Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Justin Lazaro Nyamoga (25 total)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa ni zaidi ya miaka 30 sasa tangu wakulima wa chai wa Kilolo wapande chai yao na kujengewa kiwanda ambacho hakijawahi kufanya kazi; na kwa kuwa katika muda huo wako Mawaziri kadhaa na Manaibu wameenda kule wakapiga picha kwenye mandhari nzuri za mashamba yale na kuahidi wananchi wale kwamba shughuli hiyo itakamilika mapema iwezekanavyo na hawakurejea tena. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi wa Kilolo kwamba sasa kiwanda kile kilichojengwa na hakikuwahi kufanya kazi, kitafanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa michakato mingi imepita ya kumpata mwekezaji na mchakato wa mwisho ulikuwa mwaka 2019 na wawekezaji walijitokeza na wakapatikana na wako tayari, na kwa kuwa uwekezaji huu haukukamilika kutokana na urasimu wa Serikali. Je, Serikali iko tayari kuwawezesha wale wawekezaji kwenda kuwekeza badala ya kuanza mchakato mwingine ambao unaweza ukachukua miaka mingine 30?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali imefanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kiwanda hicho kinafanya kazi. Kwa taarifa tu ni kwamba katika miaka ya nyuma tayari kuna wawekezaji walikuwa wamejitokeza kwa ajili ya kuwekeza katika kiwanda hicho na mmojawapo ni Mufindi Tea and Coffee Company chini ya DL Group. Hata hivyo, baada ya kupitia mchakato wa upatikanaji wa mwekezaji huyo ilionekana kwamba kuna baadhi ya vipengele vilirukwa lakini pia baada ya kuwa na due diligence ya kutosha ilionekana kwamba mwekezaji huyo alikuwa hana uwezo wa kuwekeza katika kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, juhudi hizo bado zinaendelea na kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba sasa tunaandaa andiko maalum ambalo litaangalia namna bora ya uendeshaji wa kiwanda/shamba lile likihusisha ushirikishwaji wa wadau wote kwa maana ya wakulima wadogo, halmashauri ya Kilolo lakini pia na Msajili wa Hazina ambaye ndiye anasimamia kiwanda hicho. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo inafanana kabisa na Wilaya ya Mufindi; na kwa kuwa vyanzo vya mito kama Mto Mtitu na Mto Lukosi vinachangia kwa kiwango kikubwa kwenye vyanzo vikubwa vya mabwawa na pia ni vyanzo ambavyo vinasaidia katika nchi yetu. Je, ni lini Wizara itajibu kiu ya wananchi kwa kutatua tatizo la maji kwa kutoa fedha kwenye Mradi wa Mto Mtitu ambapo tayari RUWASA walishatoa na maji hayo yatafika hadi Iringa Mjini lakini pia yatahudumia kata zaidi ya 15 za Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge alivyokiri kwamba tayari shughuli zinaendelea pale kupitia Wakala wetu wa Maji Vijijini (RUWASA). Kadiri tunavyopata fedha tunahakikisha tunagawa katika maeneo yote ambayo miradi ipo kwenye utekelezaji.

Kwa hiyo, pamoja na mradi huu ambao upo katika Jimbo lake na ni Jimbo ambalo tumelitendea haki kwa sehemu kubwa sana, tutaendelea kupeleka fedha kadiri tunavyopata ili kuhakikisha mito yote ambayo mmebarikiwa watu wa Kilolo na maeneo mengine yote tunashughulikia kwa wakati. Lengo la Wizara ni kuhakikisha wananchi wanapata maji bombani na si vinginevyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri ambayo yanatoa matumaini kwenye maeneo yale ambayo kumewekwa ahadi za kuweka minara. Hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Kata ya Masisiwe na Kata ya Udekwa hakuna mawasiliano kabisa na tayari watu wawili wameanguka kutoka kwenye miti wakijaribu kutafuta mtandao na kuumia na kulazwa katika Hospitali ya Ilula mmoja na ya Kilolo mmoja.

