Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Constantine John Kanyasu (25 total)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika Kituo cha Afya cha Nzela ambacho kimekuwa kikihudumia wananchi wa Jimbo la Geita na ni kikubwa na tayari kimekwishafanyiwa maamuzi na Halmashauri ya Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika kituo hicho na kuona kama kinafaa kufanywa kuwa Hospitali ya Wilaya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, baada ya Hospitali ya Geita ambayo ndiyo ilikuwa Hospitali ya Wilaya kuwa Hospitali ya Mkoa, hivi sasa kuna vifaa vingi ambavyo zimeletwa na Mkoa lakini hakuna Madaktari na watumishi mbalimbali. Je, lini Mheshimiwa Waziri atapeleka watumishi na watalaam katika Hospitali ya Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nipende kuwapongeza Wabunge wote wa Geita kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kushirikiana na Geita Gold Mine (GGM) kwa kuhakikisha kwamba Hospitali yao ya Wilaya ya Geita imekuwa na structure ambayo inarahisisha sasa kufanya hospitali hiyo kuweza kutoa huduma bora. Nishukuru sana kwa sababu tulikuwa na Makamu wa Rais pale na Waziri mwenye dhamana wa sekta ya afya na kushuhudia hospitali ile kukabidhiwa vile vifaa kwa kweli tunawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jinsi gani ya kuambatana nami, naomba nikiri wazi mchakato huu wa Bunge la Bajeti ukiisha nilikuwa na ziara maalum ya Mkoa wa Geita, hili litakuwa ni miongoni mwa eneo moja ambalo tutakwenda kulifanyia kazi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala zima la kupatiwa wataalam, naomba niwajulishe ndugu zangu si muda mrefu mtasikia sasa Wizara ya Afya inatoa idadi ya waajiriwa katika sekta hiyo na Hospitali yetu ya Geita itakuwa ni kipaumbele kwa sababu ina hadhi ya kutosha ili wananchi wa Mkoa wa Geita wapate fursa kubwa ya kupata matibabu katika Mkoa wao.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimwia Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa amejibu kwamba ni jukumu la Mkurugenzi kuandika na kuomba shule hii iwe ya bweni; ni lini sasa ofisi yake itamuagiza Mkurugenzi huyo ambaye anaonekana hafahamu kama yeye ndiyo anawajibika ili aweze kuandika barua na kuomba? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa mwezi huu au mwisho wa mwezi ujao, Serikali itaajiri walimu wapya na uchunguzi wangu shule nyingi za Jimbo la Geita za Vijijini hazina walimu; ni maagizo gani Serikali itatoa kwa walimu wapya ili waelekezwe zaidi Vijijini badala ya Mjini? Nashukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini nitamwagiza Mkurugenzi, nadhani huu mchakato unaanza kwenu ninyi katika Baraza la Halmashauri, kwa sababau hii ni need ambayo ninyi mnahitaji. Kama Baraza la Madiwani mtaona kwamba ninyi mnahitaji hilo, baadaye Mkurugenzi ataandika barua, akishaandika barua maana yake ikifika katika Wizara ya Elimu, Wizara ya Elimu inatuma wataalamu chini ya Kamishna wake, wataenda kufanya uhakiki, baadaye vigezo vikishapita ndiyo shule hiyo itasajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niliache suala hili katika Baraza lenu la Madiwani, maana inawezekana Mkurugenzi akaandika halafu Madiwani wakamgeukia kwa nini umegeuza shule hii kwa mahitaji yako bila kutaka maelekezo kutoka katika Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niache jambo hili katika mchakato wa Baraza la Madiwani litaamua kumwelekeza Mkurugenzi aweze kufanya haraka kupeleka Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuhusu suala la upelekaji wa walimu. Ni kweli hivi sasa tupo katika mchakato siyo muda mrefu sana tutaajiri walimu wapya. Katika kuajiri, kuna Mikoa ambayo inabidi ipewe kipaumbele, tuna Mikoa takribani sita ambayo ina changamoto kubwa sana ya walimu ikiwepo ni pamoja na Mkoa wa Kigoma, Rukwa, Katavi na Geita. Kwa hiyo, katika maeneo hayo yote tutaangalia walimu watakaopatikana basi tutawapa maelekezo maalum. Wakifika pale lazima waende maeneo ambayo wananchi wanataka huduma, bahati mbaya wakati mwingine inajitokeza walimu tukiwaajiri, tukiwapeleka kule inawezekena wengine sisi Waheshimiwa tunapeleka vi-memo ili yule mwalimu arudi mjini, tunasababisha maeneo ya vijijini yanakosa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Ofisi ya Rais TAMISEMI tunaelekeza walimu watakaopangwa lazima waende kufanya kazi katika maeneo husika.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika REA Second Phase ambayo ilikuwa inaendelea ni robo tu ya vijiji vya Jimbo la Geita na Geita Mjini ambavyo vimepata umeme, vijiji kama Nyawilimilwa, Kagu, Senga, Bulela bado havijafikiwa; naomba kujua ananipa uhakika gani kwamba Vijiji hivi ambavyo bado havijapata umeme vitapata umeme kwenye Awamu ya Tatu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Mji wa Geita tumekuwa na tatizo la umeme kukatika katika kila siku kutokana na umeme mdogo ambao tunatoka Mwanza. Hata mji wenyewe wa Geita pale Mjini umeme unakuta upo lakini sehemu nyingine hauwaki. Ni lini Mheshimiwa Waziri atahakikisha Geita inapata umeme wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu kujumuisha vijiji vya Nyawilie na Bulila nimhakikishie kwamba vijiji hivyo vyote vitaingia kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza Julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kukatika katika kwa umeme nichukue fursa hii kuwataarifu kwamba ni kweli kabisa karibu nchi nzima siyo Geita tu umeme bado unakatika katika na suluhisho la kukatika kwa umeme kama tulivyosema miji ya Geita na maeneo ya Kanda ya Ziwa pamoja na maeneo mengine, itapata sasa umeme wenye kilovoti 400 unaotoka North West Grid unaotoka Mbeya unaopita Sumbawanga, unaopita Mpanda, unaokuja Kigoma unakwenda mpaka Nyakanazi na baadaye Geita na umeme huo utatoka Geita kwenda Bulyanhulu na utatoka Bulyanhulu kwenda maeneo ya Biharamulo. Umeme huu utakuwa na nguvu kubwa ya kilovolt 400 na unatembezwa kwa takribani ya kilometa 1148.
