Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya (28 total)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa lami barabara yenye urefu wa Kilometa 50 toka Mbulu kwenda Haydom ambayo ipo kwenye mpango wa Bajeti tangu 2019/2020, 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu swali na ni mara yangu ya kwanza, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa Mbunge. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, pia nikishukuru sana chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua na hatimaye kunipitisha kuwa mgombea wa Jimbo la Ileje, lakini niwashukuru sana….

SPIKA: Sasa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba nijibu swali laMheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,Barabara ya Mbulu - Haydom yenye urefu wa kilometa 70.5 ni sehemu ya barabara yaKaratu – Mbulu – Haydom– Sibiti – Lalago – Maswayenye urefu wa kilomita 398 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali (Preliminary Design) wa barabara hii (kupitia mradi wa Serengeti Southern Bypass) ili kuijenga kwa kiwango cha lami umekamilika. Kazi hii ilifanywa na Kampuni iitwayo H.P. Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG mwaka 2016 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa wananchi wa Mbulu pamoja na Hospitali ya Haydom, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi kwa sehemu ya Mbulu
– Haydom yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami, ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020, ilitenga Shilingi milioni 1,450.00 na mwaka wa fedha 2020/2021, imetenga Shilingi milioni 5,000.00. Ujenzi wa barabara hii utatekelezwa kwa njia ya Kusanifu na Kujenga (Design and Build) na zabuni ya kazi hii itatangazwa wakati wowote katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Katika mwaka wa fedha 2020/2021, zimetengwa shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa Barabara ya kutoka Kahama - Nyang’holongo – Kharumwa – Nyijundu – Busolwa - Ngoma hadi Busisi Sengerema kwa kiwango cha lami itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika,Barabara ya Kahama - Nyang’holongo - Kharumwa - Nyijundu - Busolwa - Ngoma hadi Busisi Wilayani Sengerema (yenye urefu wa kilometa 162.99), inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Barabara hii inaunganisha mikoa mitatu ya Shinyanga, Geita na Mwanza kupitia Wilaya za Msalala (Shinyanga), Nyang’hwale (Geita) na Sengerema (Mwanza).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii, hivyo inatafuta fedha za kufanya usanifu, ikiwa ni maandalizi ya kuijenga barabara hiyo, kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 581.827 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha changarawe. Aidha, Wizara kupitia TANROADS inaendelea kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI (K.n.y MHE. ABUBAKAR D. ASENGA) Aliuliza: -

Je, ni lini Ujenzi wa Barabara ya Kidatu hadi Ifakara utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshmiwa Abubakar Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kidatu – Ifakara ni sehemu ya Barabara Kuu ya Mikumi - Kidatu - Ifakara - Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye urefu wa jumla ya kilometa 547. Barabara hii ni miongoni mwa barabara muhimu katika Taifa kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Morogoro na mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara ya Njombe, Ruvuma na Lindi kupitia Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara kati ya Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa kilometa. 66.9 pamoja na Daraja la Ruaha Mkuu vinajengwa na Mkandarasi M/S Reynolds Construction Company Limited (Nigeria).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii kwa gharama ya Euro 40,441,890.81 takribani sawa na shilingi bilioni 113.13 bila VAT. Mradi ulitegemea kukamilika tangu tarehe 29 Septemba, 2020. Mradi huu umechelewa kukamilika kwa sababu za kimenejimenti kwa upande wa Mkandarasi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kumsimamia Mkandarasi kwa karibu ili akamilishe mradi kama ilivyopangwa. Mradi huu umepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.
MHE. JACQEULINE N. MSONGOZI (K.n.y MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ni miongoni mwa viwanja vya ndege vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga vinavyotarajiwa kujengwa na kukarabatiwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB).

