Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Constantine John Kanyasu (48 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa lakini niwashukuru sana wapiga kura wangu kwa kunipa ridhaa hii ya kuwawakilisha. Niseme kwamba nitajitahidi kutimiza wajibu wangu kadri Mungu atakavyoniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya nikasema kidogo kuhusu tukio lililotokea hapa kwamba limenisikitisha. Kwanza kwa namna ambavyo niliamini baada ya wewe kutoa amri kwamba sasa watu hawa washughulikiwe na baadaye nikaona watu hawashughulikiwi wanabembelezwa, haikunifurahisha sana. Mimi nilitarajia askari wakiwa nje wangepanga mkakati wao wa namna ya kuwashughulikia na wanapokuja ndani wanakuja straight wamekwishajua wanawashughulikia namna gani. Matokeo yake wameanza kutukanwa hapo, vyombo vya dola vinatukanwa na vyombo vya habari vinachukua. Nataka niseme, matukio haya hayawezi kukoma katika mfumo wa Jeshi legelege namna hii. Mwenyekiti anapotoa amri wanaoingia ndani kutimiza amri wanapaswa waache mjadala na wahalifu. Ipo siku watu watakuja hapa wamekamia kufanya maovu na watakuja kuchukua hatua tayari wamekwishaua mtu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati mchangiaji mmoja anachangia aliwashambulia sana Wakuu wa Wilaya akasema yeye angetamani kuona Wakuu wa Wilaya wanafutwa. Pengine inawezekana yeye katika Jimbo lake haoni umuhimu wao kwa sababu anatazama zaidi vyeo vyao vile vya kisiasa na namna wanavyoshughulikia wahalifu lakini wananchi wa kawaida nafasi ya Mkuu wa Wilaya ni ya muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya, kwa siku nilikuwa naweza kumaliza migogoro mingi ambayo ingeenda yote Mahakamani, Mahakama ile isingeweza kufanya kazi. Tuna migogoro mingi ya ardhi, kuna watu wanaonewa huko hawawezi hata kufika polisi wakajieleza, hawawezi kwenda mahakamani wakajieleza hata kama haki ni ya kwake akifika mahakamani hawezi kujieleza, kwa Mkuu wa Wilaya wanaongea kwa uhuru na matatizo yao yanasikilizwa.
Kwa hiyo, mimi nasema wananchi waache kupokea hizi propaganda ambazo zinaweza zikawafanya wakashawishika kufikiri kwamba Mkuu wa Wilaya siyo mtu muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumefika hapa watu wanaongea hovyo kwa sababu mwanzo watu wametumia sana vyombo vya habari kupata publicity. Mimi naunga mkono TBC isirushe live na sababu za msingi ziko kwamba watu wametumia vibaya sana nafasi hii na matokeo yake badala ya kuzungumzia vitu vyenye manufaa kwa wananchi, wamekuwa wakiitukana Serikali na wananchi. Kwa hiyo, naomba kusema kwamba msimamo huo ulikuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie sasa kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ana vision ya kuona Tanzania inaelekea kwenye viwanda, mimi pia naunga mkono na nafikiri vision yake iko sahihi. Hata hivyo, yapi ni mahitaji muhimu ya kuwa na viwanda na viwe wapi. Tunachokitazama sasa hivi, ikitokea bahati mbaya likatokea tatizo, karibu 75% ya nchi itakuwa giza kwa sababu source ya umeme iko sehemu moja. Katika nchi hizi ambazo tunafikiri tunataka kuanzisha viwanda, kama viwanda vyote vitawekwa sehemu moja basi siyo ajabu siku moja Tanzania tukajikuta zaidi ya 30% ya watu walioko kwenye viwanda wamekosa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanze kwanza kwa kutambua maeneo yapi tunataka kuweka viwanda. Ningetamani kuona tunaanzisha miji ya viwanda. Kwa mfano, kama tutasema tunafanya Singida kuwa mji wa viwanda na likatambuliwa eneo kubwa kuwa la viwanda, basi eneo hilo lipelekewe kila aina ya miundombinu ambayo itasababisha wawekezaji waweze kufika. Hatuwezi kuweka viwanda Singida tukategemea umeme unaotoka Dar es Salaam, ipo siku njia hii ya umeme wa kutoka Dar es Salaam itapata matatizo na viwanda vyote vitasimama. Lazima tuwe na alternative route ya umeme kutoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, pamoja na wingi wa gesi, tunavyo vyanzo vingine vya umeme. Pale Singida tuna upepo, hadithi hii imeongelewa kwa muda mrefu sana lakini kule Ngara tuna mto Ruvuvu, haukauki, una maji mengi sana. Tuna mradi wa umeme pale ambao Tanzania, Rwanda na Burundi wameamua kufanya kwa ubia, wamekadiria kutengeneza megawatts 70 peke yake lakini wataalamu walisema wangeweza kupata megawatts 300 kama wangewekeza vizuri. Mimi nafikiri ule mto kwa sababu ni source ya Mto Kagera na una maji mengi, badala ya Tanzania kulazimisha kutegemea mpaka kuingia ubia na nchi nyingine tungefikiria namna ya kupata umeme mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda inawezekana wawekezaji wakawa wanakuja lakini wanatukimbia kwa sababu hata waliopo wanalalamika uzalishaji gharama zake ni kubwa sana, tuna kodi nyingi na urasimu mwingi. Kama haya yote tutayarekebisha na tukapata maeneo ambayo ni industrial na yakawekewa kipaumbele cha kuwekewa kila aina ya miundombinu, vision ya Mheshimiwa Rais ya kuweka viwanda inaweza ikatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu ninalotoka tunachimba madini. Limekuwepo tatizo kubwa sana la wawekezaji wakubwa kuchukua maeneo yote mpaka ambayo walikuwa wanachimba wachimbaji wadogo wadogo. Ni kweli, tunaunga mkono wawekezaji wakubwa wapewe maeneo lakini kama Serikali itaendelea kupata pesa wananchi wanaendelea kuwa maskini tutaendelea kuona uchumi unakuwa kwenye Serikali lakini wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kuchimba. Kila wanapogundua madini anakuja mjanja anawahi Dar es Salaam analipia PL watu wanafukuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Geita Mjini, Mgodi wa Geita umepewa kilometa za mraba 192 lakini hata katika maeneo ambayo walikuwa wanachimba wananchi kabla hawajapewa walifukuzwa wakapewa wao. Matokeo yake mji ule umedumaa na hauwezi kukua tena kwa sababu kazi ya asili ya watu wa pale ni kuchimba dhahabu. Naomba Serikali, wakati tunafikiria namna ya kuyafanya madini haya yawe na maana zaidi katika uchumi wa kwetu lazima tufikirie namna ya kuwafanya Watanzania waweze kupata maeneo ya kuchimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la namna ambavyo Tanzania haifaidiki na mifugo na madini. Wakati miji hii ikiwa midogo wananchi wenye mifugo walikuwa wanaishi karibu na miji hii. Kadri miji inavyopanuka maeneo ya kuchungia mifugo yanazidi kupimwa na kujengwa nyumba, Serikali haijawahi kutenga eneo kwa ajili ya wafugaji ambao inawaondoa. Matokeo yake maeneo yote haya ambayo tunapima watu wanahamia ambayo zamani yalikuwa machungio ya mifugo sasa hivi kuna nyumba, sehemu zenye majosho kuna nyumba, hivi tunatarajia mifugo hii iende wapi? Hata kama tunasema mifugo hii ipunguzwe, huyo anayekuja kuweka kiwanda hapa Tanzania atapata wapi mifugo ya kulisha kiwanda chake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri Serikali haijatimiza wajibu wake hapa. Tunayo mapori mengi ambayo hayana faida kwa nchi hii. Tukimuomba hapa Waziri wa Maliasili atuletee taarifa ya Pori la Biharamulo limeingiza shilingi ngapi, inawezekana tukachukua wazo la Mheshimiwa Waziri wa Mifugo la wafugaji kulipia wakawa na faida kuliko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanza Cooperative Union wameshindwa kuendesha viwanda vya pamba kutokana na kuwa na madeni makubwa Benki. Pia kutokana na kupitwa na teknolojia ya viwanda walivyonavyo ambavyo sasa haviwezi kushindana katika soko kutokana na gharama za uzalishaji, kwa kuwa Serikali hivi sasa inataka kufufua viwanda vyote. Napenda kushauri Serikali kwanza kuwasaidia Nyanza kupata mbia ambaye atasaidia mitaji na teknolojia mpya katika ginneries.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunalima mananasi bora kabisa hapa Tanzania. Kwa muda mrefu zao la nanasi halijatumika kama kivutio cha uwekezaji na hivyo kupunguza uzalishaji kwa kuwa wakulima hawana soko la uhakika. Naiomba Serikali kupitia agenda ya Tanzania ya viwanda kutupatia mwekezajiwa Kiwanda cha Nanasi Geita na soko la nje la zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda, nashauri kila Mkoa upewe maelekezo ya kupima maeneo maalumu ya viwanda, yaani industrial area. Maeneo haya yatengenezewe hati na yamilikiwe na Halmashauri ili mwekezaji akifika usiwepo usumbufu wa kupata maeneo. Maeneo haya yapewe miundombinu ya umeme, barabara na maji ili kumfanya mwekezaji kuvutika na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa mitaji, naomba kushauri kwamba Serikali mara itakapokuwa imefanya utafiti katika eneo fulani na kuona panafaa kiwanda, lakini hakuna wawekezaji, utumike mtindo uliotumika Rwanda ambao ni kwamba watu wenye mitaji ya wastani wanaunganishwa kwa hisa na kupewa access ya kukopa kwa collateral kwenye Benki maalumu kama TIB na kuwafanya wazawa kadhaa kumiliki kwa pamoja kiwanda. Haya yamefanyika Rwanda na viwanda vingi vinafanya kazi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Waziri aangalie upya ongezeko la kodi eneo la mapato ya ndani. Kila mwaka tunapoongeza budget projection ya nchi matokeo yake kila biashara inaongezewa kodi. Kuongezeka kwa kodi katika biashara ileile, mtaji uleule na mauzo yaleyale au yaliyopungua kwa zaidi ya asilimia 50, kunasababisha wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa kodi, kufilisika na kufukuza wafanyakazi. Serikali iangalie vyanzo vipya kama kuanzisha malipo au tozo kwenye pikipiki zote kwa kuwa wanaoziendesha siyo wamiliki wake. Kuruhusu biashara hiyo kuwa bure maana yake wapo matajiri wengi hawalipi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iongeze uwekezaji katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula. Kwa kuwa kama wananchi watawezeshwa vizuri katika kilimo tatizo la fedha litapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke mpango mahsusi kuhusu maji. Mpango huo uhusishe ongezeko la Sh.50 kwenye lita ya mafuta ambayo yanaingia nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ulipaji wa Road Licence uwe tofauti na sasa na nashauri kodi hiyo iunganishwe kwenye bei ya mafuta ambapo kila lita moja iwekewe ushuru maalum wa mafuta kulipia kodi hii. Mfano gari moja linatumia lita 20 kila siku zidisha kwa mwaka mmoja (20x360=7,200 lita). Ukichukua lita 7,200x50% tu ambayo itaongezwa kwa gari ndogo (tax) italipa ushuru wa Sh.360,000. Ushauri wangu hapa ni kwamba Road Licence fixed ikiondolewa na kuwekwa kwenye mafuta Serikali itapata pesa nyingi zaidi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni desturi wawekezaji wa madini kupewa Mining License katika maeneo ya hifadhi ya misitu. Katika maeneo mengi wanayopewa hufyeka miti ovyo na kuchimba humo na kuharibu kabisa mazingira ya asili ya eneo hilo. Mfano katika Mkoa wa Geita maeneo ambayo yalikuwa na misitu mikubwa yote yamefyekwa na sasa ni jangwa. Aidha, sheria inawataka kufanya recovery (reforestation) baada ya kumaliza kazi (exit plan).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba katika kipindi ambacho mgodi unaendelea kuleta madhara ya uharibifu huwapata wenyeji. Hivyo, madhara hayo huwezi kuyafidia baada ya mika 20 kwa kupanda miti. Maoni yangu ni kuwa:-
(i) Serikali ianzishe Sheria mpya ambapo mmiliki wa mgodi awajibike kutunza Maliasili zote katika eneo lake la license tangu siku ya kwanza ya kutoka, kwani kwa utaratibu hivi sasa mwenye license huangalia madini pekee (ardhini) na kutowajibika na uharibifu unaofanywa na wananchi katika eneo lake, isipokuwa kama watagusa madini. Mfano mzuri Geita Mjini msitu wote katika eneo la GGM umekwisha.
(ii) Serikali ianzishe mfumo maalum (Nature Resources Extract Fund) kama ulivyo Norway, USA na nchi za Kiarabu, maalum kwa ajili ya kuja kushughulika na rehabilitation kwenye maeneo yote yanayoathirika na miradi ya wawekezaji ambayo huvuruga kabisa mfumo wa maisha ya watu na wanyama wa eneo husika. Hivyo mfuko huo utasaidia kutoa elimu, majanga ya asili na kurudisha maisha yanayohusika kama kawaida baada ya miradi kukoma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kutoa pole sana kwa familia zote ambazo zimeguswa na msiba ambao umetokea mjini Arusha kwa kipekee kabisa. Kwa kweli msiba ule ni pigo kubwa kwa nchi yetu, na tunafahamu kwamba kuna tukio linaendelea pale Arusha tunawatakia kila la heri na kwa kweli tunawapa pole nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yupo rafiki yangu mmoja yuko Marekani jana alinipigia simu akaniuliza na nikashindwa kutoa jibu na nilikuwa nataka watu wa Kiswahili watusaidie kutafuta, inawezekana likawa ni neno jipya ambalo linaitwa “Bashite” kutafuta maana ya Kiswahili ili liwekwe kwenye Kamusi. Kwa sababu kuna wakati walioko nje wanashindwa kupata connection ya mazungumzo hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwanza kwa kutoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwanza kwa kuonesha kwamba anajali michezo, lakini pili kwa upendeleo kabisa wa kuleta uwanja mkubwa wa michezo hapa Dodoma. Mikoa mingi sana haina viwanja vizuri vya michezo na ni nafasi pekee hii katika Mkoa wa Dodoma kupata uwanja ambao unaweza ukawa ni uwanja wa pili wa Kimataifa baada ya uwanja wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu katika suala hili, naiomba Wizara ihakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na vitu vingi vya lazima. Hapa tunapoongea Tanzania hata pamoja na mchango mkubwa wa wasanii wa muziki, wasanii wa ngumi na aina nyingine za michezo, tuna maeneo machache sana ya michezo ya aina hii ambayo yapo. Hatuna ukumbi wa kisasa wa muziki, hatuna ukumbi wa kisasa wa ngumi, tuna maeneo tu ambayo ni ma-hall ambayo ni ya kawaida hayawezi kuhamasisha michezo hii ya Kimataifa. Kwa hiyo kuja kwa uwanja huu niombe wale ambao wanasaidia kwenye mipango wahakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na complex ili uweze ku-accommodate michezo mingi na ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana wanamichezo wetu wengi, nianze na under 17 ambao kipekee sasa wanaelekea Gabon kwa ajili ya michezo hiyo ya Afrika; niwatakie sana mafanikio mema.

Vilevile niwapongeze sana wachezaji wetu wa Kimataifa walioko nje ambao wanacheza mpira wa kulipwa kama Samatta, Ulimwengu na wengine, niwapongeze sana Mwanariadha Simbu, Cecilia, Ginoka, Magdalena, Emmanuel, hawa wameendelea kuiuza Tanzania kwenye ramani ya Kimataifa. Wasiwasi wangu ni mmoja tu; ni mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mafanikio haya yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, ni bahati kubwa leo tunao akina Samatta, tunao hawa wanariadha wengine na kwa kweli kimsingi nchi hii kwa ukubwa wake na idadi yake ya watu, tungeterajia iwe na watu kama hawa zaidi ya 100.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa kinachoendelea ni kwamba anajitokeza mmoja na yeye anakuwa kama wa dawa. Hii maana yake ni kwamba maandalizi ya kuwapata ha watu huku chini yamekuwa ni madogo na matokeo yake kila anayechomoza anachomoka kwa bahati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye eneo hili, miaka ya nyuma tulipata wanamichezo wengi sana walitokea kwenye Majeshi hasa JKT, Polisi na JWTZ. Nadhani sasa Serikali inapoelekeza kwenye kuchagua vijana hawa kutoka kwenye maeneo mbalimbali kwenye Wilaya iweke kipaumbele sana katika suala la michezo ili kuwapata vijana hawa wanaopelekwa kwenye maeneo haya waweze kuandaliwa vizuri waweze kuiwakilisha nchi yetu. Ni kwa sababu tu kwamba zamani pia tulikuwa na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yanaweza kuwa na timu hizi za michezo. Baada ya mabadiliko ya sera, mashirika haya yakabadilisha mfumo matokeo yake ni kwamba hayana tena nafasi ya kuandaa wanamichezo wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani kwamba vyombo hivi vya dola ambayo kimsingi bado vina uwezo mkubwa wa kuwa na bajeti ya kutosha lakini na nafasi ya kuwaandaa vingeendelea.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kwa kweli niseme ni hotuba nzuri sana, nampongeza yeye pamoja na Naibu wake na Katibu wake Mkuu ambaye ni Mwalimu wangu, lakini napenda kusema upungufu kidogo ambao nimeuona hapa. Kwanza nilitarajia katika taarifa hii nione kwa kina inazungumzia uongozi mbovu na migogoro mingi iliyopo TFF. Kwa sababu ni kupitia mpira nchi yetu inaweza ikatengeneza wanamichezo wengine wapya kama Samatta.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa kabla timu ya Taifa ya Vijana haijaondoka, tulishuhudia vijana wale wanateremshwa kwenye basi kwa deni kubwa la kodi ambalo wanadaiwa TFF pamoja na TRA. Nikatarajia kuona ni namna gani sasa Wizara inaondoa aibu hii.

