Supplementary Questions from Hon. Issa Jumanne Mtemvu (27 total)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji Chunya unafanana na ule mradi wa 2F2B pale Tegeta A, ujazo wa lita milioni sita. Je, Wizara inaweza ikatuambia ni lini mradi ule utakamilika ili uweze kusaidia wananchi wote wa Goba?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ule mradi wa tanki Mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mpiji Magohe, Makabe yote na Msakuzi.
Je, ni lini pia mradi huo utakamilika ili wananchi wapate maji salama?
SPIKA: Swali sio lako, kwa hiyo unapaswa kuuliza swali moja tu, sasa chagua mojawapo katika hayo ya kwako.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niweze kufahamu mradi unaotaka kujengwa mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mbezi, Makabe na Mpiji Magohe utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Mtemvu kutoka Kibamba kama ifuatavyo:-.
Mheshimiwa Spika, Wizara sasa hivi inapitia miradi hii yote ambayo usanifu wake ulikamilika. Kwa hiyo nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge huo mradi upo katika miradi ambayo inakwenda kutekelezwa awamu hii kabla mwaka huu wa fedha haujaisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa Busanda unafanana sana na ule mradi uliopo Wilaya ya Ubungo, hasa mradi wa 2f2b, unaoanzia Changanyikeni, Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo na hasa ujenzi wa tanki kubwa la lita milioni sita pale Tegeta A, Kata ya Goba. Je, mradi huu utakamilika lini ili wananchi wote wa Kata ya Goba wapate maji safi, salama na yenye kutosheleza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu kutoka Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote hii ambayo tayari utekelezaji wake unaendelea Wizara tunasimamia mikataba na namna ambavyo mkataba unamtaka yule mkandarasi kukamilisha mradi ule. Mheshimiwa Mbunge ninakupa uhakika kwamba tutasimamia kwa karibu na mradi ule utakamilika ndani ya muda ambao tumeupanga.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo ahadi ambayo ndani ya Ilani ya miaka mitano mfululizo 2015/2020 na 2020/2025 ujenzi wa barabara ya Makabe – Msakuzi – Mpiji Majohe ikiungana na barabara ya Kibamba Njiapanda – Mpiji Majohe kwenda Bunju kupita Mabwepande. Lakini pia ikumbukwe barabara hii pia ni ahadi ya mwisho kabisa ya Mheshimiwa Hayati Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba ni kati ya ahadi za mwisho kabisa za Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Nadhani aliitoa wakati yuko kwenye ile stand na bahati nzuri nilikuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ikishakuwa na Mheshimiwa Rais ni utekelezaji. Lakini atakubaliana nami kwamba ahadi aliyotoa isingekuwa rahisi kwamba tumeanza kuitekeleza, lakini ahadi ambayo tunaizingatia na tayari shughuli zimeshaanza kuona namna ya kuanza kutekeleza ile ahadi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi kama zile zikishatolewa, kinachofuata ni utekelezaji na mimi nimhakikishie kwamba Serikali kupitia Wizara yangu hiyo ahadi tutaitekeleza. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ya kuridhisha kwa kiasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamekuwa na watumishi wengi ambao wamekaa muda mrefu, zaidi ya miaka kumi hadi ishirini wakiwa wanalilia suala la muundo huu ambapo umetoka Waraka Na.3 wa Mwaka 2015 bila kutekelezwa kwa wakati. Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyeo vyao kwa mserereko ili kuzingatia muda waliotumia kazini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la hadhi ya Kitengo cha Uhasibu, ni kweli Serikali inajibu juu ya vigezo ambavyo vinafanyiwa tathmini mara kwa mara na Ofisi ya Rais, Utumishi. Natambua vigezo vyenyewe vinazingatia job analysis na job design. Kwa msingi huo, ni ukweli kada hii imeacha kutumia local standards kwa muda mrefu sana na sasa wanatumia international standards katika kutengeneza mizania mbalimbali ya taasisi. Vilevile hata ripoti za CAG tunaziona jinsi gani zinavyotoka tayari kila mmoja anahamaki juu ya kuiona hadhi ya taasisi inabebwa na sehemu au kitengo hiki. Tunao mfano, juzi tu taarifa ya CAG baada ya kuitoa tayari viongozi wa Serikali wametoa maelekezo magumu kwa section hii, yaani Wakuu wa Idara au Vitengo hivi.
Mheshimiwa Spika, lakini mwisho hadhi hii inategemea kazi kubwa wanayoifanya. Tayari uchumi na mipango wana hadhi ya Kurugenzi…
SPIKA: Mimi nilifikiri swali huwa linakuwa ni swali.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni swali, natengeneza hoja ya kuuliza swali la mwisho hili.
