Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Khamis Hamza Khamis (71 total)

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ya Mambo ya Ndani, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia katika maeneo mengi, Jeshi la Polisi limeshindwa kufika kwa wakati kwenye matukio kwa sababu za kukosa mafuta na matengenezo ya magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ustawi wa jamii yetu unategemea sana ulinzi na usalama unaofanywa na Jeshi letu la Polisi. Swali la kwanza, je, Wizara haioni sasa ni wakati muafaka wa kufanya marekebisho hayo ya kisheria?

Mheshimiwa Spika, pili, Wizara haioni ni muda muafaka sasa kupeleka hizo fedha moja kwa moja kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya badala ya kupitisha kwa Wakuu wa Polisi wa Mikoa ambapo imetengeneza urasimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amesema kwamba hatuoni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii? Mabadiliko ya sheria siku zote yanakwenda na mahitaji. Inawezekana ikawa kuna hitaji la kufanya hivyo, lakini sheria hii ikawa iko hivi hivi mpaka tufike wakati tuone namna ambavyo tunaweza kufanya mabadiliko ya sheria hii.

Mheshimiwa Spika, nataka kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba ukiangalia Sheria ya Bajeti, kuna kitu kinaitwa vote holder na kuna kitu kinaitwa sub-vote holder. Sasa vote holder moja kwa moja anayo IGP na sub- vote holder anayo RPC. Kwa hiyo, fungu likitoka kwa IGP linakuja kwa RPC. Huo ndiyo utaratibu halafu sasa ndiyo zinagawiwa Wilaya husika kama ambavyo tumeeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama sasa inafika wakati tunahitaji mabadiliko ya sheria hii, basi acha tulichukue hilo tukakae na wadau halafu tuone namna ambavyo tunaweza tukalifanyia mabadiliko. Kwa sababu, suala la kufanya mabadiliko ya sheria is a matter of procedure… (Makofi)

SPIKA: Unajua Waheshimiwa Wabunge huwa mnapiga makofi ambapo hamjui hata mnapiga makofi ya nini? (Kicheko)

Ahsante, malizia kujibu. Umemaliza eeh!

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Ndiyo.
MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba tunajua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inajitahidi kupunguza ajali za bodaboda, tukiangalia kwa mwaka 2019 tulikuwa na ajali 567 lakini mwaka 2020 tuna 240. Je, Jeshi la Polisi lina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizi zinapungua zaidi? Tukiangalia wahanga wakubwa ni vijana na wanawake ndiyo wanaopata shida ya kupoteza vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; utafiti unaonyesha askari wastaafu wanachelewa kupata mafao yao, je, Wizara husika ina mpango gani wa kuhakikisha askari hawa baada ya kustaafu wanapatiwa mafao yao kwa haraka ili kuepusha wanapokuwa kazini kuchukua rushwa ili kujilimbikizia akiba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi inaonekana Mheshimiwa tumempa sababu moja au njia moja ambayo tunaweza tukaitumia katika kuepuka hizi ajali. Zipo njia ambazo tumeshazichukua kama Serikali na nyingine tuko mbioni kuzichukua kwa kushirikiana na Wizara nyingine au kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba hizi ajali za barabarani zinapungua. Cha kwanza tumefikiria kuendelea kuwafundisha zaidi hasa vijana wa bodaboda namna ya kutumia alama za barabarani ambazo zina uwezo mzuri wa kuwaeleza kwamba wanakoelekea wanaweza wakapata ajali.

Mheshimiwa Spika, lingine tuna mpango sasa wa kutengeneza mfumo wa kufunga au ku-control ajali kwa kutumia vidhibiti mwendo, ambapo tunahisi hivi vinaweza kupunguza ajali. Pia tuna mpango wa kufanya marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda moja kwa moja kwenye masuala ya faini na adhabu katika mambo haya ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie pia kuwaelimisha vijana kwa sababu naamini katika mkoa wake vijana wa bodaboda wapo, basi azidi kuwaelimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu mafao ya Askari. Kwa kweli Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunawalipa wastaafu posho zao mara tu baada ya wao kustaafu. Katika kipindi cha 2018/2019 tumejitahidi kati ya wastaafu 591; jumla ya wastaafu 479 tayari tulishawapatia mafao yao na sasa hivi wengi wanaishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kinachokuwa kinatukabili kama sehemu ya changamoto, inafika wakati inakuwa OC nazo na bajeti nayo inakuwa mtihani, kwa hiyo, ndiyo maana kuna wakati wanachelewa kidogo kulipwa. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama itakuwa kuna mtu ambaye hajapata mafao yake na amestaafu, basi tukitoka hapa tuonane, tuone tunamsaidia vipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la msingi la ajali za barabarani kwa bodaboda na vyombo vingine vya usafiri. Tatizo hili ni Kitengo cha Usalama Barabarani kugeuza kitengo hiki kama chanzo cha mapato. Watu wanakwepa matrafiki, wanakimbia kwa sababu ukikamatwa hakuna onyo, ni faini. Bodaboda siku hizi wanakamatwa kwa kukimbizana na trafiki. Nadhani hii inasababishwa na uzee wa sheria hii ni ya mwaka 1973. Ni lini Serikali italeta mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ili tufungue mjadala wa namna gani tutaiboresha ili kupunguza ajali za barabarani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDAIN YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Salome, Muswada huu uko njiani, muda wowote tutauleta tuje tuujadili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya mabadiliko ya baadhi ya sheria hizi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, tuko mbioni kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba dai la ekari 495 ni jipya, bali ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani mbele ya Mheshimiwa Rais wakati huo alipofanya ziara Mkoa wa Rukwa kwamba watawakabidhi wananchi ekari 495. Lililokuwa linasubiriwa ni kukabidhi kwa maandishi kwa sababu Jeshi la Magereza limekuwa likisema kwamba hatuwezi kufanyia kazi matamko ya wanasiasa mpaka tupewe barua kutoka Wizarani. Ni lini Wizara itawapa barua Jeshi la Magereza ili kukabidhi hizo ekari 495 kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tamko hili limepelekea Askari Magereza sasa kuingia kwenye mgogoro mkubwa na wananchi na kuwanyanyasa kwa kuwapiga na mara ya mwisho juzi tu hapa nilikuwa huko Jimboni, mama mmoja (na nikikurushia clip utaona) amepigwa na kugaragazwa kwenye matope. Je, Wizara iko tayari kuunda Tume itakayokuja kuchunguza unyanyasaji unaofanywa na hawa Askari Magereza na watakaobainika kunyanyasa wananchi hatua kali za kisheria zichukuliwe iwe fundisho kwa wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tufike wakati tukiri kwamba kuna baadhi ya maeneo bado yana mivutano baina ya wananchi na Kambi za Magereza. Swali kwamba ni lini tutatoa hilo eneo, suala la utoaji wa eneo linahitaji taratibu, siyo suala la kusema tunakwenda na kutoa.

Mheshimiwa Spika, lingine amesema watu wananyanyaswa, wanapigwa, kitu ambacho tunakifanya kupitia Wizara, kwanza tutachunguza, tukiona kwamba kuna Maafisa wetu wa Magereza ambao wanahusika na unyanyasaji huo, hatua kali tutazichukua kupitia Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DAIMU IDDI MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jimbo la Tunduru Kusini lina tarafa tatu, Tarafa ya Nalasi, Lukumbule na Sakata na zote zimepakana na Mto Ruvuma, kwa ng’ambo ni Msumbiji, lakini katika Jimbo hilo Kituo cha Polisi kiko kimoja tu kipo kwenye Tarafa ya Nalasi peke yake. Swali la kwanza, je, Serikali haioni ni muhimu sana kwa sasa kukamilisha Kituo cha Polisi Lukumbule ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa mipakani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Lukumbule ni sehemu ambayo watu wengi wanapitia kwenda na kutoka Msumbiji katika harakati za kufanya biashara. Wananchi wa Msumbiji wakija Tanzania hamna mahali popote wanapopita tunawapokea kiurafiki, lakini sisi Watanzania tukienda Msumbiji tunakamatwa wanapigwa, wananyanyaswa na kunyang’anywa mali zao. Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuharakisha mazungumzo ya kuanzisha Kituo cha Uhamiaji katika kijiji au Makao Makuu ya Tarafa ya Lukumbule?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduru Kusini kulikuwa kuna vituo vitatu, Kituo cha Nalasi, Masuguru na Lukumbile lakini kwa bahati mbaya hiki kituo kimoja kilikuja kikatiwa moto baada ya kutokea machafuko ya wananchi. Hata hivyo, baada ya Serikali kuona umuhimu sasa wa kuwepo kituo ili sasa kuimarisha hali ya ulinzi pale, Serikali ikashusha Waraka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili sasa watusaidie kujenga kile kituo hili eneo la Lukumbile. Hivi ninavyokwambia tayari kituo kimeshaanza kujengwa na kimeshafikia katika hatua ya lenta. Sasa kikubwa tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tunaenda kutengeneza mazingira sasa ya kuona namna na kupitia umuhimu wa kuwepo kituo hiki ili sasa tuweze kuweka kituo hiki ili wananchi waweze kuishi katika mazingira ya usalama zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, hakuna Serikali yoyote duniani ambayo inapenda wananchi wake wapate tabu; wanyanyaswe, wapigwe, wadhulumiwe. Sasa kitu ambacho nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, kutokana na umuhimu wa suala hili tunakwenda kuona namna ambavyo tutakapotengeneza bajeti yetu hii Wilaya ya Tunduru hasa katika hii sehemu ambayo wanahitaji Kituo hiki cha Uhamiaji tutaipa kipaumbele ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata kituo cha uhamiaji hapa ili wananchi waweze kuepukana na huo usumbufu. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu na takwimu zilizotolewa na Serikali, ukweli ni kwamba kutoka ngazi ya Mkaguzi Msaidizi kwenda Mkaguzi kamili inapaswa kufanyika ndani ya mwaka mmoja mpaka miaka miwili. Je, Mheshimiwa Waziri anayo taarifa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka muda huu ambapo nimesimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuna Wakaguzi Wasaidizi ambao hawajapandishwa madaraja?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri atueleze hapa ikiwa anazo hizo taarifa ni kwa nini basi hao Wakaguzi hawajapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, si kweli kwamba tangu 2015 mpaka hapa tulipo watu hawajapandishwa madaraja. Kama ataangalia kwenye jibu langu la msingi nilitoa takwimu ambazo zinaonyesha kwamba kuna watu walipandishwa madaraja.

Mheshimiwa Spika, kingine nimfahamishe tu Mheshimiwa kwamba ni vizuri wakapata nafasi wakaipitia hii PGO (Police General Order) itawasaidia kujua baadhi ya taratibu ambazo zinatumika kupandisha madaraja. Kuna mambo ya msingi huwa yanaangaliwa, siyo kwamba watu wanapandishwa tu kwa sababu hawajapandishwa muda mrefu. Kwanza, lazima kipatikane kibali cha kupandisha majaraja. Pili, tunaangalia pia uwezo wa kiuongozi wa yule ambaye anatakiwa kupandishwa daraja. Tatu, tunazingatia zaidi vigezo vya kimaadili kwamba tunayekwenda kumpandisha cheo ana maadili gani katika kutumikia Taifa hili. Nne, tunaangalia kama hana mashtaka mengine. Tano, huwa tunaangalia na bajeti maana tukimpandisha cheo lazima tumpandishie na mshahara wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa afahamu kwamba utaratibu ndiyo huo lakini tumeanza na tumepandisha madaraja mbalimbali kwa watumishi wa Jeshi la Polisi kama ambavyo taratibu zimeeleza.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada inazochukua katika kupiga vita ukatili wa watoto kwa suala la ubakaji. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza litalenga kwenye majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na tafiti ambyao amefanya na kututaka sisi sasa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuweza kusaidia katika kutatua changamoto hizi.

Swali langu liko kwamba, je, ninyi kama Serikali mmejipangaje kuhakikisha kwamba vitengo vyote vinavyoshughulikia masuala ya sheria na kutoa haki vinashirikiana kikamilifu ili kuweza kutokomeza masuala haya ambayo mmeyatafiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na Sheria Namba 21 ya Mtoto ya mwaka 2009. Sheria hii imeweka wajibu na jukumu la wazazi ama walezi kuweza kuwalinda watoto dhidi ya ukatili ikiwemo hili la ubakaji.

Je, mmekwama wapi katika kutekeleza sheria hii kiasi kwamba tunaona hakuna mzazi au mlezi anayeweza kuchukuliwa hatua pale ambapo mtoto anapatikana na makosa haya tukizingatia ndoa zinavunjika kwa wingi na watoto wanatelekezwa na inasababisha kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, lakini pia wale wazazi ambao wanabaki, akina baba wanaweza kufanya vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto wao wenyewe. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza lilikuwa linasema kwamba, je, Serikali ina mpango gani au je, kuna jitihada gani nyingine ambazo zimechukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, tunatokomeza vitendo hivi. Kama Serikali tumechukua jitihada nyingi na tumechukua jitihada mbalimbali, lakini bado tunaendelea kuchukua jitihada ya kwanza ikiwemo ya kuendeleza kutoa elimu kwa jamii kwa sababu, tunaamini jamii ikipata elimu ya kutosha kwenye masuala haya maana yake masuala haya yanapungua au yatamalizika moja kwa moja. kwa hiyo, kama Serikali tumeanza kutoa taaluma kwanza kupitia kwenye madawati ya kijinsia ambayo mara nyingi yapo katika Jeshi la Polisi, tunayatumia yale kutoa taaluma hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunao hawa para legals, wasaidizi wetu wa sheria ambao wako huko, wanatusaidia kuipa jamii taaluma. Pia tunavitumia vyombo vya habari kuhakikisha kwamba, taaluma inafika kwa jamii, lakini kizuri zaidi tunaenda kutengeneza mazingira ya kuipa nguvu sheria hii Namba 21 ya mwaka 2009 ili kuhakikisha kwamba, sheria inafuatwa na wananchi kwa kiasi kikubwa jamii inapungukiwa na matendo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la pili ameuliza kwamba, sheria hii inakwama wapi? Naomba pia kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati tunaipitia sheria hii tumegundua kwamba, sheria hii ipo kimadai zaidi rather than kijinai. Sasa ukitazama unakuta kwamba, watu wanaweza wakafanya vitendo hivi wakitegemea kwamba, wao watafunguliwa kesi zaidi za madai na kwa sababu, madai si analipa. Kwa hiyo, sasa unakuta haiko kijinai zaidi. Kwa hiyo, unakuta sheria ndio maana unafika wakati utendaji wake wa kazi unakuwa haupo vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni ugumu wa wananchi kwenda kutoa ushahidi, ugumu wa mashahidi. Ukimchukua mtu akitoa ushahidi huko nyumbani ukikaa naye atatoa ushahidi vizuri tu, tena atatoa ushahidi maana yake ambao uko evident, lakini kesho twende mahakamani ndio inakuwa ngumu. Sasa na mahakama nayo ikiwa siku mbili, tatu, mara nne tano umeitwa hujaenda kutoa ushahidi maana yake mahakama inatoa uamuzi kwa upande mmoja. Kwa hiyo, upo ugumu kwenye utoaji wa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine sasa wanafamilia, wanamalizana tu kienyeji. Jambo limetokea kwa sababu, baba mkubwa, baba mdogo wanamalizana huko mwisho wa siku huku sheria inakuwa haipewi nguvu. Nakushukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa Serikali imekiri kuleta Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2009 Bungeni, je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mabadiliko ya sheria ambayo inawafanya makosa ya jinai kwa wafungwa waliokaa mahabusu kwa muda mrefu iletwe ili iweze kupunguzwa muda wa kukaa muda mrefu kwa mfano wale wafungwa Masheikh wa Uamsho?

