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nimemuelewa vizuri kwamba Serikali itashirikiana naye kutafuta mkandarasi, utaratibu wa kutafuta wakandarasi ni utaratibu ambao uko kisheria na ni utaratibu ambao unatekelezwa na Serikali kupitia mamlaka husika.

Mheshimiwa Maibu Spika, kwa kuwa tumeahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake barabara anayoizungumzia ameiahidi, hivyo, nimhakikishie tu kwamba itajengwa na kukamilika katika kipindi hiki cha miaka mitano ambayo Ilani hii itakuwa inatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Makete naomba kuuliza kuhusu ujenzi wa barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo kilometa 51, ilikuwa ni ahadi ya Waziri Mkuu mstaafu, kwa muda wa miaka 10 hadi sasa haijatekelezwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete ni kati ya barabara ambazo zimetajwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia ukurasa wa 72 – 76. Pia katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Rais ameeleza kwamba katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hii pamoja na ahadi alizozitoa atahakikisha kwamba anajenga na kukamilisha barabara zote ambazo zinaendelea zenye urefu wa kilometa 2,500 lakini pia ataanza ujenzi na kukamilisha barabara zenye urefu wa kilometa 6,006 na barabara hii ya Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete ni kati ya barabara ambazo zimetajwa ama zimetolewa ahadi na mwenyewe Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, nimpe uhakika kwamba barabara hiyo itajengwa na kukamilika.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya Bugeme – Nkwenda – Isingiro mpaka Mrongo yenye urefu wa takribani kilometa 135 ikiunganisha Wilaya ya Kyerwa na Karagwe, lakini Kyerwa na Uganda. Swali, ni lini Serikali itakamilisha, ni lini Serikali itajenga hii barabara kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia umuhimu wa hiyo barabara na hasa wakazi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Anatropia swali lako lilivyoisha nilikuwa nimekata maneno. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge ambaye ameelezea barabara yenye urefu wa kilometa 135 ambayo ni ya Kyerwa – Karagwe, lakini pia inakwenda Uganda:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika swali la nyongeza Mheshimiwa Rais amesema atakapokuwa anakamilisha barabara zote za kilometa 2,500 na kilometa 6,006 tutakuwa tumeunganisha wilaya zote za Tanzania kwa kiwango cha lami, mikoa yote ya Tanzania kwa kiwango cha lami, lakini pia na barabara kuu zote (trunk roads) ambazo zinaunganisha nchi na nchi kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza kwamba, barabara hiyo ni kati ya barabara ambazo zitatekelezwa. (Makofi)
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na TANROADS kujitahidi kukarabati barabara ile, lakini nyakati za masika imekuwa ikikata kabisa mawasiloiano; na kwa kuwa, amekiri kwamba, ni muhimu sana kwa kusafirisha mazao na isitoshe wananchi wale wanaitegemea sana barabara ile kwa huduma mbalimbali za kijamii kupeleka wagonjwa hospitali, lakini bidhaa mbalimbali za matumizi ya kila siku. Je, Serikali haioni kwamba, sasa ipewe kipaumbele ili ujenzi wa barabara ile kwa kiwango cha lami uanze haraka iwezekanavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mkoa wa Mbeya tuna uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa na Mheshimiwa Rais amenunua ndege kubwa, Dreamliner na barabara ile inapita kandokando mwa lango kuu la Kusini kuingia Hifadhi ya Ruaha (Ruaha National Park), sasa watalii wangepitia lango lile la Kusini kwa urahisi kabisa. Je, Serikali haioni kwamba inakosesha pato la Taifa hasa pesa za kigeni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwa sababu ya umuhimu wa hiyo barabara ndio maana tayari taratibu za kuanza kujenga kwa kiwango cha lami zimeshaanza na zimeshatengwa tayari bilioni 3.38 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali kwamba, kwenye bajeti zinazofuata nina hakika barabara hii itatengewa fedha zaidi, ili iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya umuhimu huu kama alivyosema kwenye swali lake la pili kuhusu uwanja wa ndege nasema ndio maana tayari hii barabara kwa Serikali kutambua umuhimu wake ikiwa ni kupokea wageni kutoka uwanja wa Songwe, lakini na kuwapeleka kwenye mbunga, ndio maana tayari taratibu za Serikali zimeanza za kukamilisha ama kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imefanya kazi nzuri ya kujenga barabara kwenye Jiji la Arusha na hasa ukizingatia kwamba, barabara ya mzunguko ya bypass ambayo imesaidia sana kwa watalii na wananchi wa Jiji la Arusha, lakini bado kuna kipande cha Kata ya Moshono ambacho kinatoka eneo la kona ya Kiseliani kuunganisha barabara ya bypass maarufu kama barabara ya T Packers Osunyai kama kilometa saba. Je, Wizara ya Ujenzi haioni sasa ni wakati sahihi wa kumalizia kipande hiki ili kupunguza msongamano na kuweka mazingira mazuri zaidi ya utalii pamoja na wananchi wa Kata ya Moshono?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye ukurasa wa 77 barabara za bypass kwa ajili ya kupunguza msongamano zimeainishwa zikiwemo Miji ya Dar-Es-Salaam, Mbeya na Arusha ni kati ya miji ambayo zitanufaika na barabara hizi za mizunguko kwa ajili ya kupunguza misongamano. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha kwamba, barabara hii aliyoitaja ni moja ya barabara ambazo zitatekelezwa katika kipindi hiki tutakachoanza bajeti katika kipindi hiki cha miaka mitano. Ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Mbozi napenda kuuliza swali kuhusu Barabara la Mloo – Kamsamba mpaka Kilimamatundu na kutoka Utambalila mpaka Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Chitete, kilometa 145. Kwa kuwa, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika; na kwa kuwa nyaraka za tenda ziko tayari.

Je, ni lini barabara hii itatengewa fedha na kutangazwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi na kama Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inavyoelekeza kwa mwaka 2020 - 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema ya Mbozi – Mtambalila mpaka Kamsamba ni barabara ambayo, kama alivyosema imeshafanyiwa usanifu na ni kati ya barabara ambazo zimeahidiwa kwanza kwa bajeti zinazokuja zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mwenisongole kwamba, barabara yake iko kwenye mpango na zitaendelea kujengwa barabara kadiri ya fedha itakavyopatikana katika kipindi hiki cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/2022 mpaka 2025/2026, asante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza kwa kuwa Barabara ya Rujewa – Madibira inafanana na ile barabara ya Arusha – Simanjiro – Kiteto pamoja na Kongwa kilometa 430 ambayo imeahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 - 2025 pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu langu la msingi na bado natambua kwamba, barabara anayoulizia, kama mwenyewe alivyosema, iko kwenye ilani lakini pia iko kwenye ahadi ya Rais, lakini pia iko kwenye hotuba ya Rais.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hiyo pia, kadiri Serikali itakavyoendelea kutafuta na kadiri fedha zitakavyopatikana ni kati ya barabara ambazo tunategemea kuzikamilisha ili tuweze kuunganisha wilaya zote, mikoa yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali yetu yenye kutia matumaini lakini bado kwa umuhimu wa barabara hii wananchi wa Jimbo la Nachingwea watapenda kusikia commitment ya Serikali. Kwa kweli, katika hili viongozi wengi wanahukumiwa kutokana na barabara hizi pamoja na mambo mengine. Je, nini commitment ya Serikali juu ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, viko vijiji vya Ikungu, Chiola kuelekea Ruangwa, hapa tayari walifanyiwa tathmini na wenzetu wa TANROADS. Watu wa TANROADS walikuja wakafanya tathmini wakiamini kwamba barabara itapita upande wa kulia baada ya muda wakarudi tena wakafanya tathmini upande wa kushoto. Kwa hiyo, hawa wananchi wamezuiliwa kwenye maeneo yale wasifanye maendelezo. Ni lini Serikali itakwenda kutoa ufafanuzi wa jambo hili, ili wananchi wa maeneo yale waweze kuendelea na shughuli zao? Ahsante sana.