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za makubaliano ya mkataba wa miradi hiyo baina ya Serikali (kupitia Wizara ya Fedha na Mipango) na Mfadhili (Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – EIB) tayari zimekamilika na idhini (No Objection) ya kuanza utekelezaji wa miradi yote minne (4) imetolewa na Mfadhili wa miradi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Mkandarasi (M/ s Sino Shine Overseas Construction & Investment East Africa Limited) na Mshauri Elekezi (SMEC International PTY Limited) ikishirikiana na Kampuni ya SMEC International Tanzania Limited) kwa ajili ya kutekeleza kazi hii, wamepatikana. Hivyo hivi sasa, Serikali iko katika hatua za awali za kuanza utekelezaji wa mradi huu.
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Karatu – Dongobesh – Hydom hadi Singida iliyotengewa fedha katika bajeti iliyopita utaanza?
NAIBU WAZIRI WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala kama hili lilijitokeza, swali namba 7 ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Mbulu Mjini, kwa hiyo, inaonyesha ni kwa kiasi gani barabara hii ni muhimu na majibu yangu ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbulu – Haydom yenye urefu wa kilometa 70.5, ni sehemu ya barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Lalago – Maswa (km 398) inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali (Preliminary Design) wa barabara hii (kupitia mradi wa Serengeti Southern Bypass) ili kuijenga kwa kiwango cha lami, umekamilika. Kazi hii ilifanywa na kampuni iitwayo H.P. Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG mwaka 2016 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).

Mheshimiwa Naubu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii ambayo itawezesha wananchi wa Mbulu kupata huduma katika Hospitali ya Haydom, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Mbulu – Haydom (km 50) kwa kiwango cha lami; ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021, shilingi bilioni tano zilitengwa. Utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua za manunuzi na ujenzi wake utafanywa kwa njia ya Kusanifu na Kujenga (Design and Build). Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga fedha shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay, swali la nyongeza.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba barabara hii ina umuhimu na sasa kwa miaka miwili imekuwa ikiwekwa kwenye bajeti na haikujengwa na amesema imetegwa shilingi bilioni 5, je, atuambie ni lini atatangaza tenda ili barabara hii ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa anajua wazi kwamba bilioni 5 haiwezi kujenga barabara na barabara hii iko kwenye Ilani ya uchaguzi mwaka 2015-2020 na 2020-2025 na Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni juzi hapa, je, yupo tayari kuweka fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ili kumaliza kilomita zingine 20 kufika 70 kufikia eneo la Haydom?
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya Kitahi – Lituhi kupitia Ruanda itaanza kujengwa ili kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, magari yote makubwa yanatakiwa yachukue makaa ya mawe katika eneo la Amani Makoro kwa ajili ya kupeleka maeneo mbalimbali nchini. Makaa ya mawe huchukuliwa na magari yenye uzito usiozidi tani 15 kutoka Mgodini (eneo la Ngaka) hadi Amani Makoro.

Ili kurahisisha uchukuaji wa makaa ya mawe kutoka Amani Makoro kwenda maeneo mengine nchini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kitahi – Lituhi (km 84.5) kwa awamu ambapo mpaka sasa km 5 kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro (Coal Stockpile) zimekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 9,000 katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kiwango cha lami kwa kilometa tano nyingine. Kazi za ujenzi kwa sehemu hii zinatarajia kuanza mwishoni mwa Aprili, 2021. Aidha, ili kuhakikisha barabara yote inapitika kipindi chote cha mwaka, Serikali imetenga kiasi cha shillingi milioni 1,800 za matengenezo mbalimbali katika mwaka wa fedha 2020/ 2021.
MHE. HASSAN S. MTENGA Aliuliza: -

Je, Serikali haioni sababu kwa sasa kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha korosho zinazolimwa Kusini badala ya kutumia njia ya magari ambayo yanasababisha uharibifu mkubwa wa barabara kwenda Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, wafanyabiashara wamekuwa wakitumia bandari ya Mtwara kusafirisha korosho zinazolimwa kusini mwa nchi kwa kuzingatia ushawishi wa Serikali wa kutumia zaidi bandari hiyo badala ya kutumia njia ya magari ambayo ni kweli inachangia uharibifu wa barabara na wakati mwingine ajali za mara kwa mara. Katika kufanikisha nia hii, Serikali imeendelea kufanya vikao na wadau mbalimbali ili waweze kutumia Bandari ya Mtwara na hasa baada ya kufanya maboresho makubwa katika bandari hiyo kwa kujenga gati jipya na kuongeza kina cha maji ili meli kubwa zaidi ziweze kutia nanga katika bandari hiyo ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, changamoto za Bandari ya Mtwara ni utegemezi wa shehena ya aina moja tu ya korosho inayotoka Mtwara na hakuna shehena nyingine inayoingia katika Bandari hiyo. Hali hiyo inasababisha gharama za usafirishaji kuwa juu kutokana na meli kuja zikiwa tupu bila mzigo ili kufuata shehena ya korosho Mtwara tofauti na Dar es Salaam.

