Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Constantine John Kanyasu (39 total)

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mji Mkongwe wa Mikindani uliopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani unakuwa kivutio cha utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara imeweka mkakati mahsusi wa kuendeleza Mji Mkongwe wa Mikindani na kuutangaza ndani na nje ya nchi kama kivutio cha utalii. Mwaka 2016 Wizara kupitia Idara ya Mambo ya Kale ilianzisha kituo kipya cha mambo ya kale ndani ya Mji wa Mikindani. Kwa kuanzia Wizara imepeleka watumishi wawili na itaendelea kuongeza idadi ya watumishi kadri upatikanaji utakavyokuwa. Kituo hicho kimelenga kusimamia uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale zinazopatikana katika Mji Mkongwe wa Mikindani. Aidha, mwaka 2017 kupitia Tangazo la Serikali namba 308 Wizara ilitangaza mji huu kuwa urithi wa utamaduni wa Taifa. Mji Mkongwe wa Mikindani ni kati ya maeneo…
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-

Kilwa ni moja kati ya miji mikongwe katika Afrika Mashariki tangu 900 – 1700 AD ikiwemo Lamu, Mombasa, Sofaa na Zanzibar. Miji hii ilipewa heshima ya jina la urithi wa dunia (World Heritage Sights) na husaidiwa na mataifa mbalimbali kama Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza na Taasisi ya UNICEF;

Je, Serikali ya Tanzania inafaidika na nini kutokan kwenye mataifa hayo yanayosaidia nchi zenye Miji ya Urithi wa Dunia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Urithi wa Dunia yanaratibiwa kimataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization – UNESCO) kupitia mkataba wa mwaka 1972 na ulinzi na uhifadhi wa urithi wa dunia. Mji wa Kilwa una magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo ni miongoni mwa maeneo ya urithi wa utamaduni ambayo yalipewa hadhi ya urithi wa dunia mwaka 1981. Maeneo mengine ya urithi wa utamaduni yenye hadhi hiyo ni pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, Michoro ya mapangoni ya Kolo – Kondoa na urithi mchanganyiko wa Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo manufaa ambayo Serikali ya Tanzania inafaidika kutoka kwa mataifa mbalimbali na nchi wahisani kwa kuwa na maeneo yenye hadhi ya urithi wa dunia. Kuwa na maeneo ya aina hii kunasaidia kuwepo kwa juhudi za pamoja za kimataifa za kuhifadhi, kulinda na kuyaendeleza maeneo haya. Manufaa haya yanaweza kugawanywa katika makundi matatu ambayo ni ushauri wa kiufundi katika masuala ya uhifadhi, misaada ya kifedha na kulitangaza eneo kiutalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya manufaa ambayo Mji wa Kilwa umepata kwa kuwa ni hadhi ya urithi wa dunia ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2002 – 2005 ulifanyika ukarabati wa msikiti mkuu na mdogo pamoja na kubwa, yalitolewa mafunzo kwa mafundi sanifu, ilinunuliwa gari na ukarabati wa boti kwa ufadhili wa Serikali ya Ufaransa wenye thamani ya Euro 660,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2005 - 2008 ulifanyika ukarabati wa Kasri ya Sultani, ununuzi wa mashine ya boti, ukarabati wa nyumba ya wageni ya Kijerumani, ujenzi wa kinga maji eneo la Gereza la Kale na ujenzi wa Birika la Maji la Songo Mnara kwa ufadhili wa UNESCO na Norway wenye thamani ya USD 201,390.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 – 2009 yalitolewa mafunzo kwa waongoza wageni, mapishi, usindikaji wa chakula pamoja na uanzishaji wa vikoba kwa wananchi, uandaaji wa kitabu cha urithi wa Kilwa kwa ufadhili wa UNESCO na Serikali ya Ufaransa wenye thamani ya USD 159,780.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 – 2014 ukarabati wa majenzi Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kwa ufadhili wa Ubalozi wa Marekani wenye thamani ya USD 700,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi hii yote unafanyika kwa kushirikisha wananchi kwa kuwapatia mafunzo ya uhifadhi na kufanya ukarabati wenyewe. Aidha, wananchi wanapatiwa mafunzo ya namna ya kutumia fursa za utalii ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uongozaji watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuishukuru UNESCOna nchi wahisani kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza maeneo haya yenye urithi wa utamaduni.
MHE. VEDASTO E. NGAMBALE aliuliza:-

Hifadhi ya Akiba ya Selous imekuwa ikihamisha alama za mipaka na kuchukua eneo la ardhi ya vijiji katika Jimbo la Kilwa Kaskazini bila ya kushirikisha Serikali ya Vijiji:-

Je, Serikali iko tayari kusimamia Mamlaka ya Hifadhi hiyo kurudisha alama za mipaka katika maeneo ya awali ili kuepusha mgogoro unaoweza kutokea?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii inalo jukumu la kusimamia uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu kwa kuzingatia uwepo wa mahusiano mazuri kati ya wananchi na maeneo yanayohifadhiwa. Jukumu hilo linatekelezwa kwa pamoja na mambo mengine kwa kutambua kulinda, kupitia upya na kuweka vigingi (beacons) katika mipaka ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliagizwa kuweka vigingi kwenye mipaka ya hifadhi zote nchini kwa lengo la kuonesha mipaka kati ya hifadhi na vijiji ili kuepusha migogoro na uvamizi unaofanywa na wananchi na kusababisha malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza maagizo haya, Wizara inafanya kazi ya kusimika vigingi kwenye mipaka ya mapori yote ya akiba likiwemo Pori la Akiba la Selous. Aidha, zoezi la upitiaji, uhakiki na usimikaji wa vigingi katika Pori la Akiba la Selou upande wa Kilwa Kaskazini limefanyika katika Kijiji cha Namatewa. Zoezi hili limefanyika kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya pamoja na Uongozi wa Vijiji kwenye maeneo hayo. Kazi ilifanyika kwa kutumia Tangazo la Serikali Na. 275 la Mwaka 1974 lililoanzisha pori hilo na ramani za vijiji husika kwa kushirikiana na Wapima wa Ardhi wa Wilaya zinazopakana na mapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mpaka wa Pori la Akiba la Selous ambalo halijasimikwa vigingi upande wa Kilwa Kaskazini ni katika Vijiji vya Mtepera na Zinga Kibaoni. Hii ni kutokana na wananchi wa vijiji husika kutotambua ukomo wa mpaka kwa mujibu wa ramani za vijiji vyao wakidai eneo linalosalia ni la kijiji na siyo la hifadhi. Kwa mantiki hiyo, hakuna uhamishaji wa alama za mpaka uliofanywa kwa nia ya kuchukua eneo la ardhi la kijiji karibu na Pori la Akiba la Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara zingine sita, imeelekezwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya maeneo yenye ubishani na migogoro ikiwa ni pamoja na vijiji na kuangalia mipaka ili kuondoa migogoro hiyo. Kwa sasa Wizara inaendelea kuweka utaratibu mzuri wa namna ya utekelezaji wa agizo hilo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga geti la kuingilia Hifadhi ya Mkomazi katika Kijiji cha Kivingo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII aljibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Mkomazi ipo Wilaya za Same, Mwanga, Lushoto, Korogwe na Mkinga. Kwa sasa wageni wote wanaotembelea hifadhi hii hutumia lango la Zange lililopo katika Wilaya ya Same.

Mheshimiwa Spika, katika mpango na bajeti wa mwaka fedha 2019/2020, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa lango la wageni katika eneo la Kamakota, jirani na Kijiji cha Kivingo Wilayani Lushoto. Lango hilo limetengewa kuhudumia wageni wanaotumia barabara ya Tanga – Lushoto - Mlalo - Kihurio na Same.

Mheshimiwa Spika, sanjari na ujenzi wa lango la wageni eneo la Kamakota, Shirika la Hifadhi za Taifa limeweka kwenye mpango wake maeneo yanyotarajiwa kuwekewa malango ambayo ni Njiro (Wilaya ya Same), Ndea (Wilaya ya Mwanga) na Umba (Wilaya ya Mkinga).
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Msitu wa Nyera – Kipelele ni miongoni mwa misitu ya asili iliyopo Wilaya ya Liwale. Serikali imekuwa ikiandaa taratibu za uvunaji wa mazao ya msitu huo.

(a) Je, taratibu hizo zitakamilika lini?

(b) Je, Serikali imepata manufaa gani kutokana na uhifadhi wa msitu huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Nyera – Kipelele ni hifadhi ya msitu ulio chini ya umiliki wa usimamizi wa Serikali Kuu (Wakala wa Misitu wa Huduma Tanzania). Misitu hiyo ipo katika Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi, Msitu wa Kipelele ulitengwa kuwa hifadhi ya Serikali Kuu katika Tangazo la Serikali Na. 79 la mwaka 1956 ukiwa na eneo la hekta 98,423. Msitu huo umezungukwa na vijiji tisa, ambavyo ni Kichonda, Nyera, Kimambi, Mtawatawa, Kitogoro, Litou, Legezamwenda, Kipelele na Naujombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kuandaa uvunaji wa mazao ya msitu katika msitu huo zimekamilika mwaka 2018, baada ya kuandaliwa kwa mpango wa usimamizi wa msitu (Management Plan) na mpango wa uvunaji (Harvesting Plan). Kwa mujibu wa mpango wa usimamizi, kiasi cha hekta 59,053 katika msitu huo zina miti ya kuweza kuvunwa. Aidha, miti ya ujazo 19,970 zimepangwa kuvunwa kuanzia mwaka
2019/2010 kwa kufuata mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu.

Mheshimiwa Spika, manufaa yanayopatikana kutokana na uhifadhi wa msitu huo ni makazi ya wanyamapori aina tofauti wakiwemo tembo, uboreshaji wa mifumo ya kiikolojia ikiwemo hifadhi ya hewa ya ukaa. Aidha, ni vyanzo vya maji katika Vijiji vya Mtawatawa, Kitogoro, Legeza mwendo, Kipelele na vilevile hifadhi hiyo ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali.
MHE. JORAM I. HONGOLI (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:-

Ili kuboresha utalii katika Hifadhi ya Kitulo, Serikali iliahidi kupeleka wanyama wasio wakali yaani pundamilia 25, lakini mpaka sasa bado wanyama hao hawajapelekwa licha ya Serikali kuahidi kuwa itatekeleza mwezi Mei na Juni mwaka 2018.