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Wakati wa kampeni tulihamasisha sana vijana kujiunga kwenye SACCOS ili baadaye waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji wa madini. Nataka kufahamu Mheshimiwa Naibu Waziri anawaahidi nini vijana waliolundikana kwenye maeneo ya Samina, Mgusu, Nyakabale kwamba watapata lini maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Kasema, Wanela pamoja na eneo la Geita Mjini, lakini siyo Geita Mjini tu, Nyakabale na maeneo mengine wanahitaji maeneo. Namhakikishie Mheshimwia Constantine kwamba mwaka huu tumetenga hekta 12,000 na kati ya hizo, hekta 2,000 ni maeneo ya Geita kwa hiyo wananchi wa Nyakabale, wananchi wengine wa Mtakuja na wengine ambao walikosa mgao wa Geita watapata maeneo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kwa Mkoa wa Geita, mwaka 2015 na mwaka 2014, kuna SACCOS sita zilizoundwa. SACCOS mojawapo ambayo haijapata eneo la uchimbaji, ni pamoja na wakeretwa wa SACCOS ambayo ilipata lesseni tano; lakini Tupendane SACCOS walipata ekari sita pamoja na Tunakuja SACCOS walipata ekari nane; Ujamaa SACCOS kwa sababu zote zinatoka Geita walipata ekari tisa, pamoja na Mapinduzi SACCOS Kwa hiyo, wananchi wote wa Geita tunaomba wajiunge na SACCOS ili kusudi tuendelee kuwagawia maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Constantine sana kwamba, ningependa sana waanze kuziunda SACCOS sasa hivi, kwa sababu utaratibu sasa wa kuwatengea maeneo unaanza mwezi wa Kumi mwaka huu. Kwa hiyo, tunaomba sana SACCOS zote na siyo kwa Geita tu, ziwe tayari ili kuanzia mwezi wa Kumi waanze kugawiwa pesa. Hata hivyo, tumewatengea ruzuku sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walipitisha shilingi bilioni 6.68 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, pamoja na kuundwa SACCOS, lakini pia tutawagawia ruzuku kwa ajili ya kuendeleza uchimbaji wao.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwamba sehemu kubwa ya askari ambao wanalinda maeneo ya kuzunguka Mgodi wa GGM wanalinda mawe ambayo hayana thamani ambayo hata mgodi hawayahitaji, matokeo yake ndiyo wanakamata watu kila siku. Je, ni lini Serikali itaondoa askari hao kwenda kulinda usalama wa raia sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tutalichukua swali lake tuone umuhimu huo kama bado upo, kama utakuwa haupo kama Mbunge anavyoshauri basi tutaondoa kama upo wataendelea kubakia.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mpaka wa Tanzania katika eneo la Rusumo mpaka unapoenda Kagera ni hifadhi, lakini mpaka huo kwa upande wa Rwanda ni vijiji ambavyo viko mpaka kwenye Mto Kagera, kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba changamoto zilizopo katika hifadhi hiyo ni pamoja na hifadhi hiyo kutumiwa na wahamiaji haramu, watu wanaopitisha silaha na ujambazi.
Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atahakikisha kwamba eneo hilo linalindwa kwa usalama wa nchi? Hilo swali la kwanza.
Swali langu la pili, katika hifadhi hizo za Burigi na Kimisi kuna Maziwa Ngoma na Maziwa Burigi, ambayo miaka yote yamekuwa yakitumiwa na watu kutoka nchi za jirani kwa uvuvi katika maziwa hayo na kwa ulinzi mkubwa wa askari wa wanyamapori. Ni lini Serikali itaanzisha seasonal fishing kwa Watanzania ili waende kuvuna maliasili hiyo?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza lini Serikali itaimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo, nimejibu kwenye swali la msingi, kwamba mpaka sasa hvi tunavyozungumza, changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika eneo tunalolizungumzia zimekuwa zikishughulikiwa kwa pamoja kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamati ya Ulinzi ya Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ameeleza kwamba yapo mashaka ambayo yanaendelea kuongezeka kila siku, basi Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa kuweza kuona namna gani tunaweza kuboresha vizuri zaidi au kufuatilia zaidi ambazo zinaonekana kujitokeza upya kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ni lini, napenda pia nimkumbushe Mheshimiwa Kanyasu kwamba tumesema mara tu baada ya Bunge hili tunapita maeneo yote ambayo yana changamoto za kiulinzi na usalama kuhusiana na masuala ya mipaka ili tuweze kuboresha vizuri zaidi changamoto za ulinzi na usalama na changamoto za migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mabwawa yaliyopo ambayo yana samaki na kwamba kwa sababu yapo ndani ya hifadhi basi kwa mujibu wa sheria wananchi hawaruhusiwi kufanya uvuvi. Napenda kujibu kwamba sababu za kuzuia kufanya uvuvi zitakuwa ni sababu za kiuhifadhi, lakini kwa kuwa kuhifadhi maana yake siyo kuacha kutumia maana yake ni kutumia kwa busara na hekima, kuhifadhi maana yake ni kutumia ukijua kwamba ipo kesho na kwamba unaweza ukatumia leo ukijua kabisa kwamba kesho utahitaji kutumia kitu kile unachokitumia leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa maana ile ya kufanya uhifadhi endelevu tutaliangalia suala hili kuona ni namna gani tunaweza tuka-engage wananchi waliopo katika maeneo haya waweze kufanya uvuvi kama taratibu za kisayansi za uhifadhi zitaruhusu. Lakini tunakwenda kufanya jambo hili kwa pamoja liwe shirikishi ili wote tuone ukweli sasa kwamba kitakachofanyika kiwe kwa maslahi ya Taifa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha, moja ya sababu ambazo zinasababisha shilingi yetu kushuka ni matumizi makubwa ya fedha za kigeni na katika bidhaa ambazo zinaagizwa ni makaa ya mawe. Ni kwa nini makaa ya mawe ya Tanzania hayatumiki tunaagiza makaa ya mawe kutoka South Africa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anataka kujua kwa nini makaa ya mawe yaagizwe kutoka nje badala ya kutumika ya hapa nchini? Ni kweli kabisa, sasa hivi makaa ya mawe yanayopatikana yangeweza kupatikana kwa wingi sana pale Kiwira kwenye eneo la Kiwira lenyewe, lakini hata Kabulo. Kiwira ni kweli kabisa, kutokana na utafiti wa mwaka 2007 iko reserve ya tani milioni 30 na pale Kabulo ni tani milioni 50 lakini bado kuna maeneo mengi ya Mchuchuma na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ilizochukuwa Serikali sasa ni kuhakikisha kwamba wawekezaji wote wanapata makaa ya mawe kwa sababu yanajitosheleza. Hata hivyo, wako wawekezaji kama Dangote alikuwa anaagiza kutoka Afrika Kusini na maeneo mengine sasa hivi tumesitisha kutoa vibali vya kumruhusu kuingiza isipokuwa tunamlazimisha aanze kutumia makaa ya mawe ya hapa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema Serikali itaanza sasa kuchukua hatua kuhakikisha makaa ya mawe yatakayopatikana hapa yananunuliwa hapahapa nchini.