Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Benaya Liuka Kapinga (7 total)

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufanya marekebisho, Naibu Waziri amesema Mbunge wa Mbinga Mjini mimi ni Mbunge wa Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Pia nashukuru katika bajeti inayokuja ametutengea kilometa 5. Hofu yangu ni kwamba ikiwa mpango utakuwa ni wa kilometa tano tano barabara hii tunaweza kuikamilisha kwa muda wa miaka kumi na sita na kidogo. Je, Serikali ipo tayari kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hii ambayo imesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Jimbo la Nyasa na wananchi wa Mkoa wa jirani wa Njombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hali ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS kwa jimbo la Mbinga Vijijini sasa hivi hazipitiki ama zinapitika kwa shida sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzifanya barabara hizi zipitike msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimuombe radhi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba huyu ni Mbunge wa Mbinga Vijijini na si Mbinga Mjini. Kwa hiyo, hata wananchi huko wanajua kwamba Mheshimiwa wao wa Mbinga Vijijini yupo anatetea barabara zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, sasa nijibu maswali yake mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mbunge anafahamu mara baada ya kuteuliwa hii barabara ni kati ya barabara ambazo mimi nimebahatika kwenda kuzitembelea, kwa hiyo, ninaifahamu vizuri sana. Hata hivyo, tukubali tu kwamba ni jitihada za Serikali kwamba fedha inapopatikana hata kama ni kiasi kidogo zile barabara ziendelee kutengenezwa. Hata hizi kilometa 5 zilizotengenezwa zimesaidia sana kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe, kwa hiyo, magari makubwa yanayopita pale hayawezi kukwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tutatenga fedha zote, Serikali inafanya jitihada fedha zitakazopatikana naamini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha barabara hii. Kwa sasa kadri tunavyopata fedha tutaendelea kutengeneza barabara kwa awamu na ndiyo maana hata hizi kilometa tano zilizotengenezwa zimetoa msaada mkubwa sana. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali japo siridhiki nayo kwa sababu maeneo ya kujenga Hospitali ya Wilaya katika Jimbo la Mbinga Vijijini yapo mengi katika maeneo tofauti tofauti, ni uamuzi tu wapi tujenge hospitali hiyo. Je, Serikali inawahakikishia nini wananchi wa Mbinga Vijijini katika bajeti ijayo ikiwa bajeti mbili tofauti zimepangwa na hizi fedha hazikupelekwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mbinga Vijijini kwa kuunga mkono juhudi za Serikali wamejenga na kukamilisha zahanati sita; zingine zina miaka miwili toka zikamilike. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wahudumu katika zahanati hizi ili zifunguliwe zianze kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, kigezo muhimu cha kupeleka fedha katika Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ambacho Serikali iliweka ilikuwa ni Halmashauri husika kuainisha eneo na kuwasilisha taarifa ya uwepo wa eneo husika ndipo fedha ziweze kupelekwa kwenye Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mbinga Vijijini imekuwa na mivutano ya muda mrefu kuhusiana na wapi Makao Makuu ya Halmashauri iwepo. Januari hii wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipopita ndipo ilipata majibu ya kuwa na Makao Makuu ya Halmashauri yawepo. Kwa sababu hizo, hawakuwa na eneo rasmi ambalo liliwasilishwa Serikalini na ndiyo maana fedha haikupelekwa. Hata hivyo, kwa sasa, kama nilivyosema kwa sababu wamekwishawasilisha eneo ambalo limetengwa, katika shilingi bilioni 27 ambazo zimetengwa na Serikali, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba watapata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na zahanati sita ambazo zimekamilika na hazijaanza kutoa huduma kwa sababu ya upungufu wa watumishi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kapinga kwamba Serikali inathamini sana kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mbinga Vijijini. Kwa sababu zahanati hizi zimekamilika tutakwenda kuona utaratibu mzuri kwanza kwa kutumia watumishi waliopo ndani ya halmashauri kufanya internal redistribution ya watumishi hao angalau kuanza huduma za afya. Katika kibali cha ajira kinachokuja Halmashauri ya Mbinga Vijijini tutawapa kipaumbele ili watumishi hao waweze kwenda kutoa huduma katika zahanati hizo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nishukuru kwa Serikali kuzitamka barabara hizi lakini kwa namna majibu yalivyosemwa yanatofautiana kabisa na uhalisia ahadi hizi zilitolewa na Mheshimiwa Rais Samia Hassan Suluhu mwaka jana. Ujenzi wa kilomita nne unazosema ulijengwa miaka ya nyuma sana, nikiri mwaka jana kulikuwa na ukarabati wa eneo korofi kama mita chache sana siyo ujenzi. Sasa swali langu la msingi lilikuwa lini tutaanza kutekeleza lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi hizi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wetu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Serikali ilitoa ahadi hapa kwamba tutaanza kujenga barabara ya Kitai hadi Kigonsera kilomita tano juzi nimepita pale hakuna kilichofanyika wananchi wananiuliza. Je, Serikali mnawaambia nini wananchi wa Jimbo hili la Mbinga Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa Makamu haingekuwa imeanza kutekelezwa lazima itaanza kutekelezwa katika awamu hii ya bajeti tunayoiendea.