(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?

(b) Je, ni lini Serikali itaongeza aina ya wanyama kama vile paa na swala?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norman Adamson Sigalla, Mbunge wa Makete, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishatekeleza ahadi ya kupeleka Wanyamapori wasio wakali katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo mnamo mwezi Oktoba, 2018 ambapo pundamilia 24 walihamishwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kupelekwa Kitulo. Zaoezi lilifanyika mwezi Oktoba kipindi ambacho hali ya hewa ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo inafanana na hali ya hewa ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuongeza pundamilia wengine 26 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenda Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, kufikia mwisho wa mwaka 2019/2020. Lengo ni kupandisha idadi ya pundamilia katika Hifadhi ya Kitulo kufikia 50. Pia sambamba na hilo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali inatarajia kupeleka katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo wanyamapori wengine aina ya swala pala wapatao 50 na kuro wapatao 30.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mwaka 2017 wakati Mheshimiwa Rais akiwa katika ziara Mkoa wa Kigoma, katika Wilaya ya Kasulu aliwaruhusu wananchi waliokuwa wakilima katika maeneo ya Hifadhi ya Makere (Kagera Nkanda) kwa sharti kwamba wasiongeze maeneo mengine zaidi ya yale waliyokuwa wakilima:-
Je, kwa nini TFS wanapingana na agizo la Mheshimiwa Rais na wanawatesa wananchi kwa kuwapiga na kuwanyan’ganya baiskeli na pikipiki?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Rais kuagiza kumegwa kwa sehemu ya msitu wa Makene Kusini ili kutoa maeneo kwa wananchi kulima Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu ilitekeleza agizo kikamilifu kwa kupima eneo la msitu huo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia upimaji huo jumla ya hekta 10,012.61 zilitengwa kwa ajili ya kilimo kwa wananchi wa maeneo hayo. Hivyo Kijiji cha Uvinza kilipewa hekta 2,174 na Kagera Nkanda kikapewa hekta 2,496; na eneo lingine la hekta 5,342.61 zilitengwa kwa ajili ya wananchi wengine wa vijiji vya Nachenda, Mgombe na Nyakitonto.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kijiji cha Uvinza kililalamika kuwa eneo walilopata halitoshi hivyo wakaomba waongezewe eneo ambalo ni ardhi chepechepe yaani ardhi oevu karibu na Mto Makene na Mto Malagarasi ambalo kitaalam hairuhusiwi kulima kwa sababu itasababisha uharibifu mkubwa na kupotea kwa sifa ya uhifadhi. Mto Malagarasi ni muhimu kwa ikolojia na kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya umeme wa maji katika maporomoko ya Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa wananchi wanaendelea na shughuli za kilimo katika maeneo hayo yaliyotengwa na kuridhiwa na vikao vyote vya Mabaraza ya Mkoa na Wilaya. Wizara kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa imekamilisha mchakato wa ramani mpya ya msitu huo.
Mheshimiwa Spika, tatizo lililojitokeza sasa ni kwa wananchi wachache kwa maslahi yao kukataa kufuata taratibu na kutaka kulima ndani ya msitu nje ya maeneo yaliyotengwa huku wengine wakiendelea na uwindaji haramu wa wanyamapori. Wananchi hao wasiofuata sheria ndio waliozuiwa na mamlaka husika kwa Sheria ya Misitu namba 14 ya mwaka 2002, Sura 323 katika kifungu cha 26 ambacho kinakataza kufanya shughuli zozote za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo na ufugaji ndani ya msitu wa hifadhi. Mtu yoyote akibainika kufanya hivyo hatua za kisheria hufuatwa.
Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wananchi kuendelea na kilimo katika maeneo yaliyotengwa na kuachana na kilimo cha kuhamahama ambacho ndicho kinachowafanya kuvamia maeneo ya hifadhi za misitu. Aidha, natoa ushauri kwa wananchi kufuata kanuni bora za kilimo kwa kutumia mbolea ili mashamba yao yaendelee kuzalisha mazao wakati wowote.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-

Mipaka ya Mradi wa Mafunzo ya Msitu wa Kijiji cha Igwata, Kata ya Nyabubinza, Wilaya ya Maswa imepanuliwa na kuchukua baadhi ya Mashamba ya Wanakijiji na hivyo kusababisha wananchi kukosa maeneo ya kulima:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wananchi hao ili waweze kununua maeneo mengine ya kufanya shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa Hifadhi ya Igwata unahifadhiwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Na. 324 la Mwaka 1953. Msitu huo una eneo la ukubwa wa hekta 132,851 ambapo hekta 85.19 ziko Wilaya ya Kwimba na hekta 47.678 ziko Wilaya ya Maswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ilianza kusimamia Msitu wa Igwata tangu mwaka 2010. Aidha, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1953 msitu huu haujawahi kupanuliwa; katika mwaka 1915/1916 kazi zilizofanyika ilikuwa ni uimarishaji wa mpaka, uwekaji wa maboya ambao ulifanywa na TFS kwa kushirikiana na uongozi wa vijiji vyote vinavyozunguka msitu huo. Vilevile mwaka 2015/2016 kazi ya tathmini, Forest Inventory, ilifanyika kwa ajili ya kutayarisha mpango wa usimamizi wa msitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara haijawahi kupokea malalamiko au madai yoyote ya wananchi kuchukuliwa mashamba yao kwa lengo la kuongeza ukubwa wa eneo la msitu. Aidha, hakuna mgogoro kati ya wananchi na taasisi zinazosimamia msitu huu, wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano katika usimamizi na ulinzi wa msitu huo ambao ni hazina kubwa ya mbegu za miti asilia na urithi wa aina ya miti iliyopo katika hatari ya kutoweka ambayo inatumika katika tiba za jadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Wananchi wengi wameendelea kupoteza maisha na kujeruhiwa na mamba katika Mto Ruvuma:-

Je, ni lini wananchi walioathirika na mamba katika Vijiji vya Miesi Utimbe, Naliongolo, Mtolya, Geuza na Mchoti watalipwa fidia zao kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikilipa kifuta machozi kwa wananchi ambao wameshambuliwa na wanyamapori wakali kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Machozi za Mwaka 2011. Kuanzia mwaka 2013 mpaka 2018 jumla ya Sh.37,300,000/= zimelipwa kwa wananchi 65 waliopatwa na madhara kutokana na wanyamapori wakali, hususan mamba, katika Wilaya ya Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza matukio ya wananchi kuendelea kupoteza maisha na kujeruhiwa na mamba, hasa wanapokwenda kuchota maji mtoni, Wizara kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imechimba visima vya maji tisa katika vijiji vilivyo kandokando ya Mto Ruvuma. Vijiji hivyo, ni chipingo, Nalimbudi, Chikolopora, Maparawe, Mbangala, Geuza na Mkowo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika kukabiliana na changamoto za athari zilizosababishwa na mamba, mwezi Julai, 2016, Wizara ilitoa kibali kwa Kampuni ya Ontour Tanzania Limited ambayo ilivuna mamba nane katika Mto Ruvuma na kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya wananchi kujeruhiwa na kuuawa na mamba. Mfano katika kipindi cha Februari, 2018 mpaka sasa Wizara yetu haijapokea taarifa yoyote kuhusu wananchi waliouawa na kujeruhiwa na mamba katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Katika kijiji cha Fanusi, Kata ya Kisiwani, Wilayani Muheza wapo wananchi wanaofanya biashara ya kutega vipepeo na kuvipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata kipato na pia njia ya kukuza utalii:-

(a) Je, ni lini wataruhusiwa kupeleka tena vipepeo nje ya nchi badala ya Serikali kuzuia kama ni wanyama hai?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuboresha maeneo hayo ili kuwavutia watalii waweze kuja kwa wingi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Jimbo la Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipepeo ni moja ya aina za wanyamapori waliokuwa wakifanyiwa biashara ya wanyamapori hai kwa kusafirishwa nje ya nchi kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wafanyabiashara kukiuka Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni zake; Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Mei, 2016. Aidha, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, Serikali imeamua kuendelea kufunga biashara ya usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi. Kufuatia uamuzi huo, Wizara inaandaa namna bora ya kushughulikia wanyamapori waliopo kwenye mashamba/ mazizi. Aidha, wafanyabiashara walioathirika kutokana na zuio la kusafirisha wanyamapori nje ya nchi watarudishiwa fedha zao walizotumia kulipia Serikalini kwa ajili ya huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaboresha maeneo ya kuvutia watalii yaliyopo katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Amani ambapo Kijiji cha Fanusi na vijiji vingine 20 vinapakana. Hifadhi hiyo ina vivutio vingi ikiwemo misitu minene, mito, wanyamapori na mimea adimu isiyopatikana maeneo mengine duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu huo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS inatekeleza mpango wa kuendeleza utalii wa ikolojia na kiutamaduni katika hifadhi ya Amani. Mpango huu unahusu kuboresha miundombinu ikiwemo barabara ya kuelekea Msitu wa Amani, nyumba za kulala wageni zilizopo ndani ya msitu, vituo vya kupumzikia watalii (camp sites) na njia za watalii (nature trails). Juhudi hizi zinatarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kuongezeka kwa biashara, fursa za ajira na uwekezaji kwa maeneo yaliyo karibu na msitu huo.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-

Kulikuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo; wananchi wa vijiji hivyo walienda mahakamani na wakaishinda TANAPA kwa sababu mipaka iliyokuwa iwewekwa na TANAPA haikuwa shirikishi na haikufuata GN iliyoanzisha SENAPA:-

(a) Je, ni lini Serikali itapitia upya mipaka hiyo kwa kushirikisha vijiji husika na kuzingatia GN iliyoanzisha SENAPA?

