Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Khatib Said Haji (18 total)

MHE. KHATIBU SAID HAJI aliuliza:- Mheshimiwa Spika, Sheria za FIFA zimekataza mambo yanayohusiana na mchezo wa soka kupelekwa Mahakamani:-
(a) Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya makosa yanayofanyika katika klabu za soka?
(b) Je, ni kwa kiasi gani sheria hizi za FIFA zinakinzana na Sheria za nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Sheria za FIFA zinakataza mambo yanayohusiana na soka kupelekwa Mahakamani. Hatua hiyo inalenga kuwezesha masuala yote yanayohusiana na soka kuendeshwa kwa kufuata na kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na mamlaka za mchezo huo katika ngazi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, aidha, hatua hiyo imewezesha mchezo wa soka kuchezwa na kupata matokeo kwa wakati na hivyo kuepusha mazuio ya Mahakama ambayo yanaweza kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa washiriki wengine.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huo unazifanya mamlaka mbalimbali zinazosimamia mchezo huo kuwa na Katiba zinazowawezesha kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi dhidi ya malalamiko, rufaa na kero za wadau wa klabu au chama cha soka husika.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa vyama, vilabu na mashirikisho ya mpira wa miguu kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba zao ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika uendeshaji na uendelezaji wa soka nchini.
(b) Mheshimiwa Spika, maendeleo ya michezo hapa nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 6 ya mwaka 1971. Sheria hii ni kongwe na ina baadhi ya mambo ambayo yanakinzana na Sheria za FIFA. Serikali inafanya mapitio ya sheria hiyo ili iendane na wakati kwa lengo la kuboresha na kuendeleza michezo nchini.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamezidi kuongezeka siku hadi siku na kusababisha madhara na vifo kwa watu wasio na hatia:-
Je, Serikali inafanya juhudi gani ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili huu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya mtu ama watu kujichukulia sheria mikononi ni uhalifu ambao umeanza kushamiri katika jamii yetu ikiwemo Visiwa vya Zanzibar katika kipindi cha mwaka 2013/2014. Jumla ya matukio 2,041 yaliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 kulikuwa na matukio 1,112 ambapo Zanzibar yaliripotiwa matukio 14. Mwaka 2014 yalipungua na kufikia matukio 929, kati ya hayo Zanzibar yalikuwa ni matukio matano. Aidha, matukio yote yalichukuliwa hatua stahiki ikiwemo wahusika kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, limekuwa likichukua hatua mbalimbali za kupambana na wimbi la uhalifu huo, miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kufuata sheria. Aidha, Jeshi la Polisi huwakamata na kuwafikisha Mahakamani watu wanaojichukulia sheria mkononi, kutenda makosa mbalimbali ya jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu, kutoa rai kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, naomba Waheshimiwa Wabunge wote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha wananchi kuepuka vitendo hivyo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa huduma za dawa bila malipo kwa baadhi ya maradhi kama vile UKIMWI, TB na kadhalika:-
(a) Je, ni maradhi ya aina gani yaliyo katika orodha ya kupatiwa dawa bila malipo?
(b) Je, ni kwa kiasi gani Serikali imefanikiwa kufikia malengo katika mpango huo wa kusaidia wananchi kupata dawa hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde, lenye Sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu cha 5.4.8 (3) kuhusu msamaha wa uchangiaji wa gharama za huduma za afya kwa makundi maalum ambayo yanapatikana (uk.29) wa Sera ya Afya, inayataja maradhi ambayo yatatibiwa bure kuwa ni Saratani, UKIMWI, Kisukari, magonjwa ya Moyo, Pumu, Seli Mundu (Sickle cell), Kifua Kikuu, Ukoma na magonjwa ya akili.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wagonjwa wote walioandikishwa na wenye vigezo vya kupata dawa zinazotolewa bure wanapata dawa hizo.