SPIKA: Hapana, unahutubia Mheshimiwa.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi kwa misingi hiyo miwili sasa Serikali haioni ni muda mwafaka wakifanya analysis yao wa kukipa hadhi Kitengo hiki cha Uhasibu na Idara ya Ukaguzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu kwa kuwatetea watumishi hawa, lakini nimjulishe kwamba ni dhamira ya Serkali na Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka kuhakikisha kwamba inapandisha vyeo na hadhi za wafanyakazi na watumishi wake ambao wanafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hao Wakaguzi wa Hesabu, Wahasibu pamoja na Wasaidizi wao watapandishwa vyeo pale ambapo hali ya bajeti itaruhusu lakini kwa kuzingatia vigezo ambavyo vimewekwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na vigezo hivyo, kama ambavyo nimejibu katika swali lake la msingi ni kwamba utaratibu huu ambao umewekwa upo kwa mujibu wa Sheria ile ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi ambayo ndiyo imesababisha kutayarishwa Waraka huu Na.3. Kwa kuzingatia sheria hiyo na Waraka ule, ndiyo utaratibu huohuo ambao utaendelea kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa changamoto zilizopo ndani ya Jimbo la Kinondoni kuhusiana na Mto Msimbazi ni sawa kabisa na changamoto zilizopo katika Mto Mbezi na Mto Mpiji ndani ya Jimbo la Kibamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ni lini sasa itaanza kutengeneza kingo za mto Mbezi ili kuokoa taasisi za Serikali mashule lakini vile vile na nyumba za wananchi, kuondolewa na maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa juhudi yake ya kupitia na kufanya mambo yaliyomengi ndani ya Jimbo la Kibamba. Kwa hakika Serikali ipo tayari kufanya tathimini ama inafanya tathmini juu ya jambo hilo mara tu mwaka wa fedha tutakapopata idhini ya fedha za kutosha basi tutapita ndani ya Jimbo hilo na kutatua changamoto ambazo zinazikabili Jimbo la Kibamba.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo barabara ya Temboni – Msingwa kwenda Kinyerezi ina changamoto kubwa sana kwa muda mrefu. Je, mchakato unaoendelea kupata mkandarasi ni lini utakamilika na barabara hiyo kuanza kujengwa chini ya TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha kwamba, barabara ya Temboni – Msimbwa kwenda Kinyerezi imeharibika na anataka kujua lini barabara hii itaanza kujengwa. Nimwambie tu kwamba, mchakato unaendelea na mchakato utakapokamilika kama ambavyo yeye ameainisha, tutakapomaliza huu mchakato hii barabara itaanza kujengwa mara moja kwa sababu, tumeshaitenga katika bajeti. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali yanayoridhisha kwa wastani, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, majibu ya Serikali yanaeleza wazi juu ya utoaji wa hati 845 tu kati ya upimaji uliokamilika wa watu 100,041 asilimia 0.0056 katika kipindi chote cha miaka miwili. Je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi wa kupunguza lile tatizo la premium ambalo linasababisha bei kubwa kwa wananchi ambao wanashindwa zaidi ya ile 180,000 ambayo wamelipa kwa wale wa kampuni? Sasa hapa ni kupunguza ile premium.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni kweli kwenye majibu ya msingi inasema wachangiaji ni 30,000, lakini kwa taarifa nilizonazo kama Mbunge ni zaidi ya wachangiaji 80,000. Kwa hiyo, jumla ya fedha ni bilioni nne wanazisema, mimi nasema bilioni 15. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kupeleka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ili akafanye ukaguzi maalum tuje na takwimu zilizo sahihi kwa ajili ya fedha za wananchi zilizopotea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali yake mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimsahihishe, si kweli kwamba, hati 847 tu ndio zimeandaliwa. Kwenye jibu langu la msingi nimesema hati 1,754 kati ya waombaji 1,925 tayari zimeandaliwa na wamechukua, lakini tunaendelea kuandaa hati kwa sababu, viwanja vilivyokamilika ni 8,316 kwa hiyo sio 845 kama alivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia suala la kupunguza premium kwamba, pengine wananchi wanashindwa kuchangia. Naomba tukumbuke tu