SPIKA: Hiyo ni kwa barabara ya Nachingwea – Ruangwa?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, commitment ya Serikali ni kwamba tayari fedha ya awali za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami zimeshatengwa. Pia barabara hii imeahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia ni kati ya barabara ambayo Mheshimiwa Rais ameahidi kuijenga kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ameuliza kwamba kuna wananchi ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa sababu ya watu wa TANROADS waliokwenda kupima, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kwamba suala hili linaendelea kufanyiwa kazi. Naomba kama kuna changamoto yoyote tofauti ambayo pengine mimi nitakuwa siifahamu basi tuwasiliane naye ili niweze kujua changamoto halisi ni ipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sambamba na barabara ya Masasi – Nachingwea, barabara hii vilevile ina jina la Lukuledi
– Liwale yenye jumla ya kilometa 175 kwa maana kutoka Masasi mpaka Liwale kilometa 175. Barabara hii tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Wanaliwale wanataka kusikia barabara Nachingwea – Liwale lini itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja kama nilivyosema tunatambua ni muhimu na zimeahidiwa kujengwa katika bajeti ambayo tutaanza kuijadili. Kwanza ni barabara ambayo ipo kwenye Mpango wa Miaka Mitano na tunategemea katika bajeti inayoanza itatengewa fedha ili ianze kujengwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni adhma ya Serikali kuunganisha miji yote ya mikoa na wilaya kwa barabara za lami; na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wa Mpwapwa, je, Serikali ipo tayari kuipa kipaumbele maalum barabara hii ili ikamilike mapema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu na ndiyo maana hata hapa tunapoongea yeye atakuwa ni shahidi kwamba mkandarasi yuko site akiwa anajenga hizo kilometa 5. Naamini katika bajeti ijayo tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza hiyo barabara.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama kwa namna ambavyo halali usiku na mchana anafuatilia kuona kwamba barabara hii inajengwa ili kuweza kuchochea uchumi wa wananchi wa maeneo husika Mkoa wa Ruvuma na Nchi yetu ya Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Ruvuma ni mkoa ambao umeshika nafasi ya kwanza mara tano mfululizo kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka. Wananchi wa maeneo hayo wanajishughulisha na kilimo, uzalishaji wa makaa ya mawe, soko la mazao la Kimataifa, lakini pia kuna shamba la miwa.

Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najenga hoja. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kuwa kuchelewesha ujenzi wa barabara hii ni kuendelea kufanya udumavu wa maendeleo kwenye maeneo husika hasa kwa Mkoa wa Ruvuma na Jimbo la Peramiho na kwa nchi yetu kwa ujumla? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nafahamu kwamba Kamati ya Bajeti imetenga fedha shilingi milioni 110 kwa ajili ya kufanya usanifu wa ujenzi wa daraja, daraja ambalo limekwishajengwa, daraja la Mkenda. Je, ni kwa nini Serikali sasa isihamishe fedha hii shilingi milioni 110 ikaanze ujenzi wa barabara mara moja ili kuweza kuchochea uchumi wa maeneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii na kwa kutambua umuhimu wa uzalishaji ambao uko katika Mkoa wa Ruvuma lakini pia na makaa ya mawe; katika jibu langu la msingi tumesema barabara hiyo pia ni muhimu sana kwa ulinzi wa nchi yetu na pia ni moja ya vipaumbele vya nchi kuunganisha nchi na nchi na hii ni trunk road wala sio regional road. Ndiyo maana tayari barabara hii imeanza kutengewa fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kama Mheshimiwa Mbunge amenisikiliza vizuri, kulifanyika usanifu wa awali ambao wakati huo barabara haikuwa na matumizi ambayo inayo sasa hivi na ndiyo maana kukafanyika redesign yaani usanifu mpya kwa sababu tayari sasa kule kuna makaa ya mawe na mgari yaliyokuwa yanapita wakati ule wakati barabara inafanyiwa usanifu siyo ambayo sasa yanapitika. Kwa hiyo lazima lile daraja lifanyiwe usanifu mpya ili liweze kumudu shughuli ambazo sasa zitaweza kufanyika kwa maana ya kuwa na uwezo wa kuhimili magari ambayo yatapita na uzito wake hasa baada ya kugundua makaa ya mawe na kuongezeka kwa traffic kwenye hiyo njia. Ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, lakini pia swali hilo linafanana na hali ya kule Mufindi. Kwa kuwa Mufindi ni kitovu cha viwanda nchini na zaidi ya viwanda tisa viko pale na miundombinu imekuwa ni mibovu sana; na kwa kuwa barabara ya Nyololo - Mtwango na Mafinga - Mgololo zimeahidiwa kuanzia wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja na Rais Magufuli, zimeahidiwa na Mawaziri Wakuu, Mzee Pinda na Mzee Kassim Majaliwa, zimetajwa kwenye Ilani ya CCM karibu mara tatu…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuingiza kwenye bajeti barabara hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara zote alizozitaja zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa sana ambao yanachangia fedha nyingi sana kwenye Mfuko wa Serikali na kama alivyosema barabara hizo zimeahidiwa na viongozi wengi wa Kitaifa, lakini pia barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizo kwa sababu ya umuhimu wake, kuanzia bajeti inayokuja zitaanza kutengewa fedha ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya barabara hiyo kutoka Kijiji cha Misegese kufika Malinyi Mjini huwa haifikiki kipindi chote, hata mvua ikinyesha siku moja tu, tunalazimika kutumia mitumbwi kufika Malinyi Mjini na magari hayafiki kabisa. Mkandarasi ambaye yuko site anaweka calavat moja badala ya yanayotakiwa kama sita au saba. Amepewa kazi ya kuinua tuta mita 200 badala ya kilometa moja ambayo ni uhitaji halisi. Je, Serikali haioni haja ya kumuongezea uwezo kujenga kulingana na uhitaji ambao nimeutaja?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda Malinyi baada ya Bunge hili ili kujionea hali halisi ya miundombinu na kutafuta suluhisho la pamoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgungusi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la mwisho, naomba niseme kwamba barabara hii imekuwa inaulizwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao ni wanufaika wa barabara hiyo. Kwa hiyo, niwadhihirishie ama niwaaminishe kwamba mara baada ya kikao hiki nitahakikisha naitembelea barabara hiyo ili niweze kuifahamu vizuri kwa sababu kila mara Wabunge wa eneo hilo wananifuata kwa ajili ya kutafuta utatuzi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili alilouliza kuhusiana na tuta linalojengwa na mkandarasi, naomba Mheshimiwa Mbunge Mgungusi kwa sababu, bahati nzuri mkandarasi yuko site, tutaongea na Meneja wa TANROADS ambaye ndiye anamsimamia mkandarasi huyu ili kama kuna shida ya kitaalamu ama ya uwezo, Serikali tutahakikisha kwamba tunampa maelekezo ya afanye vile inavyotakiwa kama ambavyo ipo kwenye design. Ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mara kwa mara Serikali imekuwa ikizungumzia kujenga barabara inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati ambako kuna mitambo na visima vya gesi. Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara hiyo muhimu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Shamsia kwamba katika kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inakifanya, kwanza tumetoa ahadi kujengwa kwa barabara za wilaya, mkoa na za kitaifa na barabara zile ambazo zinaenda maeneo muhimu kwa maana ya uchumi wa Taifa. Kwa hiyo, kama barabara hiyo inaangukia humo, nataka nimhakikishie kwamba kuanzia bajeti tunazoanza na katika Mpango huu ambao tunaendelea nao, nina hakika katika miaka mitano barabara hii itakuwa imejengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama ilivyo kwa barabara hii ya Lupiro – Malinyi, barabara ya Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Soni iliahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, lakini pia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika. Napenda kujua, ni lini sasa kazi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami itaanza ili kuwasaidia wananchi wa Korogwe na Lushoto kwenye eneo la usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge ambaye ameuliza barabara ya Korogwe hadi Soni ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wabunge wawe na imani na Serikali hii ya Awamu ya Tano kwani kwanza ni ahadi za viongozi wetu wa kitaifa Mheshimiwa Rais lakini pia zimetajwa katika Ilani. Naomba tuanze bajeti na nina hakika hizi barabara ambazo tunaziulizia zimo, kwa sababu tumeahidi tutatengeneza hizi barabara kwa kiwango cha lami. Nashauri Waheshimiwa Wabunge wawe na imani kwamba barabara hizi zitajengwa ikiwa ni pamoja na barabara ya Korogwe kwenda Soni. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni nini kauli ya Serikali kwa kumalizia kipande cha Mbande – Kisewe ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Kata ya Chamazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, barabara ya Zakhem – Mbagala Kuu imepata fedha za Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar-Es-Salaam na imeshindwa kujengwa kwa sababu ya uwepo wa bomba la mafuta la TAZAMA. Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia walao corridor ya mita saba ili barabara hiyo ambayo tayari inayo fedha iweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaurembo, Mbunge wa Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tunavyoongea sasa hivi, Mheshimiwa Chaurembo ni shahidi, tulikuwa na kilometa 6.05; kilometa moja imeshakamilika zimebaki kilometa 5.06. Nimhakikishie Mheshimiwa Chaurembo katika mwaka huu wa bajeti, kupitia fedha ya matengenezo, sasa tutaanza barabara ya kutoka Mbande kuja Msongola ambapo tunajenga kilometa 1.5 kwa kiwango cha lami. Pia kwa fedha ya maendeleo tutaendelea kutoka Msongola kwenda Mbande kilometa 1. Kwa hiyo, tutabakiwa kama na kilometa 2.5 ambazo zitakuwa bado hazijakamilika na fedha itakapopatikana tutaendelea kukamilisha barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuhamisha bomba ama barabara Serikali imelipokea na itakwenda kulifanyia kazi tuone kama tutahamisha kwa sababu inapita karibu na bomba. Tutaangalia namna ya kufanya ili barabara ile muhimu sana iweze kuanza kujengwa. Pia kwa sababu suala hili siyo la Idara yangu pekee kwa maana ya Wizara ya Ujenzi ni Wizara nyingi, kwa hiyo, tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi kuona ni namna gani tufanye kuhamisha barabara hiyo. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana kwa shughuli za uchumi wa wananchi wa Lushoto, hasa ukizingatia kwamba, mazao tunayozalisha kule ni mbogamboga na matunda ambayo ni rahisi kuharibika. Kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, angalau sasa barabara hii ijengwe japo kwa kiwango cha kilometa 10 kwa mwaka. Je, tunapoelekea kutengeneza bajeti Serikali haioni ni muhimu kutenga kiwango hicho cha kilometa 10 kwa kila mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii imeendelea kutia hasara wananchi wa Mlalo, hasa nyakati za mvua. Je, Serikali sasa iko tayari kuwalipa fidia mara ambapo wananchi wanapata hasara ya mazao yao kuoza barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambako kunazalishwa sana matunda na mbogamboga. Kwa kutambua umuhimu huo ndio maana Serikali tayari imeshakuwa na mpango wa kujenga hii barabara. Tunatambua pia kwamba, Serikali ilitoa ahadi kwamba, itaendela kujenga hii barabara walao kwa kilometa 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza kama kwenye bajeti ijayo je, tutajenga. Itategemea pia na upatikanaji wa fedha na kama itapatikana si tu kilometa 10 bali inawezekana ikawa ni kukamilisha kabisa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; endapo kama tutatoa fidia kwa wale wanaopata matatizo hasa pale ambapo mazao yao yanaharibika. Tumeshaongea na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, ili badala ya kuendelea kutengeneza kile kipande wanachokiendeleza, basi atengeneze yale maeneo ambayo ni korofi, ili yaweze kuimarika na kusitokee tatizo kama hilo. Kama kuna changamoto nyingine basi namwomba Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, anipatie. Nimwahidi Mheshimiwa kwamba, nitafika kuona hizo changamoto ambazo anazisema. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, nilitaka kunyosha mikono miwili. Naomba niulize swali moja. Kwa vile Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa kwenye kampeni kule Vunjo aliahidi kujenga barabara ya Kilema a.k.a barabara ya Nyerere ambayo ni kilometa tisa; barabara ya Uchira kwenda Kisomachi kilometa nane tu na Mabogini – Kahe na Chekereni ambayo na yenyewe ni kilometa 22 tu kwa kiwango cha lami. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuhakikishia kwamba, barabara hizo zimeingizwa kwenye mpango wa 2021/2022? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kimei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi alizosema ni ahadi za Rais na ni ahadi katika kipindi cha uchaguzi wa 2020. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Kimei avute subira kwa sababu, bajeti ndio inaenda kwa hiyo, tutaangalia. Siwezi nikasema kwa sasa kwa sababu, hiyo bajeti bado haijapitishwa, lakini kama ni ahadi ya Rais, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kimei kwamba, ahadi za Rais zitazingatiwa katika kutekelezwa kwa bajeti zinazokuja kuanzia 2021/2022. Ahsante. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali nataka kufahamu ni hatua gani za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa na Serikali kwa wataalam wetu wanaosababisha variation ya miradi kuwa na gharama kubwa, kwa mfano, daraja hili la Mbaka ambalo limechukua muda mrefu sana. Kuna kitu tunaita geotechnical investigation hakikufanyika na ndiyo maana imechukua muda mrefu zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa daraja hili litakapokamilika kutakuwa kuna madaraja mawili, kutakuwa kuna daraja hili ambalo linajengwa pamoja na lililokuwepo la chuma.