Mheshimiwa Spika, tuliona mwaka 2016 vyombo hivi vya mpira kama FIFA, CAF na TFF vilikuwa haviingiliwi na chombo chochote cha uchunguzi cha Serikali, lakini mwaka 2016 FIFA, FBI waliingia ndani, miaka kama kumi huko nyuma chombo cha Italia cha Usalama kiliingia ndani kuchunguza.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu sasa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wakati nachangia katika ripoti yangu mwaka 2016 na hasa nilipogusia suala la rushwa katika Chama cha Mpira cha Tanzania, nilimtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na awaeleze Watanzania ni chombo gani independent ambacho kilifanya uchunguzi kama ilivyo FIFA, kama ilivyokuwa Italia na kama ilivyokuwa kwenye CAF hapa juzi, Rais mpya wa CAF alipochunguzwa kwa tuhuma za rushwa ambacho kiliihakikishia TFF kwamba sasa ilikuwa na uhalali wa kufanya maamuzi ya kuzishusha timu tatu za Majeshi ya Polisi na JWTZ, lakini pia na timu moja ya Geita Gold Sport ambayo ilishushwa daraja na kupandishwa timu nyingine kutoka nafasi ya tano kwa sababu za kuhisia.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo tunazungumza na nimetazama sijawahi kupata hiyo taarifa, pamoja na uchunguzi huo mkubwa uliofanywa na PCCB.

Mheshimiwa Spika, niliahidiwa hapa na Mheshimiwa Waziri, kwamba baada ya uchunguzi huo wahusika watapelekwa mahakamani na hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo hapa kwa Serikali, mahakamani mara nyingi tunashindanisha maneno na inawezekana kabisa kwamba mwenye haki akakosa haki mahakamani kwa sababu ameshindwa kujenga kesi. Hii maana yake ni kwamba pamoja na uchunguzi mzuri wa PCCB na ushahidi wote waliopewa na wahusika kwamba palikuwa na harufu ya rushwa kubwa TFF, mpaka leo inavyoonekana wale watu ambao walituhumiwa na ushahidi wote wanaelekea kuokoka.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nipate ushauri wa Mheshimiwa Waziri, ni kwa namna gani, ameitaja TFF, amezungumzia namna ambavyo anafikiria itaweza kusimamia michezo, lakini hajasema ni kwa namna gani anafikiria kuimarisha utawala bora kwenye TFF? Tunafahamu kwamba kwa mujibu wa sera, hizi ni taasisi ambazo zinajiendesha zenyewe, lakini kimsingi kama kuna rushwa, kama maamuzi yanayofanyika pale siyo ya haki, inakatisha tamaa wadau wa michezo.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, leo ni mwaka mmoja na nusu tangu Geita Gold Sport walipoomba review ya kesi yao baada ya kukata rufaa, TFF hawajawahi kutoa maamuzi wala hawajawahi kusema rushwa alitoa nani? Alipewa nani? Shilingi ngapi? Wameishia kwenda kumfungia mchezaji miaka kumi, wamemfungia kocha miaka kumi ambaye haijulikani pesa alitoa wapi, kwa sababu viongozi wake wote wanaonekana hawana hatia.

Mheshimiwa Spika, nilitaka pia Mheshimiwa Waziri aje atuambie hapa, inapotokea suala kama hili, ni nini hasa nafasi ya Serikali? Kwa sababu tukiruhusu hali hii kuendelea tutafika mahali tutajikuta kwamba michezo ambayo inasemekana ni ajira haiwezi kuwa ajira tena. Wapo Watanzania wengi ambao sasa hivi wanafikiria wafike level ya Samatta, lakini kwa kukatishwa tamaa na matukio yanayoendelea katika TFF unaweza ukajikuta kwamba baadaye watu wote wanaona ni bora waachane na michezo wafanye kitu kingine.

Mheshimiwa Spika, nimelisema hili kwa muda mwingi kwa sababu ni suala ambalo linaigusa timu ya Geita Gold Sport ambayo ni timu inatoka Geita, ambapo wananchi wa Geita waliipandisha kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka kusema, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kuhusu kiwanja cha michezo, tumeona kwenye bajeti hii, lakini pia bajeti ya TAMISEMI, ni sehemu ndogo sana ya pesa ambayo inaelekezwa kwenye kuimarisha michezo. Kule kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba nitoe pongezi kwa hotuba nzuri na kwa kweli ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kushiriki katika tukio la uwashaji wa Mwenge pale Geita Mjini, nimpongeze sana kwa hotuba yake nzuri, lakini niwapongeze sana Wizara pamoja na watendaji wote ambao tulishirikiana nao kwa kiwango kikubwa na kwa kweli niwapongeze pia wananchi wa Jimbo la Geita Mjini ambao walijitokeza kwa wingi sana na kuvunja record katika siku ile ambapo Mwenge ulikuwa unawashwa na watu wa Geita hatuna cha kuwalipa tunawashukuru sana kwa sababu ni tukio la kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mliona tulipeleka sherehe zile za kuwasha Mwenge sehemu ambapo ni katikati kidogo ya msitu, lile ni eneo maalum la hekta 12 ambalo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo na wananchi wa Mkoa wa Geita kama wangepewa nafasi ya kusema neno moja kupitia mwakilishi wao, basi ombi lao kubwa lilikuwa ni msaada wa kupata namna ya kujenga uwanja wa michezo wa Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba sana hilo lisikike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niende kwenye suala la uvuvi, ninaunga mkono zoezi la kupiga vita uvuvi haramu na tangu nimeanza kuzungumza Bungeni hakuna sehemu niliwahi kukosoa au kuunga mkono uvuvi haramu. Tatizo langu kubwa limekuwa ni approach iliyotumika kupambana na operation yenyewe lakini pia na namna ambavyo huko chini linavyotekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unakumbuka katika matukio tulipokuwa hapa Bungeni niliomba mwongozo baada ya majibu ya Mheshimiwa Waziri alipokiri kwamba nyavu ya dagaa ya milimita nane inaweza ikakamata samaki aina ya Sangara ambao wako chini ya sentimita 55 na akakiri kwamba nyavu ya dagaa inaweza ikaja na samaki wadogo wadogo. Naibu Spika baada ya Naibu Waziri kukiri aliiagiza Serikali tangu siku hiyo iache kusumbua wananchi wanaokamatwa hovyo, wanaopigwa faini hovyo kwa sababu ya kukutwa na samaki wadogo wadogo, kumbe nyavu zina uwezo wa kukamata samaki wa aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maagizo hayo ya Bunge hili, wananchi waliendelea kukamatwa, wameendelea kutesema na hali ya maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa ni moja tu tumefikiria sana size ya samaki wa kuuza nje wanaoanzia sentimita 50 kwenda juu wa sangara tukaacha kufikiri kwamba samaki ni maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa. Samaki sangara ambae anauzwa nje anaanzia sentimeta 50 lakini sato ambae hauzwi nje anaanzia sentimeta 25; sasa samaki sangara ambae analiwa Tanzania lazima aanzie sentimeta 50 sawa na anayeuzwa nje kitu ambacho hakiwezekani kwa sababu nyavu zilizoruhusiwa na Serikali zinaweza kukamata samaki size ndogo kuliko ambao wameruhusiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mateso wanayoyapata wananchi ni makubwa sana hivi sasa tunavyozungumza Mtendaji wa Kijiji anakamata samaki, Mgambo anakamata samaki, Polisi anakamata samaki na matukio mabaya kabisa ambayo yanaendelea. Siku moja nilikuwa Geita mama mmoja anakwenda kumsalimia mwanae hospitali ana samaki wanne wamebanikwa amebeba kwenye box ndani ya hiace, ikakamatwa hiace, akakamatwa na mwenye samaki, kosa la mwenye hiace ni kwa nini amesafirisha samaki wanne kwenye box na kosa la mwenye samaki kwa nini amesafirisha samaki wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria haisemi hivyo, sheria inataja kama unataka kusafirisha samaki uwe na usafiri maalum wa samaki, lakini samaki wale ni wa biashara siyo samaki wa kula. Kuna matumizi mabaya sana ya sheria. Tulipotunga kanuni za uvuvi tuliweka Sheria ya Adhabu inasema kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 2,000,000, Waziri amekwenda amechukua Sheria za Mazingira akaziingiza kwenye Sheria za Uvuvi, akasahau mukhtadha wa uvuvi ni wa watu maskini anapiga faini kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 50,000,000, matokeo yake mtu mwenye mitumbwi miwili; mwenye mtaji wa milioni sita anaambiwa faini ya milioni tano, matokeo yake wavuvi wote wamefilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi tulikamata nyavu mpya tukazichoma moto. Katibu Mkuu wa Wizara wakati anachoma moto alikuwa anasikitika anasema ninachoma moto huku roho inaniuma nyavu za bilioni mbili. Mimi nikajiuliza, mimi nimesoma Mbegani Fisheries, kwa nini hakuchukua nyavu zile akapeleka chuoni wale wanafunzi wakajifunza kukata, kutengeneza single au akawapelekea Nyegezi Fisheries wakajifunza kutengeneza single ili wawape vijana wafanyakazi za uvuvi. Unachukuaje mtaji wa bilioni tatu unachoma moto nyavu mpya halafu unasikitika huku unafanya unachotekeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho angefanya angechukua zile nyavu akasema kumbe nyavu iliyoungwa mara tatu inaweza kukatwa ikapatikana single akawapelekea chuoni, akawaambia ninyi chuoni jifunzeni kushona, jifunzeni kukata, wapeni watu wanaohitaji mitaji ingewasaidia. Sasa mtu huyu aliyechomewa nyavu amekubali masharti, amepata hasara. Amendika kibali cha kuomba kuagiza nyavu nje mwezi wa kwanza, leo mwezi wa nne barua zake ninazo hapa hajaruhusiwa, kule wavuvi hawana nyavu, wamekaa, Serikali imekaa, wanaangaliwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kambi ilikuwa na wavuvi 50 hakuna mvuvi hata mmoja, viwanda vile vya samaki vya Mwanza vime-paralyze, wananchi wame- paralyze, Waziri hafanyi maamuzi nini tatizo hapa? Maagizo tukilalamika hayachukuliwi hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana inawezekana Waziri hafahamu yanayoendelea kule chini. Alichokisema Mheshimiwa Musukuma hebu tuunde tume tukasikilize watu. Kuna watu wamekufa kwa sababu ya kukimbia, wanawakimbia mgambo wanakufa kwenye maji na huu ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Kanda ya Ziwa maisha yetu ni uvuvi na ufugaji. Kwenye ufugaji kilichotokea mnajua, kwenye uvuvi kilichotokea mnafahamu, tunakwenda wapi sasa? Kwa sababu bahati mbaya sana Waziri wa Kilimo naomba nikuambie hata pamba tuliyokuwa tunaitegemea juzi imeanza kuliwa na wadudu na bahati mbaya sana matunda nayo yanaliwa na wadudu inawezekana isipatikane. Tunawasababishia umaskini Watazania.

Mheshimiwa iti, tunalolisema hili mimi ninazo karatasi hapa za watu walioomba vibali mwezi wa kwanza mpaka leo hakuna kinachoendelea. Inatuuma sana kwa sababu hatukuingia humu kwa bahati mbaya, tuliingia humu kuja kutetea wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala la Watendaji, nilifunga safari nikaenda kwa Katibu Mkuu wa Utumishi kwenda kumuuliza hivi ni kwa nini tangu mwaka 2004 mpaka leo 2018 walikuwa hawajachukua hatua akaniambia mwaka 2004 ilipotolewa maelekezo na Katibu Mkuu Utumishi tuliwapa miaka mitatu, ilipoisha tukawapa miaka mitatu, ilipoisha waliokuwepo wakakaa kimya. Busara ya kawaida ya waliokuwepo kukaa kimya waliona zoezi hili halitekelezeki, ndiyo maana walikaa kimya kwa sababu kama ingekuwa yule aliyekuwepo wakati ule anajua hili suala ni gumu, tangu mwaka 2010 angeagiza watu wafukuzwe kazi, sasa baada ya hapo watu walipata barua za ajira, watu wengine ni pensionable leo unawafukuza kazi unasema hawa wameiingizia Serikali hasara, hili siyo la kweli na halikubaliki na hatuwezi kulikubali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo naomba niliongee ni la wananchi wangu wa Geita. Geita tuna mgogoro na watu wa GGM. Tangu miaka mitatu, minne iliyopita Mawaziri walikuja karibu sita, nyumba za wananchi karibu 800 zimepasuka kwa sababu ya milipuko ya GGM, leo ni miaka mitatu Serikali ikitoa maagizo GGM hawatekelezi. Kuna wananchi pale wanakaa ndani ya vigingi vya GGM miaka 18 hawalipwi fidia, Serikali inatoa maagizo hayatekelezwi. Kuna wananchi Nyakabale, kuna wananchi Mgusu, kuna wananchi Manga wako ndani ya vigingi vya GGM hawaruhusiwi kufuga, hawaruhusiwi kulima, wanakamatwa na maliasili, wanakamatwa na mgodi lakini Serikali ilitoa maagizo mgodi hautekelezi. Nilitaka kufahamu ni nani…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Kwanza naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili naomba nimshukuru sana Mungu, kwa kunijaalia kufikia nafasi hii, na kwa kweli kwa kupata nafasi ya kushiriki katika Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kipekee kupata nafasi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika juhudi zake za kuwakomboa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa nafasi, na kufanya kazi hii, naamini sifa ya ziada kuliko watu wengine lakini ilimpendeza niweze kumtumikia katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ili kuyaweka vizuri maneno yangu, naomba wale ambao huwa wanasoma biblia watasoma katika zaburi ya 116 mstari wa 12 na inasema nimtumikie nini Bwana katika mambo yote aliyonijalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana viongozi wote, Makamu wa Rais, na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote ambao nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa. Kipekee naomba nitumie nafasi hii, kumshukuru sana Waziri wangu wa Maliasili na Utalii kwa namna ambavyo ananipa ushirikiano na kwa kweli kwa namna ambavyo ananipa miongozo mingi katika kufanikisha kazi yake. Ninaishukuru sana ofisi yako na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, nimepata ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati na naishukuru sana Kamati kwa namna ambavyo imekuwa ikitusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niwashukuru pia wapiga kura wangu. Tulizoea siku zote baada ya Bunge nilikuwepo muda wote jimboni lakini sasa hawanioni lakini wameendelea kuwa na imani na mimi. Ninaishukuru pia familia yangu, kwa uvumilivu wote ambao wameupata hasa katika muda huu ambapo muda mwingi sipati muda wa kufanya kazi na familia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani zote hizo, naomba sasa nitumie nafasi hii kujibu maeneo machache ambayo naweza kupata nafasi kwa dakika hizi kumi na tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, nianze labda na tatizo la udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu. Serikali imechukua hatua nyingi za kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo, mamba na viboko. Kimsingi pamoja na hatua zote ambazo tulikuwa tunachukua, tulikuwa na tatizo kubwa la kanuni; kwa hiyo tumeanza kuandaa kanuni za shoroba na maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori kwa lengo la kuhifadhi na kupunguza migongano baina ya wananchi na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuendesha doria za kawaida za pamoja ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya mbinu tofauti kama vile kuweka mizinga ya nyuki, kulima pilipili kwenye mipaka ya mashamba, kuweka oil chafu kwenye maeneo ya mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kushirikiana na halmashauri kuunda na kuwezesha vikundi vya kijamii vinavyodhibiti wanyama waharibifu, kufatilia mienendo ya wanyamapori hususan tembo; na hivi karibuni tulimshuhudia Mheshimiwa Waziri akiwavalisha mikanda ya kielektoniki
yaani (callars) kwa lengo la kubaini mienendo yao. Pia kuendelea na mipango mikakati ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba hivi karibu kumekuwepo sana na tatizo kubwa sana wanyamapori kuzagaa katika maeneo mengi, na hii inatokana kwa kweli na sasa wanyama wamekuwa huru. Mwanzo walikuwa wanawindwa hovyo na kwa sababu hiyo ulikuwa unaweza kufikiri kwamba sasa wanyama wamekwisha Tanzania, lakini baada ya udhibiti mkali, sasa wanyama imekuwa kila unapoamka asubuhi unasikia wanyama wako kila eneo wamezagaa. Kwa hiyo tumeendelea kuweka Mipango Mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo tunaamini kwamba baada ya mikakati hiyo Wizara yetu itafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kukabiliana na changamoto ya watu ya kuuwawa na Mamba. Wizara imefanya sensa nchi nzima ambapo mwezi Oktoba mwaka jana mpaka Novemba taarifa ya sensa imeonesha kwamba, mamba wameongezeka katika maeneo yaliyohifadhiwa na mamba wamepungua katika maeneo ambayo hayakuhifadhiwa. Wizara itafanya utaratibu wa kuwavuna hawa mamba na utaratibu huu tayari tunauandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya sensa ya Viboko katika maeneo ya Mafia na maeneo mengine. Takwimu zinaonesha kwamba katika Kisiwa cha Mafia viboko wako sasa kumi na sita na kuna mabwawa matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Changamoto ya wanyama hawa katika kisiwa hiki inaonekana kwamba inapanuka kwa sababu wanashambulia watu na kuvamia mashamba. Wizara itafanya juhudi za kutoa elimu kwa wananchi lakini pia tutawavuna viboko wakorofi ambao wamekuwa wakishambulia watu na mashamba ili kuwapunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inafahamu kwamba ziko changamoto za malipo yanayotokana na shambulio la wanyama waharibifu. Ni kweli kwamba kifuta jasho kimekuwa ni kidogo lakini na kifuta machozi. Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi na tayari wataalamu wa Wizara wameandaa andiko na mapendekezo hatua inayofuata ni kupeleka rasimu ya Kanuni ya hizo kwa wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya kanuni hizo yanakwenda sambasamba na mabadiliko ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009. Wizara pia inaendelea kulipa malipo ya kifuta jasho cha machozi kadiri madai yanavyowasilishwa, na kwa mwaka 2018/2019 jumla ya shilingi bilioni moja, milioni mia nne na ishirini sita, laki sita na thelathini na sita na mia tano zimelipwa kwa wananchi 7,320, hawa ni kutoka katika Wilaya 57. Kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni arobaini na mbili zimelipwa kwa wananchi 148 kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa. Malipo hayo yamefanyika tarehe 12 Februari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba madai yako mengi na yanashughulikiwa; na Mheshimiwa Catherine alitaka orodha ya watu waliolipwa Serengeti, namuomba Mheshimiwa Catherine kama hatajari baada ya kikao hiki, tunaweza tukawasiliana tukampatia hiyo orodha kwa sababu ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ya kifuta jasho au kifuta machozi yalikuwa yanachelewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuchelewa kwa kuwasilishwa kwa taarifa kutoka kwa waathirika kwa sababu zipo taratibu nyingi ambazo zinatakiwa kupitiwa kabla ya kufikia hatua ya kupata malipo. Wizara kwa kushirikiana na Giz, inaboresha mfumo wa kuwasilisha taarifa kwa kuanzisha kanda nne ambazo zitakuwa zinapokea na kufanya tathimini ya athari zinazotokana na shambulio hilo, ambazo tunazipokea Wizarani kwa njia ya elektoniki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kuwasilisha madai kwa mujibu wa sheria lakini pia ndani ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maeneo machache tu ya Waheshimiwa Wabunge ambayo walisema yalishatolewa maelekezo na Wizara yangu lakini hayajafanyika. Nikianza na Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, amezungumza kuhusu suala la watu wetu wa TANAPA kugonga mtu na baadaye hawakusimama na haijulikani malipo hayo. Suala hili ni la kisheria linashughulikiwa kisheria na ninaamini pale ambapo mfumo wa kisheria utakapokamilika haki za aliyegongwa zitapatikana kulingana na kheria kwa sababu gari zile ziko insured