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hivi karibuni JKT wametangaza nafasi za vijana wanaomaliza form six na wametangaza nafasi 1,500 mpaka 2,000. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri anasema uwezo wao ni kati ya 5,000 mpaka 7,000. Nataka kufahamu, sasa ni mpango upi mwingine wa Wizara hii kuhakikisha kwamba hao zaidi ya 20,000, ambao hawajapa nafasi wanakwenda?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleweke kwamba kuna vijana wanaojiunga na JKT wa aina mbili. Kuna vijana tunaowaita wanajiunga kwa mujibu wa sheria, ni wale ambao wamemaliza form six kabla ya kujiunga na vyuo vikuu. Vijana hawa idadi yao tuliyoichukuwa mwaka huu ni 14,000 na sio wote ambao tunaweza kuwachukuwa kwa sababu waliohitimu form six ni wengi zaidi ya hapo, kwa hiyo, tunaendelea kujenga uwezo ili tuweze kuwachukuwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale vijana 5,000 mpaka 7,000 niliozungumzia, hao ni vijana wanaoingia kwa kujitolea, ambapo idadi yao ndiyo hiyo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hawa wa mujibu wa Sheria, idadi yao ni kubwa zaidi ni 14,000 na wanakaribia kuanza ndani ya wiki moja ili waweze kupata mafunzo hayo ya Jeshi la Kujenga Taifa.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nakubaliana na agizo la Serikali kwenye sentensi nne za jibu lake za mwisho, lakini sikubaliani kabisa na majibu aliyoyatoa na sababu za msingi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Mpira kabla ya adhabu yoyote kutolewa Chama cha Mpira (TFF) kinasubiri taarifa ya Refa na taarifa ya Kamishna au Msimamizi wa Mechi. Taarifa hizo mpaka wakati Rais wa TFF ana-twit, dakika ya 80 mechi inaendelea, alikuwa hana mezani, ni wakati gani Waziri ananiambia Rais huyu alitumia Kanuni? (Makofi)
Swali langu la pili; baada ya adhabu hii baadhi ya wanamichezo wamefungiwa maisha kwa tuhuma kwamba, palikuwa na makosa ya rushwa ambayo ni makosa ya jinai. Tunavyo vyombo ambavyo vinachunguza rushwa na ni kosa la jinai, ni uchunguzi gani ambao vyombo vya jinai vilitoa kwa sababu vilipewa agizo la kuchunguza suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kanyasu kwa jinsi ambavyo anajitahidi kutetea timu yake ya Geita Gold Sports.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alitaka kujua wakati ambao vikao hivi vilikaa, swali la kwanza hilo. Kama nilivyosema katika jibu la msingi vikao hivi vilikaa baada ya kupata malalamiko kutoka timu za Kundi „C‟ na ndipo vikao vikakaa, lakini Rais wa TFF alichukua tahadhari, sio kwamba, alitoa maamuzi, alikuwa anatoa tahadhari. Vikao vilivyofanya maamuzi ni vile ambavyo vilikaa baada ya kupata malalamiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili ni kwamba, ni ruksa kwa mtu binafsi au taasisi au timu kukata rufaa kwa kutumia taratibu ambazo zipo. Ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Costantine John Kanyasu Mbunge wa Geita, naongezea katika majibu ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza, kama alivyosema Naibu Waziri, maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Mbunge na tuliwahi kuyatoa hapa Bungeni, tukasema wale ambao hawakuridhika na uamuzi uliofanywa na TFF, TFF uamuzi wao siyo wa mwisho, wafuate taratibu na watumie hayo ambayo wanaona ni upungufu katika uamuzi uliofanyika kukata rufaa. Sehemu ya kwanza hii, watumie nafasi hiyo wakate rufaa na Serikali tutasimamia haki yao ipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ni kweli katika mchakato huu kuna tuhuma nyingi za rushwa na niliwahi kusema hapa Bungeni, tuhuma zile waliotuhumiwa sio wadogo wa chini peke yake ni pamoja na wa katika mhimili wenyewe unaosimamia soka. Hivi tunavyoongea chombo ambacho kinahusika na suala la rushwa, TAKUKURU wanakamilisha kazi yao ya uchunguzi, wakikamilisha na kama kutakuwa na watu watabainika kuhusika na rushwa hatua za Kisheria zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni kuthibitisha kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kufuta suala la rushwa kwenye michezo kwa sababu linatafuna na kuharibu michezo yetu.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimshukuru Mheshimiwa
Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika jibu lake naomba nifanye marekebisho kidogo kwamba kwanza
haiwezekani watu wakalipwa halafu wakadai, kwa sababu wanaolipwa wanalipwa kwa coordinates na eneo
linajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa miaka 17 wananchi wa maeneo ya
Mizingamo, Ikumbiyaga, Compound pamoja na Mtakuja wako ndani ya eneo ambalo ni leseni ya mgodi, lakini
hawaruhusiwi kujenga, hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, lakini mgodi haujajiandaa kulitumia eneo hilo sasa wala kesho. Sasa ni nini hatima ya wananchi wa eneo hilo, kama mgodi sheria inasema utalipa tu fidia pale ambapo watataka kulitumia, lakini hawaruhusiwi kufanya chochote kwa miaka 17? Swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa muda tofauti, Serikali kupitia Waziri wa Wizara husika, Naibu Waziri wa Mazingira, wamekuja na wameshuhudia aina ya uchimbaji wa madini wa Mgodi wa GGM ukiwa na madhara makubwa kwa wananchi wa Kata ya Kalangalala, Mjini Geita. Matokeo ya uchimbaji mbovu ni mipasuko ya nyumba inayotokana na mitetemo mikubwa, watu wengi wamezimia, lakini maji machafu yanatoka kwenye eneo la kuchimba na Mkurugenzi wa Mgodi aliyekuwepo ambaye alitaka kuleta suluhisho la migogoro hiyo, mgodi ulipoona anataka kuchukua hatua, ukamfukuza. Maagizo yote yaliyotolewa na Serikali hayajawahi kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itahakikisha mgodi unawalipa fidia wananchi ambao nyumba zao