(b) GN iliyoanzisha IKorongo Game Reserve inatofautiana na mipaka iliyowekwa; je, ni lini marekebisho yatafanyika ili iendane na GN?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, migogoro ya mipaka kati ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti na baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo haujatatuliwa kwa kuwa yapo madai ya Rufaa ya Ardhi Namba 256 ya mwaka 2018 katika Mahakama Kuu ya Jiji la Mwanza dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama. Utatuzi wa mgogoro huo unasubiri matokeo ya rufaa iliyowasilishwa Mahakama Kuu dhidi ya hukumu iliyotolewa awali. Baada ya maamuzi ya mahakama kutolewa, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na vijiji husika itapitia upya mipaka kati ya hifadhi na vijiji kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama.

(b) Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Ikorongo lilianzishwa kisheria kwa GN 214 ya tarehe 10 Juni, 1994. Hapo awali pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambayo iliweka alama za mipaka ya pori hilo mwaka 2000 kwa kuzingatia GN husika. Aidha, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha Park Nyigoti yaliyoifikia Wizara yangu, kuwa sehemu ya eneo la kijiji hicho lipo ndani ya Pori la Ikorongo.

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuwepo kwa malalamiko hayo, Wizara itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi yenye malalamiko ikiwemo kijiji cha Park Nyigoti ambacho kinapakana na Pori la Akiba Ikorongo.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-

Je, Serikali iko tayari kubadilisha sheria/kanuni ili kuruhusu mazao ya misitu kusafishwa usiku na mchana (saa 24)?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kuzuia Kusafirishwa kwa Mazao ya Misitu Na. 68 ya 2000, iliwekwa kutokana na changamoto za usafirishaji haramu wa mazao ya misitu ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni vigumu sana kudhibiti uhalifu huo wakati wa usiku. Ukaguzi wa kina wa mazao ya misitu hufanyika kwenye kituo cha mwanzo cha safari na vituo vya ukaguzi vilivyoko barabarani kwa kukagua nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kibali cha usafirishaji na kuangalia aina ya mazao, jamii ya miti na kiasi kinachosafirishwa. Kutokana na ugumu wa ukaguzi nyakati za usiku Serikali ilitunga Sheria ya Kuzuia Usafirishaji wa Mazao ya Misitu Nyakati za Usiku.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine iliyopelekea kuwepo kwa zuio la kusafirisha mazao ya misitu usiku wakati huo ni pamoja na uhaba wa watumishi, udanganyifu na ubadhirifu hali ambayo kwa sasa imeshughulikiwa. Hivyo, Wizara itaanza kutoa vibali maalum kwa wasafirishaji wa mazao ya misitu ya kupandwa kusafirishwa masaa 24. Mfano, mwaka 2018 kupitia Tangazo la Serikali Na. 478, Serikali imetoa kibali cha kusafirisha usiku nguzo za umeme kwa saa 24 ili kuharakisha usambazaji wa umeme vijijini.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE aliuliza:-

Katika kikao cha kazi, Mheshimiwa Rais akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alitoa maelekezo ya kutoondoa Vijiji vilivyomo katika maeneo ya Hifadhi:-

(a) Je, tangazo hilo linamaanisha kuwa wameruhusiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi katika maeneo yao wanayoishi?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itashughulikia migogoro ya mipaka baina ya Vijiji hivyo na Hifadhi au kwa tamko lile maana yake Wanavijiji waendelee kama vile hakukuwahi kuwa na migogoro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Januari, 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo la kutoviondoa vijiji 366 vilivyoainishwa kuwa na migogoro na maeneo ya hifadhi. Aidha, alisisitiza kwamba agizo hilo halina maana kwamba sasa wananchi wanaruhusiwa kuvamia maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo hayo, Kamati Maalum kwa lengo la kumshauri Mheshimiwa Rais namna bora ya kutekeleza agizo hilo iliundwa. Kamati hii inaongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi. Wizara nyingine zinazohusika ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Wizara ya Maliasili na Utalii, Mifugo, Uvuvi, TAMISEMI, Ulinzi, Kilimo na Maji. Jukumu la Kamati litakapokamilika, taarifa itawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na maelekezo yatatolewa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kufuatia Kamati kukamilisha kazi yake na taarifa kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii itapitia upya mipaka ya hifadhi mbalimbali kwa kuzingatia ushauri wa Kamati na maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Kazi hii itahusisha uwekaji wa vigingi vipya (beacons) katika mipaka yote.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itachukua hatua za kimkakati kuhakikisha kwamba migogoro kati ya wafugaji na wananchi wanaoishi pembezoni mwa mbuga za wanyama inakwisha kabisa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuwepo kwa migogoro mingi baina ya wafugaji na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa agizo la kutoviondoa vijiji 396 vilivyoainishwa kuwa na migogoro katika maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mheshimiwa Rais kutoa agizo hilo kamati maalum iliundwa kwa lengo la kumshauri juu ya namna bora ya kutekeleza agizo hilo. Kamati hiyo iliongozwa na Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara zingine zilizohusika ilikuwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Ofisi ya Maliasili na Utalii, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Kilimo na Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imekamilisha utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo ya Serikali kuhusu suala hilo yatatolewa na kwa wananchi.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-

Kuna taarifa kwamba nchi ya Kenya inatarajia kutekeleza mpango wa kujenga mabwawa makubwa kwa ajili ya uzalishaji umeme. Kwa kuwa ujenzi huo unatishia ustawi wa uwepo wa Hifadhi ya Taifa Serengeti. Je, Serikali ya Tanzania inachukua hatua gani kuhusu mpango huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maluum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 Serikali ilipata taarifa ya mpango wa ujenzi wa mabwawa ya umeme uliopangwa kutekelezwa na Serikali ya Kenya. Wizara ilifanya uchunguzi wa madhara yatakayosababishwa na miradi hiyo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa kukusanya takwimu za mtiririko wa maji na kulinganisha na mahitaji halisi ya miradi iliyotarajiwa. Uchunguzi ulibaini kuwa utekelezaji wa miradi hiyo, ungesababisha athari kubwa ya kiikolojia ya Serengeti kwani takwimu zilizotumiwa na wataalam wa nchini Kenya kuhalalisha mradi huo hazikuwa sahihi. Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kuhatarisha ustawi wa maisha ya viumbe hai kutokana na ukosefu wa maji katika Mto Mara wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya Mto Mara yanajadiliwa na Tume ya kuratibu Bonde la Ziwa Victoria (Lake Victoria Basin Commission) chini ya Wizara ya Mambo Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aidha, majadiliano mbalimbali kuhusu hatima ya Mto Mara au miradi inayoathiri maji ya Mto Mara ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Ewaso, Ngiro nchini Kenya yanaendelea kujadiliwa katika mpango wa Bonde la Mto Mara uliosainiwa mwezi Septemba, 2016 chini ya Wizara ya Maji. Katika pango huo suala la athari za ujenzi mabwawa kwa maliasili zitakazoathirika kutokana miradi itakayofanyika nchini Kenya na Tanzania limejadiliwa na mapendekezo kutolewa kuhusu namna ya kukabiliana na matumizi yenye utata.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-

Hivi karibuni Mheshimiwa Rais alitoa agizo la kutatua migogoro ya vijiji na hifadhi mbalimbali na orodha ya vijiji vyenye migogoro toka Jimbo la Nkasi imefikishwa na kupokelewa na Wizara:-

Je, ni lini migogoro ya vijiji vya Kasapa, King’ombe, Mlambo, China, Nkomanchindo na vinginevyo vilivyoondoshwa vitapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Mbunge anavyofahamu, utatuzi wa migogoro iliyopo katika vijiji vyote nchini na hifadhi vikiwemo vijiji Kisapa, King’ombe, Mlambo, China na Nkomanchindo umetolewa maelekezo na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba mara utekelezaji wa maelekezo hayo utakapokamilika, ufumbuzi wa migogoro hiyo utakuwa umepatikana. Nitoe rai kwa wananchi kuacha kuvamia maeneo mapya ya hifadhi wakati huu, wakati migogoro huo unasubiri yanatafutiwa ufumbuzi.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-

Tabora Manispaa kuna Zoo ya Wanyamapori ambayo ilijengwa muda mrefu na mpaka sasa wanyama wanapungua na kuifanya kukosa maana:-

Je, Serikali iko tayari kupeleka wanyama hao katika zoo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bustani ya wanyamapori ya Tabora ina ukubwa wa ekari 35.67 ambapo ekari 28.15 ni eneo la wanyamapori na ekari 7.52 ni eneo la makazi. Bustani hii ilianzishwa na Idara ya Wanyamapori mwaka 1967 ikiwa na aina mbalimbali za wanyamapori wakiwemo chui, simba, duma, fisi, pundamilia nyumbu, swala na ngiri. Kwa sasa, bustani hiyo ina jumla ya wanyamapori 256 wa aina tofauti 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1972 bustani hii ilikabidhiwa kwa Mkoa wa Tabora ili kuisimamia kwa ukaribu. Mwaka 2001, Ofisi ya Mkoa wa Tabora ilikabidhi shughuli za usimamizi wa bustani hii kwa Manispaa ya Tabora. Manispaa ya Tabora iliisimamia hadi mwaka 2012 ilipoirejesha kwa Idara ya Wanyamapori kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji. Katika Idara ya Wanyamapori, bustani hii ilisimamiwa na Mfuko wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Protection Fund). Mwaka 2018 bustani hii ilihamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori-TAWA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza tija katika bustani ya wanyamapori, TAWA inaandaa mkakati wa kusimamia bustani ya wanyamapori zilizopo chini yake ikiwemo hii ya Tabora. Mkataba kati ya TAWA na mtaalam mwelekezi wa kuandaa mkakati huo umeshasainiwa ambapo mtaalamu huyo ataanza kazi hivi karibuni. Mkakati utakapokamilika utaainisha aina na idadi ya wanyama watakaowekwa katika bustani, aina ya huduma zitakazotolewa kwa wageni na kiwango cha tozo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha utalii wa picha badala ya utalii wa uwindaji kwenye Mapori yetu ya Akiba nchini: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na lango la utalii wa picha kwenye Pori la Akiba la Selous kwenye Ukanda wa Kusini kwenye Wilaya za Tunduru na Liwale?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohammed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Niabu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imendelea na jitihada za kupanua wigo wa mazao ya utalii kulingana na rasilimali zilizopo. Mazao hayo ni pamoja na utalii wa uwindaji, utalii wa picha, utalii wa utamaduni na utalii wa fukwe na namna ambayo itanufaisha Taifa na Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa azma hiyo, tarehe 26 Julai, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akiwa katika ziara yake ya kikazi kwenye uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Nyerere, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa sehemu ya Pori la Akiba Selous ipandishwe hadhi kwa kuanzisha Hifadhi Taifa Nyerere. Azimio la kuanzisha Hifadhi ya Taifa Nyerere lilipitishwa na Bunge lako Tukufu kwenye kikao cha tarehe 9 Septemba, 2019 na kuridhiwa na Mheshimiwa Rais kwa GN. No. 923 ya mwaka 2019. Kwa mujibu wa Sheria, shughuli za utalii zinazoruhusiwa kwenye hifadhi za Taifa ni zile za kuangalia na kupiga picha tu na uwindaji hauruhusiwi.

Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa, kufuatia kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa Nyerere, Wilaya za Tunduru na Liwale ni miongoni mwa wilaya zitakazonufaika na fursa za moja kwa moja za utalii wa picha katika maeneo hayo. Aidha, tathmini itafanyika ili kuona sehemu ya kuweka lango la kuingilia katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere itaweza kuwekwa kuendeleza utalii.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-

Nchi yetu imebarikiwa kuwa na Hifadhi nyingi zenye wanyama wengi wa kuvutia lakini mapato yatokanayo na utalii ni kidogo: Je, Serikali ina mikakati gani ya kuongeza mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MAIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Mathalan idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia watalii 1,505,702 mwaka 2018. Katika kipindi cha mwaka 2018 pekee Sekta hii imechangia katika uchumi wa nchi Dola za Marekani bilioni 2.4, sawa na takriban trilioni 5.4. Sekta hii imechangia kwa wastani wa asilimia 17 ya Pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, inatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja milioni 1.6. Hata hivyo, kiwango cha mchango wa sekta hii bado ni kidogo ukilinganisha na rasilimali tulizonazo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Wizara yangu imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini na mchango utokanao na sekta hii. Mikakati hiyo ni pamoja na kupanua wigo wa mazao ya utalii kijiografia kupitia Mradi wa REGROW ambapo Serikali inaendelea kufungua utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini kwa kuimarisha miundombinu ili kuboresha shughuli za utalii hususani katika hifadhi za Taifa za Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Nyerere. Aidha, Serikali imeanzisha Hifadhi mpya za Taifa sita ambazo ni pamoja na Burigi-Chato, Ibanda-Kyerwa, Rumanyika-Karagwe, Mto Ugalla, Nyerere na Kigosi. Lengo la Serikali ni kufungua na kutumia fursa za utalii nchini katika mikoa yote.

Mheshimiwa Spika, kadhalika Serikali imekusudia kuongeza mazao ya utalii. Hivi sasa, hapa nchini tumejikita zaidi katika kuziendeleza hifadhi za Taifa. Tunataka kuhakikisha kw amba mazao mengine ya utalii kama utalii wa kuvinjari kwa meli, utalii wa kupunga upepo fukwe na utalii wa mikutano ukiongezeka.

Mheshimiwa Spika, sanjari na juhudi hizo, Mwezi Septemba, 2019 Wizara yangu kwa kushirikiana na Nyanda za Juu Kusini iliandaa kwa kushirikiana na Sekta Binafsi maonesho makubwa ya utalii Jukwaa la Uwekezaji yajulikanayo kama Karibu Utalii Kusini ambapo zaidi ya washiriki mia tano kutoka ndani na nje ya nchi walishiriki. Vilevile, Mwezi Oktoba, 2019 Wizara iliandaa Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo lililohusisha wafanyabiashara wakubwa wa utalii takribani 400 na Mawakala wa Kimataifa 200 kutoka ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kigoma na Tabora imeanza maandalizi ya maonesho makubwa ya Kimataifa ya jukwaa la utalii na uwekezaji yanayojulikanayo kama Great Lakes International Tourism Expo ambayo yatafanyika Mwezi Juni, 2020. Imani yangu kuwa mikakati hii itasaidia kutangaza vivutio vya utalii, vya uwekezaji na kuongeza watalii nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hiyo, Wizara imeendelea kuimarisha shughuli za utangazaji wa vivutio vya utalii wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kufungua masoko mapya nchini China, India, Urusi na Israeli. Aidha, katika kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali, Wizara imekamilisha ujenzi wa mfumo funganishi wa kieletroniki kwa ajili ya kusajili na kutoa leseni, na kukusanya takwimu sahihi.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Awamu ya Tano, katika kuboresha miundombinu nchini ikiwemo viwanja vya ndege, ujenzi wa reli, upanuzi wa bandari, kuimarika kwa Shirika la Ndege ambalo limeanza kuhudumia watalii wa ndani na nje ya nchi. Juhudi hizi zitasaidia sana kukuza Sekta ya Utalii nchini. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-

Je, ni kwa namna gani Wakala wa Misitu (TFS) inashirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hususan Wilaya katika kusimamia misitu hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Tathmini ya Rasilimali za Misitu Tanzania (National Forest Resources Monitoring and Assessment - NAFORMA) ya mwaka 2015, Tanzania ina rasilimali za misitu zinazokadiriwa kufikia hekta milioni 48.1 ambapo asilimia 34 inasimamiwa na Serikali Kuu, asilimia 6.5 inasimamiwa na Halmashauri, asilimia 45.7 inasimamiwa na vijiji, asilimia 7.3 inasimamiwa na Sekta Binafsi na asilimia 6.0 ya misitu iko katika ardhi huria (general land). Kulingana na taratibu za Serikali, misitu ya Tanzania inasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hiyo, Mamlaka za Usimamizi wa Misitu Nchini zipo katika Wizara mbili, nayo ni Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo imekasimu mamlaka hayo kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo una jukumu la kusimamia misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu na misitu mingine yote ambayo haijahifadhiwa kisheria; na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inayosimamia misitu iliyopo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri na Vijiji).

Mheshimiwa Spika, kwa tafiti zilizopo, misitu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa mbili; kwanza, uharibifu mkubwa wa misitu ambao kwa sasa umefikia kiasi cha hekta 470,000 kwa mwaka; na pili, mahitaji ya mazao ya misitu yanayozidi uwezo wa misitu kwa zaidi ya meta za ujazo millioni 19.5. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeendelea kufanya jitihada za pamoja kati ya Wizara hizi mbili zinazosimamia rasilimali za misitu. Kupitia ushirikiano huo, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi yake ya TFS imekuwa ikishirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kutatua changamoto hizo.

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango huo wa pamoja, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ambayo ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa misitu na ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania. Ushirikiano huo unashirikisha ngazi ya wilaya ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Uvunaji wa Mazao ya Misitu katika Wilaya ni Mkuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, aidha, Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ni Mjumbe wa Vikao vya Uvunaji na ndiye anayetoa leseni za uvunaji wa mazao ya misitu katika Wilaya husika. Vilevile, ushirikiano mwingine upo katika kutoa elimu kwa Umma, kuhifadhi misitu kwa njia shirikishi, kuanzisha magulio ya mkaa na kusimamia doria za kudhibiti uvunaji na usafirishaji haramu wa mazao na bidhaa za misitu.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ushirikiano huo, tarehe 26 Mei, 2016 Wizara ya Maliasili na Utalii ilisaini Mkataba wa Makubaliano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ya kuimarisha zaidi ushirikiano katika usimamizi wa misitu nchini na utawala bora. Kufuatia makubaliano hayo, vikao vya pamoja katika ngazi ya wilaya vya kujadili utekelezaji vimekuwa vikifanyika kila mwaka ili kuchambua changamoto mbalimbali.

Mheshiwa Spika, kwa ujumla utunzaji na uendelezaji wa misitu nchini unakabiliwa na changamoto mbalimbali kulingana na mazingira ya mikoa na wilaya husika.

Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara hizi mbili itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ili kuwezesha rasilimali za misitu kuendelea kutumika kwa kufuata taratibu zilizopo ili rasilimali hizo zinufaishe vizazi vya sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE (K.n.y. MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) aliuliza:-

Utalii wa uwindaji, utalii wa picha na ufugaji wa mapori ya misitu na Hifadhi ya Ugunda, Isuvangala na Ipembampazi ni miongoni mwa fursa kuu za utalii kwenye Jimbo la Sikonge:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege uliokuwa umeanza kujengwa karibu na Mlima wa Ipole ambao ulijumuisha pia ujenzi wa nyumba za kufikia watalii (tourist rest houses) kwenye Kijiji cha Ugunda?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini ili yaweze kufikika kwa urahisi na muda wote wa mwaka. Lengo kuu ni kuwezesha watalii kuyafikia maeneo hayo na hivyo kuiongezea mapato Serikali. Aidha, katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori katika Pori la Akiba Ugalla, mwaka 2005, Wizara ilifanya maandalizi ya ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege (airstrip) karibu na Milima ya Ipole. Kazi ya awali iliyofanyika ikiwa ni maandalizi ya kutengeneza uwanja husika ilikuwa ni kuweka mipaka kwa kufyeka miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2006, Wizara ya Maliasili na Utalii iliomba Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ifanye tathmini ya eneo hilo ili kuona kama linakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilibaini kuwa eneo pendekezwa lipo katikati ya milima na hivyo kupelekea usalama kuwa mdogo kwa ndege kutua na kuruka. Kutokana na ushauri huo, Wizara ya Maliasili ilisitisha maandalizi ya ujenzi wa uwanja husika na kujikita zaidi kuimarisha viwanja vilivyopo ndani ya Pori la Akiba Ugalla.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-

