Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deogratias Francis Ngalawa (27 total)

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado ulipaji wa fidia huu umeonekana kuwa ni kitendawili, kwa mara ya kwanza tuliambiwa kwamba fidia hizi zitalipwa tarehe 16 Februari, lakini sasa hivi Serikali inakuja na majibu mengine kwamba itaanza kulipa mwezi Juni. Sasa tunaomba kujua specific date ya fidia hiyo itakuwa ni lini?
Pili, kumekuwa na usumbufu mkubwa katika ulipaji wa hiyo fidia, je, kwa sababu muda utakuwa umeshapita fidia hii italipwa pamoja na fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli fidia ilianza kulipwa tangu mwezi Februari mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, lakini tutambue kwamba suala la ulipaji fidia ni suala endelevu, kadri tathmini inavyofanyika ndiyo fidia inavyoendelea kulipwa na ndiyo maana tunasema hata mwezi huu na mwezi ujao wataendelea kulipwa fidia. Suala kubwa Mheshimiwa Mbunge ni kwamba shughuli za ujenzi wa mradi huu zitaanza mapema tu baada ya fidia kukamilika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kama wananchi watalipwa pia pamoja na nyongeza ya mapunjo ya awamu iliyopita.
Mheshimiwa Spika, taratibu za fidia kwa waathirika hufanyika wakati tathmini inapofanyika, kwa hiyo malipo ya fidia hulipwa kulingana na viwango wakati tathimini inafanywa na siyo vinginevyo.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na umuhimu mkubwa wa bonde hili ikiwa ni pamoja na kufua umeme ili kuweza kupeleka katika Gridi ya Taifa: Je, ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kuitengea hela bila kutegemea ufadhili?
La pili; katika Wilaya ya Ludewa kuna mabonde kama ya Bonde la Mkiu na Bonde la Lifua: Je, ni lini Serikali itaiwekea mpango mkakati ili mabonde haya yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Mheshimiwa ameshauri kwamba ni lini Serikali itaacha kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi yake. Nimfahamishe Mheshimiwa Ngalawa kwamba mwaka 2006/2007 tulianza programu ya utekelezaji wa maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kushirikiana na marafiki na wadau mbalimbali wenye nia nzuri ya kutusaidia sisi Watanzania. Programu hiyo ya kwanza iliisha mwezi Desemba, 2015. Januari mwaka huu, tayari tena tumesaini memorandum ya utekelezaji wa maendeleo ya maji kwa kushirikana na wadau hao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hatua hii, kwa sababu tuna memorandum tayari, hatuwezi kusema Watanzania tujitenge peke yetu. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa miradi ya maji ikiwemo ya umwagiliaji kwa kushirikiana na fedha ya Seikali ya Tanzania ambayo ni kodi ambazo Mheshimiwa Rais amesisitiza kwamba tulipe ili tufanye miradi ya maendeleo pamoja na wafadhili. Pia Mheshimiwa Mbunge ujue, bila wewe mwenyewe kutenga fedha, wafadhili hawawezi kukusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ni kwamba ni lini sasa? Yapo maeneo mengi yanayofaa kwa umwagiliaji, Serikali itahakikisha kwamba inajenga miundombinu. Ni kwamba nchi yetu tayari ilishafanya utafiti kwamba tuna hekta zinazofaa kwa umwagiliaji milioni 29.4 na kati ya hizo, hekta 461,000 zimeshaendelezwa na zinafanya kazi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba hekta zote tumezikamilisha tumeziwekea miundombinu ya umwagiliaji ili tuweze kuondokana na tatizo la maji pamoja na tatizo la njaa. Katika hiki kipindi cha miaka mitano cha Awamu ya Tano, tumepanga kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu, tunapata hekta milioni moja kuendeleza Sekta ya Umwagiliaji.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Juu ya suala la upembuzi yakinifu wa barabara hii limeshakuwa ni la muda mrefu sana. Bahati nzuri tayari hata Mkandarasi alishapatikana na tayari hilo tangazo lilishatolewa toka Desemba, 2015. Sasa leo hii mnapozungumza kwamba, process za kumpata mkandarasi zinaendelea ni mkandarasi gani tena mwingine huyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, imeshakuwa ni kawaida kwa Serikali kuwa inatoa utaratibu wa kwamba hiki kitu kitashughulikiwa muda fulani, lakini matokeo yake muda unapita na hicho kitu kinakuwa hakijafanyika. Sasa ningependa kujua kwa sababu 2016/2017 ni muda mrefu, ni muda ambao unachukua miezi 12, wananchi wa Ludewa wangependa wajue ni lini hasa itaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi mkandarasi yupo katika hatua ya mwisho kupatikana. Vilevile ujenzi wa barabara hii atakumbuka kwamba, alisaidia sana Bunge limepitisha bajeti ya Wizara yetu na katika bajeti ile kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii, kwa hiyo, ujenzi utaanza katika mwaka ujao wa fedha unaoanza tarehe Mosi, Julai.
MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado tunauliza. Wadau mbalimbali wamekuwa wakichangia michango hii ya maji kwa karibu sana lakini Serikali imekuwa ikusuasua kupeleka hizi hela.
Je, Mheshimiwa Waziri ananithibitishiaje kwamba tutazipata fedha hizi kwa haraka?
