Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Jaku Hashim Ayoub (2 total)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Nami nikushukuru na vilevile nikutakie afya njema na kila zito Mwenyezi Mungu afanye jepesi kwa upande wako.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali hii isingekuweko madarakani bila kuwepo wananchi na wananchi ndiyo Serikali na Serikali ni wananchi, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe mwenyewe bila kuweko wananchi usingepata Uwaziri Mkuu hata Mheshimiwa Rais pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani.
Mheshimiwa Spika, swali, afya huwezi kupata bila kupata chakula, mwanzo upate chakula ili upate afya. Hivi sasa kumekuwa na harufu inaweza ikawa nzuri au ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu wa chakula ikiwemo bidhaa muhimu ya sukari, na sijui kama Serikali mmefanya utafiti gani kuliangalia suala hili. Msemo wa Waswahili husema, usipojenga ufa, hutajenga ukuta. Mmechukua jitihada gani kama Serikali kuangalia hali ya sukari na mchele ilivyo sasa? Na wanaoumia ni wananchi na ukizingatia kesho kutwa tuna sikukuu na inahitaji sukari kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Je, kuna harufu Serikali imeagiza sukari. Ni kweli suala hilo kwa ajili ya kuwajali wananchi wake?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ameeleza maneno mengi lakini muhimu ni kwamba kuna harufu ya upungufu wa bidhaa ya sukari nchini. Ni kweli huko nyuma tulikuwa na tatizo la sukari nchini kote na Serikali ikafanya jitihada ya kutambua mahitaji ya nchi, na yale mapungufu tuliyafanyia kazi kwa kuagiza sukari nje ya nchi na kuleta ndani kwa kiwango ambacho hakitaathiri uzalishaji wa ndani ili tuweze kuendelea kutoa huduma hiyo. Tumeendelea kufanya hilo mpaka pale ambapo tumeridhika kwamba viwanda vyetu vya ndani vimeanza kuzalisha na kuona uzalishaji ule na sukari ambayo tumeingiza vinaweza kutufikisha tena msimu ujao wa uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, suala la sukari hatujaishia tu kuwa na maazimio ya kuagiza toka nje. Mkakati mkubwa tuliofanya ni kuhakikisha tunaimarisha viwanda vya ndani viweze kuzalisha. Tumekutana na wazalishaji wote wa sukari, TPC, Kilombero, Kagera pamoja na Mtibwa kupata picha ya uzalishaji kwenye viwanda vyao na mkakati walionao kuendeleza uzalishaji. Lakini bado tumegundua kwamba viwanda vyetu havitakuwa na uwezo kwa kipindi cha miaka minne ijayo kuzalisha sukari ikatosheleza nchini. Lakini pia kumekuwa na wasiwasi wa takwimu za mahitaji ya sukari nchini kwa sababu nchi jirani ya Kenya yenye watu milioni 45 mahitaji ya sukari ni tani 800,000, lakini tathmini ya Idara yetu ya Kilimo nchini kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 45 ile ile wanatuambia takwimu zile zinahitaji tani 420,000; kwa hiyo utaona tuna upungufu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya; kwanza tumeagiza Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina kuona mahitaji ya sukari nchini, lakini pili kutokana na maelezo tuliyopata kutoka kwa viwanda tumewapa maelekezo ya kuzalisha zaidi ili tuongeze sukari, na tumekubaliana hilo. Tatu, tumeamua kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda na uhamasishaji wa kilimo cha miwa ili tuweze kuzalisha sukari inayoweza kutosheleza mahitaji ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshapata wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza kwenye ulimaji wa miwa pamoja na uzalishaji wa sukari nchini ili na sisi tufikie kiwango ambacho kitakwenda kutambulika baada ya Wizara ya Kilimo kufanya sensa yake. Lakini wakati wote huu Serikali itahakikisha kwamba nchi haikosi sukari na wananchi wanaweza kupata kinywaji ambacho kinahitaji sukari, uendeshaji wa sukari kwenye viwanda kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayohitaji sukari ili tuweze kuhakikisha kwamba biashara hii na zao hili linatosheleza kwa matumizi ya ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Jaku ametaka kuzungumzia upungufu wa chakula na jana Mheshimiwa Keissy aliomba Mwongozo wa kutaka maelezo ya hali ya chakula nchini na bado Serikali tumeahidi kutoa taarifa hapa Bungeni kabla ya mwisho wa wiki hii ya hali ya chakula nchini na mkakati wa taifa kama kuna upungufu huo wa kiasi hicho ili sasa kila mmoja wetu nchini aelewe nafasi tuliyonayo ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kuondoa tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo taarifa ambayo itatolewa na Wizara ya Kilimo juu ya hali ya chakula ikiwemo na zao la sukari inaweza kusheheneza mahitaji ya uelewa kwenye eneo hili ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa umakini na utendaji wake na kilichonivutia zaidi anapotoka hapa akienda ofisini kwake haifiki hata dakika, watu anaokutana nao njiani anasalimiana nao ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri bila kujali itikadi ya chama. Ninakupongeza sana, mara nyingi huwa nikikaa nje pale na nikienda kunywa chai ninakuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakaribiwa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama wiki mbili tu panapo majaaliwa tukifika, hali ya kusikitisha ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, sukari inahitajika kwa wingi matumizi yake. Hata wananchi wa Ruangwa na Peramiho wanahitaji sukari. Mwenyezi Mungu alitupa mtihani wa mvua, viwanda vyetu vya ndani havikuweza kuzalisha sukari ya kutosha na uchunguzi au harufu niliyoipata tunahitaji kama tani laki moja na ushee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha kwa taarifa niliyo nayo ni kuwa mmetoa vibali vya tani 30,000 na baya zaidi kuna msemo Waislamu husema nguo ya Ijumaa hufuliwa Alhamisi na mvua hii pengine isikauke. Sasa hawa mliowapa vibali, sukari yao navyotegemea hata ikifika Ramadhani itakwisha, itawasaidia nini wananchi? Mnatumia utaratibu gani kuwapa vibali hawa watu, wanarudia ndiyo wale wale au na wengine? Kuna formula gani ili kuokoa hatua hii.