Mikoa ya Kanda ya Ziwa imeathirika na mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu mkubwa wa mazingira:-

Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya uhifadhi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira na elimu ya utalii hasa baada ya kuanzishwa kwa hifadhi za Taifa Burigi- Chato, Kigosi, Ibanda – Rumanyika, Rubondo na Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina vyuo vinavyotoa mafunzo katika fani za uhifadhi wa wanyamapori, utalii na misitu ambapo uhifadhi wa mazingira ni sehemu ya mafunzo hayo. Mafunzo hutolewa katika ngazi za astashahada, stashahada, shahada na elimu nyingine za juu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Chuo cha Pasiansi kilichopo Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Mwanza kinatoa Astashahada ya awali ya uhifadhi wa wanyamapori na himasheria, na Stashahada ya uhifadhi wa wanyamapori na himasheria, Chuo cha Wanyamapori - MWEKA kilichopo Kilimanjaro, kinatoa Astashahada na Shahada ya uhifadhi wa wanyamapori na utalii. Chuo cha mafunzo ya Uhifadhi wa maliasili kwa jamii - Likuyu Sekamaganga kilichopo Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Namtumbo kinatoa mafunzo kuhusu mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa askari wanyamapori wa vijiji (VGS), viongozi na wajumbe wa Kamati za Maliasili za vijiji.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Chuo cha Misitu Olmotonyi kinatoa mafunzo yanayohusu misitu katika ngazi za astashahada na stashahada pamoja na mafunzo ya ufugaji nyuki katika chuo cha Ufugaji Nyuki – Tabora. Vilevile, Wizara kupitia Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi hutoa mafunzo ya teknolojia ya viwanda vya misitu katika ngazi ya astashahada ya awali, astashahada na stashahada.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii inatoa mafunzo ya utalii, ukarimu na uongozaji watalii katika ngazi za Astashahada na Stashahada.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha vyuo vilivyopo na haina mpango wa kujenga chuo kipya ili kukidhi mahitaji ya nchi nzima.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KITETO Z. KOSHUMA) aliuliza:-

Bodi ya Utalii pamoja na mambo mengine ina jukumu la kutunza utalii wa ndani ya nchi:-

Je, Serikali inasimamiaje Bodi hiyo ili kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unatangazwa kama Mji wa Kitalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimisha Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Mwanza vinatangazwa ipasavyo, Wizara inayo ofisi ya kanda ya Idara ya Utalii Jijini Mwanza na mwaka 2011 ilielekeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kufungua Ofisi ya Kanda jijini Mwanza. Aidha, Wizara imeelekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA kufungua Ofisi ya kanda ya kaskazini magharibi Mkoani Mwanza. Lengo likiwa si tu kusogeza karibu huduma kwa wadau wa sekta ya utalii lakini pia kuhakikisha vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii Mkoani Mwanza na maeneo yote ya kanda ya Ziwa zinatangazwa kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Wizara yangu kwa kushirikiana na Sekta binafsi imekuwa ikishiriki na kuratibu matukio na matamasha yanayolenga kutangaza vivutio vya Mkoani Mwanza ikiwemo; Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani, Tamasha la Bulabo na Afro Calabash, Tamasha la Urithi (Urithi Festival), Rocky City Marathon na Mashindano ya Urembo. Lengo ni kuvutia wageni na watalii wa ndani na nje kutembelea mikoa hiyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua kuwa Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa maeneo machache yenye rasilimali nyingi za utalii ikiwemo fukwe nzuri za Ziwa Viktoria, visiwa vinavyovutia, Hifadhi ya Taifa ya Saanane, wanyamapori, utamaduni, miamba ya mawe yenye kuvutia na mandhari nzuri ya jiji. Vivutio hivi kwa miaka ya karibuni vimekuwa vivutio wageni wengi kutembelea mkoa huo.

Mheshimiwa Spika, Kwa sasa Wizara inaendesha zoezi la kubainisha vivutio vya utalii kwa dhumuni la kuviendeleza na kuvitangaza. Katika mwaka wa Fedha 2019/2020 Wizara imelenga kutekeleza zoezi hilo katika Mikoa sita ikiwemo Mkoa wa Mwanza. Kazi hii inatekelezwa kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), uongozi wa mkoa, Wilaya, Vijiji na wadau wa sekta ya utalii.

Mheshimiwa Spika, aidha, tarehe 16 na 17 Machi, 2019 Wizara ilifanya kikao na wadau wa utalii kanda ya ziwa na magharibi ikiwa ni jitihada za kuimarisha utalii Mkoani Mwanza na Kanda ya ziwa kwa ujumla. Katika kikao hicho kilichofanyika Mkoani Mwanza kilihusisha viongozi kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Mara, Kagera, Shinyanga na Kigoma. Vilevile Wizara inaendelea na jitihada zingine za kuhamasisha uwekezaji kwenye shughuli za utalii na vijana kujifunza uongozaji watalii katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya utalii ni mtambuka, hivyo kazi ya utangazaji na uendelezaji sekta hii inahitaji juhudi za pamoja za wadau wa sekta ya umma na binafsi. Nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge na Uongozi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Wizara yangu katika jitihada za kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii vya Mkoa wa Mwanza.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-

Miundombinu mibovu ya barabara zinazoelekea Hifadhini husababisha Watalii kuwa wachache Mathalan; barabara inayotoka Iringa Mjini hadi Hifadhi ya Ruaha kilometa 104 ni ya vumbi na vilevile barabara ya kutoka Babati Mjini hadi Tarangire kilometa 20 ni ya vumbi:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara hizo kwa kiwango cha lami ili kuwavutia Watalii wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Hifadhi ya Taifa Ruaha ambayo inajulikana kama barabara ya Iringa – Msembe ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADs) Mkoa wa Iringa. Barabara hii ina urefu wa kilomita 104 kati ya hizo kilomita 18.4 ni za lami na kilomita 85.6 ni za changarawe. Barabara hii inapitia katika maeneo muhimu ya makumbusho ya Mtwa - Mkwawa (Kalenga), maeneo yenye kilimo cha Mpunga na Mahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, TANROADs imefanya Upembuzi yakinifu, Usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi hii imefanywa na Mhandisi Mshauri M/s ENV Consult (T) Ltd wa Dar es Salaam na tayari imekamilika. Ambapo jumla ya shilingi billioni 4.22 zimetengwa Katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Taasisi zake imekuwa ikishirikiana na Mamlaka zingine kuhakikisha kwamba barabara mbalimbali zinazoelekea maeneo ya Hifadhi zinapitika wakati wote kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara. Kwa mfano, Hifadhi ya Taifa Tarangire imeshirikiana na TARURA kurekebisha barabara ya kutoka Minjingu kwenda Tarangire yenye urefu wa kilometa 7 na barabara ya kutoka lango la Sangaiwe kwenda kijiji cha Usole – Mwada – Sangaiwe kwa kufanya matengenezo ya kuchonga na kuweka moram.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, usanifu wa barabara ya Minjingu – Tarangire kilometa saba kwa kiwango cha lami umekamilika na sasa inatafutwa fedha kwa ajili ya ujenzi. Barabara kutoka Babati Mjini hadi Hifadhi ya Taifa Tarangire kilomita 20 inafanyiwa ukarabati wa mara kwa mara kila mwaka kwa ushirikiano kati ya TARURA na Hifadhi ya Taifa Tarangire.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-

Utalii wa baharini (Diving unakua kwa kasi sana na hakuna chuo kinachotoa elimu hiyo hapa nchini:-

Je, Serikali haioni kuwa tunapoteza ajira nyingi kwa vijana wetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya Uzamiaji kwenye Maji kwa kutumia vifaa vya kupumulia ndani ya maji (Self Contained Underwater Breathing Apparatus – SCUBA Diving) yanatolewa nchini na Chuo cha Wakala wa Mafunzo ya Uvuvi Tanzania – FETA, Kampasi ya Mbegani, iliyopo Bagamoyo. Kwa sasa chuo kinakabiliwa na uchache wa watumishi wenye utaalam kwenye fani hiyo. Aidha, wakufunzi watatu (3) wapo nje ya nchi (Uingereza wawili na Uturuki mmoja) kwa ajili ya mafunzo katika fani hizo ambapo wanatarajiwa kurejea nchini mwaka 2020/21. Baada ya kurejea kwa wakufunzi hao, chuo kitaendelea kutoa mafunzo hayo mwakani. Aidha, vyuo vyote vina kozi ya lazima ya Swimming na Snorkelling ambayo inahusisha kipengele cha diving kwa wanafunzi wanaochukua masomo ya Sayansi ya Viumbe Maji (Aquatic Science).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia taasisi yake ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu inaendelea kuhamasisha Sekta Binafsi kuanzisha vituo vya uzamiaji (Diving Centres) ambapo sambamba na vituo hivyo kutoa elimu ya uzamiaji kwa wananchi katika maeneo ya fukwe za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Hatua hii itawezesha kuhudumia watalii wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi na pia kusaidia kuimarisha aina hiyo ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa vituo vya Sekta binafsi vinavyotoa huduma ya uzamiaji pamoja na elimu ya uzamiaji nchini vinapatikana katika maeneo ya Hifadhi ya Bahari ya Mafia, Mkoani Pwani (Big Blue, Shamba Kilole na Mafia Island Dive); Maeneo tengefu ya Mkoa wa Dar es Salaam (Yatch Club na White Sands); Hifadhi ya Bahari ya Silikanti Tanga (Kasa Dive na Fish Eagle Point) na Fukwe za Mkoa wa Mtwara (Mikindani Diving Centre).
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-

Wananchi wa Kijiji cha Kasapa walikuwa na ombi la kuongezewa maeneo ya kilimo kutoka kwenye eneo la Hifadhi ya Kalambo TFS:-

Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa ombi hilo la wananchi wa Kijiji cha Kasapa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Msitu wa Kalambo River ulihifadhiwa rasmi kwa kupitia tangazo la Serikali Na. 105 la mwaka 1957. Msitu huo upo katika Wilaya ya Kalambo na Nkasi Mkoani Rukwa na una jumla ya hekta 41,958.