Sasa, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi katika kata hizi, kwanza ili kutoa pole kwa watu hao, lakini pili ili kuweza kuona yeye mwenyewe na nafahamu yeye ni mtu ambaye ametembelea maeneo mengi ili aweze kujionea hali halisi na kuweka msisitizo wa kuweka minara katika maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo yenye mitandao, yenye wananchi wenye matumiani makubwa sana yakutumia vifurushi vya bei ndogo, yalikatishwa tamaa na ongezeko la bei ya vifurushi ambapo ilitarajiwa vishuke. Tunaishukuru Serikali kwamba imerudisha katika ile hali ya kawaida, lakini matumaini ya wananchi ilikuwa ni kushushwa. Sasa je, ni lini Serikali itarudia ule mpango wake wa awali wa kushusha vifurushi, ili Watanzania wakiwemo wananchi wa Kilolo ambao wanataka sana kutumia vifurushi hivi katika shughuli zao za kibiashara, waweze kufurahia bei nafuu ya vifurushi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba maswali yangu hayo mawili madogo yajibiwe.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, nimesema kwamba Serikali tayari imeshaanza kufanya tathmini katika Kata ya Irole pamoja na Masisiwe ili tuweze kuingiza katika mpango wa awamu ya tano na ya sita katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la pili, nafahamu kabisa hili ni swali ambalo Waheshimiwa Wabunge wote wangeweza kuliuliza. Naweza kusema kwamba kazi ya Serikali ya kwanza ni kuhakikisha kwamba ina-stabilize bei iliyopo na hilo ndilo ambalo tumelifanya kwa sasa. Naona kwamba kulikuwa na changamoto ambapo makampuni yaliweza kuwa na bei tofauti tofauti ambazo ziliwaumiza sana wananchi, lakini Serikali ikatoa maelekezo ya kuhakikisha kwamba bei ya hapo awali inarejea kama ambavyo Watanzania walikuwa wanakusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu kwamba, katika kurejesha hizi gharama za vifurushi, kuna changamoto yake. Kupandisha kifurushi ni mchakato ambao unahusisha ujenzi wa mifumo ambayo itaweza ku-support hicho kifurushi kipya ambacho utakiingiza sokoni. Vile vile unaposema kwamba urudishe maana yake kwamba unaaanza kufanya reverse engineering maana yake unaanza kurudisha kwenye mfumo ule ulioko zamani, kama ulikuwa umeshautoa maana yake sasa inabidi uanze kuusuka tena ili uanze kutoa bei ambazo zilikuwa zinatolewa hapo kabla.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge pia ameongelea namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba bei hizi, zinashuka zaidi ya sasa ambavyo Watanzania wangetarajia. Changamoto ya biashara ya mawasiliano, kitu ambacho tunakiangalia Serikali ni kwamba hapa tunatakiwa kuangalia tuna-balance namna gani kati ya consumer, watumiaji wa huduma, Serikali pamoja na mtoa huduma. Ni lazima tuangalie ile production cost yake, ni lazima aweze kufanya biashara katika kiwango ambacho anaweza akapata faida ili Serikali pia iendelee kupata kodi lakini kodi hizohizo ziweze kurudi kujenga barabara na zahanati na hatimaye Wabunge katika Majimbo yao wanayotoka tuweze kushuhudia kuna mabadiliko ya barabara na zahanati ambazo zitakuwa zinajengwa. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Wilaya ya Kilolo haina majengo ya Mahakama na hivi sasa majengo yanayotumika ni ya Mahakama ya Mwanzo. Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Kilolo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Tarafa ya Mazombe kuna Mahakama ambayo ilijengwa enzi za mkoloni na haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote. Je, ni lini Serikali itakarabati majengo hayo ili yaweze kuendana na hadhi ya sasa na haki iweze kutolewa katika mazingira mazuri?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Kilolo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi Kwa kipindi cha mwaka 2022/2023. katika kipindi kijacho cha fedha tunajenga ile Mahakama ya Mwanzo ambayo ipo Tarafa ya Mahenge na kwa ile ya Wilaya tutaanza kuiweka kwenye mpango nilioutaja.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu ukarabati wa ile Mahakama ya Mazombe, hii nayo tutaiweka kwenye mpango wa 2022/2023. Hii itaendana na ukarabati wa maeneo mengine yote ambayo tumeendelea kuweka mikakati kwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 baadhi ya miradi yetu ambayo itaendeshwa katika kipindi hicho tumeiainisha tayari na katika ngazi ya wilaya tutakuwa na Mahakama nyingi sana ingawa kwenye mpango huo wilaya yake haipo. Kutokana na muda ningeweza kuziorodhesha wilaya hizi lakini kwa sasa inatosha kusema hivyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kata ya Udekwa, Kata ya Ukwega, Kata ya Kimara na Kata ya Idete hazina mawasiliano kabisa kutokana na mvua ambazo zimeharibu kabisa barabara.

Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura kwa ajili ya barabara ya kata hizi ambazo zina mazao mengi ili ziweze kutengenezwa na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura katika barabara ambazo ameziainisha hapa. Nimwambie tu moja ya kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TARURA katika kipindi hiki ni pamoja na kupeleka fedha za dharura katika maeneo yote ambayo yalikuwa yemeathirika sana na mvua kubwa ambazo zilikuwa zimenyesha. Pamoja na fedha ndogo ambayo tunayo kwa sababu katika fedha za dharura ambayo tunayo kwa mwaka huu ambayo unakwisha ni kama bilioni 12 ambazo tulikwenda kuziainisha katika yale maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameainisha maeneo hayo, niseme tu kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itapitia hayo maeneo na ione kama kuna udharura wa haraka kabisa ili tuweze kupeleka fedha na hizo barabara ziweze kupitika. Ahsante sana.
MHE. LAZARO J. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali inatarajia kupata fedha hizo lini ili wale wananchi waweze kulipwa fidia badala ya kuendelea kusubiri kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na umbali uliopo kati ya Makao Makuu ya Wilaya na Kituo cha Polisi ambacho kinatumika kama Makao Makuu ya Polisi, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha za OC ili ofisi ile ya Polisi ya Wilaya iweze kujiendesha bila karaha wala kuombaomba fedha kwa wadau wengine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameuliza, je, lini Serikali italipa fidia? Nataka nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inao mpango na italipa fidia wananchi hao kwa ajili ya eneo hilo kwa sababu inatambua umuhimu wa uwepo wa Kituo hicho cha Polisi ili wananchi waweze kupata huduma hizo. Kubwa zaidi tayari tumeshatoa maelekezo na wameshafanya tathmini wataalam kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Kilolo inayohitajika kwa ajili ya fidia hiyo na tayari tumeshaelekeza pa kwenda kupata fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hao. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kufanya juhudi kuona namna bora ya kuwalipa fidia wananchi hao. Kubwa Mheshimiwa Mbunge aendelee kuzungumza na wananchi wake ili waendelee kuwa na subra jambo hilo limo mbioni kushughulikiwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anauliza kama Serikali ipo tayari kuongeza OC. Niseme tu kwamba Serikali ipo tayari kuongeza OC lakini ni pale ambapo tutakuwa na fedha ya kutosha kufanya hivyo. Kwa hiyo, kwa sasa waendelee kuwa na subra hivyo hivyo tubananebanane lakini tunao mpango huo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo upo mbadala ambao tumeshauchukua, kwanza tumeongeza operesheni ama doria za mara kwa mara katika maeneo ambayo wananchi wako mbali na vituo vya polisi ili waweze kupata hizo huduma za ulinzi. Vilevile tunaendelea kusisitiza ulinzi shirikishi ambapo inasaidia huduma za ulinzi kufika mpaka maeneo ya vijijini kwenye kata. Lengo na madhumuni ni wananchi waendelee kupata huduma za ulinzi na waishi kwa amani.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, aHsante kwa nafasi hii.

Kwanza nashukuru sana kwamba Waziri wa Kilimo ametembelea shamba la chai pale Kilolo Jumamosi wiki iliyopita na kujionea mwenyewe lile pori ambalo nimekuwa nikilisema hapa. Na kwa kuwa Benki ya Kilimo iko tayari na ina fedha tayari kwa ajili ya kukopesha mwekezaji yeyote, sasa je, ni lini ule mchakato wa kutafuta mwekezaji utaanza tena bada ya kuwa ulisimama katika kipindi hiki cha mwaka karibu mmoja uliopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Waziri wa Kilimo Profesa Mkenda amekuwepo huko wiki iliyopita akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Tanzania Agricultural Development Bank. Baada ya muda mrefu kuhangaika kutafuta mwekezaji, position ambayo tunayo kama Wizara ya Kilimo na ambayo tutaenda kuitekeleza ni kuanzisha special purpose vehicle ambayo shareholding structure itawahusisha wakulima wadogo na Tanzania Agricultural Development Bank kwa sababu wao ndio wanaleta mtaji na wao wataleta menejimenti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba ule mpango wa kuhangaika kutafuta mwekezaji wa nje tumeachana nao, tutatumia our own resources kufufua hilo shamba na tutaweka menejimenti ambayo ita- run, kwa sababu tumefanya majaribio kwenye Vyama vya Ushirika vya KAKU, Mbogwe na Chato tumefanikiwa.