kwamba, premium hii awali ilikuwa ni 15% kwa viwanja vyote. Ikapungua ikawa 7.5%, lakini badaye Wizara ikapunguza zaidi kwenye zoezi la urasimishaji wanalipa 1% ya premium ambayo wanatakiwa kulipa tofauti na ule upangaji wa kawaida, ilitoka 7.5% wao wanalipa 2.5%. Kwa hiyo, kama ni suala la kupunguza ni kweli upunguzaji tumepunguza, lakini kwa sababu ni hoja inatolewa na Serikali ni sikivu basi tutaona namna kama kuna haja ya kupunguza tena au tuendelee na ileile 1%. Tukumbuke kodi hizi pia ndio zinarudi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili amezungumzia kwamba, pesa ambazo zimekusanywa tulizotoa takwimu hapa ni tofauti. Si kweli anachosema, kwa mitaa mitano haiwezi kukusanya bilioni 15 kwa zoezi la urasimishaji, ukizingatia kwanza walipaji wenyewe ni wachache na nimetaja kati ya waombaji 147,000 tunaoshughulika nao sasa hivi ni 1,925 tu ambao wamekamilisha malipo yote. Kwa hiyo, si kweli kwamba, kuna pesa nyingi ambazo zipo,
Mheshimiwa Naibu Spika, kama pengine Mheshimiwa Mbunge anajua kuna mahali ambapo kuna pesa zimekusanywa na pengine hazijulikani zilipo, ameomba ukaguzi ufanyike, tutalifanyia kazi ili tuweze kujua ukweli wa Mheshimiwa Mbunge aliouleta na takwimu tulizonazo Wizarani ili tuweze kuwa na uhakika na alichokisema. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa Jimbo la Kibamba sasa changamoto yake kubwa ni usambazaji wa mabomba tu katika maeneo mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa kauli au maelekezo ya utoaji wa mabomba yale ili wananchi wa maeneo mengi wapate maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kidhati ya moyo nikupongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mtemvu. Moja katika bajeti yako umeonesha masikitiko yako eneo ambalo halina maji na tumekwishakubaliana na commitment yangu mimi baada ya Bunge tunakwenda Kibamba tunakwenda kumaliza kabisa tatizo la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na tumeshatoa maelekezo mahususi kwa DAWASA, wamefanikiwa maeneo mengi sana, walipe kipaumbele Jimbo la Kibamba katika kuhakikisha kwamba, tunaenda kumaliza kabisa tatizo la maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa ipo barabara ambayo ilitolewa ahadi na hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, barabara ya Kibamba – Mpiji – Mabwepande na tayari bajeti ya Wizara hii imepita.
Sasa nataka kauli ya Serikali juu ya bajeti husika juu ya barabara hii; ni nini kimefanyika juu ya utengenzaji wa barabara hii katika mwaka huu ikitegemea Hayati alisema wapelekewe kwa udharura?
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba bajeti yetu imepitishwa tarehe 27 na 28 Mei, 2021 hapa Bungeni tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti yetu. Tunaomba tuwahakikishie kwamba ahadi zote za viongozi wakuu, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli, Mama Samia aliyepo madarakani sasa, Mheshimiwa Waziri Mkuu na ambazo zimetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi zitatekelezwa. Tupeane muda tu. Mheshimiwa Mbunge, tutapitia kwa haraka haraka tuweze kujua ni barabara gani zimetajwa, zipo nyingi nchi nzima. Siwezi kukudanganya hapa lakini tukipitia kama ipo na fedha yake imetengwa tutaisimamia na kazi itafanyika na bahati nzuri tumepanga kwamba eneo hilo tutoe malalamiko mkoa wa Dar es Salaam, tumewekeza fedha za kutosha kuboresha barabara ili uchumi wa Tanzania uendelee kuku ana fedha hizo zifanye kazi za kujenga uchumi wa Watanzania kutoa huduma za kijamii. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Swali la kwanza; kwa kuwa majibu ya Serikali yanathibitisha kuwepo kwa watumishi 332 kukaimu wakiwa na sifa lakini zaidi ya watumishi 1,164 wanakaimu bila sifa yaani hawana kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Sasa na ni ukweli kuwepo kwa viongozi wengi wanaokaimu kunazorotesha utendaji kazi na hivyo kutofikia malengo tarajiwa. Je, ni ipi sasa commitment ya Serikali kuwathibitisha au kuwaondoa watumishi wenye kukaimu zaidi ya miezi sita? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa mchakato wa uteuzi unachukua muda mrefu sana hata zaidi ya miaka kumi na mfano upo, Katibu Tawala Msaidizi upande wa uchumi na uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro Ofisi ya Mkuu wa Mkoa anakaimu mwaka wa tisa toka 2012. Je, Serikali ipo tayari kutengeneza kanzidata au database ya wale watumishi waliofanyiwa vetting wengi kwa ujumla wao ili waweze kusaidia kupunguza muda ule wa watumishi kukaimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza tumekuta kuna changamoto kubwa sana ya waajiri kukaimisha watu wasiokuwa na sifa bila ya kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi kama mwongozo unavyotaka, matokeo yake mtu anakaa kwenye nafasi muda mrefu anakuwa hafanyiwi upekuzi na hivyo kufanya mtu kukaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka mingi. Sasa tayari tulishawaagiza waajiri wote mapema mwaka huu kuleta majina yote ya watu wanaokamimu nafasi zao kwa zaidi ya miaka mitatu ili tuweze kupitia na kuangalia ni wapi wenye sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tayari tumegundua kuna watumishi 1,164 wasiokuwa na sifa na tunazidi kuwaomba waajiri waweze kuhakikisha wanakaimisha watu wenye sifa lakini vilevile kwa kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Waache kukaimisha kwa sababu anamtaka fulani au fulani mimi naweza nikafanya nae kazi na kumburuza, bali wakaimishe mtu kwa sababu ndie anayetakiwa kuwepo kwenye nafasi hiyo na hiyo itasaidia sana katika upekuzi na kuweza kuwathibitisha watumishi ndani ya miezi sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la nyongeza Mheshimiwa ameuliza kama tuna kanzidata, sasa tayari tumeshaanza kukusanya taarifa na tumeshapeleka majina zaidi ya 2,300 kwa ajili ya upekuzi ili yawepo na wiki hii tunapeleka tena majina 2,400 kwa ajili ya upekuzi ili tuweze kuwa tuna watu katika kanzidata yetu wenye sifa. Tunapoona mwajiri amekuweka mtu asiye na sifa, Utumishi tutam-post moja kwa moja mwenye sifa ili akashike nafasi hiyo na aweze kuifanya kwa weledi na kuweza kufanya maamuzi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wabunge na watumishi wote wale wenye sifa muda si mrefu mtaanza kuwaona na tatizo hili la kukaimu litaondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa majibu mazuri yametolewa na Serikali, kwa umuhimu barabara hizi pamoja na kuondoa msongamano sehemu ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia zinasaidia kufungua uchumi wa wananchi wa pembezoni. Aidha, barabara hizi zilipata baraka za Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuzitamani zijengwe kwa haraka na udharura. (Makofi)
Je, Serikali sasa haioni inayo kila sababu kukamilisha barabara hizi katika mwaka wa fedha 2022/2023? (Makofi)
(b) Kwa kuwa kilomita zilizotajwa 33.7 ina sehemu ya kilometa 1 ya barabara ya njiapanda ya shule na wanahitaji fidia. Je, Serikali imejipanga vipi kulipa fidia wananchi hawa? (Makofi)
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais aliahidi kwamba, barabara za Jimbo la Kibamba angetamani zijengwe zote kwa kiwango cha lami. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wa Kitaifa, zote tunazichukulia kwa umuhimu mkubwa sana na ndio maana hata akienda kwenye kitabu chetu cha bajeti, tumetenga tayari fedha, kwa ajili ya kuanza upembuzi kwa sababu, barabara zote zilizotajwa katika Jimbo lake ni za vumbi. Kwa hiyo, lazima hatuwezi tukaruka hatua ni lazima tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na uhakika kwamba tunatambua pia tutafungua uchumi wa Jimbo lakini pia kurahisisha mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kawaida barabara zote zinapojengwa tutahakikisha kwamba hiyo fidia aliyoitaja, tunailipa kabla ya ujenzi na kama kuna changamoto zaidi ya hii ambayo tunafahamu ya kuilipa kwa kawaida, basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana naye kwa ajili ya kupata maelezo zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam lina idadi kubwa ya watu zaidi ya milioni sita na tunategemea Chuo cha VETA kimoja tu maarufu cha Chang’ombe na Wilaya ya Ubungo sasa ipo pembezoni na idadi kubwa ya watu na eneo tunalo: -
