Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Augustine Philip Mahiga (10 total)

MHE. HAFIDH ALI TAHIR aliuliza:-
Baadhi ya Watanzania wanajitafutia maisha katika nchi mbalimbali duniani na wamepata maendeleo katika sekta mbalimbali:-
(a) Je, ni Watanzania wangapi wanajulikana rasmi kuwa wako ughaibuni, wanachangiaje maendeleo ya nchi yao na kwa kiasi gani?
(b) Je, ni Watanzania wangapi wakiwemo kutoka Tanzania Zanzibar ambao hawakufuata taratibu walipoondoka lakini Balozi zetu zina taarifa ya uwepo wao kwenye nchi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania waishio nje ya nchi wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja kote duniani. Makadirio hayo yanatokana na takwimu tunazokusanya kupitia Balozi zetu ambazo zinashirikiana kwa karibu na Jumuiya za Watanzania katika maeneo yao ya uwakilishi. Hata hivyo, idadi hiyo inaweza kuwa ndogo kwa kuwa bado hatujaweza kukamilisha uwezo wa kuwafikia Watanzania wote ughaibuni kwa ajili ya kuwatambua na kuwahesabu. Mipango ya kutekeleza azma hiyo inaendelea na hivyo tunatarajia siku za usoni tutaweza kuwa na takwimu bora kabisa za wenzetu walioko ughaibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na juhudi za kuhamasisha Watanzania waishio ughaibuni kuona umuhimu wa kuchangia maendeleo ya nchi yao. Tumeweza kupata mafanikio kadhaa yanayopatikana kutoka kwenye mwitikio wa baadhi ya Watanzania hao. Taasisi zetu za fedha hazijaweza kukusanya takwimu zote za fedha zinazotoka ughaibuni kwa Watanzania kama kama remittance, kwasababu ya changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za utumaji wa fedha nyumbani. Changamoto hizo zinawalazimisha kutumia njia mbadala kama hawala. Hata hivyo, imeweza kuthibitika kuwa kaya nyingi zinapata misaada ya fedha kutoka kwa ndugu zao na jamaa zao waishio ughaibuni. Mathalani, asilimia 12 ya kaya za Zanzibar zinaishi kwa kusaidiwa na ndugu zao hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania hao wameendelea kuratibu na kuleta misaada hapa nchini hususan katika sekta ya afya na elimu. Mifano michache, mwezi Februari, 2015 Watanzania waishio Marekani walifanikisha upatikanaji wa mashine ya kupimia saratani ya matiti yenye thamani ya dola za Marekani 200,000 iliyotolewa katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Aidha, mwezi Julai 2015 Watanzania wengine kutoka huko huko Marekani, waliratibu ziara ya kitabibu ya Madaktari wa Marekani kuja kutoa huduma za tiba bure za magonjwa kama ya moyo, meno na saratani ya kizazi na matiti katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam pamoja na Hospitali ya Mnazi Mmoja kule Zanzibar. Vilevile walitoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya dola za Marekani 300,000 katika hospitali hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo rahisi kubaini idadi ya Watanzania walioondoka bila taratibu zilizopo hapa nchini. Watu wanaondoka kwa sababu tofauti na wakifika huko siyo rahisi kufahamu yanayotokea. Hata hivyo wale wanaojiandikisha katika Balozi zetu, mara nyingi taarifa za muhimu zaidi ni kuthibitisha Utanzania wao. Madhumuni yetu ni kuwatambua kama Watanzania wenzetu, kuwapa huduma wanapohitaji na kuwahamasisha kusaidia ndugu zao walikotoka na kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha, kupitia Balozi zetu, tumekuwa tukiwasisitiza Watanzania waishio ughaibuni kuheshimu sheria na taratibu za nchi wenyeji ili kuendelea kulinda heshima na sifa nzuri ya nchi yetu.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Sudan Kusini imekubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Je, ni lini Serikali itafungua Ubalozi katika nchi hiyo ili kutengeneza mazingira ya kunufaika na fursa zilizoko katika nchi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa la Sudan Kusini lilianzishwa mwezi Julai, 2011 baada ya kura za maoni za wananchi wa nchi hiyo kuamua kujitenga kutoka nchi ya Sudan na kuunda Taifa jipya ya Sudan Kusini. Aidha, mwezi Aprili, 2016 nchi ya Sudan Kusini ilijiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa sasa Tanzania haina Ofisi za Ubalozi nchini Sudan Kusini. Katika kipindi hiki ambacho Serikali haijafungua Ubalozi nchini Sudan Kusini, shughuli za Kibalozi kwa nchi hiyo zinafanywa na Ubalozi wetu, Nairobi nchini Kenya.
Malengo ya Wizara kwa mwaka 2016/2017 ni pamoja na kuongeza uwakilishi wetu nje ya nchi kwa kufungua Balozi mpya na Ofisi za Kikonseli hususan katika nchi ambazo Taifa linanufaika zaidi na fursa za kiuchumi kama vile soko la bidhaa zetu, biashara, uwekezaji, ajira pamoja na utalii.
Aidha, naomba ieleweke kuwa licha ya kuwepo kwa fursa hizo, maamuzi ya kufungua Ofisi za Ubalozi nchini Sudan Kusini pamoja na uendeshaji wa shughuli za Ofisi za Ubalozi zitakazofunguliwa zitategemea na Serikali itakapokuwa tayari Kibajeti.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Ofisi nyingi za Balozi zetu katika nchi mbalimbali zimekodishwa. Aidha, ofisi nyingine ujenzi haujakamilika au hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu sasa na ofisi nyingine zina madeni makubwa.