Swali la pili, Serikali haioni umuhimu sasa badala ya kuwekeza kujenga mahabusu mpya nyingi iwekeze kwa kumsaidia DPP kujenga uwezo wa kusimamia kesi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa mahakamani, ushirikishwaji na ujibuji wa maswali yao wakienda mahakamani inakuwa bado upelelezi unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatib Said Haji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza lilikuwa linasema je, hatuoni haja sasa ya kuweza kufanya baadhi au mabadiliko katika hii Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba akipata muda akiipitia sheria hii atagundua kwamba tayari kuna baadhi ya maeneo yalishafanyiwa marekebisho kitu ambacho sasa kimeelekea katika kupunguza kwa asilimia kubwa huu mrundikano. Kwa mfano, ukiangalia katika kifungu cha 170; ukiangalia kifungu cha 225 na ukiangalia katika maeneo ya 163 na hayo na baadhi ya mengine ni maeneo tuliyoyafanyia marekebisho ili kuona tunapunguza hii changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tunapotaka kufanya marekebisho ikiwa addendum ama amendment ya sheria kuna mambo ya msingi tunakuwa tunayaangalia. Kwanza tunaangalia applicability ya ile sheria, je, ipo applicable? Ikiwa kama sheria ina tatizo katika utekelezaji wake pale tunasema sasa tuna haja ya kufanya mabadiliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hilo halitoshi tunakuwa tunaangalia na mahitaji ya jamii kwa wakati ule, sasa kikubwa mimi niseme tu kama wanahisi au Mheshimiwa Mbunge anahisi kwamba kuna haja basi tutakwenda kukaa tuipitie tena tuone, pamoja na mabadiliko tuliyokwisha kuyafanya tutakwenda kukaa ili tuone kwasababu lengo na madhumuni ni kuhakikisha kwamba changamoto za mrundikano wa majalada na mrundikano wa mahabusu katika mahakama na wafungwa inapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hilo halitoshi swali la pili Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba tuone namna ya kuwapa uwezo au kwa nini tusifanye maarifa DPP tukampa kazi ya kuweza kufanya upelelezi ili mambo yakaenda. Kazi ya kufanya upelelezi kwa mujibu wa taratibu kuna vyombo maalum vinavyohusika kufanya upelelezi. Wenye kufanya upelelezi ni polisi na siyo polisi wote kuna vitengo maalum vya kufanya upelelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenye kufanya upelelezi labda ni watu wa TAKUKURU, wenye kufanya upelelezi labda watu wenye kazi maalum tukisema leo DPP tunampa kazi ya kufanya upelelezi tunamuongezea jukumu lingine na usije ukashangaa akasema na kamshahara nako kapande. Mimi niseme tu kwamba kwa kuwa haya mashauri yametolewa tunayachukua tunakwenda kuyafanyia kazi nakushukuru.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimwa Naibu Waziri maswalli mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri aliyoyatoa. Swali la kwanza; ni ukweli usiopingika kwamba kama alivyosema ziko pikipiki ambazo labda wakati mwingine zinaokotwa na zinapelekwa pale. Kwa maana yake ni kwamba hakuna jalada lolote llinalofunguliwa kwenda mahakamani na matokeo yake pikipiki na magari kama hayo yanaweza kukaa zaidi ya miaka kumi.

Je, tunakubaliana kwamba sasa viendelee kukaa hapo na kuozea hapo au ni vizuri vikafanyiwa utaratibu mwingine ili hiyo fedha ikapatikana kwa ajili ya maendeleo ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wakati tunaunda Sheria ya kuruhusu bodaboda ili waweze kufanya kazi na kupata ajira kilichotokea ni kwamba zilezile faini zilizokuwa zinatumika kwenye vyombo vya usafiri ndio zilizochukuliwa na wakaanza kubandikwa bodaboda, lakini ikumbukwe kwamba bodaboda anabeba abiria mmoja, akikutwa na kosa analipa Shilingi elfu thelathini basi lenye abiria 60 akikutwa na kosa hilo hilo analipa elfu thelathini. Sasa napenda kujua ni lini Serikali itabadili hizi adhabu inayolingana na bodaboda ambayo ni ya chini ukilinganisha na adhabu iliyopo ambayo pia inatozwa kwa magari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vedastus M. Manyinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameulizia, je, Serikali haioni haja ya bodaboda hizi ambazo zimelundikana katika vituo hivyo vya polisi basi ziuzwe au zipigwe mnada ili sasa Serikali iweze kujipatia mapato? Jibu ni kwamba, uwepo wa pikipiki hizi kwenye vituo hivi kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kutokana na sababu tofauti. Ukiziona pikipiki zimekaa kwenye Kituo cha Polisi usifikirie kwamba zimekaa kwa muda mrefu kwa sababu, utaratibu ni kwamba baada ya miezi sita endapo mwenye pikipiki yake asipokwenda kwenda kuikomboa pikipiki ama kulipa faini au taratibu nyingine akaziruhusu zikaendelea, maana pikipiki ile itaendelea kubakia pale.

Mheshimiwa Spika, baada ya miezi sita itaenda kupigwa mnada. Kwa hiyo inawezekana pikipiki hizo ambazo mnaziona kwenye Vituo vya Polisi ni kutokana na kwamba muda wake haujafika. Kwa mujibu wa taratibu hatutaweza kuipiga mnada ama kuiuza pikipiki ya mtu bila ya muda uliokusudiwa ama uliowekwa katika utaratibu kuwa haujafika.

Mheshimiwa Spika, utaratibu upo na kanuni na sheria zipo; ukiangalia kwenye PGO, ile 304 ukiangalia kwenye kifungu cha (1), (2), (3), (4), (5) na kuendelea imeelezwa Jeshi la Polisi limepewa mandate au limepewa mamlaka ya kuuza na kupiga mnada endapo itazidi zaidi ya miezi sita. Kwa hiyo hizo pikipiki zilizopo huko ni kwa sababu muda wake wa kufanyiwa hivyo haujafika, utakapofika hazitaonekana hizo. Aidha, nipende kusema kwamba tuendelee kushirikiana kutoa elimu huko kwa vijana wetu ili wasiendelee kuzifikisha huko.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali la pili, anasema, basi litapakia watu zaidi ya 30 faini yake ni Shilingi elfu thelathini, bodoboda ambayo inapakia mtu moja faini yake ni Shilingi elfu thelathini; sasa Serikali haioni haja hapa sasa ya kufanya marekebisho? Serikali katika hili bado haijaona haya ya kufanya marekebisho ya hili. The way itakavyofanya marekebisho kwa sababu nilivyomfahamu Mheshimiwa tushushe, maana kama basi watatoa shilingi 80,000, maana yake bodaboda watoe shilingi 10,000.

Mheshimiwa Spika, hizi Shilingi elfu thelathini ambazo zimewekwa bado matukio yanaongozeka na lengo letu sio kuwakomoa wananchi ama kuwakomoa vijana watumiaji wa bodaboda na pikipiki, lengo ni watu kufuata sheria kuepuka na kupunguza idadi ya ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka kufika Disemba, 2020 ajali za bodaboda ni 164; waliokufa ni 134 ambao wamekuwa injured 129 tu, tukizipunguza hizi tukisema sasa tuweke shilingi elfu kumi, vijana watazidi kufanya zaidi na hapo lengo na madhumuni ana uwezo wa kulipa Shilingi elfu kumi. Kwa hiyo tu niseme hatufanyi hayo kwa ajili ya kuwakomoa, tunafanya ili watu wafuate.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa kuna utaratibu, nimekuwa nauona sana kule Zanzibar, vijana wanajazana kwenye magari makubwa yanaitwa mafuso, wanakwenda ufukweni huko muda wanaorudi huko wanarudi na bodaboda pikipiki hazipungui 30 au 40 njiani, lazima ajali inatokea, sasa kwa sababu analipa shilingi elfu kumi watafanya vyovyote kwa hiyo.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba tunayachukua mawazo tutakapo ona haja ya kufanya mabadiliko ya hii sheria tutafanya lakini kwa sasa naomba tuwe na hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, swali langu lilikuwa linaendana na haya mahusiano kati ya bodaboda na Trafiki na kule Makete mahusiano ya bodaboda na traffic ni kama Refa ambaye yuko uwanjani ana kadi nyekundu tu, mahusiano yao ni mabaya sana kwa kiwango ambacho Traffic wanatoza faini ya shilingi laki mbili, tofauti na utaratibu wa kawaida. Tumejaribu kufanya vikao vya negotiation kati ya sisi na watu wa Trafiki lakini imeshindikana. Pili, Traffic wanafuata bodaboda wangu mashambani kule Matamba, kule Makete, kitu ambacho ni kunyume na utaratibu. Sasa je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatupa kauli gani na maelekezo yapi kwa Trafiki Mkoa wa Njombe hususani Wilaya ya Makete dhidi ya vitendo viovu ambavyo vinafanywa na wao dhidi ya bodaboda wa Makete? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu wetu kwenye PGO na utaratibu uliowekwa kwenye ile sheria au kanuni ya 168 ambayo imefanyiwa mabadiliko mwaka 2002, umesema ni Shilingi elfu thelathini, sasa kama kutatokezea askari au yoyote ambaye anayehusika na hili akawatoza watu zaidi ya kiwango kilichowekwa maana huyo anafanya kosa kwa mujibu wa taratibu kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Spika, watu kuwafuata huko, unajua mtu anapokuwa mhalifu kwa mujibu wa utaratibu vyombo vinavyohusika kumkamata vina uwezo wa kumfuta popote alipo endapo amefanya makosa, lakini sasa hiyo namna ya kumfuata nayo ina utaratibu wake. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, kama kutakuwa kuna askari amechukua zaidi ya hizo, maana huyo anavunja sheria, nadhani Mheshimiwa tushirikiane katika hili kuweza kuwakamata na kama tunawajua tuwalete katika ofisi yetu, tujue namna ya kuwashughulikia kwa mujibu wa taratibu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, je, ni njia zipi kama Serikali mnazitumia kuwajulisha wale ambao hadi leo hawajapatiwa vitambulisho vyao kwenye vituo vya NIDA?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatambua kuwa kwenye ofisi za NIDA kuna uhaba wa watumishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Saada Mansour Hussein, lakini pia nataka kutumia fursa hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaifanya katika Mkoa wa Kaskazini ya kuhakikisha kwamba akina mama au wananchi, lakini zaidi akina mama na watoto wanaishi katika mazingira mazuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni njia zipi ambazo tunazichukua kama Serikali kuhakikisha kwamba wale ambao hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao taarifa zinawafikia.

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nichukue fursa hii, niwashukuru wananchi na viongozi kwa kuwa wametambua kwamba bado kuna baadhi ya wananchi hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao mpaka muda huu, badala yake wanakaa wanalaumu Serikali. Kwa hiyo kikubwa ambacho nataka niseme ni kwamba, zipo njia nyingi ambazo huwa tunazitumia kuwafikishia ujumbe au taarifa kwamba vitambulisho vipo na waje.

Mheshimiwa Spika, ya kwanza; huwa tunawatumia ujumbe mfupi, kwa wale ambao namba zao zipo hewani zinapatikana. Pia huwa tunawapigia simu kabisa kuwajulisha. Vile vile kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya na kupitia Ofisi za Masheha na Watendaji huwa tunatoa taarifa hizo ili wananchi ambao wameshatengenezewa vitambulisho vyao, lakini hawajaenda kuvichukua, waende wakavichukue.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nikiri kwamba, bado tuna changamoto ya rasilimawatu katika Ofisi zetu za NIDA, lakini nimwambie Mheshimiwa aendelee kustahimili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia NIDA tupo katika mchakato wa kutengeneza mazingira ya kuajiri vijana, lengo na madhumuni, shughuli za NIDA ziweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja tu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza kituo hiki kwa sababu kituo hiki ni chakavu, cha siku nyingi na kibovu. Sasa naiomba Serikali tufuatane, tuongozane na Waziri ili akajionee mwenyewe katika kituo hicho cha Bububu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa juhudi kubwa anayoifanya na najua anataka kile kituo kifanyiwe ukarabati ili kiweze kutoa huduma kwa sababu jimbo lake ni jimbo ambalo lina harakati nyingi za kiutalii ambazo zinachangia pato kubwa la Taifa. Kwa hiyo harakati hizi sometime zinakuwa zinapelekea athari za kiusalama.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa kwamba nipo tayari kufuatana naye kwenda kukagua kituo kile chumba kwa chumba, eneo kwa eneo ili kuona wapi panahitaji marekebisho na tuko tayari kama Serikali kukirekebisha kituo kile. Nakushukuru.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza japo majibu walionipa angalau yanaridisha.

Swali la kwanza, natamani kufahamu; kwa kuwa magereza wao wamekiri bado uwezo wa kulisha mahabusu na wafungwa ni mgumu, upo kwa asilimia 54. Je, hawaoni sasa ipo haja ya hawa mahabusu kuweza kushirikishwa kuzalisha chakula chao tu kwa sababu maandiko yanasema kila mtu atakula kwa jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili natamani kufahamu; tunafahamu kabisa Magereza changamoto ya magodoro ni kubwa sana. Katika changamoto hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha magodoro yanakuwepo kule, lakini hali bado ni ngumu; na tunafahamu kuna taasisi nyingi sana zinazokuwa zinahitaji magodoro kama shule na Serikali haiwapatii:-

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya mahabusu au wafungwa wote wanaokuwa wanafungwa wakawa na kigezo cha kwenda na magodoro yao ili kuweza kupunguza changamoto ile kwa sababu sio wote wanashindwa kuwa na godoro hilo kuliko kuiongezea Serikali mzigo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kanuni au Sheria, hakuna eneo ambalo linakataza kwamba watu kuingia na vitu wanavyovitaka katika Magereza, lakini sasa sababu mbili ndizo ambazo zinatufanya mpaka tufike hatua ya kusema kwamba haiwezekani kila mtu aingie na kitu chake Gerezani. Sababu ya kwanza, moja ni busara ya Jeshi la Magereza kama Jeshi la Magereza. La pili, ni sababu za kiusalama.

Mheshimiwa Spika, unapochukua kitu ukakiingiza kwenye Magereza, maana yake kinaweza kikachomekwa kitu kingine ndani yake ambacho kinaweza kikaja kuwadhuru wengine. Ndiyo maana hata ukifika wakati ukitaka kuleta chakula au dawa au kitu kingine, lazima tukithibitishe tukihakikishe na tujue kwamba hiki kina usalama kwako, kwetu tunaokipokea na kwa yule ambaye anakwenda kukitumia. Kwa hiyo, suala la kila mtu aingie na godoro lake, pazito kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine tunaweza tukajikuta tunatengeza tabaka kwamba kuna mtu anaweza kuingia na godoro lake na mwingine akashindwa. Kwa nini sasa na mahabusu nao wasishiriki katika shughuli za uzalishaji? Mahabusu na wafungwa wote ni binadamu, lakini hata akiitwa mfungwa, maana yake kesi yake imeshakuwa held, kwa maana ya kwamba imeshahukumiwa aende jela miaka mingapi? Kwa hiyo, yule tunayo sababu ya kumwambia sasa nenda kalime, nenda kazalishe kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya gereza. Sasa huyu mahabusu bado kesi yake haijahukumiwa kwa hiyo, yupo pale. Kusema tumchukue tukamfanyishe kazi, tukamlimishe bado kidogo busara hiyo hatujafikia. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri, kwanza naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutupa majibu ya uhakika ya kupata ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, suala la ajira kwa vijana wa Jeshi la Polisi, hasa wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari 150 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo ndiyo tatizo kubwa kwa sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba; Jeshi la Polisi linapoajiri vijana kupitia Jeshi hili kuna tatizo/ changamoto moja kubwa kabisa; vijana wengi wanaondoka kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kuomba ajira ya Jeshi la Polisi,

Je, changamoto hii wamejipangaje kuhakikisha kwamba vijana wa Mkoa wa Kaskasini Pemba ndio wale wanaohusika hasa kutokana na sifa walizonazo kajiriwa katika Jeshi la Polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie fursa hii kwanza kumpongeza kwa kuwa Mheshimiwa Omar siyo tu amekuwa mwakilishi ama Mbunge wa Jimbo la Wete, lakini pia amekuwa anafanya kazi na kuusemea mkoa wake kwa ujumla katika mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya siasa, uchumi na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba nafasi hizi zimekuja na zitakwenda katika kila mkoa. Na zitapita katika kamati za ulinzi na usalama kama utaratibu ulivyokuwa umepangwa. Lakini kikubwa nimwambie kwamba idadi ya nafasi alizozitaja zinaweza zikaenda mahali ambapo patakuwa pana uhitaji zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yana uhitaji zaidi. Kwa mfano kuna maeneo yana idadi kubwa ya watu (wananchi), kwa sababu utaratibu ulivyo ni kwamba askari mmoja analinda raia kuanzia 350 mpaka 400, kwa hiyo ikiwa mahali pana watu wengi panaweza pakapelekwa idadi hiyo. Lakini pia tutaangalia na crime rate (hali ile ya vitendo na matukio ya uhalifu ya mara kwa mara) pia yatatupa sisi impetus ya kuona wapi tuangalie itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa nimwambie Mheshimiwa, kwamba katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, nafasi hizi zitakwenda na vijana wataomba na Serikali itaendelea kutekeleza azma yake ya kuwaahidi wananchi na kuwatekelezea. Asiwe na wasiwasi wananchi/vijana wake wataajiriwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya vijana kutoka mkoa mmoja ama wilaya moja kwenda nyingine kuomba hizi nafasi. Kiutaratibu sifa inayokuja anatakiwa awe Mtanzania, haikusema kwamba atoke Pemba au Unguja au wapi. Kwa hiyo anaweza akatoka sehemu moja akaenda nyingine.

Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa tuwaambie kwamba watakaosimamia nafasi hizi wahakikishe vijana ambao wako katika mkoa husika wapate hizi nafasi ili lengo na madhumuni vijana waweze kupatiwa ajira kama ambavyo Serikali iliwaahidi wakati wa kampeni. Nakushukuru.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya kuridhisha kiasi ya Naibu Waziri, lakini vitendo vya udhalilishaji na uhalifu katika Wilaya ya Magharibi “A” ambapo Jimbo langu la Mtoni lipo, lakini pia na kituo hicho cha polisi tunachokizungumzia kipo, vimekuwa vikiongezeka sana.