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili amezungumzia kuhusu kisima; TANAPA tayari wameshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Kanda hiyo kukamilisha kisima hicho kama nilivyonitoa maelekezo wakati najibu swali. Kwa hiyo kisima hicho kitakamilika na wananchi watapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Malocha, alizungumzia usumbufu wanaoupata wananchi wa Ziwa Rukwa wanapokwenda kuvua, na akaeleza kwa masikitiko makubwa kwamba wananchi wamekuwa wakinyang’anywa mali zao na mitumbwi yao kubomolewa na afisa wetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara yangu ilishachukua hatua, Katibu Mkuu wa Wizara alituma ujumbe wa maafisa watatu kwenda kuchunguza malalamiko haya ya kinidhamu, ambayo Mheshimiwa Malocha aliyaleta ofisini, pamoja na Mbunge wa Viti maalum na tayari taratibu za kiofisi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Malocha, baada ya tu ya Bunge hili nilikuwa nimekuahidi kwamba tutakwenda katika eneo hilo kufanya mkutano na wavuvi na kuwasikiliza, na pale ambapo hatua italazimika kuchukua pale pale tutachukua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Getere, amekuwa akilalimikia kuhusu Kituo chake cha afya ambacho kimejengwa na taasisi yetu ya TANAPA, kimekamilika kwa miaka miwili iliyopita lakini hakifanyi kazi. Ni kwamba tayari uongozi wa TANAPA umeshamwelekeza Mkurugenzi wa Kanda hiyo ya Magharibi kukamilisha kituo hicho ili kiweze kufanya kazi haraka, na tayari pesa za Kituo hiki zimekwisha tengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo ahadi ya Mheshimiwa Waziri katika eneo la Kihibu, Waziri alifanya ziara na akaahidi milioni thelathini kwenye jimbo la Mheshimiwa Getere. Tayari aliwaelekeza TANAPA kuhakikisha kwamba pesa hizo zinatolewa na zinatolewa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, kwanza kwa pongezi zao ambazo wametupatia katika Wizara, lakini kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupa. Tuwahakikishie kwamba sisi ni watumishi wao; kwa hiyo pale ambapo wanadhani tunahitaji kutoa ushirikiano tuko tayari muda wote masaa yote kufanya kazi hiyo bila kubagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru sana, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara muhimu kabisa kwetu sisi tunaotoka kandokando ya ziwa, lakini pia maeneo ambayo kwa sasa kilio cha wananchi ni kwa kweli unyang’anyi mkubwa unaoendelea kufanywa na Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kusikitika kidogo, kuna bahati mbaya kwamba tunazungumza hapa kwa nguvu kubwa sana tukiwa tunazungumza maoni ambayo tunaamini waliotutuma ndiyo tunaleta, lakini majibu mepesi yanayokuja ni kwamba tumekamata Wabunge, tumekamata Madiwani ndiyo maana wanalalamika. Kama ziko kumbukumbu za Mbunge aliyewahi kukamatwa anavua samaki au na zana haramu, tungeomba sana leo wakati Waziri anahitimisha aseme ni Mbunge gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hili linatia woga watu kuchangia kwa kuogopa kutuhumiwa na wengine wanaamini kila anayesema anasema kwa sababu ana maslahi. Kauli hii ilienda mbali zaidi, Mheshimiwa Waziri alikuwa na kikao na viongozi 260 akiandaa Operesheni yake ya Sangara awamu ya tatu. Kauli walizozitoa viongozi aliokuwa nao ni kwamba wanasiasa wanapotosha zoezi hili kwa sababu wana maslahi binafsi na kwa maana nyepesi wanasiasa ni sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kuliweka vizuri hili, kwanza ni vizuri sana akaweka kumbukumbu hizi sawa; anawazungumzia wanasiasa wapi wanaopotosha? Kwa sababu tunayoyazungumza sisi tunayazungumza kwa sababu tunayafahamu. Hata hivyo, ni vizuri sana pia viongozi wenzetu huko waliko kwa kuwa tunazungumza kuwawakilisha wananchi, wakafahamu kwamba sisi tunapokuja hapa tunakuja tumetumwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kuchangia; kwanza nianze na suala la operesheni ambayo inaendelea hivi sasa. Tulizungumza hapa na tukaomba mwongozo na tatizo kubwa halikuwa kupinga operesheni ya wavuvi haramu. Naomba niweke kumbukumbu vizuri; naunga mkono operesheni ya kupambana na uvuvi haramu, naunga mkono operesheni ya kupambana na zana haramu, naunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza kipato kinachotokana na uvuvi na mifugo, yote ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, unapotaka kufanya operesheni lazima uiwekee mipaa, lakini pawe na ile sense of humanity, kwamba ninaokwenda ku-deal nao ni binadamu. Tunao wavuvi kule ziwani, niliuliza swali na halijawahi kujibiwa mpaka leo. Unapotumia nyavu ziwani ya inchi sita iliyoruhusiwa na Serikali ambayo siyo zana haramu, ukaenda nayo ziwani ikiwa single ina uwezo wa kukamata samaki wanaozidi sentimita 50 na wanaopungua sentimita 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na watu wake wote wanakiri kwamba nyavu hiyo kwa kawaida ratio inaweza ikawa mpaka ten percent ya nyavu ambazo ziko under size. Ni kwa nini operesheni ya Mheshimiwa Waziri inaendelea kukamata watu hata wenye samaki wawili? Kwa nini inaendelea kupiga watu faini ya mamilioni ya shilingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye sheria, sheria zote za mambo ya uvuvi ambazo zipo kwenye Sheria ya Mwaka 2003 na regulations zake, zinazungumzia faini na ziko very clear. Hata hivyo, kwa sababu operesheni ililenga kukusanya pesa, ililenga kwenda kuhakikisha kwamba watu wanatoka barabarani, mtu anapigwa faini mpaka ya milioni 50 kwa kosa la kukutwa na samaki 10, 15 kwenye mtumbwi, na operesheni hii inalenga wavuvi wakubwa peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza wanakwenda kwenye mwalo wanaangalia mvuvi mwenye mitumbwi zaidi ya 30, wakifika wanamkamata, wakimkamata wanam-detain kwenye gari tangu asubuhi mpaka jioni yuko chini ya ulinzi. Wanamwambia faini ni milioni 20 wanatembea naye, akikosa wanamweka ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye wanasema wewe bila kuleta milioni 20 tutakufungulia kesi ya uhujumu. Watu wanakwenda kuuza nyumba, wanakwenda kuuza ng’ombe. Kwa nini tunafanya hivi kama tuna nia njema na operesheni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliposema maneno haya, majibu yaliyotoka mepesi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri anasema ni kwamba nikiondoa hiyo exemption ya ten percent zoezi zima la operesheni halina maana. Maana yake ni nini kama wataalam wake wamekiri kuna kasoro na lazima iwepo, kwa nini anasema akiondoa haina maana; maana yake ni kwamba lengo la Mheshimiwa Waziri ni kufilisi watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua nyavu ya dagaa ukaenda nayo ziwani leo, ukizungusha ile nyavu ya dagaa utapata sangara, utapata furu na sangara utakaowapata ni wadogo wadogo na watakufa kabla hujawatoa ziwani. Nataka kujua Mheshimiwa Waziri, anawapeleka wapi hao samaki? Kwa sababu hao samaki atakapovua lazima waje na kokoro na dagaa, unawapeleka wapi? Wavuvi wote wa dagaa sasa hivi wanaogopa kuvua samaki, tulikuwa tunanunua kisado cha dagaa Sh.2,500, sasa kimepanda mpaka Sh.15,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niikumbushe Serikali, pamoja na lengo la kutafuta pesa kwenye samaki, samaki ni chakula kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa. Yaani kwa sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa, samaki ni chakula namba moja. Wewe unapofikiria mapato ya nje, fikiria kwanza watu ambao wanafaidika na samaki hao. Kinachoendelea katika zoezi hili ni uonezi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la nyavu; hivi tunavyozungumza, nyavu hakuna madukani. Nyavu za dagaa license amepewa mtu mmoja, yuko Arusha, alikuwa anatengeneza neti za mbu, anatengeneza nyavu za dagaa, matokeo yake nyavu ikiingia ziwani miezi miwili imepasuka. Wavuvi wameacha kununua nyavu za Tanzania wananunua nyavu za magendo kutoka Kenya na Uganda, Serikali inakula hasara. Waziri amezuia nyavu zisiingie Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyavu za sangara; nilizungumza hapa wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu, wafanyabiashara wamelipia nyavu tangu mwezi wa kwanza ziko bandarini, wanaomba kibali nyavu ziingie Tanzania. Wengine wamelipia na ushuru miezi miwili, Waziri hasemi kwa nini anazuia, hasemi ataruhusu lini, watu wanaenda kupigwa storage. Hebu tuwaambie Watanzania tunataka nini hapa kwenye nyavu, nyavu zile Mheshimiwa Waziri anazozitaka ziko bandarini hataki ziingie kwenye soko. Tunataka watu wavulie nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nafahamu na elimu yangu ndogo ya uchumi inaniambia ukitengeneza mazingira ya kupunguza supply kwenye soko ukasababisha demand ambayo haitarajiwi, bei ya nyavu itapanda na matokeo yake watu hawatanunua; ndiyo elimu yangu ya uchumi inavyoniambia. Sasa matokeo yake ni kwamba nyavu imepanda kutoka Sh.16,000 mpaka Sh.45,000 piece moja. Hiyo ambayo imepanda vifaa vyake vimepanda mara nne zaidi kwa sababu wanaoleta wote mali zao zimezuiliwa mpakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka Mheshimiwa Waziri aniambie, anazuia kwa maslahi ya nani? Sielewi. Kwa sababu kama anataka ku-control, apeleke mtu akakague kontena, kama anataka kuzuia atangazie watu wasilete nyavu. Watu wamelipa kodi wanamwomba kibali hataki, wanamwambia hiki, hataki, anataka nini, aseme. Kwa sababu ni rahisi sana kuwatangazia Watanzania wasiingize nyavu kutoka nje
tunategemea viwanda vya ndani, watu hawataleta. Sasa hasemi chochote, amekaa kimya, watu wanakula hasara, nyavu ziwani hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema hapa, nyavu sasa watu wanaanza kuendea nje ya nchi kwa sababu wanaona kuna urasimu; tunakula hasara. Kwa nini hili linatokea; tunamlinda nani? Kwa sababu lengo ni kulinda viwanda vya ndani, wakati huu viwanda vya ndani havina uwezo lazima uvuvi uendelee. Hiki ninachokizungumza ninavyo vielelezo; Mheshimiwa Waziri nimemwomba zaidi ya mara tatu hataki kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, tulifanya semina akasema amezuia mitungi ya gesi na yenyewe ni uvuvi haramu. Kwenye uvuvi wa bahari, tulipozuia trolling tuliruhusu wavuvi waende zaidi ya mita 50 deep, deep sea ya mita 50 kwa pumzi ya kawaida lazima utumie mitungi ya gesi. Hii inatusaidia sana kwa sababu uvuvi pekee siyo majongoo bahari. Kama lengo ni ku-control majongoo bahari, tungeweka mfumo wa kuweka season fishing kwenye maeneo unasema kuanzia sehemu hii mpaka sehemu hii tutavua kwa miezi mitatu, kuanzia hapa tutavua kwa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya burning totally wale wanaotumia mitungi hawaendi tu kwenye majongoo bahari, kuna uvuvi ambao ni selective ndani bahari. Hii mitungi watu wanaitumia kuzamia chini, maana yake ni nini sasa, tunajielekeza kwenye kufikiri kwa jambo moja tu kwamba wavuvi wote wa mitungi wanakwenda kwenye majongoo bahari. Pia kuzuia kabisa wala sio economically, sio kitu ambacho nafkiri ni sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siungi mkono hoja kabisa, lakini namtaka Mheshimiwa Waziri kwa nia njema kabisa atakapokuja hapa aturidhishe na mateso makubwa wanayopata wavuvi wa Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Madini. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Serikali yangu kwa sheria ambayo tuliitengeneza mwaka 2017 ambayo imeenda kuboresha kabisa shughuli za madini na mpaka sasa tayari waombaji zaidi ya 5,000 kwa taarifa ambazo tunazo, waliyokuwa wamekaa zaidi ya mwaka mmoja kusubiri license wameshapata, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kwenye suala la CSR, tulipitisha Sheria ya CSR hapa mwaka jana na tukaitengenezea utaratibu ambao utawahusisha Halmashauri ili ziweze kushiriki pamoja na migodi kwenye matumizi ya pesa hasa katika kuchambua miradi na kukubaliana na mgodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, nadhani kuna maeneo ambayo hatukuyaona vizuri, sisi katika maeneo ya migodi tulikuwa na tatizo la migodi hii kuja na mahesabu makubwa sana yanayoonesha wametumia kwenye miradi, wakati miradi iliyofanyika ni midogo na tatizo hili linaonekana bado linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Geita akaomba watu wa Mgodi wampe orodha ya pesa ambazo zimetumika na miradi, hawakumwambia mradi huu wametumia shilingi ngapi. Nadhani angeona suala hilo angeshangaa sana. Mwaka huu baada ya vikao na Halmashauri tumeona tatizo hili litakuja kuwa kubwa zaidi. Kwa mfano, katika hesabu ambayo Halmashauri ya Mji wa Geita wametuletea kwenye miradi ambayo tumependekeza, cement wao wanasema ni Sh.48,000/= mfuko, wakati pale mjini mfuko ni Sh.18,000/=. Bati la gauge 28 wanasema ni Sh.78,000/=, wakati bati pale mjini ni Sh.22,000/= bati moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nondo ya milimita 16 wamewekwa Sh.52,000/= na kokoto trip moja wameweka Sh.80,000/=. Sasa unaona sheria hii imewapa loophole ya kuendelea kudanganya kama ilivyo kwenye transfer pricing, matokeo yake itakuwa ni Kampuni zao zile zile ambazo wanaziteua, zinawauzia material kwa bei kubwa mara nne zaidi. Mradi wa shilingi milioni 10 watajenga kwa shilingi milioni 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Sheria tutazame upya sheria hii ili ikiwezekana Halmashauri Kitengo chake cha Manunuzi kishiriki kwenye Procurement System nzima kwa bei ambazo ni shindani kwenye maeneo husika na kwa kutumia wazabuni na local contents. Bila kufanya hivyo tutarudi kule kule tulikotoka, takwimu zitaonesha mabilioni ya shilingi lakini miradi iliyofanyika ni midogo na pesa zote zinarudi kule zinakotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, ni suala ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri pia alikuja Geita kulishughulikia. Pale Geita tunao mgogoro mkubwa wa Mgodi wa GGM pamoja na wananchi wa Geita pale, nyumba zaidi 800 zimepasuka kutokana na milipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi wengi ambao wanaishi kwenye vigingi vya migodi kwa zaidi ya miaka 18. Mheshimiwa Waziri alikuja akatoa maelekezo mazuri na kabla ya maelekezo yake Mgodi wenyewe ulifanya study kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Waziri aliyekuwepo, Waziri Kalemani alitoa maelekezo watu wa GST wakafanya study kuonyesha sababu za mipasuko kupitia GST, taarifa zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Ametoa maelekezo lishughulikiwe tangu mwezi wa pili, mpaka leo ninavyozungumza, wananchi wa Geita hawajui hatma ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu hawaoni kinachoendelea. Wenye nyumba zile, wengine wanakufa, nyumba zile zilizopasuka zinaanguka, ripoti zote mbili za Serikali zipo mezani, lakini mambo hayashughulikiwi na hayaendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri sehemu ambazo tuna migogoro ya muda mrefu kama Geita, kabla Mheshimiwa Waziri hajaja kwenye ziara ya Jimbo langu iwe ni vyema kupitia zile documents zilizopo mezani kwake na kujua wenzake walitoa maagizo gani; kuliko kuja kutoa maagizo yale yale yaliyotolewa na Waziri mwingine na yasitekelezwe, wananchi wanaona kama vile Mgodi huu unaidharau Serikali. Tunao wananchi katika maeneo ya Magema, tunao wananchi ambao wameteseka kwa muda mrefu sana na hawajapata haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la tatu. Katika eneo la Mgusu tunao wananchi watatu ambao wamekuwa na kesi na Mgodi tangu mwaka 1995. Majaji sita ambao wameshiriki kwenye kesi ambalo lilikuwa ni kosa la Serikali, Serikali ilikuwa imewapa license wananchi watatu; Felix Isidory Ngowi, Ezekiel Magese na Philipo Paskali na walikuwa wanaendesha leseni zao za utafiti na uchimbaji mdogo mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya, siyo kwa makusudi Kamishna akatoa leseni nyingine juu ya leseni zile zikiwa bado ziko hai, wananchi hawa wakakamatwa, wakapigwa, wakafungwa lakini wakaenda Mahakamani. Majaji sita wote wametoa hukumu iliyowapa haki wananchi kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2005.