Je, ni lini sasa Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Ubungo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kutoa jibu dogo kwa Mheshimiwa Mtemvu Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye maeneo mengine, nitoe rai na wito kwa Mheshimiwa Mtemvu, kwa sababu Ubungo ni Jiji na ni eneo kubwa na mapato yake ni makubwa, kwa hiyo, aone umuhimu nalo wa jambo hili. Basi angalau kwenye mapato ya ndani pale kama wanaweza wakatoa kasma kidogo wakaanza mchakato huu wa ujenzi, pindi pale Serikali itakapopata fedha kwa ajili ya vyuo hivi vya wilaya, basi tutakwenda kuongezea nguvu na kukamilisha chuo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri naona Wabunge wengi wanauliza vyuo vya VETA huko kwenye maeneo yao, hebu tuambia kwa ujumla mpango wa Serikali kuhusu ujenzi wa vyuo vya VETA. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mpango uliokuwepo hivi sasa kwa mwaka huu wa fedha, bado tunaendelea na ukamilishaji wa vyuo vile 29 na vile vile kununua vifaa. Kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha vyuo hivi siyo tunajenga tu majengo, bali vile vile kuhakikisha kwamba tunapeleka pamoja na vifaa ili viweze kufanya kazi na kutoa elimu kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mwaka ujao wa fedha, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kwamba sasa tunaweza kutenga bajeti kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa vyuo vingine vya wilaya. Huo ndiyo mpango uliopo mpaka hivi sasa. Ahsante sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, wananchi wengi wa maeneo ya pembezoni katika Jimbo la Kibamba, hasa maeneo ya Mpijimagohe kule Mbezi, Tegeta A kule Goba na maeneo ya Ukombozi kule Saranga, wameanza kujenga maboma ya vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wa maeneo yao. Je, Serikali ni lini sasa itakuwa tayari kukamilisha maboma yale ili wananchi wale wapate usalama katika maeneo wanayoishi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu tena swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mambo yote ambayo yanaelezwa au vitu vyote ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kufanyiwa wananchi kutoka katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, hasa kwenye Jeshi la Polisi, ni mambo ambayo yanahitaji fedha. Tukizungumza vituo vya polisi, fedha, tukizungumza magari, fedha, tukizungumza nyumba za askari, tunahitaji fedha. Nimwambie tu mheshimkiwa Mbunge kwamba, kwa sasa tunakwenda kutafuta fedha na tumeshaanza hiyo michakato ya utafutaji wa hizo pesa. Lengo na madhumuni ya kufanya hivyo ni ili tuweze kumaliza maboma yote nchini ambayo yanahitaji kumalizwa kuwawezesha wananchi kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika majibu yaliyotolewa ya swali la msingi imeonekana changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti kwa mwaka hadi mwaka, pamoja na ongezeko la bajeti tuliyoelezwa, lakini ni ukweli kwamba, wanafunzi wenye sifa wanakuwa wengi na wale wanaokosa nafasi katika mwaka husika wengine wamekuwa wana kiu ya kuendelea na wananchi wamekuwa wakiwasaidia au jamii wanayoishi, sasa wakienda mwaka wa pili na watatu wanaendelea kukosa. Je, Serikali haioni inayo kila sababu sasa katika miaka inayofuatia wale wanafunzi waliosaidiwa katika njia mbalimbali wawaingize katika mwaka wa pili kabla hawajaendelea kuwachukua wengine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, utaratibu huo upo. Sio kwamba, ukikosa mkopo katika mwaka wa kwanza basi unakuwa hu-qualify kwenye mwaka wa pili, provided ulikuwa umeomba katika ule mwaka wa kwanza. Unachofanya katika ule mwaka wa pili, unakuwa wewe sio mwombaji mpya, unakuwa uko katika dirisha la rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu huo upo Mheshimiwa Mbunge na tumekuwa tukiufanya na wanafunzi hao wamekuwa wakiwa-absorbed wakati wako mwaka wa pili ikiwa mwaka wa kwanza amekosa au mwaka wa tatu, hali ya mwaka wa kwanza na wa pili akiwa amekosa. Kwa hiyo, nikutoe wasiwasi na jambo hili tutaendelea nalo na ndivyo lilivyo.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara hii tayari inaona ina changamoto sana ya kupata fedha kwa ajili ya kundi hili la wazee, lakini bado wazee hawa wana changamoto sana ya uwezo.
