Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Condester Michael Sichalwe (11 total)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kunipa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ubovu mkubwa wa miundombinu ndani ya Jimbo la Momba. Je, ni lini Serikali itatusaidia kutujengea kilometa 15 za kiwango cha lami kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba katika Kata ya Chitete ikiwa ni sambamba na ahadi ya mama yangu mpendwa Mheshimiwa Makamu wa Rais alipotembelea Jimbo la Momba tarehe 13 Oktoba, 2020 alituahidi angeweza kutusaidia barabara hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naombakujibuswali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-

MheshimiwaNaibu Spika, ni kweli ahadi ya Makamu wa Rais wakati wa kampeni ilitolewa mwaka huu wa kampeni 2020; kwa hiyo, kama Serikali ahadi hii tumeichukua na tunaifanyiakazi. Kwa hiyo, katika awamu inayokuja ya bajeti tunategemea kwamba zitakuwa ni kati ya barabara ambazo zitatengewa fedha na once zikitengewa fedha barabara hiyo itajengwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuongeza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kutokana na wawekezaji hawa wakati mwingine kujichukulia sheria mkononi na kuwafungulia watu kesi na kuwaweka ndani ikiwa hata wao hawafuati Sheria ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwa na hati sahihi, kuendeleza maeneo yale pamoja na kulipa kodi ya ardhi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati usimamizi bora wa matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo inaendelea kushika kasi ndani ya Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester.