zimepasuka kutokana na mitetemo ya uchimbaji wa dhahabu Geita?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Kanyasu jinsi ambavyo anapambana na kuhangaikia maendeleo ya wananchi wa Geita Mjini. Hongera sana Mheshimiwa Kanyasu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la kwanza, ni kweli kabisa maeneo ya Compaund, Nyakabale,
Katoma pamoja na eneo lingine la Kagema, yako katika maeneo ya beacon. Kama ambavyo nilieleza kwenye jibu
langu la msingi, wananchi hawa ambao mgodi unahitaji eneo lile, tutakapolihitaji wakati wa uchimbaji, tutawalipa
fidia kwa wale ambao hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa wako wananchi wachache ambao baada ya kulipwa fidia, pia walirejea katika maeneo yale. Kama haitoshi, mgodi ulilipa fidia ya umbali wa mita 570 badala ya mita 200 ili kuhakikisha
kwamba hakuna mwananchi ambaye anabaki bila fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu kwamba suala hilo tumelipokea,
tutaendelea kulifanyia kazi. Kama kuna wananchi hawajafidiwa, basi itabidi wafidiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili, kuhusu mipasuko. Kwanza kabisa niendelee kumpongeza
Mheshimiwa Kanyasu na Wabunge wote wa Geita, wakiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Busanda na
Waheshimiwa wengine, pamoja na Mheshimiwa dada yangu yule wa Chama cha Upinzani wa Mkoa, waliita Mkutano, nilifika kule mwenyewe nikaangalia taarifa ya kampuni.
Taarifa ya kampuni ya awali ilionesha kwamba mpasuko hausababishwi na kampuni. Tuliunda tume, ikaleta matokeo, ikaonesha baadhi ya maeneo kwa kweli yanasababishwa na mpasuko wa kampuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tuliunda tume nyingine kwenda kutathmini majengo yaliyoharibika.
Nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu, ilionekana nyumba takribani 890 zilisababishwa kwa kiasi fulani na mlipuko wa Mgodi wa GGM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Kanyasu alitaka kujua ni lini sasa Serikali itatoa tamko? Tarehe
20 mwezi huu wa Aprili, timu ya wataalamu saba wakishirikiana na uongozi wa Wilaya pamoja na Jimbo lako
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na GGM watakwenda sasa kuangalia nyumba ngapi zinahitaji fidia ili fidia sasa itakapothibitika waweze kulipwa fidia wale ambao itaonekana kuwa halali.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Geita na Kasamwa kuna shida kubwa sana ya maji na Mheshimiwa Waziri tangu mwaka jana alisema wamepata pesa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika Mji wa Geita. Je, ni lini sasa mradi huo wa maji utatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Geita una miradi miwili, mradi mmoja ni ule ambao tunashirikiana na GGM na umeshatekelezwa mpaka tukafikia asilimia 30 tayari Mji wa Geita unapata maji. Pia unapata kutokana na ufadhili unaotokana na uboreshaji wa mazingira wa Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Kanyasu, tayari katika mkopo tuliopata wa milioni 500 kutoka Serikali ya India, sehemu ya fedha hiyo inatarajiwa kuboresha maji katika Mji wa Geita. Sasa hivi tunaendelea vizuri kwa ajili ya kumpata consultant atakayefanya mapitio na kuandaa tender document baada ya hapo kutangaza tenda ili tuweze kupata sasa maji ya uhakika kwa Mji wa Geita.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa pamekuwepo na unyanyasaji mkubwa sana wa wafanyakazi katika migodi, ikiwepo tabia ya ku-blacklist wafanyakazi na mfanyakazi anapokuwa blacklisted hawezi kuajiriwa sehemu yoyote katika mgodi, mara nyingi wanapokuwa blacklisted hawapewi nafasi ya kusikilizwa. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwa kiwango gani vyama vya vya wafanyakazi vina uwezo wa kuwatetea wafanyakazi linapoteka tukio kama hili? (Makofi)
Swali langu la pili, migodi mingi imekuwa ikiwashirikisha wananchi wanaozunguka migodi kwa ajili ya ulinzi lakini wananchi hao wamekuwa wakipwewa mikataba ya mwaka mmoja na miezi sita, hawana bima na hawana mikataba ya aina yoyote, hili linafanyika ili kukwepa sheria ya kuwalipia NSSF na faida zao zingine. Je, ni lini migodi hii itaelekezwa kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapewa mikataba na wanalipwa haki zao kama wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kwanza la unyanyashaji na blacklisting ambayo imekuwa ikifanyika, kama Wizara tumeshapata malalamiko hayo kutoka kwa wafanyakazi wengi walioko katika migodi, ambao wamekuwa wakilalamika kwamba waajiri wengi katika migodi hii hasa baada ya kuwa wafanyakazi hawa wametoka katika maeneo yao, wamekuwa wakiwa- blacklist ili wasipate nafasi yakuweza kuajiriwa katika migodi mingine na makampuni zingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumeshachukua hatua na tayari katika ukaguzi wetu huu ambao tumeufanya katika migodi yote, moja kati ya taarifa ambayo tunaisubiri ambayo itafanyiwa utekelezaji ni pamoja na jambo hilo na Serikali itatoa maelekezo kwa waajiri wote kwamba wanachokifanya ni kinyume na utaratibu wa sheria za nchi na hairuhusiwi kwa mwajiri yeyote kum-blacklist mfanyakazi. Kwa hiyo, tutaendelea kuwachukulia hatua kwa wale wote watakaoendelea kufanya jambo hili, ambalo linawaondolea haki ya kimsingi kabisa wafanyakazi wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusu mikataba, kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya mwaka 2004 imeanisha vema katika Kifungu Na. 14 aina ya mikataba ambayo mwajiri anapaswa kumpatia mfanyakazi. Kama Mwajiri anakiuka katika eneo hilo, anashindwa kutoa mikataba kwa mujibu wa sheria inavyosema, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba kwa sababu umeleta lalamiko hili rasmi tutalifanyia kazi na tutachukua dhidi ya wale waajiri wote ambao wanashindwa kukidhi matakwa ya Kifungu Na. 14 cha Sheria za Kazi.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Uhaba wa mbegu bora uliokuwepo mwaka 2015/2016 na kiwango kidogo cha ubora wa dawa ya pamba uliokuwepo mwaka 2015/2016 umeendelea kuwepo 2016/2017. Sasa swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwa kiwango gani Wizara imejiandaa kumaliza tatizo hilo mwaka 2017/2018?