Je, Wizara ya ina mkakati gani sasa wa kutumia ile sera ya asilimia 10 kuweza kuwaweka na wazee kupata kama asilimia mbili ili ziwasaidie?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Issa tunakuomba kwamba sheria bado zinafanya kazi na zitakapokamilika basi wazee hawa watapewa haki zao na watapewa msaada wa kuongezewa kiasi cha fedha kwa ajili ya mahitaji ya maisha yao. (Makofi)
MHE ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ukweli mwenye dhamana ya kutafsiri sheria ni Mahakama na kumekuwepo na kesi ya ardhi chini ya Jaji Bongoyo ya mwaka 2005 ikahukumiwa mwaka 2013. Kesi ya Prochesta Lyimo na wenzake 72 dhidi ya AG na Wizara ya Ujenzi. Katika dhamana hiyo wadai walihalalishwa kwamba eneo ni la kwao na kama Serikali inalihitaji inatakiwa illipe fidia. Swali langu la kwanza, je, ni lini Serikali itatekeleza hukumu hii ya Mahakama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, Sheria ya Barabara ya mwaka 1932, Kanuni ya Mwaka 1955 na marekebisho Na. 13 mwaka 2009 inakinzana sana na Sheria nyingine za Mipangomiji na Sheria ya Vijiji ya mwaka 1999 ambayo ilifuta mikataba mingine na sheria nyingine zote zilizotangulia kwa kuweza kuwamilikisha watu ardhi ikiwa ilienda sambamba na zoezi la Operesheni Vijiji ya Mwaka 1974 na 1975 iliyoleta watu pembezoni mwa barabara kubwa na kuwapa miundombinu ya maji na elimu na kadhalika. Je, ni ipi kauli ya Serikali katika mchangamano huu au mchanganyiko wa sheria hizi ya barabara ya mwaka 1932 na hizi nyingine za ardhi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kiamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, kwanza nimshukuru na kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akilifuatilia suala hili kila wakati ili kuhakikisha tu wananchi wake hawa wanapata hicho ambacho anawapigania. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria iliyopo. Moja ya wajibu wa Serikali ni kulinda wananchi pamoja na mali zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi aliyoisema ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ipo kwa Wakili Mkuu wa Serikali ambae yupo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hatua waliyochukua wananchi hawa kupeleka suala hili kwenye vyombo vya kisheria, naomba nimhakikishie kwamba sheria itakapotamka mara ya mwisho nadhani haki itatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu sheria kukinzana naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tunatumia Sheria yetu ya Barabara, lakini suala la kukinzana kwa sheria nadhani Serikali imelichukua na itaenda kuangalia sheria mbalimbali zinavyokinzana ili ziweze kusomeka na kueleweka kwa pamoja. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, majibu yanatuonesha kwamba yapo malalamiko mengi sana ya fedha hizi takribani shilingi bilioni 60 ambazo zinarudi kila mwaka zinapatikana kutokea kwenye fungu hili la 10% na mifano imeoneshwa; Dar es Salaam kwenye Wilaya mojawapo tayari kuna ubadhirifu mkubwa sana wa fedha hizi: -
Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kupeleka ukaguzi maalum kwa nchi nzima ili tupate tathmini ya kweli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya maeneo nchini kote kuhusiana na matumizi ya fedha za 10% na Serikali kama ambavyo Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Bashungwa ametoa maelezo mwanzoni, ni kwamba tunafanya tathmini ya kuona wapi kuna mafanikio, maeneo gani yana changamoto, na changamoto ni zipi; ili sasa baada ya tathmini hiyo, tuwe na direction ambayo itatuwezesha kuwa na fedha ambazo zinaleta tija kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na sababu ya kutazama uwezekano wa kufanya ukaguzi maalum tutalifanya kwa sababu kazi ya Serikali ni kudhibiti fedha hizo ili ziweze kuleta tija kwa watarajiwa. Kwa hiyo, tumelichukua wazo hilo na tutaendelea kulifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Imekuwepo Barabara ya Makondeko – Kwembe – Kisokwa ambayo imekuwa ndani ya bajeti katika kipindi cha miaka miwili mfululizo, 2021/2022 na 2022/2023. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu na atakubaliana nami kwamba tumefika kwenye jimbo lake. Barabara hii ni kati ya zile barabara ambazo zinapunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam na ipo katika mpango wa kuanza kuijenga kwa awamu hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ni ukweli pamekuwa na migogoro mingi sana kwenye Jimbo la Kibamba kuhusiana na kutokamilika kwa urasimishaji, sasa je, Serikali ina mkakati gani kumaliza kabisa migogoro hii inayohusiana na urasilimishaji kwenye Jimbo la Kimbamba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mtemvu kwamba kama ambavyo nimeeleza katika swali la msingi kutoka kwa Mbunge Kunambi, hatua hizo ambazo zimechukuliwa kule Mlimba ndiyo ambazo pia zinaendelea kuchukuliwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kama nilivyoeleza; kuendelea kutoa elimu na kuendelea kuhakikisha Halmashauri zetu zinaendelea kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwemo mipango iliyowekwa na kushirikisha wananchi katika kuweka taratibu za ardhi katika maeneo yao.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa, ripoti ya sensa ya sasa ya mwaka 2022 imeonesha wazi kwamba ongezeko la watu ni zaidi ya Milioni 16 katika kipindi cha miaka Kumi, hii imeshabihiana sana na wananchi wengi wasio na ardhi kuvamia mapori yasiyo endelezwa kwa miaka mingi.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kufanya tathmini upya ili yale maeneo ambayo hayajaendelezwa na wananchi wako mle wamejenga waweze kurasimishwa rasmi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwangu mimi na upande wa Serikali ninaamini ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mtemvu Mbunge ni jambo nzuri na ni jambo la kufanyiakazi nasi ndani ya Wizara nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tumekwishapokea taarifa ile ya sensa na ndani yake yako mambo mengi sana ikiwemo kuangalia jinsi gani Serikali sasa inaenda kuondokana na maeneo ambayo hayajapangwa vizuri lakini pia kurasimisha maeneo ambayo yameiva kwa ajili ya urasimishaji.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya jumla ya Serikali kwenye changamoto hii kwamba imeandaa mwongozo wa usafishaji mchanga, kutoa tope na taka ngumu. Hili ni jukumu ambalo halmashauri yetu ya Manispaa ya Ubungo imeshafanya sana, lakini madhara ni makubwa sana kwenye mto ule, unazidi kupanuka na kuvunja shule na taasisi za Serikali pamoja na makazi ya watu.