Kufuatia kuwepo kwa changamoto hiyo Serikali inaendelea kuwashawishi wenye meli kupunguza gharama za usafirishaji ili kufidia gharama za kusafirisha korosho kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa njia ya barabara. Aidha, Serikali kupitia TPA (Mamlaka ya Bandari) inaendelea kuitangaza bandari ya Mtwara ili zipatikane shehena zinazoingia katika bandari hiyo, ahsante.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani kuhusu kujenga daraja katika Mto Maragalasi Ilagala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja katika Mto Maragalasi katika eneo la Ilagala liko katika barabara ya Mkoa wa Kigoma (Simbo – Ilagala – Kalya) yenye urefu wa kilometa 235. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 345 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa kutambua umuhimu wa daraja husika kwa wananchi, hususan wa Mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani, baada ya kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali imejipanga kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza na kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.
MHE. HAMISI S. TALETALE Aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Bigwa – Kisaki itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 2020 – 2025 inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 133.28 ambapo kilomieta 18.4 ni za lami na kilomita 115.14 ni za changarawe. Barabara hii ni kiungo muhimu kwa Mkoa wa Pwani na Morogoro na pia ni barabara inayoelekea katika Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji ambalo ujenzi wake unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ilikamilika mwezi Novemba, 2017 chini ya Kampuni ya Uhandisi ya UNITEC Civil Consultants Ltd ya Tanzania kwa ushirikiano na Kampuni ya Multi-Tech Consult (Pty) Ltd ya Gaborone, Botswana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Wakati Serikali inatafuta fedha za ujenzi, imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 1,492 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara husika. Ahsante.
MHE. FRANCIS L. MTEGA Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Rujewa – Madibira – Mafinga (kilometa 151) utaanza kwa kuwa upembuzi yakinifu umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Rujewa – Madibira – Mafinga yenye urefu wa kilometa 152.1 ni Barabara ya Mkoa ambayo ipo chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS). Sehemu ya barabara hii, yani Rujewa hadi Madibira yenye urefu wa kilometa 97.1, inahudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya na sehemu iliyobaki kipande cha Madibira hadi Kinyanambo chenye urefu wa kilometa 55, kinahudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa. Barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 na ahadi za Viongozi Wakuu wa Nchi kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii ambayo inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya mpunga na mahindi, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii. Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi, Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea kufanya matengenezo ya barabara hii ili ipitike majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, barabara hii imetengewa kiasi cha shilingi milioni 757 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na shilingi bilioni 3,380,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara ya Masasi – Nachingwea inayounganisha makao makuu ya wilaya ya Masasi na Nachingwea, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tangu mwaka 2015. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, barabara yenye urefu wa kilometa 45. Katika mwaka wa fedha huu 2020/2021, jumla ya shilingi bilioni 1.43 zimetengwa kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi pia imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali kwa barabara hii ambapo katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 232.66 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika katika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kuanzia Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa Mjini yenye urefu wa takribani kilometa 30 ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa ulianza kutekelezwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014. Ujenzi huu ulianza baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2013 uliohusisha barabara ya Mbande – Kongwa Junction. Kongwa Junction – Ugogoni kilometa 17.5, Kongwa Junction – Mpwapwa – Ving’awe kilometa 38.85 na Mpwapwa – Gulwe – Kibakwe kilometa 46.93.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi kwa kiwango cha lami ulianza, ambapo hadi sasa ujenzi wa sehemu ya Barabara ya Mbande – Kongwa Junction kilometa 16.7 umekamilika. Serikali kwa sasa inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa. Katika mwaka wa fedha huu tunaondelea nao Serikali imetenga shilingi bilioni 4.95 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami katika mji wa Mpwapwa. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa utaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ya barabara hizi ili ziendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1.1 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Pandambili – Saguta – Mpwapwa – Ng’ambi na shilingi milioni 751.596 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Manchali – Ng’ambi – Kongwa Junction – Hogolo Junction ambapo barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa imezingatiwa. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 124 kwa kiwango cha lami ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi kati ya nchi yetu na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye km 124 ni barabara muhimu kwa kuwa inaunganisha Nchi ya Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma.