Pili, kwa sababu wadau wa maendeleo wamekuwa wakileta ile michango na kazi inakuwa imeshafanyika, kutokana na Serikali kuchelewesha michango yao inakuta kwamba baadhi ya miundombinu inakuwa tayari imeshabomoka.
Je, Serikali inaweza ikagharamia ile miundombinu iliyobomoka kwa sababu ya kucheleweshwa kwa fedha?
NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS-TAMISEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze wazi kwa sababu Serikali kuna commitment ya shilingi milioni 50, na kwa sababu jukumu letu kubwa ni kuhakikisha miradi ya maji iliyotengwa katika kipindi hichi inaweza ikapata msaada wa haraka. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Deogratius, ofisi yetu itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunasukuma pesa hii milioni 50, kama ni matching grands ya kuhakikisha mradi huo unatekelezeka, tutaweza kulifanya hili wala usihofu, mimi mwenyewe naomba nitoe commitment hiyo kama Serikali kuhakikisha jambo hili linakaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima kwamba miradi mingine imetekelezwa lakini mpaka imechakaa. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha miradi ile sasa inarekebishwa kuweza kufanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Deo kuwa tutakachokifanya kwanza ofisi yetu itawasiliana na Ofisi wa RAS Mkoa wa Njombe, kuangalia ni jinsi gani kama kuna miradi ambayo ina changamoto kubwa na kubainisha ni kitu gani kinatakiwa kifanyike. Kwa sababu mwisho wa siku, mradi kama umetekelezwa lakini mradi saa nyingine umeharibika kabla ya kuwapatia wananchi fursa hiyo ya maji ina maana tutakuwa hatujafikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Ofisi ya RAS Mkoa wa Njombe naomba niiagize kupitia mkutano huu, kwamba wahakikishe wanafanya follow up katika Jimbo hili la Ludewa kuangalia changamoto iliyokuwepo halafu tuangalie mkakati sasa, tutafanyaje ili mradi miradi hiyo iweze kufanya kazi. Lengo kubwa wananchi wako Mheshimiwa Deo waweze kupata fursa ya maji, na hiyo ndio azma ya Serikali kwamba kuhakikisha inawahudumia wananchi wake.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kuzungumza hapo kwamba tarehe 19 mwezi wa nne liliulizwa swali kwenye Bunge lako Tukufu kuwa Mradi wa Chuma, Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma, utaanza lini? Majibu ya Serikali yalikuwa kwamba kwanza fidia italipwa mwezi Juni, 2016 ambayo fidia hiyo haijalipwa mpaka leo na pili miradi hii kwamba itaanza mwezi Machi, 2017.
Je, mkanganyiko huo unatokana na nini na majibu hayo yote ambayo sasa hivi inaonekana hayajitoshelezi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa anavyosema Mheshimiwa Mbunge ni sahihi. Kwenye Bunge la mwezi Aprili tulisema kwamba mradi huu utaanza mapema ifikapo mwezi Machi. Hivi sasa bado tupo Januari, hivyo Mheshimiwa Mbunge nadhani avute subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kuhusu suala la fidia; fidia inayotarajiwa kufidiwa wananchi wale inafikia takribani shilingi bilioni 13.34, ni kiasi kikubwa. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kupitia tathmini halisi ya fidia hiyo, halafu baada ya zoezi hilo kukamilika, basi wananchi watalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba yapo masuala ya kimkataba ambayo Serikali pamoja na mwekezaji inayapitia, likiwemo suala la incentives kwa maana ya vivutio, mara baada ya kukamilika, basi mradi huu utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yetu zoezi hili likikamilika kabla ya mwezi Machi, basi kweli mradi huu utaanza mara moja.
