Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Florent Laurent Kyombo (4 total)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali naomba kuongeza maswali ya nongeza mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kupitia Mheshimiwa Dkt. Magufuli, lakini pia na Waziri wa Wizara ya Maji pamoja na Naibu Waziri kwa usimamizi mzuri wa mradi unaoendelea katika Jimbo la Nkenge wa Kyaka Bunazi wa bilioni 15.1 na Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana juzi ulitoka kule kuangalia maendeleo ya mradi.

Mheshimiwa Spika, mradi huo unahudumia vijiji saba katika Kata za Kyaka na Kasambia lakini kata zingine na vijiji ambavyo vimezunguka mradi huo. Je, ni lini Serikali itaongeza thamani ya mradi ya huo ambao una tenki lenye zaidi ya lita milioni mbili kuzunguka Kata za Nsunga, Mutukula, Bugorora, Bushasha ili thamani ya mradi iweze kuongezwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili Wilaya ya Misenye ambayo ni ndani ya Jimbo la Nkenge, ina vyanzo vingi vya maji na vyanzo hivi ni pamoja na Mto Kagera, lakini tuna Mto wa Ngono. Je, ni lini Serikali itaona ni vizuri kutumia vyanzo hivyo vya maji kuweza kupeleka maji katika vijiji ambavyo vinazunguka vyanzo hivyo vya Kata za Kakunyu, Kilimile, Mabale pamoja na Miziro? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nipende kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge na niseme kwamba mradi huu mkubwa ambao umeutambua na Mheshimiwa Waziri alifika pale na nikupongeze wewe binafsi kwa namna ambavyo umekuwa ukitoa ushirikiano katika Wizara yetu na nikuhakikishie tu kwamba mradi huu kuongezwa thamani tayari michakato imeanza na wataalam wetu wanafika huko hivi karibuni na kila kitu kitakwenda sawa kama ambavyo uliweza kuongea na Mheshimiwa Waziri alipokuwa ziarani katika jimbo lako.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia vyanzo vingine vya maji ili kukidhi na kuondoa shida ya maji katika vijiji vile vingine Mheshimiwa Mbunge nikuahidi tu kwamba tunatarajia kufikia mwezi Juni, tutakuwa tumekamilisha hatua mbalimbali za kuona namna gani tunaibua vyanzo vipya lakini vyanzo vile vilivyoko tunaviboresha na kuona mtandao wa maji unaendelea kutawanyika katika jimbo lako vijiji vyote ambavyo havina maji kwa sasa viweze kupata maji. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali na nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri na weledi katika masuala yote ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza na swali la kwanza ni barabara ya Katoma - Bukwali ambayo ni barabara inaunganisha nchi yetu nanchi ya Uganda na ni barabara muhimu kwa uchumi kwa wananchi wa kata za Gera, Ishozi, Bwanjai, Kashenye na Kanyigo; barabara hiyo yenye kilometa 39.5 nishukuru Serikali sasa hivi kilometa nne zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami na je ni lini kilometa 35.8 zilizobaki zitawekwa kwenye bajeti na kuweza kukamilishwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni barabara ya Bunazi - Nyabiyanga - Kasambya - Kakindo na Minziro ambayo barabara hiyo inaunganisha Makao Makuu ya Wilaya pamoja na nchi yetu ya Uganda lakini kuwa ni barabara kiungo kwa wananchi wote wa Tanzania kila mwezi Januari wananchi wanaenda kuhiji katika eneo takatifu la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi aliyezikwa hapo na ni mojawapo ya mashahidi 22 wa Uganda.

Je, ni lini barabara hiyo yenye kilometa 35.8 na yenyewe itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami nakushukuru kwa nafasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Katoma - Bukwali tayari ipo inaendelea kujengwa na kilometa
4.2 kama alivyosema zinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba bado wakandarasi wawili wako site wakiwa wanaendelea kufanya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kilomita ambazo tunaamini kilometa 2.2 zitakamilika mwezi Aprili na Serikali bado inaendelea kutafuta fedha na katika bajeti ijayo barabara hii tunaamini kwamba itapata fedha kuendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja zote hizo za vijiji mbalimbali na kata mbalimbali tunatambua kwamba ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Nkenge na bado Serikali tunaahidi kwamba itaendelea kuzikarabati na pale fedha itakapopatikana kuzijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililoko Singida Magharibi ni sawa na lililoko katika Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi na hasa wananchi wa Misenyi chakula kikubwa ni ndizi na baada ya kukumbwa na ugonjwa wa mnyauko ambao haujapata majibu majibu mpaka leo, wananchi wamejielekeza katika kulima mazao mengine mbadala. Mazao hayo yameendelea kushambuliwa na wanyama aina ya ngedere na hivyo kufanya wananchi hao kuhangaika sana kupata chakula.

Je, Serikali ina utaratibu gani kuweza kudhibiti wanyama hao waharibifu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niseme kitu kimoja na nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya maswali hapa tuweze kukutana na sisi kama Wizara tuko committed kupeleka wataalamu ili tuweze kupata solution ya wanyama hawa.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza, lakini niseme sijaridhika kabisa na majibu ya Serikali. Changamoto hii ipo tangu mwaka 78 ambapo sasa hivi ni takribani miaka 43 mpaka leo. Nilivyotumwa na wananchi wa Nkenge kuja kuleta malalamiko ya wananchi mwezi wa saba ndipo timu ikatumwa.

Mheshimiwa Spika, unaweza ukaona majibu ya Serikali. Anayelalamikiwa ni Wizara ya Ulinzi, ameenda yeye na JKT, hakuna kuhusisha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, hakuna kuhusisha halmashauri, hakuna kuhusisha Mbunge aliyeleta malalamiko, hatuoni nia ya dhati ya kuweza kutatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi, kama ni kweli tunatambua kazi nzuri ya jeshi letu, Wizara ya Ulinzi kama ni kweli wanahitaji hilo eneo kuna utaratibu wa kuchukua eneo. Na swali langu la msingi lilikuwa ni hilo, kama linatakiwa kuchukuliwa na jeshi letu la ulinzi na usalama kwa nini wasifuate taratibu za Serikali ili eneo hilo basi lichukuliwe kwa mujibu wa taratibu? Hilo ni swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Anaposema kwamba, hilo eneo halitagawiwa kwa wananchi:-

Mheshimiwa Spika, siamini kama hiyo timu waliyounda ilienda site kwa sababu, wananchi wanaishi katika eneo hilo miaka 43 iliyopita. Sasa maana yake leo katika swali langu la pili atuambie hao wananchi walioko katika eneo hilo watapelekwa wapi? Nakushukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, maeneo kama haya ambayo yanashika historia, lakini pia tunafahamu kwamba, eneo hili linalosemwa ndio lilitumika kama base dhidi ya Vita ya Kagera mwaka 78. Lakini tunafahamu pia madhara makubwa na madhila makubwa waliyoyapata watu wa Kagera na hususan wa maeneo haya. Maneno haya ya Mheshimiwa Mbunge na concern anayoiweka hapa inanifanya nitafakari zaidi na niombe kwa ruksa yako, acha tuchukue maoni yake na twende tukatafakari zaidi namna bora zaidi ya kutekeleza jambo hili kwa maslahi ya nchi, lakini kwa maslahi pia, ya watu wetu walioko katika eneo hili. Nakushukuru. (Makofi)