Kwa mfano, kwa magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu, aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge kwenye swali lake, wagonjwa wote kwa asilimia 100, walioandikishwa na wenye vigezo wanapata dawa hizo bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mara chache sana hutokea wagonjwa wakakosa dawa. Serikali inaendelea kuongeza fedha za bajeti ya dawa pamoja na kutumia asilimia 50 ya mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha pale penye upungufu wa dawa zinakuwepo kwa ajili ya kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Kumekuwa na mfululizo wa migomo, misuguano na migongano ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wa viwandani na Kampuni binafsi zinazotokana na malalamiko ya mishahara na maslahi ya wafanyakazi:-
Je, ni mfumo upi na viwango gani vilivyowekwa kisheria wanavyotakiwa kulipwa wafanyakazi wa viwanda na Kampuni binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika katika kupanga viwango vya chini vya mshahara unasimamiwa na taratibu zilizoainishwa katika Sheria Na. 7 ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, sheria imetoa madaraka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, kuunda Bodi ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi. Bodi hii inaundwa na Wajumbe 17 ikiwa na Wawakilishi wa Wafanyakazi, Waajiri na Serikali. Majukumu ya Bodi hii ni kupanga kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha chini cha mshahara kilichopangwa na kinachoendelea kutumika hadi sasa katika Sekta ya Viwanda ni shilingi 100,000/= kwa mwezi na viwango vingine vya mshahara katika sekta 12 vimetajwa kwa GN.196 ya mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)(a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Rais anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani.
Je, Rais anayo mamlaka kisheria ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 45(1)(a) mpaka (d) inampa Rais mamlaka ya kwanza kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama, pili kumuachilia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa au kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote, tatu, kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu na nne kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na mahakama. Watuhumiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako katika hatua ya upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo basi, Rais hawezi kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchungu, upelelezi au mahakamani. Hatma ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka husika za uchunguzi, mashitaka na mahakama.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza hapa nchini kutokana na kuchelewa kwa upelelezi wa mashauri mengi.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji huo wa kesi zilizopo mahakamani?
(b) Je, ni muda gani umewekwa kisheria pale upande wa mashtaka unaposhindwa kupeleka ushahidi mahakamani ili mahakama iweze kumuachia huru mshitakiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiri, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali na za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji wa kesi mahakamani ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa majalada ya kesi unaofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuundwa kwa Jukwaa la Haki Jinai na kutembelea mahabusu magerezani na kufanya mahojiano na mahabusu gerezani ili kushirikisha wadau wengine wa sheria katika kesi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa kisheria wa kuondoa shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika ni siku 60 na mtuhumiwa kuachiwa huru.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani hasa katika Miji Mikuu ya nchi yetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani kupunguza tatizo hilo ili watoto hao walelewe katika mazingira salama na maadili halisi ya Kitanzania?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa sana, kaka yangu Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kumekuwa na ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa katika miji mikubwa. Kwa mujibu wa takwimu zilizofanyika katika Majiji ya Dar es Salaam na Mwanza mwaka 2012 zilionesha kuwa Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na watoto 5,600 kutoka mikoa kumi ya Tanzania ambayo ni Dar es Salaam yenyewe 28%, Dodoma 9%, Mwanza 7%, Morogoro 7%, Tanga
6%, Lindi 6%, Iringa 5%, Pwani 5%, Kilimanjaro 5% na Arusha 4%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inalo jukumu la msingi kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto. Katika kutekeleza wajibu huu, Serikali kwa kushirikiana na wadau, inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuwezesha jamii kuwa na mipango shirikishi ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wa mitaani. Hadi sasa mpango huu unatekelezwa katika Halmashauri 111 nchini.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI imeanzisha mpango wa kuimarisha ulinzi na usalama kwa watoto ambapo Halmashauri 51 zimewezeshwa kuunda timu za ulinzi wa watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kueneza mpango huu katika Halmashauri nyingine nchini.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
(a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani?