Swali langu la pili, wakati wa kampeni Mheshimiwa
Rais alipokuwa Kanda ya Ziwa aliagiza Bodi ya Pamba ihamie karibu na wazalishaji wa zao la Pamba. Sasa swali langu, ni kwa kiwango gani uwepo wa Bodi ya Pamba Kanda ya Ziwa umesaidia kuhakikisha kwamba zao hili la pamba linapata uzalishaji mkubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini Serikali itaongeza kiasi au kiwango cha mbegu za pamba ili kukidhi mahitaji ya wakulima, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu unaokuja wa kupanda pamba, tayari Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na Mfuko wa Pamba wameweka mikakati kuhakikisha kwamba kutakuwa na mbegu za kutosha.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo suala la kuongeza tu kiasi cha mbegu inayopatikana, lakini vile vile kuhusu ubora wake.
Mhshimiwa Spika, Bodi ya Pamba kwa kushirikiana
na Wizara na vituo vyetu vya utafiti, tayari kwa muda sasa tunafanyia utafiti mbegu aina ya UKM08 ambayo haina tatizo la ugonjwa wa unyaufu na hivyo tuko mbioni kuondokana kabisa na mbegu UK91 ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikileta usumbufu.
Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba tunapofikia mwaka 2018/2019 tayari mbegu hii mpya, yenye ubora ambayo haina magonjwa itakuwa imeingia sokoni na ifikapo mwaka 2020, mbegu aina ya UK91 itakuwa imeondoka sokoni moja kwa moja. Kwa hiyo, katika miaka hii michache inayokuja tutahakikisha kwamba tuneondokana kabisa na adha ya ugonjwa na ubora usio mzuri wa mbegu ya pamba.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Bodi ya Pamba kuhamia katika maeneo ambayo yanazalishwa pamba, nimfahamishe tu kwamba agizo lile la Mheshimiwa Rais tayari limeshatekelezwa, Bodi ya Pamba wameshahamia Mwanza na kwa kiasi kikubwa tayari imesaidia sana kwa sababu watendaji wanaoshughulika na zao la pamba kila siku tayari wapo karibu nao. Kwa hiyo, inakuwa ni rahisi wao kuweza kufika katika Ofisi za Bodi za Pamba na kupata huduma, lakini vilevile watendaji wenyewe maana ni rahisi wao kufika katika maeneo ya wakulima na kutoa huduma zinazotakiwa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mwezi mmoja uliopita Wizara ilikuwa inazindua umeme wa REA Awamu ya Tatu katika maeneo mbalimbali lakini baadaye wamesimama. Ni lini wanafanya uzinduzi huo katika Mkoa wa Geita na hasa Jimbo la Geita Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli tulianza kuzindua mikoa kumi kwa Tanzania Bara na tulibakiza mikoa takribani 15. Nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu kwamba tumemaliza taratibu zote za kuwapata wakandarasi. Nitumie nafasi hii kwa heshima ya Bunge lako Tukufu kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wote na wananchi kwa ujumla, kesho tarehe 18 Mei, saa 08.00 mchana hapa Mjini Dodoma, kupitia Ukumbi wa Mikutano wa Hazina, wakandarasi wote katika mikoa ya nchi nzima watakabidhiwa katika mikoa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia niwakaribishe Waheshimiwa Wabunge watakaokuwa na nafasi ya kuhudhuria katika ukabidhiwaji wa mikataba hiyo na majukumu yale ili muweze kushiriki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo tutakwenda kuwatambulisha wakandarasi wote mkoa kwa mkoa ili Waheshimiwa Wabunge muweze kufuatilia uwajibikaji wao na orodha pia mtakabidhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue nafasi hii pia kuwataka wakandarasi wote watakaokabidhiwa mikataba yao kesho, waende katika maeneo yao ya kazi na waanze sasa kutekeleza mradi wa REA kwa nchi nzima, kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji na bila kuruka kijiji wala tarafa.
Nichukue nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo umeme haubagui itikadi, umeme pia wa REA hautabagua aina ya nyumba, iwe nyumba ya tembe au vinginevyo, kila aina ya nyumba watapatiwa umeme kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Geita kuna mradi wa maji ambao unafahamika kama LV WATSAN ambao unafadhiliwa na African Development Bank. Ulitakiwa kuwa umekamilika tangu Novemba mwaka wa jana lakini mpaka leo haujakamilika. Nataka kujua mradi huu utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mradi huo hupo na ni mradi mkubwa unakwenda kwa phases. Una financing tatu; iko financing ya Serikali, watu wa madini wa GGM, lakini na financing pia kutoka lile fungu la Lake Victoria Water and Sanitation Project. Mheshimiwa Mbunge, tunakwenda kwa phases, kwa hiyo, kiasi tumeshakamilika na wananchi wanapata maji kama asilimia 30, lakini tunaendelea, hatimaye tuhakikishe tumekamilisha mradi huo ili wananchi wengi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nilitaka kumtaarifu kwamba hiyo Blast Monitoring Committee ilivunjwa na haipo tena, na ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mgodi huu unaendelea na mfumo huu wa ku-blast ambapo kutokana na blasting hii watu wameendelea kupata madhara na tarehe 30 Machi watu nane walizimia, mama mmoja ambaye alikuwa ni mama lishe alizimia karibu siku tatu na kulazwa hospitali, lakini juhudi za Mkuu wa Wilaya za kuwataka watu wa mgodi kwanza walipie matibabu, lakini walipe gharama za mama lishe huyu ziligonga mwama baada ya watu wa mgodi kukataa.
