Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jaku Hashim Ayoub (14 total)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Serikali Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliyotolewa mwaka 2014 Kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka) ni mali ya Zanzibar tangu kilipotangazwa rasmi mwaka 1898. Hata hivyo, zipo taarifa zilizothibitishwa kuwa Serikali ya Muungano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliiandikia SMZ kuwataarifu kwamba kisiwa hicho ni cha Tanzania Bara.
(a) Je, Serikali haioni mgogoro huo wa umiliki wa kisiwa hicho ni aibu kutokea kwa nchi moja na kuonesha kwamba bado kero za Muungano hazijapatiwa ufumbuzi?
(b) Kisiwa cha Latham kimepakana na vitalu namba 7 na 8 ambavyo tayari TPDC imeshavigawa bila ridhaa ya SMZ; je, Serikali haioni kuwa mgogoro huo sio wa mpaka bali ni wa mafuta na gesi?
(c) Je, Serikali inachukua hatua gani kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa swali ni kwamba kuna barua kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu hili suala, barua hiyo tumeitafuta kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hatujaiona. Kwa hiyo, Mheshimiwa atusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye swali; kwanza (a) hakuna mgogoro wowote kuhusu umiliki wa eneo lolote baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa tafsiri na suala zima la mipaka la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar limewekwa wazi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar kabla na baada ya Muungano.
Vilevile katika orodha ya changamoto 14 za Muungano zilizokwishashughulikiwa na zinazoshughulikiwa hakuna suala lolote linalohusu umiliki wa eneo lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mgogoro wowote wa mafuta na gesi baina ya Serikali zote mbili, huko nyuma ni kweli kwamba leseni za utafutaji mafuta zilitolewa na TPDC katika eneo husika kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 1980 kwa sababu suala la mafuta lilikuwa ni suala la Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya Serikali hizi mbili kuhusu suala hili, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali. Hata hivyo, Serikali zote mbili zilikubaliana kwamba suala la mafuta na gesi liondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano na kuwezesha Zanzibar kuanza harakati za kutafuta gesi na mafuta na kwamba mpaka sasa Sheria mpya ya Mafuta ya mwaka 2015 imetoa fursa kwa Zanzibar kusimamia shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo ya Zanzibar na ndio maana Zanzibar sasa pia ipo katika mchakato wa kutunga Sheria yake ya Mafuta na Gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata pale ambapo mgogoro unaweza kuibuka tunao utaratibu mzuri wa kukabiliana na changamoto hiyo na watu wa pande zote mbili za Muungano ni ndugu na jamaa na hawawezi kufarakana hata siku moja kuhusu umiliki wa eneo lolote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Hivi karibuni tumeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua Daraja la Kisasa la Kigamboni ambalo limepewa jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye hakuwahi kuishi Kigamboni;
Kwa nini daraja hili halikupewa jina na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Muungano, Mheshimiwa Aboud Jumbe ambaye ana historia kubwa katika Mji huo kwa kuishi karibu miaka 32.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kigamboni una historia ndefu kwa viongozi mbalimbail wa Taifa letu wakiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Hayati Rashid Mfaume Kawawa na Hayati Aboud Jumbe na wengine wengi. Daraja la Kigamboni lilipewa jina la daraja la Nyerere kwa heshima ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendaeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba wazo la ujenzi wa daraja la Kigamboni lilianza wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo katika mipango ya maendeleo ya miaka 60, Serikali chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianza mikakati ya ujenzi wa madaraja makubwa matano ya Kigamboni, Rufiji, Malagarasi, Kirumi na Kilombero.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna barabara, madaraja na miundombinu mbalimbali ya umma iliyopo na inayoendelea kujengwa. Mheshimiwa Mbunge anaweza kupeleka mapendekezo katika mamlaka zinazohusika ili moja ya barabara, daraja au miundombinu iliyopo au itakayojengwa iweze kuitwa kwa jina la Aboud Jumbe kadri itakayoonekana inafaa.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya masomo yao kwa fedha za kigeni badala ya fedha za Kitanzania wakati wao ni Watanzania na vyuo hivyo viko hapa nchini licha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kulipigia kelele sana jambo hilo:-
(a) Je, Serikali inatambua kuwa kuna tatizo hili na kama inatambua imechukua hatua gani dhidi ya tatizo hilo?
