Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sonia Jumaa Magogo (6 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema mpaka wakati huu na kuweza kusimama mbele yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukishukuru Chama changu cha Wananchi CUF chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, akisaidiana na Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Magdalena Sakaya. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijafanya busara kama sitalishukuru Bunge lote kwa kutupokea vizuri na kutupa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango wa Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Mpango uko vizuri. Pamoja na uzuri wa Mpango huo, nami ninayo machache ambayo natamani yaingie au yatiliwe mkazo katika Mpango ambao upo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa ni suala la lishe. Katika Mpango huo sikuona kama suala la lishe limetiliwa umuhimu sana kama lilivyo katika jamii yetu. Kila mtu anafahamu umuhimu wa lishe na hata sisi tusingekuwa hapa kama tusingekuwa na afya njema na kupata lishe iliyo bora. Hivyo, naishauri Serikali iliangalie sana suala la lishe. Iziwezeshe taasisi ambazo zinahusika na suala la lishe ili wananchi wapate elimu na kuelewa umuhimu wa lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna utajiri wa vyakula na kama wananchi wangepata elimu ya kutosha, tusingekuwa na watoto wanaozaliwa wakiwa wamedumaa akili. Hivyo, naishauri Serikali itilie mkazo kwenye suala la lishe kwa sababu kuna usemi unasema prevention is better than cure. Kwa hiyo, naishauri Serikali i-stick katika kuepusha maradhi kwa kizazi kilichopo na kijacho kuliko kusubiri tumeshapata matatizo tunanunua dawa kwa pesa ambazo zingesaidia kwenye vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viwanda, kitu cha kwanza napenda tujiulize ni kwa nini vile viwanda vilivyokuwepo vilikufa. Je, zile sababu zilizosababisha vile viwanda vikafa leo hazipo tena? Kama zipo tunafanyaje ili kuhakikisha kwamba viwanda hivyo ambavyo vinakwenda kuanzishwa tena havitakufa na vitakuwa endelevu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano suala la malighafi. Naishauri Serikali ijiandae vizuri kwenye suala la malighafi kabla ya kuanzisha viwanda vingi. Tulikuwa na mazao ambayo sasa hivi tunaona yameshuka ama mengine hayapo kabisa, kama mazao ya mkonge, pamba na michikichi. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kabla hatujaenda kufungua viwanda vingine zaidi tuangalie uwepo wa malighafi ili viwanda hivyo visije vikaenda na vyenyewe vikafa kama vile ambavyo vilikufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie workforce, je, workforce iliyopo inatosha kwa hivyo viwanda ambavyo tunahitaji kuvianzisha? Elimu ikoje kwa wale watu ambao wanakuja kufanya kazi kwenye viwanda hivyo, ujuzi wao ni kiasi gani katika kuendesha viwanda hivyo? Kwa sababu kama tukiwa hatuna workforce ya kutosha hivyo viwanda na vyenyewe vitakwenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mitaji, nauliza Serikali imejipangaje kwa suala la mitaji ya kuendesha viwanda hivyo. Je, tumeiandaa vipi Benki yetu ya TIB katika suala hilo la kuendesha viwanda? Kama tunategemea watu binafsi, je, Serikali imejiandaaje katika kukusanya kodi kuhakikisha kwamba kodi zetu hazipotei na zinapatikana kwa wakati muafaka na kuendeleza Taifa letu kama tulivyopanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kugusia suala la elimu, natamani kuona Serikali ikiwa imetilia sana mkazo kwenye suala la elimu hasa elimu ya msingi. Watoto wanajazana kwenye madarasa na pale hatutegemei