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge uvute subira lakini kama tulivyosema ahadi hizi zote ambazo zimeahidiwa ni ahadi ambazo zinatakiwa zitekelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu barabara ya Kitai, Litui barabara hii ni kati ya barabara za kimkakati ambayo inaenda inapita kwenye makaa ya mawe ya Ngaka na atakubaliana nami Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kilometa tano zimeshajengwa na naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba muda si mrefu kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha barabara hiyo tena inaendelea kujengwa itatangazwa mapema sana kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na kwa kuhakikishia Mheshimiwa Mbunge unaweza ukawasiliana na TANROAD watakuambia taratibu wako kwenye hatua za mwisho kabisa ili mkandarasi aanze kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lako kwamba barabara zilijengwa muda wa nyuma ndiyo mpango wenyewe kwamba tayari tulishaanza kujenga na kwa hivyo tayari hizo kilomita tano tunazitambua tulizijenga na bado tutaendelea na hasa baada tena ya Mheshimiwa Rais kuongezea ahadi yake.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbinga wafahamu kwamba barabara zao zitajengwa kwa kiwango cha lami kama Serikali ilivyoahidi na kama ilivyo kwenye mpango ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja dogo la nyongeza. Mradi wa Maji wa Litembo una uchakavu mkubwa wa miundombinu hali iliyopelekea Kijiji cha Langandondo kukosa maji kwa miaka minne mvululizo, lini mradi huu unaenda kukarabitiwa na wananchi wale wa Langandondo waweze kupata maji Kata ya Litembo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Liuka Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, uchakavu wa Mradi wa Litembo kama Wizara tunautambua na tayari tumetoa maagizo kwa Meneja wa RUWASA tayari na yeye anaendelea kujipanga ili kuhakikisha kwamba mwaka ujao wa fedha nao tuweze kutupia jicho la utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumpongeza Mheshimiwa Liuka amekuwa ni mfuatiliaji mzuri, tumeondoka hapa wakati wa weekend tumekwenda Mbinga Vijijini tumefanya kazi nzuri na miradi hii yote ya uchakavu pale anafahamu tulishakubaliana utekelezaji wake utafanyika kwa haraka.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru kwa majibu yanayoridhisha ya Serikali. Ni kweli kituo hiki cha Mapera kuanzia mwezi Julai kimeanza kutoa huduma. Kituo cha Muungano, wananchi hawa kituo hiki wamekijenga wenyewe kwa asilimia 100 kwa kusaidiwa na mapato ya ndani kidogo sana, hiyo shilingi milioni 60, lakini sasa wanahangaika kujenga jengo la wazazi. Je, Serikali ina mpango gani kuunga jitihada hizi mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kata ya Kipololo imejenga Zahanati ya Kipololo, Kata ya Mbuji imejenga Zahanati ya Mnyao, Kata ya Litembo imejenga Zahanati Lituru lakini pia Kata ya Mkako Kiukuru wamejenga zahanati. Zahanati hizi zimekamilika, zingine sasa zina miaka mitatu, miwili mpaka leo hazijaanza kazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika zahanati hizi ili ziweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu Kituo cha Afya Muungano ambacho kimejengwa na wananchi kwa asilimia 100 na sasa hivi kuna jitihada za kujenga jengo la wazazi, anataka commitment ya Serikali. Niseme tumelipokea na tutaliweka katika mipango inayofuata ili kuhakikisha tunaingiza katika bajeti zetu hiki Kituo cha Afya cha Muungano ili kiweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kata alizozitaja katika vijiji alivyoviainisha kama Kata ya Kipololo, Mbuji, Litembo na Likako ambazo zimejenga zahanati na mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Niseme tunalipokea na naamini watendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao wanasimamia Idara ya Afya wamelisikia hili, hivyo sasa tutajua namna ya kupanga watumishi waliopo na vile vile kama Serikali itaajiri hapo mbele kidogo tutapeleka watumishi ili vituo hivi vianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Utekelezaji wa REA III, round ya pili Jimbo la Mbinga unakwenda kwa kusuasua sana. Mpaka nakuja hapa Mkandarasi alikuwa bado hajafanya chochote.