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika mwaka 1977, mpaka
leo hii ni miaka 40. Shirika hili limekuwa likisuasua sana lakini moja kati ya vigezo inavyolifanya lisuesue ni kwamba hela yake ambayo ilitakiwa iingie kwenye operesheni ndiyo hiyo ambayo inatumika kuwalipa wale wastaafu wa Afrika Mashariki. Je, Serikali ina mpango gani sasa hivi kuanza kuwalipa wale wastaafu yenyewe moja kwa moja bila kutumia fedha za shirika? Pili, fedha hizi ambazo tayari Shirika la Posta linaidai Serikali ni lini zitakamilishwa kulipwa kwa sababu imefikia kipindi Shirika linasuasua, ikafikia kipindi hata ule mwaka 2016 Shirika hili lilifungiwa akaunti zake kwa sababu TRA ilikuwa inalidai sh. 600,000,000. Je, kulikuwa na fairness gani ya kufungia zile hela wakati shirika hilo linaidai Serikali shilingi bilioni tano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza Serikali ina mpango gani wa
kulipa yenyewe, naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali sasa hivi iko kwenye jitihada za kuhakikisha kuwa malipo haya yanalipwa na Serikali yenyewe na kwa kuwa tayari watumishi wote wa Shirika la Posta wanaendelea kuchangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wastaafu hawa wataendelea kulipwa na Mifuko hii badala ya kulipwa tena na Shirika la Posta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni lini fedha hizi zitalipwa. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba, tutaendelea kulipa kwa kadri fedha zinapopatikana na ni jukumu la Serikali kulipa fedha hizi tunafahamu, tumejipangia mpango itakapofika Juni 30, shilingi bilioni 3.2 zote zitakuwa zimeshalipwa.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa ruhusa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto nyingi za ukaguzi kwenye shule zetu za sekondari, msingi na vyuo vya ualimu, je, Serikali haioni sasa imeshafika wakati wa kuunda mamlaka au taasisi itakayosimamia ubora wa elimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Idara zetu za Ukaguzi wa Elimu, shule za sekondari na msingi zimekuwa zikipata changamoto nyingi hasa za vyombo vya usafiri na watendaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Idara hiyo ya Ukaguzi ili iweze kufanya kazi yake katika ubora unaotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kweli Idara yetu ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan katika ukuaji wa sekta ya elimu kama ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyemiti, mwanzo idara hii ilikuwa inakaguliwa kupitia kwenye kanda zetu, lakini kwa sasa ni kanda pamoja na Wilaya, hata hivyo tunaona kwamba kuna mapungufu kidogo katika mfumo mzima, na ndio maana kupitia mabadiliko haya ya sheria tutaangalia namna bora zaidi ya kuendesha shughuli ya ukaguzi katika shule zetu za primary, sekondari na vyuo. Hali kadhalika kwa upande wa uwezo wa Idara za Ukaguzi, ni kweli kuna mapungufu hasa yanayotokana na vifaa kama vitendea kazi kama magari, ofisi na Wizara imeshaona hilo na tayari tumeshaanza kufanyia kazi, tayari kuna magari yamekuwa yakipelekwa kwenye Wilaya na mwaka huu tumeagiza magari mengine kwa ajili ya kupeleka kwenye Wilaya nyingine na wakati huo huo tunatarajia pia kwa mwaka huu kuanza kujenga angalau ofisi 100 kwa ajili ya wakaguzi katika Wilaya zetu.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tarehe 19 Aprili, 2016 niliuliza swali hili hili katika Bunge hili hili. Bunge lilielezwa kwamba fidia ingeweza kulipwa Juni, 2016 na mradi kuanza Machi, 2017. Je, tushike kauli ipi kati ya haya majibu mawili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mwekezaji tayari anayo hela, yuko tayari kulipa, kwa nini Serikali isichukue jukumu la kulipa fidia ili wale wananchi wale waendelee na shughuli zao nyingine za kiuchumi halafu mwisho Serikali itakapokuwa tayari ije ichukue kwa mwekezaji hiyo hela ambayo tayari anayo sasa hivi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ametaka kujua achukue kauli ipi ya Serikali kati ya jibu nililompa tarehe 19 Aprili na hili ninalompa leo. Katika jibu langu nimeeleza kwamba Serikali imechukua hatua ya kupitia makubaliano na mwekezaji ili kuhakikisha kwamba uwekezaji unaowekezwa unakuwa na manufaa kwa Watanzania na kwa mwekezaji. Mheshimiwa Ngalawa huo ndiyo mchezo wa siku hizi, Serikali itahakiki kuhakikisha uwekezaji unaowekezwa unaleta tija kwa mwekezaji na kwa Watanzania. Naogopa usije ukanirudia mwaka 2030 nikiwa Mbunge niko hapa Waziri ukaniuliza mbona mmeacha mashimo Ludewa, nitashindwa kukujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kulipa fidia Serikali, nina imani hii timu yangu inayofanya kazi, nayoisimamia mimi mwenyewe, hatuondoki hapa Bungeni bila kukubaliana. Wawekezaji wako Dodoma, watendaji wangu wote wako Dodoma, mimi nawasimamia mwenyewe lazima tukubaliane Mchuchuma na Liganga ianze.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ukijaribu kuangalia suala hilo jinsi lilivyo, hawa wote walikuwa wanastahili kulipwa lakini kilichotokea ni kwamba wenzao walikuwa na uwezo wakaajiri advocate na kwenda mahakamani.
Je, Serikali haioni busara kwa sababu kesi hiyo ni kama inawahusisha wote isipokuwa tu hawa wengine hawakuwa na uwezo wa kumpata advocate kwamba hata hawa wakienda mahakamani watalipwa sawa na kama ambavyo wenzao wamelipwa?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngalawa kwamba majibu ya Naibu Waziri katika swali lake la msingi amesema msingi wa malipo yale na hawawezi wakalipa kwa madai ambayo hayajathibitishwa kisheria. Natambua pia kwamba hawa wafanyakazi wamemuomba Waziri wa Katiba na Sheria kusudi wapate fursa ya kufungua mashauri. Kama wanataka kufanya ambavyo wenzao walifanya basi wafungue kesi, lakini Serikali haiwezi kulipa tu madai ambayo hayajathibitishwa kisheria.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kuipongeza Serikali kwa kuanza na miundombinu wezeshi ili miradi hii ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga iweze kuanza. Mfano ni ile barabara ya kutoka Mchuchuma kupitia Kijiji cha Ibumi - Amani mpaka Mundindi ambako Liganga ipo. Sasa maadam kuna timu ya wataalam ambayo imeundwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaongea na mwekezaji.
Je, timu hii ya wataalam itachukua muda gani kumaliza mazungumzo yao na kufanya miradi hii ya Mchunchuma na Liganga ianze ikiwa ni pamoja na kulipwa na fidia?