ma- engineer, ma-doctor wala Wabunge na Mawaziri ambao watakuwa na akili tulivu kama tulivyo sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wetu tumesoma kwenye shule za kulipia lakini population kubwa iko kwenye shule zile ambazo tunaita za kata, lakini ukiangalia wale watoto mazingira wanayosomea ni magumu sana, hata wale Walimu wanaowafundisha hawapati ile motisha ya kutosha kuweza kuwahudumia wale watoto. Hivyo, naishauri Serikali iangalie kwa sababu msingi wa elimu unaanzia chini, hata sisi tusingekuwa na msingi mzuri mimi na wewe leo tusingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie elimu zinazotolewa kwenye vyuo vyetu. Wasomi wengi wanatoka vyuoni lakini wanakuwa kama wame-cram, ukimpeleka kwenye kufanya kazi ile aliyoisomea, hawezi. Kwa hiyo, tuangalie ile quality ya elimu inayotolewa katika vyuo vyetu na inatolewa kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutoe elimu ya ujasiriamali hasa kwa vijana. Vijana wengi wanamaliza vyuo wakiwa na mentality ya kwamba nakwenda kuajiriwa Serikalini. Tunaweza kuwajengea uwezo kuanzia chini ya kwamba sio lazima kila mtu aajiriwe, unaweza kujiajiri na ukawa na maendeleo zaidi hata ya yule mtu aliyeajiriwa. Hivyo, naiomba Serikali iangalie sana juu ya elimu ya ujasiriamali kwa vijana na vilevile kuwawezesha mitaji pale wanapopata hiyo elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila aliyesimama hapa aligusia suala la maji. Mimi pia naomba nichangie kuhusu maji. Maji imekuwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu, kuendesha viwanda kunahitaji maji, shughuli zote maofisini zinahitaji maji, hospitali zinahitaji maji na shule zinahitaji maji. Hivyo, tunaomba sana Mpango huu utilie mkazo suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi vijijini wanateseka sana na suala la maji. Kama mwananchi ananunua ndoo moja ya maji kwa Sh.1,000/= kijijini, je, ana uwezo kweli wa kuhimili maisha yake? Kwa sababu tunajua kipato cha wananchi wa chini, wale wa vijijini, lakini kama anatakiwa
kununua ndoo moja ya maji ya Sh.1,000/= kwa siku maisha yake yanakuaje? Naomba sana na hilo litiliwe mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi kukazia kwenye bomba la mafuta linalopita Tanga. Huu ni mradi mkubwa sana unaopita mkoani kwetu. Naiomba Serikali iwasaidie wananchi wa Tanga kupitia mradi huu waweze kunufaika zaidi kwa kuwapa elimu na vitendea kazi na kuwapa kipaumbele hata katika zile ajira ambazo zinatokea ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kabisa nianze kwa kuzipongeza Kamati zote kwa uwasilishaji mzuri. Pili, ningependa pia kuipongeza Kamati ya Maliasili ambayo imeona umuhimu wa mapango ya Amboni na kuishauri Serikali kuyafanyia ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Tanga una vivutio vingi sana ambavyo vilikuwa vinausaidia mkoa wetu kuinuka zaidi kiuchumi, lakini kwa sasa vivutio hivyo vimekuwa kama vimetelekezwa. Hivyo, ninaishauri Serikali kupitia upya vivutio hivi na kuona inafanya nini ili kurudisha ile hadhi ya Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda kuchangia kuhusu migogoro ya ardhi. Hapa katika migogoro ya ardhi, ukiangalia sana chimbuko linakuwa ni Serikali ambazo ziko kule vijijini hasa viongozi wa Serikali za Vijiji. Viongozi hawa wamekuwa wakiuza ardhi za wananchi bila kuwashirikisha na kusababisha migogoro mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakikosa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, hivyo kupeleka wenyewe kwa wenyewe kugombana na kusababisha uhasama mkubwa baina ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie na kudhibiti hivi vyanzo vya migogoro ya ardhi hasa kwa hawa Wenyeviti wa Serikali kwa kuwachukulia hatua ambazo zitasababisha waache hii tabia ya kuuza ardhi na kusababisha wananchi kushindwa kuendeleza kilimo chao ambacho ndiyo sehemu kubwa ya utegemezi ya kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine na mimi naomba kuchangia kuhusu maji. Wewe mwenyewe umekuwa shahidi hapa, kila Mbunge anayesimama analia kuhusu maji katika eneo lake. Maji ni kama uti wa mgongo, hakuna shughuli yoyote inayoweza kuendelea bila uwepo wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia viwanda, lazima kuwe na maji, tukizungumzia afya, lazima kuwe na maji na hata kilimo hakiwezi kuendelea bila uwepo wa maji. Mathalani mkoa wetu wa Tanga una vyanzo vya maji kama Ruvu na Pangani, lakini bado tatizo la maji limekuwa ni kubwa sana. Naishauri Serikali ingalie sehemu zile ambazo zina vyanzo vya maji iweze kuvitumia ili kupunguza haya matatizo ya maji kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna miradi mikubwa ambayo bado Serikali inaitekeleza, nilikuwa naishauri Serikali, wakati inatekeleza miradi hiyo, iangalie njia mbadala za kuwasaidia wananchi kama kuchimba mabwawa na visima ili waweze kujikimu wakati wanasubiri utatuzi wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niongelee kuhusu kilimo. Kipindi cha nyuma tulikuwa tunaona watu ambao wanajikita kwenye kilimo zaidi ni wazee, lakini kwa sasa tunaona asilimia kubwa ya vijana nao wameamua kuingia kwenye kilimo. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwape motisha hawa vijana ili wasirudi nyuma kwa kuwapatia mitaji, kuwasaidia kupata masoko, kuangalia miundombinu, kuwapatia elimu ya nini walime na kwa wakati gani na kutokana na ardhi iliyoko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda ni muhimu sana. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Tanga, vijana wanalima matunda kwa wingi, lakini yale matunda yamekuwa yakiozea mashambani kwa sababu hakuna viwanda vya kuweza kusindika yale matunda. Iwapo watakuwa na miundombinu mizuri, watapatiwa viwanda vya kuwasaidia kusindika mazao yao, nina imani wale vijana hawatarudi nyuma na tutaondoa Taifa la wazembe na tutakuwa na Taifa la wachapakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iangalie kuhusu suala la pembejeo. Wakulima wawezeshwe kuhusu pembejeo, pia zipatikane kwa wakati ili waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zinapotokea ahadi, kwa mfano, kama kipindi walichoambiwa walime mbaazi na kwamba zitakwenda kuuzwa India na ikashindikana, Serikali ni lazima ije na mpango mbadala kuliko kuwaachia wananchi ule mzigo wa mazao kuwaaharibikia mikononi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kuona umuhimu wa mazingira na afya kwa wananchi kwa kutoa tamko la kusitisha matumizi ya mifuko ya plasitikic kuanzia tarehe 1 Juni, 2019. Kama tujuwavyo, mazingira bora na usafi ni kiunganishi kikubwa cha kuondoa umasikini na kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii ni lazima ihamasishwe kuwa rafiki wa mazingira na waelimishwe kuwa uharibifu wa mazingira ndiyo unaopelekea kuharibika kwa miundombinu, upungufu wa maji, matatizo ya kiafya, upungufu wa mazao kutokana na uharibifu wa rutuba katika udongo. Vile vile kukosekana kwa mvua na ongezeko la joto vyote hivyo vinachangiwa na uharibifu wa mazingira hayo. Elimu ya kutosha kwa wananchi ni lazima iendelee kutolewa kwa kasi ili wajue umuhimu wa kutunza mazingira. Maana ukiangalia vijijini suala hili la elimu ya mazingira bado sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingine ya wazoa taka mitaani. Unapomwambia Mtanzania wa kawaida, yaani mwenye maisha duni atoe shilingi 5,000/= ili taka zake zibebwe kila wiki, hapa suala la utunzaji wa mazingira tunaweza kulifanya kuwa gumu. Serikali iangalie inafanya nini katika hili ili kila mtu aweze kumudu kutoa taka kila wiki (gharama za wazoaji taka).