Mheshimiwa Spika, hifadhi hii imekuwa na umuhimu wa kipekee kwa uhifadhi wa viumbe haia na vyenye umuhimu wa kipekee wakiwemo tembo. Aidha, hifadhi ina umuhimu mkubwa katika kutoa huduma za Kiikolojia kama maji. Maji haya ni muhimu kwa matumizi ya wananchi wa eneo hilo, pia kwa ajili ya maporomoko ya Kalambo ambayo ni pili kwa urefu mita 240 Barani Afrika baada ya yale ya Victoria yaliyoko Zimbabwe.

Mheshimiwa Spika, aidha, maporomiko ya Kalambo yana upekee kwa kuwa ni moja ya vivutio muhimu ambavyo vinaendelezwa kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia Sekta katika Mikoa ya Rukwa na Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 5 Julai, 2017 Waziri wa Maliasili na Utalii alitembelea Hifadhi ya Kalambo na baadaye Vijiji vya Kisapa ili kusikiliza maombi yao ya uhitaji wa ardhi. Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Waziri aliagiza TFS kushirikiana na Halmashauri kufanya upimaji na tathmini ya maeneo yanayolimwa na kutoa taarifa ya mapendekezo ya hatua stahiki zitakazochukuliwa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia maelekezo hayo, TFS kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ilifanya soroveya na kubaini kuwa maeneo mengi ya vijiji hivyo yamo ndani ya hifadhi ya misitu. Katika kushughulikia changamoto ya migogoro hiyo Mheshimiwa Rais aliunda Kamati ya Wizara nane kisekta kushughulikia migogoro baina ya wananchi na hifadhi. Mojawapo ya maeneo yanayofanyiwa kazi na Kamati hiyo ni pamoja na ombi la kuongezewa ardhi kwa wananchi wa Vijiji vya Kisapa na King’ombe. Taarifa ya Kamati imewasilishwa kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kupata maelekezo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati tunasubiri maelekezo ya Serikali.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Asilimia 70 au zaidi ya maeneo ya Kata za Isakamaliwa, Mbutu, Igunga, Nguvumoja, Lugubu na Itumba katika Jimbo la Igunga na Kata za Igoweko katika Jimbo la Manonga yapo ndani ya Mbuga ya Wembere ambayo kwa sasa imekosa sifa ya kuwa hifadhi ya wanyama na wananchi katika Kata hizo wameongezeka na kufanya kukosekana kwa maeneo ya makazi, kilimo na ufugaji na kwa kutokuwepo mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi kwa sababu ya hifadhi hiyo na kusababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji na kuleta mauaji:-


Je, ni lini Serikali italitenga na kulipima eneo la Hifadhi ya Wembere hususan katika maeneo ya Kata hizo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Pori Tengefu Wembere, Serikali inakusudia kulibadilisha hadhi pori hili kuwa Pori la Akiba. Katika zoezi hili alama za mipaka ya hifadhi na maeneo yanayopakana zitapitiwa na kuhakikiwa upya.

Mheshimiwa Spika, aidha, mipango ya matumizi bora ya ardhi hufanyika katika maeneo ya vijiji na husimamiwa na Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wizara yangu iko tayari kushirikiana na mamlaka hizi na wadau wengine pale itakapohitajika.

Mheshimiwa Spika, mbuga ya Wembere ina ukumbwa wa kilimeta za mraba 8,784 na ilitambuliwa kisheria kuwa Pori Tengefu kwa Tangazo la Serikali Na. 269 la mwaka 1974, pori linapatikana katika Mikoa ya Singida (Wilaya ya Manyoni) na Mkoa wa Tabora (Wilaya za Igunga, Sikonge na Uyui).

Mheshimiwa Spika, Pori Tengefu Wembere ni ardhi oevu (Chepechepe) ambayo ni muhimu Kitaifa na Kimataifa kwa kuwa ni chanzo cha maji dakio na chujuo la maji ya Ziwa Kitangiri na Eyasi. Pori hili ni mazalia na ushoroba wa wanyamapori ambao ni kiunganishi pekee cha mfumo wa ikolojia wa Hifadhi za Taifa ya Ruaha na Serengeti, mapori ya akiba ya Rungwe, Kizigo, Muhezi na Ugalla. Aidha, pori ni makazi na mazalia ya ndege wahamao ambapo mwaka 2001 utafiti wa Kimataifa ulibaini uwepo wa zaidi ya spishi 12 za ndege walio hatarini kutoweka.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, pori hili linatumika kwa uwindaji wa kitalii na utalii wa picha ambapo fedha inayopatikana hutumika kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za jamii kupitia Halmashauri za Wilaya husika.
MHE. ALEX R. GASHAZA (k.n.y. MHE. OSCAR R. MUKASA) aliuliza:-

Mwanzoni mwa mwaka 2016 wananchi wa Kijiji cha Kabukome Kata ya Nyarubungo Wilaya ya Biharamulo walivamiwa na tembo na kupoteza asilimia kubwa ya mazao yao:-

Je, ni lini wananchi hao watapata fidia ya mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuongezeka kwa juhudi za uhifadhi nchini na kupungua kwa ujangili, wanyamapori hususan tembo wamekuwa wakitoka ndani ya hifadhi na kupita maeneo ambayo ni shoroba au maeneo ya vijiji yanayopakana na maeneo ya hifadhi, ikiwemo baadhi ya vijiji vinavyopakana na yaliyokuwa mapori ya akiba ya Biharamulo na Burigi, kwa sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato katika Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo, Wilaya imekuwa ikichukua hatua kadhaa ili kunusuru maisha na mali za wananchi ambazo ni pamoja na kushughulikia matukio ya uvamizi wa wanyama kama tembo kwa haraka ikiwezekana pindi yanapojitokeza na kutoa elimu ya uhifadhi kuhusu namna ya kujilinda, lakini pia wananchi kuepuka kulima kwenye shoroba na mapito ya wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikitoa fedha kama pole kwa wananchi wanaoathirika na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja na kifuta jasho na kifuta machozi, siyo fidia kwa mujibu wa Kanuni ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi ya Mwaka 2011. Aidha, Kanuni husika zinafanyiwa marekebisho ambapo kwa sasa maoni ya wadau ndani na nje yamekusanywa, hatua inayofuata ni kuwasilisha kanuni hizo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na baada ya hapo zitasainiwa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2019, Wizara yangu haijapokea maombi yoyote kutoka Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubongo, Wilaya ya Biharamulo. Hivyo ninashauri Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri ya Wilaya kuwasilisha maombi husika ili yafanyiwe kazi kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za Mwaka 2011. Wananchi watakaokidhi vigezo watalipwa kifuta jasho mara baada ya taratibu kumalikika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Visiwa vya Ukerewe bado havitumiki ipasavyo kama eneo mahsusi kiutalii ingawa vimo vivutio vingi vya utalii ikiwemo jiwe linalocheza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na vikundi kama vile vya mila na desturi Ukerewe (KUMIDEU) katika kukitangaza Kisiwa cha Ukerewe kama eneo la utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua kuwa Ukerewe ni miongoni mwa Visiwa vichache nchini vyenye rasilimali mbalimbali ikiwemo fukwe nzuri, utalii wa utamaduni pamoja na jiwe linalocheza. Vivutio hivi kwa miaka ya hivi karibuni vimekuwa vikivutia wageni wengi kutembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara inaendelea na zoezi la kuainisha vivutio vya utalii kwa dhumuni la kuviendeleza pamoja na kuvitangaza. Katika mwaka wa Fedha wa 2019/2020 tunatarajia kutekeleza zoezi hilo hilo katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza. Kazi hiyo hutekelezwa kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa, Wilaya, Vijiji na wadau wa Sekta ya Utalii katika maeneo hayo, hivyo nimjulishe Mheshimiwa Mbunge, zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, Wataalam wangu watapita katika Kisiwa cha Ukerewe ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na kikundi cha Mila na Desturi cha Ukerewe cha (KUMIDEU)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hilo ni juhudi za makusudi za Wizara yangu za kupanua wigo wa mazao ya utalii kwa kubainisha vivutio vya utalii wa asili sehemu mbalimbali nchini. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kusimamia na kuendeleza Sekta ya Utalii Kanda ya Ziwa, Wizara ilifungua Ofisi ya Kanda iliyohusisha Idara ya Utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika Jiji la Mwanza. Lengo likiwa ni kusogeza kwa karibu huduma kwa wadau wa Sekta ya Utalii walio katika Kanda ya Ziwa na maeneo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha Sekta ya Utalii inazidi kuendelea na kukua hususani katika Kisiwa cha Ukerewe na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla. Ifahamike kwamba Sekta ya Utalii ni Mtambuka na hivyo kazi ya uendelezaji sekta hii inahitaji juhudi za pamoja za wadau wa Sekta hii, Umma na Binasfsi. Hivyo, Wizara yangu itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa Sekta ya Utalii kuendeleza utalii nchini ahsante.
MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI aliuliza:-

Katika kuboresha utalii katika Hifadhi ya Ruaha:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa kiwango cha lami barabara iendayo Hifadhi ya Ruaha pamoja na kuimarisha miundombinu ya ndani ya Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Nuhu Mwamwindi Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mipango ya kukamilisha ujenzi wa barabara iendayo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa kilomita 130 kwa kiwango cha lami. Hadi sasa, kipande cha barabara hiyo kutoka Iringa mjini hadi Kalenga chenye urefu wa kilometa 14 kimeshajengwa kwa kiwango cha lami. Sambamba na ujenzi wa barabara hiyo, pia miundombinu ya ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha inaimarishwa.