(b) Kwa kuwa kilio hiki kipo kwenye taasisi mbalimbali kama vile bandarini, uwanja wa ndege, hoteli na taasisi za fedha na kadhalika, je, Serikali inatoa tamko gani juu ya jambo hili?
(c) Je, kuna sheria yoyote ya nchi inayomtaka mwanachuo wa Kitanzania kulipa ada kwa pesa ya kigeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, kutoka Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa swali kama hili lilijibiwa Bungeni mnamo tarehe 7/9/2016 na lilikuwa ni swali namba 24. Baada ya maagizo yaliyotolewa kwa wamiliki wa vyuo kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa hakuna malalamiko kuhusiana na vyuo kutoza ada kwa Watanzania kwa fedha za kigeni yaliyowasilishwa. Hivyo, kama kuna chuo chochote kinachotoza ada kwa Watanzania kwa fedha za kigeni naomba tupate taarifa rasmi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, sarafu inayotakiwa kutumika Tanzania ni Shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa kifungu cha 25 na 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka 2006. Aidha, kwa Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa kulipwa kwa Shilingi ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni hakuna.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB Aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko makubwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar wanaotumia Bandari ya Dar hulipishwa fedha nyingi na mizigo kupimwa kwa CBM tofauti na ilivyokuwa kabla; huku baadhi ya wafanyabiashara wengine wanachajiwa kwa tani ambapo ni nafuu kutokana
na hali halisi ya mizigo yenyewe. (a) Je, ni sawa kwa vyakula (local goods) kama vile viazi mbatata, dagaa, mahindi, dawa zinazopelekwa hospitalini, vitunguu kuchajiwa kwa CBM; na je, ni kweli kunasaidia wafanyabiashara au kuwakandamiza kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa bidhaa zenyewe ni vyakula?
(b) Je, nia ya Serikali ni kuwakwamua wananchi kiuchumi au kuwakandamiza hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao ni wafanyabiashara wadogo wadogo?
(c) Je, ni sababu gani za msingi kwa bandari hiyo kuchukua fedha wakati huduma nyingine hawazipati kwa miaka yote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Tozo zote bandarini huzingatia uzito yaani tonnage au ujazo wa shehena (CBM) kwa mujibu wa kitabu cha Tozo cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Viwango vya tozo vilivyopo vimelenga katika kuwasaidia wafanyabiashara kupata huduma bora na pia kuhakikisha kuwa bandari inajiendesha na gharama za uendeshaji zinarudishwa (cost recovery). Aidha, hufanyika mashauriano ya wadau kabla ya viwango vilivyopo kuridhiwa.
(b) Serikali siku zote imekuwa na nia njema ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kwa kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kufanya biashara kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma za bandari. Aidha, Serikali kupitia mamlaka ya usimamizi wa bandari imenunua vifaa vya ukaguzi wa mizigo, vifaa vya kuhudumia shehena na kuboresha maeneo ya kupumzikia abiria. Serikali itaendelea kuboresha huduma za bandari na kuangalia tozo ambazo ni stahiki kwa wadau wa bandari.
(c) Sababu za msingi kwa TPA kutoza tozo kisheria ni kurejesha gharama za utoaji wa huduma za bandari ili kufanya huduma hizo kuwa endelevu na kuendelea kuwekeza katika mifumo ya usimamizi ambayo itaongeza ufanisi na hatimaye kupunguza gharama za utoaji wa huduma za bandari.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa meli za mizigo za Zanzibar zimetengewa eneo maalum la kufunga gati linaloitwa Malindi Wharf (lighter key) kwenye bandari ya mizigo ya Dar es Salaam na kuna taarifa kuwa sehemu hiyo sasa inatarajia kujengwa katika upanuzi wa bandari, jambo ambalo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, ingawa sehemu hiyo ni muhimu sana katika kutoa huduma ya meli za upande wa pili wa Muungano (Zanzibar).