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la mitaro katika mitaa yetu; watu wamekuwa wakikamatwa kwa kumwaga maji nje ya nyumba zao na wakati mwingine kutozwa faini hadi shilingi 50,000/= ili mradi tu pakiwa pabichi hata kama ni maji safi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutunza mazingira na kuweka urahisi na amani kwa wananchi ili wawe rafiki na mazingira yao, Serikali iwatengezee mazingira mazuri ya kuyatunza. Kama hilo la kuwa na mitaro mitaani, tozo ya shilingi 5,000/= kwa wanaomwaga maji ovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusikiliza hotuba hii, pia nimeona upungufu kwa sehemu kubwa ya hotuba kugusa mazingira kuliko Muungano na hiyo kupelekea kuziacha changamoto nyingi za Muungano bila majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka elimu ya Muungano kwenye vyombo vya habari ili watu wengi wajifunze na kupata majibu ya maswali waliyonayo, ikibidi elimu hii ianzie Shule za Msingi, watoto wakue na uelewa wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto zinazokua addressed zipatiwe ufumbuzi ili tuudumishe Muungano wetu na kuondoa malalamiko yanayokuwa yanajirudia rudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na leo tena nimeweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya PAC na ningependa kuchukuwa fursa hii kumpongeza Mwenyekiti wangu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa kuwasilisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza, nilikuwa na ushauri kidogo kwenye haya Mashirikia na Taasisi ambazo Serikali inawekeza fedha zake. Ninachoona hapa kwanza haya Mashirika yenyewe kwa yenyewe wanatakiwa yawe na mahusiano mazuri. Ikiwa haya mashirikia yatajitangaza vizuri na ikajulikana yanafanya nini na wenyewe kwa wenyewe wakawa wanapeana huduma, kwa mfano SUMA JKT, wanatengeneza furniture nzuri sana, wanatengeneza product ya maji ambayo walileta kwenye Kamati yetu na tuliyaona ni mazuri na bei yake ni nzuri. Hivyo kama Serikali itaunga mkono na wenyewe kwa wenyewe wakasaidiana, kwa mfano, kukawa kuna maelekezo kwamba furniture zote zinunuliwe kutoka SUMA JKT, ama sehemu kubwa furniture za Serikali ziwe zinatoka SUMA JKT, itawasaidia kutengeneza faida zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari, tukiangalia bandari yetu ya Dar es Salaam, ina mlundikano wa mizigo mingi sana; lakini kuna bandari ya Tanga na bandari ya Mtwara. Kama kutakuwa na categorization ya mizigo mingine inakwenda Tanga, mingine inakwenda Mtwara, itasaidia na zile bandari nyingine kuweza kujiendesha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaona Serikali yetu inavyotumia fedha nyingi katika kutengeneza miundombinu ya barabara. Bandari wanaweza wakawatumia zaidi TRC kusafirisha mizigo kuliko kutumia malori ambayo yanapita na mizigo mikubwa kwenye barabara na kuharibu miundombinu ya barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni bajeti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Kama tulivyoona, hii Ofisi ina mashirika mengi sana ya kusimamia. Kama watapewa bajeti nzuri ya kutosha na ikaenda kwa wakati na wakawa wanafanya performance contract na zile Taasisi, pia wakawa na ufuatiliaji wa expenditure kwenye zile taasisi mara kwa mara, itasaidia kufanya zile taasisi