(a) Je, ni lini ujenzi wa baadhi ya ofisi za Ubalozi zitakamilika ikiwemo ya Msumbiji?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati ofisi chache za Ubalozi zilizopo pamoja na kununua samani mpya?
(c) Je, kwa nini Serikali isilipe madeni ya Balozi zetu kwa wakati ili kuepusha aibu kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi zetu umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha za bajeti ya maendeleo. Mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilipanga kutekeleza miradi ya ujenzi katika Balozi zake ikiwemo Maputo, Nairobi na Stockholm na uboreshaji wa mifumo ya mawasiliano kati ya Balozi na Makao Makuu wa Wizara. Mradi wa Maputo umepangiwa shilingi 1,316,435,000. Tunategemea utekelezaji wa mradi huu ufanyike pale Wizara itakapopokea fedha kutoka Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua kuwa fedha za bajeti ya maendeleo hazikidhi mahitaji, Wizara inaendelea kushirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu katika ujenzi wa majengo ya ofisi na vitega uchumi katika Balozi zetu. Wizara inaamini uamuzi wa kuishirikisha mifuko hiyo itaongeza kasi ya ujenzi wa majengo ya ofisi katika Balozi zetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Wizara uliopo hizi sasa katika kukarabati majengo ya ofisi yaliyopo kwenye Balozi zetu ni kuendelea kuiomba Serikali kutenga fedha za bajeti ya maendeleo; pili, kuelekeza Balozi zetu kutumia utaratibu wa karadha (mortgage finance) ili kuwezesha Balozi kupata fedha za ukarabati, kununua na kujenga majengo ya ofisi na vitega uchumi; na tatu, kuishirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyopo nchini kutekeleza miradi ya Wizara Balozini kwa Wizara kuingia makubaliano na vyombo hivyo. Aidha, Wizara itaendelea na utaratibu wa kununua kwa awamu samani mpya za ofisi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya Balozi zake nje. Serikali ilitoa kiasi cha shilingi 7,315,720,301.84 kulipa madeni ya Wizara yaliyohakikiwa na Wakaguzi wa Hesabu. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 deni lililobaki ni shilingi 15,540,603,526. Madeni haya yameanza kukaguliwa na Hazina, hivyo ni matarajio yetu kuwa baada ya kukamilika kwa ukaguzi huo, Hazina itatoa fedha za kulipa madeni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Hazina imetoa mwongozo unaoelekeza kuandaa mpango wa bajeti ambao unaelekeza madeni yote ya Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali kulipwa moja kwa moja na Hazina.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM aliuliza:-
Kwa kuwa Mabadiliko ya Kumi (10) ya Katiba ya Zanzibar yanaitambua Zanzibar kuwa ni nchi.
Je, ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itairuhusu Zanzibar kuwa na uwakilishi rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamad Salim Maalim, Mbunge wa Kojani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 2(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake imebainisha kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo. Aidha, Jedwali la Kwanza kwenye Katiba hiyo limebainisha kuwa masuala ya mambo ya nje ni masula ya Muungano.
Kwa muktadha huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa maslahi yote ya Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yanazingatiwa ipasavyo. Kabla ya kushiriki katika Mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kumekuwa na vikao vya maandalizi ambavyo hushirikisha pande zote mbili za Muungano ili kuandaa msimamo wa pamoja wenye kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hushiriki katika ngazi zote za Mikutano ya Wakuu wa Nchi Wanachama, Baraza la Mawaziri la Jumuiya na Mabaraza ya Mawaziri ya Kisekta yafuatayo:-
(a) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uwekezaji, Fedha, Viwanda na Biashara;
(b) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya;
(c) Baraza la Mawaziri wa Kisekta la Uchumi, Mawasiliano na Hali ya Hewa;
(d) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo;
(e) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Jinsia, Vijana, Watoto na Maendeleo ya Jamii;
(f) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati;
(g) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula; na
(h) Baraza la Mawaziri la Kisekta la Amani na Usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikutano hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hushiriki katika ngazi za wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri. Aidha, kati ya Wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki, Wabunge watatu wanatokea Zanzibar. Ahsante.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Utaratibu wa kutunga Sheria wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unahusisha maslahi ya nchi zote tano wanachama wa EAC kuelekea fungamano la kiuchumi na siasa.