Je, Serikali ipo tayari kulichukua hili daraja la chuma kupeleka katika mto huo huo Mbaka lakini kwa kuweza kuunganisha kati ya Majimbo ya Busokelo, Kyela pamoja na Rungwe katika Kijiji cha Nsanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari ni utaratibu wa Serikali pale ambapo mfanyakazi yeyote amefanya kinyume na utaratibu anachukuliwa hatua na kwa sababu umakini huo ndiyo maana ilionekana kwamba daraja hili lilikosewa design na ikafanyiwa redesign na tayari ujenzi unaendelea kwa hiyo ni utaratibu wa kawaida pale panapotokea tatizo hatua zinachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza endapo daraja la chuma lililokuwepo litakwenda kwenye daraja lingine alilolisema ni utaratibu wa Serikali kwamba madaraja haya ya chuma ni madaraja ambayo yanatumika kwa ajili hasa ya dharura. Kwa hiyo utaratibu utawekwa kama itaonekana ni muhimu liende hapo litakwenda lakini vinginevyo tunayatunza maeneo ambayo ni ya kimkakati ili kunapotokea tatizo la dharura basi hayo madaraja yatakwenda hapo. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu wa kipande cha Ifakara – Kihansi chenye kilometa 125 umekamilika. Je, Serikali iko tayari kuanza kutenga fedha ya kujenga hiki kipande katika mwaka huu wa fedha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili barabara ya Lutamba- Chiponda-Mnara-Nyengedi inayounganisha Halmashauri ya Mtama na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambayo pia inaunganisha barabara ya Mkoa ya kwenda Ruangwa lakini pia ya kwenda Masasi kwa maana ya Mkoa wa Mtwara, ni barabara ya muhimu sana kwa uchumi wa eneo hili, lakini hii barabara imekuwa chini ya TARURA kwa muda mrefu na TARURA kwa kweli hawana uwezo wa kuendelea kuijenga. Je, Serikali iko tayari kuipandisha hadhi barabara hii sasa ianze kuhudumiwa na TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoiuliza ya Mheshimiwa Kunambi ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa na Mkoa na kwa kuwa usanifu wa kina umekamilika, tunaamini katika bajeti ijayo Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Nikiri Mheshimiwa Kunambi kila anaposimama imekuwa akiipigia sana kelele barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kwamba katika bajeti tunazoanza kuzitekeleza kwa mwaka ujao naamini itatengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Nape Mbunge wa Mtama sitazitaja barabara zake zimekuwa ni nyingi Lutamba-Chiponda-Mtama-Lindi na kwamba ni barabara za TARURA, naomba Mheshimiwa Nape nimshauri waweze kupitia kwenye taratibu za kawaida za kupandisha hadhi hizi barabara kutoka TARURA kwenda TANROADS ambapo lazima watakaa na Bodi ya Barabara ya Mkoa halafu itakwenda kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa na baadaye zinakuja kwenye Wizara kwa ajili ya kuziangalia kama zinakwenda kupandishwa hadhi. Kwa hiyo kama zitakuja kwa utaratibu huo nadhani kuna utaratibu zitafikiriwa na Serikali itaona namna gani ifanye ili kuzipandisha hizo hadhi. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali na nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri na weledi katika masuala yote ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza na swali la kwanza ni barabara ya Katoma - Bukwali ambayo ni barabara inaunganisha nchi yetu nanchi ya Uganda na ni barabara muhimu kwa uchumi kwa wananchi wa kata za Gera, Ishozi, Bwanjai, Kashenye na Kanyigo; barabara hiyo yenye kilometa 39.5 nishukuru Serikali sasa hivi kilometa nne zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami na je ni lini kilometa 35.8 zilizobaki zitawekwa kwenye bajeti na kuweza kukamilishwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni barabara ya Bunazi - Nyabiyanga - Kasambya - Kakindo na Minziro ambayo barabara hiyo inaunganisha Makao Makuu ya Wilaya pamoja na nchi yetu ya Uganda lakini kuwa ni barabara kiungo kwa wananchi wote wa Tanzania kila mwezi Januari wananchi wanaenda kuhiji katika eneo takatifu la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi aliyezikwa hapo na ni mojawapo ya mashahidi 22 wa Uganda.

Je, ni lini barabara hiyo yenye kilometa 35.8 na yenyewe itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami nakushukuru kwa nafasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Katoma - Bukwali tayari ipo inaendelea kujengwa na kilometa
4.2 kama alivyosema zinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba bado wakandarasi wawili wako site wakiwa wanaendelea kufanya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kilomita ambazo tunaamini kilometa 2.2 zitakamilika mwezi Aprili na Serikali bado inaendelea kutafuta fedha na katika bajeti ijayo barabara hii tunaamini kwamba itapata fedha kuendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja zote hizo za vijiji mbalimbali na kata mbalimbali tunatambua kwamba ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Nkenge na bado Serikali tunaahidi kwamba itaendelea kuzikarabati na pale fedha itakapopatikana kuzijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kunipa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ubovu mkubwa wa miundombinu ndani ya Jimbo la Momba. Je, ni lini Serikali itatusaidia kutujengea kilometa 15 za kiwango cha lami kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba katika Kata ya Chitete ikiwa ni sambamba na ahadi ya mama yangu mpendwa Mheshimiwa Makamu wa Rais alipotembelea Jimbo la Momba tarehe 13 Oktoba, 2020 alituahidi angeweza kutusaidia barabara hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naombakujibuswali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-

MheshimiwaNaibu Spika, ni kweli ahadi ya Makamu wa Rais wakati wa kampeni ilitolewa mwaka huu wa kampeni 2020; kwa hiyo, kama Serikali ahadi hii tumeichukua na tunaifanyiakazi. Kwa hiyo, katika awamu inayokuja ya bajeti tunategemea kwamba zitakuwa ni kati ya barabara ambazo zitatengewa fedha na once zikitengewa fedha barabara hiyo itajengwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naomba niulize Serikali na wananchi wa Sikonge wanasikiliza na Mkoa wa Tabora; je, baada ya kuwa Serikali imekamilisha maandalizi yote ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Ipole - Lungwa yamekamilika usanifu kila kitu. Je, sasa bado fedha na mkandarasi Serikali itaanza lini kujenga barabara hiyo ili kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ipole - Lungwa ni kati ya barabara zinazounganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya na kama alivyosema taratibu zote zimekamilika, kinachotegemewa tu ni lini itatangazwa kwa sababu sasa hivi tuko kwenye maandalizi ya manunuzi kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na kama alivyosema wananchi wake wanamsikia ni barabara muhimu inayounganisha na mkoa na mkoa, kwa hiyo ninahakika barabara hii itatengewa bajeti na taratibu za manunuzi once zikikamilika basi tutakuwa tumepata mkandarasi na itaanza kutekelezwa, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yanayowapata wananchi wa Tunduru yanafanana kabisa na matatizo ambayo yanawapata wananchi wa Kigamboni katika Mkoa wa Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga barabara ya Kibada - Kisarawe Two - Mwasonga - Tumbi Msongani ili kuwasaidia wananchi Wilaya ya Kigamboni waweze kupata unafuu wa usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam kuhusu barabara za Kigamboni. Hiki ni kipindi cha bajeti na kama tulivyoahidi barabara hizi zitajengwa ndani ya miaka mitano, kwa hiyo kwenye bajeti pengine suala la kuanza usanifu wa awali na wa kina litajitokeza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi kama tulivyoahidi zitajengwa. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Mgakolongo kwenda Kigalama mpaka Mlongo inayounganisha na nchi ya Uganda, usanifu wake umeshakamilika muda mrefu. Ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye Ilani na nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira tuone bajeti ambayo tunaiandaa hiyo barabara itashughulikiwaje. Kwa sasa siwezi nikasema chochote maana ndiyo tuko kwenye kipindi cha bajeti, kwa hiyo, naomba awe na subira aone kama barabara yake itajengwa lakini tunatambua ni barabara muhimu sana. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Changamoto ya barabara iliyoko Tunduru Kusini inafanana kabisa na changamoto iliyoko wilaya ya Ngara ya barabara ya Murugalama - Lulenge - Mizani yenye urefu wa kilomita 85. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali la nyongeza la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara aliyoitaja ambayo inapita eneo la Mgalama - Lulenge nina hakika zitajadiliwa katika kipindi hiki cha bajeti, kwa hiyo, awe na subira.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua jitihada za Serikali kuboresha usafiri kati ya Rugezi kwenda Kisorya. Hata hivyo, kutokamilika kwa hili eneo la Lot III na hasa barabara ile ya kilometa 14 kutoka Rugezi – Nansio inaathiri sana uchumi wa wananchi wa Ukerewe, na ndiyo maana tarehe 04 Septemba, 2021 Hayati Dkt. John Magufuli akiwa Ukerewe, kwa kutambua changamoto hizi alitoa maelekezo eneo hili lifanyiwe kazi mara moja. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Ukerewe alisisitiza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwanini sasa Wizara isione umuhimu wa jambo hili ikatenga pesa kwa haraka ikaufanya kama mradi wa haraka ili Lot III, hasa wakati wanasubiri pesa za kujenga daraja basi barabara km. 14 kati ya Rugezi kwenda Nansio iweze kukamilika kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi Mbunge wa ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Ukerewe. Lakini Mheshimiwa Mbunge yeye pia atatambua kwamba Serikali inafanya jitihda kubwa sana kuhakikisha kwamba inatengeneza barabara na ndiyo maana imegawanywa kwenye Lot III. Lot ya pili imeshakamilika, lot ya kwanza mkandarasi yuko site na Serikali imeahidi kwamba inatafuta fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja tunaloliongelea urefu wake unafanana na daraja karibu lile linalojengwa la pale Surrender Bridge, ni takriban kilometa moja. Kwa hiyo Serikali lazima ihakikishe kwamba inajitahidi kupata fedha ya kutosha ili kuweza kujenga daraja hilo; na ndiyo maana tayari usanifu wa kina umeshafanyika. Tayari Serikali imeonesha jitihada za makusudi, kwamba kwanza ni ahadi ya Hayati Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo Serikali kama nilivyosema kwenye jibu la msingi inaendelea kutafuta fedha na fedha ikipatikana nina uhakika kipande hiki cha Lot ya tatu kitajengwa. Ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tuko katika Wizara ya Ujenzi, na Wizara hii ndiyo inayoshughulikia barabara pamoja na madaraja, sasa nilitaka kuuliza swali linalohusu barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitutembelea kule Milola na tukampa kero yetu ya barabara ambayo inatoka Ngongo inapitia Rutamba, Milola hatimaye inamalizikia Ruangwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu alituahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami.