ziwe na uwoga na kutengeneza faida kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo tunaona kuna madeni mengi sana hizi taasisi zinadai. Serikali ingeweza kuwasaidia ili waweze kukusanya yale madeni yao pale ambapo wao wamefikia ukomo. Kwa mfano, tunaona wengine ni waajiriwa Serikali na wengine wanajulikana wako wapi, wanaweza kutaifishiwa mali zao. Serikali iwasaidie kama vile ilivyowezekana kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na wenyewe wasaidiwe ili hizi fedha zirudi ziwadaidie kuendesha shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni suala la kukaimu. Mtu anapokuwa anakaimu, anakuwa na hali ya uwoga. Yaani anakuwa hana ile full mandate, anakuwa na wasi wasi kwenye kile kitu anachokifanya, hasa kwenye zile level za Management. Kwa hiyo, kama watasaidiwa kuondoa hili tatizo la kukaimu na wakawa wanawapa wale watu wanaokaimu madaraka au kuziba zile nafasi kwa wakati, itasaidia sana kuchochea maendeleo katika zile taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote ningependa kuupongeza uongozi mzima wa Chama changu cha Wananchi (CUF) ukiongozwa na Mwenyekiti wetu mahiri kabisa, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuaminiwa na Wanachama wote na kupewa tena ridhaa ya kukiongoza chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye hoja na nitaanza na suala la uwekezaji. Katika kuwekeza, Serikali pia inawekeza kwenye Mashirika ya Umma ambayo yapo nchini kwetu na inaweka mtaji wake kwa lengo la kupata gawiwo ambalo litakuja kuisaidia Serikali katika shughuli zake mbalimbali za kuinua uchumi pamoja na huduma mbalimbali za jamii na tumeona mwaka jana baadhi ya Mashirika haya yametoa gawio zuri kwa Serikali. Ndhani kama Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ndio msimamizi mkuu wa mashirika haya, ikiwezeshwa vizuri na kupewa bajeti ya kutosha na kwa wakati ikayasimamia zaidi haya mashirika gawio hili litaongezeka maradufu ya lile ambalo tulipata mwaka jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuongelea kuhusu wazee waliokuwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wazee hawa waliitumikia nchi yetu kwa uaminifu, walisaidia kuleta mahusiano mazuri baina ya nchi yetu na waliokuwa Washirika wetu wa Afrika Mashariki, lakini bado wazee hawa wanahangaika kila kukicha na madai ambayo bado hayajapata suluhu mpaka leo. Kumekuwa kuna kesi mbalimbali wanaendesha, kwa hiyo, inabidi wakati mwingine watoe michango kwa ajili ya zile kesi, wakati mwingine inabidi wasafiri kutoka sehemu mbalimbali kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mikutano yao ya kukutana kufuatilia madai na ukizingatia wazee hawa hali yao ya kiuchumi siyo nzuri. Kwa hiyo napenda kuishauri Serikali katika suala hili watoe tamko rasmi kwa hawa Wazee. Kama kuna chochote ambacho wanadai basi Serikali iwalipe ili waweze kupumzika na kama hakuna madai vilevile lingetoka tamko ili wakajua ni nini ukweli wa haya madai ambayo wanafuatilia kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine bado nipo kwa Wazee na nazungumzia suala la pensheni wanayopata kila mwezi. Kwa kweli pension wanayopata kila mwezi baadhi ya Wazee ni ndogo. Kumlipa Mzee pension ya chini ya kiwango cha laki moja kwa mwezi ni kama unamwonea. Tukilinganisha hali ya maisha tuliyonayo kwa sasa na kile kiwango wanachopata, wazee wale wana familia, wazee wale wanatunza wajukuu lakini kile kiwango wanacholipwa kwa ajili ya kuendesha maisha yao ni kidogo sana. Hivyo naiomba Serikali iangalie inawasaidiaje ili kuongeza hiki kiwango cha pensheni ya kila mwezi hawa wazee waweze kujikwamua