Sasa je, nini kauli ya Serikali katika wakati huu wa vitendo vikiongezeka na kituo kimefungwa nini kauli ya Serikali juu ya mapambano yake ama inafanya nini kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya uhalifu na udhalilishaji unapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Jimbo la Mtoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuambie Mheshimiwa Abdul kwamba nipo tayari kufuatana na yeye kwanza kwenda kukiona kituo hicho, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na uongozi wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Mjini ili lengo na madhumuni kuweza kufanya nao mazungumzo, ili ikiwezekana baada ya kujiridhisha tuone namna ambavyo tunaweza tukakifungua kituo hiki na kikaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nipo tayari kwenda kukaa na wananchi kuweza kuwaambia maneno mazuri ambayo yatawapa imani ya kuendelea kuwa amani na salama na utulivu katika Jimbo lao. Lakini kikubwa nimuambie kwamba hili suala lake aliloliuliza la kuongezeka kwa matukio haya ya udhalilishaji katika Mkoa huu, katika Jimbo lake na katika Wilaya hii, Serikali tuna mipango mingi ambayo tumeshaanza kuifanya. Lakini kubwa nimuambie kwamba kwanza tunakwenda kuongeza nguvu kwenye masuala mazima ya ulinzi shirikishi. Ulinzi ambao unawapa nafasi wananchi wenyewe kushiriki katika ulinzi huu wa wananchi wao binafsi na hapa nataka nichukue fursa hii, nimpongeze sana Mheshimiwa Abdul-Hafar amekuwa anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza amewatafutia kituo hawa walinzi shirikishi, lakini kubwa amewatafutia vifaa vya ulinzi kwa ajili ya kufanya doria zao. Lakini pia anafika wakati anawagawia hata posho ili lengo na madhumuni shughuli za ulinzi katika Jimbo lake ziendelee. Lakini kingine ni doria, misako na operesheni mbalimbali tunaziendesha katika Jimbo hili, ili lengo na madhumuni wananchi waishi kwa amani. Lakini kikubwa ziara za Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa tutajitahidi tuziongeze katika Jimbo hili na maeneo mengine ili lengo na madhumuni wananchi waweze kujua wajibu wao na waishi kwa ulinzi, amani na utulivu. Nashukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Niishukuru Serikali kwa mpango wake wa kujenga mahakama kule Mbulu, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbulu iko ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 30 na kwa kuwa barabara hiyo ya kwenda Haydom iko kwenye mpango wa kutangazwa tender kwa kiwango cha lami. Je, Serikali ni lini itakuja kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ili kuondoa kadhia hii ambayo itasababisha huduma kusimama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia na ninajibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali tunatambua changamoto ya ulinzi au changamoto ya ukosefu wa Kituo cha Polisi hilo eneo ambalo Mheshimiwa amelitaja, lakini kikubwa nimuambie kwamba moja ya miongoni mwa kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inawapelekea wananchi huduma za ulinzi na usalama. Nimhakikishie mbele ya Bunge lako hili kupitia Wizara yetu, Kituo cha Polisi Mbulu kitafika na wananchi wataendelea ku- enjoy ama kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa vile sasa Kituo cha Geita sasa kitakuwa kinahudumia mkoa mzima, nami ninachojua ni kwamba pale Geita hata gari la zimamoto halipo: Je, ni lini Geita itapata gari la Zimamoto ili iweze kuhudumia mkoa mzima kutoka kwenye center moja ya Geita? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa vile kutoka Geita ni mbali na Katoro, ni lini sasa Kituo cha Polisi cha Geita kitapewa gari la Polisi ili liweze kuwahudumia wananchi wakati wakisubiri huduma ya gari la zimamoto kutoka Geita ili mali zao zisiporwe wala kuharibika baada ya moto kutokea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Geita kuna jumla ya magari manne ya zimamoto. Magari haya ni mazima na yanafanya kazi katika mkoa huo. Kwa bahati nzuri, pia sasa Serikali imeshafikiria kupeleka gari la zimamoto katika mji mdogo wa Katoro. Kitu cha msingi ambacho namwomba Mheshimiwa Mbunge, aendelee kustahimili kidogo, Serikali tumo mbioni kupeleka gari la zimamoto katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba wakati wao wanaendelea kustahimili, zipo njia mbadala ambazo tunazitumia kuhakikisha kwamba itakapotokea majanga hasa ya moto na mengine, wananchi hawa wanaweza kupata msaada wa haraka. Hivi karibuni tulifunga mkataba ama makubaliano na wale skauti, kwamba watusaidie kuendelea kutoa taaluma, washirikiane na Jeshi la Zimamoto ili kuhakikisha kwamba taaluma inaenea na majanga yanapotokea wanaweza kupata msaada wa haraka. Sisi kama Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto pia tunaendelea kutoa taaluma. Kikubwa ambacho tumesisitiza hasa kwa Jeshi la Zimamoto, waweze kuwahi kwenye matukio kwa haraka panapotokea majanga haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa, ni lini sasa tutapata gari la Polisi ambalo litakwenda angalau kuweza kutoa huduma? Katika Mji Mdogo wa Katoro, Kituo cha Polisi cha Katoro tayari gari la Polisi lipo, ipo gari ya One Ten, ambayo inatumika, sema tu, kwa kweli gari ni ya muda mrefu, limechakaa. Tunachowapongeza Jeshi la Polisi, Geita wameshaomba magari katika Jeshi la Polisi ili waweze kupelekewa magari hayo yaweze kuwasaidia katika harakati mbalimbali za ku-serve maisha ya jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimjibu maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kumetengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Je, Mheshimiwa Naibu Spika uko tayari kuambatana ili twende ukajionee katika eneo hilo mwenyewe kwa macho yako hali halisi ya kusaidia kuhamasisha wananchi wako wa Mkoa wa Kusini Unguja, ili na wao wajue kwamba, wewe Naibu wao unafanya kazi vizuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi, kukwama kwa kituo hiki kulikuwa kunasababishwa na upungufu wa fedha ambao sasa unatokana na ufinyu wa bajeti. Je, naulizwa, katika bajeti hii tumeingiza hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie kwamba, katika bajeti hii haikuingizwa, lakini nimuahidi tu kwamba, katika bajeti ijayo tutajitahidi hii Ofisi ya OCD Wilaya ya Kusini Unguja na ofisi nyingine na maeneo mengine ambayo yana uhitaji wa vituo hivi tutajitahidi tuhakikishe kwamba, tunapeleka au tunaendeleza ujenzi. Hasa ule ujenzi ambao umekwama wa vituo vya polisi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali jingine je, nipo tayari kuambatananaye mama yangu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie. Kwa ridhaa kabisa niko tayari kuambata na Mheshimiwa Mbunge tuende huko tukaangalie hilo eneo. Na itakuwa vizuri kwa sababu, tukifika huko tutawakusanya wananchi…

MBUNGE FULANI: Sio wewe.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …lakini
pia tutakaa na wadau ili kuhakikisha kwamba, tunawashajihisha kujenga kituo hiki, ili wananchi wa maeneo hayo, hasa maeneo ya Makunduchi, Kizimkazi, Mtende, Bwejuu, Paje na Jambiani na maeneo ya karibu waweze kupata huduma za ulinzi na usalama kama wanavyopata wananchi wengine. Nakushukuru.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Kisaki ambacho kiko Morogoro Vijijini kwa umuhimu wake kina matatizo ya usafiri. Je, ni lini kitapewa usafiri angalau pikipiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nikiri kwamba, bado tuna changamoto ya usafiri hasa katika maeneo ya vituo vya polisi, ikiwemo pikipiki na gari na aina nyingine za usafiri. Sasa nimwambie tu Mheshimiwa kwamba, aendelee kuvuta subira, Serikali kama Serikali tumo mbioni kuhakikisha kwamba, vituo vya polisi na maeneo mengine ambayo yanatoa huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi tunahakikisha tunapeleka hivyo vyombo vya usafiri, ili sasa wananchi waweze kupata hizo huduma kama inavyotakiwa. Nakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la Mkoa wa Kusini Unguja ni sawasawa na suala la Mkoa wa Kaskazini Unguja. Je, ofisi iliyokuweko Mkokotoni itamalizika lini? Maana huu mwaka wa tano unakwenda wa sita, bado kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ofisi ile ipo kwa muda mrefu na ujenzi wake ulikwama hapa katikati, lakini nimhakikishie tu kwamba, Mheshimiwa Mbunge ukarabati na kuendelea kumalizika ujenzi wa jengo lile sasa hivi umo mbioni. Na kama atakuwa ameanza kupita kwa muda huu anaweza akayaona mabadiliko ya ujenzi ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe wananchi, hasa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, jambo lao tayari lipo na linatekelezwa na muda si mrefu sana wataanza kutumia kituo kile na wataendelea kupata huduma za ulinzi na usalama katika maeneo yale, hasa ya Mkokotoni, maeneo ya Donge, maeneo ya Mkwajuni na maeneo mengine ya Mkoa wa Kaskazini Unguja. Ninakushukuru.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana; na mimi kwa niaba ya wananchi wa Biharamuro ningependa niongezee swali la nyongeza. Wilaya ya Biharamuro ni miongoni mwa wilaya kongwe kabisa za nchi hii lakini ukiingia katika mazingira ya polisi wa Biharamuro wanapoishi, bado wanaishi kwenye nyumba zilizojengwa na Mkoloni pale. Lakini mazingira ya kazi ni magumu wote mnajua kumekuwa na majambazi kule lakini vijana wale wanajitahidi kupambana nao usiku na mchana na hali yetu ni shwari kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maswali niliyonayo ni mawili, ni lini tutajengewa kituo kipya cha Polisi, ikizingatiwa tayari hati iko pale na kiwanja kipo tayari? Lakini pili…

NAIBU SPIKA: Moja tu Mheshimiwa; moja tu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ruhusa yako, nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kukiri tena kwamba bado tuna changamoto hasa kwenye usafiri, makazi na Vituo vya Polisi. Kwa kuwa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tayari wana hati ambayo inawamilikisha wao waweze kujengewa eneo zuri waweze kupata jengo zuri ambalo litatoa huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi, nimwambie tu kwamba aendelee kustahimili na mimi nalichukua hili tunakwenda kulifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba katika eneo lake wanapata kituo kikubwa kizuri na cha kisasa ambacho kitaendelea kutoa huduma kwa wananchi na wananchi wakaendelea ku-enjoy hiyo huduma ya ulinzi na usalama katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Je, ni lini nyumba za Askari wa Wilaya ya Kusini zitafanyiwa marekebisho kwasababu hali yake ni mbaya sana? Inafikia hatua kwamba baada ya kupigiliwa misumari hizo nyumba zimewekewa vipande vya matofali na mawe; kwa katika kipindi hiki cha mvua ni hali ngumu sana za wale askari. Je lini nyumba hizo zitafanyiwa marekebisho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ravia Idarus Faina Mbunge wa Jimbo la Makunduchi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sikuwa na uhakika sana kama kuna nyumba zimewekwa mawe badala ya kuwekwa bati; lakini kubwa niseme kwamba hata katika bajeti ambayo tuliyonayo mwaka huu tayari ujenzi wa nyumba hizi umezungumzwa na hatua za ujenzi wa nyumba hizi upo mbioni. Na si nyumba hizi tu tayari tuna mpango wa kujenga kituo kikubwa cha Polisi katika Mkoa wa Kusini na nyumba za kukaa maaskari katika Mkoa wa Kusini. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa Mbunge tuendelee kustahimili kidogo. Najua hili linamgusa na linamuuma kwasababu anawaona askari wanavyopata tabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini binafsi nafahamu hili kwasababu huo Mkoa ni wa kwangu. Niseme tu kwamba ninalichukua hili tunakwenda kulifanyia kazi na nyumba za kukaa askari polisi Wilaya ya Kusini hasa Makunduchi zitapatikana Inshallah.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yametolewa, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa sababu ni muda mrefu sasa toka marehemu alipofariki na hadi leo hajapata na alikuwa ni mtendaji wa Jeshi la Polisi. Je, ni lini sasa Serikali itawapatia mafao yao hawa wahusika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; naamini changamoto hii haiko kwa hawa tu, iko kwa watu wengi. Sasa je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Tanzania ambao wana matatizo kama haya juu ya kutatua tatizo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Jimbo la Chwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, je ni lini warithi wa marehemu watapata urithi wao. Baada ya kukaa na kupekua, kwanza tumegundua kwamba kweli marehemu alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la Polisi, lakini changamoto kubwa ambayo tulifika tukakutana nayo, tulifika wakati tukakosa kujua ni nani anayesimamia mirathi ya marehemu. Sasa hii kwa kweli kwetu ikaja ikawa ni changamoto. Kwa kuwa tayari msimamizi wa mirathi hii tumeshampata, kikubwa tumwahidi tu Mheshimiwa Mbunge, tutashirikiana tuhakikishe kwamba mirathi au mafao haya yanapatikana kwa wale ambao wanasimamia mirathi hii.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie binafsi niko tayari kwenda kukutana na huyo msimamizi wa mirathi na wengine wanaohusika na mirathi hii ili tuone namna ambavyo tunahakikisha watu hawa wanapata mafao yao au mirathi yao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, lakini je ni nini sasa kauli ya Serikali katika suala hili au tuna mpango gani? Kikubwa ambacho nataka nimwambie Mheshimiwa cha mwanzo linapojitokeza jambo kama hili kwa wananchi wengine basi cha kwanza kabisa wateue au wafanye uchaguzi wa kuteua msimamizi wa mirathi, kwa sababu sisi la mwanzo tukutane na msimamizi. Yeye ndiye atakayesimamia na kutupa taarifa zote zinazohusika.

La pili, tuhakikishe kwamba wanawasilisha vielelezo kwa sababu hatutaweza kujua nini shida yake kama hakuna vielelezo vilivyowasilishwa vikiwemo vya taarifa ya kifo, vikiwemo labda kituo ambacho alikuwa akifanyia kazi, mkoa na kadhalika. Hivyo ni vitu ambavyo vitatusaidia sisi katika kuhakikisha kwamba anapata mirathi yake kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kingine wakati wanawasilisha hivyo vielelezo viende kwa watu husika. Wengine huwa wanawapa tu kwa sababu jirani yake ni askari atampa nipekee. Sasa pengine sio mhusika, matokeo yake sasa lawama zinakuja kwenye Serikali, Wizara au kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho nataka niseme, ufuatiliaji wa mara kwa mara, kwa sababu na sisi tutakuwa tunalifuatilia lakini na wao sasa wawe wanalifuatilia kuhakikisha kwamba hii mirathi inapatikana kwa wakati. Nakushukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kwenda eneo lenyewe la mgogoro ili aweze kujionea hali halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ikidhihirika kwamba katika utaratibu huo wa kugawa mipaka kuna makosa ambayo yatakuwa yamejitokeza wakati huo: Serikali iko tayari kuchukua hatua kwa wale ambao watakuwa wamekiuka taratibu za utoaji mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Kamamba ni: Je, nipo tayari kwenda katika eneo hilo ili nikajionee mwenyewe huo mgogoro? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya kipindi hiki cha Bunge la Bajeti nikipata nafasi ambayo itaniruhusu kuweza kwenda kwa sababu ni sehemu ya wajibu wangu kuyajua, kuyaona na kusikiliza changamoto za wananchi, nimhakikishie tu kwamba naenda kupanga ratiba na nitajitahidi nimjulishe tuweko pamoja ili kwa kushirikiana na maafisa kutoka hiyo Idara ya Wakimbizi, tuone namna ambavyo tunaenda kutatua hiyo changamoto ambayo kwa sasa wananchi inawakabili. Kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba, nipo tayari kufuatana naye kwenda katika eneo.

Mheshimiwa Spika, swali lingine ni: Je, ikidhihirika kama kuna makosa kuna watu wamefanya mambo mengine, mengine, Serikali ipo tayari kuchukua hatua? Serikali ipo kwa ajili ya kuwatetea, kuwasemea na kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi. Tumegundua kuna baadhi ya mambo yanafanywa na baadhi ya maafisa au baadhi ya watu ambayo yanavunja utaratibu na sheria katika maeneo haya. Kama Serikali tuko tayari kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wengine wawe ni funzo na wasiendelee kufanya makosa hayo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakimbizi hawa tuliamua kuwapokea kwa sababu ya Mkataba wa Kimataifa ambao tuliukubali sisi wenyewe, kwamba ikitokea machafuko katika nchi fulani, basi kama wakija na tuki-prove kwamba kweli kuna tatizo, sisi tunawapokea.