(b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE,
KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze muuliza swali leo kwa kukaa upande ule alioulizia swali. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Kimataifa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha ari ya wananchi kujitegemea na kuwekeza katika maeneo mbalimbali katika Taifa letu; kuwa ni chombo pekee cha kujenga umoja, mshikamano na kudumisha amani pale ambapo Mwenge unapita bila kujihusisha na itikadi za kisiasa; kuendelea kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa Watanzania wa pande mbili za nchi yetu; na kila mwaka hufungua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya wananchi na kuhamasisha uzalendo wa kuendelea kujitolea. Mfano mzuri ni kutokana na takwimu zilizopo ambazo zinaonyesha miradi ya maendeleo iliyozinduliwa pamoja na kuwekwa mawe ya msingi kupitia Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2015/2016 ni pamoja na miradi 1,342 yenye thamani ya shilingi 463,519,966,467.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kimataifa Mwenge
wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana na maudhui yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu kwa kuwa msuluhishi wa amani katika Bara la Afrika na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ya Afrika duniani kote. Umoja, mshikamano, upendo na ukarimu wa Watanzania ni matunda pia ya Mwenge wa Uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na faida na mafanikio makubwa yanayopatikana kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru, Serikali inaamini kuwa zipo faida za kuendelea kukimbiza Mwenge huo wa Uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali haina mpango wowote wa kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru. Dhana hii itakuwa ni endelevu na tungependa kuiendeleza kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa kusisitiza misingi hii bila kuchoka.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la tatizo la Wanaume kupungukiwa nguvu za kiume, jambo ambalo linaleta tafrani kubwa na kusababisha ndoa nyingi kuvunjika na zilizobakia kuwa katika hali ya mashaka:-
(a) Je, Serikali inalijua tatizo hilo?
(b) Kama inalijua, je, inachukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, nijibu swali hili muhimu la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa tatizo hili japokuwa hakuna jibu la moja kwa moja la kufahamisha umma ukubwa wa tatizo hili, kwa sababu tendo la ndoa ni tendo ambalo hufanyika katika mazingira ya usiri kati ya wanandoa wenyewe.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuelezea kwa kifupi ni jinsi gani mwanaume hupungukiwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili kwa kawaida huwapata kwa kiasi kikubwa watu wenye umri mkubwa, hasa kuanzia umri wa miaka 60 na wagonjwa wenye magonjwa sugu mbalimbali kama vile shinikizo la damu, kisukari, kifua kikuu, kansa, UKIMWI na wale wanaotumia dawa kwa muda mrefu. Hata hivyo, mwenendo wa tatizo hili kwa sasa umekuwa hauzingatii umri kuwa mkubwa, linawapata watu wa rika zote, vijana na hata watu wazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wazee tatizo la nguvu kupungua kwa mara nyingi ni jambo la kawaida na naomba ieleweke kwamba, kwa wanaume kadri umri unavyozidi kuongezeka uwezo wa kufanya tendo la ndoa unapungua taratibu. Pia, huchangiwa na ukosefu wa afya njema.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiwataka Watanzania waliopo nje ya nchi kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini ili kusaidia kukuza uchumi wetu na hatimaye kuongeza ajira kwa Watanzania.