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Mgodi unaendelea kuonesha unakata rufaa. Jaji Matupa, Jaji Bukuku, Jaji Mero, Jaji Nyangarika, wote hawa wamewapa haki wale wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha sana ni kwamba hukumu nyingine ya mwisho ilitolewa mwaka 2016 na ikatoa permanent injunction ya kuzuia mgodi kuwaondoa wananchi hao kwenye eneo hilo. Kwa namna yoyote wanapokuwa wanaendelea na kesi nyingine, bado Mkurugenzi wa Mgodi na Polisi na wengine walioko pale wameendelea kuwakamata na kuwafukuza na eneo lile lina wachimbaji wadogo zaidi ya 5,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwanza ni aibu kwa Serikali. Majaji hawa wote wameonesha kwamba wachimbaji hawa wadogo wana haki na kosa ni la Kamishna, lakini bado wanaendelea kuonesha kwamba huyu mwenye Mgodi mtu mmoja ana haki ya kuwafukuza watu na kuwanyanyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wapewe haki yao, wamekamatwa zaidi ya mara 20, wanawekwa ndani miezi sita, Mgodi hauji kuendelea na kesi, wanatoka, wanapigwa, mali zao zinachukuliwa, wanafukiwa mashimo bila sababu yoyote ile ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa kwa kweli hawana sababu yoyote ile ya kuendelea kuteseka, kwa sababu vyombo vya Sheria; tuna mazoea wananchi wakifukuzwa huwa wanasalimu amri, wanaondoka. Hawa walikwenda Mahakamani wakafuata utaratibu kwa miaka 20 wameipigania haki yao na wameshinda na hukumu wanayo, lakini Mgodi unaendelea kuwafukuza. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala hili lishughulikiwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la nne, naomba kuishauri Serikali, tunao Mgodi wetu wa GGM pale awali ulikadiriwa kuchukua miaka 30 au 25, lakini baada ya sheria hizi mpya tulizozitengeneza, ule Mgodi unaanzisha pits nyingi na wanafanya kama lashing, matokeo yake ninayoyaona, baada ya miaka mitano watafunga Mgodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoendelea sasa, wakiona tu gharama za kupata madini zimeongezeka, wanahama wanaanzisha pit mpya. Matokeo yake wanakwenda wana-lash badala ya kuchukua miaka 30, tutaachiwa mashimo na mashimo yale ni makubwa, wataondoka kabla sisi wenyewe tuliotarajia kwamba tutachimba madini haya kwa miaka 30 hatujafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna ya ku-control. Kuna maeneo migodi inachukua zaidi ya miaka 50 kwa sababu wanalazimishwa kufanya utafiti na kumaliza madini yaliyoko chini. Shimo lililokwenda milimita 200 ukiondoka leo anayekuja hawezi kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la GST. GST nawapongeza kwa kazi wanazozifanya, lakini nina tatizo moja na GST. Mwaka 2016 walikuwa kule Bukombe, nami nikaomba leseni kupitia wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo langu kama tulivyoshauriwa na Mheshimiwa Waziri, wakapewa leseni. Utafiti wa GST unaonyesha kuna dhahabu. Wamechimba wamekwenda mpaka mita 100 watu hawapati dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana GST, kabla ya kuishauri Serikali iwape wananchi maeneo haya yenye dhahabu, kwa sababu wananchi wanakopa, wanajichanga na pesa zao ndogo, nawaomba GST wahakikishe wanatoa elimu ya kutosha kwamba dhahabu hii ipo umbali gani kwa miamba iliyolala vipi? Tunafika mahali sasa tunaacha kuwaamini, ni bora ukatafute private watu wengine huko waje wakufanyie utafiti kuliko GST kwa sababu wanafanya utafiti wa kijanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Waziri naomba sana wananchi wangu wa Geita Mjini na wananchi wa Mgusu waweze kupatiwa haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuja kusimama tena kwenye Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naunga mkono pia miradi yote ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wameileta. Naomba nitumie nafasi hii kuipongeza pia Serikali yangu kwa miradi yote ambayo imekuwa ikiendelea nchi nzima. Tumekuwa tukiona mambo mazuri yanaendelea kufanyika katika nchi nzima. Naamini kwamba haya yanayoendelea yanatokana na kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali nzima pamoja na Wizara yenyewe ambayo anaisimamia Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na tatizo dogo ambalo lipo sasa hivi. Wakati tunahamasisha ununuzi wa EFD tulikuwa na makampuni mengi ambayo tumeyapa license ya kufanya kazi hiyo. Ipo kampuni ilikuwa inauza mashine za Prima, hawa walikuwa wanaitwa Boston Solution Ltd, mashine zao zinalalamikiwa kwamba hazifanyi kazi na inasemekana wamevunja mkataba na TRA na sasa wale walio na mashine hizo wanaambiwa wanunue mashine nyingine. Kwa hiyo, nataka kupata ufafanuzi kutoka Mheshimiwa Waziri na pia kuomba suala hili liangaliwe vizuri kwa sababu kama mzabuni amemaliza mkataba halafu mashine zile zinakosa kazi tutakuwa tunawarudisha nyuma wananchi wetu ambao wananunua mashine hizi bei ghali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze TRA kwa makusanyo mazuri ya kodi. Wameendelea kufanya vizuri na kuwa na lugha nzuri kwa wananchi katika maeneo yetu tunayofanya kazi. Nadhani speed ya ku-recruit new tax payers ku-enlarge tax base imekuwa ndogo kwa sababu tunaweza tukaendelea kukusanya hela nyingi kwa walipa kodi walewale na kama tax base haiongezeki basi tatizo letu la kuwa na bajeti finyu litaendelea kuwepo, nadhani hata mwaka jana nilijaribu kusema haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mpango kwenye Wizara ya Kilimo. Tunajenga viwanda na nilisema mwaka jana, lakini watumiaji wa bidhaa za viwanda zaidi watakuwa ni Watanzania ambao zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Tuna bahati mbaya sana kwamba katika nchi yetu jua likiwaka hasara ni ya mkulima, mvua zikizidi hasara ni ya mkulima, mazao yakipungua na yakizidi pia hasara ni ya mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema kuhusu Price Stabilization Fund, bado sioni kama ni solution namba moja hiyo peke yake. Nafikiri Wizara na wahusika wajaribu kufanya market intelligence kwani yapo maeneo ambayo wakati wakulima wanaingia kwenye kilimo unaweza uka-forecast ukaona mwaka huu tutakuwa na mahindi mengi, dengu nyingi na vitu vingi, unajaribu kuwatengenezea wakulima soko mapema kabla ya kwenda kwenye mgogoro huu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye vipaumbele vya kilimo pale, suala la kutafuta masoko kwa maana ya sehemu ya kuuzia mazao haya halimo, lipo suala la kujenga maghala na masoko ya mazao kwenye maeneo ya wakulima. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ikipatikana surplus, Serikali kwa sababu inaweka restrictions za kuuza mazao haya nje, tuwe na uwezekano wa kuchukua ile surplus ili isionekane ni laana tena mkulima anapovuna mazao yake. Inapoonekana kwamba sasa Serikali imetosha kununua yale mazao basi tuwe tayari na information kwamba wanaweza kupeleka wapi hawa wakulima mazao yao. Hivi tunavyozungumza watu wengi wanakimbia kilimo kwa sababu wanaona sehemu zote zina hasara, jua likiwaka na mvua zikinyesha kuna hasara na suala hili lina hatari sana siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye suala la bidhaa za viwanda. Sasa hivi tunapozungumza hasa sisi tunaotoka pembezoni mwa nchi kama Geita bidhaa zote hata zinazozalishwa Tanzania ni bei kubwa sana. Amesema hapa mchangiaji mmoja mimi nikawa nakumbuka bei ya nondo ya milimita 16 imetoka Sh.15,000 kwenda zaidi ya Sh.28,000 mpaka Sh.30,000. Sasa tunajiuliza hizi bidhaa zote zinazalishwa Tanzania, tatizo liko wapi? Ukiangalia bei ya bati imetoka Sh.160,000 mpaka Sh.450,000, tatizo lipo wapi na ni ndani ya miaka mitatu. Watumiaji wakubwa wa bidhaa hizi ni wakulima, kama wataendelea kuona bidhaa hizi zinapanda maana yake ni kwamba wataacha kulima na watahamia mjini. Kwa hiyo, tutaanza kutengeneza mgogoro wa watu kutoa vijijini kwenda mjini kwa sababu kile anachokifanya kijijini hakimlipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wenzangu wamesema inawezekana ni utitiri wa kodi, lakini inawezekana tunahamasisha wawekezaji waje na wakati huo huo hatujaangalia ni kwa namna gani huyu mtumiaji wa mwisho hii product inamfikia. Sasa hivi maeneo yetu yale ni rahisi kuagiza bati za kutoka Uganda na Kenya ukazinunua kwa bei rahisi kuliko kununua bati za Tanzania, sielewi tatizo lipo wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Naipongeza sana Serikali mwaka jana ilitenga pesa kwa ajili ya kukarabati shule kongwe, naipongeza sana. Lipo tatizo naliona kuhusu shule za msingi. Nilikusikia juzi unasema hapa ipo shule ina watoto zaidi ya 5,000, mimi kwangu Geita Mjini nina shule tatu ambazo zina watoto zaidi ya 4,500 kwa shule moja na madarasa yapo 16 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, kama inawezekana tuje na mpango kabambe kwenye mpango huu wa kuboresha miundombinu ya shule za msingi, halmashauri zetu haziwezi. Shule yenye watoto 5,000 maana yake ndani ya 5,000 kuna shule 7, lakini miundombinu iliyopo ni ya shule moja. Watoto wanaingia asubuhi wanatoka saa sita, wengine wanaingia saa sita wanatoka saa nane, mwalimu mmoja anafundisha watoto 400, hakuna uniformity. Huyu mwalimu hata angekuwa genius namna gani watoto hawawezi kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama tulivyofanya kwenye vituo vya afya na zile shule maalum, tuje na progamu maalum ya kuboresha hizi shule za msingi. Tuzitoe hizi shule kwenye watoto elfu moja na kitu twende kwenye watoto 800 au 1,200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hapa kwenye shule, lipo tatizo la watoto ambao wanamaliza sasa darasa la saba na hawawezi kuchukuliwa wote kwenda sekondari za Serikali na hata sekondari za Serikali zenyewe zimejaa. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Elimu, unajua zamani ilikuwa watu wote tunafanya mtihani unaambiwa haukuchaguliwa, si kwa sababu walikuwa hawapendi twende shule, walikuwa wanaangalia uwezo wa shule. Sasa siku hizi shule moja ya sekondari form one inapokea watoto 700, miundombinu iliyopo ni ya watoto 120, kwa hiyo, miezi sita ya kwanza yote Halmashauri inahangaika kuwatafutia watoto pa kusoma, hawa watoto watakuja kupimwa na mtihani ule ule wa watoto walioanza Januari, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tu-come up na mfumo, tujue kwamba Halmashauri hii ina nafasi 2,000, watoto watakaochaguliwa ni watoto 2,000 na watakaobaki watafute shule nyingine, ndiyo maana zamani watu walikuwa wanasoma kwa bidii. Hauwezi kuwa na mfumo wa kuchukua watoto wote, haiwezekani kwa sababu itakuwa kila mwaka hakuna halmashauri ambayo imekamilisha miundombinu. Tulikamilisha madawati mwaka juzi, sasa hivi hakuna shule yenye madawati ya kutosha na tulikamilisha madarasa hakuna shule yenye madarasa ya kutosha kwa sababu mfumo tulionao sekondari ni kuzoa watu wote, hauwezi kuwa na mfumo wa namna hiyo. Kwa hiyo, ni lazima tufike mahali tuseme kwamba nafasi tulizonazo ni hizi na kunakuwa na cutting point kwamba hapa tumekata cutting point, kama nafasi zipo ziende sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo pia la watoto sasa ambao inaonekana kwamba wanapomaliza darasa la saba au wanamaliza form four katika shule binafsi wanakwenda chuo kikuu halafu inaonekana kigezo cha kupata mkopo chuo kikuu unatakiwa uwe umesoma kwenye shule ya watu wanyonge, hiki kigezo si sahihi. Tunafahamu kwamba wapo watumishi ambao walikuwa na uwezo wa kusomesha watoto wake wawili kwenye shule nzuri lakini amestaafu, sasa kama kigezo ni hicho maana yake ni kwamba watoto wengi sana watakosa mikopo na ndicho kinachotokea sasa hivi, watoto wote wanamaliza darasa la saba wanakwenda kurundikwa sekondari ya Serikali kwa sababu anahofia mwanaye asikose mkopo chuo kikuu. Mimi nashauri, kama inawezekana mtoto yeyote aliyefaulu kwenda chuo kikuu apatiwe mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uvuvi, tulipiga kelele sana hapa Bunge lililopita kuhusu uvuvi. Tunashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi. Hoja yangu hapa ni ndogo, wavuvi wa sangara sasa hivi kwenye Kanda yetu ya Mwanza wanalalamika bei imepungua na kosa lilikuwa ni moja. Wakati sisi tunafanya operesheni kubwa wenzetu Kenya na Uganda walikuwa wanaendelea na kuvua na kuuza Ulaya. Kwa hiyo, matokeo yake walikamata masoko yetu kule na sasa hivi wavuvi wetu Kanda ya Ziwa wanakosa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri sasa Serikali, kwa sababu lipo tatizo la wamiliki wote wa viwanda vya samaki kuwa ni wa aina moja, wanafanya cartel, wanakaa wanapanga. Tutafute uwezekano wa kutafuta mtu wa kukaa katikati pale ili asiwe anakubaliana na lugha moja wanayozungumza wale wenye viwanda vya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, Mji wa Geita ulipewa ahadi na Mheshimiwa Rais kujengewa kilomita 10 za lami. Mwaka jana nilipoongea na Waziri aliahidi kuziweka kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2019/2020. Nimeangalia kwenye kitabu lakini hakuna barabara zangu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri anionee huruma hii ni ahadi ya Rais ambayo kwa miaka yote minne imekuwa inaonyeshwa kwenye vitabu lakini barabara hazijengwi. Kwa heshima kubwa, naomba jambo hili Waziri alipe umuhimu wake.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwanza naomba
kupongeza Kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri, lakini naomba nianze na tatizo la umeme
kwenye Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku umeme Geita unakatika kila siku zaidi ya mara nne.
Nimezungumza mara nyingi sana na Waziri, nimezungumza na Naibu Waziri na tatizo hili kwa
zaidi ya miezi nane halipatiwi majibu. Nafahamu kuna mradi ambao unaendelea lakini nadhani
speed ya mradi huo ni ndogo sana, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waheshimiwa Mawaziri
wanisikie kwamba kuna tatizo kubwa sana la umeme katika Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, mji wenyewe wa Geita ule, ni nusu peke yake ndiyo
unaowaka umeme, sehemu zingine umeme hakuna. Tunaambiwa tunasubiri umeme wa REA na
niliongea na Naibu Waziri nikamuomba basi atupe ratiba ya mradi wa REA wa nchi nzima tujue
kwamba Geita unakuja lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, linguine pamekuwepo na malalamiko mengi sana kwamba
watu wanalalamika kwanini Geita uwanja wa ndege umejengwa Chato? Sisi watu wa Geita
ndiyo tunajua. Mheshimiwa Rais akitokea Geita kwenda Chato ni kilometa 160. Ili afike Chato,
magari yanayotangulia mbele yanasimamisha watu matokeo yake kwa saa sita watu
wamesimama Barabarani. Kwa hiyo, solution ni kumjengea uwanja karibu na nyumbani
kuondoa ule usumbufu. Kutoka Geita kwanda Chato ni kilometa 160 kwa hiyo, watu
wanaolalamika kujengwa uwanja Chato ni kwa sababu hawafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili, nilikuwa naiomba tu Wizara ya Mawasiliano isiondoe
sasa nafasi ya kutujengea uwanja wa Mkoa wa Geita kwa sababu hatuwezi kuzuia Mheshimiwa
Rais ule uwanja usijengwe kule. Hata usipojengwa kero yake ni kubwa sana kwa wananchi pale
barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu, Mheshimiwa Rais Mgodi ule wa Geita karibu
miaka kumi ijayo utakuwa umeshachimba dhahabu. Geita hii tunayoizungumza ambayo kwa
Mgodi ule ndiyo the leading gold producer hapa Tanzania na karibu ya pili Afrika, wananchi
bado ni maskini. Na ukitazama, sioni dalili za namna ambavyo huu mgodi utabadilisha maisha
ya Wananchi sasa hivi kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, wangeanzisha mfuko wa natural
resources rent extraction ambao unafanyika katika nchi nyingi sana. Kwa mfano, mfuko kama
huu upo Norway, mfuko kama huu upo Marekani. Wakati kazi za madini zinapokuwa
zinaendelea, mfuko maalum kwa ajili ya kuwafanya wananchi wa maeneo yale baada ya
shughuli za madini kuisha waweze kuendelea na mambo mengine unakuwa umeandaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyokwenda sasa hivi, kesho kutwa dhahabu zitakwisha
kama zinavyoisha Kahama, wananchi watabaki maskini, Geita hatuna hospitali, Geita hatuna
barabara, Geita hatuna maji, Geita hatuna kila kitu lakini dhahabu zipo nyingi. Kwa hiyo,
nilikuwa nafikiri kwamba kuna tatizo hapa, siyo suala la kwanza duniani ni tatizo ambalo watu
wengi wameshindwa kulisemea hili. Tukianzisha mfuko huu ambao utatusaidia watu wataweza
kusoma, utaweza ku-deal na humanitarian crisis lakini utaweza kushughulika pia na mambo
mengine ya development kwenye maeneo yale. Sasa hivi tunapata 0.7 CSR kwa miaka 17,
mgodi umejenga shule moja ya wasichana. Kila siku wanaonesha kwenye television, miaka 17
0.8 percent ya CSR wangeweza kuifanya Geita kuwa Ulaya, lakini kwa sababu wanaamua
wenyewe wafanye nini hakuna kinachooneka kimefanyika pale. Maisha ya wananchi wa Geita
inaendelea kuonekana kama vile hawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nashukuru kwa kunipa nafasi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. KANYASU J. CONSTATINE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia Ambulance na pia mgawo na Madaktari wanne ambao tayari wamefika Geita. Kwa bahati mbaya mmoja bado yupo masomoni China mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba yafuatayo:-

(i) Hospitali yetu ya Wilaya imekuwa ya Rufaa ya Mkoa, kwa sasa imezidiwa sana na wagonjwa, gharama za dawa na huduma ziko juu kwa level ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Naomba sana juhudi za kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mheshimiwa Waziri aipe kipaumbele ili kupunguza gharama kwa wananchi.