Kwa hiyo, huu ndio utakuwa mwelekeo kwenye maeneo ambayo tutaweka mitaji, tutaanzisha special purpose vehicle, halafu tutaendelea kufanya biashara na ushirika utashindana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana, kwanza nishukuru sana kwamba wakati wa kuchangia Mpango nilielezea kutokurudhishwa kuhusu mkandarasi aliyekuwa anaweka ile lami ya kilometa 10 na amebadiliswa na speed yake sasa yule anaeendelea kwa kweli ni nzuri na inaridhisha.

Sasa maswali yangu, kwa sababu ukiangalia kuna Project ya World Bank ambayo barabara hii kilometa zote 33.6 zilikuwemo na ninafahamu kwamba Waziri wa Fedha alisaini mkataba na hawa watu wa World Bank kwa ajili ya hiyo project. Je, upatikanaji wa fedha hizo utaondoa huo ujenzi wa awamu na kufanya barabara hii iweze kujengwa yote na kukamilika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Waziri atakuwa tayari kuambatana pamoja na mimi kwenda kuangalia hasa maeneo ya milimani kwa barabara hii ambayo hayapitiki ili tuweze kupata ufumbuzi na wananchi waweze kupita vizuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua jitihada za Serikali na kwamba ni sikivu, alichokiomba tumeshakitekeleza kama Wizara. Pia nimpongeze kwa kuwapigania sana watu wa Kilolo kuhusu hii barabara, sasa majibu yangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema kwamba Waziri wa Fedha amesha saini mkataba huu na labda tu nielezee kwamba mkataba huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambao umechukua muda kutokana na ukweli kwamba mradi huu ulikuwa una cover mikoa michache, kwa hiyo Serikali iliona huu mradi utanuliwe, pia ulikuwa unalenga sana barabara za changarawe, kwa hiyo, Serikali ikaona hatuwezi tukachukua fedha World Bank kwa ajili ya changarawe, kwa hiyo, kukawa na majadiliano ili kuuboresha, kwanza uchukue mikoa mingi pia uwe ni kwa kiwango cha lami ambapo ni barabara za kutoka vijijini kuunganisha na barabara za mikoa na barabara kuu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya kusaini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kilometa zote 33 zipo kwenye mpango, na zitajengwa ndio maana tunafanya design upya kuhuisha ile design iliyokuwepo ili iendani na kiwango cha sasa cha barabara.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mimi Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba nipo tayari kuambatana naye kwa ajili ya kwenda kuangalia hizi barabara na kuhakiki jinsi ujenzi unavyoendelea, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa moja kati ya vigezo vilivyopo katika mwongozo ni halmashauri iwe na hati safi kwa miaka mitatu mfululizo; na kwa kuwa kigezo hiki ni kandamizi kwa wananchi kwa sababu wanaosababisha hati kuwa chafu au safi siyo wananchi bali ni watumishi wa halmashauri.

Je, Serikali haioni kwamba hata kama kuna marekebisho yanafanywa kigezo hiki kiondolewe mara moja ili halmashauri zote zipate haki ya kuomba miradi hii ya kimkakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapoandaa miradi hii ya kimkakati moja katika dhamira zake kubwa ni kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa na tija kwa ujumla wake. Ndiyo maana miongoni mwa vigezo, ukiachilia mbali hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumza, ni kuangalia mtiririko mzima wa fedha katika mradi ili kuona kwamba mradi ule utaweza kujiendesha kwa faida na baadaye uweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hati chafu inapokuja inatoa kiashiria hasi juu ya ufanisi wa mradi husika. Hata hivyo kwa kuwa jambo hili ni la kitaalam, naomba nilichukue halafu tukaiwasilishe hoja yake kwa wataalam, tuone jinsi gani inaweza ikafanyika bila kuathiri lengo halisi la kuona tija inapatikana katika mradi ule, lakini wakati huohuo isiathiri dhamira njema ya wananchi kwa makosa ambayo hayawahusu.