Je, kwa nini Serikali inashindwa kuweka Sheria ya Uraia wa Nchi Mbili ili iwe rahisi kwa Watanzania hao kuitikia wito huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Diaspora na Balozi zetu nje ya nchi zina utaratibu wa kuwatambua na kuwahamasisha diaspora wenye ujuzi wa taaluma mbalimbali kuja kuwekeza kwa wingi nchini kupitia sekta ya kiuchumi, kuleta ujuzi, elimu na utaalamu wanaoupata huko ughaibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya uraia wa Tanzania yanasimamiwa na Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 ambayo imebainisha kuwa uraia wa Tanzania upo katika makundi matatu, uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajinisi. Aidha, sheria hii kupitia kifungu cha 7(4)(a)(b) kimeeleza bayana kuwa raia wa Tanzania anaacha kuwa raia kwa kigezo cha kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hivyo basi, kutokana na sheria hii na sera ya Tanzania kuhusu uraia ambayo hairuhusu wala kutambua uraia wa nchi mbili, Serikali haiwezi kuweka sheria ya uraia pacha kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili lilijadiliwa pia wakati wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, Bunge Maalum la Katiba ambalo lilijadili pendekezo hili liliona Tanzania bado haipo tayari kwa sasa na Bunge hilo Maalum likatoa pendekezo kwamba; “Mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano atakuwa na hadhi maalum kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nukuu hii imebainishwa katika Sura ya 6, Ibara ya 72 ya Katiba Inayopendekezwa ya Oktoba, 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya bado haujakamilika, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge avute subira ili mchakato huo uishe.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Kuchelewesha haki ni kunyima haki.
Je, Jeshi la Polisi limejitathmini juu ya utendaji wake, hususan katika Idara ya Upelelezi wa Makosa mbalimbali kabla ya kuyafikisha mashtaka mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upelelezi wa makosa ya jinai unafanywa kwa kuzingatia sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 Marejeo ya mwaka 2002, Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo mwaka 2002 na Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 Marejeo ya mwaka 2002, pamoja na kuzingatia kanuni za kiutendaji za Jeshi la Polisi (Police General Orders) na sheria nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya lengo la upelelezi wa makosa ya jinai ni kukusanya ushahidi utakaothibitisha kosa lililotendeka na kuripotiwa kituoni. Aidha, kuna baadhi ya makosa yaliyotendeka huhitaji muda mrefu ili ushahidi wake kuweza kupatikana, mathalani makosa ya mauaji na yanayofanana na hayo. Inapodhihirika kuwa kuna ushahidi uliopatikana unaweza kuthibitisha kosa, jalada hupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kusomwa na kuandaa mashtaka pale ambapo wanaona ushahidi umejitosheleza na kupeleka mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi hufanya tathmini ya kutosha katika utendaji wake kupitia Kitengo cha Ndani cha Tathmini na Uangalizi (Internal Monitoring and Evaluation) na kutoka kwa Waangalizi wa Nje (External Oversight) ambao hulisaidia Jeshi la Polisi kurekebisha kasoro mbalimbali za kiutendaji.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitangaza kukua kwa hali ya uchumi wa nchi yetu kila mwaka:-
Je, ni vigezo gani sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, vigezo sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote duniani ni ongezeko la pato la Taifa, ongezeko la pato la wastani la mwananchi kwa mwaka, ongezeko la uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, kupungua kwa uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, utulivu wa bei za bidhaa na huduma, utulivu wa viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni na kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo na huduma za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji unaofanywa katika nchi ni kigezo kingine cha msingi cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa huongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na huduma, ajira, kipato cha mwananchi mmoja mmoja, pato la Taifa na hatimaye kupunguza umaskini katika jamii. Aidha, mchango wa Serikali katika ukuaji wa uchumi ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuwekeza zaidi kwenye shughuli zinazochochea ukuaji wa uchumi, kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa na huduma nchini.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
Viwango vya riba katika benki hapa nchini ni vikubwa na vimekuwa ni kikwazo kwa Watanzania wengi kuweza kukopa na kufanya biashara:-
Je, Serikali inachukua hatua gani ili Benki ziweze kupunguza viwango hivyo vya riba?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara huria ya sekta ya benki ilianza tangu mwaka 1991 mara baada ya kupitishwa wa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya mwaka 1991. Kupitia sheria hiyo, wawekezaji walifungua benki binafsi hapa nchini na gharama za huduma za bidhaa kuamuliwa na nguvu ya soko. Hivyo basi kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Benki na Vyombo vya Fedha ya mwaka 1991, Serikali haina mamlaka ya moja kwa moja ya kupunguza viwango vya riba katika soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukweli kwamba bei ya huduma na bidhaa katika sekta ya fedha inaamuliwa na nguvu ya soko, Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba katika soko zinapungua. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ni kama ifuatavyo:-
(a) Kuzitaka benki za biashara kutumia mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (credit reference bureau system).