(a) Je, Serikali haioni kwamba ipo haja ya kutengwa eneo lingine maalum kwa ajili ya kufunga gati meli za mizigo za Zanzibar ili Wazanzibar waendelee kupata huduma kwenye bandari ya nchi yao?
(b) Endapo itaonekana ipo haja hiyo, je, ni sehemu gani kwenye bandari iliyopangwa kwa ajili ya meli za mizigo za Zanzibar endapo sehemu ya sasa itajengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Bandari ya Dar es Salaam inafanyiwa marekebisho makubwa ikiwa ni pamoja na kujenga gati jipya katika eneo la Gerezani Creek, kupanua na kuongeza kina cha lango la meli, kupanua na kuongeza kina cha eneo la kugeuzia meli, kuimarisha na kuongeza kina cha gati kutoka Namba 1 mpaka Namba 7 na kuongeza eneo la kuhudumia shehena kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Mheshimiwa Spika, kazi hizi zinafanywa katika sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa kuboresha bandari yote ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub kwamba katika awamu hii ya kwanza maboresho yanayoendelea hayatahusisha miundombinu ya eneo la Kighter Quay, hivyo huduma zinazotolewa katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na zile za meli za mizigo za Zanzibar, zitaendelea kutolewa kama kawaida.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kuna mjenzi aliyejenga Vituo vya Polisi kupitia Kampuni iitwayo Al Batna Building Co. Ltd. Vituo alivyojenga ni Kituo cha Polisi Mkokotoni - Unguja na Kituo cha Polisi cha Madungu kilichoko Chakechake Pemba kwa gharama ya shilingi 223,440,000.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni hilo tangu 2012 hadi leo hii?
(b) Je, Serikali inayo taarifa kwamba mwenye kampuni hiyo aliyejenga vituo hivyo amepata maradhi makubwa huku akihangaika kufuatilia haki yake hiyo bila mafanikio?
(c) Je, ni lini Serikali itamtembelea na kumpa pole kwa maradhi hayo mabaya yaliyompata?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub, kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi aliyejenga Kituo cha Polisi Mkokotoni kupitia Kampuni ya Al Batna Building Co. Ltd. alishalipwa shilingi za Kitanzania 560,000,000 na anadai shilingi za Kitanzania 525,000,000 ili kumalizia ujenzi katika kituo hicho. Deni hilo limehakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani na atalipwa mara fedha zitakapokuwa zimetolewa.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali nitoe pole kwa mkandarasi wetu kwa maradhi yaliyompata na nimhakikishie kuwa deni lake atalipwa na Serikali iliamua kusitisha malipo kwa Wazabuni wote katika kipindi fulani kwa ajili ya kufanya uhakiki ili kuepuka kulipa madeni mara mbili.
(iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, tutamtembelea kumpa pole baada ya kumalizika kwa Mkutano huu wa Bunge lako Tukufu kwa kadri ya upatikanaji wa nafasi.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Tarehe 25/5/2017 Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akijibu swali Na. 274 kuhusu madai ya mkandarasi aliyejenga vituo vya polisi Mkokotoni Unguja na Madungu alisema, deni tayari limeshahakikiwa na kwamba atalipwa mara fedha zitakapotolewa lakini huu ni mwaka wa tano deni hilo halijalipwa:-
(a) Je, Serikali ina nia thabiti ya kumlipa mkandarasi?
(b) Je, Serikali inasubiri ipelekwe Mahakamani ndipo ilipe deni hilo?
(c) Je, huu ndiyo utawala bora ambao nchi yetu ina dhamira ya kuujenga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a), (b), na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua madeni ya wakandarasi wote akiwemo Albatna Building Contractor na ina nia ya dhati ya kuyalipa madeni yote ya wakandarasi na Washauri Elekezi waliohusika katika miradi mbalimbali ikiwemo miradi iliyohusisha Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni ambao umetengewa jumla ya shilingi milioni 200 ikiwa ni sehemu ya deni ambalo anadai mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa hakuna deni la mzabuni au mtumishi ambalo halitalipwa kwani madeni yote yaliyohakikiwa yanaendelea kulipwa kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Utaratibu wa kuingiza mafuta nchini unaosimamiwa na Petroleum Bulk Procurement Agent (PBPA) kwa mfumo wa Bulk Procurement System, wakala hukusanya mahitaji kutoka kwa makampuni ya ndani na nje ya nchi lakini kampuni zote zikiweko zile zinazopeleka mafuta nje ya nchi zinalipa Dola za Marekani tatu hadi nne kwa tani kwa mafuta yanayopitia transit ya Dar es Salaam isipokuwa mafuta yanayopelekwa Zanzibar ambayo hutozwa Dola za Marekani 10 kwa tani.