Sasa, je, ni lini barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongezala Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo kwenye mipango, na ninaamini usanifu wa awali unaweza ukaanza kwa sababu hatujapita bado kwenye bajeti. Niombe kujiridhisha, Mheshimiwa Salma nimuombe baada ya kikao hiki pengine tuweze kukutana naye ili tuweze kuona barabara hii iko kwenye mpango kwasababu sasa hivi tuko bajeti kwa hiyo ni ngumu kusema barabara hii iko kwenye hatua gani. Kama ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama iko kwenye ilani naamini itakuwa ni barabara ambazo ziko kwenye matazimio ya kufanyiwa kazi na hasa upembuzi yakinifu. Ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa barabara inayoanzia King’ori, hadi Ngarenanyuki imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, na Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi kujenga barabara ii katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kufahamu ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Magige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba ni lini barabara ya Kilole kwenda Ngarenanyuki itajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hizi zote ambazo zimeainishwa tuna uhakika tutazikamilisha katika kipindi hiki cha miaka mitano. Lazima kutakuwa na mahali tutaanza na barabara chache lakini tutamaliza zote. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa na ambazo zimeahidiwa zipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kipaumbele ni zile barabara ambazo zinaunganisha mikoa na mikoa, wilaya na wilaya. Ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Iringa Mjini kupitia Jimbo la Kalenga kwenda Kilolo kilometa 133 ambayo ina madaraja ni barabara ambayo ilikuwa ni ahadi ya hayati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, alipofika pale akatoa ahadi hiyo, ni miaka mitano sasa imepita haijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lini Serikali itaijenga barabara hii ili angalau kumuenzi hayati kwasababu alienda akaona wananchi wa kule wanavyohangaika katika kuuza mazao yao kwenda katika sehemu mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii yenye urefu wa km. 133 iliyoko Mkoani Iringa na ambayo ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli naomba nimhakikishie kwamba Serikali haitaacha ahadi zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Nataka nimhakikishie kwamba barabara zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais ikiwa ni pamoja na hiyo zitajengwa kwa kiwango cha lami awamu kwa awamu. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu, iko study ambayo ilifanyika enzi za mkoloni kwamba, kuna umuhimu wa kujenga reli kuanzia Tunduma kwenda Kasanga, lakini kwenda mpaka Ziwa Nyasa kwa maana ya Kyela na study hiyo iko NDC hadi leo ninavyoongea. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufuatilia study hiyo ambayo ilifanywa na mkoloni na akaona viability ya mradi huo ili sasa ianze kutekeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mheshimiwa Rais ambaye wakati ule alikuwa Makamu wa Rais, wakati amekuja kuomba kura kwa ajili ya CCM, katika mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa ilikuwa ni pamoja na ujenzi wa kipande hicho cha reli na akasema amepokea na ambaye leo ndio ndio Rais; na kwa kuwa mahusiano yetu na Serikali ya China hayana shida hata kidogo na kwa sababu, wao ndio walitusaidia katika ujenzi wa Reli ya TAZARA. Je, Serikali haioni umuhimu uleule ili tutumie window ya uhusiano mzuri na China ili vipande hivi viweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, study aliyosema Mheshimiwa Mbunge ya mkoloni ni wazi kwamba haiwezi ikatumika kwa sasa. Kitakachofanyika inaweza kuwa tu ni kufanya review ya hiyo study kwa sababu, mazingira yamebadilika sana. Pia kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba, miradi hii ni miradi ambayo inahitaji fedha nyingi sana. Ikumbukwe tu kwamba, kwa sasa hivi kipaumbele cha Serikali ya Tanzania ni kujenga reli ya SGR Awamu ya Kwanza kutoka Dar-es-Salaam mpaka Mwanza ambayo nina hakika ikishakamilika tutakwenda na awamu nyingine. Kwa hiyo, kama Serikali hasa kwa kulingana na ufinyi wa bajeti, naamini hatuwezi kwenda na miradi yote miwili. Ndio maana nimesema upembuzi yakinifu utatuambia gharama ni kiasi gani, ili huo mradi uweze kuanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kandege, Mbunge wa Kalambo ameeleza pia kwamba, Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba, ujenzi huu uweze kufanyika wa reli na ilikuwa ni ahadi. Nakubaliana naye na hatusemi reli hii haihitajiki kujengwa. Tunachosema ni kwamba, tutakwenda kwa awamu na study ndio itakayotuambia gharama iliyopo, lakini pia itazingatia na vipaumbele vya Taifa, tuanze nini tumalizie na nini. Ahsante.
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa umuhimu wa reli hii ya kutokea Tunduma kwenda Kasanga unafanana kabisa na umuhimu wa barabara inayoanzia Mwandiga na kuelekea Chankere na inayopita nyuma ya Hifadhi ya Gombe na mpaka kwenda kwenye Bandari ya Kagunga. Je, Serikali haioni kuna umuhimu sana wa kuikamilisha barabara hii haraka iwezekanavyo kwa sababu, barabara hii ni barabara kwanza ya kiuchumi, lakini barabara hii pia ni barabara ya kiulinzi kwa sababu, ukanda huu hatuwezi kuwafikia wananchi wetu pasipo kupita nchi jirani ya Burundi. Je, Serikali haiwezi kututoa kwenye utumwa huu wa kupitia nchi jirani kwenda kuwahudumia watu wetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara maana anayoongelea ni Barabara ya Mwandiga – Chankere hadi Kagunga. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusanifu barabara hiyo kwa sababu, barabara hiyo bado haijafunguliwa na tunajua kwamba, ni barabara muhimu sana kwenda Bandari ya Kasanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kuwahudumia wananchi wa Kagunga. Mheshimiwa Makanika amekuwa anafuatilia sana hii barabara, nimhakikishie kwamba, Serikali inalifahamu na nadhani pia, ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, hii barabara iweze kufunguliwa. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha kuona kwamba, barabara hii inafunguliwa. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya swali la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali imejikita katika umaliziaji wa reli ya mwendokasi kwa jina lingine SGR kutoka Dar-es-Salaam awamu ya kwanza mpaka Morogoro na kutoka Morogoro mpaka Makutupora awamu ya pili; na kwa kuwa, TAZARA ni reli ya kimkakati na TAZARA inaanzia Mlimba inachepuka mpaka Kidatu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendelea na hiyo reli mpaka Kilosa kuungana na hii reli ya mwendokasi, ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka reli ya kati na reli ya SGR kutoka Kilosa kuja Kidatu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Denis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, kuna umuhimu mkubwa sana wa kuunganisha reli ya SGR na reli ya TAZARA kuanzia Kilosa hadi Mikumi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Denis Londo kwamba, Serikali ina mpango huo wa kuziunganisha hizo reli, lakini upembuzi yakinifu utafanyika pale tu ambapo Serikali itakuwa imepata fedha, lakini tunaona kabisa ni muhimu kuziunganisha hizi reli kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa nchi, lakini pia kuziunganisha hizi reli eneo la Kilosa na Mikumi. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Umuhimu wa reli ya kutoka Tunduma kwenda Kasanga ni sawa kabisa na umuhimu wa reli ambayo ilishakuwepo kabla ya Tanganyika kupata uhuru ya kutoka Mtwara – Nachingwea kwa Mikoa ya Kusini. Je, ni nini mpango wa Serikali wa kufufua reli ya Mtwara – Nachingwea mpaka Nyasa kwa manufaa ya kiuchumi na shughuli za kijamii kwa Mikoa ya Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Kasinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge atakubaliana nami kwamba, Serikali ina mpango wa kujenga reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay kwa kiwango cha SGR ambapo tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na usanifu wa awali umeshafanyika. Serikali imeshatafuta tayari transaction adviser kwa ajili ya kuandaa andiko ili kutafuta mbia ambapo reli hiyo tunategemea itajengwa kwa mfumo wa PPP. Kwa hiyo, itategemea na kama mbia huyo atapatikana haraka, basi hiyo reli itajengwa. Reli hiyo itahudumia corridor ya Mtwara kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, lakini pia itakuwa na branch kwenda Liganga na Mchuchuma kwa ajili ya kusafirisha madini ambayo tunategemea yatazalishwa katika migodi hiyo. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo ya Naibu Waziri juu ya swali langu Namba 24, napenda kuuliza maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ni uchumi, barabara ndiyo kila kitu. Swali hili naliuliza kwa mara ya pili katika Bunge lako tukufu lakini majibu ni yale yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza: kwa kuwa barabara hii kipindi cha mvua imekuwa hapitiki na ndiyo maana nimekuwa naomba muda mrefu kwamba barabara hii itengenezwe kwa kiwango cha lami, ni kwa sababu ni barabara ambayo ina uchumi wa hali ya juu sana; barabara hii ina ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba bajeti haitoshi, fedha hakuna.