na umasikini ambao wanao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi nikizingatia wazee hawa pia hawana mfuko maalum kama walivyo vijana, walemavu, wanawake ambao wanapata asilimia 10 kwenye Halmashauri zao, lakini kwa upande wa Wazee wao hawamo katika hii asilimia 10. Kwa mujibu wetu ni kwamba vijana wanaishia miaka 45. Kwa hiyo, kuanzia miaka 46 tunasema tunawachukulia kwamba wapo kwenye kundi la Wazee, lakini bado ni watu ambao wana nguvu, wanaweza kuitumikia nchi yetu, wanaweza kujenga uchumi. Kwa hiyo, wakiwezeshwa na Serikali kama wanavyowezeshwa vijana, akinamama na walemavu nao wataweza kuchangia kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni vijana; mara nyingi tumekuwa tukiwalaumu vijana kwamba wana akili mgando ya kutaka kuajiriwa hawataki kujiajiri. Hata hivyo, hili mimi nalitazama kwa mtazamo mwingine kwamba, je, hawa vijana tunawaandaa vipi ili waje kujiajiri? System yetu ikoje kuanzia shule ya msingi, sekondari hata vyuoni, wanaandaliwa vipi ili baadaye wanapomaliza elimu yao waje kujiajiri na kuondokana na lile wimbi la kuwaza kwamba nitaajiriwa, nitaajiriwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kuna wale ambao wana mawazo yale ya kujiajiri lakini mazingira yenyewe ya kujiajiri yanakuwa ni magumu. Mlolongo wa kuanzisha mathalan biashara au sehemu yake ya kazi unakuwa ni mrefu sana au unakuwa na gharama ambazo yule kijana anashindwa kuzikidhi na kuweza kufungua biashara yake na kujiajiri. Pia wakati huo huo tuna mapori mengi sana katika Tanzania yetu. Ingewezekana Serikali kuwakusanya wale vijana kwenye makundi, kuwapatia zana za kilimo ama kwa kuwakopesha au kuwasaidia wakaweza kuanzisha kilimo na kuweza kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye ndugu zetu walemavu; kumekuwa na kesi mbalimbali za walemavu na wengine wanasababishiwa ulemavu huo na watu ambao ni wageni katika nchi yetu, labda wawekezaji ama watu mbalimbali. Hata hivyo, zinapokwenda zile kesi za hawa ndugu zetu walemavu na ukiangalia na mazingira ambayo wanakuwa tayari wanayo zile kesi zinachukua milolongo mingi sana, zinakuwa na ucheleweshwaji ndani yake hivyo kuwasababishia kuwa na maisha magumu zaidi. Hivyo, ningependa pia Serikali iwasaidie hawa ndugu zetu kwa kuwasimamia kwenye kesi zao na kuwahakikisha ufumbuzi unapatikana haraka kwenye hizo kesi ili waweze kuendelea na harakati za maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa
kuleta muswada huu wa kuunganisha mifuko. Ninaona ni wakati muafaka kabisa kwa kuwa hiki kilikuwa ni kilio cha muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali, nilikuwa napenda kutoa angalizo, kwa vile tunakwenda kuunganisha mifuko na kunakuwa kuna monopolization, kwa hiyo hakuna ushindani kati ya mfuko mmoja na mfuko mwingine kama ilivyokuwa mwanzo, napenda kuishauri Serikali iwe makini sana katika huduma zinazokwenda kutolewa na mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo kulikuwa na mafao ambayo yanatolewa ambayo yalikuwa yanatumika kama kichocheo cha kuvutia wanachama kutoka mfuko mmoja kwenda mfuko mwingine. Vilevile mifuko ilikuwa inajitahidi kila mfuko utoe huduma bora zaidi ya mwingine ili kuweza kuvutia wanachama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuweka hili suala la kuwa na mifuko miwili ambapo mwanachama hatakuwa na nafasi ya kuchagua aende mfuko gani, nilikuwa naishauri Serikali iwe makini sana kuhakikisha kwamba wanachama hawa hawapati usumbufu katika huduma wanazokwenda kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea kuhusu suala la fao la unemployment ambalo limekuwa introduced kwenye muswada. Hili fao kwa kweli nami naliunga mkono. Mimi ni mmoja wapo wa watu ambao walikuwa wanatoa huduma kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kwa hiyo, wakati mwingine nilikuwa nakutana na wanachama ambao walitamani kuwepo na fao kama hili ili liweze kuwasaidia kulinda credit zao pindi watakapostaafu. Kwa kuwa kulikuwa hakuna hili fao, ilibidi kipindi kingine wa- withdraw hata bila kupenda pamoja na kwamba walikuwa bado wana credit chache ili waweze ku-qualify kuwa pensioners.