Aidha, barabara hii inahudumia wasafiri wanaotumia uwanja wa ndege wa Songea wanaotokea Nchi jirani ya Msumbiji na maeneo mengine ya Mkoa wa Ruvuma. Vile vile, barabara hii ni muhimu kwenye suala la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ilikamilisha usanifu wa kina wa barabara hii chini ya Kampuni ya Crown Tech - Consult Limited ya Tanzania. Hata hivyo, kufuatia uchimbaji wa makaa ya mawe kwenye eneo la Mhukulu lililopo kilomita 80 kutoka Songea na kilomita 60 kutoka Likuyufusi, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS, ilikamilisha mapitio ya usanifu wa kina wa barabara hii (mwaka 2020) ili iendane na mahitaji na mazingira ya sasa. Vile vile, katika Mwaka huu wa Fedha 2020/2021, Daraja la Mkenda limetengewa shilingi milioni 110 kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 shilingi bilioni 1.59 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilomita 10. Kazi inatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2021 baada ya kukamilisha taratibu za manunuzi. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni
1.346 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ili barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo, yenye urefu wa kilometa 296 ambayo ipo katika Ilani ya CCM 2020?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo yenye urefu wa kilometa 296 ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi – Kidatu – Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye kilometa 547 ambayo inaunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Wizara kupitia TANRAODS, imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2018. Ujenzi wa sehemu ya Kidatu – Ifakara kilometa
66.9 kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Ruaha Mkuu unaendelea. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu iliyobaki ikiwemo ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo zinaendelea kutafutwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi, Serikali pia imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ya barabara hii, ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 720 na shilingi milioni 377.2 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii katika mikoa ya Morogoro na Ruvuma mtawalia ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza kipande cha barabara kutoka Mbagala Zakhem hadi Mbagala Kuu na kipande cha barabara toka Mbande – Kisewe hadi Msongola?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Jafari Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbagala Zakhem – Mbagala Kuu yenye urefu wa kilometa 5.1 ni miongoni mwa barabara ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne alitoa ahadi mwaka 2017/2018. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilijenga kilometa moja ya lami katika barabara hii ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara ya Mbande – Kisewe – Msongola ni sehemu ya barabara ya Chanika – Mbande – Mbagala Rangi Tatu yenye urefu wa kilometa 29.4 inayounganisha barabara ya Kilwa na barabara ya Nyerere. Kati ya kilometa 29.4 kilometa 22.8 zimekwishajengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 6.06 zilizobaki zipo kwenye kiwango cha changarawe. Barabara hii inasimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Msongola mpaka Mbande kilometa 6.06 kwa kiwango cha lami. Ujenzi unaendelea kwa awamu kupitia fedha za maendeleo ambapo kuanzia mwaka 2018/2019 hadi mwaka 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1.05 zimetumika kujenga kilometa moja kwa kiwango cha lami nyepesi. Kazi hiyo imeanza Msongola kuelekea Mbande. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:-

Je, ni lini ahadi ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Lushoto – Muyanta hadi Mlalo itaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Lushoto – Mlalo yenye urefu wa kilometa 41.93 ni sehemu ya Barabara ya Lushoto – Mlalo – Umba junction yenye urefu wa kilometa 66.23 ambapo kati ya hizo, kilometa tisa ni za lami na kilometa 32.93 ni za changarawe. Katika mwaka wa fedha wa 2020/ 2021 kiasi cha milioni 420 zimetengwa kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa mita 400 za barabara hii kwa kiwango cha lami. Ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu zilizobaki utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Barabara ya Lushoto – Mlalo – Umba Junction kiuchumi, kiulinzi na kiutalii na hivyo wakati ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu ukiendelea, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo mbalimbali kila mwaka. Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 jumla ya Shilingi milioni 475.5 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo inapitika majira yote ya mwaka.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa Daraja la Mto Mbaka linalounganisha Jimbo la Busokelo na Rungwe litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Mbaka ambalo lipo katika barabara ya Katumba - Lwangwa - Tukuyu yenye jumla ya kilometa 81, linaunganisha Halmashauri ya Busokelo na Mji wa Tukuyu. Barabara hiyo ni ya mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, hapo awali daraja hili lilikuwa la chuma (Bailey) lakini kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hilo lililopo kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mazao ya misitu, Serikali iliamua kulijenga kwa kiwango cha zege kuanzia mwaka 2018. Hata hivyo, wakati ujenzi ukiendelea kulijitokeza changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na usanifu ambao ilibidi urudiwe kuendana na hali halisi ya eneo husika. Usanifu huo ulikamilika mwezi Oktoba, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mkandarasi anaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ambapo kazi za ujenzi zimefikia asilimia 68 na kazi zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI Aliuliza: Serikali ina mpango wa kuunganisha mikoa yote kwa mtandao wa barabara za lami, ikiwemo barabara yenye urefu wa kilometa 223 inayounganisha Mikoa ya Njombe na Morogoro kupitia Mlimba ambayo pia iko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM):-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara anayozungumzia Mheshimiwa Mbunge ni Barabara ya Ifakara – Mlimba – Taweta – Madeke yenye urefu wa kilometa 220.22 ambayo ni barabara ya mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya kutoka Ifakara hadi Kihansi (kilometa 126) ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami (kilometa 24) kilichojengwa hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba.

