Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Tumaini Bryceson Magessa (1 total)

MHE. BRYCESON T. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, je, ni lini atakuwa tayari yeye na STAMICO twende kupitia katika maeneo ambayo mimi najua bado kuna tatizo ili tuweze kumaliza matatizo yaliyopo kule?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa STAMICO kazi yake, pamoja na majukumu mengine, ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo waliopo Busanda wengi wanabahatisha kujua dhahabu iko wapi. Je, ni lini STAMICO itakuwa tayari ama kuwakodisha vyombo au kujitolea ili waweze kutambua mahali wanapochimba kuna madini au hakuna badala ya kubahatisha?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge Tumaini Magessa kutoka Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, baada ya kikao hiki nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ipo tayari kutembelea Jimboni kwake na kuona maeneo wanayodhani kama yanahitaji kugawiwa kwa wachimbaji wadogo au la.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba Serikali imeendelea kuyatoa haya maeneo kila inapoona kuwa inafaa. Nadhani hata yeye mwenyewe katika jimbo lake ni shahidi kwamba maeneo mengi yameendelea kutengwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imewathamini sana wachimbaji wadogo na ndipo wakati ambapo wachimbaji wadogo nchini wamepewa maeneo mengi sana kwa ajili ya kuchimba.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi Serikali inaendelea kuimarisha Shirika letu la STAMICO na siku za karibuni shirika limeweza kununua mitambo ya drilling ya kwake yenyewe. Kwa jinsi hiyo, tunaamini kwamba jitihada hizi zinazochukuliwa na Serikali za kuimarisha Shirika la STAMICO zitawezesha sasa kuweza kupata namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kufanyia utafiti ili sasa tunapoelekea maeneo yanayotengwa yawe ni yale ambayo yamefanyiwa tafiti na hatimaye kuwawezesha kuchimba kwa tija. Ahsante sana.