Je, ni utaratibu gani utumike ili wanaoathirika kiafya waweze kulipwa fidia?
Swali la pili, kupitia Bunge na kupitia mikutano kadhaa Mheshimiwa Naibu Waziri na Nishati, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri wa Nishati aliyeondoka walitoa maagizo mengi ya kuhakikisha kwamba waathirika, wa milipuko hii wanalipwa fidia katika eneo la Katoma, lakini mpaka sasa tunapozungumza ni mwaka mmoja umepita. Je, ni lini ahadi hii ya Serikali itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Constantine anavyohangaika na matatizo ya wananchi hasa wa Katoma na Nyamalembo Compound na ninaamini wananchi wanaona juhudi zako Mheshimiwa Constantine.
Mgodi wa GGM kweli umekuwa ukifanya shughuli za ulipuaji na tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu, ulifanya ulipuaji na kama alivyosema Mheshimiwa Constantine kuna mtu mmoja ambaye alipata madhara, kampuni tumeendelea kujadiliana nao na wanaangalia namna ya kufanya fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine huyo mwananchi pamoja na wananchi wengine watafidiwa fidia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini, tuliunda timu kama ambavyo nimeeleza na kwa kweli tumetuma timu zaidi ya mara mbili na sasa hivi timu itakayokwenda sasa kutathmini yale wananchi wenye nyumba 890 ambao nyumba zao zimeathirika, tarehe 05 Juni watakwenda sasa kujadiliana pamoja na wenye nyumba zilizoathirika ili hatima yao ya kulipwa fidia iweze kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine wewe pamoja na uongozi wa Halmashauri pamoja na mgodi na timu itakayoundwa mtashirikishwa ili wananchi hao sasa waanze kulipwa fidia zao.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hospitali ya Geita ambayo sasa hivi ni Hospitali Teule ya Mkoa ilikuwa Hospitali ya Wilaya. Hata baada ya kuipandisha hadhi na kuwa hospitali ya mkoa imeendelea kupata huduma kutoka Serikali Kuu kama hospitali ya wilaya. Je, ni lini Serikali itaipatia huduma kama hospitali ya mkoa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba, kwa sababu imepandishwa, tunalifanyia kazi. Hata hivyo juhudi tuliyofanya kubwa kama Serikali ni kuhakikisha tunaanza hospitali ile kubwa ya Rufaa ya Mkoa, juzi Naibu Waziri wangu nimemtuma kuna kazi kubwa imeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie wananchi wa Geita kwamba Serikali tumejipanga kuboresha sekta ya afya katika Mkoa wa Geita kwa ujumla wake ili kuimarisha hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa na hospitali ya Mkoa na hali kadhalika vituo vya afya, tukijua kutokana na uchimbaji wa madini population imekuwa kubwa katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama Serikali tumelichukua, tutalifanyia kazi kuhakikisha tunapata idadi ya dawa zinazohitajika katika hospitali. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ingawa hakuwa na takwimu kabisa kwenye eneo la madaktari maana yake amekili upungufu uliopo nilioutaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Geita inahudumia takribani wagonjwa 400 kila siku. Na mwaka jana wakati Waziri wa Afya amefanya ziara kwenye Hospitali hiyo aligundua kwamba mpaka wakati tunatoka kwenye bajeti tulikuawa bado tunaichukulia Hospitali ya Geita kama Hospitali ya Wilaya, haikuwa kwenye Hospitali za Mkoa na ndiyo sababu mpaka leo pale tuna specialist mmoja ambaye ni surgeon hatuna kabisa Physiotherapy Doctor, hatuna mtu wa mionzi, hatuna gynaecologist, hatuna mtu wa usingizi kwa sababu ilikuwa inachukuliwa kama Hospitali ya Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu kwa kuwa tumeongeza vituo vingine vya Nyamkumbu na Kasamba tumejenga theater kwa ajili ya upasuaji na kuna wataalam wengi wamezagaa ambao wanaomba ajira. Ni lini Wizara italeta wataalamu wanaoweza kukudhi kiwango cha Hospitali ya Mkoa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Geita ambapo nimesema hatuna wataalam tuna ujenzi wa Hospitali ya Mkoa baada ya kuchukua Hospitali ya Wilaya ambayo tulifanya kuwa Hospitali ya Mkoa, tunajenga Hospitali y Mkoa, lakini speed ni ndogo. Nini kauli ya Serikali ili kuifanya ile Hospitali ya Halmashauri irudi kwa wananchi na huduma ziweze kupungua gharama yake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ilikuwa ni kuhusiana na idadi ya wataalam. Ni kweli lazima nikiri katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kuna changamoto kubwa sana ya Madaktari Bingwa na hilo sisi tumeliona kama nilivyojibu katika swali langu la msingi. Ni kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba tunafanya training ya kutosha Madaktari Bingwa na pale watakapopatikana basi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tutaipa kipaumbele kuongeza idadi ya Madaktari Bingwa ili waweze kutoa huduma pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake lingine la pili lilikuwa lina husiana na kwa nini sasa Serikali isiongeze mkono wake katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na ile iliyokuwepo pale iweze kurudi kuwa Hospitali ya Wilaya.
Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge ni kwamba mwishoni mwa mwaka jana Serikali ilifanya maamuzi ya kuziondoa Hospitali za Rufaa za Mkoa kutoka ngazi za Serikali za Mitaa na kuzipeleka Serikali Kuu. Jukumu hilo sasa na sisi tumelipokea, tumekabidhiwa rasmi na mimi nimuhaidi tu Mheshimiwa Mbunge sasa na sisi tutajielekeza nguvu zetu kuhakikisha kwamba tunazijenga na kuziboresha Hospitali za Rufaa za Mkoa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tulifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini na katika kudhibiti na kusimamia CSR tulielekeza Halmashauri husika kushirikishwa katika mipango. Inaonyesha kwamba huko nyuma taarifa ambazo zipo kwenye Halmashauri zetu ni miradi hii ilikuwa inakuwa inflated na mingi ilikomea njiani.