(ii) Bado tuna uhaba mkubwa sana wa Madaktari Bingwa, Madaktari wa kati na wahudumu wa Afya, kama Nurses na watu wa Maabara. Naomba sana mwaka huu wakati wa mgao wa Watumishi wa Afya, Wizara isaidie kuitazama Hospitali ya Geita kwa jicho la huruma. Pamoja na suala hili kuwa la TAMISEMI bado Wizara ndiyo yenye jukumu.

(iii) Bado hospitali ya Rufaa ya Geita tunahitaji Duka la Dawa la MSD. Kosa kubwa limefanyika Geita ni kupeleka Duka la MSD Hospitali ya Wilaya Chato ambapo hakuna wagonjwa wengi, matokeo yake mahitaji ya msingi yamesahaulika au kupuuzwa. Ombi langu, Duka hili la Makao Makuu ya Mkoa lifunguliwe.

(iv) Ufanisi duni wa MSD, Halmashauri zetu zimekosa dawa muhimu kwenye bohari ya dawa, mafunzo yake, pesa hiyo inatumika kununua vifaa ambavyo siyo vya lazima na kuacha uhaba wa dawa ukiwa pale pale, matokeo yake MSD wanatoa O/S release kwenda kwa Private Vendor’s ambao huuza dawa na vifaa tiba kwa gharama kubwa, mara kumi zaidi ya bei ya soko ambalo watu wa kawaida wananunua. Hii maana yake ni kwamba pesa ya kutosha kutoa huduma mwezi mmoja kwa gharama za Private Vendor’s inatumika siku 10 tu.

Mheshimiwa Mwenyekti, naishauri Serikali kuhakikisha MSD wanazo dawa wakati wote kuepuka kupoteza fedha za umma.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nami naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kunipa afya na kunijalia kufika siku ya leo niweze kuchangia kwenye huu Mpango.
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kasi kubwa ambayo ameanza nayo. Kasi hii inawatisha watu wote. Ukiona maadui zako wanaendelea kukusifia, basi lazima ujue kuna tatizo. Kwa hiyo, wale ambao wanaona hawafanyi kazi, nadhani wanaogopa kivuli chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kurudisha nidhamu ya Watumishi wa Serikali. Nchi yetu ilikuwa inarudishwa nyuma na mambo mengi sana, likiwemo suala la Watumishi wa Serikali kutokuwa na nidhamu; nidhamu ya muda, lakini hata nidhamu ya utendaji. Hili kama litasimamiwa vizuri, tunaanza kujenga spirit ambayo mtu akiingia ofisini, anafahamu kwamba yuko pale kwa ajili ya kufanya kazi ya wananchi. Hili ni lazima lisimamiwe vizuri pamoja na viongozi wengine walioko ngazi ya chini.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kurudisha nidhamu ya matumizi. Naamini tulikuwa ni nchi ambayo tunaweza angalau kujitegemea kwa kiwango fulani lakini matumizi yetu yalikuwa yanakiuka baadhi ya mambo na kuonekana ni nchi maskini sana. Nampongeza pia kwa zoezi lake la kuhakikisha kwamba Watanzania wanalipa kodi.
Mheshimiwa Spika, suala la kodi ni suala ambalo Tanzania ilikuwa inaonekana anayelipa kodi ni mshamba. Watu wengi walikuwa wanajisifu kwa kutokulipa kodi. Sasa hivi utasikia malalamiko ya watu wengi kwamba wamebanwa. Watumishi wa Serikali tulikuwa tunalipa kodi kubwa zaidi kuliko wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, ombi langu tu hapa ni kwamba, zipo lugha ambazo zinatuchonganisha; zinamchonganisha Mheshimiwa Rais. Wapo Watumishi wa Serikali wanakwenda kulazimisha watu walipe kodi kuliko ambayo inatakiwa kulipwa anasema na ni kwa sababu ya Serikali yenu. Naamini watu hawa wakifuatiliwa, kodi ni kwa manufaa ya umma.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Fedha kwa kuja na Mpango wake huu. Naamini kwamba hivi vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye Mpango huu kama vitasimamiwa, tunaweza tukaifikisha Tanzania sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, tunalo ongezeko la mapato ya TRA, mapato yetu ya kodi. Nawapongeza sana! Wasiwasi wangu ni mmoja tu hapa, yapo malalamiko sana kwa wafanyabiashara; hakuna uniformity pale bandarini. Leo atakuja mtu ana container, declaration inaonesha vifaa vilevile ataambiwa Shilingi milioni 20, lakini mtu yuleyule akirudi next time ataambiwa Shilingi milioni 50, lakini jana yake utaambiwa mtu mwingine amelipa Shilingi milioni tisa.
Mheshimiwa Spika, nadhani iko haja ya kuweka utaratibu, badala ya kuacha hii freelance ambayo mhusika anaweza aka-gamble nayo na kuhamasisha rushwa, uwekwe utaratibu ili kila mtu kabla ya kufanya importation, ajue kwamba mzigo huu nikiufikisha Tanzania anakwenda kulipa kodi ya shilingi ngapi.
Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo, tutaendelea kuruhusu watu kukaa mezani na kujadili na matokeo yake yatakuwa kama aliyosema Mheshimiwa Keissy jana kwamba gari ile ile unanunua Dola 10,000, ukija pale, mtu wa TRA analazimisha iwe Dola 50,000, anakadiria kodi anayoitaka. Matokeo yake, watu wanakimbia gari pale bandarini, halafu Serikali inauza gari zile kwa bei rahisi zaidi kuliko ambayo alikuwa ameisema mhusika. Mimi nasema Serikali inafanya kazi nzuri, tunaipongeza, lakini ni lazima itoe macho zaidi katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta. Kwanza nianze na suala hili la elimu. Nimekuwa napata tabu kidogo kuona Tanzania ina output ya wasomi wengi sana, lakini kila kona wasomi wanalalamika ajira. Tatizo ni kwamba hata anayemaliza Chuo Kikuu akimaliza hawezi kujitegemea, akimaliza hawezi kujiajiri, hata yule aliyesomea ufundi, ukimwingiza ukampa kiwanda leo, akifika mle ndani hawezi kufanya kazi aliyosomea. Nasema kwamba, katika kipindi hiki cha miaka mitano, ni lazima mfumo wetu wa output katika vyuo vyetu usimamiwe vizuri ili watu wanaotoka waweze kuwa ni material ambayo inakwenda kupata kazi kwenye soko.
Mheshimiwa Spika, niende mbali, tuna output kubwa sana ya darasa la saba na output kubwa sana ya form four na form six ambao hawapati bahati ya kwenda kwenda kwenye Vyuo. Nataka kushauri, katika nchi zote ambazo zimefanikiwa kupambana na tatizo la ajira hasa kwa vijana, wameimarisha sana kwenye Polytechnic Colleges ambazo ndiyo zinaweza zikasaidia kupunguza tatizo la ajira. Kama tunaweza tukaweka katika Mpango wetu huu wa miaka mitano, tuweke mpango kuhakikisha kila mtoto aliyemaliza kidato cha nne, anakwenda Chuo cha Ufundi na iwe ni lazima. Hawa watu wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tumepeleka umeme katika kila kijiji, lakini mafundi wa umeme wanatoka Makao Makuu ya Wilaya. Hii sasa ilikuwa ni wajibu wa Serikali kuona kwamba tunaweka vyuo vya kutosha. Tunavyo Vyuo vya VETA, bado vyuo hivi ni gharama kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Chuo ambacho ulidhani angeenda mtu kusoma akapata ufundi, bado vyuo hivi vinachukua watu kwa kuchagua, wanakwenda watu 100 kati ya watu 10,000. Matokeo yake, bado kundi kubwa la vijana limezagaa mitaani, halina ujuzi wowote na Serikali nina uhakika hata tukizungumza kuwapa ajira, hawa sio sehemu ya kundi tunalofikiria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kushauri, pamoja na kuzagaa kwa vyuo, pamoja na mpango mzuri wa Serikali, tuweke mpango kabambe wa kuwa na vyuo vya ufundi ambavyo vitamlazimisha kila mtoto anayemaliza kidato cha nne, aende Chuo cha Ufundi ili apate kazi mbadala.
Mheshimiwa Spika, huwa nawaambia rafiki zangu tunaokwenda China; kule China ziko simu watu wanatumia hapa, zinatengenezwa mitaani tu, kwenye nyumba ya mtu. Ziko nguo zinashonwa mitaani, viko vitu vinatengenezwa hata ukitafuta kiwanda, huwezi kukipata kwa sababu kuna msambao wa viwanda vidogo vidogo katika kila kona na ndiyo namna tunavyoweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana, lakini na tatizo la viwanda.
Mheshimiwa Spika, kwenye Mpango kuna suala la viwanda. Tatizo langu ni kubwa. Hivi tunazungumzia viwanda vya namna gani? Viwanda hivi vitapata raw material wapi? Sehemu kubwa ya viwanda tunavyozungumza ni viwanda vya kilimo. Wilayani kwangu tuna Kiwanda cha Pamba cha Ginnery, kipo pale Kasamwa. Kile kiwanda hakijafanya kazi karibu miaka 15 sasa. Ukitazama uzalishaji wa zao la pamba umeshuka kwa kiwango ambacho kinatisha. Tatizo, kwa nini uzalishaji unashuka? Productivity ya uzalishaji inapungua wakati gharama za kilimo zinaongezeka! Viwanda tunavyozungumzia vinakwenda kupata raw material wapi?
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwenye suala la kilimo, kwanza tu- invest kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka maradufu ili watu watakaoanzisha viwanda wapate raw material. Leo watu wanalima pamba wanapelekewa mbegu feki, halafu mwisho wa siku kwenye uzalishaji mdogo waliopata, wanakwenda kudaiwa na kulazimisha walipe. Matokeo yake ni watu wote wameacha kulima pamba, wanahamia kwenye mazao mengine.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri katika Mpango huu tuwekeze kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji kwenye mashamba, uzalishaji wa mazao katika viwanda ambavyo tunafikiria tunakwenda kuvipeleka, lazima tufikirie namna ya kuongeza mazao yawe makubwa zaidi. Uzalishaji uwe mkubwa zaidi; na njia hapa ni rahisi tu!
Mheshimiwa Spika, cha kwanza ni kuwa na wataalam wetu katika kila kijiji na kuhakikisha wanafanya kazi; lakini kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati. Tulikuwa na tatizo la pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua. Pembejeo zinafika kwa wakulima mwezi wa kwanza. Wakulima wamekwishalima, wameshapalilia ndiyo pembejeo zinafika. Hawa watu wanalipwa!
Mheshimiwa Spika, tumeiambia Serikali kwamba kuna watu wanadanganya kwenye pembejeo, Serikali inatumia pesa nyingi sana, lakini haziwafikii wakulima; zinachelewa kufika. Ndiyo maana mtu analima heka tano za pamba anapata kilo 300. Ni kwa sababu pembejeo zinachelewa kufika. Kwa hiyo, nasema suala la viwanda liangaliwe vizuri kwenye suala la kilimo. Vile vile twende pia kwenye namna ambavyo tunaweza tukawaimarisha wananchi wa kawaida
Mheshimiwa Spika, sina tatizo sana na masharti ambayo yanayowekwa na watu wa Mazingira na kadhalika, lakini nadhani tume-copy sana mambo kutoka Ulaya kiasi kwamba tunashindwa kufikiria katika mtazamo wa Kitanzania, ni viwanda gani vinaweza vikasaidia wananchi wetu? Unaona kila siku tunapambana na watu wanaotaka kujikwamua.
Mheshimiwa Spika, kule Ulaya ukienda, mtu mwenye ng‟ombe wanne anaweza kuanzisha Kiwanda cha Siagi nyumbani kwake na akapeleka mazao yake kwenye Supermarket. Sisi kila siku tukienda kwenye mtu aliyeanzisha kiwanda, tunamfungia, huyu tunamfungia. Badala ya kuwasaidia hawa watu waimarike na wakue, tunawapunguzia uwezo. Utaona Serikali inapambana na watu wapunguze ng‟ombe, lakini haiwambii hao ng‟ombe wanaowapunguza itawasidiaje wabadilike kuwa na maisha tofauti.
Mheshimiwa Spika, mfugaji wa ng‟ombe anafanana sana na mtu mwenye mabasi kumi. Siku zote mtu mwenye mabasi kumi anataka afikishe mabasi 20. Hivi tuliwahi kumfuata mtu mwenye mabasi 20 tukamwambia apunguze idadi ya mabasi? Kwa nini tunafikiria kumwambia mwenye ng‟ombe apunguze, lakini hatumwambii apeleke wapi hizo fedha zake?
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye hili suala la viwanda, tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wa kawaida kuimarisha viwanda vidogo vidogo. Haijulikani SIDO ilifia wapi? Haijulikani kama ipo, inafanya kazi gani?
Nilitarajia tuone Tanzania ina Viwanda vya Sabuni kila Mtaa, Viwanda vya Nguo kila Mtaa na Viwanda vya kila kitu kila Mtaa. Sasa haya mambo hayafanyiki kwa sababu ya masharti mengi yanayowabana Watanzania na kuwafanya waendelee kutegemea bidhaa za kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala linguine. Kwenye Mpango naona kuna mpango wa kuongeza nishati. Nilisema wakati nachangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nikasema naipongeza sana Serikali na mkakati wake wa kuimarisha njia ya umeme inayokwenda Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa na wasiwasi sana ya kuwa na njia moja kuu ya umeme ya kupelekea robo tatu ya nchi. Napenda kushauri, katika Mpango huu, ile njia iliyotajwa katika Mpango; ya Nyakanazi, ni njia ya muhimu sana. Nchi nyingi zinapata majanga! Linaweza kutokea janga katikati hapa, nusu ya nchi ikawa giza na nchi hii inakwenda kuwa nchi ya viwanda. Ina maana tutasimama uchumi wetu siku hiyo hiyo. Ni lazima tutafute namna ya kuimarisha njia ya pili ya umeme.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Geita, bado umeme unazimika na kuwaka muda wowote kwa sababu njia iliyopo ni ile iliyokuwa inapelekea umeme Sengerema. Umeme ni mdogo sana. Wananchi pale kukatika kwa umeme kwao ni suala la kawaida, lakini umeme mzuri upo jirani tu Katoro pale.
Mheshimiwa Spika, nimezungumza na Waziri mara kadhaa na nimeomba sana katika mwaka huu wa fedha, umeme wa uhakika upelekwe Geita. Ni Mkoa mpya, Mkoa ambao tunatarajia utakuwa na viwanda vingi. Sisi katika Kanda ya Ziwa ni wakulima wakubwa sana wa nanasi, ingawa nanasi zile Mheshimiwa Mbunge mwenzangu alisema zinafaa kutengeneza madawa ya kienyeji, lakini tunapozungumzia viwanda, basi lazima wakulima waambiwe ni mananasi yapi yanayofaa kwa ajili ya kuuza kwenye viwanda, kwa sababu ardhi inakubali kulima nanasi, kahawa na mazao mengine. Ni lazima tukubaliane kwamba tunahitaji umeme ili huu umeme uweze kuwasaidia wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Spika, katika Mpango huu, naomba sana, sisi Kanda ya Ziwa kama walivyosema wenzangu, tunalo tatizo la bidhaa zote zinazotoka Dar es Salaam kufika Kanda ya Ziwa zikiwa zimepanda bei. Ukifika Geita leo, utakuta bandali moja ya bati inauzwa Sh. 280,000/= wakati bandali hiyo hiyo Dar es Salaam inauzwa Sh.160,000/=. Ni kwa sababu ya matumizi ya barabara. Tunaomba sana reli, reli ikiimarika, itasaidia kupungua gharama za vifaa vya viwandani ambavyo vinapanda bei kila siku Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, hata gharama ya mafuta iliyoko Geita ni kubwa kuliko iliyoko hapa, ni kwa sababu tatizo kubwa ni Usafirishaji. Hatuwezi kuendelea kujenga barabara zinazobomoka kila baada ya miaka miwili kwa sababu inabeba mizigo mikubwa. Tuwe wakweli! Kama barabara hizi zinatumia mamilioni ya shilingi, tunakopa, wenzetu wanakaa wanasema hawaoni faida ya mikopo na barabara hizo zinakufa, keshokutwa tutalazimika kuzijenga upya kabla ya kulipa madeni. Njia pekee ya kufanya suala hili ni kuimarisha sana mfumo wetu wa reli ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na bidhaa zinazopungua bei.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Mpango, kuna mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege Chato. Kutoka Geita kwenda Chato ni kilometa zaidi ya 150. Geita ni Makao Makuu ya Mkoa. Naomba sana Wizara hii itakapofika, tunataka kujua kama kutakuwa na mpango wowote kwa Geita kupata uwanja wake wa ndege. Watu hawawezi kutembea kilometa 160; tunakubali kwamba Mheshimiwa Rais anatoka Chato na sisi tunafurahi kuwa na Mheshimiwa Rais Chato, lakini Geita kama Makao Makuu ya Mkoa, tunataka uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Spika, Geita tunayo machimbo mengi sana ya dhahabu. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa inapambana zaidi na maskini kuliko inavyopambana na umaskini.
SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, kama unaunga Mkono hoja, dakika zako zimekwisha.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOHN C. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niseme kwa kifupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niwaombe wahusika Mfuko wa Jimbo bado unakwenda Halmashauri ya Wilaya hauji Halmashauri ya Mji walishughulikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la TASAF, tatizo lililosemwa na Wabunge wengine liko kwangu pia, naomba litazamwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati yangu ya UKIMWI tulikutana na Group of Donors, wanasema ufadhili unaendelea kupungua na wanaitaka Serikali kuongeza uwezo wake kwenye mfuko wa AIDS Trust Fund. Kwa sababu kadri wanavyoonesha inaonekana mwaka huu itapungua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa hapa kwamba jukumu la Ofisi za Wabunge liko chini ya TAMISEMI kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunaomba watoe maelekezo tunapotoka hapa tupate ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme lingine, katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita kuna madeni ya watumishi ya tangu mwaka 2007. Madeni hayo yamefanyiwa uhakiki zaidi ya mara tatu lakini fedha hizo haziendi na hawalipwi. Nilitaka kufahamu kwenye bajeti hii kama fedha hizo zimetengwa na wataanza kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita yalifanyika mazungumzo ya Serikali ya Mkoa pamoja na mfadhili COTECNA, ambaye walikubaliana kujenga diagnostic centre. Baada ya mabadiliko haya ya Mkuu wa Mkoa yule mfadhili amekwishaandaa fedha anakwenda pale anasema waliopo wote hawatoi ushirikiano. Naomba sana apewe ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo la ukusanyaji wa service levy. GGM wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi lakini 90% ya hizo kampuni ziko nje ya nchi. Nilitaka kupata mwongozo hizo kampuni zilizoko nje ya nchi ambazo GGM hawataki ku-disclose kwamba zinatoaje service levy, tunazipataje hizo fedha Halmashauri ya Mji wa Geita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu tulitembelea Buhangija, tukaenda kwenye kituo cha watoto albino. Tulipofika pale tulikuta kuna taarifa kwamba wake wa viongozi walifanya harambee kuchangia kituo kile miaka miwili iliyopita lakini fedha hizo hazijawahi kufika na tulikuwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Possi. Tunaomba kujua waliofanya harambee hizo fedha zilikwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchangia kwenye suala la ujenzi wa ofisi. Nchi hii kila Halmashauri ina ramani yake, nataka kushauri pawe na common ramani ya Halmashauri zote. Halmashauri yangu ina fedha za kujenga ofisi miaka minne sasa fedha ziko ndani, ofisi haijengwi na kwa taarifa zilizopo wamepunguza karibu shilingi milioni 300 kuchoresha ramani mpya. Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo alikuwa amewaletea ramani ambayo tayari imechorwa na imejengwa sehemu zingine. Naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie ili Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya iweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu ya muda nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu ada elekezi, Serikali iwaache wamiliki kupanga bei kwa kuwa gharama za uendeshaji wa shule hizo ni kubwa sana kutokana na michango mingi na kodi. Pia shule hizi hazifanani kutoka moja hadi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nizungumzie kuhusu vibali vya Walimu wa nje. Serikali iangalie namna ya kuondoa vizuizi vya Walimu wa kutoka nje kufundisha Tanzania hasa Walimu wa masomo ya hesabu na sayansi. Urasimu mkubwa wa Serikali wa kupata working permit na kodi kubwa inayotozwa na Serikali inakatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Chuo cha VETA Geita. Naiomba Serikali kunipatia majibu ni lini chuo cha VETA kitajengwa katika Mkoa wa Geita ambao ni mpya na eneo la kujenga chuo hicho lilitengwa toka mwaka 2014. Kwa mujibu wa VETA, ujenzi wa chuo hicho ulikuwa umefadhiliwa na ADB kwa thamani ya 6.7 billion, leo miaka miwili hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu utitiri wa vyuo binafsi. Serikali ichunguze sana viwango vya elimu vinavyotolewa na vyuo mbalimbali vilivyosajiliwa na NECTA. Mfano ni Chuo cha Elimu ya Utalii Musoma kimefungua matawi katika wilaya za Kanda nzima ya Ziwa, je, ubora wa certificate na diploma hizi unafanana? Hii ni pamoja na matawi ya vyuo vikubwa na vidogo Tanzania ikiwemo CBE, Mipango na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, madeni ya wazabuni mashuleni. Serikali itoe taarifa ni lini itawalipa wazabuni fedha zao walizotumia kutoa huduma mashuleni. Hivi sasa hali ya huduma katika shule zetu ni mbaya kutokana na madeni haya ya wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, nyumba za Walimu vijijini. Naishauri Serikali kuanzia sasa itoe tamko la kuzuia kabisa halmashauri zote kujenga nyumba za watumishi wa mjini, kuacha kujenga ofisi za vijiji na kuacha kununua magari mapya na kuhamishia pesa yote kwa miaka mitatu kwenye nyumba za Walimu. Nashauri pia ramani ya nyumba simple iandaliwe kwa ajili ya nchi nzima mfano vyumba viwili vya kulala, sitting room na jiko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Nakushukuru sana Mwenyekiti, na naomba nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, niwashukuru pia wapiga kura wangu wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Geita kwa ujumla wake kwa uvumilivu wao mkubwa wanaoupata kwenye matatizo ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kusoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 ambapo amesema Serikali iliajiri kampuni ya Shaka Consult Group ya Misri kuwa mshauri mwekezaji wa kusimamia utekelezaji wa mradi wa Bulyanhulu - Geita KV-220 kwenye urefu wa kilometa 55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameendelea kusema hapa lakini interest yangu ni kule chini; anasema gharama za mradi huu ni dola milioni 23 sawa na takriban bilioni 41. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni shilingi bilioni sita, very interesting, na unatarajiwa kukamilika 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mradi huu ambao ameukusudia kuupeleka Geita. Ninaamini kwamba una nia njema, lakini natazama fedha zilizotengwa sasa na pia natazama muda ambao umejiwekea kutekeleza nayaona matatizo makubwa ya umeme katika Mji wa Geita kwa sasa yataendelea kuwa kero kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu nimsumbua sana mara kwa mara, umeme wa Geita Mjini unazimika kila saa, umeme wa Geita Mjini ambao unatokea Sengerema kuja Geita ni mdogo, ulikuwa umefikiriwa kwa ajili ya Mji wa Sengerema na baadaye ukapelekwa Geita. Umeme ule inapofika saa moja jioni unawaka lakini taa haziwaki. Nimemueleza hili Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri analijua, sasa nilitarajia kwenye taarifa yake hii atakuwa angalau na mpango wa dharura kwa sababu Geita pale ni Mji mkubwa, lakini ni Mkoa ambao tungeweza kuweka mpango mzuri wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninayo mapendekezo, tunao umeme kilometa 22 tu kutoka Geita Mjini ambao uko Katolo ambao ni umeme wenye nguvu. Wakati unafikiria mradi mkubwa huu ambao utaisha 2018, na inawezekana ukaisha 2020. Umeme huu ambao uko kilometa 22 tu kutoka Katoro kuja Geita, na ambao gharama yake inakadiriwa haifiki bilioni moja kuuvuta kuufikisha Geita Mjini, ingelikuwa ni suluhisho la kwanza la kupeleka umeme katika Mji wa Geita. Hivi ninavyozungumza na wewe kata zinazotengeneza Mji wa Geita wenyewe, kata za Nyankumbu, Bombambili, Buhalahala, Mtakuja zote hazina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani umeme upo pale pale kati kati ya Mji lakini Vitongoji vyote vya Geita Mjini havina umeme. Pamoja na huo uliopo kutokuwa hautoshi lakini havina umeme. Kuna sehemu wameweka transfoma ambayo kila inapofika jioni saa moja umeme unazimika. Nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na nia njema ya mradi huu unaokwenda mpaka 2018 ambao pia naona fedha zake zimewekwa za kuanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe suluhisho la sasa, kwa sababu umeme uliopo Katoro una nguvu, utolewe umeme upelekwe pale. Bahati nzuri sana Geita tuna Meneja mzuri wa TANESCO, ana-respond haraka, hana matatizo makubwa, kinachosumbua pale sasa ni kumwezesha ili aweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye umeme wa REA. Katika Jimbo la Geita Mjini umeme wa REA bado katika kata zote 13 haujaenda, nimefanya mawasiliano na Meneja wa REA wa Kanda ile amesema ametuingiza kwenye awamu hii, lakini nilikuwa naomba sana, kwa sababu tatizo hili naliona hata katika Jimbo la Geita Vijijini, kazi ya mkandarasi imekamilika mpaka sehemu ya kutoka Nyamadoke tayari; pale panatakiwa tu kuunganishwa ule umeme, leo karibu miezi sita hapajaunganishwa. Nilikuwa naomba sana kwenye umeme wa REA Mheshimiwa Waziri suala hili lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la wachimbaji wadogo wadogo. Mheshimiwa Waziri alikuwepo Geita, na nashukuru kwamba tulifanya mkutano naye na akatoa takwimu nyingi sana. Lakini anakumba nilitoa ushauri wangu pale sikumpinga nilitoa ushauri, ana takwimu nyingi sana zinazoonesha wachimbaji wadogo wamepewa maeneo lakini wanaopewa ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayepewa leo London – Singida, anayepewa leo Nyarugusu, anayepewa Kahama, majina ni yale yale. Nilimshauri atengeneze database, atagundua yako majina yale yale yanazunguka. Kila yanapogunduliwa madini wanakwenda wanafukuza wenyeji, wanaunda ka-SACCOS wananunua watu wanahamia pale. Nashauri kwamba wananchi wale wa kawaida bado hawapati maeneo, na ndio maana kelele za magwangala zitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunazungumzia maeneo ya wachimbaji wadogowadogo lazima tuangalie watu wanaojirudiarudia, watu ambao kila mara yanapogundulika madini wanakwenda pale kwenda kutafuta maeneo mapya. Tulipokutana na Mheshimiwa Waziri kwenye ziara yetu Geita tulimgusia kuhusu milipuko. Mheshimiwa Naibu Waziri tulikuwa naye Geita, tulikwenda kwenye nyumba ambazo zimeathiriwa na milipuko, tulikwenda kwenye nyumba ambazo vigingi vya GGM viko ndani ya makazi yao, wale watu hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, wanaonekana eneo ni la mgodi lakini mgodi wanasema hawana kazi nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauriana na Mheshimiwa Naibu Waziri na akatoa muda, akawaambia wafanye declaration kama wanalihitaji lile eneo walipe fidia watu watoke na kama hawalihitaji, wawaruhusu watu waendelee na maisha yao mpaka leo hili suala halijafanyika, matatizo ya watu yanaendelea kuwa pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niseme kwamba kuendelea kukaa katika vigingi watu hawa wanaendelea kuwa maskini. Hawawezi kupima, hawawezi kukopeshwa, hawawezi kujenga nyumba za kudumu. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie anafanya nini kwa sababu hali hii inasababisha wananchi wangu wa Jimbo la Geita kuendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kuhusu magwangala. Kama wanavyosema wenzangu magwangala inatokana na vijana wengi na wanotaka biashara za madini kukosa maeneo ya kuchimba; si suluhisho la matatizo ya wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu nina uhakika magwangala yale hata yakitolewa leo baada ya miezi miwili, yatakwisha na yatakapokwisha yale magwangala tutatengeneza tatizo jingine kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka kusema pamoja na nia njema ya kutoa magwangala haya ambayo wananchi wanayapigia kelele, wananchi walikuwa na maeneo yao walikuwa wanachimba ya asili pale Geita, kama Nyamatagata, Samina wakaja wakatolewa, lakini maeneo yale dhahabu yake iko juu juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa Geita akisema yeye hawezi kubadilisha hata mtu ampige risasi. Mimi nataka nimshawishi Mheshimiwa, sheria inasema kila baada ya muda, wanapofanya revision ya license kuna maeneo watu wanayaachia, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo wanayaachia yawe ni maeneo ambayo wananchi wanaweza wakachimba wakapata dhahabu ya juu juu.
Mheshimiwa Mwnyekiti, matatizo tuliyonayo sasa hivi Geita ni kwamba hata kama watu wa GGM wangejenga hospitali, shule na barabara kama jamii inayowazunguka pale inalala njaa, kama jamii inayowazunguka pale bado wanaishi katika mazingira kama wako utumwani bado wataendelea kuwachukia wawekezaji na tutaendelea kuuchukia mgodi.
Kwa hiyo, mimi nilitaka niwashauri kwamba ni lazima wananchi wapewe maeneo ya kuchimba, na hili liko ndani ya uwezo wako kwa sababu maeneo tunayo. Tatizo kubwa ni moja walipelekwa maeneo ya Isamilo, wakapewa license karibu 17 za SACCOS wamechimba watu wameweka karibu milioni 200 madini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechimba pale wanakutana na maji madini hakuna, kwa hiyo mara nyingi migodi inaachia maeneo ambayo imefanya utafiti imegundua kwamba dhahabu zilizopo pale ni ndogo na hazifai. Kwa hiyo nikuombe sana utakapotaka kutoa maeneo tuhakikishe kwamba maeneo haya yana madini ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la service levy. Mheshimiwa Waziti alipokuwa Geita, tulimwambia hatuna mgogoro na Geita Gold Mine ingawa mchango wao wa service levy ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita ule ni mgodi wa pili Afrika kwa dhahabu nyingi, wanatupa bilioni nne. Tuliuliza swali, hizi ni asilimia ngapi ya mapato yao? Kwa sababu tunaamini mapato yao ni makubwa sana, lakini la pili, wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi. Katika hizo asilimia 80 kampuni zile ziko Ulaya, Australia, New Zealand na Marekani, wanafanya nazo electronic business. Kwa hiyo, anampa Mkurugenzi wa Halmashauri aende akakusanye service levy kwa kampuni ambayo haina license Tanzania, hailipi kodi Tanzania, haina address Tanzania. Tulimwambia Mheshimiwa Waziri, watu wa mgodi walazimishwe kufanya kazi na kampuni za Tanzania ambazo tunaweza kuzi-trace na kujua zinapatikana wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wanakupa kampuni iko New Zealand halafu wanakwambia ukusanye service levy kampuni hii haijulikani, haina leseni, hailipi kodi za Serikali, hata Tanzania haina address na Mheshimiwa hili niliwahi kufika mpaka ofisini kwako nikakutana na Katibu Mkuu wa Wizara, nikamshauri, nikazungumza naye na akasema atalishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa watu pamoja na kuwaibia Halmashauri ya Geita, bado pia wanaiibia Serikali. Huwezi ukalipa mtu dola milioni moja kampuni yake iko South Africa, Tanzania haina leseni, hailipi kodi, haina ofisi na Serikali ipo inakubali hizo hesabu wakati wa kufanya Cooperate tax.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana hili liangaliwe vizuri. Na inawezekana kabisa haya yanafanyika kwenye makampuni yote katika nchi hii, kwa sababu visingizio ni kwamba kuna vipuri ambavyo vinaagizwa Ulaya na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuviuza, yes tunakubali, lakini procedure za kufanya biashara Tanzania zinajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Watanzania hamuwaruhusu hata kufungua kibanda cha soda bila kupata TIN Number. Kwa nini huyo anayellipa mamilioni ya shilingi anaanza kufanya biashara na Mgodi na analipwa pesa na inakuwa declared kwenye hesabu wakati hana leseni Tanzania na halipi kodi? Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri asaidie kupata hizi fedha kwa sababu ni fedha nyingi na tunazihiitaji kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama unavyoitaza Geita sasa hivi, kuna mashimo makubwa, ambayo tayari dhahabu zimekwisha. Inawezekana kabisa miaka ishirini ijayo tukabaki na mashimo yale na wananchi wa Geita wakaendelea kubaki maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ni kwamba wakati mgodi unafikiria kufanya CSR washirikiane na Halmashauri kuangalia miradi ambayo sisi tunadhani ina tija kwetu. Siyo wao wanabuni mradi wao halafu ule mradi wanaugeuza kuwa mradi wa wananchi wa Geita. Tunaunga mkono juhudi zao tunapenda waendelee kuwepo, tunataka wawekezaji zaidi lakini lazima waangalie mipango ya Halmashauri namna gani wataingia kwenye mipango hiyo kuliko kuja na mipango yao wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekwenda wameanzisha, chuo cha kushona cherehani wameanza na watu 90 sasa hivi wako watu kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba pia nitumie nafasi kukupongeza kwa namna ambavyo unaendesha Bunge letu na niwape pole wenzetu ambao wanasubiri siku ambapo utalegeza msimamo. Nadhani hii ndio namna bora ya watu kuheshimu taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kuchangia kwa hoja ya Mkoa wa Mwanza, Geita na Kagera kuonekana ni mikoa maskini zaidi Tanzania. Mwanzo ni kweli na nilikuwa napata shida, na nilikuwa sielewi mantiki ya suala hili linatoka wapi? Lakini nimekuja kugundua sababu za msingi ni kama ambazo wenzangu wamezieleza. Yapo mazao na kazi za msingi ambazo zilikuwa zinafanya maeneo haya yaonekane maeneo ambayo uchumi wake uko juu, yanaenda yanakufa polepole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Geita, ambao miaka yote tulikuwa tunajivunia pamba, sasa hivi pamba imekufa hakuna dalili kuna mkakati maalum wa Serikali wa kurudisha zao hili kwenye chati na ukiangalia trend yake ya uzalishaji kwa miaka mitano, mwaka jana ilikuwa even worse. (Makofi)