(b) Kwa sasa Benki Kuu inatoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89.
(c) Benki Kuu imeshusha riba (discount rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.
(d) Benki Kuu imepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirement) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.
(e) Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hatua hizi za kisera kuchukuliwa na Serikali, baadhi ya benki za biashara hapa nchini zimeanza kupunguza riba ya mikopo. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinaendelea kupungua. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-

FIFA inatoa misaada ya fedha kwa Tanzania kupitia TFF:-

Je, ni kiasi gani cha fedha TFF imekuwa ikiipatia Zanzibar kupitia ZFA?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli FIFA inatoa msaada wa fedha kwa mashirikisho ya mpira wa miguu ikiwepo TFF kwa ajili ya miradi na programu mbalimbali. Fedha hizo huwa ni maelekezo maalum kwa lengo la kusaidia na kuendeleza maeneo mahususi yafuatayo: Ligi ya Wanawake, ligi ya vijana, masuala ya kiutawala, kuinua vipaji kwa (Grassroot Program), Women’s Football Promotion, pamoja na Maendeleo ya Waamuzi.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka huu FIFA itakuwa inatoa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 1.25 kila mwaka kwa wanachama wake wote ikiwepo ZFA, ambayo ni sehemu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kwa mchanganuo ufuatao: fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha Dola za Kimarekani 750,000, fedha kwa ajili ya kuendesha ofisi, Dola za Kimarekani 500,000.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa muda wa miaka mitatu sasa kutokana na kutokuwepo kwa uwazi katika matumizi ya fedha na kutokidhi vigezo vya utawala bora, TFF wamekuwa hawapati fedha hizo. Kazi kubwa imeshafanyika kurekebisha dosari zilizokuwepo za kiuhasibu na kiutawala bora. Hivyo, uwezekano ni mkubwa kwa TFF na ZFA kupokea fedha za msaada huo wa fedha mapema mwaka huu.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-

Fedha za kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF), zimekuwa msaada mkubwa katika kusaidia Maendeleo Majimboni.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza viwango vya fedha hizi ili kuleta ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge Konde kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo yaani Constituency Development Catalyst Fund, ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 16 ya Mwaka 2009 yaani The Constituency Development Catalyst Fund Act, 2009. Lengo la Mfuko ni kuhakikisha miradi ambayo ni vipaumbele vya wananchi katika Jimbo husika na ambayo haikupata fedha katika bajeti inapata fedha za utekelezaji. Kwa tafsiri ya Sheria iliyoanzisha Mfuko, fedha za Jimbo ni kwa ajili ya Majimbo ya uchaguzi ambayo yameanzishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania. Vigezo vinavyotumika kugawa fedha ni ukubwa wa eneo, idadi ya watu na kiwango cha umasikini katika Jimbo husika.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiongeza fedha hizi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha ambapo mwaka 2018/ 2019, Serikali iliongeza kiasi kinachotolewa kutoka shilingi bilioni 10 zilizokuwa zikitolewa kipindi cha nyuma mpaka shilingi bilioni 12.5 na Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha fedha kinachotolewa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo umeainishwa katika Sheria ya Mfuko Kifungu Na. 10(1) kwamba kutakuwa na Kamati ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo katika kila halmashauri ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Jimbo husika. Miongoni mwa majukumu ya msingi ya Kamati hii ni kuchambua miradi inayowasilishwa kutoka kwenye jamii na kuidhinisha miradi itayotekelezwa na jukumu la Mkurugenzi Mtendaji ni kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Kamati hii. Ahsante.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-

Ni kosa la Jinai kwa Mtu au Vyombo vya Habari kutoa, kuandika, kusambaza au kutangaza habari za uongo. Je, Jeshi la Polisi linachukua hatua gani stahiki kwa watu au vyombo vya habari vinavyofanya makosa hayo?