Ni nini maelekezo ya Serikali kwa sababu migodi itaendelea kusimamia yenyewe na kutangaza kazi yenyewe katika sheria ijayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze tu kwa kueleza kwamba Mheshimiwa Kanyasu kwa muda mrefu amekuwa mtu ambaye ana kilio kikubwa juu ya matumizi ya hizi fedha za CSR zinazotolewa na migodi hapa nchini, wananchi wa Geita wanajua hilo na amekuwa akilisema hata hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sheria mpya ya madini, marekebisho mapya kwenye Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2010 imetoa utaratibu maalum kwa watu wote wenye migodi kutengeneza plan ya matumizi ya CSR na kuipeleka kwenye Serikali ya Halmashauri ili iweze kupata approval.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto imejitokeza kwenye migodi mingi ambapo ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu inflation ya bei ya vitu imekuwa kubwa mno na miradi mingi imekuwa miradi ambayo haifiki mwisho. Sasa kama Wizara tunaandaa utaratibu wa kukagua CSR ambazo zimekwishakutolewa ili tuone kama kweli fedha hizi zilizotolewa ziliwafikia wananchi na halikuwa jambo la kutegeshea tu. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Tanzania ni nchi pekee ambayo mwakilishi wa nchi akifungwa, Waziri anakuja anashangilia Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu lilikuwa relevant kwenye msimu wa 2016/2017 na limechelewa. Lakini naomba niishukuru Wizara kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu huu wa 2018/2019 katika Kata za Ihanamilo, Nyanguku na Bulela nilimjulisha Mheshimiwa Waziri kwamba limekuwepo tatizo la pamba kurefuka na hazitoi matunda. Kutokana na sababu hiyo wakulima katika maeneo hayo wameshindwa kufahamu kama utafiti huu wa mbegu za pamba ulikuwa universal katika nchi nzima.
Sasa swali langu ni lini Wizara itatuma wataalam kwenda katika maeneo hayo ili tuweze kufahamu sababu za kwa nini pamba hiyo imerefuka tu na imeshindwa kuzaa matunda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wakulima katika maeneo yao walikopeshwa pembejeo na msimu wa ununuzi wa pamba umeanza na uzalishaji ulikuwa mbaya na ni lazima wakatwe, ni nini kauli ya Serikali katika suala hilo? Nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kusema kweli kwamba swali lenyewe la msingi lilikuwa limepitwa na wakati kwa sababu katika msimu huu hatukuwa na ushahidi wa mahali popote kwamba mbegu tuliyoisambaza ilishindwa kuota, taarifa tuliyokuwa nayo ni kwamba imeota vizuri maeneo yote na kwa hiyo namshukuru sana kwa uungwana wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika maswali yake ya nyongeza, ni kweli taarifa kwamba pamba imerefuka kuliko ilivyotarajiwa ipo maeneo mengi, na tumewatuma tayari watafiti wetu wa Chuo cha Ukiriguru kwenda maeneo mbalimbali kujionea wenyewe na kutafiti ni sababu gani inayosababisha pamba ile irefuke. Suala ambalo kwa tafiti ya awali wamesema ni kuongezeka kwa mvua, mvua imenyesha nyingi kuliko ilivyokuwa kawaida kwa hiyo pamba imerefuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukosa vitumba, yapo maeneo ambako viuadudu vilichelewa kufika na wakulima wa maeneo hayo hawakuwa wamepulizia kwa wakati kwa hiyo vitumba vingi vikawa vimekwishaharibiwa na ndiyo maana huenda pamba ile inarefuka. Wale ambao hawakuvuna vizuri, tusubiri kwanza kwa sababu sasa hivi baada ya mvua kuanza kupungua pamba nyingine bado iko inatoa matunda na huenda pia mavuno yao yakawa mazuri tu bila tatizo lolote ingawa tayari watafiti wetu wako maeneo mbalimbali wanafuatilia jambo hili.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ziwa Victoria lina samaki wa aina nyingi, ukiacha sangara tuna samaki aina ya gogogo, nembe na furu, lakini aina ya nyavu ambazo Wizara na Serikali inaruhusu kuvua ni nyavu ambazo zinavua sangara peke yake. Nataka Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie hawa samaki wengine wanavuliwa kwa zana za aina gani, ikizingatiwa kwamba wanapatikana kwenye maji marefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli Ziwa Victoria lina aina nyingi ya samaki wakiwemo hawa aliowataja samaki aina ya gogogo, nembe na furu. Samaki hawa upo wakati ambapo hawakuwepo na ni kweli kanuni na sheria zetu haziwataji moja kwa moja samaki hawa. Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tupo katika hatua sasa ya kuhakikisha kwamba samaki hawa nao wanatajwa na sheria na kanuni zetu ilimradi waweze kuingizwa katika hata vifaa vya kuweza kuwavulia na wananchi na wavuvi waweze kupata faida ya rasilimali hizi za nchi yetu. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kwa mujibu wa Kanuni za Uvuvi, ukienda kifungu cha 45(3)(b), naomba nisome, kinasema:-
“No person shall: (b) fish, land or possess, process or trade in Nile tilapia or fish locally known as “Sato” the total length of which is below 25 centimetres.”
Mheshimiwa Spika, ukisoma Kanuni hii, ni kama inafikiria source ya Sato ni moja tu, Nile Tilapia lakini sasa Tanzania tuna-encourage watu kufanya aquaculture, maana yake sources za sato ziko nyingi, lakini tuna maziwa na mito na Kanuni hii imetumika kusababisha usumbufu mkubwa sana kwa watumiaji wa sato nchi nzima. Ni lini Serikali au ni kwa nini Serikali isisitishe sasa kukamata watu kwa kutumia Kanuni hii ambayo yenyewe tu inajichanganya na ina makosa mpaka itakapofanyiwa marekebisho? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kwa swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Kanyasu, lakini nimpongeze sana Naibu wangu kwa majibu mazuri sana aliyoyatoa hapo awali.