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu iliyosalia kati ya Kihansi na Madeke (kilometa 94.2) umepangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha wa 2020/2021 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Kazi hii ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ina kamilisha usanifu wa kina, imeendelea kutenga fedha na kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika kipindi chote cha mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021, jumla ya shilingi bilioni 2.29 zimetengwa. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO Aliuliza:-

Pamoja na kazi nzuri ya miradi ya kutengeneza barabara Nkenge, viongozi wetu kwa nyakati tofauti wameahidi kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara za Kabyaile/Shozi – Njiapanda ya Gera, Minziro – Mutukula, Kaja Hospitali ya Mugana (Bwanja).

Je, ni lini barabara hizo zitatengenezwa ili kuondokana na kero hizo zinazowapata wananchi wanaotumia barabara hizo kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mutukula – Minziro (kilometa 15.8) ni barabara ya ulinzi na pia ni moja ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Barabara hiyo inatakiwa kufunguliwa na tayari kilometa mbili zipo na zinatumika. Kilometa 13.8 zilizosalia zinapita katika mashamba na Hifadhi ya Msitu wa Minziro na zitaendelea kufunguliwa kwa awamu. Makisio ya ujenzi wa barabara hiyo yamefanyika na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)ambapo jumla ya shilingi bilioni 3.63 zinahitajika kwa ujenzi wa kiwango cha changarawe na shilingi bilioni 9.994 zinahitajika kwa ujenzi wa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zingine ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, Serikali itaendelea kuziboresha ili kuhakikisha kuwa zinapitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE Aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Mtwara Pachani – Nallasi – Tunduru itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mtwara Pachani – Lingusenguse – Nallasi Tunduru yenye urefu wa kilometa 300 kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilitekelezwa na Mhandisi Mshauri GEG wa Ureno kwa gharama ya shilingi bilioni 2.559 na ilikamilika mwaka jana (2020). Kwa sasa, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi wa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini, inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 2.293 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI Aliuliza:-