NAIBU WAZIRI YA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linao utaratibu unaotumika pindi mtu anapokuwa ametenda makosa ya jinai ambapo ushahidi hukusanywa kisha jalada huandaliwa kwenda kwa Mwanasheria wa Serikali; na ushahidi ukijitosheleza, mtuhumiwa hufikishwa Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya Mwaka 2016 ambapo inaelekeza kuchukua hatua kwa chombo cha habari kilichotoa taarifa za uongo ikiwa ni pamoja na kufuta leseni au kusimamisha leseni kwa muda pale ambapo chombo cha habari kimekiuka masharti ya leseni hiyo.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-

Athari za mabadiliko ya tabianchi zimesababisha uharibifu mkubwa katika Bandari ya Tanga eneo la deep sea lango kuu la kuingia na kutokea katika bandari hiyo:-

Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura kudhibiti uhalibifu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said haji Mbunge wa Konde kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, athari za mabadiliko ya tabianchi zinatofautiana katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo maeneo ya Ukanda wa Pwani ambapo ni muhimu kwa shughuli za uchumi. Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na athari hizo ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2007 na Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2012. Mipango hii imeelekeza hatua za haraka za kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika sekta muhimu ikiwemo maji, maliasili, miundombinu, afya, nishati, Ukanda wa Pwani na maeneo ya bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la ufukwe lijulikanalo kama deep sea lililopo katika Jiji la Tanga linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo athari za kimazingira kama vile utupaji holela wa taka hasa za plastiki na taka zingine ambazo huletwa na mifereji ya maji ya mvua inayoingia baharini kuto katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hatua zilizochukuliwa na Serikali na Halmashauri ya Jiji la Tanga katika kuhifadhi na kulinda eneo hili dhidi ya uchafuzi wa mazingira ni pamoja na kufanya kampeni za usafi wa mazingira zikihusisha wavuvi, wafanyabiashara na vikundi vya mazingira. Pia kutoa elimu kwa wavuvi na wadau wengine katika eneo hili kuhusu usafi wa mazingira na kuhifadhi miti na uoto wa asili kuzunguka fukwe hizo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. KHATIB SAID HAJI Aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani ya dharura kukabiliana na mrundikano mkubwa wa mahabusu katika magereza nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia nichukue fursa hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa na imani na sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, nalijibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2021 idadi ya wafungwa na mahabusu nchini ilikuwa ni 33,473 kati ya hao waliohukumiwa ni 16,735 na mahabusu ni 16,738 huku uwezo wa magereza yetu nchini ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na kutatua changamoto hizo Serikali imechukua baadhi ya hatua nyingi ambazo tunaamini kwa njia moja ama nyingine zinakwenda kutatua ama kuondoa kabisa tatizo hili la mlundikano wa mahabusu katika magereza.

Kwanza Serikali imeamua ama inaendeleza ushirikishwaji wa vyombo vya haki jinai, lakini kingine kufanya mabadiliko ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2009, lakini pia ushirikishwaji wa Mahakama na Jeshi la Magereza katika kutumia mfumo wa TEHAMA (video conference), lakini kingine kufanya upanuzi na kujenga magereza mapya ya Wilaya ambazo hazikuwa na Magereza kama vile Chato na Ruangwa, lakini kingine utoaji wa dhamana kwa masharti nafuu, lakini pia kuanzishwa kwa mahakama zinazotembea (mobile court) kwa mashauri madogo madogo yanayotolewa uamuzi pasipo watuhumiwa kupelekwa magerezani. Aidha, kutoa elimu kwa raia ili, kutojihusisha na vitendo vya kihalifu, jambo ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa likapunguza mlundikano wa mahabusu katika magereza. Ahsante. (Makofi)