(a) Je, ni utaratibu gani unaotumika kutoa nafuu ya malipo ya Wharfage kwa kampuni za nje zinazopitisha mafuta Dar es Salaam na kuitoza Zanzibar malipo makubwa?
(b) Mafuta yanayopitishwa transit ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar yanalipiwa aina zote za ushuru, je, Serikali haioni kuwa inawabebesha wananchi gharama kubwa ya ununuzi wa mafuta kuliko nchi nyingine?
(c) Je, ni hatua gani Serikali inachukua katika kuhakikisha mafuta yanayopita transit ya Dar es Salaam yanalipwa kama mafuta mengine yanayopita transit ya bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu unaotumika kupanga tozo za bandari hautoi upendeleo kwa upande wowote. Tozo hizo zimewekwa kwa kuzingatia gharama za kutoa huduma, hali ya soko na umuhimu wa kuvutia shehena ya nchi jirani ili kutekeleza sera ya uchumi wa kijiografia na kufanya bandari ya Dar es Salaam kuwa kitovu yaani hub ya usafirishaji. Ushindani wa shehena ya mafuta ni mkali sana (cut throat competition) kwa bandari za TPA hususani Dar es Salaam na bandari za nchi jirani za Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia na Angola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kutokana na hali ya soko (market place exigencies), tozo za bandari kwa shehena ya nchi ya jirani hutofautishwa na shehena ya ndani ya nchi ili kuvutia shehena nyingi kuhudumiwa na bandari ya Dar es Salaam. Kwa hivi sasa gharama ya Wharfage kwa shehena ya Tanzania ya kupakuliwa (imports) ni asilimia 1.6 ya thamani ya mzigo ulioidhinishwa na TRA na kwa kiwango cha chini kilichowekwa cha Dola za Marekani 10 kwa tani moja.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Bara na Zanzibar ni nchi moja na kwa hiyo shehena yoyote iendayo Zanzibar ikiwa ni pamoja na shehena ya mafuta hutambuliwa kama ni shehena ya nchini (local cargo) na sio shehena ya nchi jirani yaani transit. Kwa mantiki hii, tozo zinazotumika ni tozo za shehena ya ndani (local cargo) ambayo ni sawa kwa Bara na Zanzibar.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia majibu ya (a) na (b) hapo juu ni dhahiri kwamba matumizi ya tozo ni miongoni mwa mikakati maalum ya kibiashara na masoko kwa ajili ya kuvutia shehena za nchi jirani ambazo huleta faida ya uchumi na kijamii hapa nchini (multiplier effect) siyo tu kwa bandari bali kwa wadau wote wa bandari na wananchi kwa ujumla.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y MHE. JAKU HASHIM AYOUB) aliuliza:-
Pamoja na kuwepo viwanda vingi vya sukari hapa nchini bado kuwekuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo kususan kwa upande wa kilo 50 ni shilingi 65,000 kwa upande wa Zanzibar ambako kuna kiwanda kimoja tu cha sukari, lakini kwa Tanzania Bara mfuko huo wa kilo 50 ni shilingi 120,000:-
• Je, kuna tatizo gani linalofanya sukari iuzwe kwa bei juu kiasi hicho kwa upande wa Tanzania Bara?
• Je, Serikali itachukua hatua gani ili kuweza kuwapatia wananchi unafuu katika upatikanaji wa bidhaa hiyo?
