Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deus Clement Sangu (2 total)

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba dai la ekari 495 ni jipya, bali ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani mbele ya Mheshimiwa Rais wakati huo alipofanya ziara Mkoa wa Rukwa kwamba watawakabidhi wananchi ekari 495. Lililokuwa linasubiriwa ni kukabidhi kwa maandishi kwa sababu Jeshi la Magereza limekuwa likisema kwamba hatuwezi kufanyia kazi matamko ya wanasiasa mpaka tupewe barua kutoka Wizarani. Ni lini Wizara itawapa barua Jeshi la Magereza ili kukabidhi hizo ekari 495 kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tamko hili limepelekea Askari Magereza sasa kuingia kwenye mgogoro mkubwa na wananchi na kuwanyanyasa kwa kuwapiga na mara ya mwisho juzi tu hapa nilikuwa huko Jimboni, mama mmoja (na nikikurushia clip utaona) amepigwa na kugaragazwa kwenye matope. Je, Wizara iko tayari kuunda Tume itakayokuja kuchunguza unyanyasaji unaofanywa na hawa Askari Magereza na watakaobainika kunyanyasa wananchi hatua kali za kisheria zichukuliwe iwe fundisho kwa wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tufike wakati tukiri kwamba kuna baadhi ya maeneo bado yana mivutano baina ya wananchi na Kambi za Magereza. Swali kwamba ni lini tutatoa hilo eneo, suala la utoaji wa eneo linahitaji taratibu, siyo suala la kusema tunakwenda na kutoa.

Mheshimiwa Spika, lingine amesema watu wananyanyaswa, wanapigwa, kitu ambacho tunakifanya kupitia Wizara, kwanza tutachunguza, tukiona kwamba kuna Maafisa wetu wa Magereza ambao wanahusika na unyanyasaji huo, hatua kali tutazichukua kupitia Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; katika operesheni za askari wa Wanyamapori kumekuwa na tabia ya askari kunyang’anya wananchi mali ikiwemo mashine za boti, mikokoteni na mali nyingine za wananchi. Nataka kujua kauli ya Serikali ni nini kwa sababu askari hawa wamekuwa wakizikamata hizo mali, wanakuwa nazo zaidi ya miaka miwili mpaka mitatu, ambayo hiyo ni hasara kwa Serikali na kwa wananchi kuwasababishia umaskini?

Swali la pili; naomba kutokana na unyeti wa tatizo hili na hali kuwa tete katika maeneo haya; je, Naibu Waziri yuko tayari kama Wizara kuja baada ya Bunge hili ili wajionee uhalisia wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kisheria yanapokuwa yako chini ya kimahakama, sisi kama wahifadhi tunategemea zaidi Mahakama jinsi itakavyoamua. Kwa hiyo, ushahidi mara nyingi lazima ubaki kama kielelezo tosha pale ambapo kesi inapopelekwa Mahakamani, basi ushahidi utolewe ukionyesha na vitu ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala hili, kwa kuwa mhimili wa Mahakama ni sehemu nyingine tofauti na mhimili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, hivyo kwenye masuala ya kisheria tunayaacha yanaendeshwa kisheria na vifaa vyote ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa inakuwa kama ushahidi, hivyo vinaendelea kutumika mpaka pale ambapo Mahakama inakuwa imeshatoa maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la kuamba na Mbunge, Wizara iko tayari na tutaenda kuangalia hiyo migogoro iliyoko katika eneo hilo na tutalisuluhisha kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)