Pili, kwa nini Serikali isichukue jukumu la kulipa fidia ili kuwafanya hawa waliopisha huu mradi wa Liganga na Mchuchuma waendelee na shughuli zao huku yenyewe ikiendelea na mazungumzo na mwekezaji?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianzie kumshukuru sana Mheshimiwa Deogratias Ngalawa kwa pongezi alizotumpa Serikali, lakini pia tumshukuru na kumpongeza yeye mwenyewe kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kabisa nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wanachi wa Ludewa hususani katika maeneo ya Mchuchuma na Liganga kwa uvumilivu wa kuona kwamba mradi huu unaendelea kushughulikiwa kwa manufaa ya nchi wakati wakisubiri fidia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Mchuchuma na Liganga ni mradi ambao ni wa kimkakati, kuna maliasili kubwa sana ambayo ipo pale. Mlima wa Liganga ambao ni chuma tupu, mimi mwenyewe nimeshafika pale, lakini pia na makaa ya mawe ambayo yapo Mchuchuma ni kiasi kikubwa sana cha rasilimali ya nchi ambayo majadiliano yake lazima yafanyike kwa kina na tuweze kuona kwamba tunapata haki kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo nikijibu kwa pamoja, niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikitoa fidia katika baadhi ya maeneo, lakini sasa tunaona fedha nyingi ya Serikali imekuwa ikikaa mahali wakati mwekezaji anakuwa bado hajapatikana, kiasi kwamba ingeweza kutumika pia katika kutengeneza miundombinu wezeshi maeneo mengine.
Hivyo mkakati wa Serikali sasa hivi ni kuona kwamba tunamshawishi mwekezaji achukue pia na dhamana ya kulipa fidia kwa wananchi katika maeneo ya uwekezaji. Kwa misingi hiyo nikupe tu uhakika kwamba tutajitahidi kwa kila hali kuhakikisha kwamba majadiliano yanaenda kwa kasi, lakini sio kasi tu kuwa yenye tija kwa faida ya wananchi wa Tanzania.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini hasa Mkandarasi ataanza kujenga minara hiyo ya mawasiliano ya simu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, baada ya majibu hayo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, je, wananchi waishio Tarafa ya Mwambao mpakani mwa nchi ya Malawi, ni lini wataanza kupata mawasiliano hayo.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumeongea naye siku za nyuma, taratibu za manunuzi siyo rahisi sana mimi kama Waziri kuja hapa kutamka, kwa sababu siwezi kuziingilia taratibu za manunuzi. Taarifa niliyopewa kutoka kwenye Bodi imeniambia kwamba Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya hayo maeneo manne lakini hawawezi kunitajia mpaka taratibu zile zingine zikamilike za kum-engage huyo Mkandarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge, asubiri taratibu hizo za manunuzi zitakapokamilika ambazo nina uhakika hazitachukua muda mrefu kabla ya mwezi huu kuisha tutamjulisha lini kwa sababu inakuwa ndani ya mkataba wa yule Mkandarasi, anatakiwa aanze lini na akamilishe lini, tutakapokamilisha hilo tutamjulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la lini mawasiliano yataanza kupatikana nalo litajibiwa vizuri zaidi baada ya ule mkataba kati ya UCSAF na Mkandarasi kukamilika. (Makofi)
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Shirika hili la Posta na Simu limekuwa likijiendesha kwa kusuasua sana na moja kati ya mambo ambayo yanaifanya shirika hili lisuesue ni hela za pensheni inayolipa wale waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki. Je, Serikali haioni sasa umeshafika wakati kulitua mzigo shirika hili ili iweze kulichukua hilo jukumu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, malipo ya pensheni kwa hawa wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inalipwa kama kawaida, lakini kuna mabadiliko ambayo yalifanyika Julai, 2015 kupanda kwa pensheni kutoka Sh.50,000 kwenda Sh.100,000, lakini kuna baadhi ya hao wastaafu hawajabadilishiwa hizo pensheni zao, mfano, Mr Mbalamwezi. Je, ni lini Serikali itawabadilishia pensheni hizo ili ziwe sawa na wenzao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu inafanya jitihada zote na kwa sasa tunapoongea na namshukuru Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba kwa sasa wastaafu hao wanalipwa inavyotakiwa na pale tu wanapokuwa wameshalipwa na Shirika la Posta, Shirika la Posta linapowasilisha madai hayo Hazina walikuwa wakilipwa na hakuna madai mengine yoyote ambayo yamebaki. Kwa hiyo, tupo current kila mwezi wanapokuwa wamelipa wanaleta madai na Hazina imekuwa ikifanya malipo hayo kwa Shirika letu la Posta.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa sasa tusubiri mfumo huu wa kiutaratibu wa kuunganisha Mifuko utakapokamilika then Serikali itafanya maamuzi ya aidha, wastaafu hawa wahamishiwe kwenye moja ya Mifuko hii au wahamishiwe hazina moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwamba ni lini watalipwa, nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu hapa kwamba Mifuko yetu yote ilishaanza kulipa ongezeko lile la pensheni na wastaafu waliobaki kama alivyotaja ni mmoja mmoja na tumekuwa tukishughulika na kila kesi ya mstaafu anapokuja, kila mstaafu ana mambo yake tofauti ambayo yamesababisha kwa nini wasiongezewe pensheni hii na sisi tumekuwa tukishughulika nao. Kwa huyu aliyemtaja kama kweli hajaanza kulipwa tunamwomba afike Hazina na hili tutaweza kulishughulikia. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyopo katika Jimbo la Longido ni sawa kabisa na matatizo ambayo yapo katika Jimbo la Ludewa. Jimbo la Ludewa kwa sasa lina upungufu wa walimu 500 wa shule za msingi. Je, Serikali ina mpango gani kutuletea walimu wa shule ya msingi katika Jimbo la Ludewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Deo Ngalawa kwa kunirejesha vizuri katika kumbukumbu zangu kwamba tunaendelea na mchakato chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi Baraza la Mitihani linaendelea kuchakata na kuvikagua vyeti vya walimu 1,0140 ambao tunategemea waajiriwe kwa ajili ya shule za msingi ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Ngalawa tuendelee kuwasiliana ili tutakapofika wakati wa kuwapangia maeneo ya kwenda, basi tuwe na mawasiliano ya karibu. Ahsante.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2016/2017 uliwekwa mpango wa kujenga bwawa la umwagiliaji la Bonde la Mto Ruhuhu ambalo linahusisha Wilaya ya Nyasa na Wilaya ya Ludewa. Je, mpango ule umefikia wapi kwa sababu kwenye bajeti ya mwaka huu hatujauona?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge lakini kikubwa tunatambua kabisa kilimo cha umwagiliaji ndiyo kitakachotoa Watanzania na kufikia azma ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sisi kama Wizara tumeona kumekuwa na changamoto kubwa sana katika miradi ya umwagiliaji. Moja, miradi imekuwa mingi lakini haijakamilika na hata iliyokamilika imekuwa ikilima msimu mmoja tu kwa sababu hakuna chanzo cha maji. Kwa hiyo, tunapozungumzia umwagiliaji maana yake ni kilimo mbadala. Wizara kwa kupitia wahisani wetu wameona haja sasa ya kupitia miradi yote ya umwagiliaji ili tuwe na mpango mahsusi utakaoweza kusaidia miradi michache lakini itakayokuwa na tija katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wananufaika na kilimo cha umwagiliaji. Baada ya mapitio hayo na katika eneo la Jimbo la Ludewa tutaangalia namna ya kuweza kusaidia jimbo hilo. Ahsante sana.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Tatizo la maji katika Wilaya ya Ludewa limekuwa ni la kudumu na ikizingatiwa kwamba Wilaya ya Ludewa ina vyanzo vya maji vingi sana. Je, Serikali inajipangaje katika kuhakikisha kwamba Ludewa inapata maji ya uhakika hususan Ludewa Mjini na Mavanga?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge wa Makambako pamoja na Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Mheshimiwa Mbunge wa Makambako, kwanza kabisa tunaishukuru Serikali kwamba mkataba wa kifedha kati ya Serikali ya India na Tanzania umeshasainiwa tayari. Pili, kulingana na masharti ya mkataba huo, Serikali ya India imeshaleta Wahandisi Washauri tayari, wengi ambao sasa hivi tutafanya manunuzi kupitia kwenye hilo group.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba shughuli hii inakwenda kwa kasi sana na matarajio yake ni kwamba kabla ya mwaka huu tulionao 2018 haujafika Desemba, tunataka tuhakikishe kwamba Wakandarasi wako site na wanaanza utekelezaji wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa. Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ni shahidi kwamba nilishaelekeza mamlaka yangu ya maji ya Iringa na wanaendelea kutekeleza miradi katika Jimbo lake na mwaka huu tumetenga fedha. Kwa hiyo, tutaendelea kutekeleza pamoja na pale Mjini ambapo mimi mwenyewe nilipatembelea, tutahakikisha kwamba tunawapatia maji safi na salama wananchi wake. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wananchi wa Jimbo la Ludewa huwa wana kawaida ya kujiongeza. Miradi mingi ambayo inafanyika kwenye Jimbo la Ludewa wananchi wanakuwa wameianza kabla ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni shahidi alipofika maeneo ya Mlangali alishakuta watu wameshajichangisha shilingi milioni 90 na wakawa wanaiomba Serikali shilingi milioni 50 kwa ajili ya kumalizia. Niishukuru Serikali ilitupa ile hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna miradi mbalimbali inaendelea kwenye Kata ya Mavanga na Ludewa Mjini. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia na kuhakikisha mfano miradi ile ya Ludewa Mjini, Iwela na Lifua inakamilika katika kipindi kifupi iwezekanavyo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama na kwa muda mfupi. Kwa hivyo, nitahakikisha kwamba miradi ya Ludewa Mjini na maeneo mengine aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tutatekeleza kwa muda mfupi ili Watanzania wa maeneo yale na maeneo mengine yote Tanzania waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Serikali kwa kutupatia fedha hizo shilingi milioni 500 na ni kweli Mkandarasi G.S Contractor yupo site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nazungumza kwamba tuna baadhi ya vijiji wananchi wa Tanzania walioko kule hawajawahi kuona gari, baiskeli wala pikipiki, hiyo imeshuhudiwa hata na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Nditiye tulipokuwa naye kule. Je, baada ya kuwa tayari kipande hiki kidogo tumeshakipata, TARURA ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inafanya kazi hiyo kwa haraka ili Vijiji vya Makonde, Kilondo, Nsele, Lumbila, Nkanda, Nsisi na Lifuma viweze kupata barabara? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, kazi ambayo inaenda kufanyika ni kufanya usanifu kujua gharama ambazo zitatumika katika ujenzi wa barabara hii ni kiasi gani ili hatua ya pili iweze kufuata. Pia mimi mwenyewe nimepata fursa ya kutembelea Wilaya ya Ludewa, Jimboni kwa Mheshimiwa, kama kuna maeneo ambayo jiografia ni changamoto ni pamoja na eneo la Ludewa, ndiyo maana unaona kwamba kipande kidogo kinagharimu kiasi kikubwa cha fedha kama hivyo ambavyo nimetaja katika jibu langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, maeneo ya Lupingo ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba yanafikika kwa njia ya barabara. Avute subira, nia ya Serikali ni njema yeye mwenyewe anashuhudia, naomba tuvumiliane hili litakamilika kwa wakati. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Bonde la Mto Ruhuhu ambalo linaunganisha Wilaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa, liliwekwa kwenye bajeti ya 2016/2017 juu ya ujenzi wa bwawa la umwagiliaji. Cha kushangaza, katika miaka hii miwili bwawa lile halipo kwenye bajeti. Je, Serikali ina mpango gani na ujenzi wa Bwawa la Mto Ruhuhu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, tunatambua umuhimu wa umwagiliaji, lakini katika suala zima la umwagiliaji tangu tumeingia katika Wizara hii tumekuta changamoto kubwa sana. Kutokana na changamoto tulizobainisha katika umwagiliaji, Waziri wangu akaona haja sasa ya kupitia mpango kabambe wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ya mwaka 2002 ili tuweze kubainisha zile changamoto na kuweza kuzipatia majibu.
Mheshimiwa Spika, tumeona baadhi ya miradi ya umwagiliaji imejengwa lakini haijakamilika, vile vile hata hiyo iliyokamilika imekuwa ikiwasaidia wakulima katika kuvuna msimu mmoja wakati tunapozungumzia umwagiliaji ni mbadala kwa maana ya wakulima waweze kulima kiangazi na hata masika.
Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya mapitio, sisi kama Wizara ya Maji na Umwagiliaji, tutaona umuhimu wa kuhakikisha kwamba tunampa kipaumbele, wananchi wake waweze kupata kilimo cha umwagiliaji.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ludewa kijiogrofia ni tambarare, milima na mabonde na kwa maeneo mengi inayosikika inasikika Redio Malawi. Je, ni lini TBC itasikika maeneo ya Ludewa yote?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeshajibu kwamba, katika mwaka wa fedha 2018/2019 TBC imetengewa bajeti ya shilingi bilioni tano. Kati ya mikoa ambayo itashughulikiwa ni Mkoa wa Njombe. Kwa sababu natambua kabisa kwamba Wilaya ya Ludewa ipo ndani ya Mkoa wa Njombe, kwa hiyo, ni hakika kabisa kwamba TBC ndani ya mwaka huu wa fedha itaweza kusikika na maboresho makubwa yatafanyika katika Wilaya hiyo ya Ludewa pamoja na Mkoa mzima wa Njombe.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kutokana na usanifu ambao unafanyika sasa na timu ya wataalam wa bandari ili eneo hili liweze kupatiwa vituo vya kushusha na kupakia abiria, je, timu hii ni lini itamaliza kazi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tayari kuna tengo la mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kujenga gati katika Bandari za Lupingu na Manda. Je, wananchi hawa ambao walipisha maeneo haya watalipwa lini fidia yao ili waendelee na shughuli nyingine? (Makofi)
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA - NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana huduma ya usafiri wa majini lakini huduma ya usafiri wa nchi kavu. Niseme tu kwamba zoezi hili litakamilika kwa muda mfupi kwa sababu hivi ninavyozungumza wataalam wanaelekea maeneo haya na najua adha wanayoipata wananchi kule ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, litakapokuwa limekamilika, siyo lazima vijiji vyote alivyovitaja tuweze kuweka vituo vya kushusha na kupakia lakini wataweza kutambua maeneo gani ambayo yatawafanya wananchi hawa wasisafiri sehemu ndefu sana kwa ajili ya kupata huduma. Kwa hiyo, avute subira na sisi tutampa mrejesho. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo haya watoe ushirikiano ili tupate information za kutosha tuweze kukamilisha zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wale wananchi ambao wanapisha maeneo yao kwa ajili ya maendeleo na sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba fedha zikipatikana tunawalipa mara moja. Kwa sababu tunajua kwamba fidia kama itachelewa kulipwa pia huduma itachelewa kwenda kwa wananchi hawa.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu hivyo vijiji alivyovitaja nilizunguka naye kuanzia kijiji kimoja mpaka cha mwisho. Kwa hiyo, anaelewa vizuri umbali wa bandari kutoka bandari moja kwenda bandari nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na azma nzuri ya Serikali ya kujenga gati katika eneo la Wilaya ya Ludewa, Mwambao wa Ziwa Nyasa, je, ni lini hasa hivyo vijiji alivyovitaja kwa maana ya Yigha, Makonde, Nsele, Chanjale, na Nkanda vitapata huduma hiyo ya kupakia na kushusha abiria?