Kwa hiyo, nadhani kwamba, hatuna sababu kwa nini tusiwe maskini. Mkoa wa Kagera walikuwa kahawa inakosa soko, walikuwa na migomba, migomba inaugua, ndivyo ilivyo katika mikoa mingine mingine ya Mwanza na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaanza msimu wa pamba, lakini nataka kukuambia mpaka leo bei haijulikani na wananchi wana pamba iko ndani na ni haya haya ambayo mwakani zikija takwimu hapa itaonekana mikoa hii ni maskini sana. Kwa hiyo, nilikuwa nasema, Serikali pamoja na kutoa takwimu hizi bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha kwamba, ina-coordinate mazao haya na kazi hizi za wananchi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia katika Mkoa wa Geita, ambao una dhahabu katika kila Wilaya, haijulikani mpaka leo wale wachimbaji wenyewe wa dhahabu wanauza wapi? Wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu haijulikani wanauza wapi? Wanaojulikana ni wanunuzi wa dhahabu wakubwa wakubwa. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba uchumi huu mdogo katika level ya chini hauko coordinated, haujulikani. Lazima wananchi hawa waonekane ni maskini, lakini influx inayosababishwa na machimbo katika Mikoa ya Geita na Mwanza na wapi ni kubwa sana na watu wote hawa wako bize kwenye kazi za kiuchumi. Nilikuwa nadhani watu wa uchumi wanatakiwa wafanye kazi vizuri zaidi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi kwenye bidhaa ambazo walikuwa wanauziwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Naweza nikaunga mkono suala hili, lakini naomba nitoe mapendekezo yangu kwamba bidhaa hizi zinaweza zikalipiwa kodi, lakini uwekwe utaratibu ambao utavifanya vyombo yetu vya ulinzi na usalama viwe na credit card wakati wa kufanya manunuzi. Kwa mfano kama askari hawa wataweza kwenda kwenye duka lolote bila kujali duka hili ni lile ambalo limetengwa, wakiwa na credit card au debit card na wakaweza kupata punguzo la kodi pale pale, mantiki ya maduka haya itaendelea kuwa ile ile na mantiki ya kuwapa huduma nyepesi wanajeshi watu itakuwa ile ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongeza mshahara au ukaongeza pesa kwenye mshahara wake haijulikani huyu mtu atanunua nini kwa mwezi, nina uhakika kwamba tutaendelea kufanya maisha ya vyombo hivi kuwa vigumu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na naomba nichangie pia kwenye suala la kufutwa kwa misamaha kwenye taasisi mbalimbali. Ni kweli kwamba, Serikali ilikuwa inapoteza karibu shilingi trilioni mbili kwenye kodi kwa sababu ya misamaha, lakini ninataka tu kutoa hoja hapa kwamba kama vyombo hivi vitalipa kodi, urasimu wa namna ya kurejeshewa kodi hii lazima Serikali ijipange vizuri. Kwa sababu nitapa wasiwasi namna wanavyokwenda kugagua na kujiridhisha kwamba, bidhaa hizi zilizoingizwa zimetumika kwa mujibu wa malengo yaliokusudiwa na matokeo yake tuta-demoralize hawa waliokuwa wanasaidia. Maana yake ni lazima tukubaliane nchi yetu mpaka leo, sehemu kubwa ya Hospitali zilizo kwenye Wilaya, sehemu kubwa ya taasisi ziliko hapa, shule pamoja na nini zinamilikuwa na taasisi mbalimbali. Kama watu hawa watakatishwa tamaa na wataacha tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa hiyo, lazima Serikali iangalie namna ya kulifanya hili ili lisije likatela usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamefanyika marekebisho mbalimbali kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Waziri kwa kuondoa baadhi ya tozo kero kwenye maeneo mbalimbali. Lakini nilitaka kusema bado mazingira ya kufanya biashara kwenye nchi yetu ni magumu sana. Nitoe mfano sehemu moja tu. Sehemu ya hoteli, mtu akiwa na hoteli leo pamoja na kupata leseni, pamoja na kupata tax clearance kutoka TRA itaanza kulipa OSHA, atalipa Fire, atalipa hotel levy, ana aina ya tozo pale karibu kumi, ambazo zote hizi zinafanya mzunguko wa pesa kwa wananchi kuwa mdogo. Sasa inaonekana Serikali inajiaanda tu kukamata pesa kila kona na kuzirudisha kwake.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba bado kuna haja ya kuangalia vizuri, kwenye hoteli hapo utakuna na mtu wa afya, utakutana na mtu wa TFDA, utakutana na kila aina ya ushuru na wote hawa ni vyanzo vya mapato, nilikuwa nadhani kuna haja nzuri ya kuliangalia vizuri upya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi za majengo, naweza kusema kwamba nilikuwa naunga mkono watu wa Halmashauri waendelee kutoza hizi, lakini nitaunga mkono TRA iwapo Mheshimiwa Waziri, utatuambia ni kwa namna gani pesa zilizokadiriwa kwenye Halmashauri atahakikisha zinapatikana kama zilivyo kwenye bajeti, vinginevyo tutajikuta kwamba, wakishindwa kukusanya TRA madhara yakuwa makubwa sana kwenye Halmashauri zetu za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makato kwenye gratuity ya Mbunge; nilitaka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, sisi Wabunge wa Bunge la Tanzania kwanza ni Wabunge tunaolipwa kidogo zaidi kuliko Mabunge yote Afrika Mashariki. Nataka nitoe takwimu hapa, ukichukua salary na allowance, Bunge la Kenya walipwa dola 11,000, Rwanda dola 9,000, Uganda dola 8,000, South Sudan dola 7,000, Burundi dola 6,000, Tanzania ni least pay dola 5,000, hii ni salary na allowance. Sasa atuambie baada ya kuingiza haya makato anakwenda kuboreha wapi ili tufanane na nchi zingine? Kama hilo halifanyiki nataka kumshawishi Mheshimiwa Waziri afikirie namna mpya ya kutanua hii tax base kwa sababu kinachomsumbua sasa ni kufikiri kwenye base ile ile wakati unaongeza projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na njia rahisi ya kutanua tax base, akumbuke kati mwaka 2007 na 2010, Serikali iliweka stimuli kwenye baadhi ya viwanda na mazao ili kuwa inalinda visife ili Serikali isipoteze walipa kodi. Sasa ushauri wangu hapa tunavyo viwanda vingi vimesimama, kama tunataka kuongeza kukusanya mapato tupeleke pesa huko viwanda vifufuke tuanze kukusanya kodi vinginevyo leo wataanza kukata kodi kwenye gratuity, kesho watakuja kwenye allowance, atakuja kwenye per diem baadaye pataisha pa kukata kodi wakati huo anaendelea kupanua projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba pia suala la polisi ambao wamewekwa kwenye chanzo cha mapato. Unapo-commercial raise service ukawambia polisi wakae barabarani ukawapa malengo ya kukusanaya shilingi bilioni moja, maana yake unawambia wakamate sana watu barabarani na kwa tabia ya polisi hawa-negotiate na wateja tutaanza kupata migogoro mingi kwa sababu watajielekeza kwenye kufikia malengo ya kukusanya shilingi bilioni moja kwa mwezi. Nilikuwa nadhani hawa wangeachwa watoe huduma na inapotekea wanatoa faini iwe ni faini ya kawaida, lakini wanapowekwa kwenye kikapu cha kuanza kukusanya pesa na kwamba lazima walete shilingi bilioni fulani lazima tunatengeneza mgogoro mkubwa kati ya watumiaji wa barabara na poilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na lingine ni kuhusu kodi kwenye withdraw mbalimbali M-pesa na benki. Nataka tu kufahamu kwamba Serikali imejiandaaje kuweka regulatory board ambayo ita-control sasa wasipandishe hovyo hovyo. Walizoea hizi pesa zote kuzichukua wao, sasa tumepeleka kodi pale matokeo yake wataongeza, tutajikuta watu wanaogopa kupeleka fedha benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunipa afya njema na kupata nafasi ya kusema machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia na Kamati ambazo ziliwasilisha maoni yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 21. Waziri Mkuu ametoa takwimu za upatikanaji wa chakula kwa mwaka uliopita na akagusia kwamba mwaka huu kuna maeneo ambapo hali ya hewa haikuwa nzuri sana. Nilichokuwa nakitegemea hapa kidogo na nitoe ushauri ni kwamba kutokana na hali hiyo kutokuwa nzuri, kwanza nilitarajia nione hapa kama kuna akiba kiasi gani sasa ya chakula lakini tunakitumia kwa namna gani ku-control bei inayoendelea kupanda kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza jana Mwanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 125,000 na wakati kelele za uhaba wa chakula zinaanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 80,000. Hii maana yake ni nini? Kadri tunavyokwenda kuja kufikia mwezi wa kumi kama hakuna
mechanism ya Serikali ku-control bei ya mahindi yatafika shilingi 160,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza hapa sio njaa, hatuzungumzi njaa tunazungumzia kwamba bei ya chakula inapanda kwa sababu Serikali ni kama haijachukua position yake ya ku-control bei ya chakula kwenye soko. Wakati tunazungumza wakati ule bei ya mchele ilikuwa
shilingi 1,200 leo ni shilingi 2,500, Mwanza ni shilingi 1,800. Maeneo yote haya ninayoyazungumzia hawakulima kwa sababu mvua hazikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama tunayo stock ya chakula kwenye godowns, Wizara ichukue position yake, chakula kingie kwenye masoko na bei elekezi itolewe ili kisiendelee kupanda, vinginevyo purchasing power ya wananchi
inapungua. Wananchi kipato ni kilekile, chakula kinapanda, matokeo yake watajikuta hata hiyo shilingi 2,000 ya kula kwa siku inakosekana. Hilo ndiyo lilikuwa ombi langu kwenye huu ukurasa wa 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 25 amezungumzia kuhusu hekta 38,567 za wachimbaji wa madini. Tatizo langu mimi sio utengaji wa maeneo, nilimwambia Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita akazungumza takwimu kubwa za
kuwapa watu maeneo ya kuchimba. Nikamwambia tatizo kubwa lililoko hapa wanaopewa ni walewale. Ukiingia kwenye database utamkuta Kanyasu huyu ana-appear kwenye karibu kila eneo dhahabu inapotokea wale ambao wanatakiwa kabisa wapewe maeneo haya hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe tuna vikundi zaidi ya 100 Geita vimejiandikisha vinasubiri maeneo ya kuchimba havipewi, lakini ukienda kwenye takwimu za Wizara atakutajia kubwa ya watu ambao kimsingi ni walewale wachimbaji wakubwa ambao wanahama toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, ni ahadi yetu kwenye Ilani ya CCM, tutawapa watu maeneo ya kuchimba, lini? Huu ni mwaka wa pili sasa. Kama yapo tunaomba yaanze kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 28 limeongelewa suala la umeme. Geita kila siku umeme unakatika. Hivi ninavyozungumza na wewe umeme hakuna, unakatika zaidi ya mara nne. Nimezungumza na Waziri na Naibu Waziri, wana matengenezo ya kutoka Busisi kwenda
Geita karibu miaka miwili hayaishi. Nataka kufahamu hili tatizo la umeme Geita linakwisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, kuna maeneo tumepeleka umeme wa REA baada ya umeme wa REA kufika kazi imeisha, jirani akiomba umeme TANESCO hakuna vifaa. Ina maana REA peke yake ndiyo sasa inafanya kazi ya kusambaza umeme, TANESCO wenyewe hawana uwezo? Naomba sana eneo hili lifanyiwe kazi vizuri kwa sababu linakatisha tamaa, kama umeme umefika kijijini, kuna watu wanne wamepewa umeme, jirani hapewi umeme kwa sababu TANESCO hana vifaa, nadhani hapa kuna mipango mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la fao la kujitoa. Mimi natoka Geita na naomba Waheshimiwa Wabunge wote wanisikilize vizuri sana. Geita pale karibu nusu ya watu wanaofanya kazi pale Geita Mjini ni watumishi wa mgodi. Kinachotokea kwenye mgodi pale ni kwamba
hakuna mwenye ajira ya kudumu. Kuna watu pale wanafanya kazi kwa mikataba ya miezi sita, miaka miwili, miaka mitatu. Anapofukuzwa kazi hawezi kupata kazi ya aina ile tena katika nchi hii, kuna wengi ni vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wanafukuzwa kazi, kwa sababu kandarasi iliyokuwa imempa kazi mkataba wake umekwisha, imeondoka imekwenda South Africa. Akienda kufuata pesa zake NSSF anaambiwa hizo pesa hawezi kupewa mpaka afike umri uliolezwa. Mtu leo ana
miaka 25 au 30 asubiri pesa hizi mpaka afikishe miaka 55 ndiyo aweze kulipwa na hana kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja ametoa hoja kwamba wapewe asilimia 25, hapana. Ziko kada ambazo wanaweza wakasubiri, ukimwambia mwalimu, polisi, daktari asubiri sawa. Pale mgodini kuna tabia supervisor akikuchukia anaku-blacklist,
akiku-blacklist huwezi kuajiriwa mgodi wowote duniani. Sasa unakaa unasubiri hiyo pesa mpaka utakapofikisha miaka 60 unaendelea kuwa maskini kwa misingi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri, sekta ya madini iangaliwe kwa jicho tofauti. Kuna watu pale wanaacha kazi kwa sababu ni wagonjwa. Mgodi ule hauchukui watu wagonjwa, ukitibiwa mara mbili unaumwa kifua wanakufukuza, Mheshimiwa Jenista unafahamu nilikuletea watu wanaumwa, walipokuwa vilema walifukuzwa kwenye kazi, wana miaka 25, 30 halafu wananyimwa zile pesa wanaambiwa wasubiri mpaka watakapozeeka, anazeeka hizo pesa aje atumie nani? Ushauri wangu ni kwamba sekta ya madini ichukuliwe kwa namna tofauti, hatuwezi kuwa na jibu moja kwenye maswali yote magumu, lazima tuliangalie hili suala tofauti. Kama tuna nia ya kuwekeza NSSF wana mitaji mikubwa waangalie sehemu nyingine, lakini haya maisha ya watu kwa pale Geita tutawafanya kuwa maskini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gereza pale Geita Mjini, uwezo wake ni kuchukua watu 100 na zaidi, hivi sasa lina watu 800, sababu kubwa ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatafuta pesa ndogo ndogo ya kula, akikamatwa anarundikwa pale. Kuna tatizo sasa hivi kwenye Jeshi la Polisi na watu wa Idara ya Sheria, kesi ya madai inageuzwa inakuwa jinai wanarundikwa mle, matokeo yake watu wanalala wamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu na nafikiri nilizungumza na wewe, pale kuna tatizo tuna OC-CID hafanyi kazi yake vizuri, kazi yake ni kukusanya pesa, anachokifanya yeye ni kuhakikisha kwamba kila anayetuhumiwa pale, iwe ni jinai, iwe ni civil lazima
abambikwe kesi ambayo itamuweka magereza zaidi ya miezi mitatu, gereza limejaa. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikuja aliona, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ulikuja uliona, tunaomba mtusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hizi kesi ndogo ndogo za kupita tu mgodini anakamatwa mtu anawekwa ndani miezi sita. Unapita tu na baiskeli unakamatwa unawekwa ndani miezi sita. Serikali ina pesa za kuchezea, kwa nini hizi pesa ambazo zinakwenda kulisha watu humo
wasipewe hawa wanasheria wakapeleka hizi kesi haraka? Mimi nadhani kuna haja ya kuisaidia Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni uwepo wa migodi mingi sana kwenye Mkoa wa Geita na tatizo la huduma za afya. Wilaya ya Geita peke yake ina watu 800,000 kwa sensa ya mwaka 2012, lakini hospitali yetu iliyokuwa ya Wilaya tuliigeuza kuwa ya Mkoa, matokeo yake hatuna tena Hospitali ya Wilaya. Sasa ufikirie population ya watu 800,000 wa Wilaya moja na ile hospitali imegeuka kuwa ya mkoa, watu milioni mbili matokeo yake ile hospitali imezidiwa kabisa uwezo. Tuna vituo viwili vya afya tumeanza kuvitengeneza, tunaomba support yako Mheshimiwa Waziri wa Afya, tunakushukuru ulitupa gari lakini hatuna madaktari. Daktari aliyepo pale kuna specialist mmoja ambaye ni surgeon waliobaki wote ni AMO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali, tulitaka kuleta muswada hapa wa kuwaondoa Madaktari Wasaidizi kwenye mfumo wa madaktari, lilikuwa ni kosa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule vijijini madaktari wetu ni ma-AMO na ndiyo wanaofanya kazi usiku na mchana. Ukiwaondoa wale kwenye mfumo wa madaktari waliobaki wengine wote ni mabosi wakienda kwenye wilaya kazi yao ni research, hawakai kwenye ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mtusaidie sana Hosptali yetu ya Mkoa wa Geita ianze ili Hospitali ya Wilaya irudishwe Wilayani ili gharama za matibabu ziweze kupungua. Hivi sasa navyozungumza na wewe gharama za matibabu ziko juu sana kwa sababu tunalipa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa sababu ya muda naomba nizungumze mambo machache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Geita Mjini tulipopata bahati ya kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Geita karibu nusu ya eneo la upande wa Mashariki miaka ya 1954 lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, hakuna msitu wowote kuna bushes. Nilimwandikia barua na kumuomba kwamba wananchi wa Geita ule mkoa hauwezi kutanuka kuelekea Kaskazini wala kuelekea Magharibi kwa sababu ni eneo ambalo limepewa mgodi, eneo pekee la kutanuka ni kuelekea Kusini, na Mkoa kupitia RCC wameomba katika vikao tangu mwaka 2012 kuomba eneo la Msitu wa Usindakwe na eneo ambalo lilikuwa Msitu wa Geita (Usindakwe) liwe eneo ambalo Mkoa uruhusiwe kutoa maeneo ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza karibu nusu ya Mji wa Geita ni eneo ambalo zamani lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, sasa nilikuomba Mheshimiwa Waziri kwa maandishi lakini sasa ni karibu miezi sita naomba leo uniambie ni hatua gani zimefikiwa? Sababu moja ni kwamba mpaka leo watu wa TFS wanazunguka, wanaweka alama kwenye nyumba, wana-disturb watu, lakini hakuna mti, hakuna chochote. Katika maeneo ya Nyakabale na Mgusu wananchi katikati ya kijiji kuna vigingi na katikati ya eneo la vijiji hivyo tayari mgodi umepewa eneo hilo, hivyo, wanashindwa kufanya chochote kwa sababu eneo hilo linaonekana kama ni hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni TFS katika Mkoa wa Geita, limetoka tangazo kupitia kwa Waziri kwamba ni marufuku kutumia pikipiki, baiskeli kubeba mkaa wala kubeba chochote. Vijiji vyetu vyote ambako wananchi wanakaa hakuna magari, hakuna chochote, kwa hiyo matokeo yake watu wa TFS wamerundika pikipiki na baiskeli Makao Makuu ya Ofisi zao na wanategemea kuzipiga mnada. Baiskeli ambayo imenunuliwa shilingi 150,000 inauzwa shilingi 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo hili ni uonevu mkubwa kwa sababu wananchi katika maeneo hayo ya vijiji hawana usafiri mwingine wowote mbadala zaidi ya baiskeli. Sasa sheria inaposema kwamba ni lazima tutumie magari, kusafirisha mkaa, hivi wananchi kwenye vijiji wanapata wapi magari? Kwa sababu inavyonekana ni kama mkakati wa kuwadhulumu wananchi baiskeli zao, ananunua mtu baiskeli, anakamatwa anakimbizwa porini ananyanganywa na sasa hivi watu wa TFS wanakwenda kwenye masoko kusubiria watu. (Makofi)
Mimi nafikiri TFS wamesahau core function yao. Core function yao ni kulinda misitu, wanachokifanya sasa siyo kulinda misitu tena, ni kusubiri barabarani waendasha baiskeli na pikipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuambie na tangaza leo hawa wananchi wanatumia nishati gani? Tuambie tu mimi niko tayari kuwaambia wananchi sasa acheni, ni nishati gani mbadala ambayo Wizara yako imeandaa kwamba sasa hii ndiyo itakuwa nishati mbadala? Kinachoendelea sasa hivi na kwa wananchi ni kwamba wananchi wanalazimishwa sasa waanze kulala njaa kwa sababu mkaa unakamatwa sokoni, unakamatwa barabarani, anakamatwa mwenye baiskeli, pikipiki, gari haijulikani utaratibu huu sasa unatupeleka wapi.

