Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza (4 total)

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu niipongeze Serikali kwa siku za karibuni imeongeza kiwango cha usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Nyakanazi kuelekea mpaka Kabingo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa barabara hiyo inajengwa na inaishia katika kijiji cha Kabingo; na kwa kuwa kipande cha kutoka Kabingo kwenda mpaka Kibondo, Kasulu hadi Kidahwe bado ni vumbi. Je, kwa muendelezo huohuo ambao Serikali imetuonyesha, ina mpango gani sasa kipande cha kutoka Kabingo kwenda Kibondo, Kasulu mpaka Kidahwe kiweze kutekelezwa ili Mkoa wa Kigoma uweze kufunguka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Chiza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Buyungu kuwa Mbunge na Mwakilishi wao na namkaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga barabara katika Mkoa wa Kigoma. Nafahamu na Mheshimiwa Chiza anafahamu pia kwamba barabara ya kutoka Nyakanazi kuja eneo lake ujenzi unaendelea, lakini utaratibu ule wa manunuzi unafanyika na hivi karibuni kilomita karibu 87 hivi zitaanza kujengwa zikipita katika eneo hili la Kabingo kama alivyolitaja. Pia kilomita zote 300, Serikali iko katika hatua nzuri ya kujenga kwa maana ya kutoka sasa upande wa Kakonko, Kibondo kwenda Kasulu na viunga vyake vinavyoenda kuunganisha nchi ya Burundi kwa maana ya Manyovu na kipande kile cha Mabamba.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua iliyofikiwa ni nzuri na kwa vile Mheshimiwa Mbunge yupo nafikiri itakuwa ni vizuri sasa tuzungumze ili angalau nikupe picha ili uweze kuona na kutimiza wajibu wako kama Mbunge wakati ukiwawakilisha wananchi wako kwamba Serikali imejipanga vizuri kujenga barabara hizi.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naishukuru pia Serikali kwa kututengea Sh.500,000,000 za kujenga kituo cha Afya cha Gwanumpu na nimetoka Jimboni kazi sasa imeanza, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo sasa nina swali moja tu. Pamoja shukrani hizo, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa anajua kabisa Ubunge wangu bado mbichi; sasa ananiahidi nini kwa awamu hii inayofuata; kwamba itaanza lini ili Kata za Kiziguzigu, Kasanda, Rugenge, Gwarama na Nyamtukuza nazo zipate fedha za kujenga vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kama ambavo tumeainisha kwenye ilani yetu ya CCM kwamba kila kata tutajenga kituo cha afya na kila Wilaya ambako hakuna Hospitali ya Wilaya tutaenda kujenga, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, miongoni mwa maeneo ambayo tutahakikisha yanajengwa vituo vya afya ni yale ambayo yana upungufu mkubwa ikiwa ni pamoja na Wilaya yake ya Kakonko.
Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie, hakika pale ambapo bajeti itaweza kupatikana ikaongezeka hatutawasahau Kakonko na hasa tukiwa tunajibu fadhira ambazo wananchi wa Kakonko na hasa Buyungu walitoa kwa Chama cha Mapinduzi.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kuniona. Serikali imejenga miradi ya maji ya Kakonko mjini Gwanu, Mbuki, Dudu A, Nyagwijima, Mamuhange katika Wilaya ya Kakonko. Lakini miradi hii ambayo imetumia takribani shilingi bilioni mbili mingine haifanyikazi hata iliyokamilika haifanyikazi na mingine haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini namshukuru Mheshimiwa Waziri Mbarawa amesikia kilio chetu na amekuja, ameikagua miradi hii tarehe 26 Novemba. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa ma-engineer ili wafanye usanifu pamoja na makadirio ya kuikarabati miradi hii kuokoa gharama iliyokwishatumika na akawaelekeza waweke utaratibu wa kubadilisha mfumo wa kusukuma maji kutoka Nishati ya mafuta kwenda nishati ya jua. Je, sasa shughuli hiyo imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Lakini la pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa anafanyakazi kubwa sana na nzuri katika kuhakikisha tunamtua mwanamama ndoo kichwani. Sasa kwa yale ambayo aliyoagiza Mheshimiwa Waziri kwetu ni utekelezaji, tunamuagiza Katibu Mkuu aweze kutatua tatizo hilo kwa haraka ili wananchi wa Kigoma waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yanaleta matumaini. Nina swali moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita aliniahidi yeye mwenyewe jua linawaka kwamba angefuatana na mimi kwenda kuwasaidia wananchi hawa ambao tayari wameanza kuchimba madini haya, lakini bahati mbaya mambo yakawa mengi.

Sasa kwa kuwa wananchi hawa wameanza kuchimba madini kwa kutumia nyenzo duni, utaalam duni na wakati mwingine hata hawajui uzito wala purity ya madini; je, sasa anawaahidi nini wananchi hawa ambao wameanza kuchimba madini ili waweze kutumia sasa fursa hii na fursa za masoko ya madini ambayo yamefunguliwa kama lile la Geita ambalo amezindua Waziri Mkuu juzi, anawaahidi nini hasa katika uwezeshaji waweze kufanya shughuli hii kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Chiza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na yeye kwamba nilimuahidi kweli nitakwenda Kigoma, hasa maeneo ya jimbo lake. Mimi tu nipende kusema kwamba nitashiriki naye, nitakwenda, tutakwenda hadi kwa wachimbaji, tutakwenda kufanya kazi na tutakwenda kuwaelimisha na kuwapa maelekezo ya Serikali yanavyostahili. Kwa hiyo kwa hilo mimi sina tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala la wachimbaji wadogo. Kweli tuna matatizo makubwa sana ya kimitaji, teknolojia, maeneo, tafiti kwa wachimbaji wadogowadogo. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga vizuri na tumeamua sasa hivi kupitia Geological Survey of Tanzania pamoja na STAMICO tutaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogowadogo ili tuweze kuwapa yale maeneo ambayo tukiwapa tunakuwa na uhakika kwamba wataweza kupata madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza STAMICO tayari tumekwisha kununua rig machine ambayo inaweza kufanya kazi ya drilling kwa wachimbaji wadogo kwa gharama ndogo. Kwa hiyo tunawaomba wachimbaji wadogowadogo waje waombe maombi yao katika Wizara yetu tuwafanyie tafiti mbalimbali kwa gharama ndogo kwa sababu kufanya tafiti ni gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaendelea kutoa elimu ya uchimbaji, uchenjuaji, na uwepo wa masoko haya ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelifungua kule Geita na lingine juzi nimekwenda kufungua pale Kahama na maeneo mengine, tunaendelea na mikoa yote ambayo inakwenda kufungua masoko ya madini. Tunakwenda kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata ile tija ambayo wanadhamiria kuipata tofauti na sasa hivi walikuwa wanakwenda kuuza katika masoko ya pembeni wanadhulumiwa, wanauza kwa bei ndogo, vilevile wanaibiwa. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kwa kuhakikisha kwamba wanapata tija. Ahsante sana.