Mheshimiwa Spika, pia tulikubaliana kwamba migogoro ikimalizika katika maeneo yao, sisi tupo tayari kuwarejesha katika maeneo yao kwa kushirikiana na mashirika na kwa kushirikiana na nchi zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu kwamba eneo hili ikitokea wakimbizi hawa wameondoka na ikawa hakuna machafuko, maana yake ni kwamba eneo hili tutalirejesha kwa Serikali, halafu Serikali itaona namna ya kufanya. Unless ikitokea fujo nyingine huko kwenye nchi za wenzetu ikawafanya wakimbizi waje, tutawapokea na kuwahifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JAFAR SANYA JUSSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atafanya ziara kuvitembelea vituo hivyo vya Jambiani na Paje na nyumba za askari wa Jeshi la Polisi Makunduchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali italipatia Jeshi la Polisi, Wilaya ya Kusini gari kwa ajili ya doria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sanya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Sanya. Hakika amekuwa anafanya kazi kubwa sana ya kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Paje hasa wa maeneo ya Jambiani, Paje, Bwejuu, Makunduchi, Kizimkazi, Mtende na maeneo mengine ya jirani ili kuhakikisha kwamba wanapata kwa utulivu na uhakika huduma za usalama na ulinzi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie tu ndani ya Bunge hili tumeshapanga na Mheshimiwa Sanya twende tukakabidhi mabati kwa ajili ya kuezeka Kituo cha Paje na fedha hizi zitatoka ndani ya mfuko wake. Kwa hiyo nimpongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sanya. Kwanza anauliza je, niko tayari kwenda kuangalia maeneo hayo? Nimejibu tu kwamba niko tayari na nimuahidi tu kwamba ndani ya Bunge hili la Bajeti tutapanga siku tuchupe mara moja twende tukakague, tukayaone hayo maeneo. Tukazione hizo hali na changamoto, halafu tujue namna ya kuzitafutia ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini je, tuko tayari kutoa gari? Nimwambie tu kwamba awe na Subira, katika bajeti ijayo tutajitahidi Vituo vya Paje na Jambiani, Wilaya wa Kusini Unguja tuvizingatie zaidi katika kuhakikisha kwamba wanapata gari kwa ajili ya kufanya doria za ulinzi na usalama katika Jimbo lake. Nashukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya miundombinu inayoikabili Jeshi la Polisi nchini inaikabili sana Wilaya ya Mbulu. Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Mbulu kilijengwa mara baada ya uhuru, kwa sasa kina uchakavu mkubwa. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili la uchakavu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Mbulu na makazi ya askari katika Wilaya yetu ya Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kama Serikali na Wizara ni kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama wa nchi unaenea kila mahali. Hilo la kujenga vituo vya polisi na kuvipatia magari, yote ni sehemu ya jukumu na wajibu wetu. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge, awe na subira kidogo kwa sababu kasungura bado kadogo lakini kakija kakichononoka kidogo, basi hilo ni jambo ambalo linawezekana na tukipata fedha ya kutosha, basi tutampelekea kituo cha polisi na huduma nyingine za polisi katika Jimbo lake. Nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile tokea mwaka 2012 hadi leo hii ni miaka tisa imepita na idadi ya askari polisi imeendelea kupungua kutokana na askari wengi kustaafu katika maeneo ya Zanzibar.

Vilevile kuongeza kwa vitendo vya uhalifu katika baadhi ya maeneo, je, Mheshimiwa Waziri au Serikali haioni haja ya kuajiri askari zaidi katika maeneo ya Zanzibar na hasa mashambani ili kuweza kuziba hilo pengo kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, kwa vile askari jamii katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, wamekuwa ni msaada mkubwa na tayari kuna good practices katika baadhi ya maeneo. Je, Serikali haioni haja ya kuweza kupanua wigo wa askari jamii kwa kuwapatia mafunzo na motisha, ili kuweza kufanya kazi na kuweza kusaidia kupunguza vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Zanzibar? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya uajiri kuna mambo lazima tuyaangalie. La kwanza, lazima tuhakikishe kwamba, tumepata kibali cha kufanya uajiri kitu ambacho nataka nimuambie Mheshimiwa Mbunge, tumeshakifanya na tumo mbioni kuhakikisha kwamba, tunapata ruhusa ya kufanya uajiri.

Mheshimiwa Spika, lingine ili tuweze kufanya uajiri maana yake lazima tuhakikishe kwamba tuna bajeti ya kutosha kwasababu tukisha waajiri lazima tuwalipe. Sasa kikubwa ambacho nataka nitoe wito hapa leo kwa Waheshimiwa Wabunge, hasa Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali na Waheshimiwa Wabunge leo tukijaaliwa hapa tunaenda kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, tunaomba bajeti hii tuipitishe kwasababu, ndani ya bajeti hii imezungumzwa taarifa za ajira za vijana hasa kwenye jeshi la polisi. Kwa hiyo, nawaomba tupitishe hii bajeti ili sasa tuweze kufanya hizo harakati za uajiri.

Mheshimiwa Spika, nimeulizwa pia suala kuhusu namna bora ya kuweza kuwaboresha askari jamii. Nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi tunavyozungumza tayari Kamishna anayeshughulika na masuala ya askari jamii na ulinzi shirikishi Zanzibar kwanza, anachokifanya ni kutoa mafunzo kwa masheha na kamati za ulinzi na usalama za shehia na vijiji, ili lengo na madhumuni ni kuona namna bora ya kuweza kuwashirikisha wananchi katika kupata ulinzi. Lakini tayari kuna mfumo mzuri, mwongozo mzuri ambao umeshatolewa umeshaanza kutumika Unguja na Pemba soon inshalah utaanza kutumika. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ni Wilaya ambayo iko mbali sana na makao makuu ya Mkoa ambako ni Lindi. Na pale Liwale hakuna kituo cha polisi kwa maana ya jengo hawana kabisaa, wanaishi kwenye nyumba ambayo ilipangwa na benki mpaka leo hii. Lakini, mwenyewe ni muhanga katika hili, mwaka huu mimi nimechomewa nyumba mbili na magari matatu wakati wa uchaguzi. Kimechangiwa sana na uhaba wa askari polisi na hatuna msaada wa karibu kutoka Liwale mpaka Nachingwea ni zaidi ya kilomita 120 mpaka Lindi zaidi ya kilomita 300. Sasa, je, Serikali ina mkakati gani kwanza, kutuongezea polisi Wilaya ya Liwale ikiwepo pamoja na majengo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza niko tayari kama ambavyo umenishauri kwenda kutembea Liwale, bahati mbaya kidogo sijafika Liwale. Lakini najitahidi katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti tunaweza tukatenga siku moja tukaenda Liwale kwenda kuangalia hiyo hali, halafu tutarudi tuje tuone sasa namna ya kufanya tathmini kuona namna ya kuweza kusaidia.

Mheshimiwa Spika, lakini, suala hili la uhaba wa askari mimi nadhani tuje pale pale, tuhakikishe kwamba tunaipitisha bajeti yetu, bajeti ambayo imezungumza suala zima la uajiri wa polisi, vijana hawa wa polisi, ili tuweze kuajiri. Tukikwamisha hii maana yake tutakuwa hatuna namna ya kufanya. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; kwa kuwa katika majibu yake ya msingi ameeleza wazi kwamba, Zimamoto huwa wanahusika sana katika kutuliza moto huo endapo majanga yanatokea. Hata hivyo, sio siri mara nyingi Jeshi hilo likifika linakuta magari hayana maji au wamechelewa sasa swali langu kwa Serikali, imejipangaje kuimarisha Jeshi hilo la Zimamoto ili wawe more efficient? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mioto hiyo ipo katika maeneo yetu tunayoishi au vijijini au kwenye kata zetu au mitaa yetu, lakini wananchi hao nikiweko mimi hatujapatiwa mafunzo ya kutosha kwenye kuzima mioto mikubwa kama hiyo. Wengi ni waathirika wa maeneo hayo na sitaki kurudi nyuma kukumbusha vilio vya Shauritanga na mashule mengine ambayo sitaki kutaja ikaja kuharibu sifa za shule hizo kupata wanafunzi. Je. Serikali itatoa lini mafunzo na kwa msisitizo kabisa ili watu hawa wapate elimu ya kusaidia kuzima mioto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nachukua fursa hii kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza, je, ni nini sasa Serikali inafanya au hatua ambazo inazichukua katika kuhakikisha kwamba inapunguza haya majanga ya moto ambayo yanajitokeza mara kwa mara? Ziko hatua nyingi ambazo kama Serikali tumezichukua ili kuona namna ambavyo tunapunguza, hatuwezi kuondosha moja kwa moja kwa sababu, mengine yanakuja, lakini tunapunguza. La kwanza, ni kuendelea kutoa elimu ama kuendelea kutoa taaluma kwa jamii, kwa sababu tunaamini jamii ikipata taaluma ama ikishiba taaluma ya kutosha majanga haya yatapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunaendeleza ukaguzi wa majengo. Yapo majengo lazima tuyakague kwanza, yako majengo ya binafsi, yako majengo ya Serikali na yako majengo mengine. Kwa hiyo, tunakuwa tunafanya ukaguzi wa kwenye majengo ili kuona namna ambavyo tunawaelimisha namna ya kujikinga na haya majanga ya moto. Kikubwa zaidi tunao mpango na tumeshaanza, wa kuongeza visima vya dharura kitaalam tunaviita fire hydrants ili ikitokezea taharuki kama ya moto tuwe tuna maeneo ya kuweza kuchota maji na kuweza kuokoa maisha ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba Je. taaluma huko vijijini inafikaje? Tunavyo vitu vingi ambavyo tumeviandaa ambavyo vinaendelea kutoa taaluma, tunazo zile fire clubs ambazo ziko huko vijijini kwenye kata kwenye vijiji, kwenye shehia ambazo zinaendeleza kutoa taaluma kwa watu. Pia hivi karibuni nimewahi kusema sana tu, hivi karibuni tulifanya makubaliano na watu wale wa skauti ambao wengi wao ni wanafunzi na wako vijijini huko ambao wanafanya kazi kubwa ya kuendelea kutoa taaluma na kuelimisha jamii namna bora ya kujikinga na haya majanga. Vile vile kuelimisha jamii namna bora ya kutoa taarifa mapema kwa sababu changamoto inakuja kwenye utoaji wa taarifa. Nakushukuru sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza; kwanza nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nataka kujua namna ambavyo Wizara ya Mambo ya Ndani inashirikiana na Wizara ya TAMISEMI wenye shule kuhakikisha kwamba matukio haya sasa yanakoma kwa sababu, yamekuwa yakisumbua mara kwa mara katika shule zetu hasa za mabweni. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunao ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na TAMISEMI na hata hawa watu wa Wizara ya Elimu katika kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi kubwa ya majanga ya moto na majanga mengine hasa katika maeneo ya shule na maeneo mengine. Tayari tumeshakuwa tunakaa vikao mbalimbali, tumeshapanga mipango mbalimbali ambayo ni mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza haya majanga.

Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa asiwe na wasiwasi juhudi zinaendelea kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba tunapunguza haya majanga kwa kiasi kikubwa. Nakushukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Lakini, hata hivyo ningependa kujua kuna mfano gani kwa waganga hao wa ramli chonganishi na manabii wa uongo hatua ambazo wamechukuliwa baada ya kupatikana na kadhia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa wale manabii ambao wanadai wanao uwezo wa kuwafufua waliokufa ili kukaa nao kwa karibu ili kuweza kuwafufua wapendwa wetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza je ni mfano gani wowote ambao uliowahi kuchukuliwa hatua wa hawa waganga matapeli na Manabii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Khalifa atarejea kwenye jibu langu la msingi ni kwamba mpaka kufika kipindi cha mwaka 2020 jumla ya kesi 57 za waganga chonganishi na wengine tayari zimesharipotiwa kwasababu ili kesi iwe kesi kwanza iwe reported. Kwa hiyo, kikubwa nimwambie kwamba zipo kesi ambazo zimeshafika kwenye ofisi yetu au zimeshafika Mahakamani, tayari zimo katika mchakato wa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nimwambie kwamba hili jambo ni jambo amablo linahitaji utulivu wa kukaa tukafanya utafiti na takwimu za kutosha ili tukilileta hapa tuliseme kwa mujibu wa uhalisia lilivyo. Kikubwa ni kwamba zipo kesi ambazo zimeshakuwa reported. Kuna kesi ilijitokeza Mkoa wa Njombe, yupo kijana aliambiwa na babu yake ili uwe Tajiri na huo utajiri tupate mimi na wewe basi lazima uwe unawaua watoto mpaka wafike idadi fulani. Mwisho wa siku ile kesi ikaripotiwa na tukamshtaki huyo mtu kwa kosa la mauaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kesi imejitokeza Misungwi huko ya mtu mmoja aliambiwa na mganga hivyo hivyo tapeli ili mimi na wewe tuwe matajiri hakikisha unawaua wanawake halafu unatembea nao. Lengo na madhumuni tuwe matajiri. Hii kesi imeletwa na tumeichukulia hatua kwa hivyo. Kikubwa niseme kwamba hizi kesi zipo kwa zile ambazo zimeripotiwa na hatua za kisheria kwa mujibu wa taratibu zinachukuliwa na majibu yatapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali jingine lilikuwa linauliza je, hakuna haja ya kukaa sasa na hawa wafufuaji ili tuweze kuwafufua wapendwa wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, imani ya kibinadamu inaamini na ndivyo ilivyo kwamba mwenye uwezo wa kuondosha na kurejesha, yaani kufanya mtu akaondoka, akafa ni Mwenyezi Mungu peke yake. Ndiyo maana ilifika wakati tukawa tunasema kwamba kama kutakuwa kuna watu wa namna hii kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge, tuko tayari kukaa nao tuwaeleweshe, tuwafahamishe ili wafike wakati wasije wakazua migogoro katika jamii. Kwasababu anaweza akatokezea mtu akasema mimi nina uwezo wa kufufua, akachukua pesa za watu. Mwisho mtu akazikwa akafa akasahauliwa. Mwisho wa siku migogoro katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa nimwambie tuko tayari kukaa na hao watu ili tujue namna ya kuwaelimisha kuwaeleza kwamba mwenye uwezo wa kufufua na kuondosha mtu kwa maana ya kufa ni Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa usalama ni jambo muhimu sana kwenye jamii yetu, je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia magofu ambayo yamejengwa na wananchi hususan maeneo ya pembezoni mwa miji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kutokana na changamoto ya kiusalama hasa maeneo ya pembezoni mwa miji je, Serikali imeandaa utaratibu gani au ina mpango gani wa kupeleka magari ya doria hasa nyakati za usiku kwenye maeneo ambayo hayana vituo vya polisi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza sasa maboma?

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inawapelekea wananchi huduma ya ulinzi na usalama karibu ya maeneo yao. Hiyo ni sehemu ya wajibu kabisa. Lakini na wananchi nao wanafika wakati wanakuwa wanao wajibu kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali kusaidia sasa kuona namna ambavyo nao wanajisaidia kujikaribishia hizo huduma kwa kushirikiana na Serikali. Kikubwa tu nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Tutajitahidi katika bajeti ijayo tutakapopanga mipango yetu basi tutajitahidi katika maeneo haya ya pembezoni hasa katika mkoa huu basi baadhi ya maeneo hayo tuyape kipaumbele ili tuone namna bora ambayo wananchi wanaweza wakafikishiwa hizo huduma kama ambavyo maeneo mengine yanafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini je, kutokana na changamoto hii Serikali sasa ina mpango gani katika kupeleka magari haya kwa ajili ya kufanya doria. Mpango upo, kama ambavyo tumefanya katika mikoa na wilaya na vituo vingine na maeneo mengine na hapa katika maeneo hayo ambayo Mheshimiwa ameyakusudia au ameyataja tunao mpango wa kupeleka magari hayo kufanya doria ili sasa wananchi na wao waweze kupata huduma hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho tumekifanya huko, tayari tuna mfumo au tuna utaratibu wa ulinzi shirikishi ambao askari polisi/Jeshi la Polisi wanashirikiana na raia/ jamii katika kuhakikisha kwamba maeneo ya wananchi yanapata huduma ya ulinzi kama maeneo mengine. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, atulie awe na Subira. Mambo mazuri yanakuja maana kazi inaendelea.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Wilaya ya Ngara ina changamoto ya uhaba wa askari na Wilaya hii inapakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari wakutosha ili wananchi waweze kulindwa na mali zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, tuna mpango gani sasa wa kupeleka askari ama ulinzi katika maeneo ambayo ameyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, narejea tena kusema kwamba wajibu na jukumu la Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapata huduma ya ulinzi na usalama ili wananchi waishi kwa amani. Ikiwa pana watu wageni, ndani ya Tanzania hii lakini wajibu wetu ni kupeleka. Nimtoe hofu, asiwe na wasiwasi, maeneo hayo kwa kuwa amehisi kwamba yana upungufu wa ulinzi, tunayachukua na tunapeleka ulinzi ili wananchi na wao waweze kuishi kwa amani na wapate huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuongeza maswali mawili ya ziada. Swali langu la kwanza, nataka nijue kwa kuwa, suala la ubakaji na ulawiti na unyanyasaji kwa watoto haliko Tanzania pekee, lipo katika nchi mbalimbali. Nilitaka kujua Serikali inashirikiana na mashirika gani, ili kuhakikisha suala hili linakomeshwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa, kuna maafisa wa madawati katika maeneo kadhaa, ili kusaidia kupambana na masuala ya ulawiti, ubakaji na unyanyasaji kwa watoto, nilitaka kujua wanawawezeshaje maafisa wale, ili waepukane na rushwa, lakini pia waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, anataka kujua ni mashirika gani ya kimataifa au mashirika gani ambayo tunashirikiananayo katika kupambana na jambo hili. Kwa kweli, niseme tu kwamba, yapo mashirika mengi ambayo tunashirikiananayo. Yapo ya ndani na nje ya nchi ambayo tunashirikiananayo katika kupambana dhidi ya matukio haya ya uhalifu, hasa ya udalilishaji wa kijinsia. Kwa upande wan je huko tuna mashirika kwa mfano ya UNICEF, kuna shirika La WHO (World Health Organization), tuna UN Women, tuna USAID, tuna Save the Children, hapa tuna akina taasisi zile zinazoshughulikia masuala ya kisheria. Kwa hiyo, kwa ufupi tuna taasisi nyingi ambazo tunashirikiana nazo katika kuhakikisha kwamba, tunapambana dhidi ya haya matukio ya udhalilishaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu vipi tunawawezesha hawa maafisa wa madawati; maafisa wa madawati tuna mambo mengi. La kwanza tuna mfumo maalum ambao upo kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa matukio ya udhalilishaji, lakini pia tumekuwa tunawapa elimu ya kisheria, tunawapa elimu ya protections, tunawapa elimu ya kijamii. Elimu ambazo zinawasaidia wao kuweza kuchukua hatua pale tukio linapotokea, lakini zaidi tumeanzisha kwenye vituo pamoja na kwamba sio vyote, lakini vipo vituo ambavyo tumewawekea usafiri ambao huwa wanatumia kwa ajili ya kufuatilia hayo matukio mara tu yanapotokea. Nakushukuru.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, asante. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Njombe, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Serikali imesema kwamba, wanatafuta hizi fedha shilingi milioni 322. Ningependa kujua mkakati mzima wa upatikanaji wa hizi fedha na zitakuwepo kwenye bajeti ipi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; eneo ambalo wamepanga kujenga Ofisi ya Mkoa wa Njombe (Central Police), ni eneo hilohilo Ofisi ya Mkoa imepangwa kujengwa na Mahakama ya Mkoa; Ofisi ya Mkoa na Mahakama zimeshajengwa, sasa hii bado.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Njombe wangependa kujua ni lini hasa ofisi hii itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe, maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa anauliza; je, katika bajeti hii tumepanga kuweza kupata hizo fedha?

