Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri na watendaji wote kwa kuleta hotuba hii. Napenda kuchangia maeneo mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzishwa kwa Mfuko wa Kinga ya Bei za Mazao (Price Stabilization Fund). Eneo hili limechangiwa pia na Mheshimiwa Bashe. Nilitamani kumpa taarifa lakini nikaamua kuleta mchango kwa maandishi. Kati ya miaka ya 2012 – 2014, Wizara ya Kilimo ilianzisha mchakato wa kuanzisha Price Stabilization Fund kwa mazao ya korosho, kahawa, pamba na tumbaku kwa lengo la kukabiliana na madhara yanayotokea pindi bei ya mazao zinapoanguka hasa katika masoko ya dunia. Sijapata habari kwa nini mchakato huo haukuendelezwa au kama uliendelezwa ulifikia hatua gani. Nashauri Mheshimiwa Waziri alipeleleze suala hili, inawezekana bado lina umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maafa yako ya aina mbalimbali kama vile njaa, ukame, moto, matetemeko, mafuriko na kadhalika. Leo napenda kuchangia suala la maafa yanayotokana na mafuriko. Mafuriko yanapotokea yanaathiri mazao, miundombinu kama ya biashara, reli, nyumba na kadhalika. Yako maeneo yenye mito ambayo mara kwa mara inaleta mafuriko yanayoharibu madaraja, barabara, reli, simu na kadhalika kama kule Kilosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ijipange kujenga mabwawa makubwa ambayo yatakuwa na manufaa makubwa mawili. Kwanza kuepusha uharibifu wa miundombinu na pili yatumike kwa kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi. Suala hili linahitaji utayari wa kukabiliana na majanga, je, Serikali inao mkakati wa disaster preparedness? Hasara ambayo Serikali inapata kutokana na gharama za kurudishia miundombinu inayohabiriwa na mafuriko ni kubwa lakini pia uharibifu unapotokea unasababisha fedha na rasilimali nyingine kuelekezwa katika ukarabati wa miundombinu badala ya kuelekezwa kenye maeneo (miradi) mipya ya maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE.DKT. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri. Nimesikiliza hotuba kwa makini sana, imenikumbusha mambo kadhaa yanayohusu mawasiliano Serikalini Standing Orders na hata Financial Orders (Stores Regulations) nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC.Katika kupitia hoja za ukaguzi za CAG zinazohusu Serikali za Mitaa na baada ya ziara ya kukagua miradi katika Halmashauri 12, nimejiridhisha kwamba Serikali inaweza kupunguza hoja za ukaguzi kama watumishi wanaopewa dhamana kuwa Maafisa Masuuli (DEDs) wangepata uelewa wa shughuli za Serikali.Watendaji wengi wakiwemo Wakuu wa Idara wapo wasiojua kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za Serikali. Baadhi yao hata hawajajua nini maana ya uwajibikaji na utunzaji wa siri za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kamani gharama kuwapeleka viongozi wa Serikali kufundishwa katika Chuo cha Utumishi Serikalini, nashauri Chuo na Maafisa Waandamizi wa Serikali wafanye semina hizo katika maeneo ya kazi. Athari ya kuwa nawatumishi wasiojua Miiko ya Utumishi (The DOS and DONTS) inaweza kuigharibu Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ENG.CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri na wasaidizi wenu wote kwa kazi nzuri katika masuala ya Muungano na Mazingira. Kipekee, naipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuondoa mifuko ya plastiki sokoni ifikapo tarehe 31 Mei, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo matatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania siyo kisiwa. Kwa kuwa nchi nyingi zilizoendelea zinaratibu matumizi mazuri ya mbegu za GMO, nashauri wataalam waendelee kufanya utafiti wa kitaalam hususan kwenye mbegu za mazao zinazotumia teknolojia ya GMO ili kujua faida na madhara yanayotokana na teknolojia hiyo badala ya kuchukua uamuzi wa jumla wa kuikataa teknolojia ya GMO. Kwa mfano, utafiti umeonesha kuwa uzalishaji wa pamba kwa kutumia teknolojia ya GMO umeongezeka maradufu katika nchi zinazozalisha pamba kwa GMO (Wizara ya Kilimo wanazo takwimu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongeza uzalishaji wa pamba tutawezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vya nguo tunavyoanzisha sasa. Hata hivyo, kutakuwa na haja ya kufanya utafiti wa kina kuhusu matumizi ya mafuta ya kula yanayotokana na pamba itakayozalishwa kwa teknolojia ya GMO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi makubwa ya maji ni yale ya kilimo cha umwagiliaji kwa sababu consumptive use ya mimea inayomwagiliwa ni kubwa kuliko matumizi ya nyumbani (domestic use), viwandani na yale ya miradi ya kuzalisha umeme ambayo consumptive use ni sawa na hakuna kwa sababu karibu maji yote yanayotumika kuendesha mitambo yanarudishwa kwenye mto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kushirikiana kwa karibu na Wizara inayohusika na kilimo cha umwagiliaji na Wizara ya Maji, makampuni makubwa ya miwa (sukari) na mashamba makubwa ili wazingatie mambo muhimu yafuatayo:-

(a) Matumizi sahihi ya maji kwa mazao husika (crop water requirements) na water rights ili kuepuka matumizi makubwa yanayosababisha vyanzo vya mito kukauka.

(b) Kulinda uharibifu wa ardhi kwa chumvi na kuwa na kilimo endelevu. Kila mradi wa umwagiliaji, hasa ile ya flooding iwe na miundombinu ya kutoa maji ya ziada shambani (drainage systems) kwa sababu ukosefu wa miundombinu hiyo husababisha chumvi kuongezeka (salinity) na ardhi inaharibika. Gharama za kurejesha ardhi inayoharibika kwa salinity ni kubwa sana.

(c) Usimamizi wa sheria nyingine zinazoshabihiana na Sheria ya Mazingira, mfano Sheria ya Rasilimali za Maji ya 2009. Wenye viwanda vinavyotumia maji ni lazima waheshimu sheria hii pamoja na sheria nyingine. Katika miaka ya 1990, kulikuwa na mgogoro mkubwa kwenye Kiwanda cha Karatasi Mjini Moshi (Kibo Pulp and Paper Board). Tatizo lilianza pale ambapo kiwanda kilipewa water right kwa ajili ya kutumia kiwandani kuzalisha karatasi. Katika kiwanda hicho, matumizi mengine yalikuwa ya kemikali ya aluminium sulphate ambayo ina sumu (toxic).

Sheria ya Rasilimali Maji iliwataka wenye kiwanda kujenga mtambo wa kusafisha maji (treatment plant) kabla ya kuyarudisha maji katika Mto Karanga baada ya kuyatumia kiwandani. Kiwanda hakikufanya hivyo badala yake kilichepusha maji katika mfereji na kuwapelekea wakulima wa mpunga. Matokeo yake yalikuwa mawili; moja, wakulima waliwashwa na sumu ya Al (SO ) ; pili, mazao ya mpunga yalipungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana suala hili lilisharekebishwa kwa sababu wanamazingira waliingilia. Ushauri wangu ni kwamba sheria zote ambazo zinashabihiana na utunzaji wa mazingira, zisimamiwe vizuri na zieleweke kwa ngazi zote katika Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.