(i) Je, hadi sasa ni sheria ngapi zimeshatungwa na kwa mgao wa maeneo yapi?
(ii) Je, hatua gani huchukuliwa unapotokea mgongano baina ya sheria ya ndani na ile ya Jumuiya?
(iii) Je, kuna utaratibu gani wa kutoa elimu ya umma kuhusu Sheria za Jumuiya?
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwa Bunge la Afrika Mashariki mwezi Novemba, 2001 hadi hivi sasa jumla ya sheria 78 zimeshatungwa. Kati ya hizo, sheria 20 zimesharidhiwa na Wakuu wa Nchi na Wanachama na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za kusainiwa na kuridhiwa. Sheria zilizotungwa zimelenga katika kuimarisha biashara, kukuza uchumi baina ya nchi wanachama na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwezesha taasisi na vyombo vya jumuiya kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya sheria hizi ni Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004, Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kusimamia Uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiushuru ya mwaka 2017, Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2013 na Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uanzishwaji wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani ya mwaka 2013.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 8(4) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sheria za Jumuiya zina nguvu kuliko za nchi wanachama. Hivyo basi, ikitokea mkingano baina ya Sheria za Jumuiya na zile za nchi wanachama, nchi wanachama hazina budi kuzifanyia marekebisho sheria hizo ili ziendane na Sheria za Jumuiya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Tanzania sheria mbalimbali za kodi zilifanyiwa marekebisho, ili ziendane na utekelezaji wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 ambayo ndiyo sheria inayotumika kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ili kuendana na makubaliano yaliyofikiwa katika Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Tanzania imefanya marekebisho katika Sheria ya Masoko na Mitaji na Dhamana, Sura ya 79; Sheria ya Kubadilisha Fedha za Kigeni Sura ya 271; pamoja na Kutunga Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Nchini Na. 1 ya mwaka 2015. Vilevile Serikali inaendelea na mapitio ya sheria mbalimbali ili kuainisha na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na kuwapatia uelewa wa sheria zilizopitishwa na Bunge la Afrika ya Mashariki. Elimu hii hutolewa kupitia vyombo vya habari, tovuti ya Wizara, makongamano, vikao vya wadau, warsha, blog za kijamii na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani mwezi Julai Wizara iliratibu kampeni ya kuhamasisha vijana wa Kitanzania kutumia fursa za biashara zitokanazo na mtangamano wa Afrika Mashariki iliyojulikana kama Chungulia Fursa, iliyolenga kuwahamasisha vijana kufanya biashara za kuvuka mipaka ya Tanzania iliyofanyika katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Manyara na Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ilitoa elimu ya faida na fursa za mtangamano kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Wajumbe wa Baraza la Vijana wa Zanzibar. Mafunzo hayo yalifanyika mwezi Machi, 2018 na yaliongozwa na kaulimbiu iliyosema Vijana na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Chemba?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Wilaya ya Chemba ni moja ya wilaya zinazokabiliwa na ukosefu wa huduma za mahakama ya wilaya. Kwa nyakati tofauti, nimekuwa nikilieleza Bunge lako Tukufu kwamba Mahakama ya Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya kutolea huduma za kimahakama katika ngazi zote. Kati ya Wilaya 139 zilizopo nchini, ni Wilaya 34 tu zenye majengo ya mahakama.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Mahakama ya Tanzania imekuwa ama ikiazima majengo kwenye Ofisi za Halmashauri, Mkuu wa Wilaya au kupanga pale yanapokosekana kabisa majengo hayo, ili kuendelea kutoa huduma za kimahakama. Katika maeneo ambayo Mahakama ya Tanzania haina kabisa majengo huduma hiyo imekuwa ikiendelea kutolewa na mahakama ya wilaya nyingine iliyopo jirani kwa utaratibu wa kuitembelea kwa ratiba walizojipangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhaba wa miundombinu takribani wilaya mpya 29, ikiwemo ya Chemba mkoani Dodoma ambayo imetokana na Wilaya ya Kondoa bado haina Mahakama ya Wilaya. Hivyo, Wilaya hiyo kwa sasa inaendelea kuhudumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kondoa. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2019/2020, mpango wa Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chemba linajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa lengo la Serikali ni kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi, naomba kumthibitishia Mbunge kwamba tutafanya kila jitihada ya kuendeleza ujenzi wa mahakama kila wilaya hapa nchini inapokuwa inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-