• Kwa upande wa Zanzibar katika kipindi ambacho matumizi ya sukari kwa wananchi yanaongezeka mfano, mwezi wa Ramadhani Serikali inahusisha ushuru wa kuingiza sukari nchini, je, kwa nini Serikali ya Muungano isizingatie utaratibu huu mzuri ili kuleta unafuu kwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Zanzibar lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa maafisa masoko katika masoko ya Dar es salaam na Zanzibar unaonyesha kuwa bei ya sukari kwa gunia la kilo 50 ni shilingi 101,000 hadi 105,000 kwa Dar es salaam na shilingi 71,000 hadi 77,000 kwa uzito huo huo upande wa Zanzibar. Mapitio ya bei hizo na kama Mheshimiwa Mbunge alivyoeleza kwenye swali hili kipengele (c) tofauti ya bei katika eneo la Dar es salaam na Zanzibar kwa kiasi kikubwa inatokana na utozaji wa ushuru na kodi. Inaonekana dhahiri kuwa kiasi cha kodi inachotozwa kwenye gharama ya mfuko wa kilo 50 Zanzibar ni kidogo wakati Dar es Salaam ushuru na kodi ni asilimia 25 na 18 vyote kwa pamoja.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya sukari nchini kwa wastani vinazalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya sukari ya mezani ni tani 455,000. Chini ya utaratibu maalum Serikali huagiza upungufu katika uzalishaji (gap sugar) ili kutosheleza mahitaji ya soko. Katika kipindi hiki cha Februari – Mei ambapo viwanda vyetu vimefungwa kwa ajili ya matengenezo na kupisha msimu wa mvua za masika kiasi cha tani 135,000 kimeagizwa kuziba pengo na sehemu kubwa ya shehena hiyo imeshawasili nchini.
Aidha, chini ya utaratibu wa maalum wa kulinda na kuhamasisha viwanda vya sukari ni viwanda vya sukari nchini vinaruhusiwa kuagiza upungufu wa sukari. Utaratibu wa wenye viwanda unaambatana na masharti ya kupanua mashamba na viwanda vyao ili katika kipindi cha miaka mitatu tuwe na uzalishaji wa kutosha mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje.
(iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika sehemu (b) ya swali hili zimeagizwa tani 135,000 ili kuhakikisha kuwa tunakidhi mahitaji ya soko. Kulingana na sheria za kodi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, sukari inayoagizwa toka nje ya Jumuiya hutozwa ushuru kwa kiwango cha 100% na 18% ya gharama (CIF) ila kwa kulenga kuwapa nafuu walaji sukari hapo juu inatozwa kwa kiwango cha 25% na 18% ya gharama.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Mawaziri kama walivyo viongozi wengine wa Serikali, wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kwamba wananchi wamewachagua Wabunge na Mawaziri (Serikali) ili kuwasiliana, kushirikiana na kushauriana katika kutatua kero zao; lakini kwa bahati mbaya sana wapo baadhi ya Mawaziri ambao kupatikana kwao hata kwenye simu ni jambo gumu kupita kiasi:-
a) Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya Mawaziri wenye tabia hiyo ya kujichimbia na kutopatikana kwenye simu kuacha tabia hiyo kwa maslahi ya wananchi?
b) Je, Serikali itakubaliana nami kuwa ipo haja ya kuweka utaratibu maalum wa kuifikia Serikali iwapo wananchi kupitia Mbunge wao wana shida ya kumuona Waziri anayehusika na akawa hapatikani hata kwa simu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge anayewakilisha pia Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni B.3(1) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, simu ni moja ya njia za mawasiliano halali Serikalini. Waheshimiwa Mawaziri wanafanya kazi zao kwa lengo la kuwahudumia wananchi na wananchi nao wana nafasi ya kutoa maoni na shida zao na hatimaye kupata mrejesho. Mpaka sasa Serikali haina ushahidi wa kuwepo Mawaziri ambao kwa makusudi hujichimbia na kutopatikana kwa simu. (Makofi)
(b) Mheshimiwa Spika, zipo njia mbalimbali ambazo wananchi wanaweza kuzitumia kuwasilisha maoni na kero zao ofisini kwa Waziri licha ya simu peke yake. Wananchi wanaweza kuandika barua, kupiga simu, barua pepe kwa viongozi na watendaji wa Wizara kama Makatibu Wakuu au Makatibu wa Waheshimiwa Mawaziri na taarifa za wananchi zitamfikia Mheshimiwa Waziri na kufanyiwa kazi.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inalo jukumu la kuzisimamia benki nyingine hapa nchini pamoja na kulinda haki za wateja wa benki za biashara. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa Benki ya FBME imefungwa kwa sababu ya ukiukwaji wa sheria za kifedha na mpaka sasa jambo hilo halijapatiwa ufumbuzi.