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa sababu tulikuwa naye Mheshimiwa Naibu Waziri katika ziara ile na ameona malalamiko na usumbufu ambao watu wanaupata. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia na kuhakikisha kwamba wanaondokana na kero hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deogratias Ngalawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilifanya ziara ya Mwambao wa Ziwa Nyasa, Tarafa ya Mwambao tukiwa na Mheshimiwa Deogratias Ngalawa ambapo nilipata nafasi ya kupitia vijiji vyote alivyovitaja. Nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana na kubwa anayoifanya kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya meli katika eneo lile ambalo lina changamaoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mbunge kwamba baada ya mchakato wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao utajumuisha pamoja na mambo mengine kulipa fidia, ambayo nichukue tena nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Deo Ngalawa kwa jinsi anavyoishi vizuri na wananchi wake na wanavyotoa ushikiano kwa TPA, tuna hakika baada ya taratibu hizo ujenzi utaanza mara moja. Nimhakikishie tu kwamba kabla ya Juni, 2019 lazima baadhi gati zitaanza kutumika na wananchi wataanza kupata huduma hiyo.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, Wilaya ya Ludewa eneo la Kandokando mwa Ziwa Nyasa kuna vijiji takribani kumi na mbili, gari, baiskeli wala pikipiki haijawahi kufika huko. Niishukuru Serikali kuna kipande cha Mwambahesa kwenda Makonde, kimeanza kufanyiwa kazi. Je, TARURA inafikiriaje sasa kutuongezea wananchi wa Ludewa hususani waishio kandokando wa Mwambao wa Ziwa Nyasa kutoka eneo la Makonde mpaka kihondo ili tuweze kupata barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kutembelea jimbo la Mheshimiwa Ngalawa, kama kuna maeneo ambayo kuna changamoto ya milima maana kule milima ya Livingstone ndio inapita kule, ukanda ule, ni ukanda wa kutizama kwa jicho tofauti kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Mbunge naye amekiri kwamba kuna kazi nzuri ambayo inafanyika juu ya kuhakikisha kwamba wananchi wale wanakuwa na barabara ambayo inapitika vipindi vyote. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo wako wananchi wetu, barabara zinapitika vipindi vyote, kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu na yeye pia tutahakikisha kwamba wananchi wake wanapata barabara ya uhakika.
MHE. DEORATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Eneo la Manda ni bandari nzuri ambayo ingeweza kutumika ku-tap soko la nchi ya Malawi. Eneo la Malawi au nchi ya Malawi ina tatizo kubwa sana la bidhaa au vyakula kama mahindi na kadhalika ambako Ludewa mahindi yanalimwa kwa wingi kiasi ambacho mengine yanaoza kwenye maghala. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kujenga hicho Kituo cha Forodha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili. Utaratibu wa kupata forodha ni kama ulivyoelezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha. Je, baada ya kuandika proposal hiyo inachukua muda gani mpaka kukamilika kwake? Ahsante.
NAIBU WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ngalawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza alivyoanza kuipongeza Serikali kwa kufungua miundombinu kuwafikia wananchi ambao walikuwa hawajafikiwa nami naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba niwapongeze sana wananchi wa Manda kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya shughuli za kiuchumi zinazowaondoa katika mzunguko wa umaskini kama ambavyo wenzetu wanaendelea kutangaza sifa za Taifa hili ambazo si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambe Watanzania kwamba Taifa hili, alisema Mheshimiwa Waziri wa Fedha siku mbili zilizopita, kwamba kiwango cha umaskini kimepungua kwa kiwango kikubwa na sasa tunasubiri utafiti huu watakapotoa matokeo yao rasmi (household based survey) Watanzania wataona na wapuuze haya yote yanayoendelea kuenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalisema kwa sababu sisi kama Serikali tunaitambua Manda kama eneo la kimkakati na ndiyo maana Bunge lililopita nilipojibu swali la 73 la Mheshimiwa Mbene kuhusu ujenzi wa Kituo cha Forodha Ileje na swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngalawa nilimwambia tayari Serikali na namhakikishia tumeshaanza kufanya utafiti, tunachosubiri ni maombi hayo rasmi kutoka kwenye mkoa ili nasi tuifanyie kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwamba kwa muda gani unachukuliwa; kwa sababu tumeshaanza utafiti kama Serikali, namhakikishia, tutakapopata maombi hayo, tutayawasilisha rasmi Wizara ya Afrika Mashariki ili waweze kuwasilisha katika Sekretarieti ya Afrika Mashariki na haitachukua muda kwa sababu Manda ni eneo la kimkakati kwa Taifa hili.