Mheshimiwa Spika, jukumu la ujenzi wa barabara zilizoko nje ya hifadhi ni la Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA na Wakala wa Ujenzi wa barabara TANROADS. Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu mamlaka zinazohusika ili kuzishawishi ziweke barabara hiyo katika Mpango Kazi wa uendelezaji wa barabra za Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa ina utaratibu wa kufanya ukarabati wa miundombinu ndani ya hifadhi za wanyamapori kila mwaka, pamoja na kuongeza miundombinu mipya pale inapohitajika. Hifadhi ya Taifa Ruaha, ina mtandao wa barabara za utalii zenye urefu wa takriban kilometa 1,590. Hifadhi ya Taifa Ruaha kupitia mpango wake kukuza na kuendeleza utalii Kanda ya Kusini REGROW imepanga kukarabati na kufungua barabara za utalii zenye urefu wa kilometa 1,055 katika kipindi cha miaka mitano ya mradi huo.
MHE. LEAH J. KOMANYA (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) aliuliza:-

Ongezeko la tembo na wanyama waharibifu imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wanaoishi maeneo ya kando kando ya hifadhi na ziwa.

Je, Seikali ina mkakati wa kudhibiti tatizo linalosabishwa na kadhia hiyo?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali Mheshmiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kanuni za wanyamapori wakali na waharibifu za mwaka 2011 zimeanisha aina wanyamapori ambao wanapaswa kushughulikiwa kama wanyamapori wakali na waharibifu. Kwa mujibu wa kanuni hizo, jedwali la tatu limeorodhesha wanayapori hao ambao ni tembo, kiboko, mamba, nyati, chui na simba.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati ifuatayo katika kunusuru maisha na mali za wananchi kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu:-

Mheshimiwa Spika, moja kufanya doria za udhibiti wa wanyamapori hatari na waharibifu, kupitia askari wa wanyamapori Tanzania, TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Halmashauri za Wilaya na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro na wadau wengine. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu linashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, mbili kutumia mbinu na teknojia mbalimbali mfano kupanda pilipili na kutundika mizinga ya nyuki pembezoni mwa mashamba, kufunga vitambaa vyenye vilainishi vya magari yaani oil kuzungushia mashambani na kutumia ndege zisizokuwa na rubani kwa ajili ya kudhibiti tembo.

Mheshimiwa Spika, tatu kuendelea kutoa elimu za uhifadhi kwa jamii ili wananchi waepuke kulima kwenye maeneo ya shoraba.

Mheshimiwa Spika, wapo wanyamapori waharibifu ambao wanaweza kushughulikiwa na mkulima mmoja mmoja pamoja na Wizara ya Kilimo. Wanyamapori hao ni pamoja na nyani, ngedere, tumbili, nguruwepori na ndege aina ya kwelea kwelea na wengine. Aidha, Wizara intoa rai kwa Maafisa Ugani wa kilimo kushirikikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na wanyamapori jamii.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-

Wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wako tayari kuanzisha misitu ya vijiji kwenye maeneo yenye ukame kama vile Kata za Bendera, Kihurio, Ndugu na Maore ili kuhifadhi mazingira.

Je, Serikali ipo tayari kuanzisha miradi ya utunzaji wa mazingira katika kata tajwa kwa kufundhisha wanavijiji uanzishwaji wa misitu ya vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Same kiikoloji na kijiografia imegawanyika katika Kanda kuu mbili, yaani ukanda wa mlimani ambapo hali yake ya hewa ni nzuri ukilinganisha na ukanda wa tambarare ambapo hali ya hewa ni ukame. Kwa maana hiyo, kata zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge zipo katika ukanda wa tambarare na kwa bahati nzuri zina uoto wa misitu.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeweka utaratibu wa kushirikiana na halmashari za wilaya na wananchi katika kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa maliasili. Mathalani, katika halmashauri ya Wilaya ya Same, utunzaji wa mazingira umehusisha utoaji wa elimu kwa wananchi na kuanzisha Kamati za Maliasili na Misitu, kuandaa mipango ya usimamizi na kutunga sheria ndogo za usimamizi wa maliasili. Vilevile, kupitia utaratibu huu wananchi wanashirikiana na Wizara na halmashauri kupanda miti kwenye maeneo ya wazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kuendelea kutekeleza azma ya kuwasaidia wananchi wa Kata za Bendera, Kihurio, Ndungu na Maore kuhusu shabaha yao ya kutunza misitu hiyo ya asili. Hii inatokana na ukweli kwamba pamoja na kuwa vijiji hivi viko nyanda za ukame bado vina uoto mzuri wa asili ambao ukitunzwa vizuri utasaidia kuboresha hali ya hewa, uhifadhi wa baionuai na huduma za kijamii kama maji.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-

Utalii wa Baharini kupitia “diving” unakua kwa kasi sana Duniani kote hali ambayo inaongeza soko la ajira katika sekta hiyo.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na changamoto za soko la ajira kwa vijana wa Kitanzania?

(b) Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha usalama wa watalii wanapokuwa chini ya maji hasa kutokana na uvuvi haramu wa kutumia mabomu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utalii wa kuzamia (diving) ni moja kati ya shughuli za kitalii ambazo zinafanyika hapa Nchini katika bahari ya Hindi kwenye meeneo ya hifadhi ya bahari ya maeneo tengefu. Idadi ya watalii wanaotembelea maeneo hayo imekuwa ikiongezeka ambapo hadi hivi sasa idadi imefikia watalii 46000. Aidha, kutokana na idadi hiyo ya watalii na uwekezaji unaofanyika katika maeneo hayo, ajira nyingi zinaendelea kuzalishwa na kipato kuongezeka kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla. Vilevile Serikali kupitia uongozi wa maeneo hayo imekuwa ukihamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya uzamiaji na kuongoza watalii ili waweze kunufaika na ajira katika sekta husika.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mafunzo ya utalii wa kuzamia yanatolewa katika vituo vya uzamiaji vya diving centres vinavyotambuliwa Kisheria katika maeneo ya hifadhi ya bahari ya maeneo tengefu ya Mafia vituo vinne, Dar es salaam vituo viwili na Tanga vituo viwili. Mafunzo hayo yanatolewa kwa vijana wanaoishi katika maeneo jirani na hifadhi ya bahari ya maeneo tengefu ili kuwajengea uwezo utakaowawezesha kupata ajira katika sekta husika.

Mheshimiwa Spika, utalii wa kuzamia ni taaluma ambayo hupatikana baada ya mtu kupata mfunzo ya kuzamia ambapo huambatana na mafunzo ya usalama na uokoaji. Aidha, kwa mujibu wa taratibu za Kimataifa, wazamiaji hupaswa kuwa na Bima ya Maisha ambayo husaidia kutoa fidia na matibabu endapo ataumia na kupata ajali wakati za uzamiaji.

Vilevile wazamiaji huhimizwa kutumia vifaa vyenye ubora ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa uzamiaji. Vifaa hivyo ni pamoja na Mitungi ya gesi, Boyance control device, Regulator, Mask, Fins, Wet or Dry suit, Dive computer na Snorkel na vifaa vingine muhimu.

Mheshimiwa Spika, maeneo yanayotumika kwa ajili ya shughuli za uzamiaji katika hifadhi yameainishwa na kuhakikishwa kuwa uvuvi haramu na vilipuzi havipo. Hata hivyo Serikali imeendelea na jitihada za kudhibiti uvuvi haramu ikiwemo matumizi ya vilipuzi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Hadi sasa uvuvi huo umedhibitiwa kwa kiwango kikubwa katika maeneo yote ya bahari ya Hindi na hivyo kufanya maeneo hayo kuwa salama kwa watalii wanaozamia.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kutekeleza mojawapo ya malengo katika Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 kwa Taifa 2016/2017, 2020/2021 katika kupanua wigo wa Utalii nchi (diversification)?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kupanua wigo wa mazao ya utalii, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa utalii inaendelea na jitihada za kuendeleza mazao mbalimbali ya utalii na kutangaza ikiwemo; kuanzisha mradi wa utalii wa utamaduni kwenye maeneo mbalimbali nchini; utalii wa fukwe kwa kuanzisha kurugenzi itakayosimamia uendelezaji wa utalii huo nchini; utalii wamali kale kwa kuimarisha vitu mbalimbali vya mali kale, pamoja na kuimarisha utalii wa mikutano na maonesho (Meetings Incentives Conference and Events-) kwa kuboresha muundo wa Bodi ya Utali(TTB) utakaowezesha kuwa na kitengo kinachosimamia utalii huo, pamoja na kufanya tathmini ya ujenzi wa kumbi za mikutano katika eneo la Pwani la Bagamoyo na Dar es Salaam, na utalii wa meli kubwa za kitalii (Cruiseship Tourism) ambapo tunashirikiana na Mamlaka ya Bandari kuboresha miundombinu ya bandari ili kukidhi mahitaji ya utalii huo nchini pamoja na kuendeleza utalii wa Jiolojia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Wizara imeanzisha shughuli mpya za utalii zikiwemo; safari za puto (Hot air balloon) katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha; utalii wa kutembea katika kamba(canopy walkway) katika Hifadhi ya Taifa Manyara; Utalii wa kuzoesha Sokwe (habituated chimpamzees) katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo pamoja na kuimarisha na kutangaza Hifadhi za Misitu ya Asili nchini ili kuvutia watalii kutembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kutekeleza Mradi wa Resilient Natural Resource Management for Tourism and Growth (REGROW) ambao kazi zake ni kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Sekta ya Utalii pamoja na kuboresha miundombinu inayozunguka katika vivutio vya utalii vilivyopo Nyanda za Juu Kusini ikiwemo barabara na viwanja vya ndege. Ni imani yangu kuwa, utekelezaji wa mradi huu utasaidia ukuaji wa Sekta ya Utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini sambamba na kupanua wigo wa mazao ya utalii katika utalii katika Ukanda wote wa Kusini kwa ujumla.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-

Wilaya ya Mbozi ina vivutio vingi sana vya utalii, baadhi yake ni Kimondo kilichopo Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, Majimoto na Mapango ya Popo katika Kata ya Nanyara, lakini baadhi ya vivutio hivyo hasa Majimoto na Mapango ya Popo havitambuliwi na havipo hata kwenye orodha ya kumbukumbu za Serikali:-

(a) Je, ni lini Serikali itavitambua rasmi vivutio hivyo?