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ningependa tu kujua ni lini Serikali sasa itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilolo ambayo tayari ina ongezeko la vijana na chuo kinahitajika ili nao waweze kujiendeleza kama ilivyo kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Serikali inaendelea na ukamilishaji wa vyuo vile vya VETA katika wilaya 29 ambazo sasa zinakwenda kukamilisha, lakini siyo tu kukamilisha na kuhakikisha vile vile vifaa kwa ajili ya mafunzo vinaweza kupatikana. Kwa hiyo katika mwaka huu wa fedha, juhudi za Serikali tunajikita kwenye eneo hilo, kukamilisha vyuo hivi vya wilaya 29, lakini na vile vya mikoa vinne. Kwa hiyo, nimhakikishie, baada ya ukamilishaji wa vyuo hivi, Serikali sasa tunajipanga vizuri kutafuta fedha ili kuweza kufikia wilaya zote kama sera yetu inavyosema kwamba kila wilaya ni lazima iwe na Chuo cha Ufundi cha VETA. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nakiri ni kweli nimeona kazi hiyo inaendelea katika kata hizo zilizotajwa. Pamoja na hayo nina maswali yangu mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; katika utekelezaji wa miradi hii maeneo mengi ya huduma za jamii, hasa shule za msingi, shule za sekondari, makanisa na misikiti, hasa maeneo ambayo yako mbali kidogo na katikati ya miji, haziwekewi kipaumbele sana kupata umeme. Je, Serikali haioni kwamba ni vizuri kutenga bajeti maalum kwa ajili ya huduma za jamii, hasa sehemu ambazo watoto wetu wanasoma kwa sababu ni muhimu sana kuwa na umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika miji mbalimbali midogo kwa mfano Mji wa Ilula uliopo Kata ya Nyalumbu, lakini pia Mji Mdogo wa Boma la Ng’ombe pamoja na Mji Mdogo wa Kidabaga, kumekuwa na kero kubwa ya kukatika umeme mara kwa mara. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza kero hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye utekelezaji wa Mradi wa REA III, Mzunguko wa Pili, tuliwaelekeza wakandarasi wanaopeleka umeme katika maeneo yetu pamoja na wale wanaoshirikiana nao, wenzetu wa TANESCO, kuhakikisha kwamba maeneo ya taasisi na miundombinu mingine kama elimu, afya na taasisi za dini yanakuwa ni maeneo ya kipaumbele. Kama alivyosema Mheshimiwa Nyamoga, ni kweli maeneo yale ambayo tayari umeme umeanza kwenda kwenye maeneo ya makao makuu ya vijiji tayari tunapeleka.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Nyamoga pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba kadri tunavyozidi kupeleka umeme kwenye maeneo ya pembeni kwa maana ya vitongoji, tutazidi pia kufika katika taasisi hizo na ni maelekezo ya Serikali kwamba umeme ufike katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kufurahisha zaidi ni kwamba, sisi Wizara ya Nishati pia tumepewa kipande kidogo cha bajeti katika ile 1,300,000,000 za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan zinazopeleka maeneo ya UVIKO tunaopambana nao na sisi katika miundombinu hiyo mipya ambayo inajengwa tumepatiwa pesa kiasi fulani ambapo tutaweza kuongeza kasi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, ni kweli kwamba kumekuwa kuna makatizo ya umeme kwenye maeneo mbalimbali, lakini ni jambo ambalo lililopangwa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya miundombinu. TANESCO katika mwaka huu wa fedha inazo bilioni karibu zaidi ya 200 kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuvumilia kidogo tukiwa katika hatua hizi na harakati za kuhakikisha tunaboresha miundombinu yetu. Na kwa Iringa tuna takribani bilioni moja na milioni 500 kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu. Tutaendelea kuwahimiza wenzetu watoe taarifa sahihi na kwa wakati sahihi ili Waheshimiwa umeme unapokatika, basi wananchi waweze kufahamu nini kinaendelea. Nakushukuru.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika uendelezaji wa sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kuna watumishi ambao wanahitajika sana sasa hivi, kwa mfano clinical officers, wafamasia na hawa hawasomi vyuo vikuu. Kumekuwa na pendekezo la muda mrefu sana la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati ambalo ni hitaji kubwa sana katika nchi yetu kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati pia wanapata mikopo kwa sababu, ndio mahitaji makubwa katika nchi yetu kulingana na miundombinu tunayoijenga kwenye maeneo ya vijijini ambayo yanahitaji sana hiyo kada ya kati kulitumikia Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli analozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba, uhitaji uko mkubwa sana kwenye vyuo vyetu vya kati, lakini kama tunavyofahamu na kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, jambo