Mheshimiwa Spika, kubwa tu nimwambie kwamba katika bajeti hii hakuna fungu hili, lakini tutajitahidi katika bajeti ijayo pesa hizi ziwepo na tumuahidi Mheshimiwa kwamba, tutampa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba, eneo hili linapata kituo hicho cha polisi ambacho kitatoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini je, ni lini sasa Serikali italipa hiyo fidia? Nimwambie tu kwamba, tutajitahidi na tumuahidi mwaka ujao wa fedha tutajitahidi tulipe hiyo fidia, ili sasa ujenzi huu uweze kuanza haraka na wananchi waweze kupata huduma hizo za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni je, Serikali inatumia utaratibu gani wa kulipa madeni ya askari ambao unaendelea kwa kuwa wameanza kulipa 2018/2019 na wameacha 2017, lakini pia askari waliopandishwa vyeo kutoka Mainspekta kuwa Warakibu wa Polisi 99, askari 99 ambao walipanda mwaka 2013 mpaka 2017 hawajalipwa mshahara kwa cheo hicho wameanza kulipwa 2018? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali hili la Mheshimiwa Jesca kwamba suala hili ni suala ambalo linahitaji takwimu na linahitaji data za uhakika. Kwa hiyo, kubwa tu nimwambie Mheshimiwa kwamba pamoja na kwamba utaratibu umeshaanza kupangwa, lakini nimuombe tu kwamba, suala hili aendelee kulipa muda ili tukalifanyie kazi halafu tutajua namna ya kuja kumjibu, nakushukuru.
MHE. LAZARO J. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali inatarajia kupata fedha hizo lini ili wale wananchi waweze kulipwa fidia badala ya kuendelea kusubiri kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na umbali uliopo kati ya Makao Makuu ya Wilaya na Kituo cha Polisi ambacho kinatumika kama Makao Makuu ya Polisi, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha za OC ili ofisi ile ya Polisi ya Wilaya iweze kujiendesha bila karaha wala kuombaomba fedha kwa wadau wengine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameuliza, je, lini Serikali italipa fidia? Nataka nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inao mpango na italipa fidia wananchi hao kwa ajili ya eneo hilo kwa sababu inatambua umuhimu wa uwepo wa Kituo hicho cha Polisi ili wananchi waweze kupata huduma hizo. Kubwa zaidi tayari tumeshatoa maelekezo na wameshafanya tathmini wataalam kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Kilolo inayohitajika kwa ajili ya fidia hiyo na tayari tumeshaelekeza pa kwenda kupata fedha hizo kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hao. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kufanya juhudi kuona namna bora ya kuwalipa fidia wananchi hao. Kubwa Mheshimiwa Mbunge aendelee kuzungumza na wananchi wake ili waendelee kuwa na subra jambo hilo limo mbioni kushughulikiwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anauliza kama Serikali ipo tayari kuongeza OC. Niseme tu kwamba Serikali ipo tayari kuongeza OC lakini ni pale ambapo tutakuwa na fedha ya kutosha kufanya hivyo. Kwa hiyo, kwa sasa waendelee kuwa na subra hivyo hivyo tubananebanane lakini tunao mpango huo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo upo mbadala ambao tumeshauchukua, kwanza tumeongeza operesheni ama doria za mara kwa mara katika maeneo ambayo wananchi wako mbali na vituo vya polisi ili waweze kupata hizo huduma za ulinzi. Vilevile tunaendelea kusisitiza ulinzi shirikishi ambapo inasaidia huduma za ulinzi kufika mpaka maeneo ya vijijini kwenye kata. Lengo na madhumuni ni wananchi waendelee kupata huduma za ulinzi na waishi kwa amani.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba posho ya shilingi 100,000 ambayo ilikuwa inatolewa kwa ajili ya kuwawezesha askari wetu waweze kukidhi haja ya kuweza kujenga, tukiangalia kwa mtazamo ni kwamba posho hiyo ilikuwa ni ndogo na hata askari wakipewa miaka 100 hawawezi kufanya ujenzi kwa posho hiyo.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwawezesha askari wetu kuwaongezea posho hii ili iendane na utaratibu wa kuweza kujenga kwa askari wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili; je, sasa Serikali haioni kwamba kuna haja kwa Wizara kuhakikisha kuona kwamba pamoja na kwamba askari wetu wanaintelijensia ya hali ya juu, hatuoni sasa kwamba kuna haja sasa ya ule utaratibu wa mwanzo kuweza kutumika ili kwamba askari wetu tuweze kuwaweke katika mazingira mazuri waweze kulinda nchi hii, raia pamoja na mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari ama ina utaratibu gani sasa wa kuongeza hii posho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo dhamira kwa sababu kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba vyombo vyetu vya ulinzi hasa Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri na kwa kweli tunayo kila sababu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuendelea kufanya kazi vizuri, katika hili tunawapongeza sana. Kikubwa ni kwamba utaratibu wa kuongeza hizi posho upo, tumeshaupanga/tumeshaufikiria maana hata katika bajeti ambayo tuliiwasilisha juzi tulilizungumza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa awe na stahamala kwa sababu hii mipango inahitaji fedha na tupo mbioni kuhakikisha kwamba tunatafuta hizo fedha ili tuweze kuwaongezea kwa sababu hatuwezi tukasema kwamba kesho tutawaongezea, kwa hiyo, kesho watazipata lakini the way ambavyo kasungura ketu kananenepa ndivyo ambavyo tutakapokuwa tunawaongezea na wao hii posho ili sasa waendelee kufanya kazi nzuri zaidi ya kulinda raia na mali zao. Kwa hiyo, hiyo nia ya kuwaongezea posho ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, hakuna haja ya kurejesha ule utaratibu wa mwanzo, mimi nadhani Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tuende tukakae na wenzetu tukalifikirie hili, tukapange halafu tutaona sasa namna bora ya kuboresha haya mambo ili sasa kuweza kurejesha ule utaratibu wa mwanzo ambao kama yeye Mheshimiwa Mbunge ameuzungumzia. Nakushukuru. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Khamis, lakini nataka nikubaliane na muuliza swali la msingi Mheshimiwa Lambert pamoja na maswali yake ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni kweli tunakubaliana kwamba vijana hawa askari polisi wanafanya kazi nzuri kwa nchi na Taifa lao na pengine wanafanya hivyo katika mazingira magumu na wengine kulingana na vyeo vyao ni vigumu sana kujikomboa na kupata hata maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lililosemwa katika swali la msingi ni kama je, Serikali haioni haja ya kuwapatia vijana hawa viwanja kwa bei nafuu? Nataka niseme sisi kama Wizara tunalichukua hili, tutajadiliana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone uwezekano huo kwa sababu ni jambo jema kabisa na wengine kweli wanamaliza/wanastaafu wakiwa kwanza na umri mdogo kulingana na Kariba ya ajira yenyewe ya Jeshi la Polisi, mtu ana miaka 54 anastaafu, halafu hana hata nyumba wala kiwanja. Nataka nikubaliane kwamba acha tulifanyie kazi, tuone kwa mfumo ambao uliopo kama tunaweza tukawapatia vijana hawa angalau viwanja, angalau kwa wale wa vyeo fulani fulani ambao unajua wapo kidogo underprivileged. Nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri, mmezungumzia upande wa viwanja nafikiri pia Serikali mtajipanga na hoja ya pili ya muuliza swali ameuliza mambo mawili; msamaha wa kodi katika vifaa vya ujenzi pamoja na viwanja kwa bei elekezi. Kwa hiyo, nafikiri…, karibu.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa na utaratibu wa duty free shops kwa ajili ya hawa askari. Maduka haya yalitumika na ukatokea ukiukwaji mkubwa sana wa taratibu za kikodi na kutokana na mazingira hayo mambo mengi mabaya yalitokea, Serikali ikaona bora kuondoa ile kwa sababu waliokuwa wananufaika ni watu fulani, fulani tu hata walengwa pengine walikuwa hawanufaiki, tukaona bora waingiziwe fedha zao na kwa utaratibu wa sasa wanalipwa shilingi 300,000 kila baada ya miezi mitatu, ni kitu fulani kuliko wengine ambao walikuwa vijijini huko hata duty free shops hizo hawazioni. Na utaratibu huo wa ku-institutionalize leo ni vigumu sana. Kwa hiyo, utaratibu wa fedha kuingizwa kwenye akaunti zao umekuwa ni bora na wanaufurahia sana. (Makofi)
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa eneo tayari lipo na kwa kuwa nafahamu kwamba kuna matofali ya kutosha katika Kambi ya Mfikiwa yaliyobaki kwa ajii ya ujenzi wa nyumba za Polisi Mfikiwa na mimi nikiwa mdau wa upatikanaji wa matofali hayo.

Je, ni lini Wizara itatupatia matofali hayo ili kwa kushirikiana na wananchi wangu wa Jimbo la Kiwani tuweze kuanza ujenzi wa kituo hicho?

Swali la pili, wananchi wa Shehia ya Kendwa kwa kushauriwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba walitakiwa waanzishe Jengo kwa ajili ya polisi jamii na wananchi hao kwa kutii walianzisha jengo hilo ambapo sasa lina miaka nane.

Je, ni lini Wizara italimaliza jengo hilo ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdalla, Mbunge wa Jimbo la Kiwani kutoka Kusini Pemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linazungumzia kuhusu matofali; ni kweli katika eneo lile la Mfikiwa yapo matofali na matofali yale jumla yake ni 32,000 na matofali yale yaliletwa pale kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari makazi ya askari pale Mfikiwa na siyo matofali tu, lakini yapo na mabati ipo na rangi. Lakini kwa bahati nzuri au bahati mbaya ikafika wakati kidogo tukapungukiwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huu.

Kwa hiyo, matofali haya nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hayapo tu kwamba maana yake kazi imekwisha, kazi ya ujenzi wa nyumba zile azma ya Serikali iko pale pale, kwa hiyo, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba aendelee kustahimili tupo mbioni tutahakikisha kwamba kwa kushirikiana yeye na wadau wengine werevu tupate matofali na vifaa vingine vya kutosha ili tukajenge Kituo cha Polisi hapo Kiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwambie tu kwamba azma ya Serikali ni kuendeleza kujenga nyumba hizi na nyumba hizi zipo katika hali ya kujengwa kwa sababu tayari ipo nyumba moja imeshaanza kujengwa na imeshafikia katika hatua ya lenta.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni lini sasa Serikali itamaliza boma lile la polisi jamii. Kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya katika Jimbo la Kiwani, kwa sababu amekuwa ni mdau mzuri ambaye anatusaidia Serikali hasa katika masuala ya ulinzi na usalama, hiki kituo ambacho kinazungumzwa cha polisi jamii amesaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba anasaidia wananchi kuweza kupata huduma hizi. Kwa hiyo kikubwa nimwambie tu kwamba tutajitahidi katika mwaka ujao wa fedha tuweke hilo fungu kwa ajili ya kumsaidia kumalizia hili boma ama hiki kituo ambacho kimeshaanza cha askari jamii katika Shehia hii ya Kendwa. Nakushukuru.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa naangalia kwenye jibu la msingi linaonesha kwamba huko Kiwani mpaka sasa hivi hakuna eneo lililotengwa; wakati huo huo kuna mahali kuna matofali yamewekwa na ujenzi umefika mahali. Sasa hebu fafanua kidogo, haya matofali yako wapi ili nijue swali la nyongeza la Mbunge linaendana na hili jibu la msingi au hapana?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali aliloliuliza kwamba kule Kusini Pemba kuna eneo la tuseme ni Kambi ya Askari Polisi panaitwa Mfikiwa, pale Mfikiwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi iliamua ijenge nyumba za makazi ya askari polisi yaani Mfikiwa na huko Jimboni kwake ni mbali kidogo.

Kwa hiyo, kilichokuja kuamuliwa kwamba kuna matofali yale yeye ameona kwamba yako kwa muda mrefu yamekaa, kwa hiyo, anaona kwanini Serikali yale matofali yasichukuliwe yakapelekwa Kiwani ili wananchi wa Shehia za Jombwe, Kendwa, Muwambe, Mchake, Mtangani, Kiwani wajengewe kituo kile cha polisi sasa yale matofali azma ya Serikali ilikuwa ni kujenga nyumba za askari na kila kitu kipo tulipungukiwa kidogo na fedha ndicho ambacho anataka apelekewe yale matofali tukamwambia kwamba tutamfanyia maarifa tumpelekee matofali mengine.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kituo cha polisi cha Itaka ambacho kinahudumia kata zaidi ya tano ikiwepo kata ya Nambizo pamoja na Halungu kinakabiliwa na changamoto kubwa sana kwanza jengo lake limechakaa, lakini pili hakuna pia vitendea kazi lakini kama haitoshi kituo kile cha polisi kina polisi wanne tu. Naomba kufahamu Serikali imejipanga vipi katika kukabiliana na hiyo changamoto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo; Serikali tunafahamu na tunatambua changamoto iliyoko katika Jeshi la Polisi na tunafahamu kwamba bado kuna vituo vimechakaa, tunafahamu kwamba tuna changamoto ya vitendea kazi, lakini pia tunafahamu kwamba tuna baadhi ya upungufu wa watumishi katika Jeshi. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa aendelee kutustahimilia kwa sababu hatua za kuhakikisha kwamba tunachanganua ama tunatatua hii changamoto ama hizi changamoto tumeshazianza zikiwemo za uajiri, za upatikanaji wa vitendea kazi na za kurekebisha majengo yaliyochakaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kubwa nimuombe tu Mheshimiwa aendelee kustahimili sisi kama Serikali kama Wizara tupo mbioni kuhakikisha kwamba watengenezea mazingira mazuri wananchi kwa ajili ya kupata huduma nzuri za ulinzi na usalama.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; kama ilivyo vituo vingi vya polisi vilivyochakaa, Kituo cha Matangatuwani kilichoko katika Jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kimechakaa na kwa kweli ni kibovu, ikinyesha mvua ni bora ukae chini ya mwembe utapata stara kuliko Kituo cha Matangatuwani.