Je, wananchi wa maeneo haya ya Gairo na Kilindi ni liniwatarajie barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: barabara hii ambayo ina magari mengi na shughuli nyingi za kiuchumi, ina madaraja au mito ya Chakwale, Nguyami na Matale; kipidi cha mvua haipitiki na Serikali kwa kweli imejitahidi mara kadhaa kujenga madaraja.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutuma timu yake kwenda kukagua kuona hali halisi, kwa sababu barabara hii kwa sasa hivi haipitiki na wananchi wanapata adha kubwa? Ahsante.
NAIBU WAZII WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi kwa kuendelea kuwatetea wananchi wa Jimbo la Kilindi ili kuhakikisha kwamba wanapata barabara ya kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, barabara zote ni muhimu sana kwenye masuala ya uchumi, lakini pia katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na usafiri wa wananchi. Ndiyo maana tuna ilani ya miaka mitano ambapo katika ilani hiyo tunaamini kwamba katika miaka mitano hatuwezi kutekeleza miradi yote kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ni kweli ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, nalo tunalijua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zitajengwa katika kipindi hiki cha miaka mitano mara tu fedha zitakapopatikana na katika bajeti tunazoendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara ya madaraja hayo matatu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi tunavyoongea nimewasiliana na kutaka kupata changamoto za barabara hii. Wiki hii Meneja wa TANROADS wa Tanga na wa Mkoa wa Morogoro, watatembelea hii barabara na kuona changamoto ambazo zinaendelea katika haya madaraja ili tusije tukakatisha usafiri kati ya mikoa hii miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo suala litafanyika na Mameneja wote kwa sababu ni barabara inayounganisha mikoa miwili. Ahsante. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Nyamisati – Bungu ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti hasa wakazi wa Kata za Mwambao, Maege, Mlanzi, Waluke na Kata ya Salala.

Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha ili shughuli za awali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ziweze kufanyika, barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bungu – Nyamisati ni barabara ambayo inaunga kwenye barabara ya Dar es Salaam – Lindi – Mtwara na ambayo ina kilometa takribani kama 43 na bahati nzuri nimeitembelea barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kati ya barabara muhimu sana kwa sasa kwa sababu ndiyo baada ya kujenga bandari ya Nyamisati na kuwa na kivuko ambacho kinafanya kazi kati ya Nyamisati na Mafia, kwa hiyo Wizara inatafuta fedha ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu sasa ndiyo barabara inayotumika sana na wananchi wa kutoka Kisiwa cha Mafia kuja Nyamisati na kwenda sehemu nyingine za Tanzania.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mpembenwe kwamba barabara hii tunatafuta fedha ili wananchi hawa waweze kufanya shughuli zao kwa uhakika zaidi na hasa tukizingatia kwamba ndiyo barabara muhimu inayounganisha watu wa Mafia na watu wa huku bara. Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ujenzi wa barabara inayotoka Tabora Mjini kuelekea Mambali Bukene, imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu. Barabara hii ilikuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 lakini mpaka sasa barabara hii imekuwa ikisuasua hivyo kusababisha wananchi wanaotoka Tabora kuelekea Shinyanga na Mwanza kupata usumbufu mkubwa kuzunguka:-

Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wa Tabora kuhusu barabara hii ili kurahisisha usafiri katika mikoa hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Bukene – Tabora ni barabara ambayo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, tayari Serikali imeshaonesha commitment kwamba ni barabara ambayo iko kwenye mpango wa kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na vipindi vya bajeti, lakini bado tuna mpango wa miaka mitano wa kuzijenga hizi barabara. Kwa hiyo, wananchi wa Tabora na wote wanaonufaika na barabara hii wawe na uhakika kwamba barabara hizi zitajengwa kama zilivyoahidiwa na kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
MHE. FESTO T. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Naomba kuuliza, changamoto ya barabara ya Kilindi – Gairo ni sawasawa kabisa na changamoto ya kutoka Isyonji Mbeya kuelekea Kitulo Makete, barabara ambayo ina urefu wa kilometa 97.6 na kwa muda mrefu imekuwa na changamoto wananchi wetu wa Makete wamekuwa wakipata changamoto.

Naomba kuuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa sababu ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano mfululizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Tuntemeke Sanga, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Sanga amekuwa anaifuatilia sana hii barabara ya Isyonje – Kitulo – Makete na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Sanga, Mbunge wa Makete kwamba barabara hii iko kwenye mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami, kwa hiyo, labda tusubiri bajeti itakapopitishwa nadhani tutapata majibu sahihi zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweka maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napongeza kwa majibu mazuri Serikali kwa namna ambavyo wameweza kutolea majibu katika swali hili lakini barabara hii ya Kolandoto kwenda Mwangongo - Kishapu ikiwa na kilometa 53 imekuwepo katika mpango wa utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015/2020 lakini barabara hii haikuweza kutekelezwa katika kipindi hicho.