kubwa hapa ni suala la bajeti. Iwapo kama bajeti yetu inaruhusu tunaweza tukavifikia vyuo vikuu vyote, lakini vilevile pamoja na vyuo vya kati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, bajeti itakaporuhusu tutahakikisha tume-cover kwanza eneo lote la vyuo vikuu halafu tutaangalia namna gani sasa mikopo hii inaweza kwenda kuwafaidisha au kuwanufaisha wenzetu wale ambao wako katika vyuo vya kati. Ahsante sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni zaidi ya miaka 10 sasa tangu Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula imeanzishwa, ningependa kujua ni tathmini gani au ni utaratibu gani unatumika ili kupandisha hadhi kutoka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo kwenda kuwa Halmashauri?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ningependa kujua katika ugawaji wa halmashauri kipo kigezo cha idadi ya watu na katika maeneo yenye hifadhi kubwa ya misitu na maeneo yaliyohifadhiwa na mbuga kama Kilolo kigezo hiki kinakuwa tishio kusababisha kuchelewa kugawa kwa halmashauri pamoja na ukubwa wake. Je Serikali iko tayari kuangalia kigezo hiki na kuangalia zaidi ukubwa ili wananchi waweze kufikiwa na huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa mamlaka mpya zikiwepo halmashauri za miji zinategemea kukidhi vigezo vilivyowekwa ili halmashauri iweze kupewa mamlaka halisi ya kuwa halmashauri kutoka malmaka ya mji mdogo. Ni kweli kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ilula ina zaidi ya miaka 10 lakini taratibu za kuomba kuwa Halmashauri ya Mji ni zilezile ambazo zinatumika kuomba Halmashauri ya Wilaya. Kwa maana vikao vya kisheria katika vijiji na mitaa, kata ngazi ya wilaya pamoja na DCC na RCC. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na kuomba Wilaya igawiwe kuwa wilaya mbili lakini pia wafuate utaratibu huo kwa Halmashauri ya Mji wa Ilula ili tathmini ifanyike kuona kama kama inakidhi vigezo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukubwa wa kijografia wa Wilaya ambayo ina misitu mingi lakini wananchi wachache. Kigezo cha wananchi ni kigezo muhimu sana kwa sababu tunapeleka mamlaka mpya kuhudumia wananchi kwa hiyo idadi ya wananchi ndio sababu ya msingi zaidi ya kutenga halmashauri mpya badala ya eneo la misitu, lakini pia kwa maana ya ukubwa ambao hakuna idadi ya watu. Kwa hiyo, suala hilo ni muhimu na tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunalizingatia katika kugawa mamlaka mpya. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Huu ukanda wa Milima ya Udzungwa unaelekea kwa kiwango kikubwa kwenye Wilaya ya Kilolo na huu ukanda unaungana na Kata ya Udekwa na Kata ya Ukwega ambayo pia, inaaminika kuwa na madini. Je, Wizara iko tayari kutuma wataalam kufanya utafiti ili kama madini hayo ya dhahabu yapo, kama ilivyo kule Ulanga, yaweze pia kuchimbwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama nilivyotangulia kusema, kama Wizara ya Madini, kupitia taasisi zake GST na hata STAMICO, tuko katika mpango mahususi wa kuendelea kufanya utafiti wa kubaini maeneo yote yenye madini nchini na itahusisha pia, eneo lake na sehemu alizozitaja kwa sababu, lengo letu kama Taifa ni kuhakikisha kwamba, rasilimali madini inakwenda kuzalishwa ili iletee Taifa letu tija. Nimhakikishie kwamba na nitumie pia nafasi hii kuiagiza taasisi yetu ya GST katika mpango kazi wao wa mwaka huu waweke katika utaratibu na ratiba safari ya kuelekea kule kufanya utafiti kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza; katika Kijiji cha Mgowelo ambacho kiko katika Kata hiyo hiyo ya Nyanzwa, kumetengwa zaidi ya hekta 3000 kwa ajili ya block farming. Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti kwenye eneo hilo na kuona umuhimu wa kuweka skimu pia kwenye hilo eneo kwa sababu ni hekta nyingi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwenye Bunge lililopita, niliomba Naibu Waziri au Waziri kutembelea eneo hili na kuangalia changamoto tunazopata za skimu mbalimbali, lakini mpaka sasa ziara hiyo haijafanyika. Je, Waziri ananiahidi lini atafika Jimboni Kilolo kwa ajili ya kutembelea na kuona tunaweza tukashauriana vipi? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kufika jimboni kwake naomba nimuahidi yeye na wananchi, nitakwenda mwenyewe baada ya Bunge hili kwa ajili ya kwenda kufanya kazi hiyo pamoja na kuangalia mwendelezo wa mradi wetu wa pamoja wa chai ambao yeye mwenyewe alikuwa muasisi wa kuanzisha huo mradi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hii block farm, naomba nimwombe baada ya kikao cha Bunge tukutane ofisini ili nimkabidhi timu ya watu ambao wataenda kufanya soil analysis na kuchukua mipaka ili tuiweke kwenye mipango ya Wizara.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya DDH ya Ilula, bado inategemewa sana wananchi wa Tarafa ya Mazombe na Tarafa ya Mahenge. Je, Serikali ina mpango gani wa kuendelea kuipelekea fedha hospitali ili iweze kutoa huduma bora kama ilivyokuwa ikitoa mwanzo ilivyokuwa DDH kabla ya kujengwa hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justine Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha inawezesha hospitali zetu hizi za DDH kuendelea kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo hayo. Kwanza kwa kuhakikisha kwamba fedha za mfuko wa pamoja health center basket fund zinaendelea kupelekwa, Hospitali hii ni moja ya hospitali zinazoendelea kupewa fedha hizo ili kuziwezesha kujiendesha na kutoa huduma bora, lakini pia kuangalia uwezekano wa kuendelea kuwapatia watumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuiunga mkono hospitali hii ili iendelee kutoa huduma kwa wananchi wa Mazombe na Tarafa zingine za karibu.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, kwa miaka 20 sasa Wilaya ya Kilolo haina Makao Makuu ya Polisi na wala kwenye Wilaya penyewe hakuna Kituo cha Polisi.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi za viongozi mbalimbali kujenga Makao Makuu ya Polisi katika Wilaya ya Kilolo kwenye Mji wa Kilolo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba Mheshimiwa kwenye Jimbo lake la Kilolo kama ambavyo Wilaya kadhaa zimekuwa zina ukosefu wa Vituo vya Polisi vya Wilaya na hii ni moja kati ya mambo ambayo jana niliyazungumza na mikakati ya Kiserikali ya kiujumla ya kukabiliana na tatizo hili, hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute Subira, lakini suala hili tumelichukua kwa uzito wake.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa TANROADS Mkoa wa Iringa walitii agizo la kwenda kuangalia barabara ya Mchepuko wa Mlima Kitonga, na tayari wameshafanya maandalizi ya awali. Je, Serikali inasemaje kuhusu kuanza usanifu na kuijenga barabara hiyo ya Mchepuko wa Mlima Kitonga ili wananchi waweze kupita kwa urahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyokiri kwamba tayari tumeshatoa maelekezo na baada ya kuipitia barabara sasa kinachofuata ni kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hilo litafanyika kwa sababu ndiyo barabara itakayotuokoa ikitokea changamoto yoyote katika Mlima kitonga. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru: -

Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa chuo cha ufundi VETA kwa Wilaya ya Kilolo kitajengwa kama ambavyo zimekuwa ahadi za Serikali kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni sera ya Wizara ya Elimu kwamba, katika kila wilaya tunakwenda kujenga chuo cha VETA. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vile sasa tumekamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 29 na vile vinne vya Mikoa ambavyo tunakadiria kunako mwezi Mei tutakwenda kumaliza katika mwaka ujao wa fedha tutaendelea na ujenzi katika maeneo ambayo bado vyuo havijaweza kujengwa. Ninakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kata ya Masisiwe haijawahi kuwa na mnara wala mawasiliano tangu uhuru wa nchi yetu.

Je, ni lini Serikali itajenga mnara katika kata hiyo ili wananchi waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali ilileta vijiji ambavyo vinaenda kupatiwa mawasiliano ikiwemo kata ya Masisiwe. Mheshimiwa Mbunge tayari tushawasiliana na iliingizwa kwenye mradi wa Tanzania ya Kidigitali, mradi amabao umefunguliwa tarehe 31 Januari, 2023. Hivyo basi mchakato wa tenda utakapokamilika tutajua kwamba ni mtoa huduma gani ambaye amepatikana kwa ajili ya kufikisha mawasiliano katika kata ya Masisiwe.

Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante.