(a) Je, ni sababu gani inayofanya benki hiyo isiwalipe wateja wake haki zao au amana zao?
(b) Je, Serikali haioni kuwa BOT imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuzisimamia benki nyingine na kuwafanya wananchi kukosa imani na mifumo ya kibenki inayorudisha nyuma utaratibu wa kuhifadhi fedha?
(c) Je, Serikali haioni kuwa tunakosa mapato ambayo yangetusaidia kwa ajili ya maendeleo ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 11(3)(i), 41(a), 58(2) na 61(1) vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 Benki Kuu ya Tanzania ilisimamisha shughuli zote za Benki ya FBME na kufuta leseni ya biashara, kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi tarehe 8 Mei, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua hiyo, jukumu la kuwalipa wateja wa Benki ya FBME haki au Amana zao kisheria lipo mikononi mwa Bodi ya Bima ya Amana na siyo Benki ya FBME. Malipo ya fidia au amana kwa wateja yamechukua muda mrefu kwa sababu ya taratibu za kisheria zinazotakiwa kuzingatiwa katika zoezi zima la ufilisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, zoezi la kulipa fidia kwa wateja waliokuwa na amana katika Benki ya FBME kwa mujibu wa sheria lilianza mwezi Novemba, 2017 na bado linaendelea. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, 2018 asilimia 60 ya wateja wa benki hiyo walikuwa wamelipwa fidia ya amana na Bodi ya Bima ya Amana.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa majukumu ya msingi ya Benki Kuu ni kusimamia utendaji wa kila siku wa taasisi za kifedha hususan benki. Katika kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu kuchukua hatua kuinusuru benki husika ikiwemo kusimamia uendeshaji wa shughuli za benki au kuifutia leseni mara tu inapobaini viashiria vya kufilisika au upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na Kanuni zake. Lengo la kufanya hivyo ni kulinda walaji, amana za wateja na kujenga imani ya wananchi kuhusu mifumo ya benki na utaratibu wa kuhifadhi fedha kwenye mabenki.
Pili, Benki Kuu husimamia taratibu zote za ufilisi kwa taasisi itakayofutiwa leseni na kuhakikisha kuwa wateja wanapata fidia kwa mujibu wa sheria. Kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo, majukumu haya mawili yanaendelea kutekelezwa na kusimamiwa vizuri na Benki Kuu. Hivyo basi, siyo kweli kwamba Benki Kuu imeshindwa kuzisimamia taasisi za fedha na benki na hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani na mifumo ya kifedha nchini
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kuwa Taifa linakosa mapato ambayo yangesaidia kuleta maendeleo, ni lazima kuzingatia matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu zilizopo ili zoezi hili liweze kufanyika kwa ufanisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, zoezi la ufilisi linafanyika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za ufilisi wa kampuni. Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba, Mfilisi wa Benki kwa kushirikiana na Benki Kuu anafanya juhudi za kukusanya madeni pamoja na fedha za benki zilizopo kwenye benki nyingine nje ya nchi ili kulipa amana za wateja kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Pamoja na kuwepo viwanda vingi vya sukari hapa nchini bado kumekuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo hususan kwa upande wa Tanzania Bara; mfano bei ya mfuko wa kilo 50 ni shilingi 65,000 kwa upande wa Zanzibar ambako kuna kiwanda kimoja tu cha sukari, lakini kwa Tanzania Bara mfuko huu wa kilo 50 huuzwa shilingi 120,000.
(a) Je, kuna tatizo gani linalofanya sukari iuzwe bei ya juu kiasi hicho kwa upande wa Tanzania Bara?