Nini kauli ya Serikali juu ya Mkandarasi huyu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wa REA wanazo hatua kadhaa za utekelezaji wa miradi. Wanafanya survey, wanafanya uhakiki, wananunua vifaa na baadaye wanaanza kujenga. Hizi hatua tatu za mwanzo mara nyingi hawaonekani site, wanapoanza kujenga ndiyo wanaonekana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkandarasi atakuwa kwenye mojawapo ya hatua hizo na kabla ya mwezi Machi ataonekana site kwa ajili ya kuendelea na kazi ambayo tayari amepewa kwa sababu deadline yake ni mwezi wa Desemba, 2022 na tunaamini ataikamilisha.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye nia ya dhati kabisa kuondoa adha kubwa ambayo wananchi wa wilaya hizi mbili, mikoa hii miwili ya Ruvuma na Njombe, kwa sababu mto huu una mamba wengi lakini ni mto mkubwa sana. Kwa hiyo, ni hatari kubwa sana kwa wananchi pale, kwa hiyo kwa majibu nashukuru sana. Ombi tu kwamba waharakishe ili daraja hili liweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ombi hili, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara ya Unyoni kuelekea Maguhu inapitika kwa shida sana lakini ipo barabara kutoka hapo Maguhu Mapera kuelekea Kambarage, barabara hii iko hatarini kutoweka. Kuna korongo kubwa sana kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.

Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura ili kuokoa ile barabara iweze kutumika kama inavyotumika siku zote? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu dogo la pili, jiografia ya Wilaya ya Mbinga hususan Jimbo la Mbinga Vijijini ni milima na mabonde hali ya kwamba inahitaji madaraja mengi lakini na barabara zinapitika kwa shida sana. Nahitaji commitment ya Serikali, je, iko tayari kuongeza fedha tofauti na ile hali ya kawaida katika Jimbo la Mbinga Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, bahati nzuri nilifika jimboni kwake, niliona kazi nzuri anayoifanya na jinsi wananchi wanavyomkubali kwa kuwa anafuatilia kwa ukaribu zaidi matatizo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba swali la kwanza alilouliza ni kwamba je, tupo tayari kutoa fedha za dharula ili kusaidi hili korongo kubwa linapita katika hizi barabara ambazo ameziainisha. Niseme tu katika Bunge lako Tukufu baada ya agizo la Mheshimiwa Spika tumeshafanya tathmini ya awali ya kugundua maeneo yote ambayo ni korofi nchi nzima. Kwa hiyo, ambacho tutakwenda kuangalia tu katika eneo lako la Mbinga kama maeneo hayo yametengwa. Kama halipo maana yake tutamuagiza meneja wa TARURA katika halmashauri yako afanye tathmini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu kuongeza fedha, tumewaagiza Mameneja wote wa TARURA Mikoa pamoja na katika Halmashauri. Katika mwaka huu wa fedha, watakavyoleta zile bajeti zao walete bajeti kulingana na uhalisia wa maeneo husika kwa hiyo, hilo ndiyo agizo. Kwa hiyo, naamini kwamba maeneo haya ambayo

Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha yatakuwepo katika bajeti hizo. Ahsante sana. (Makofi)