Mheshimiwa Spika, inawezekana changamoto hii inahitaji Wizara ya kisekta ingejibu. Naomba niruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; je, Serikali itakuwa tayari kujenga kingo imara kwenye Mto wote huo wa Mbezi ili madhara haya yaweze kuondoka?
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri husika atakuwa tayari kwenda nami jimboni ili tuutembelee mto na aone madhara ambayo yametokea kwa wananchi na yatakayotokea kwenye siku zijazo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, moja ya miongoni mwa jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ni kuhakikisha kwamba tunazingatia na tunashughulikia masuala ya vyanzo vya maji ili visiathiriwe na visiathiri wananchi. Niko tayari kufuatana na yeye kwenda kutembea katika Mto Mbezi kuona changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake lingine, Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunajenga huo mradi wa ukuta ambao utatenganisha ili sasa maji yasiweze kuingia huko yakaleta mafuriko. Ila namwomba Mheshimiwa Mbunge yeye kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kwanza wafanye tathmini ya ujenzi huo, lakini kingine waandike halafu watuletee Ofisi ya Makamu wa Rais ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata fedha kwa ajili ya kuandaa mradi huo. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimesikia majibu ya Serikali ni mazuri na yanaleta moyo katika kupunguza changamoto ya upungufu wa Wahadhiri na hasa Wahadhiri Wabobezi katika Vyuo Vikuu vyetu. Pamekuwa na tafiti chini ya Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (THTU) kwamba kuna upungufu mkubwa sana; utafiti wa 2017, lakini sababu kubwa waliyotoa ni Serikali kutumia sana wataalamu wao katika kujaza nafasi mbalimbali Serikalini: -
Je, Serikali haioni sasa ni wakati mzuri wa kushauri mamlaka za uteuzi kuacha kutumia wataalam hawa, hasa Wahadhiri Wabobezi katika nafasi mbalimbali Serikalini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mbunge ametoa wazo na Mamlaka za Uteuzi zipo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuichukue hoja yake hii ili tuweze kuifikisha kwenye vyombo hivi vya uteuzi ili waweze kufanya evaluation au tathmini toshelezi kabisa iwapo kama wanaona inafaa kufanya hivyo, basi liweze kufanyiwa kazi. Nakushukuru sana.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Pamoja na nia njema ya Serikali kupeleka miradi ya barabara za lami kwenye Jimbo la Kibamba hata hivyo pamekuwa na sintofahamu ya miradi hiyo kutobeba components za fidia zaidi ya migogoro na wananchi. Je, Serikali inasema nini juu ya jambo hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE: Mheshimiwa Spika, naomba nimwombe Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, aweze kuwasilisha swali kama swali kwa maana ya masuala ya fidia. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, niulize swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba maeneo ya King’azi A, B na maeneo ya Manzese Malamba Mawili ni maeneo ambayo wananchi wanaendelea kukosa maji safi na salama kwa kutumia maji ya chumvi ya visima vifupi; na ahadi ya Serikali ni kujenga tenki kubwa la ujazo siyo chini ya lita milioni kumi pale Kilimahewa: Je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tenki lipo kwenye hatua za mwisho kabisa kuja kuanza kutekelezwa, usanifu umekamilika. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa shughuli zote zilizotajwa ambazo zimeanza kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Mabwepande, tayari wananchi wengi hawajui na hata wananchi wa Jimbo la Kibamba pia hawajui;
(a) Je, Serikali ipo tayari kufungua geti upande wa Jimbo la Kibamba ili wananchi wengi sana waweze kushiriki kwenye shughuli zilizotajwa kwenye jibu la msingi?