Swali, je, Serikali haioni umuhimu sasa pamoja na Ilani kuainisha kuwa barabara hii sasa itakwenda kutekelezwa katika mpango wa miaka mitano kwa maana ya 2020/2025 imeweka umuhimu wa kuhakikisha kwamba barabara hii sasa inatekelezwa tofauti na kipindi cha miaka mitano ambacho haikuweza kutekelezwa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; barabara hii ni barabara ambayo ni trunk road ambayo kimsingi uchumi wake na uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kishapu unaitegemea sana na hasa katika kusafirisha mazao kama pamba, mtama na mazo mengine, lakini barabara hii ni barabara ambayo itaenda kuunganisha takribani mikoa mitatu mpaka minne; Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Singida, hadi Mkoa wa Arusha ambako itapita Sibiti na Oldeani huko Arusha.

Naiomba Serikali itoe tamko na kuipa umuhimu barabara hii ili mradi iweze kuchochea na kuharakisha maendeleo katika mikoa hii. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Butondo, lakini pia Wabunge wote ambao barabara hii inawahusu. Barabara hii ya Kolandoto – Mwingogo hadi Oldeani B ni kweli ni trunk road, kwa hiyo, Serikali inatambua umuhimu wake na ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote ambazo ni trunk roads zinakuwepo kwa kiwango cha lami. Katika jibu langu la msingi ambalo ni la utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015/2020 barabara hii iko kwenye mpango na tumesema maandalizi yanaendelea. Kwa hiyo, naamini kabla ya mwezi Juni tutakuwa tumeshaanza utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye Ilani ya mwaka 2020/2025 na kwenye mipango yetu naamini barabara hiyo bado itapata fedha kwa ajili ya kwenda kutekelezwa ili kuweza kurahisisha usafiri na usafirishaji kati ya mikoa hiyo ya Shinyanga, Simiyu, Singida na Arusha. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo inaongelewa ya kwenda Kishapu ni sawasawa kabisa na barabara ya kilometa 60 ndani ya Mji wa Njombe yaani Ntoni na kwenda mpaka Lusitu. Barabara hii tunaambiwa ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, imeshafanyiwa usanifu wa kina lakini sio tu hivyo, barabara hii vilevile imekuwa kwenye ahadi za Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mwaka 2020 – 2025.

Swali, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu sana kiuchumi na inapita katika maeneo ya Njombe Mji, Uwemba, Luponde na Matola? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Njombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema atakubaliana na mimi kwamba iko sehemu ambayo ndiyo inakwenda mpaka huko Ludewa tayari imeshaanza kufanyiwa kazi na mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kipindi hiki ni cha bajeti tunatambua umuhimu wa hii barabara na nadhani baada ya bajeti ataamini kwamba Serikali kweli ina mpango wa kuhakikisha kwamba barabara hii ya Njombe – Itoni – Lusitu inajengwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii iko kwenye mipango ya Wizara kwa maana ya Serikali kwamba itaendelea kujengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi naomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa Wilaya za Kilombero, Majimbo ya Kilombero, Mlimba, Wilaya ya Ulanga pamoja na Malinyi unategemea sana barabara ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara kukamilika kwa ujenzi wa lami. Nakumbuka mkandarasi alishafanya mobilization, lakini kwa sababu ya changamoto za mgogoro wa kikodi limesimama.

Ni lini sasa Serikali inawahakikishia wananchi wa maeneo hayo kwamba tutaanza kujenga barabara hiyo kwa lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Humphrey Polepole, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Mikumi – Ifakara ni barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi anayeitwa Reynolds.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema, kulikuwa na changamoto za kikodi lakini pande zote zimeshakaa kwa maana ya Wizara, Wizara ya Fedha na mkandarasi na kwamba zile changamoto zilizokuwepo zimeondolewa na tunaamini muda sio mrefu barabara hii itaanza kujengwa na kwa maana ya kukamilika kwa barabara hii itakuwa imerahisisha sana wafanyabiashara na wananchi wa Wilaya alizotaja za Malinyi, Ulanga, Kilombero, Mlimba na hata Ifakara yenyewe.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto zilizokuwepo tayari Serikali na mkandarasi imeshakaa pamoja na imeziondoa na tuna hakika ujenzi utaanza mara moja ambao ulikuwa umesimama. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Wizara ya Ujenzi inataka kuunganisha barabara za mikoa kwa kiwango cha lami na kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuzi- upgrade barabara zetu kuwa kwa kiwango cha lami kwa sababu itasaidia wananchi kusafirisha mazao, lakini wananchi wataweza kupata huduma bora za kupita kwenye barabara inayopitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya kuunganisha barabara katika Mkoa wa Arusha ambayo inatoka Karatu kuunganisha Simiyu na inayotoka Karatu kwenda Mbulu kwa maana inaunganisha Arusha na Manyara.

Je, ni lini barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami kama ahadi inavyoeleza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja za Karatu – Simiyu – Mbulu – Manyara ni barabara muhimu na ni barabara za Mkoa na ni kipaumbele cha WIizara na Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zimeshawekwa kwenye mpango kwa sababu zinatakiwa zijengwe, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kujenga hizi barabara kunahitaji fedha na tunapopata fedha ndiyo tunapoanza ujenzi.