Je, ni lini Daraja la Kisorya – Lugezi litakalounganisha Wilaya za Bunda na Ukerewe litajengwa ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa daraja litakalounganisha Wilaya ya Bunge na Ukerewe ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba – Kisorya – Nansio yenye urefu wa kilomieta 121.6 ambao utekelezaji wake umeanza na uko katika hatua mbalimbali. Kazi ya upembuzi yakinifu na usaniifu wa kina wa barabara ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba hadi Kisorya yenye urefu wa kilometa 107.1 ilikamilika Machi, 2013. Aidha, usanifu wa kina wa sehemu ya barabara ya Kisorya – Rugezi – Nansio (Ukerewe) yenye urefu wa kilometa 14.5 pamoja na Daraja la Rugenzi – Kisorya ulikamilika Aprili, 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu umegawanyika katika sehemu tatu, yaani Lots tatu, ambazo ni Nyamuswa – Bunda – Bulamba (Lot I) yenye urefu wa kilometa 56.1; Lot II bulamba – Kisorya yenye km. 51 na Lot III Kisorya – Lugezi – Nansio yenye urefu km. 14.5 inayojumuisha na daraja la Kisorya – Rugezi yaani daraja lina urefu wa mita 1000. Hadi sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Bulamba – Kisorya ambao ni Lot II umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba Lot I kwa kiwango cha lami unaendelea na umefikia asilimia tano. Aidha, ujenzi wa sehemu ya Rugezi – Nansio Pamoja na daraja la Kiisorya – Rugezi utaannza baada ya fedha kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa sehemu ya Kisorya – Rugezi – Nansio ikiwemo ujenzi wa daraja Serikali kupitia wakala wa ufundi na umeme TEMESA inaendelea kutoa huduma ya kuvusha wananchi wa maeneo haya kupitia kivuko cha MV Ujenzi.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE Aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga reli ya TAZARA kutokea Tunduma kwenda Kasanga ili kuwa na manufaa mapana ya kiuchumi na matumizi mazuri ya Bandari ya Kasanga na kuufungua Mkoa wa Rukwa kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya reli nchini ambayo utekelezaji wake unazingatia kipaumbele kutokana na utekelezaji wa miradi ya reli kuhitaji fedha nyingi. Hivi sasa, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa Reli ya Mpanda – Karema na ni matumaini yetu kwamba, mradi wa reli hii utakapokamilika, utaifungua Mikoa ya Rukwa na Katavi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga reli ya kutoka Tunduma hadi Kasanga, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ushauri wake umepokelewa na Wizara itaufanyia kazi. Aidha, kama nilivyosema awali, kwa kuwa miradi ya reli inahitaji fedha nyingi, utekelezaji wa ushauri huu utazingatia matokeo ya upembuzi yakinifu utakaofanywa kuhusu kipande hicho cha reli ikiwa ni pamoja na vipaumbele vya nchi. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa barabara kutoka Kilindi kwenda Gairo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindi – Yogwe – Gairo yenye jumla ya kilometa 115.7 ni barabara ya Mkoa inayounganisha mikoa ya Tanga na Morogoro kupitia Wilaya ya Kilindi na Gairo na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, kwa sasa Serikali haijapata fedha ya kuanza ujenzi wa barabara ya Kilindi – Iyogwe – Ngirori hadi Gairo kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili kuhakikisha kuwa inaendelea kupitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Kolandoto hadi Kishapu kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la na Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kolandoto hadi Kishapu inayojulikana kwa jina la Kolandoto – Mwangongo yenye urefu wa kilometa 53 ni sehemu ya barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Oldeani B, yenye urefu wa kilometa 328 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ili kuijenga kwa kiwango cha lami imekamilika. Kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri M/S. Intercontinental Consultants and Technocrats pvt Ltd ya India.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeanza maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ambapo katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao, jumla ya hilingi milioni 2,500 (bilioni 2.5) zilitengwa. Aidha, wakati maandalizi ya kuanza ujenzi yakiendelea, Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 443.31 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. ALFRED J. KIMEA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Old Korogwe kwenda Kwamndolwa - Magoma - Mashewa - Bombomtoni - Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilomita 127.54 kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa wananchi wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bongomtoni – Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilometa 127.69 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo inayopita barabara kama ilivyotajwa hapo juu. Ili kuweza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 1,450.78 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka injini mpya ya Kivuko cha MV Kitunda - Lindi Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), umetenga fedha kiasi cha Shilingi Milioni 850 kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa ajili ya ukarabati wa Vivuko nchini kikiwemo MV Kitunda ambacho ukarabati wake utahusisha ubadilishaji wa injini pamoja na matengenezo mengine. Ukarabati huu utaanza robo ya pili ya mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI K.n.y. MHE. SHANIF M. JAMAL Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Hungumalwa - Ngudu hadi Magu kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Mansoor Jamal, Mbunge wa Kwimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Hungumalwa – Ngudu hadi Magu ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 71. Barabara hii ni kiunganishi muhimu kati ya Wilaya za Kwimba na Magu kupitia Hungumalwa - Ngudu - Bukwimba hadi Isandula Wilayani Magu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) ilikamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Hungumalwa – Ngudu – Bukwimba – Magu yenye urefu wa kilometa 71 mwaka 2019. Katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 1,500 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, Serikali kupitia (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi milioni 926.711 zimetengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa barabara ya Masasi hadi Liwale kupitia Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY K. MSONGWE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Masasi hadi Liwale kupitia Nachingwea kwa kiwango cha lami ambapo kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa sehemu ya Masasi – Nachingwea – Nanganga yenye urefu wa kilometa 90 ilikamilika mwaka 2014 na sehemu ya Liwale – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 130 imekamilika mwezi Juni, 2021. Katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 1,500 yaani sawa na shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Masasi – Nachingwea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha inaendelea kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 634 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.