(b) Je, kivutio cha Kimondo kimeingiza shilingi ngapi kwenye Halmashauri ya Mbozi na Serikali Kuu tangu kigunduliwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inavitambua vivutio vilivyopo Mkoani Songwe ikiwemo vinavyopatikana Wilaya ya Mbozi vya Majimoto na Mapango ya Popo na tayari vimeorodheshwa katika kumbukumbu za Serikali. Vivutio hivyo vilitambuliwa rasmi katika maadhimisho ya siku ya Kimondo Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Kimondo cha Mbozi kilichopo Kijiji cha Ndolezi, Kata ya Mlangali tarehe 28 - 30 Juni, 2018.

Mheshimiwa Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kufanya utafiti wa kina kwa lengo la kukusanya taarifa sahihi na vivutio vilivyopo Mkoani Songwe kwa lengo la kuvitangaza katika gazeti la Serikali. Vivutio vitakavyokidhi vigezo kuwa urithi wa utamaduni wa Taifa tutavitumia kiutalii.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mwaka wa Fedha 2013/ 2014 hadi 2017/2018 Serikali imekusanya kiasi cha shilingi milioni 14,378,000/= kutoka katika kituo cha Mbozi kutokana na watalii waliokwenda kuona Kimondo. Kwa kutambua umuhimu wa kituo hicho, Serikali inaendelea kukiboresha kwa kujenga Kituo cha Kumbukumbu na Taarifa na kuandaa maadhimisho ya Siku ya Kimondo Duniani. Aidha, jitihada za kukitangaza kituo hicho zitaongeza idadi ya watalii ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Ongezeko la gharama za nishati nchini hasa umeme na gesi vimesababisha kuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya kuni na mkaa.

Je, ni lini Serikali itarasimisha biashara ya mkaa ili kupunguza makali ya maisha hasa kwa Watanzania wenye kipato duni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, biashara ya kuni na mkaa inafanyika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Misitu pamoja na Tangazo la Serikali Na. 324 la tarehe 14 Agosti, 2016 na Mwongozo wa Uvunaji wa Mazao ya Misitu wa mwaka 2007 uliofanyiwa marekebisho mwaka 2015. Hivyo biashara hii ni rasmi na haina kizuizi chochote kwa mwananchi yeyote, kinachotakiwa ni kufuata sheria na taratibu za kufanya biashara ambazo zimefafanuliwa vyema katika mwongozo wa uvunaji ambao unamtaka kila mvunaji wa miti kwa ajili ya nishati ya kuni na mkaa kuzifuata, kitu ambacho baadhi ya wafanyabiashara na wachoma mkaa hawatimizi.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya taratibu hizi ni pamoja na:-

(i) Kutambua na kutenga maeneo ya misitu kwa ajili ya kutengeneza mkaa.

(ii) Kila anayehusika na shughuli za biashara ya mkaa anatakiwa kusajiliwa na Meneja wa Misitu wa Wilaya na anatakiwa kuwa na leseni.

(iii) Maombi ya usajili na leseni yanapaswa kupelekwa kwa Afisa Misitu wa Wilaya na kujadiliwa na Kamati ya Kusimamia Uvunaji wa Wilaya; na

(iv) Kila mfanyabiashara wa mkaa anapaswa kulipia mrahaba kama ilivyoainishwa katika Jedwali Na. 14 la Sheria ya Misitu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhaba mkubwa wa nishati ya miti, Serikali inawahamasisha Watanzania na wadau wote kuanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya matumizi ya nishati.

Hata hivyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge kuisaidia Sekta ya Misitu kwa kuhamasisha matumizi ya umeme, gesi, uzalishaji wa nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo inaongeza uharibifu wa misitu.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-

Je, ni watalii wangapi walitembelea Kisiwa cha Mafia kwa mwaka 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Mafia ni moja ya eneo la kimkakati katika uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini. Katika miaka ya karibuni kisiwa hicho kimekuwa kikitembelewa kwa wingi na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Wageni hao wamekuwa wakivutiwa na vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika kisiwa hicho ikiwemo papa potwe, magofu ya kale, utamaduni wa fukwe nzuri. Aidha, watalii wamekuwa wakivutiwa na michezo ya kwenye maji (scuba diving, sport fishing and snorkelling) na kuongelea na samaki aina ya papa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uzuri wa Kisiwa cha Mafia idadi ya watlii wanaotembelea kisiwa hicho imeendelea kuongezeka ambapo katika mwaka 2017/2018 jumla ya watalii 5,412 walitembelea Kisiwa cha Mafia hususani katika Hifadhi yetu ya Bahari ya Hindi katika eneo la Kisiwa cha Mafia (Marine Park and Reserve-Mafia). Kati ya watalii Watanzania walikuwa 252 na wageni walikuwa 5,160. Idadi hii ya watalii waliotembelea Mafia ni sawa na ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na watalii 4,817 waliotembelea kisiwa hicho katika msimu wa mwaka 2016/2017. Katika kuhakikisha kuwa Kisiwa cha Mafia kinafikika kwa urahisi, Serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya kisiwa hicho ikiwa ni pamoja na kujenga meli na kuboresha maegesho ya meli katika Bandari ya Nyamisati na Mafia.

Mheshimiwa Spika, namsihi Mheshimiwa Mbunge aunganishe nguvu kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya umma na binafsi wa Wilaya ili kuboresha miundombinu itakayosaidia kukuza sekta ya utalii katika Kisiwa cha Mafia kukitangaza zaidi ndani na nje ya nchi na kuhamasisha uwekezaji.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Itilima, Mkoani Simiyu huvamiwa na kuharibiwu mazao yao na wanyama aina ya tembo na Serikali hutoa fidia kidogo na wakati mwingine kutowafidia kabisa:-

Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wakulima juu ya fidia kwa waathirika wa uvamizi huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vinavyoathiriwa na uvamizi wa wanyamapori hasa tembo katika Wilaya ya Itilima ni vile vinavyopatikana na Pori la Akiba Maswa. Kutokana na changamoto hiyo, Wizara huchukua hatua kadhaa ili kunusuru maisha na mali za wananchi. Hatua hizo ni pamoja na kushughulikia matukio ya uvamizi wa tembo kwa haraka iwezekanavyo pindi yanapojitokeza. Aidha, Wizara imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi kuhusu namna ya kujilinda na kuepuka kulima kwenye shoroba na mapito ya wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikitoa kiasi fulani cha fedha kwa wananchi wanaoathirika na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni kifuta jasho na kifuta machozi na siyo fidia kwa mujibu wa Kanuni za mwaka 2011. Mfano, katika kipindi cha miaka miwili ya 2016/2017 na 2017/2018 jumla ya Sh.35,614,000 zimelipwa kwa wananchi 336 wa Wilaya ya Itilima.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa sasa Wizara imepokea maombi ya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi ya wananchi 238 kutoka katika vijiji 7 vya Nyantungutu, Ndingho, Ngwalali, Pijulu, Mbogo, Mwamtani B, Lungwa na Longalombogo. Wizara inaendelea kuhakiki maombi hayo na itawalipa wananchi baada ya kujiridhisha na hatua za uharibifu na kiwango cha kifuta machozi wanachostahili kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kiasi kinacholipwa ni kidogo na Serikali inatambua suala hili ambapo kwa sasa Wizara inafanya mapitio ya sheria na kanuni za uhifadhi wa wanyamapori, moja ya masuala yanayozingatiwa katika mapitio hayo ni suala la kifuta jasho na kifuta machozi.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-

Je, ni mafanikio gani yameweza kupatikana katika kushirikisha jamii katika jitihada za usimamizi wa maliasili nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya Ushirikishwaji wa Jamii katika Usimamizi wa Misitu nchini (Participatory Forest Management) inatekelezwa katika nyanja kuu mbili: Kuwashirikisha wananchi katika usimamizi wa misitu iliyopo kwenye ardhi ya vijiji (Community Based Forest Management) na kuwashirikisha wananchi katika kusimamia hifadhi ya misitu kwa ubia na Serikali (Joint Forest Management). Madhumuni ya dhana hii ni kuwapa fursa wananchi kushiriki katika usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu iliyopo katika maeneo yao hali wakiboresha maisha yao kupitia mapato mbalimbali yanayopatikana kutokana na misitu iliyopo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonyesha jumla ya hekari milioni 7.7 zimehifadhiwa kupitia dhana hii ya ushirikishwaji wa jamii. Aidha, dhana hii imesaidia sana katika kupunguza matukio ya uharibifu wa misitu kama ukataji wa misitu hovyo, uchomaji wa mkaa holela na matukio ya moto yaliyokuwa yakifanyika katika misitu husika katika misitu ya hifadhi ya mazingira asilia (nature reserves). Ushirikishwaji huu umekuwa ni nyenzo muhimu ya kufanikisha ustawi wa misitu ambayo mingi kati ya hiyo ni misitu ya lindimaji (catchment forest).

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo faida mbalimbali ambazo jamii husika imefaidika kupitia dhana hii ikiwepo kupata msamaha wa mirahaba ya Serikali juu ya mazao ya misitu, kubakiza asilimia 100 ya mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya misitu japokuwa kodi zingine kama kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani zimeendelea kulipwa, kubakiza tozo ya faini mbalimbali na utaifishaji wa mazao ya misitu na vifaa kutokana na uvunaji haramu katika misitu ya hifadhi ya kijiji. Aidha, sehemu ya fedha zinazopatikana zimetumika katika shughuli za maendeleo ya vijiji kama kujenga vyumba vya madarasa, zahanati, nyumba za watumishi, walimu na waganga, kutengeneza madawati na kuchimba visima. Vilevile sehemu nyingine ya fedha hiyo imeendelea kutumika katika shughuli za usimamizi wa misitu ikiwemo kununua vifaa vya walinzi wa misitu hiyo ikiwemo sare, buti, filimbi, baiskeli na kadhalika.