Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sylivia Francis Sigula (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili tukufu, nianze kwa kumshukuru Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa kibali kuiona siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee sana, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kinachoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutuamini vijana na kutupa uwakilishi katika Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimepata bahati ya kuipitia hii Hotuba ya Mheshimiwa Rais zaidi ya mara tatu. Naomba nikiri katika Bunge hili Tukufu, kama kuna hotuba nilizowahi kuzisoma ambazo ni bora, hii ni hotuba nambari moja. Hotuba hii imebeba dira, maono, matarajio na matamanio makubwa sana ya vijana na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukianzia ukurasa namba moja mpaka ukurasa wa 41, utaona kabisa Mheshimiwa Rais amegusia sekta zote na zote hizo anamlenga kijana. Unapozungumzia viwanda, unazungumzia wanufaika ambao ni vijana; unapozungumzia nishati, wanufaika wa kwanza ni vijana; unapozungumzia mikopo, wanufaika wa kwanza ni vijana. Kwa hiyo, wakati Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake anazungumzia utengenezaji wa ajira zaidi ya milioni nane, naona ni jambo ambalo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijielekeze katika ukurasa wa 37 ambapo Mheshimiwa Rais ameelezea kukuza sekta ya sanaa, michezo na utamaduni. Ni wazi kabisa tunafahamu michezo ni ajira na ni kipato; katika kuelezea sekta hii Mheshimiwa Rais amesema kabisa kwamba ataanzisha mfuko ambao utawawezesha wasanii kimafunzo na mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hapa; kwanza naipongeza Serikali kwa kuanzisha Taasisi ya Sanaa ambapo zamani kilikuwa ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Taasisi hii inatoa kozi, lakini kozi zinazotolewa pale ni chache. Tukisema tuwezekeze katika sekta ya sanaa tutatengeneza ajira nyingi sana kwa vijana. Tunajua sanaa ipo kwa upana wake mkubwa lakini tunaona sanaa hizi zinawatoa vijana wengi na kuwatengenezea kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo tu. Juzi tulitembelewa na vijana hapa, tunaweza tukawatengeneza vijana wa aina ile zaidi. Tunaweza tukawatengeneza akina Manula na Boko wengi kutoka kwa vijana wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa huu wa 37 naomba kunukuu. Rais anasema: “Tutahuisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu ikiwemo kupata mafunzo na mikopo.” Napenda nijikite hapa, kipengele hiki ni kikubwa sana na kama tutakifanyia kazi vizuri, basi tutatengeneza ajira nyingi kwa vijana. Kwa sababu sekta ya sanaa tukisema tuwekeze kwa nguvu kubwa, itaweza kuwainua vijana wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mdogo tu wa mkoani kwetu Kigoma. Tunaelewa kabisa Mkoa wa Kigoma ndiyo kitovu cha sanaa za hapa Tanzania. Ndiyo maana ukifanya tathmini ya wasanii wengi wa Tanzania utaona wengi wanatokea Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, naiomba sana Wizara husika ione ni namna gani ya kuboresha na kuwekeza katika sekta hii ya sanaa. Sawa tumeanzisha Taasisi hiyo ya Sanaa lakini bado tuna vijana wengi wa Kitanzania wenye vipaji ambao wakipewa fursa wanaweza wakafanya vizuri. Changamoto katika sekta hii ya sanaa, vijana wengi hawana mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuna chuo hicho kimoja lakini naiomba Serikali kama itawezekana tuweze kuongeza vyuo hivi hata kwa level ya kanda. Itakuwa rahisi kuwahudumia vijana wengi kwani watapata mafunzo pale, lakini hii mikopo ambayo ameisema Mheshimiwa Rais ikawasaidie hawa vijana wajiendeleze. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda umeisha.

MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana lakini mada yangu nitaiwasilisha vizuri kwa sababu iko katika mapana yake. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Nianze moja kwa moja kwa kuchangia mapendekezo ya Mpango uliopo mbele yetu. Nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha. Kwa kweli ukiusoma mpango utaona kabisa dhamira ya dhati ya kutupeleka katika uchumi imara tunaoutarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kwa ajili ya muda nijielekeze katika Sekta ya Uvuvi. Tunapoteza sana mapato katika Sekta ya Uvuvi. Nasema hivi kwa sababu Tanzania tumebarikiwa. Tuna maziwa ambayo tungeweza kuyatumia yakatusaidia kutengeneza ajira nyingi lakini pia kukuza uchumi. Kwa sababu tukiangalia vipaumbele vyetu tunasema kipaumbele ni kukuza uchumi na pato la Taifa, lakini kwenye Sekta hii ya Uvuvi tunapoteza mapato mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hapa naona kwamba tutapanua Bandari za Kigoma na Tanga lakini pia kuboresha miundombinu. Nitoe mfano mdogo tu; tumekuwa na tatizo, japo limeahidiwa kwenye ilani, Meli yetu ya Liemba, kuanzia mwaka 2017 haifanyi kazi. Kwa kweli tumepata hasara na uchumi umezorota. Kwa hiyo maboresho haya yatakwenda sambamba na kuipatia Serikali mapato lakini pia tutatengeneza ajira nyingi kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Meli yetu hii ya Liemba na Ziwa Tanganyika, linawanufaisha watu wa Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa. Kwa hiyo kuwepo kwa fursa hii ya meli kutaweza kuchochea maendeleo kwa haraka, lakini pia kukuza kipato na uchumi. Pia tukiangalia Ziwa letu Tanganyika hili tunashirikiana na wenzetu wa Burundi na Kongo. Kwa hiyo kuwepo kwa meli hii kutachochea sana kipato na uchumi, lakini pia Serikali itaweza kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia naona kabisa kutokuwepo kwa meli hii kumezorotesha uchumi. Vijana wengi wamekosa ajira lakini pia hata usafirishaji wa mazao ambayo yanapatikana Kigoma, Katavi na Rukwa umekuwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali katika mpango wetu huu ni Mpango mzuri sana na ukiupitia Mpango mzima unaona kabisa tutatoka hapa kwenda level nyingine. Niombe marekebisho haya ya bandari hizi, upanuzi huu ufanyike kwa haraka ili Serikali isiendelee kupoteza mapato yanayotokana na Sekta hii ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais nilijielekeza katika Sekta ya Sanaa na kwa sababu muda ulikuwa mchache nilishindwa kusema; siyo vibaya sana kujifunza kwa wenzetu wanaofanikiwa. Nimepata kusoma Makala moja, tunaambiwa wenzetu wa Nigeria mwaka 2013 suala la Sanaa lilichochea maendeleo sana na liliweza kuchangia zaidi ya robo ya bajeti yao katika Serikali yao. Kwa hiyo na sisi tunaweza tukatengeneza fursa nyingi kupitia huko, lakini tukubali kujifunza kwa waliofanikiwa, siyo dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hotuba hii Mheshimiwa Dkt. Mpango amekiri kwamba pamoja na mengine tuliyoyafanya kumekuwa na changamoto. Nimeona kuna baadhi ya Wabunge wamefanya kama kebehi, lakini niseme tunapokubali changamoto au unapokiri changamoto siyo udhaifu ila ni uimara, kwa sababu changamoto ndizo zinazokujenga. Kwa hiyo wanaobeza naomba tu niseme wanakosea kwa sababu kukiri changamoto pia kunakuimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee hapo, kwa sisi watu tunaopakana na maziwa haya, nikiizungumzia Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria, tunaona kabisa kupitia maziwa haya tunaweza tukatengeneza viwanda vikatusaidia kuwaajiri vijana wengi. Hata hivyo, lazima tukubali, lazima niishauri Serikali na Wizara husika; lazima tuwekeze katika Sekta hii ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto, hatuna vifaa imara vya kuvulia. Bado tuna changamoto vifaa tulivyonavyo haviwezi kutusaidia kuendesha viwanda hivi vya uvuvi. Kwa hiyo niombe sana, bado tuna kazi ya kufanya, lazima tuwekeze ili tuweze kupata matunda bora sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)