Mheshimiwa Waziri Mkuu uko tayari kuleta watu angalau mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani wakaingiza sukari kwa kipindi hiki ili kuokoa hii hali na janga hili lilivyo? Hii sukari mliyowapa vibali hata ikifika Ramadhani itakwisha, itasaidia nini kwa wananchi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, najua amezungumza mengi na yaliyotengeneza maswali mengi sana. jambo la msingi alilotaka kuzungumza hapa ni kupungua kwa sukari na mahitaji ya sukari nchini kwa sasa. Napenda niwathibitishie Watanzania kwamba Serikali iko macho na inajua maeneo gani yanahitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji ambayo yanahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la sukari ni kweli nchi yetu hatuna uzalishaji wa kutosha wa sukari kutosheleza mahitaji ya Watanzania. Katika mwaka wa kilimo, mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya tani 420,000, lakini uzalishaji tulionao hapa nchini ni tani 320,000; kwa hiyo tunakuwa na mapungufu ya sukari inayohitajika ya tani laki moja na ikiwezekana zaidi kwa sababu ya ongezeko la watumiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka tunao utaratibu wa kuagiza sukari na mwaka huu pia tumesahafanya hilo, tumeshaagiza sukari na mwaka huu tumeagiza sukari tunataka tuagize sukari ya tani 131,000 kwa mujibu wa takwimu zilizofanyiwa utafiti na Bodi ya Sukari, kati ya hizo tayari tumeshaagiza tani 80, kati ya tani 80 tayari zimeshaingia tani 35 na nyingine ziko bandarini. Hizi tani 35 tumeshaanza kuzigawa kwenye maeneo yote ya nchi ili ziweze kufika kwa wananchi ziweze kusaidia kupunguza gharama na bei.

Mheshimwa Naibu Spika, pia kwa kuwa, tunakabiliwa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo watumiaji ni wengi, utaratibu wa kuagiza sukari zaidi kufikia malengo umeshaandaliwa. Watanzania tushirikiane kuwasihi wafanyabiashara ambao sasa hivi wamepandisha bei bila sababu na hii inaumiza sana Watanzania kwa sababu bei zilizopandishwa hazina umuhimu wowote kwa sababu uzalishaji tulionao na hii sukari pengo tunavyoleta nchini inataka tu bei zile ziendelee kuwa ambazo zinaweza kuhimilika na Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko mikakati ya kuongeza uzalishaji kufikia malengo. Natambua tuna viwanda vinne, Kagera Sugar, Kilombero, TPC na Mtibwa, tuna kiwanda cha tano kilichoko Tanzania Visiwani, Mahonda navyo pia vinasaidia uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa tatizo la kuagiza sukari nje ya nchi, tumejiwekea utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara wenye viwanda na kuwasihi kuongeza uzalishaji na tumeona jitihada kadhaa ambazo zinafanywa na wazalishaji. Bahati nzuri sana wiki moja iliyopita nilikuwa Mkoani Kilimanjaro, nimepata nafasi ya kutembelea kiwanda cha TPC ambacho kimeonesha mafanikio makubwa ya uzalishaji zaidi. Mwaka jana walizalisha tani 100,000 na sasa wameongeza tani 20,000, kwa hiyo, sasa hivi wamefikia uwezo wa kuzalisha tani 120,000 na msimu huu wa kilimo wataongeza tani nyingi zaidi, hivyo hivyo na viwanda vingine kama Kilombero na Mtibwa Sugar.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilipofanya ziara Mkoani Manyara, nilitembelea Manyara Sugar, kwa hiyo viwanda vingi vinaendelea kujengwa na sasa tunakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkoani Morogoro kuna eneo la Mbigiri kwa ushirikiano na Magereza pia na eneo la Mkulazi ambalo linaandaliwa na Taasisi ya NSSF na PPF kwa pamoja na wawekezaji ambao pia wako tayari kutuunga mkono katika uzalishaji wa sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaondoe mashaka Watanzania kwamba sukari ipo na wakati wa Ramadhani sukari ya kutosha itakuwepo wala hakuna sababu ya kuongeza bei, tutafanya hivyo na pia ufuatiliaji kuona bei haziongezeki ili kuwakera Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.