(b) Je, Serikali itachukua hatua gani ili kuweza kuwapatia wananchi unafuu katika upatikanaji wa bidhaa hiyo?
(c) Kwa upande wa Zanzibar katika kipindi ambacho matumizi ya sukari kwa wananchi yanaongezeka mfano, mwezi wa Ramadhani, Serikali inashusha ushuru wa kuingia sukari nchini. Je, kwa nini Serikali ya Muungano isizingatie utaratibu huu mzuri ili kuleta unafuu kwa Tanzania Bara?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Buyuni, Zanzibar lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa kwa vigezo vyovyote vya kupima uwepo wa bidhaa sokoni Tanzania Bara hakuna uhaba wa sukari. Kuhusu tofauti ya bei kati ya pande mbili za Muungano ni kuwa zaidi ya asilimia 53 ya sukari itumikayo Zanzibar huagizwa kutoka nje kwenye vyanzo ambavyo gharama zake ni nafuu ukilinganisha na asilimia 29 zinazoagiwa upande wa Bara kujaza mapungufu ya uzalishaji. Lakini upande wa Bara na nchi nyingine za Afrika Mashariki bidhaa ya sukari kutoka nje hutozwa ushuru wa asilimia 100 ili kulinda viwanda vya ndani. Kutokana na sababu hizo bei huweza kutofautiana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua uamuzi wa kuhamasisha kusimamia kampuni kubwa nne zinazozalisha sukari ili zipanue uwezo wa mashamba na viwanda vyao. Zoezi linakwenda vizuri ambapo Kilombero Sugar tayari inaongeza uwezo wa uzalishaji maradufu kwa kuwekeza dola milioni 200 za Kimarekani. Mtibwa Sugar kwa kuwekeza shilingi bilioni 75 za Kitanzania wataongeza uzalishaji katika kipindi cha miaka mitano na kufikia tani 100,000 kwa mwaka toka tani 30,000 za sasa. Kagera Sugar wanawekeza shilingi bilioni 360 za Kitanzania ili kwa kipindi hicho hicho cha miaka mitano waongeze uzalishaji mpaka tani 170,000 kwa mwaka kutoka 75,000 za sasa. Wakati huohuo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza katika mradi kapambe wa Mkulazi Namba Moja na Namba Mbili wakilenga kuzalisha tani 250,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uwekezaji huo na kwa kuzingatia kiteknolojia ya kisasa inayotumika bada ya miaka mitatu mpaka minne ijayo tutajitosheleza kwa sukari yenye bei nafuu na kuuza ziada nje ya nchi. Pamoja na faida hiyo sekta ya sukari itatuwezesha kutengeneza ajira zaidi ya 50,000.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikishusha ushuru au kuruhusu kuingiza sukari bila ushuru ili kutoa nafuu kwa bei kwa watumiaji wa sukari. Katika kipindi cha mwezi Machi mpaka Juni mwaka huu Serikali kwa kuzingatia maoni ya wadau imetoa vibali vya kuagiza sukari tani 135,610 kwa kutoa ushuru pungufu kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya 100 ili kutoa nafuu kwa bei kwa wananchi pamoja na kuziba pengo la uagizwaji wa sukari kutoka nje.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuza:-

ATCL Corporation ni Shirika la Ndege la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limekuwa likifanya vizuri chini ya Uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Engineer Matida:-

(a) Je, kwa nini ATCL kila Jumatatu inapoondoka Dar es Salaam kwenda Dodoma isipitie Zanzibar ili viongozi pamoja na wananchi wanaotaka kwenda Dodoma wapate huduma hiyo?

(b) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa safari za ATCL kutoka Dar es Salaam zipitie Zanzibar kwa Jumatatu zote kupunguza tatizo la usafiri kwa wananchi wa Zanzibar wanaotaka kwenda Dodoma kwa shughuli mbalimbali?