Ibara ya 13(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”; lakini kumekuwa na kiwango cha juu cha matukio na kesi zinazohusu kuvunjwa kwa haki za kiraia kwa kufanywa na vyombo vya dola:-

(a) Je, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 ni kesi ngapi zimefunguliwa Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia, na huchukua muda gani hadi kutolewa hukumu?

(b) Je, kesi hizo zimekuwa zikigharamiwa kwa kiasi gani kutoka Mfuko wa Fedha za Umma tangu mwaka 2010 – 2015?

(c) Je, Serikali inafanya jitihada gani kuhakikisha wananchi wake pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora haijafungua kesi yoyote Mahakamani kuhusu madhara yanayofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia. Tume imekuwa ikipokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu dhidi ya vyombo vya dola na kuyashughulikia kwa kufanya uchunguzi wa kawaida, usikilizwaji hadharani na kufanya usuluhishi na upatanishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbinu hizi zimeonekana kuwa na mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi haki yao wanayostahili, hivyo kutokuwa na umuhimu wa kufungua mashauri Mahakamani. Ikumbukwe kuwa ufunguaji wa mashauri Mahakamani ni hatua ya mwisho iwapo njia nyingine zote zimeshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza, kwa kuwa Tume haijawahi kufungua kesi yoyote ya haki za binadamu katika Mahakama zetu kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015, hivyo basi, hakuna gharama zozote za ufunguaji wa mashauri Mahakamani zinazohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha mwaka 2010 – 2015, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imefanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi pamoja na vyombo vya usalama wanapata elimu ya uraia. Jitihada hizo ni pamoja na kuelimisha Umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mikutano, maadhimisho, machapisho na warsha mbalimbali katika kipindi cha 2010 hadi 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vipeperushi na vijitabu 40,638, makala 18,300 za Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu, majarida yaliyowekwa kwenye tovuti ya Tume ni matano, vipindi vya redio na televisheni ni 115 na kufanya mikutano na wananchi kuhusu haki za binadamu na hasa katika kumiliki ardhi kwenye mikoa 21 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi sasa, jitihada hizi zimeendelea kufanywa na Wizara yangu Waheshimiwa Wabunge na Bunge hili kwa ujumla kwamba haki zitakuwa zinatendeka na kwamba tunaendelea kubuni mbinu na mikakati mbalimbali itakayowezesha kuendelea kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha jengo la Mahakama Wilayani Nachingwea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Tanzania haipo katika mpango wa maboresho ya majengo ya Mahakama nchini, ambapo pamoja na mambo mengine imekusudia kusogeza haduma ya Mahakama karibu na wananchi. Ili kufikia lengo hilo, Mahakama imeendelea kutatua changamoto kubwa ya uhaba na uchakavu wa majengo kwa kuendelea na kukarabati majengo nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mahakama ya Tanzania inafahamu tatizo la uchakavu wa majengo mengi ya Mahakama nchini, ikiwemo jengo la Mahakama ya Wilaya Nachingwea. Katika kukabiliana na changamoto hii, Mahakama imeweka kipaumbele katika kuboresha na kujenga majengo ya Mahakama nchini kulingana na mpango mkakati wa miaka mitano ambao umeendelea kutekelezwa kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa rasilimali na rasilimali chache zilizopo, katika mpango mkakati wa miaka mitano, Mahakama iliamua kujipanga upya na kuweka vipaumbele ili kuhakikisha tunaondokana na changamoto hii. Aidha, tayari tathmini ya jengo la Mahakama Nachingwea imeshafanyika. Kimsingi jengo hili linahitaji kujengwa upya na siyo kufanyiwa maboresho. Aidha, baada ya tathmini hiyo kufanyika ujenzi wa jengo hilo umewekwa kwenye mpango wetu wa ujenzi wa Mahakama wa mwaka 2020/2021kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-

Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataja kazi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, moja ya kazi zake ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa Haki za za Binadamu na ukiukwaji wa msingi ya utwala bora.

(a) Je, kwa nini ripoti za tume hiyo haziwekwi wazi kwa Umma?

(b) Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kujenga utamaduni wa ripoti hizo kujadiliwa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf Mbunge wa Mgogoni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijalijibu Mheshimiwa Ally Yussuf, amesema wadhurumiwa wote kwa hiyo inawezekana hata yeye kuna ambao amewadhurumu lakini naomba nijibu swali kama alivyouliza maana hakuuliza hivyo huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kwamba Ibara ya 130 ya katiba ya Jamhuri ya Muugano ikiosomwa kwa pamoja na sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya 2001) inaipa Tume mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mambo yote yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu, kifungu cha 28(1)(a) mpaka (f) cha sheria hiyo (Na. 7 ya 2001) kinafafanua kuwa, tume baada ya kufanya uchunguzi na kuthibitisha kuwepo kwa uvunjifu wa haki za binadamu itawaslisha taarifa na mapendekezo yake kwenye mamlaka kusika kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 33 (1) (a) –(c) cha Sheria Na. 7 ya 2001 kinaitaka Tume kuwasilisha taarifa yake ya mwaka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Mawaziri kupitia wanaoshughulikia masuala ya haki za binadamu kwa Tanzania Bara na Zanzabar, hata hivyo, Tume imekuwa ikitimiza jukuu hilo kwa mujibu wa sheria. Aidha, hakuna sheria yoyote inayokataza taarifa za Tume kujadiliwa Bungeni endapo Mbunge ataona kama kuna jambo la kuibua kutoka kwenye taarifa iliyowasilishwa.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMANI ALLY YUSSUF) aliuliza:-

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kumekuwa na ongezeko kubwa la makosa katika jamii jambo ambalo linasababisha mfumo wa utoaji haki pamoja na Mahakama kuelemewa.

(a) Je, kila Jaji au Hakimu anapangiwa kesi ngapi kwa mwaka ili kupunguza mlundikano wa kesi?

(b) Je, ni mambo gani kimsingi yanayosababisha mashauri kuchukua muda mrefu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleimani Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu ili kuhakikisha mashauri yote yanayofunguliwa Mahakamani yanamalizika kwa wakati. Utaratibu huu ni pamoja na kujiwekea malengo ya idadi ya mashauri yatakayoamuliwa na Jaji na Hakimu kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, malengo ni kuhakikisha tunapunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani ambapo kwa mwaka kila Jaji anatakiwa kumaliza mashauri 220; Mahakimu katika Mahakama za Hakimu Mkazi wa Wilaya kumaliza mashauri 250 na katika Mahakama za Mwanzo 260.

Mheshimiwa Spika, pia Mahakama imejiwekea ukomo wa muda wa mashauri kukaa Mahakamani. Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ni miaka mwili; Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita. Mikakati hii imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri kwa kiasi kikubwa hususan kwa Mahakama za Mwanzo ambapo kwa sasa mlundikano wa mashauri ni asilimia sifuri.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo bado Mahakama zetu zimekuwa zinakabiliwa na changamoto za mlundikano wa mashauri na baadhi ya mashauri kuchukua muda mrefu zaidi. Changamoto hizi zimetokana na idadi ndogo ya Majaji na Mahakimu ikilinganishwa na idadi ya mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama zote nchini. Vilevile upelelezi katika Mahakama na mashauri kuchukua muda mrefu na mashahidi kutotoa ushahidi wao kwa wakati katika baadhi ya mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama zetu nchini ni miongonzi mwa sababu na baadhi ya mashauri kuchukua muda mrefu Mahakamani. Hata hivyo ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kuteuwa Majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa na Majaji 39 wa Mahakama Kuu katika Awamu ya Tano, ahsante.