Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deus Clement Sangu (2 total)

MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya kukabidhi kwa wananchi wa Vijiji vya Msanda, Muungano, Songambele na Sikaungu shamba lililokuwa limechukuliwa na Jeshi la Magereza Mollo Sumbawanga lenye ukubwa wa ekari 495?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza na wananchi wa vijiji vilivyotajwa walikuwa na mgogoro siku za nyuma ambapo mgogoro huo ulimalizwa mwaka 2019 kwa Serikali kutoa eneo la ekari 1,800 kwa lengo la kumaliza mgogoro kama ilivyohitajika.

Mheshimiwa Spika, hitaji la ekari 495 ni dai jipya ambalo Wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Ofisi ya Mkoa wa Rukwa, tunaendelea kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la Akiba la Uwanda?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Uwanda lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,000 lilianzishwa mwaka 1959 na kutangazwa upya kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na.12 ya mwaka 1974 kwa Tangazo la Serikali Na. 275 la tarehe 8/11/1974. Tangu mwaka 1974 hadi 2013 pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na lilikabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 20/01/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, pori hilo linapakana na vijiji 11 kama ifuatavyo; kuna Kijiji cha Ilambo, Kilyamatundu, Mkusi, Kapenta, Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta; na vijiji saba ambavyo ni Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta, ndivyo vyenye mgogoro na Pori la Akiba Uwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia mgogoro huo, orodha ya vijiji husika iliwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Migogoro iliyojumuisha Wizara nane. Utekelezaji wa ripoti ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Mawaziri nane, chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, utaleta ufumbuzi wa mgogoro huu na migogoro mingine kama huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, tunaomba Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, pamoja na Watanzania wote tuwe na subira wakati utekelezaji wa ufumbuzi wa migogoro hii unaratibiwa. Naomba kuwasilisha.