(c) Je, ni lini safari hizo zitaanza ili viongozi, wananchi wa watalii kutoka Zanzibar waone kuwa Serikali yao inawajali na inadumisha Muungano wetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Konde, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, dhumuni la Serikali kupitia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania Bara na Visiwani wanapata huduma ya usafiri wa anga kwenye kituo (destination) chochote chenye maslahi ya kibiashara. Aidha, ATCL inatumia kituo cha Dar es Salaam kama kitovu ili kuwa na muunganiko wa kupeleka abiria sehemu nyingi na kukidhi mizania ya kibiashara kwani bila kufanya hivyo inaweza kukosa abiria wa kutosha kutoka kituo kimoja kwenda kingine.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hilo, Serikali kupitia ATCL imebaini kuwa Zanzibar ni moja ya vituo ambavyo kuna maslahi kibiashara. Hivyo, imesharekebisha ratiba zake ili kuhakikisha wasafiri kutoka Zanzibar wanakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda Dodoma kupitia kitovu (hub) cha Dar es Salaam kwa kuwa na ndege ya siku ya Ijumaa kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam ambapo abiria hao wataweza kuunganisha safari kwenda Dodoma kwa ndege ya alasiri siku hiyo hiyo ya Ijumaa Aidha, ATCL ina ndege ya Jumapili inayotoka Zanzibar kuja Dar es Salaam asubuhi ambayo itaungaisha na ndege inayokwenda Dodoma.

(b) Kama nilivyoeleza kwenye jibu la kipengele (a) cha swali hili, hivi sasa siyo wakati muafaka kwa kila Jumatatu ndege ya ATCL inapoondoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ipitie Zanzibar. Aidha, utaratibu huo wa safari za ATCL kutoka Dar es Salaam kupitia Zanzibar kwa kila Jumatatu utaanza pindi muunganiko wa kupeleka abiria Zanzibar kutoka Dar es Salaam na sehemu zingine kwa siku ya Jumatatu utakidhi mizania ya kibiashara.

(c) Safari za ATCL kila Jumatatu kutokea Dar es Salaam kwenda Dodoma kupitia Zanzibar kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali (b) zitaanza pindi muunganiko wa kupeleka abiria sehemu zingine kupitia Zanzibar utakapokidhi mizani ya kibiashara.

Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali viongozi, wananchi na Watalii kutoka Zanzibar na ndio maana inajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kuwa Viongozi, Wananchi na Watalii kutoka Zanzibar wanapata usafiri wa kuunganisha kutoka kituo cha Dar es Salaam kama kitovu kwenda Dodoma kwa kadiri inavyowezakana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-

Kumekuwa na kilio cha uchakavu wa vituo vya polisi kwa upande wa Unguja na Pemba:-

(a) Je, ni vituo vingapi vipya vya polisi vilivyojengwa kwa upande wa Unguja na Pemba?

(b) Je, vituo hivyo vimejengwa na kampuni gani na ni vigezo gani vilivyoangaliwa katika ujenzi wa vituo hivyo?

(c) Je, ni lini Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara watafuatana nami kwenda kuviona vituo hivyo vilivyochakaa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mikoa ya Unguja na Pemba vituo vingi vimejengwa au kukarabatiwa katika miaka tofauti, vikiwemo Vituo vya Mwembe Madafu na Mbweni katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Kituo cha Mchanga Mdogo Mkoani Kaskazini Pemba, Vituo vya Chwaka na Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja na Vituo vya Chakechake na Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba. Aidha, kuna ujenzi unaoendelea kwa sasa wa Vituo vya Chukwani, Dunga na Mkokotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo mengi ya vituo hivi vya polisi ujenzi ulikuwa ni wa ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, tunatambua mkandarasi aitwaye Albatina Construction Company Ltd anayejenga Kituo cha Polisi Mkokotoni ambaye kazi yake bado inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo na uchakavu wa vituo vingi vya polisi katika Mikoa ya Unguja na Pemba kama vile vituo vya Mkoani Pemba, Kengeja, Micheweni, Konde, Mahonda, Nungwi, Kiwengwa na Kiboje ambapo hali ya kifedha ikiruhusu vitakarabatiwa. Viongozi wa Wizara wataambatana na Mheshimiwa Mbunge Jaku Hashim Ayoub tarehe 3/7/2019 kwenda kuviona vituo hivyo vilivyochakaa.