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati mkubwa kituo hiki cha Matangotuwani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Khalifa amekuwa ni mdau wetu muhimu wa kutusaidia kwanza kutuonesha maeneo ambayo tunatakiwa sisi kama Serikali tuyafanyie marekebisho, lakini pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba anatoa hata kilicho mfukoni kwake au katika Mfuko wa Jimbo kuhakikisha kwamba anawasaidia wananchi katika kupata huduma za ulinzi na usalama, hili nimpongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa nimwambie kwamba nirejee tena kwamba bado tunatambua kwamba kuna baadhi ya changamoto ambayo sisi ni sehemu ya wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunazitatua ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma nzuri za kiulinzi na usalama. Kituo ambacho anakizungumza ni kweli kipo na mimi binafsi nimefika na hali nimeiona, lakini kikubwa nimwambie hata kama akinifaa kwenye bajeti ambayo tumeiwasilisha tumeisoma hivi karibuni tumezungumzia namna ambavyo tunaenda kurekebisha vituo vya polisi na nyumba na baadhi ya huduma nyingine ili sasa wananchi waweze kupata huduma bora za kiulinzi na usalama. Nimwambie tu kwamba na yeye ni miongoni mwa vituo ambavyo tutajitahidi turekebishe ili tuone namna ambavyo na wao wanapata huduma nzuri. Nakushukuru.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi; Kituo cha Polisi Nanyamba kilijengwa huko nyuma kwa ajili ya kuhudumia Tarafa ya Nanyamba lakini sasa hivi Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ni Makao Makuu ya Halmashauri hiyo mpya na kuna ongezeko la watu na kituo hicho kimechoka na keshokutwa nitakabidhi bati 70 kwa ajili ya kukarabati.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga jitihada zetu kufanya ukarabati mkubwa wa kujenga Kituo kipya cha Polisi Nanyamba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Chikota kama ifuatavyo:-

Kwanza nimpongeze sana kwa juhudi ambazo anazifanya za kutusaidia na ninajua anafanya haya kwa sababu aliwaahidi wananchi kwamba atawatumikia na atawasaidia kuhakikisha kwamba wanapata huduma bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, azma ya kutoa mabati na vingine ambavyo utahakikisha kwamba wananchi wanahitaji aendelee kufanya hivyo na sisi tuko pamoja na yeye.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu kwamba zipo jitihada ambazo sisi kama Serikali kama Jeshi la Polisi tuna mpango wa kufanya si kituo hiki tu cha alichokitaja, lakini na vituo vingine. Kwa hiyo, kikubwa tumwambie kwamba tutaangalia na bajeti itakavyoturuhusu, lakini tumwahidi kwamba moja ya miongoni mwa maeneo ambayo tutayapa kipaumbele kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kituo bora na kukifanyia marekebisho ni katika kituo chake cha Nanyamba. Nakushukuru.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; ili askari wangu pale Iringa wapate utulivu na kuimarisha ndoa zao na familia wanahitaji makazi bora. Je, ni lini Serikali sasa itatujengea makazi bora ya askari katika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana na yeye kwa juhudi kubwa ambayo anatusaidia katika kuhakikisha kwamba anawasaidia wananchi, lakini kikubwa nimuahidi kwamba katika mwaka wa fedha ujao tutajitahidi na tutahakikisha kwamba hili eneo ambalo yeye amelizungumza tulipe kipaumbele ili tu wananchi wa eneo hilo waweze kupata na wao huduma za ulinzi na usalama bila ya tatizo lolote, nakushukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa vigezo vinavyowakwamisha vijana wetu wa Kitanzania hususan waliopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ikiwemo Mikoa ya Katavi, Kigoma na mingineyo ni pamoja na ucheleweshwaji na upatikanaji wa namba za NIDA.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutokutumia kigezo hiki wakati vijana wanapokuwa wanatumia ajira ili kuwawezesha vijana wetu waweze kupata ajira kwa kuwa mchakato huo bado haujakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; ni kwanini sasa mfumo wa NIDA usiunganishwe na mfumo wa RITA wa vyeti vya kuzaliwa ili kuwawezesha Watanzania pale tu mtoto anapozaliwa aweze kupata cheti kimoja kinachounganisha kuonyesha kwamba huyu ni raia kwa kuzaliwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa kwa kuwa umefika wakati ameona umuhimu wa wananchi hasa wa mkoa wake kufanyiwa haraka katika kupata vitambulisho huku akiwa anajua kwamba vitambulisho kwa sasa NIDA ndiyo kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba sasa nianze kujibu swali la kwanza, kwamba, je, Serikali sasa haioni haja ya kuondosha hiki kigezo cha NIDA ili sasa mambo mengine yaweze kuenda yakiwemo ya vijana kuweza kupata ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tumeamua kuweka kigezo hiki ili kuweza kuwajua ni nani wenye sifa na nani wasiokuwa na sifa; na tumeamua kukiweka kigezo hiki ili kuona kwamba nani ambao wana Utanzania na nani ambao hawana Utanzania. Sasa kwa kusema moja kwa moja kigezo hiki kukitoa basi ni jambo ambalo linahitaji procedure, twende tukakae na watu wa utumishi na taasisi nyingine. Nimwambie tu Mheshimiwa kwamba jambo hili tunalichukua na tutakwenda kuona namna ya kulifikiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kikubwa kingine ninachotaka niseme ni kwamba, na hapa nataka nitoe agizo lakini pia nitoe wito kwa mamlaka hii inayosimamia; kwamba kwa sasa tuone namna ya kuwapa zaidi kipaumbele vijana ambao wanakwenda kutafuta ajira ili waweze kupatiwa hivi vitambulisho kwasababu tumeona na tumegundua kwamba kweli hii imekuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na yote hayo nichukue fursa hii niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba bado kuna wilaya vitambulisho vipo wenyewe hawajaenda kuvichukua, sasa matokeo yake tunaendelea kupata lawama. Tunataka tutoe wito tuwaambie Waheshimiwa Wabunge kwa kushirikiana na viongozi wengine huko wa Chama na Serikali muwaambie watu waende wakachukue vitambulisho vyao. Yapo maeneo vitambulisho vipo lakini hawajaenda kuvichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba, kwanini sasa tusiunganishe RITA na NIDA. Lengo na azma ya Serikali siku zote ni kuhakikisha kwamba wanatengeneza muunganiko wa mfumo ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi. Sasa kuunganisha RITA na NIDA si tatizo, Serikali ipo tayari kuunganisha mifumo lakini kuziunganisha taasisi nadhani ni jambo ambalo tunahitaji tukae sasa tufikirie tuone namna bora ya kuziunganisha hizi. Ni kweli zote ni taasisi za Serikali lakini zinao utofauti katika muundo na katika majukumu yake. Kwa hiyo nalo hili pia tutalichukua tuone namna ambavyo tunaweza tukaenda tukasaidia wananchi. Nakushukuru.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ajali inapotokea wamiliki wa vyombo vya moto hupewa mara moja bima yao wanapokwenda kudai chombo kama imeharibika, lakini hawa waathirika ambao ni abiria wanaopata ajali wamepoteza maisha au viungo wamekuwa wakisumbuliwa sana na hawa bima.

Je, nini kauli ya Serikali kutokana na usumbufu mkubwa sana wanaopata abiria wanaopata ajali barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa abiria wengi sana wanaotumia vyombo vya moto wanapopata ajali wanakuwa hawana uelewa wa kutosha na mara nyingi sana sasa hivi tumetumia electronic ticketing yaani kule nyuma hakuna elimu yoyote.

Je, sasa Serikali haioni ni wakati sasa wa kuhakikisha kwamba katika vituo vya kusubiria abiria kuwepo na mabango na matangazo ili kutoa elimu ya kutosha kwa abiria wanapopata ajali nini wafanye? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Iringa.

Kwanza nataka nichukue fursa hii nimpongeze sana kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Mkoa wake. Mheshimiwa Ritta amefika hatua ya kukarabati Kituo cha Polisi na ujenzi wa kumalizia Kituo cha Polisi katika Kata ya Semtema. Hakika amefanya kazi kubwa, kwa hili nampongeza sana lakini na wengine pia watusaidie kufanya hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe kujibu maswali mawili. Inapotokea ajali ni kweli mmiliki wa chombo anapata fidia kama amejiunga ama amejihusisha na bima, lakini je vipi kuhusu sasa hawa abiria. Ni kweli hii ni changamoto na bado kuna changamoto nyingine kwa upande wa wananchi. Hapo nataka niwaambie kitu kwamba changamoto ya kwanza wanapopata ajali wanakuwa hawajui namna bora ya uandishi wa barua za kuombea zile fidia zao, kitu ambacho mwisho wa siku kinakuja kuwafanya wao aidha kuchelewa au kukosa kabisa kuweza kupata zile fidia kutoka bima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kwa kweli ipo kwenye upelelezi kwamba wale watu wa bima hawawezi kutoa zile fedha za fidia unless mpaka wahakikishe kwamba wamepata attachment ya upelelezi kutoka Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, hapo nataka nitoe wito pia kwa Jeshi la Polisi kwamba wahakikishe wanafanya haraka kupeleka ripoti za upelelezi kwa hawa wananchi ambao wanapata ajali ili sasa waweze kupata fidia zao kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kikubwa zaidi uelewa mdogo wa hii taaluma ya bima. Hapa natala nitoe agizo kwa Jeshi la Polisi, kwamba pamoja na kazi nzuri ya utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna bora ya utumiaji wa barabara, lakini suala la elimu hii ya bima ya kuweza kupata mafao iendelee na kazi ifanyike vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine alikuwa anauliza je, sasa tuna mpango gani wa kuweka haya mabango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabango yapo, kazi imeanza na inaendelea, lakini kingine tunaendeleza taaluma ambazo kupitia mabango, vyombo vya habari, vijiwe vya bodaboda, shule pamoja na kupitia kila mahala; tunawaelewesha watu namna bora ya kutumia barabara na kuepuka na ajali. Kikubwa zaidi tumeshaweka ishara na alama za barabarani ambazo pia zinasaidia watu kuweza kujua namna ya kuepuka hizi ajali za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza nashukuru majibu ya Serikali kwa kufuatia maswali yangu haya; lakini swali langu la kwanza katika maswali yangu ya nyongeza kwamba kama kwa mujibu wa majibu aliyonipa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba inakiri kwamba Mamlaka ya kule Zanzibar pia inayo sheria yake ambayo inatambua hizi sheria za faini za papo kwa papo; je, ni kwa nini Jeshi la Polisi sasa limeshindwa kusimamia sheria hizi za papo kwa papo pale barabarani kwa kutumia hizi mashine za EFD? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba ni lini sasa Wizara ya Mambo ya Ndani itakaa na mamlaka husika za kule Zanzibar ili kuona Jeshi la Polisi zinaanza kutumia mashine hizi na ukizingatia kwamba itapunguza malalamiko ya wananchi na itapunguza masuala ya rushwa lakini pia itapunguza zile ajali ambazo zitaweza kuepukika? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, naomba ama napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Malindi Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, je, kwa nini Jeshi la polisi limeshindwa? Jeshi la polisi halijashindwa kusimamia taratibu, kanuni na sheria za usalama barabarani katika hili suala la kutumia mashine hizi hapa kuja jambo kidogo, Zanzibar kuna mamlaka inaitwa Mamlaka ya Usafirishaji au Mamlaka ya Usalama Barabarani ambayo ina sheria yake sheria namba saba na Bara kuna Baraza la Taifa la kusimamia usalama barabarani ambalo nalo lina sheria yake kama tulivyoeleza, lakini kama hilo halitoshi mamlaka hivi zote zina utaratibu wake na kanuni zake ambazo zinasimamia pamoja na kwamba Jeshi la Polisi ndio muhimili mkubwa ambao unasimamia mamlaka hizi.

Kwa hiyo, haijashindwa kusimamia tatizo lililokuwepo ni changamoto ya sheria kwamba hawa wanasheria yao, wana kanuni yao, hawa wana mamlaka yao pamoja na kwamba Jeshi la polisi ndio hilo. Kwa hiyo jeshi la polisi halijashindwa kusimamia sheria hii.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; je, ni lini sasa Serikali hasa kule Zanzibar itaruhusu matumizi ya hizi mashine? Nimwambie tu kwamba kwa kuwa sheria ipo na mamlaka inayosimamia usalama barabarani ipo na sheria yake ipo kikubwa ni kwamba sasa hivi tupo katika harakati za kukamilisha kanuni itakayokuja kusimamia sheria hizi ili sasa hii sheria ya kutumia hizo mashine kwa ajili ya kukinga hizo ajali na mambo mengine zianze kutumika.

Mheshimiwa Spika, kubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo sana ili tumalize hizo kanuni na sheria zianze kutumika kote kote.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, kituo hiki kina miaka 13 hakijamalizika, je, Waziri atakuwa tayari kuongozana nami kwenda kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa uhalifu umeongezeka katika Jimbo la Mwanakwerekwe, sasa hivi kuna vibaka na waporaji wengi lakini hata miundombinu ya Serikali nayo imekuwa ikiharibiwa kwa makusudi.

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na kadhia hii wanayoipata wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu rafiki yangu Mheshimiwa Kassim niko tayari kuambatana naye kwenda katika kituo kile na kukiona. Nimuambie kwamba kituo kile nakifahamu na kipo kwa muda mrefu ni kweli, lakini niko tayari kuambatana naye kwenda kukiangalia kituo kile na kuona namna ambavyo tunaweza tukawasaidia wananchi ili kuimarishiwa hizi huduma za ulinzi na usalaama katika eneo lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lingine ni kuhusu vitendo hivi vya uhalifu ambapo vijana wanafanya vitendo vikiwemo vya uvunjifu wa miundombinu na uharibifu wa vitu vingine. Ndani ya jimbo lake kuna kituo kingine kikubwa cha Mwanakwerekwe na hicho kinafanya kazi muda wote, hasa kupitia kituo hiki tutajitahidi tuwe tunafanya doria za mara kwa mara ili kuweza kuwakamata na kuwashughulikia wale wote ambao wanavunja amani ama wanafanya vitendo vya uhalifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine tuko tayari kuendeleza na kuimarisha ulinzi shirikishi ili wananchi na wao waweze kutoa mchango wao katika kulinda amani ya wengine. Kikubwa, tuko tayari kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wale wote ambao watakuwa wanafanya vitendo hivi. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Wilaya ya Momba makao yake makuu yako ndani ya Halmashauri ya Momba, je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha polisi ambacho kina hadhi ya wilaya ili kiweze kusaidia kuepusha changamoto na uovu wote ambao unaoendelea ndani ya Jimbo la Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapatiwa huduma za ulinzi na usalama kupitia kila chombo ambacho wananchi watakuwa wanahitaji. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba awe na Subira, tutajitahidi sana tuhakikishe kwamba ndani ya jimbo hilo au ndani ya eneo hilo ambalo limekosa hicho kituo cha polisi basi tuone namna ya kuweza kupata fedha ili tukawatengenezee wananchi kituo cha polisi waweze kupata huduma za ulinzi. Nakushukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Chumbuni lina matatizo ambayo yanafanana na Jimbo la Mwanakwerekwe ambalo swali la msingi limeulizwa. Nimekuwa nikiuliza kwa miaka mitano kuhusu Kituo chetu cha Chumbuni ambacho kinahudumia karibu wilaya nzima ya pale mjini, shehia zaidi ya sita, tangu kilikuwa kinafunguliwa asubuhi kinafungwa saa kumi na mbili sasa hivi kimefungwa kabisa. Je, ni lini na sisi tutapata kituo cha polisi kwa sababu kinahudumia zaidi ya shehia sita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza, Mbunge wa wawanachi wa Jimbo la Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna baadhi ya vituo tulivifunga kwa sababu nyingi sana. Kuna vituo vingine vilifungwa kwa sababu kubwa tulikuwa na upungufu hasa wa rasilimali watu, kwa maana ya polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa kwa kuwa sasa Jeshi la Polisi tumeshatangaza kuajiri askari wapya tutahakikisha kwamba kituo kile tutakifungua na tutapeleka askari ili wananchi waweze kupata huduma za ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na yanaleta faida kwa Watanzania. Hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uvamizi katika vituo vya Polisi siyo jambo jema, lakini nashukuru Jeshi la Polisi wameweza kudhibiti, lakini suala kama hilo huenda likajirudia. Swali langu linasema hivi: Je, ikitokea wamevamiwa katika vituo vyao na kwa bahati mbaya askari kajeruhiwa au askari kauliwa; familia ile inayomtegemea yule askari ambapo ndio tegemeo lao kimaisha, Serikali inawaambia nini au itawasaidia nini ili waweze kuishi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wanapovamia vituo, lengo kuu ni kupata zile silaha na kuwaathiri Polisi wenyewe walioko kituoni. Je, wakati wanapozungumza au wakati taarifa tunapozipata, baadhi yao wanazipata silaha; wanapokuwa wamezipata zinakuwa katika hali gani? Katika hali ya ubora ule ule wa awali au tayari zimebadilishwa ili wasiweze kuzitambua? Ni hayo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bi. Fakharia, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa Mjini Zanzibar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeweka utaratibu maalumu wa askari wake watakapopata mitihani katika harakati za kulinda amani na utulivu wa nchi hii, lakini ni ikiwa imethibitika kwamba mtihani huo umemkuta ama ameupata akiwa katika harakati za kazi zake za kawaida za kiaskari. Kwa hiyo, kuna kanuni ya fidia ya pamoja ya Jeshi la Polisi na Magereza, hiyo hutumika. Katika kanuni hiyo imeelezwa viwango ambavyo huwa mtu anafidiwa kutokana na tatizo lililomkuta; kuna viwango akipata ulemavu, kuna viwango akikatika, na kuna viwango akifa. Kwa hiyo, Serikali kupitia Jeshi, imeweka utaratibu maalumu kupitia hii kanuni ambayo inawapa watu nafasi ya kuweza kupata fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine kwamba je, Silaha hizi tunakuwa tumezipata zikiwa zimeharibika au vipi? Silaha hizi zitakavyokuwa, zikiwa zimeharibika, zikiwa nzima, wajibu wetu tukizipata katika matukio ya kihalifu, maana yake ni kuzichukua. Kama itakuwa zimeharibika, maana yake tuna utaratibu wa kuzitengeneza. Ikiwa hazijaharibika, tunaiangalia; kama silaha ile ina kesi, tunaiacha kesi ile iendelee, ikimalizika, silaha ile inarudi Serikalini, inarudi jeshini, tunaendelea kuitumia kwa ajili ya Ulinzi na Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, hali ya kufunga mpaka huu kwa muda mrefu imesababisha mkwamo mkubwa wa kiuchumi kwa wananchi katika eneo hili.