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba na watumishi katika zahanati za Lugalo, Masege na Mbawi pia katika vituo vya afya vya Ruaha Mbuyuni, Ilula na Mluhe.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Justin Nyamoga Mbunge wa Jimbo la Kilolo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vituo vyote ambavyo amevitaja ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha vinapelekewa vifaa tiba na watumishi na ndiyo maana tunakwenda kuajiri watumishi 7,600 mwaka huu wa fedha pia tumetenga Shilingi Bilioni 69.95 kwa ajili ya vifaa tiba. Nimhakikishie kwamba tutatoa kipaumbele katika vituo hivyo. Ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pale Ruaha Mbuyuni kuna mradi wa umwagiliaji ulikarabatiwa na Wizara kwa force account, lakini sasa mto ule umeanza kuchepuka tena: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari tuongozane ili tuweze kuangalia tunafanyaje katika kuukarabati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, namwahidi tu kwamba Mheshimiwa Mbunge, kabla mimi na yeye hatujaongozana Jumatatu, Afisa wetu wa Tume ya Umwagiliaji walioko pale Iringa atakwenda kuukagua kwanza na kutupa taarifa, nami na yeye pia tutakwenda pamoja.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilolo yupo mwekezaji anaitwa Udzungwa Corridor na tayari anapanda mashamba makubwa ya miti kwa ajili ya biashara hiyo. Kwenye vivjiji vinavyozunguka kuna misitu mingi ya asili inayofanana na hiyo hiyo inayopandwa.

Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha ile misitu ambayo wanavijiji wameitunza na yenyewe inaingia kwenye huo mfumo wa biashara badala ya kutegemea tu ile ambayo Mwekezaji anawekeza na anapanda miti ile ile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lazaro Nyamonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza katika kitu ambacho tunakithamini sana ni upandaji wa miti. Pili tunashughulika na suala zima la kuishughulikia miti. Kwa hiyo, kikubwa nimwambie misitu yote ya asili kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi kwamba sasa hivi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumeshaandaa muongozo wa usimamizi wa misitu yote ili lengo na madhumuni tuingize kwenye mpango huo pia tuweze kunufaisha vijiji vilivyozunguka na pia tunufaishe Serikali, pia tutunze na tuhifadhi mazingira. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninayo maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza katika skimu hizi ikiwemo hii ya Mgambalenga lakini pia skimu za Ruaha Mbuyuni na nyingine gharama za ulipiaji wa vibali katika bonde zilipanda kutoka Shilingi 70,000 hadi Shilingi 150,000 zaidi ya asilimia 100. Sasa ningependa kujua ni mpango gani wa Serikali wa kupunguza hizi gharama maana gharama za kilimo zimeongezeka kwa hiyo inakuwa ni vigumu wakulima wale wa kujikimu kuweza kumudu kulipia vibali kwa ajili ya umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili katika Kata ya Nyanzwa skimu ya umwagiliaji iliyoko pale ambayo ni ahadi ya Mawaziri Wakuu kadhaa bado haijatekelezwa, pamoja na juhudi kubwa za kuifatilia zilizofanywa na mimi mwenyewe hata Diwani wa kule amekuja kufuatilia. Sasa ningependa kujua kwa sababu ndiyo uhai wa watu wa kule kwenye kilimo cha vitunguu.

Je, ni lini Serikali itajenga ile skimu kwa kuzingatia pia mwaka huu hali ya umwagiliaji imekuwa ngumu na hali ni mbaya, ni lini Serikali itafanya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Nyanzwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza kuhusu gharama ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge gharama zimekuwa juu tofauti na ile gharama ya awali ambayo ilikuwepo. Tumeielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kukutana na mamlaka ya bonde husika kukaa na kuangalia uhalali wa gharama hizo ili tumpunguzie adha mkulima.

Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu mradi wa Nyanzwa ni kweli mradi huu Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiufuatilia sana na ninampongeza sana kwa hili. Tayari pale tuna miundombinu ya hekta 300 na tunachangamoto kubwa ya uhaba wa maji ya umwagiliaji, katika bajeti ya mwaka 2022/ 2023 Tume itafanya usanifu wa kina wa bwawa kuvuna maji ya mvua na usanifu huo pia utahusisha eneo la hekta 9,000 ili kuwahudumia wakulima wengi zaidi na baadae tutajenga kama ambavyo usanifu utakuwa umeelekeza.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya kutoka Ilula – Mlafu – Mkalanga – Kising’a hadi Kilolo kwa sasa haipitiki kutokana na uharibufu mkubwa wa mvua.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuiagiza TANROADS kufanya marekebisho ya haraka ili barabara hii muhimu iweze kuendelea kupitika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa ahakikishe kwamba anakwenda kwenye hii barabara ndani ya siku mbili ili kwenda kufanya tathmini na kufanya marekebisho ya sehemu zote ambazo hazipitiki ili wananchi wa Kilolo waweze kuendelea kupata huduma ya barabara hii.