(b) Kwa kuwa katika kila uwekezaji tunategemea mapato na seerikali imejibu hapa imeshatumia shilingi 710,789,122. Je, ni yapi makadirio ya mapato katika mwaka 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, pori hili la Mabwepande ni pori ambalo limepekena na Mikoa jirani ikiwemo Pwani na pori hili lipo katikati ya Dar es salaam, kwa sasa tumeshaanza kufanya hamasa mbalimbali na kwa kuwa mwanzoni tulikuwa hatuna miundombinu tumeweza sasa kuwekeza na sasa hivi tuna miundombinu ya kutosha na hivyo watalii wameshaanza kuingia na matamasha mbalimbali yameshaanza kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaanza pia kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wananchi, pia tunatumia televisioni matamasha mbalimbali kama ambavyo nimeyataja ikiwemo nyama choma festival hii yote ni kuwafanya wana Dar es salaam wawe na maeneo maalum ya kupumzika ikiwemo kulala ambapo tumeshaandaa maeneo ya camp site kwa ajili ya wananchi kulala.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuhamasisha Watanzania wote unapofika Dar es Salaam basi tembelea Pori la Pande utapata huduma zote za kiutalii na utaweza kuwa umepumzika kama vile upo Serengeti National Park.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa mapato tangu tulipowekeza katika pori hili kwa sasa tumesha kusanya jumla ya shilingi milioni 4.9 na kwa kuwa uwekezaji ni endelevu tunaendelea kuwekeza ili kuhakikisha kwamba eneo hili linakuwa ni kivutio kikubwa katika mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri na ya kuridhisha ya Serikali ningeomba kuuliza haya maswali mawili. Moja, stendi yetu ya Magufuli inaruhusu kuingiza mabasi yote yanayotoka mikoani bila kwenda kokote na kushusha pale abiria, lakini pamekuwepo bado na mabasi mengi kwenda Urafiki na maeneo ya pale kwa Wachina na Maghorofani. Pamoja na maelekezo mengi yanayotolewa na viongozi wa mkoa na wilaya. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kushindwa kwa muda mrefu kusimamia maelekezo yake?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni ukweli stendi ile pamoja inaenda kukamilika kwa wachache walioingia kupitia mnada wanalipa square mita au mita za mraba Sh.40,000 tofauti na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam ikiwepo hata maeneo ya pale Mlimani City, kati ya shilingi 15,000 hadi shilingi 25,000, lakini hawa wanalipa shilingi 40,000.
Je, Serikali haioni sasa ni sababu ya kupunguza kufikia hiyo kati ya shilingi 15,000 hadi shilingi 25,000 ili matumizi yaende kama yalivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mtemvu kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Kibamba na nimwakikishie Serikali itaendelea kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi wa Kibamba. Kuhusu mabasi ambayo hayaingii kwenye stendi ya Magufuli, ni kweli kumekuwa na baadhi ya makampuni ambayo hayatumii ipasavyo stendi kadri ya maelekezo na malengo ya ujenzi wa stendi ile. Kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunalichukua hili tunalifanyia kazi na tutatoa maelekezo mahususi kuhusiana na utaratibu wa mabasi kutumia stendi ile ya Magufuli.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na gharama ya upangishaji kwa square mita kufika hadi Sh.40,000 mapendekezo yake ni Sh.15,000 hadi Sh.25,000 naomba niseme tunalichukua hilo kama Serikali tutalitazama na tuweze kuona mazingira kama yanaruhusu basi tuweze ku- review bei hizo ili wananchi wapate unafuu katika upangishaji.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mbezi na Mto Mpiji ambao kwa muda mrefu wananchi wamedhurika sana na mafuriko, nyumba zao lakini pia na taasisi kama shule zimekuwa zikiondoka.
Je, Serikali ina mkakati gani sasa kukabiliana na hali hiyo katika mito hiyo miwili Mto Mbezi na Mto Mpiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunayo mikakati mingi kwa sababu tunafahamu athari za kimazingira zinazosababishwa na mito hii ni athari kubwa. Mwisho wa siku zinaharibu vipando, zinaharibu makazi lakini pia zinaweza kuleta hata maradhi kwa sababu maji yakija yanakuja na takataka, yakirudi yanarudi maji peke yake takataka zinabakia kwa hiyo tunajua hata maradhi yanatokea. Kwa hiyo iko mikakati mingi kama Serikali ambayo tumeamua kuifanya, ikiwemo kwanza kuhakikisha kwamba tunajenga hizo kingo lakini pia tunasaidia katika kuwaelimisha wananchi namna ambavyo wanaweza wakapunguza hizo athari na wakaepukana na hizo athari zinazosababishwa na mito hii. Nakushukuru. (Makofi)