Je, hivi Serikali haioni sababu ya kufungua mpaka huu kusudi wananchi wanufaike na zile fursa zilizoko katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kama ataangalia zaidi katika jibu langu la msingi nimesema kwamba, ufunguaji wa kituo hiki unategemea zaidi makubaliano ya nchi mbili baada ya kukaa na kuangalia namna ya kuweza kufungua kituo hiki kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi. Nimesema Serikali inaendelea kufuatilia hali hii ili kuona namna bora ya kuweza kukaa na jirani zetu, ili kuweza kuwafungulia.

Mheshimiwa Spika, kikubwa afahamu tu kwamba, lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma katika mpaka huu katika hatua za uingiaji na utokaji na hali ya ulinzi na usalama inaendelea. Hivi tunavyozungumza vipo vikosi vyetu ambavyo vinaweka amani na utulivu katika eneo hilo na huduma nyingine zinapatikana. Ninakushukuru.
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, NIDA walikuwa na mashine mbili za kuzalishia vitambulisho. Wakaomba kuongeza tena na mashine mbili kwa ajili ya kuzalisha vitambulisho vya Taifa. Sasa je, ni kwa nini uzalishaji na usambazaji wa vitambulisho hivyo umepungua kwa kiasi kikubwa sana na je, hawaoni wametumia fedha za wananchi vibaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Radhia Idarus Faina, Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinazalisha vitambulisho vichache kwa muda mrefu, lakini tukaomba fedha kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukanunua mashine nyingine mbili na mashine hizi zikawa zinazalisha vitambulisho hivi kwa haraka kama ambavyo tofauti na mara ya mwanzo.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyokwambia shughuli za usajili, utambuzi na utoaji wa vitambulisho hivi unaendelea mpaka ilipofika tarehe 12 Oktoba, tulishakuwa na vitambulisho karibu 10,000,000 ambavyo viko tayari na muda wowote vinategemewa kwenda kusambazwa kwa wananchi. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba mashine hizi zinafanya kazi na vitambulisho vitapelekwa kwa wananchi hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia fedha vibaya, hakuna fedha iliyoingia katika akaunti ya NIDA, aidha kwa Serikali au kutoka kwa wafadhili ikatumiwa vibaya. Hivyo nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, fedha zote zilizoingia kwenye akaunti ya NIDA zimetumika accordingly. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Njombe mpaka miaka michache iliyopita ulionekana kama ni mkoa mpya. Katika maeneo yaliyosahaulika kwa Mkoa wa Njombe ni Vituo vya Polisi. Je, Serikali ni lini sasa itaanza kukarabati Kituo cha Polisi cha Mkoa wa Njombe ili kiendane na hadhi ya Mkoa wa Njombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo ameliuliza, linalozungumzia suala la ukarabati wa Kituo cha Polisi Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba azma yetu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vinajengwa ipo pale pale. Lakini kikubwa nimwambie tu kwamba tutajitahidi pia katika mwaka wa fedha ujao tuhakikishe kwamba kituo hiki nacho tunakijenga kikawa katika hadhi ile ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kupata huduma hizi za ulinzi na usalama. Nakushukuru pia.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, jengo la Kituo cha Polisi katika Mji Mdogo wa Mlowo ambapo mpaka sasa hivi tayari kimeishawekewa alama ya X kwa sababu kimejengwa kwenye hifadhi ya barabara.

Nilikuwa naomba kufahamu nini mkakati wa Serikali wa kutujengea Kituo kipya cha Polisi pale Mlowo na ikizingatiwa kwamba tayari tunalo eneo ambalo limetengwa pale Forest maalum kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja miongoni mwa changamoto ambazo tuko nazo ni kwamba vituo vingi vipo maeneo ya barabara na wakati Serikali inataka kutanua ama kupanua miundombinu ya barabara inabidi lazima kuna vituo vipitishwe doza kwa ajili ya kuvunjwa ili sasa barabara itengenezwe. Sasa nimwambie tu Mheshimiwa kwamba kwa kuwa eneo lipo, basi tutajitahidi tutenge fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru pia.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza. Kwanza, nishukuru Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mama Samia Suluhu Hassan jinsi anavyo chapa kazi mwanamama, kweli kinamama tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri na Serikali yake inatambua uchakavu huu wa majengo ya polisi ya Makunduchi pamoja na makazi na wametenga jumla ya shilingi milioni kumi na moja na tisini na tatu mia nne, ambazo fedha hizi zinatakiwa ziende zikafanye ukarabati katika majengo haya na vituo vya polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vituo hivi vimechakaa sana, binafsi ukizingatia Makunduchi ni sehemu ya utalii hususan kila mwaka tunakwenda kule kukoga mwaka na viongozi wetu wakubwa wakubwa wanakwenda kule Makunduchi.

Kwa hiyo, je, Serikali lini itakwenda kuyatengeza majengo haya ili tuondoe kadhia hii ya majengo haya machakavu?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala langu la pili, namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri tena nasema tena, Mheshimiwa Naibu Waziri aende mwenye Makunduchi akayaone jinsi yale majengo pamoja na zile nyumba zilivyochakaa. Tuoneeni huruma jamani, tunaona vibaya? Ahsante sana naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NAMBO YA NDANIYA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu masuala mawili mazuri sana ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, Mwantumu Dau Haji nayajibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja miongoni mwa azma kubwa ya Serikali hasa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba inaboresha na inatengeneza vituo vyote vya polisi vilivyopo nchini pamoja na nyumba za makaazi za maafisa hawa wa polisi na familia zao. Kwa hiyo, kubwa ni mwambie tu Kituo cha Makunduchi ni moja miongoni mwa kituo ambacho tumeshakipanga na tayari fedha hizi tumo mbioni kuzitafuta na kupitia mwaka wa fedha ujao tutahakikisha kwamba kituo hiki tunakipa kipaumbele ili kijengwe na shughuli za kitalii na mambo mengine yaweze kuendelea vizuri na shughuli za ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo pia, nipo tayari kwenda Makunduchi kwenda kuona hilo eneo ili kuona namna ambavyo tunaweza tukashauri na tukaweza kupata fedha kwa ajili ya kukarabati hicho kituo. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuku kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ningependa kujua kituo cha polisi Mgeta ambacho niliahidiwa kujengwa na niliambiwa nilete tathmini ya ujenzi wa kituo hicho ambacho wananchi wamejenga, tumefikia kwenye boma. Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Naibu mwenye waliniahidi kwamba ikifika mwezi Agosti, 2021 kitakuwa kimeshamalizika kujengwa. Ni lini sasa watakwenda kumaliza hiyo ahadi yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Getere nalo nalijibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tulifika wakati tukaona kwamba tunaweza tukapata fedha haraka kwa ajili ya ujenzi wa kituo kile, lakini mambo yaliingiliana kwa sababu tuna nyumba za maaskari, tuna vituo vya polisi, tuna mambo mengi ambayo polisi tunahitaji tuimarishe ili wananchi waweze kupata huduma hizo. Kubwa nimwambie tu kwamba katika mwaka wa fedha ujao tutajitahidi kituo kile tukiangalie, tutakipa kipaumbele ili wananchi waweze kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Kishapu na wadau wa maendeleo katika Wilaya ya Kishapu wameanzisha jengo kwa maana ya Ofisi ya OCD ya Wilaya ya Kishapu na jumla ya shilingi milioni 60 zimetumika na jengo hilo lipo hatua ya renter. Sasa je, Seikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba ina-suport nguvu za wananchi na wadau ili mradi huduma za kipolisi ziweze kwenda sawasawa katika Wilaya ya Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniface nalo naomba nilijibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana kwa kuwa ni moja ya miongoni mwa watu ambao wanahamasisha sana wananchi ili kuweza kuanza ile miradi halafu Serikali kwa kupitia wafadhili tuje tuone namna ambavyo tunaweza tukamalizia. Kikubwa nimwambie kwanza, tutajitahidi baada ya Bunge hili tuje tuone hatua hiyo ambayo imefikia hicho kituo ili sasa tuone na sisi tathmini ya kuweza kujenga.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumwambie kwamba sasa tunakwenda kutafuta fedha, popote zilipo ili tuhakikishe kwamba kituo hiki tunakimaliza na wananchi waweze kupata hizo huduma katika maeneo hayo. Nakushukuru.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, hii habari ya vituo hayo yote tisa lakini kumi kuna Kituo Chukwani kimejengwa kwa nguvu za wananchi na kisha pauliwa tayari. Sasa ni ipi commitment ya Serikali ili kuja kumaliza kituo kile ambacho kinahitaji milioni 30 tu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge na Mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli ni kwamba kituo hiki tunakifahamu na binafsi nimeshakwenda kufanya ziara kwenye kituo hiki na hiyo amount ya fedha iliyotajwa tunaifahamu, kikubwa tulimwambia Mheshimiwa Mbunge ambaye alitupeleka katika eneo lile, ilikuwa ni Mheshimiwa Shaha. Mheshimiwa Ahmada Shaha tulikwenda kuona, kikubwa tulichomwambia kwamba sasa tunakwenda kutafuta fedha kwa sababu kama unavyojua siyo jambo la kusema kwamba tunachukua tu kesho tunakwenda kujenga. Ni jambo ambalo linahitaji taratibu za upatikanaji wa fedha kwa hiyo kikubwa nimwambie tu kwamba kituo hicho tunakifahamu na sasa tunakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniruhusu niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, licha ya majibu mazuri yaliyotolewa na Wizara. Swali la kwanza; Jimbo la Vunjo ni jimbo lililo mpakani. Majimbo yaliyo mpakani yanakuwa na changamoto tofauti kidogo, kwa mfano, magendo na unajua Wachaga wanavyopenda magendo. Dawa za kulevya zinaingia halafu kunakuwa na uhamiaji haramu. Kwa hiyo, kuna umuhimu na tunaomba Serikali ituhakikishie kwamba, itachukua hatua gani ili kuimarisha ulinzi kwenye vituo vya polisi kwa kuongeza polisi pamoja na kuongeza bajeti kwa sababu, wanahitaji kuchukua za haraka wakati mambo kama yale yanapotokea?

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, kule Vunjo unywaji wa gongo, ulaji mirungi, bangi, dawa za kulevya umekithiri kwa sababu, of course watu hawana ajira wengi, lakini ukweli ni kwamba, imekithiri sana. Najua kwamba, Serikali za Mitaa zinafahamu jambo hili, lakini linahitaji national effort na tunataka tuombe Wizara iweze kutueleza inachukua mikakati gani ya kuweza kushughulikia tatizo hili la unywaji pombe kali, bangi na vitu vyote kama hivyo, otherwise tutapoteza kizazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt. Charles Stephen Kimei, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatutasubiri mpaka tufike sasa watu waanze kuandamana. Serikali kupitia Jeshi la Polisi tuna mikakati madhubuti ambayo tumeifanya na tunaendelea kuifanya. Ya mwanzo, ni kuhakikisha kwamba, tunafanya doria za mara kwa mara ili lengo na madhumuni kuweza kukamata na kukomesha hizo tabia pamoja na kwamba, zinakuwa na changamoto kidogo, lakini tutajitahidi katika kuhakikisha kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunaendeleza sasa suala zima la ulinzi shirikishi; lengo na madhumuni sasa jamii iweze kutumia fursa ya kuchukua nafasi ya kuelimisha vijana wao ili sasa vijana waweze kupunguza hii, lakini kikubwa zaidi tunachukua hatua za kisheria. Kwa hiyo, wale vijana ambao wanafanya hili, basi tutawachukulia hatua za kinidhamu, hatua za kisheria, ili vijana waweze kuachana na tabia au vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya na utumiaji wa hiyo gongo kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, nadhani maswali yalikuwa mawili, lakini yote yalikuwa yanaangalia kwenye gongo na bangi na masuala mengine. Nakushukuru sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Niseme nimepokea kwa furaha taarifa njema za magari 369 ya Polisi yatakayokuja. Swali langu. Je, katika magari hayo na ukizingatia kwamba, Kilimanjaro ina kata 169 na za mlimani ziko kama 110 zikiwemo kata za kule Siha, zikiwemo kata za Moshi Vijijini, Kata za Same, Kata za Mwanga na Kata za kule Rombo. Je, Serikali iko tayari sasa kupatia zile kata za mlimani ambazo haziko mjini magari hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, inasogezea wananchi huduma za ulinzi na usalama popote walipo. Moja miongoni mwa mambo ya msingi ambayo Serikali imeazimia kufanya kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunatengeneza vituo vya polisi, lakini pili kuwatafutia magari ya polisi ambayo yatakwenda kufanya doria katika maeneo mengi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, miongoni mwa maeneo ambayo yatafika haya magari tutajitahidi sana maeneo hayo ameyataja na huko kwenye mkoa wake magari haya yafike ili yaweze kutoa huduma. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, wananchi wengi wa maeneo ya pembezoni katika Jimbo la Kibamba, hasa maeneo ya Mpijimagohe kule Mbezi, Tegeta A kule Goba na maeneo ya Ukombozi kule Saranga, wameanza kujenga maboma ya vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wa maeneo yao. Je, Serikali ni lini sasa itakuwa tayari kukamilisha maboma yale ili wananchi wale wapate usalama katika maeneo wanayoishi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu tena swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mambo yote ambayo yanaelezwa au vitu vyote ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kufanyiwa wananchi kutoka katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, hasa kwenye Jeshi la Polisi, ni mambo ambayo yanahitaji fedha. Tukizungumza vituo vya polisi, fedha, tukizungumza magari, fedha, tukizungumza nyumba za askari, tunahitaji fedha. Nimwambie tu mheshimkiwa Mbunge kwamba, kwa sasa tunakwenda kutafuta fedha na tumeshaanza hiyo michakato ya utafutaji wa hizo pesa. Lengo na madhumuni ya kufanya hivyo ni ili tuweze kumaliza maboma yote nchini ambayo yanahitaji kumalizwa kuwawezesha wananchi kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wizi wa mazao ya kilimo na mifugo yamekuwa yakiongezeka pamoja na takwimu nzuri ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezieleza hapa. Je, ningependa Mheshimiwa Naibu Waziri alieleze Bunge lako Tukufu tuna-fail wapi?

Swali Namba Mbili, ningeomba vilevile kuuliza kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba. Je, hatuoni kwamba kuna haja ya kukinga haya matokeo ya wizi yasitokee ili kuwasaidia wananchi na wakulima wasiweze kupata hasara ya kuibiwa mazao yao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Soud Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Donge, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi wajibu wetu mkubwa ni kulinda raia na mali zao. Kwa hiyo katika hili tunajitahidi na tunafika hatua tunakuwa tunakutana na changamoto nyingi zikiwemo zile za wananchi wenyewe kwanza kushindwa kwenda kutoa ushahidi kwamba nani ameiba na nani amechukua mazao na nani amechukua mifugo. Lakini kikubwa ni kwamba tunaendeleza jitihada za kuhakikisha kwamba tunawakamata tunawafikisha kunako vyombo vya sheria hawa wanaohusika.

Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuzuia haya, tuna mikakati mingi ambayo kama atarejea kwenye jibu langu la msingi moja ni kuendeleza ule ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ambalo pia tumelifanya kama ni sehemu ya mkakati ni kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo haya hasa yale maeneo ya Zanzibar maeneo ya Donge, Muwanda na maeneo mengine ili lengo na madhumuni hivi vituko ama hivi vitendo vya uhalifu visiweze kutokea. Lakini kubwa nataka nitoe wito kwa wananchi wetu wasiendelee kuchukua hatua mikononi mwao, tumepata matukio mengi ya watu wanachinjwa, watu wanachomwa, watu wanachukuliwa hatua mikononi kitu ambacho ni kinyume na utaratibu wa sheria. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsate kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Momba ina Halmashauri mbili. Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Halmashauri ya Wilaya Momba. Makao Makuu yapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba sehemu ambayo ni mbali kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Katika hali ya usalama Tunduma ina hali hatarishi zaidi kuliko Wilaya ya Momba nilitamani kufahamu ni lini Serikali itaweka Wilaya mbili za kipolisi katika Wilaya ya Momba yaani Mji wa Tunduma pamoja na Halmashauri ya Momba. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu kwa kifupi sana swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, suala la uwekaji wa Vituo vya Polisi au uwekaji wa huduma hizi za ulinzi na usalama zinategemea mambo mengi sana, ukiwemo utaratibu wa kuangalia kwanza mahitaji ya eneo hilo, kwa sababu inawezekana kuna mahali vituo vipo karibu na huduma zipo karibu, lakini kikubwa ni kwamba nimwambie tutakwenda tukakague ili tuone kama tutaona kuna haja ya kufanya hivyo basi tutaweka. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nitauliza maswali pamoja na majibu hayo, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba amezungumiza suala la Kanuni za Magereza ambazo zinataka watoto watengwe tofauti na watu wazima wanapokuwepo Mahabusu. Mlundikano wa Mahabusu kwenye magereza zetu hauruhusu jambo hilo ni kwa nini sasa Serikali isiongeze au isipeleke Maafisa Ustawi wa Jamii ambao watakuwa wanashughulika na Watoto wanapokuwa kule kwa sababu ni vigumu sana ku-monitor. Kwa mfano, Gereza la Segerea kuna mahabusu si chini ya mia moja watoto na Maafisa wapo wawili tu ME na KE. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; kwa nini sasa Serikali isipitie upya kujua idadi ya watoto ambao wana kesi kwenye Mahakama zetu na kwenye Mahabusu zetu yaani kwa maana ya Magereza ili sasa ile sheria kwa jinsi ilivyowekwa na ni nzuri, lakini utekelezaji wake ni mgumu ni kwa nini sasa wasipitie upya ili kuhakikisha kwamba watoto hawa wanasaidiwa kwa sababu hali za watoto wetu kwenye Magereza zetu ni mbaya mno. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum, nayo nayajibu kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa atarejea kwenye jibu langu la msingi atagundua kwamba kuna sehemu nimesema kutakuwa kuna Maafisa wa Ustawi ambao watakuwepo maalum katika magereza kwa ajili ya kusimamia haki na maslahi na kuwalinda watoto hawa. Kwa hiyo, kama changamoto ni Maafisa hawa kuwa kidogo basi nimhakikishie tutajitahidi Serikali kupitia Jeshi la Magereza ili kuona kwamba tunaongeza Maafisa hawa ili watoto wetu waweze kupata huduma nzuri za kuweza kusaidiwa na Maafisa hawa pamoja na kwamba kuna nafasi nyingine ya kushughulikiwa na wazee wao na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa amegusia suala la kwa nini isipitiwe upya sheria au tuone namna, nimwambie kwamba sheria hii kwamba ipo vizuri, lakini kwa kuwa na yeye ameshauri tuipitie upya basi tutakaa tutaipitia sheria hii ili kama kutakuwa kuna mapungufu basi tutajua namna ya kuifanyia marekebisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge pia aliuliza umuhimu wa kujua idadi ya kesi za watoto. Kesi zote zinazokwenda Mahakamani zinasajiliwa kwa namba, kwa hiyo kama atauliza swali mahsusi kwa Mahakama maalumu au kwa Gereza maalum idadi hiyo itapatikana kwa namba na kwa majina ya wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili; Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaweka misingi ya kulinda maslahi ya mtoto. Kwa hiyo, kwa mtu aliyechini ya kizuizi cha magereza anapopelekwa mahakamani kama hapati huduma inayostahili akiwa magereza anayohaki ya kutoa hiyo hoja kwa Hakimu ambapo shauri hilo lipo mbele yake na maelezo ya kisheria kwenda kwa wanaosimamia hizo selo yakatolewa. Nninakushukuru. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali. Katika kulinda haki za watoto ni lazima au ni sharti tuzingatie wale watoto ambao unakuta hawana kesi, bali mama zao aidha wameenda wakiwa wajawazito au wamekamatwa ni mahabusu au mfungwa akiwa na mtoto ambaye yuko chini ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Spika, katika Gereza la Segerea tumeshuhudia wamama wanakuja na watoto wao pale wa jinsia tofauti, lakini wanachangamana na watu wazima. Kwa hiyo, unakuta mtu mzima labda anataka kwenda kuoga anavua nguo, yuko hivi na mtoto yuko pale. Tunajua kwamba makuzi ya watoto ubongo wao ni kuanzia miezi sifuri mpaka miaka mitano. Kwa hiyo, unakuta unam-affect kisaikolojia.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa, ni hatua gani Serikali inachukua kuhakikisha kwamba wale mahabusu au wafungwa ambao wamekwenda wakiwa wajawazito, wamejifungua wakiwa Magereza au wameenda na watoto wachanga, waweze kutengwa kwenye cell special ya akina mama wenye watoto au wajawazito wasiweze kuchangamana na hawa watu wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuna hatua nyingi ambazo huwa zinachukuliwa. Huo utaratibu upo na upo tangu zamani. Inawezekana tu labda kuna maeneo yeye ameyashuhudia, ameona kwamba watu wanachanganyika na wengine wanakuwa wanataka labda pengine… kama hivyo. Kikubwa nimwambie kwamba ziko hatua ambazo Serikali inazichukua ikiwemo ya kuwatenganisha ili sasa ikitokea hali kama hiyo, waweze kupatiwa msaada maalum. Ziko hatua nyingi tu ambazo tunazichukua kama Serikali na kama Jeshi la Magereza. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, majibu haya yaliyoletwa haya reflect kabisa hali halisi iliyoko Jimboni Ndanda na Kwenye Kijiji cha Namajani hasa zaidi kwenye Vijiji wa Ngalole, Namajani, Kijiji cha Pangani na Matutwe pamoja na Mahinga.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka swali hili nilileta kwa mara ya kwanza 2016 na majibu yaliyotolewa yanafanana na kesi hii wanakijiji hawa walishinda mahakamani mwaka 2012 na mara nyingi wizara wamekuwa wanajitetea kwa kusema kwamba wanafanya tathimini na wanatafuta pesa. Kwa mara ya mwisho wamefanya tathimini mwaka jana kabla hatujaingia kwenye bajeti kuu na hakuna pesa yoyote iliyotengwa na Serikali kwa nia ya kwenda kuwalipa kwa hiyo nina amini hawana nia njema sana ili kulimaliza jambo hili. Mgogoro uliopo sasa ni wa malipo.

Sasa swali langu kama Serikali au Magereza wameshindwa kulipa fedha hii hawaoni sasa kuna haja ya ku-vacate na kuondoka eneo hili wakawaachia wananchi wafanye shughuli zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana endapo Mheshimiwa Waziri sasa atoe commitment kwamba kufikia lini jambo hili litakuwa limekwisha na wananchi wale watakwenda kupata stahiki zao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe Mbunge Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka tu tuone namna ambavyo tunaweza tukaondoka hapa katika eneo hili, lakini nimwambie tu kwamba waliokuwepo hapa ni chombo cha Serikali ambacho kwa kusema tu tuondoke tu kirahisi rahisi nimwambie hili kwamba ni jema lakini inabidi sasa tukae tuone namna itakavyowezekana kwa sababu waliokuwepo hapa ni Jeshi na wanashughulikia wananchi na wanasaidia kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini Je, lini hili jambo litakwisha akisoma katika jibu langu la msingi ni kwamba Tayari tumeshaanza hatua kwanza za uhakiki kujua nani anastahili kulipwa na nani hastahili kulipwa zaidi ukizingatia kwamba mahakama amri hapa mahali sisi tuondoke. Kikubwa ni kwamba tunaenda kutafuta fedha kwa sababu hizi fedha siyo kidogo ili tuweze kuwa compensate hawa waliokuwepo basi tuone namna itakavyowezekana, nakushukuru.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunaunga mkono jitihada za Serikali. Hata hivyo, kuna wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kilimo cha mbogamboga ambazo zinawaingizia kipato, wako ndani ya mita 60; na shughuli zao hizo haziathiri mazingira.

Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao au kuwalinda ili wazidi kujiongezea kipato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa eneo hili linaweza likageuzwa kuwa vivutio au sehemu ambazo ni center ambazo wananchi wanaweza wakatengeneza, kama vile Coco Beach au sehemu nyingine, wakaweza kupata shughuli za kujiendeshea maisha yao.

Je, Serikali iko tayari kuwasiliana na Halmashauri zetu ili wananchi wetu ambao wanaweza kufanya shughuli hizi waweze kupewa maeneo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la mita 60 ni jambo la kikanuni kabisa. Lakini kingine tunaweza tukawaruhusu wakaendelea ndani ya mita 60; lakini changamoto iliyopo, athari za kimazingira si athari za kuonekana leo na kesho. Huwezi ukachimba mgodi leo, ukawa unachimba dhahabu au chochote ukaziona athari leo. Huwezi kukata miti ukaona athari leo, huwezi ukaendesha viwanda ukaona athari leo. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo na kesho inawezekana wananchi wa Segerea wanaweza wasione athari za kimazingira, lakini baada ya muda watakuja kuona athari za kimazingira. Hicho ndicho kitu ambacho sisi Serikali tunakihofia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni vipi tutawasaidia, tuko tayari kuwasaidia kwa kuendelea kuwapa taaluma ili sasa waweze kufahamu mambo haya ili wajue athari za kimazingira. Kwa sababu tusipoyalinda mazingira hayataweza kutulinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine kwamba je, Serikali iko tayari kuwatengenezea creation centers kwa ajli ya angala ya kuweza kujiendesha. Hilo jambo wala hatuna tatizo nalo kwa sababu lengo letu ni kwasaidia wananchi; lakini nadhani watupe muda kwanza ili tutafute fedha kwa sababu hili jambo linahitaji fedha. Kupageuza pale ili tutengeneze sehemu ya kivutio yenye garden nzuri tunahitaji tupate fedha za kutosha. Lakini pia watupe muda ili tuweze kufanya ushauriano na baadhi ya wadau wengine maana pale Wizara za Maji, Maliasili na Ardhi, pamoja na sisi na Halmashauri zinahusika. Kwa hiyo jambo hilo linawezekana, lakini watupe muda kidogo ili tujue namna ambavyo tunafanya. Nakushukuru.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru; kwa kuwa leo ni Siku ya Saratani Duniani, ningependa kuiuliza Serikali, ina mkakati gani wa kuzuia wenye viwanda ambao wanachepusha machi yenye kemikali ambazo si salama? Maji haya yanakwenda kwenye Mto Msimbazi na ndiyo maji hayo hayo ambayo hawa wakulima wa mbogamboga wanatumia katika kuzalisha na kumwagilia mbogamboga hizi, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula (food safety) na hatimaye usalama wa hali ya afya ya wananchi na hivyo uwezekano wa kuchangia katika saratani ni mkubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumebaini kuwa kuna baadhi ya shughuli nyingine za kibinadamu zinasababisha uchafuzi wa mazingira, zikiwemo hizo ambazo amezitaja, za viwanda na nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Makamu Rais, Muungano na Mazingira tunazo jitihada Madhubuti ambazo huwa tunazichukua katika kuhakikisha kwamba tunazuia mambo haya ili kuweza kuzuia athari kwa wananchi, ikiwemo hiyo milipuko ya maradhi, yakiwemo ya kansa na mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tunaendelea kutoa taaluma kwa hawa wanaofanya shughuli hizi za kibinadamu, lakini la pili kuna wakati tunatoa hata faini ili waweze kuacha na iwe funzo kwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile huwa tunafanya operations za mara kwa mara kwenye haya maeneo ya uzalishaji, lengo na madhumuni ni kwamba wanaozalisha wajue kwamba wanazalisha lakini wananchi nao wanaathirika. Lakini zaidi tunafika hatua mpaka tunazuia. Inafika wakati kuna kiwanda kinafanya visivyo, kuna shell inafanya isivyo, kuna migodi inafanya visivyo. Kisheria, kwa mujibu wa utaratibu tunazuia uzalishaji ili sasa shughuli nyingine au taratibu nyingine za uhifadhi wa mazingira ziweze kuendelea. Nakushukuru.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukosefu wa taaluma za kimazingira katika Bonde la Mto Msimbazi ambayo husababisha uchafuzi wa kimazingira kutokea, hali kadhalika ukosefu huu wa elimu unawahusu hasa wavuvi ambapo bahari yetu imechafuka sana na tunakosa samaki wenye afya kutokana na wavuvi kwenda na plastics na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusikia Serikali ina mkakati gani, kwanza kuisimamia rasilimali hii muhimu ya bahari, lakini la pili, kutoa taaluma kwa wavuvi wetu ili rasilimali yetu iwe salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujibu swali lingine la Mheshimiwa Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi kubwa tunayofanya kama Serikali na kama Wizara hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ni kuwapa wananchi elimu; na ni kwa sababu tumefika wakati tumegundua kwamba elimu pekee ndiyo itakayotuokoa sisi kutokana na mazingira machafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wavuvi tumefanya jitihada kubwa. Kaskazini Unguja, kwa sababu kuna bahari tumewapa elimu, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na maeneo yote ya Tanzania yenye visiwa, mito, maziwa pamoja na bahari ambamo shughuli za uvuvi zinafanyika tumejitahidi sana tumewapa taaluma na taaluma inafanya kazi, na tutandelea kufanya hivyo. Nakushukuru.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwa kuwa kulikuwa na wananchi ambao walipata silaha hizo kihalali na kwa kufuata taratibu zote na walikuwa wanazilipia kila mwaka na wenyewe walitii amri kwa kuzipeleka katika vituo vya polisi na sasa Serikali imeamua hivyo isiwarudishie. (Makofi)

Je, Serikali inaweza sasa kuwarudishia thamani ya gharama ya silaha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Namtumbo ni la wakulima na mashamba yao yamezungukwa na mapori yenye wanyama wakali na waharibifu na kwa kuwa Serikali awali dhamira yake iliwaruhusu kuwa na silaha hizo ili waweze kujilinda wao wenyewe na mali zao ambayo ni mashamba yao.

Je, Serikali sasa ina mpango gani mbadala wa kuweza kuwasaidia wakulima na wananchi hawa, kuepukana na adha wanayoipata ya kuharibiwa mazao yao na kuuawa na wanyama waharibifu na wakali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Kawawa, lakini pia niwapongeze sana wananchi wa Jimbo la Namtumbo kwa kuendelea kuwa na subira kwa jambo hili. Wamesubiri kwa muda mrefu lakini nataka niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali na lengo lake ni kulinda raia na mali zao. Tunaposikia mahali kuna majangili, kuna majambazi, kuna magaidi, kuna watu ambao aidha wanataka ama wanafanya shughuli ama mambo ya uvunjifu wa amani, sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutuliza na ikiwezekana kukamata kila kinachohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitazama hili jambo suala la uchunguzi sio jambo la kusema kwamba tunafanya leo na kesho na silaha zimetajwa hapa katika jibu la msingi ni karibu 1,579. Lakini hazikukamatwa silaha tu kuna wahalifu waliokamatwa na silaha hizi sio hizi silaha hizi tu kuna visu, kuna mapanga na nyinginezo. Nadhani wengi wenu mnakumbuka zile operesheni za Kibiti na nyingine.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake waendelee kuwa na subira. Serikali kupitia vyombo tunafanya uchunguzi kuhakikisha kwamba nani anayehusika na silaha ipi inahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ukiangalia katika masuala ya investigation sio jambo la kusema tunafanya leo, kesho tunapata majibu na ndio maana watu wengi walilalamika jambo linachukua muda mrefu kuchunguzwa kwa sababu tunataka tutende haki.

Lakini swali la pili je, sasa Serikali ina mpango gani mbadala kusaidia kupunguza sasa hizi adha za wanyama pori. Nataka niendelee tena kumuambia Mheshimiwa Kawawa pamoja na wananchi wa Jimbo hili kwamba Serikali imekuwa ikifanya operesheni na misako mbalimbali ya kusaka hawa watu wahalifu. Lakini pia kuwasaidia kuepukana na madhara ya hawa wanyama pori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa kuna Jeshi letu hili linaloshughulika na masuala ya wanyama pori wanaweza pia tukawasaidia kupitia hili. Vilevile Serikali tumetoa namba maalum hasa kwa wale watu ambao wanafanya kazi za kilimo na shughuli nyingine katika misitu, lengo na madhumuni ikitokea mtihani wowote waweze kutuambia. Tuendelee kuwaomba radhi na kuwaambia wananchi wasubiri jambo linafanyiwa ufuatiliaji. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza ni kwamba kutokana na gharama ya fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo ambalo alisema kwamba ni chakavu lakini jengo hilo ni bovu kabisa.

Je, haoni Mheshimiwa Waziri kwamba kuna haja sasa ya kuambatana na mimi kwenda katika jengo hilo kwenda kujionea na kuona uhalisia wa gharama zinazohitajika katika kutengeneza jengo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti swali langu la (b) ni kwamba kutokana na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji na vitendo mbalimbali vya unyanyasaji wa wanawake na watoto katika eneo la Mkoa wa Kaskazini Pemba na magari ambayo yanatumika ni magari matano tu. Haoni kwamba kuna haja sasa ya kuweza kuongeza magari ya dharura kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vitendo hivi vinakomeshwa muda mfupi ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya miongoni mwa wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kuona kila jengo ikiwa nyumba za makazi, Kituo cha Polisi, mradi wowote ambao unashughulika na masuala ya Jeshi la Polisi ni wajibu wetu kwenda kuukagua. Nimwambie tu Mheshimiwa Omar kwa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Wete tupo tayari kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kukagua na kuona na sio Wete tu, lakini maeneo yote ya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla. Ni sehemu ya wajibu wetu na tuko tayari kufanya hivyo na mimi niko tayari kuambatana na yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine je, sasa si tupate hata gari kwa ajili ya doria na vitendo vya uhalifu? Nimuambie tu Mheshimiwa katika bajeti ambayo tumeisoma ya mwaka 2021/2022 tulisema kwamba tuna jumla ya magari zaidi ya 300 ambayo yatakuja kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Wete tutaliangalia kwa jicho la huruma sana kuhakikisha kwamba gari hizo zinakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.