Kwa hiyo, kwa kuwa zipo kwenye Mpango na fedha hizi zinategemea pia na mapato ambayo Serikali inapata ili iweze kuzijenga kwa hiyo kwa kuwa stadi zimeshafanyika, mara fedha itakapopatikana na tunavyotambua ni kipaumbele chetu barabara zote ni mpango wa Serikali zote zinazounganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya ziwe kwa mpango wa lami, lakini hatutazijenga zote kwa wakati mmoja. Lazima tutaanza na barabara chache, tunafuata zingine mpaka tutakamilisha. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo ahadi ambayo ndani ya Ilani ya miaka mitano mfululizo 2015/2020 na 2020/2025 ujenzi wa barabara ya Makabe – Msakuzi – Mpiji Majohe ikiungana na barabara ya Kibamba Njiapanda – Mpiji Majohe kwenda Bunju kupita Mabwepande. Lakini pia ikumbukwe barabara hii pia ni ahadi ya mwisho kabisa ya Mheshimiwa Hayati Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba ni kati ya ahadi za mwisho kabisa za Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Nadhani aliitoa wakati yuko kwenye ile stand na bahati nzuri nilikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ikishakuwa na Mheshimiwa Rais ni utekelezaji. Lakini atakubaliana nami kwamba ahadi aliyotoa isingekuwa rahisi kwamba tumeanza kuitekeleza, lakini ahadi ambayo tunaizingatia na tayari shughuli zimeshaanza kuona namna ya kuanza kutekeleza ile ahadi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi kama zile zikishatolewa, kinachofuata ni utekelezaji na mimi nimhakikishie kwamba Serikali kupitia Wizara yangu hiyo ahadi tutaitekeleza. Ahsante.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri na Naibu Waziri, pia tunashukuru kwa ajili ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo madogomadogo lakini matengenezo haya madogomadogo hayakidhi haja ya barabara hii kwani wakati wa mvua inaharibika kabisa na tunakosa mawasiliano kati ya mji mmoja hadi mwingine. Je, Serikali haioni kuna haja ya kutupa commitment ni wakati gani barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili tutatue changamoto hii kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara zote za changarawe ama za udongo na hasa maeneo ya mwinuko inaponyesha mvua huwa zinakuwa na changamoto ya kuondoka udongo ama changarawe. Commitment ya Serikali pamoja kutekeleza ahadi ya Rais na Waziri Mkuu tayari Serikali inatafuta fedha ili tuweze kufanya usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha na fedha ikipatikana barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimshukuru Waziri kwa majibu ya Serikali ambayo ameyatoa, lakini naiomba Serikali kwamba MV Kitunda ni kivuko ambacho kinawasaidia sana wananchi wa Lindi kuvusha magari na bidhaa mbalimbali na shughuli za kiuchumi zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyoongea kivuko kimesimama kwa muda wa wiki moja changamoto iliyopo injini Na.2 kwenye selecta valve kuna shida. Naiomba Serikali kusaidia kwa haraka kupatikana kwa valve hii ili kivuko kiendelee kufanya kazi na wananchi waendelee kutumia kivuko hicho.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua umuhimu wa kivuko hiki cha MV Kitunda na kutokana na umuhimu wake tayari Wizara kupitia TEMESA imeshapeleka boti na hata hivi kutokana kwa kweli na ufuatiliaji wa karibu sana wa Mheshimiwa Hamida, Mbunge wa Lindi Mjini, tumepeleka boti kwa ajili ya kusaidia changamoto ambazo zinajitokeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba, kama tulivyoahidi kivuko hiki kitatengenezwa, lakini wakati kiko matengenezo boti hilo litaendelea kubaki hapo kwa ajili ya kusaidiana na boti la Halmashauri ya Lindi ili kuhakikisha kwamba eneo hilo halisimami kufanya kazi kati ya Lindi na Kitunda. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa swali hili limeulizwa kwa muda mrefu, kuanzia katika Mkutano wa Tatu, ambapo Mheshimiwa Kiswaga na mimi Mbunge wa Sumve tuliuliza na tukapata majibu ya namna hii hii.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kulifanyia kazi jambo hili na kuanza taratibu za manunuzi ili barabara hii ijengwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa barabara hii unaendana sambamba/unaathiriana na ujenzi wa reli ya kiwango cha standard gauge kutokea Isaka kwenda Mwanza kwa sababu, barabara hii kwa usanifu mpya inapita eneo tofauti na barabara iliyopo inapita na reli hii ikishajengwa, ina maana hakutakuwa na njia tena ya kupita kutoka Kwimba kwenda Magu.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati iharakishe ujenzi wa barabara hii, ili kuepuka kufunga njia ya kutoka Kwimba kwenda Magu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara hii tuliyoitaja kwa kiwango cha lami. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa na sisi kwa upande wa Wizara tayari tumeshakamilisha taratibu zote ili fedha itakapopatikana basi tuanze utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa suala la barabara hii aliyoitaja kuingiliana na reli hii ya kisasa ya SGR, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, yote hayo yalizingatiwa kwenye usanifu na kwa hiyo, tumuhakikishie kwamba, hakutatokea hiyo changamoto anayoisema kati ya muingiliano wa hizo barabara na hiyo reli. Cha msingi tu avute subira kwamba wakati reli imeshaanza kujengwa hiyo ya SGR kati ya Isaka na Mwanza, lakini fedha ikipatikana mara moja pia barabara hii itajengwa ili basi hii miundombinu yote iende sambamba kuyafungua hayo maeneo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Katika hali halisi hiyo pesa iliyotengwa 1.5 kwa ujenzi wa barabara ya lami ni ndogo sana na upembuzi yakinifu umefanyika muda mrefu sana.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza pesa angalau hata kidogo, watutengenezee hata kilometa 30 tu, kwa mwaka huu, halafu na zile zitakazobakia waongoze pesa kwa mwaka ujao watutengenezee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hela iliyotengwa ni hela ndogo kulingana na urefu wa barabara, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii fedha iliyotengewa ni fedha ya awali kwa ajili ya mobilization na kadri fedha itakavyoendelea kupatikana kwa jinsi Serikali itakavyopata, itazidi kuongezewa ili kujengwa kwa kiwango chote.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii inatakiwa ijengwe katika kipindi cha awamu yote hii ya miaka mitano. Kwa hiyo, kadri fedha itakavyoendelea kupatikana basi barabara hii tunahakika kwamba itajengwa yote kwa kiwango cha lami, kwa maana ya Masasi, Nachingwea hadi Liwale. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hii barabara siyo kwamba fedha Serikali hawana ya kujenga, ninachokiona hapa ni kwamba Serikali bado haijaamua kujenga hii barabara, kwa sababu zipo barabara zimefanyiwa upembuzi yakinifu tangu mwaka 2018, mwaka 2017, mwaka 2016 zimeshajengwa na zingine zinajengwa. Lakini hii tangu mwaka 2014, ninaiomba Serikali iamue kwa maksudi kabisa kuikomboa Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Nachingwea ili iweze kufunguka nasi kiuchumi tuweze kuwa miongoni mwa watu waliopo duniani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya vitu ambavyo vinaongoza katika kutengeneza hizi barabara kwa kweli ni uwezo wa Serikali kwa maana ya bajeti, lakini Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi za viongozi.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nachingwea - Liwale kwenye Ilani yetu ni kati ya barabara ambazo zipo kwenye usawa wa kilometa 7,500 ambazo zinatakiwa zikamilishwe usanifu wa kina kazi ambayo tayari imefanyika. Kwa hiyo ni hatua ya awali ambayo imefanyika na sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, usanifu tayari umekamilika kama ilivyoahidiwa kwenye bajeti mwezi Juni mwaka huu. Kwa hiyo, tayari Serikali imeshapiga hatua na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Liwale kwamba kwa kuwa tayari tumeshaanza kadri fedha zitakapopatikana naamini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Kuchauka ameonesha masikitiko yake makubwa kabisa, naamini nasi umetupa nafasi kwa maana ya Wabunge wa Nachingwea, Ndanda, Masasi na maeneo mengine kwenye umuhimu wa hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nimuulize Mheshimiwa Waziri, Wizara imetenga shilingi bilioni 1.5 tu, kwa makisio ya sasa ni kama kilometa moja na nusu, wanapotaka kuanza kujenga barabara hii wataanzia kujenga upande gani? kwa sababu shida ipo Masasi, shida ipo pia Nachingwea. Watueleze wanataka kuanza kujenga upande gani kwa pesa kidogo namna hiyo waliyoitenga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara tunachojenga ni kilometa hizo 45 kati ya Masasi na Nachingwea. Lakini hata ukianza Masasi, ukianza Nachingwea bado barabara ni ileile mtu atakapopita, atapita kokote. Nadhani nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kuanza wapi ama wapi nadhani isingekuwa ni hoja kubwa cha msingi tukamilishe hizo kilometa 45 kwa sababu hata kama itaanzia Masasi, itaanzia Nachingwea, lakini atakayepita, atapita tu kwenye hiyo barabara.

Mheshimiwa Spika, nadhani hilo aiachie Wizara na wataalam wataangalia pia wapi tunapofanya mobilization inaweza kuwa ni rahisi, jambo la msingi tukamilishe hizo kilometa 45. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo kule Liwale, Nachingwea yanafanana kabisa na yaliyopo katika Jimbo la Manyoni Magharibi Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya kwa barabara inayotoka Mkiwa, Itigi hadi Rungwa.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba katika bajeti tuliyopitisha barabara hii ya kuanzia Mkiwa kwenda Rungwa, Lupa hadi Makongorosi, imetengewa bajeti kuanza kwa kiwango cha lami. Na sisi kama Wizara tunategemea muda wowote barabara hii iweze kutangazwa kwa ajili ya ujenzi, kwa sababu ni kati ya barabara chache ambazo zimebaki ambazo ni barabara kuu, trunk, yaani kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zote za manunuzi zimeshakamilika, tunachosubiri ni kutangaza hiyo tender kwa sababu fedha imeshapitishwa na Bunge lililopita kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.