Mheshimiwa Spika, napenda tu nimhakikishie; kwenye swali lake la kwanza anataka kujua nini tamko la Serikali kwa hawa wawekezaji ambao wanajichukulia sheria mkononi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe rai tu kwa wananchi kuhusu namna ya uuzaji wa ardhi kwa wawekezaji. Tuwaombe sana, kwa sababu mara nyingi wawekezaji wanaenda moja kwa moja kwenye maeneo, wanaonana na watu bila kufuata taratibu na wanauziana bila kuzingatia sheria; na hatima yake anapokuwa amepewa hati yake wewe ulimuuzia hekari 100, anakuja na hati yenye hekari zaidi ya 100, ni kutokana na nyaraka ambazo zinatakiwa kuwepo kwa kuzingatia sheria yenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niwaombe, kwanza nitoe rai, kwamba, ili kuondoa hii migogoro uuzwaji wowote wa ardhi lazima uhusishe halmashauri husika ambao ndio wanaotambua mipaka yako na namna ambavyo mnaweza kuuziana ardhi kwa wawekezaji. Na wakati mwingine unaweza ukamuuzia mtu ambaye hata si raia wa Tanzania ilhali hairuhusiwi kwa raia wa kigeni kuweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la kodi ambazo hawalipi, tayari tulishaanza mkakati wa kuwafuatilia. Tunachohitaji tu ni halmashauri husika kuona ni namna gani pia ya kuanza ule mchakato wa kufuata sheria, taratibu zile za kutoa maonyo kuanzia kwenye Kifungu cha 45 mpaka 48 ambavyo vinaelekeza njia nzuri ya kuweza kumnyang’anya mtu hati yake hata kama amepewaa kisheria.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema ni lini Wizara itaingilia kati ili kumaliza migogoro hii ya wakulima na wafugaji. Tatizo hilo linaweza likaisha pale tu ambapo kijiji kitakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi; na matumizi ya ardhi hayapangwi na Wizara, yanapangwa na maeneo husika. Kwa hiyo sisi kama Wizara intervention yetu inakuja pale ambapo tunakuja sasa kuridhia kile ambacho mnakubaliana katika kutenga maeneo. Kwamba wafugaji wanatengewa maeneo yao, wakulima maeneo yao, maeneo ya makazi nayo yanakuwepo. Kwa hiyo tunapokwenda sisi ni kuweka ile mipaka kwa ajili ya kuheshimu taratibu hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama vijiji hivi havijawa na mpango wa matumizi basi tunaielekeza pia Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ikashirikiane na Wilaya ya Momba waweze kuweka matumizi ya ardhi katika maeneo yenye mgogoro. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Miaka 20 iliyopita ndani ya Jimbo la Momba Ivuna, kuna kimondo kidogo kilidondoka (Ivuna Meteorite) na kikachukuliwa na watu wa NASA. Je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia kimondo hiki kwa ajili ya kukirudisha na kuendelea kuongeza idadi ya watalii nchini? (Makofi)
WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza kwanza Mheshimiwa Condester kwa kazi nzuri anayowafanyia wananchi wa Momba na ndiyo maana walikuchagua kwa kura nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeshaanza kufanya mawasiliano na Balozi wetu aliyeko nchini Marekani kuanza kufuatilia jambo hili. Tutakapopata majibu, tutamjulisha Mheshimiwa Condester na Bunge lako Tukufu. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nilikuwa nasema kwa kuwa barabara nyingi za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA zimeonekana kutokuwa na uteshelevu wa bajeti na angalau TANROADS kuonekana wana bajeti ya kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha barabara nyingi ambazo zipo vijijini zinazochelewa kupandishwa hadhi kwenda TANROADS ili angalau ziweze kusaidiwa kwa sababu barabara za vijijini tunapata shida sana na bajeti ya TARURA ni ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Vijijini na Mijini imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi katika mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 bajeti ilikuwa bilioni 275.034 lakini mwaka ujao wa fedha ni shilingi bilioni 400, ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 125. Jitihada hizi zote ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha uwezo wa TARURA kuhudumia barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Spika, na naomba nichukue hoja yako, tutaendelea kufanya tathmini kwenye barabara hizo ambazo zinahitaji kusajiliwa wa TARURA lakini zile ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda TANROADS kuna utaratibu ambao Serikali imeelekeza naomba tuufuate huo ili tuweze kupata barabara zenye hadhi hiyo na kufanyiwa matengenezo kwa wakati, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nilikuwa nasema kwa kuwa barabara nyingi za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA zimeonekana kutokuwa na uteshelevu wa bajeti na angalau TANROADS kuonekana wana bajeti ya kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha barabara nyingi ambazo zipo vijijini zinazochelewa kupandishwa hadhi kwenda TANROADS ili angalau ziweze kusaidiwa kwa sababu barabara za vijijini tunapata shida sana na bajeti ya TARURA ni ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Vijijini na Mijini imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi katika mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 bajeti ilikuwa bilioni 275.034 lakini mwaka ujao wa fedha ni shilingi bilioni 400, ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 125. Jitihada hizi zote ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha uwezo wa TARURA kuhudumia barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Spika, na naomba nichukue hoja yako, tutaendelea kufanya tathmini kwenye barabara hizo ambazo zinahitaji kusajiliwa wa TARURA lakini zile ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda TANROADS kuna utaratibu ambao Serikali imeelekeza naomba tuufuate huo ili tuweze kupata barabara zenye hadhi hiyo na kufanyiwa matengenezo kwa wakati, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Wilaya ya Momba makao yake makuu yako ndani ya Halmashauri ya Momba, je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha polisi ambacho kina hadhi ya wilaya ili kiweze kusaidia kuepusha changamoto na uovu wote ambao unaoendelea ndani ya Jimbo la Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapatiwa huduma za ulinzi na usalama kupitia kila chombo ambacho wananchi watakuwa wanahitaji. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba awe na Subira, tutajitahidi sana tuhakikishe kwamba ndani ya jimbo hilo au ndani ya eneo hilo ambalo limekosa hicho kituo cha polisi basi tuone namna ya kuweza kupata fedha ili tukawatengenezee wananchi kituo cha polisi waweze kupata huduma za ulinzi. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhalisia kwamba halmashauri zetu nyingi nchini zina changamoto sana ya miundombinu. Serikali haioni kuna haja ya kubadilisha usafiri kutoka kwenye pikipiki na kuwapatia magari maafisa maendeleo ya jamii hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na kwa uwanda mkubwa? Kwa mfano, kipindi cha mvua mtu huyo atatumiaje pikipiki maana yake atakuwa analowa, hawezi kutekeleza majukumu yake. Serikali haioni umuhimu wa kuwanunulia magari maafisa maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMIS): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyogeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, maafisa hawa wanatembea kwa pikipiki kwa ajili ya kufuatilia wafanyakazi hawa au vitendo mbalimbali vinavyotokea katika jamii. Serikali kama nilivyoeleza imejipanga kuzungumza na wadau ambao wanaendeleza maendeleo haya ya jamii ili kuhakikisha kwamba maafisa hawa hawatopata tabu katika kazi zao katika mazingira yao ya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo, ahsante nashukuru. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto ambayo inawapata wananchi wa Busega inafanana kabisa na changamoto ambayo inawapata wananchi wa Jimbo la Momba.

Je, ni lini Serikali itaona kuna haja ya kutupa upendeleo ili tuweze kupata Mahakama yenye hadhi ya wilaya ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya mwendo mrefu kufuata huduma za Mahakama kutoka Jimbo la Momba mpaka Mji wa Tunduma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe kutoka Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi katika Mpango Kazi wa kuendeleza ujenzi wa hizi Mahakama zetu za wilaya, 2022/ 2023 tunakwenda kuanza ujenzi wa Mahakama yake ya Momba ili kumpunguzia hiyo adha ambayo wananchi wanaikabili kwa sasa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Jimbo la Momba lina vijiji 72 na vitongoji 302. Katika vijiji hivyo, vijiji ambavyo vinapata majisafi na salama ambayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu haviwezi kuzidi 20; isipokuwa tunatumia mbadala wa maji ambayo yametuama kwenye madimbwi na kwenye mito midogo midogo ambapo tunakunywa pamoja na ng’ombe, punda, mbuzi na wanyama wote: -