Mheshimiwa Spika, kama alivyoisoma Kanuni yetu na kama Naibu Waziri alivyoeleza, mwezi huu wa Saba, Wizara yangu itakuwa imemaliza zoezi la kufanya mapitio ya Kanuni ya Uvuvi pamoja na Sheria yenyewe ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003. Vilevile kwa nyongeza ni kwamba operesheni hizi zinazoendelea na wananchi wetu ambao wanajishirikisha na ufugaji wa samaki, kila wanapofikia kuvuna samaki wao wanawasiliana na ofisi yangu ambayo inakuwa inazo taarifa za uhakika juu ya uvunaji wa samaki hao ili kusije kukatokea usumbufu wa aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kipindi ambacho Kanuni inarekebishwa, utaratibu umewekwa na Wizara kwa maana ya kwamba mawasiliano yako proper ya namna ya uvunaji kwa sasa wakati tunatengeneza Kanuni ambayo itakuwa ime-favour uvunaji wa samaki katika Ziwa Viktoria lakini wakati huohuo na wale wafugaji wetu wa samaki ambao wanafuga samaki kwenye maji.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Swali la kwanza, kiuchumi kukamilika kwa reli hii kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma itakuwa hakuna tija kama kipande cha kutoka Dodoma kwenda Mwanza na kutoka Dodoma kwenda Mpanda na Kigoma kitakuwa haijakamilika. Tumeshuhudia uwekaji wa saini mikataba hapa karibuni kwa vipande hivi viwili. Sasa ni lini mikataba hii ya kipande kinachoanzia hapa kwenda Mwanza, Kigoma na Mpanda itasainiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, moja ya sababu ya bidhaa za viwandani kuwa bei kubwa sana katika Mikoa ya Geita na Kagera ni kwa kuwa usafirishaji katika maeneo haya unategemea barabara. Kwa kuwa kipande cha Isaka kwenda Kigali kitakamilika, ni upi mpango wa Serikali kujenga reli ya kutoka kwenye chanzo chochote kwenda Geita na Kagera?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imeshaanza ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari taratibu za kuanza mchakato wa ujenzi wa kipande cha kutoka Makutupora mpaka Tabora umeshaanza. Tayari upembuzi yakinifu umekamilika na usanifu wa kina tayari umekamilika, tunatafuta pesa kama Serikali kwa ajili ya kuanza mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, tunao mpango wa kujenga kipande cha Geita – Lusahunga mpaka Uganda na taratibu zitakapokamilika, Mheshimiwa Mbunge atataarifiwa kama inavyopaswa. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kabla ya Mkongo wa Taifa ilikuwa ukinunua GB10 ni Sh.10,000 lakini baada ya Mkongo wa Taifa gharama imeongezeka sasa ukinunua GB10 ni Sh.35,000. Nilitaka kupata maoni ya Mheshimiwa Naibu Waziri anaposema gharama imeshuka kwenye data ana maana gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wakati wa Mkongo wa Taifa unapigiwa debe, tuliambiwa utakwenda katika kila halmashauri na taasisi za umma ili kusaidia taasisi hizo kwanza kuwa informed na information system lakini kusaidia katika shughuli mbalimbali. Ni kwa kiwango gani agizo hili limetekelezwa katika taasisi za umma na halmashauri zote nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Constatine John Kanyansu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utafuatilia jibu langu la msingi, nimeeleza kwa ujumla jinsi ambavyo Mkongo umesaidia kupunguza gharama za matumizi na kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanapata huduma za mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la Mheshimiwa Kanyasu linahusu kwa nini kabla ya Mkongo kulikuwa na huduma ambazo ni nafuu, kwa jinsi anavyoona yeye. Tukumbuke kwamba kabla ya Mkongo watumiaji walikuwa wachache sana sasa hivi napozungumza, huduma zimeendelea kushuka. Hiyo gharama aliyoisema ni ya kujiunga na vifurushi, kama hujiungi na vifurushi, ukiweza kupata Sh.10,000 peke yake unaweza ukapata GB nyingi za kutosha kutegemeana na aina ya mtandao ambao unautumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uunganishwaji wa taasisi mbalimbali, napenda nimweleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi tumeunganisha taasisi za Serikali na Agency zake jumla 72, Local Government Authorities nazo tumeunganisha 77, taasisi mbalimbali kama vyuo na watafiti, RITA na huduma za afya tumeunganisha jumla 207.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba kumshukuru pia Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amekiri Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mahitaji halisi ya watumishi ni 469 na tulionao ni 162 na mwaka huu wakati Serikali imeajiri ilipeleka watumishi 20 wakati huo huo tunazo tayari zahanati 24 zimekamilika ambazo zimekuwa hazifanyi kazi. Sasa swali langu la msingi lilikuwa ni lini Serikali itahakikisha inapeleka watumishi wa kutosha ili zahanati hizo ambazo tayari zimekwishajengwa ziweze kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala ya TAMISEMI katika ziara tumethibitisha kwamba hospitali na zahanati ambazo zimefungwa mifumo ya ukusanyaji mapato zinapata pesa nyingi na zinafanya vizuri Zaidi. Kwa nini Serikali haioni jambo hili linaweza kuwa la kipaumbele ili maeneo ambayo yana network jambo hili likafanyika kwa haraka kuliko kuzungumzia zahanati zaidi ya 20 kutenga milioni 20?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Constantine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Geita na kama ambavyo nimetangulia kujibu kwenye swali la msingi kwamba Serikali inatambua upungufu huu na ndio maana kwenye ajira zilizopita moja ya halmashauri ambazo zilipata kipaumbele cha kuwa na watumishi wa kutosha ni Mji wa Geita. Lakini kwenye ajira zinazofata naomba nimhakiksihie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutoa kipaumbele cha kutosha kwa Mji wa Geita ili tuweze kupunguza pengo hili kubwa la watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Geita.

Mheshimiwa Spika, pili ni kweli kwamba mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki ambao ni mfumo uliobuniwa na Serikali yetu wa GOT- HOMIS umeboresha sana mapato ya uchangiaji wa huduma za afya na mpango wa Serikali pamoja na kuelekeza halmashauri kuhakikisha zinatenga fedha za mapato ya ndani kufunga mifumo hii kwenye zahanati, vituo vya afya na ustawi za halmashauri tumeongea na wadau ili kuweka mkakati ambao utakuwa na muda maalum wa kuhakikisha tunashirikiana nao kufunga mifumo hii maeneo yote ambayo inaweza ikatumika na kuboresha mapato. Kwa hivyo suala hili tumelichukua kwa utaratibu huo pia wa kuweka mkakati maalum kabisa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kulitekeleza, nakushukuru sana.