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunakwenda kulitoa hili fao la unemployment, naishauri Serikali iangalie hili fao linakwenda kutolewaje na litawasaidiaje wale waathirika wa hii unemployment kwa kipindi kile ambacho watakuwa hawana kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo naishauri Serikali iangalie, kuna makundi kadhaa ambayo sidhani kama hii unemployment benefit ambayo ni sehemu tu ya mafao itaweza kuwasaidia. Mathalani wale wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na hawana tena room ya kwenda kupata kazi sehemu nyingine na vilevile kuna wengine ambao wanapata ugonjwa ambao kwa ripoti ya Daktari unaona kabisa huyu mtu hawezi kuja kuendelea na kazi au labda ile pesa angeweza kusaidiwa kupata, ingeweza kumsaidia katika matibabu au shida anayoipitia.

Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na kuondoa fao la withdrawal, lakini naomba waangalie makundi. Kuna kesi ambazo ukiliweka hili fao la unemployment na wakashindwa kupata ile pesa yao, bado tutakuwa hatujawatendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kuishauri Serikali, kwa kuwa sasa hivi tunakwenda kuwa na mifuko miwili, sioni tena sababu ya mfuko mmoja unakata asilimia 15 kwa asilimia tano na mfuko mwingine unaendelea kukata asilimia 10 kwa asilimia 10. Naiomba Serikali, kwa kuwa sasa hivi tunakwenda kuwa na mifuko miwili, mifuko yote iwe uniform; wote wawe wanakata asilimia 15 kwa mwajiri na asilimia tano inakatwa kutoka kwa mfanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa mafao, nilikuwa naishauri Serikali iyapite upya mafao ambayo wameyapendekeza. Ukiangalia vitu vikubwa ambavyo vinamuumiza mwanachama, ni elimu na afya na mimi napendekeza kama wenzangu waliotangulia kwamba tuangalie fao la elimu. Fao la elimu ni muhimu sana kwa wanachama na tutakwa tumewasaidia kutua mzigo na vilevile tutakuwa tunatengeneza kizazi ambacho baadaye
kitakuja kuwa wanachama wetu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali kwa sababu tayari wafanyakazi watakuwa ni wanachama wa NSSF, sioni sababu tena ya yule mwanachama kukatwa pesa kwa ajili ya matibabu ya NHIF. Kwa hiyo, ni vyema mwanachama ambaye atakuwa tayari yuko kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii akaunganisha moja kwa moja kupitia ile michango yake kikawa ndiyo kigezo cha yeye kumfanya atibiwe kupitia NHIF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho naomba kuishauri Serikali ni hili suala la kusema kwamba Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Umma utachanganywa na yale makampuni ya private. Kwangu mimi hili naona kama litakuja kuleta mkanganyiko, kwa sababu terms za public service ukiangalia na private ziko tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawa wafanyakazi wa Private Sector watakwenda kwenye Public Sector baadaye itakuja kuleta shida hata kwenye suala la unemployment, kwa sababu terms zao hawa, anaacha kazi hapa leo, anahamia hapa. Kwa hiyo, itakuwa badala ya ku-concentrate kuendeleza hii mifuko, kila siku itakuwa ni ku-deal na hilo fao la unemployment.