Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Miraji Jumanne Mtaturu (1 total)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunijalia kuingia kwenye Bunge lako Tukufu na kuweza kuwawakilisha ipasavyo Wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ikungi pamoja na Jimbo la Singida Mashariki ni kama ambavyo swali la msingi lilivyouliza lina matatizo yanayofanana na jimbo lililoulizwa katika swali la msingi. Pamoja na matatizo hayo zimefanyika jitihada, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya kipenzi chetu Dkt. John Pombe Magufuli, wameshatuletea takribani bilioni 1 na milioni 500 kuchimba visima virefu 28.

Mheshimiwa Spika, sasa nimekuja hapa kuomba kwa kupitia Waziri, wako tayari, tumeshafanya tathmini ya kutosha tuweze kupata, maana kuchimba maji na kuyapata ni jambo moja na kutoka maji ni jambo la pili. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba, kupitia tathmini iliyofanyika na iko Wizarani tunahitaji jumla ya bilioni 2 ili tuweze kutengeneza miundombinu ya maji Wananchi wa Singida wapate maji. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwanza namfahamu vizuri alikuwa Mkuu wa Wilaya, lakini nataka niwahakikishie wana-Singida Mashariki hili ni jembe wembe walitumie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika kuhakikisha kwamba, tunatatua tatizo hili la maji tumeshafanya jitihada za uchimbaji. Nimuombe baada ya Bunge Saa saba tukutane tupange mikakati ya kwenda kutatua tatizo la maji kwa haraka kabisa. Ahsante sana. (Makofi)