Je, ni lini Serikali itaona katika vijiji vilivyobaki, watusaidie kutuchimbia visima vya dharura wakati tunaendelea kusubiri miradi mikubwa ya maji ili tuendelee kupata maji safi na salama kama ambavyo binadamu wengine wanapata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jimbo la Momba bado lina changamoto ya maji na ni moja ya maeneo ambayo yapo kimkakati katika Wizara na tumetupia jicho la kipekee kabisa pale. Visima ni moja ya miradi ambayo tunakuja kuitekeleza ndani ya Jimbo la Momba. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, tutakuja kutekeleza wajibu wetu, kwa sababu wananchi wale pia wapo Tanzania. Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, amesema wanawake wote lazima tuwatue ndoo kichwani. Mantahofu, tunakuja kufanya kazi Momba. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado, changamoto ya maji kwenye Jimbo la Momba ni kubwa sana. Naomba kuiuliza Serikali niongeze maswali mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji ambavyo umevieleza tunavyo vijiji 72 na vitongoji 302 inaonyesha kwamba hata nusu ya vijiji hivyo vitakuwa bado havijapata maji safi na salama. Ombi langu kwa Serikali, viko baadhi ya visima ambavyo vilishawahi kuchimbwa nyuma na wakoloni, vilishawahi kuchimbwa nyuma na wamishionari lakini pia na baadhi ya wakandarasi ambao walikuja kujenga barabara kwenye Jimbo la Momba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, nini kauli ya Serikali kwenda kuvitembelea visima vile ambavyo vimeshawahi kufanya kazi vizuri huko nyuma kutokana bado kuna changamoto ya maji vinaweza vikatusaidia vikawa kama njia nyingine ya mbadala kutatua changamoto ya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa, baadhi ya vijiji ambavyo vimeonyesha vinao miradi hiyo ya maji lakini zipo Taasisi kama Vituo vya Afya, Zahanati pamoja na Sekondari havipati utoshelevu wa maji. Watoto wetu especially wa kike wameendelea kuteseka sana kufuata maji wakati mwingine zaidi ya kilomita 10. Mfano, Shule ya Sekondari Chikanamlilo, Shule ya Sekondari Momba, Shule ya Sekondari Uwanda, Shule ya Sekondari Ivuna, Shule ya Sekondari Nzoka na shule zingine 13 ambazo ziko ndani ya Jimbo la Momba pamoja na Zahanati na Vituo vya Afya kama Kamsamba na Kapele. Je, ni nini kauli ya Serikali kutuchimbia visima virefu ili Taasisi hizi ziweze kujipatia maji yake bila kutegemea kwenye vile vituo ambavyo tunang’ang’ania na wananchi na havitoshelezi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kutembelea visima ambavyo ni chakavu hii ni moja ya jukumu letu na tayari, Mheshimiwa Waziri amewaagiza watendaji wote kwenye mikoa yote, kwa maana ya Regional Managers (RMs) na Managing Directors (MDs) wasimamie visima vyote ambavyo ni chakavu. Vile ambavyo uwezekano wa kuvirejesha katika hali njema ya kutoa maji safi na salama vyote viweze kurejeshwa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Jimbo la Momba sisi kama Wizara tumeshaleta Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuchimba visima virefu. Hivyo, visima hivi ambavyo vya kukarabati lakini uchimbaji wa visima virefu kwenye swali lako la pili la nyongeza, navyo tayari vimeshaanza kufanyiwa kazi katika baadhi ya maeneo. Tayari visima vitano vimeshachimbwa kati ya visima 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, napenda tu kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba sisi kama Wizara tutakwenda kuhakikisha katika sehemu zote ambako Taasisi za Serikali zipo kama zile Shule alizozitaja pamoja na Vituo vya Afya na Hospitali maji ni lazima yafike na huo ndio Motto wa Wizara. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kutokana na ongezeko kubwa la wananchi ndani ya Jimbo la Momba kwa baadhi ya vitongoji na vijiji: -

Je, ni lini Serikali kwa kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili watakaa kwa pamoja ili kugawa baadhi ya maeneo ambayo ni ya hifadhi ili kuwapatia wananchi wa vitongoji vya Mbao, Ntungwa, Twentela pamoja na Kaonga ili wapate sehemu ya kulima kwa sababu wamekuwa kama wakimbizi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama mnavyojua kwamba nchi yetu inaongozwa na utaratibu wa sheria, ugawaji wa maeneo yote ni jambo linalofuata kisheria. Nami nimwagize tu au nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huu uanze kwao ili watuletee tuweze kupeleka kwa mtu aliyekabidhiwa mamlaka kugawa vipande vya ardhi katika nchi hii, yaani Mheshimiwa Rais, ili sasa utaratibu mwingine uweze kufanyika. Nashukuru. (Makofi)