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sera ya Viwanda Tanzania imetamalaki. Sasa nipende kumuuliza Mheshimiwa Waziri Kiwanda cha Kufua Chuma pale Liganga kitaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ngalawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi chuma cha Liganga kinahitaji uwekezaji mkubwa sana na pale tunazungumzia kuwekeza katika suala la ufuaji wa chuma, ambacho kimechanganyika na madini ya aina nyingine ikiwemo Titanium, Vanadium na Aluminium; wakati huo huo kuna suala la kufua umeme. Hayo yote yanafanyiwa kazi na ikizingatiwa kwamba hivi karibuni tulipitisha sheria zetu ya kutunza rasilimali zetu na kuwawezesha Watanzania kunufaika zaidi, hayo yote yanaangaliwa kwa umakini na tutakapo kuwa tayari, shughuli hiyo itaanza mara moja.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo Igalula, Jimbo la Ludewa lina eneo kubwa sana ambalo halina mawasiliano ya simu. Hivi karibuni imejengwa minara katika Tarafa ya Mwambao lakini minara ile toka ilipowashwa imeongea kwa siku tatu tu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri kuna tatizo gani minara imejengwa imewashwa siku mbili na baada ya hapo mawasiliano hakuna pamoja na ujenzi wa Kijiji cha Ibumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwishatembelea Kata ya Mwambao ambayo iko mwambao wa Ziwa Nyasa na nimekwishavitembelea vijiji mbalimbali kuanzia Lupingu, Higa, Makonde ambako kweli kabisa kulikuwa kuna tatizo kubwa sana la mawasiliano. Mheshimiwa Deo ambaye ni mfuatiliaji mkubwa sana wa suala la mawasiliano ni shahidi kwamba ndani ya miezi mitano toka nimetembelea eneo hilo tumekwishaweka minara tisa (9) ya mawasiliano kwa ajili ya wananchi wa eneo la Mwambao. Minara mitatu (3) ambayo sasa hivi haifanyi kazi ilipata hitilafu kidogo na hivi sasa tunapozungumza tumetuma wataalam kutoka Halotel wanakwenda kurekebisha hitilafu hiyo ili wananchi waweze kuendelea kupata mawasiliano.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mradi wa Mchuchuma na Linganga umekuwa ukizungumzwa kwa muda mrefu sana kipindi ambacho sasa mpaka wananchi na Watanzania kwa ujumla wanakata tamaa. Sasa je, Serikali haioni kwamba sasa hivi hii hela ya fidia ingeichukua yenyewe badala ya kumwachia mwekezaji na watu wetu wakapata fidia hiyo mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili tumeona jitihada za Serikali kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya kutoka Mkiu - Liganga mpaka Madaba na ya kutoka Mchuchuma mpaka Liganga kilometa 70. Je, ujenzi hasa wa lami na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanaweza kupitika yataanza lini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijaendelea na maswali ya nyongeza kwa umuhimu wake kwa niaba ya wanaviwanda pamoja na Wizara yetu ya Viwanda kwa ujumla napenda kutoa pole kwa msiba mkubwa uliotupata kupitia kifo cha mwanakiwanda au mfanyabiashara wetu Mkuu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tanzania Private Sector Foundation, Dkt. Reginald Mengi. Mwenyezi Mungu amrehemu na roho yake aiweke mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia swali la kwanza kuhusu Serikali uwezekano wa kulipa fidia, tunapotathmini mradi huu kuna njia mbili; ya kwanza ni kwa kumtumia mwekezaji aweze kulipa fidia, lakini Serikali inapokuwa na uwezo inaweza ikalipa yenyewe. Kwa hiyo, katika kuangalia mradi huu ambao una umuhimu sana kwa Taifa letu kutokana na rasilimali zilizoko pale, Serikali inaangalia uwezekano pia wa yenyewe kuweza kulipa fidia endapo itawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na barabara kujengwa kwa kiwango cha lami, hayo yote yapo katika mchakato huo wa Serikali kujipanga ili kuwezesha mradi huu ufanyike kwa tija na kwa manufaa mapana ya Taifa.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda tu niongezee kwamba Serikali inayo mpango wa kujenga kiwango cha lami kuzingatia kama Mheshimiwa Mbunge anavyozungumza katika maeneo ambayo tumeya-alert kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma. Tumemaliza usanifu wa barabara kutoka Madaba kwenda Mkiu kilomita mia moja kumi na mbili, lakini pia eneo la barabara ya kutoka Mchuchuma kwenda Liganga, ziko kilometa 72 tumesanifu, Serikali ikipata fedha maeneo hayo muhimu tutajenga kwa kiwango cha lami.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kata ya Ibumi katika Jimbo la Ludewa ni kata pekee ambayo haina mawasiliano kabisa na bahati nzuri yupo mzabuni TTCL ameanza kujenga, lakini toka alipojenga ule mnara mpaka leo hii hatujui kinachoendelea. Naomba kauli ya Serikali sasa kujua ni lini wananchi wa Kata ya Ibumi watapata mawasiliano ya simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kampuni ya mawasiliano Tanzania (TTCL) ilipewa zabuni ya kujenga mnara wa mawasilinao kwenye Kata ya Ibumi. Mpaka sasahivi ninavyoongea na Waheshimiwa Waunge, mnara huo ulikwishajengwa lakini bado haujawashwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulitokea tatizo la kiufundi katika kuwasha mnara huo, ambapo tatizo hilo sasa limerekebishwa na nimhakikishie Mbunge kwamba ndani ya siku 30, Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na TTCL watashirikiana kuhakikisha kwamba changamoto hiyo iliyojitokeza inatatuliwa na watu wa Ibumi wataendelea kupata mawasiliano.