Mheshimiwa Waziri inawezekana wewe huna taarifa, nguvu inayotumika kwenye suala hili kule kwenye maeneo ya wananchi ni kubwa kuliko hata thamani ya kitu kinachoenda kuzuiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikushauri Mheshimiwa Waziri, kwa nini unapata tatizo kubwa sana la kulinda misitu yako, unapata shida ya kulinda hifadhi? Kwa sababu ya mahusiano mabaya sana ya TFS na vijiji. Watu wa samaki walibuni kitu kinaitwa Beach Management Unit (BMU) kwa sababu wananchi wanatakiwa wajisimamie wenyewe. Ninyi mnatumia nguvu kubwa, amesema Mheshimiwa Mbunge asubuhi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kuna maeneo ya wananchi katika Wilaya ya Ilemela ambayo Jeshi liliyapima ili kuyachukua kwa miaka mingi bila kulipa fidia na kuwaondoa wananchi katika maeneo hayo, Mheshimiwa Waziri naomba kufahamu uthamini uliofanyika maeneo ya Nyagunguku - Ilemela, Nyanguku, Lukobe kwa miaka miwili sasa umefutwa au bado upo valid?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lengo la JWTZ lilikuwa kufanya uthamini na baadaye kuwaacha wananchi katika maeneo yao kwa muda mrefu bila kujua hatima yao, naomba kujua watalipwa lini au Jeshi limejiondoa kwenye nia ya kumiliki maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatana na timu za Orjoro JKT na Kanembwa JKT kushushwa daraja kwa tuhuma za rushwa ambazo zimeshindwa kuthibitishwa na chombo cha kisheria cha uchunguzi wa makosa hayo (PCCB). Je, ni hatua gani Wizara yako imechukua kupigania haki ya vijana wako na heshima ya vyombo hivyo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kudorora sana kwa michezo ya aina mbalimbali, mfano, riadha, sarakasi, ngumi, mitupo, volleyball, nimetaja kwa uchache tu kwa nini kuanzia sasa kipaumbele cha kijana kujiunga na JWTZ na JKT au vyombo vingine isiwe ni kipaji kimojawapo cha michezo ili kuufanya umma wa Watanzania kupenda michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili vijana hao wawe competent ni vizuri Wizara yako ikatafuta wabia (marafiki) kutoka nje ya nchi kusaidia kuongeza taaluma, mfano, China, Cuba, Urusi na Korea, ambapo vijana wetu waweze kupata ujuzi mpya au nyongeza ya ujuzi walionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara yako ina mpango mkakati upi wa kusaidia kuimarisha michezo nchini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia na kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Geita Mjini, naomba nitumie nafasi hii pia kuwataarifu kwamba lile tatizo lao la watu wa TFS kuweka alama kwenye nyumba ambazo zipo katikati ya Mji wa Geita wakidai ni hifadhi, nilishamjulisha Waziri wa Maliasili na kwamba tunachosubiri ni maombi ya RCC ili waweze kufikia maamuzi ya kuliachia eneo hilo. Maamuzi hayo yanachelewa sana na wananchi wanaendelea kusumbuliwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Geita wanaomba kuona unachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mbunge, Mheshimiwa Doto Biteko, nimesomeshwa na pamba, lakini pia nimesomeshwa na uvuvi. Nimesomeshwa na uvuvi, natoka kilometa mbili kutoka Ziwani ndiko nilipozaliwa; na eneo letu tulilokuwa sisi tulikuwa na mashamba makubwa sana ya Nyanza wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na pongezi nyingi sana ambazo nampatia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwenye Wizara hii, hasa kwa kuondoa kero nyingi kwenye zao la pamba. Pia ninaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba Nyanza Cooperative Union, mali zake ambazo zilihujumiwa kinyemela, zinarudi na hatimaye Nyanza iweze kusimama imara. (Mkofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba inaoneka sasa hivi ni suala geni lakini sisi wakati tunakua wakati ule, pamba ndiyo lilikuwa zao la kujivunia kwenye Kanda ya Ziwa na umaskini wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kudorora kwa zao la pamba. Wakati huo mashamba yote ya pamba makubwa na mazuri uliyokuwa unayaona, wananchi walikuwa wanalima yalikuwa aidha ni ya Nyanza au ni ya watu walikuwa wanakopa pembejeo. Mfumo wa kukopa pembejeo ulikuwepo tangu zamani wala siyo mgeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi walikuwa wanapewa mbegu bora, walikuwa wanapewa madawa na baadaye vyama vya ushirika kwa sababu vilikuwa vina nguvu, vilikuwa vinaweza kununua yale mazao kwa wakati na kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuimarisha vyama vya ushirika kwa sababu ndiyo reliable vinaweza kuwakopesha wakulima. Kama hilo haliwezekani, ni kuona namna ya kuwafanya hawa private buyers ambao mnawapa usajili waweze kuwa engaged namna ya kuwasaidia wakulima. Bila kutatua tatizo la kuwapatia pembejeo na mbegu bora wakulima, hatuwezi kulifanya zao la pamba likarudi kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna ambayo naiona hapa, kwanza wakulima sasa hivi wamekata tamaa kwa sababu ukiacha wastani wa heka moja kuzalisha tani mbili na kilo 200 wengi wanazalisha kilo 100 au kilo 200. Sasa kilo 200 hata kama ungempa kilo moja Sh.2,000/= bado hawezi kulipa gharama za kilimo, productivity imeshuka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mkulima kama ataweza kuzalisha tani moja kwenye heka, hata ukimpa kilo Sh.1,000/= utakuwa umemsaidia. Tatizo kubwa liko wapi? Tunao Maafisa Ugani wengi sana kwenye Halmashauri za Wilaya, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri hawa watu hawapewi target. Ameajiriwa, amepewa ofisi, amepewa Kata, hakuna mtu anayemsimamia. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu aweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu wanakaguliwa, wanapimwa kwa kitu fulani ambacho wamekifanya kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanaamka asubuhi, anakwenda anasaini, anarudi, analala, hata katika kijiji ambacho anakaa wakulima hawafahamu. Hata katika kijiji ambacho wanakaa hajawahi kutoa utaalam wa aina yoyote. Kwa hiyo, matokeo yake wakulima wameligeuza zao la pamba kuwa zao la pili na wengi wamehama. Wengi wanakwenda kwenye mazao mengine kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Geita watu wengi wanalima mpunga; na mpunga kwa sababu pia hata utaalam wa watu wengi wanalima kutokana na ulimaji wa asili, wamehamia huko kwa sababu ni zao la chakula na zao la biashara. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri Maafisa Kilimo, hata angeajiri wengi namna gani, kama waliopo hawasimamiwi, bado zao la pamba litaendelea kuwa chini kwa sababu hakuna uzalishaji ambao unaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba nilisomeshwa na samaki. Naomba hapa Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Ipo sheria ambayo ilitungwa mwaka 2003 na kanuni yake ya mwaka 2009. Sheria ambayo inasema “it is illegal to manufacture, possess, store, sell and use or cause another person to use for a fishing gear of more than 26 mesh deep in the Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha ya kawaida wanasema ni makosa kuzalisha au kukutwa una nyavu ambayo ina macho 26. Sasa macho 26 nikifanya mikono yangu miwili hapa, tayari ni macho 26 ya mtego.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatoka kisiwani, tumevua wote samaki. Naomba nimkumbushe, ukitoka Mwanza South pale ukaenda Nautical Mile 15, chini ni mita 70, hebu aende na hiyo nyavu ya macho 26 akavue samaki kama atapata kilo tano. Kinachofanyika sasa, imetungwa sheria, hiyo sheria imeipitishwa lakini inahamasisha watu waende kuvua samaki kwenye breeding areas. Wanakwenda kwenye zile breeding areas ambazo tungetarajia ziwe hifadhi, samaki wazaliane kwa sababu nyavu wanayopendekeza ambayo wanaiita illegal, ni nyavu fupi. Ni mikono yangu miwili hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Gozba ni mita 100 chini. Nataka nimpe challenge Mheshimiwa Waziri, nimefanya kazi ya samaki miaka 25. Kama ana wataalam wake wa uvuvi awaambie waweke nyavu 100 twende Gozba, wakirudi na kilo kumi naacha Ubunge. Naacha Ubunge kwa sababu wanachokifanya ni kuwaonea kabisa wavuvi. Wanaenda wanachukua zile nyavu, wanaita illegal wanazichoma moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mvuvi gani anatengeneza nyavu? Nyavu zimepita bandarini, zimelipiwa ushuru, mvuvi amekopa pesa benki, amekwenda kuweka kwenye mtumbwi, size ya nyavu anayotaka ni ile ile nchi tano au sita ambazo wameruhusu; lakini wanasema ikishazidi macho 26 ni illegal. Sasa wakati inapita bandarini watu wake walikuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu. Yeye kama ni mvuvi na anafahamu mambo ya uvuvi twende ziwani. Wavuvi wetu wengi ni local, wanafanya traditional fishing, hakuna mwenye fish finder; hakuna mwenye chochote. Kwa hiyo, hakuna anayeona samaki chini. Tuchukue hizo nyavu tuende nautical mile 50 tukatege, halafu turudi kesho tukavue; tukipata samaki kilo 50, mimi naacha Ubunge. Kwa sababu nimefanya kazi hii kwa miaka 20 na nimekimbia huko kwa sababu ya masharti mengi yasiyo na maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomaliza samaki Ziwa Victoria ni matumizi ya monofilament na matumizi ya makokoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/ 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wazungumzaji wengine waliotangulia wamesema, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao tunatoka kwenye maeneo ambayo uchimbaji wa dhahabu ni kazi kubwa kabisa ya maisha ya kwetu ya kila siku. Kwa hiyo, juhudi za Mheshimiwa Rais za kupambana na namna ambavyo madini haya yatakuwa na manufaa kwa wananchi sisi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini na Mkoa mzima wa Geita tunazipa kipaumbele kikubwa na tunaziunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara ya Fedha namna ambavyo inapoteza fedha nyingi kutokana na mikataba mibovu ambayo ilikuwepo. Nilipata nafasi ya kuchangia mwaka jana na sikuona mabadiliko yoyote yale wala hatua zilizochukuliwa. Kampuni nyingi zinazofanya kazi na migodi mikubwa ni kampuni za nje na migodi hii mikubwa imepewa uwezo inapotaka vipuli au bidhaa zozote inaweza kumpa yeyote aliyeko ndani au nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kampuni hizi zinazopewa kazi nyingi hazina ofisi Tanzania. Wanapokuletea orodha ya kampuni ili uweze kwenda kudai service levy wanakupa orodha ya kampuni ambayo ipo Canada, Australia, South Africa ambao hawana ofisi hapa, hawana license hapa wala hawana wafanyakazi. Lakini gharama ya manunuzi yao yameingizwa kwenye corporate tax, kwa hiyo, yanapunguza sehemu ya faida ambayo Serikali ingeweza kulipwa na ndiyo maana migodi mingi haiwezi kulipa kodi kwa sababu wanaweza ku-deal na kampuni iliyoko Canada ambayo ninyi Serikali hamna kumbukumbu nayo, haina ofisi, haina address, matokeo yake ni kwamba sisi tunapoteza pesa nyingi kwa sababu hatuwezi kwenda kudai service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, niliseme hili mwaka jana na miongoni mwa makampuni haya ni makampuni ya bima. Kampuni hizi za bima zime-insure wanafanyakazi lakini wana- insure strong room, processing, mgodi mzima. Kampuni hizi kubwa za bima unapoomba ile orodha ya makampuni ya service levy hawakuletei kwa sababu hazipo Tanzania. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri, hii ni sehemu kubwa ambayo tunapoteza pesa nyingi sana. Kama kampuni hii itakuwa ipo Dar es Salaam au ipo Mwanza watakuwa na ofisi, watalipa working permit, watalipia wafanyakazi wao na matokeo yake Serikali itapata fedha na itapata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Halmashauri tunataka tupate hii service levy kama Serikali wanaona hii pesa ni ndogo hawana sababu ya kuyafanya makampuni yaje Tanzania, wayaache yakae nje. Sisi tunaomba watusaidie wawalazimishe sheria watu hawa wafungue ofisi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, mwaka jana nilishauri hapa nikasema tatizo kubwa tunakwenda kwenye viwanda lakini ili viwanda viweze kufanya kazi lazima kilimo kwanza kipewe kipaumbele. Watu wengi wamezungumza kuhusu kilimo. Tatizo ninaloliona kwenye kilimo tangu tumeanza kuzungumza unaona transformation inayotupeleka kwenye kilimo ambacho kitalipa inakwenda kwa kasi ndogo sana. Mtu anayehamasisha viwanda ana kasi kubwa. Viwanda vinahamasishwa kwa kasi kubwa, raw material ni products za kilimo, lakini transformation ya kufanya kilimo kiweze kusaidia viwanda inakwenda kwa kasi ndogo ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, sisi Geita tunalima mananasi, mbegu ya nanasi ambayo ingeweza ku- supply au kuuzwa nje kwa sababu tunaambiwa mananasi tuliyonayo yanafanana sana na madawa ya kienyeji wala huwezi kuuza nje. Ili tuweze kupata product ya nanasi ambayo inaweza kuuzwa nje nilidhani kwa sababu nchi inajua tunalima nanasi, tayari wangekuwa wamepeleka wataalam wakatupa mbegu za kisasa zile mbegu ambazo tunaweza tukauza yale mananasi nje, tukawa na soko ambalo lingeweza kuwabadilisha wakulima wa mananasi katika Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumeanza kuzungumza kuhusu kilimo, wakulima wa mpunga wanalima kienyeji vilevile walivyolima miaka kumi iliyopita. Tunafikiria kuongeza ukubwa wa mashamba, sio ukubwa wa uzalishaji. Kwahiyo, matokeo yake, mbegu za mpunga zile zile ambazo tulilima miaka kumi iliyopita ndizo tunazozungumzia kuendelea kulima kwenye mfumo wa viwanda. Kwa hiyo, haiwezekani viwanda tunavyovizungumza vikaja viwaka productive kama hatuwezi kufikiria kubadilisha kabisa namna ambavyo tunalima. Ukienda kwa wakulima wetu wengine wanalima ukubwa wa shamba. Anaweza kulima ekari kumi akapata gunia tano za mahindi, lakini kumbe angeweza kulima heka mbili akapata gunia 60 za mahindi na eneo lingine akalima kitu kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mabadiliko tunayotaka kwenye kilimo lazima yaendane na speed ya ujenzi wa viwanda tunavyovifikiria vinginevyo tunakwenda mahali tutajenga viwanda, halafu tutaagiza raw material kutoka nje. Alisimama hapa Waziri wa Kilimo akasema hata Bakhresa maziwa anayopaki kwenye pakiti mengine ni ya unga kwa sababu maziwa hakuna. Lakini leo utaona vita ya Serikali na mifugo, vita ya Serikali ya wafugaji ni kuhakikisha wale wafugaji wanafilisika badala ya kuwasaidia wale wafugaji waweze kutengeneza uzalishaji mkubwa wa maziwa ili Bakhresa apate maziwa. Bila kufanya hivyo, hata viwanda tunavyovihamasisha vije vitakuja vifungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili nilitaka kuona mchango wa Idara ya Uvuvi kwenye uchumi wa Tanzania. Ziwa Victoria miaka kama 15 ya nyuma tulikuwa tunapata pesa nyingi sana za kigeni kutokana na uvuvi, taratibu taratibu productivity imeendelea kushuka sasa tunabuni mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwalinda wale samaki. Lakini tatizo kubwa lililoko Ziwa Victoria, lile ni ziwa, uvuvi ni mkubwa hakuna juhudi za ziada za Serikali za kuhakikisha kwamba tunapandikiza vifaranga vya kutosha kwenye Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, kuna maeneo mengi sana yemetengwa kwa ajili ya samaki kuzaliana na yale maeneo yaliyotengwa, Serikali ingeweza kuwa na mkakati kabambe wa kuingiza vifaranga hata milioni 100 kila mwaka vifaranga wa sangara unawaweka katika Ziwa Victoria, wakisaidiana na wale ambao wanazaliana kwa mfumo wa kawaida, samaki hawawezi kuisha katika Ziwa Victoria. Tatizo letu tunavuna tu, tunavuna tu matokeo yake badala ya kugundua kwa nini samaki wanapungua tunaweka masharti ya kuwaambia wavuvi wapunguze size ya nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa wakati nachangia kwenye Wizara ile na bahati nzuri Waziri hakutaka kulijibu. Amefanya operesheni ya kukamata wavuvi wanaovua samaki kwa nyavu ambazo zina macho zaidi ya 26 lakini hiyo nyavu ambayo inatumika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ujasiri mkubwa na hasa kwa sababu mimi na Mheshimiwa Rais mwenyewe tunatoka kwenye mkoa ambao hawa wachimbaji wa dhahabu kwa kweli wanatuachia mashimo matupu na watu wanaendelea kuwa maskini. Kwa hiyo, hizi jitihada za Mheshimiwa Rais tunaziunga mkono, tunampongeza sana na wananchi wa Mkoa wa Geita kimsingi ambao wameshuhudia miaka 19 dhahabu inachimbwa lakini Makao Makuu ya Mji wa Geita hakuna barabara, Makao Makuu ya Mji wa Geita hakuna maji, hospitalini hakuna wodi, shule watoto wanakaa chini kilometa moja kutoka kwenye mgodi pale watu ni maskini sana; wanaona juhudi hizi za Mheshimiwa Rais zinatakiwa kuungwa mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nawashangaa sana wenzangu hawa ambao wanapinga kwa sababu kama walivyosema wenzangu huko nyuma, walikuwa kila siku wanalalamika wanasema kwamba nchi hii inaibiwa lakini nataka kusema kwamba Mheshimiwa Rais aendelee na ikiwezekana na aangalie pia katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mnyika katika ukurasa wake wa saba amezungumzia kwamba Serikali iliingia mkataba wa loyalty wa four percent. Hii ni four percent siyo ya force declaration. Unapofanya force declaration, four percent yeyote haina maana yoyote ile kwa sababu unazungumzia four percent ya value gani? Hawa watu wanafanya four percent ya uongo halafu wanakuja kuwatetea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine la pili; nilikuwa namshangaa sana Mheshimiwa Mnyika kwenye ukurasa wake wa tisa anasema kwamba taswira ya Tanzania kwenye jarida moja huko la Mining journal inasema trouble in Tanzania kwa sababu Rais ameanza kufuatilia wizi, so what? Trouble, yes kuna wizi unagundulika, unataka Rais asigundue wizi? Lazima Mheshimiwa Rais afuatilie kwa sababu unaposema trouble in Tanzania, kama kuna wizi umegundulika lazima Rais afuatilie sasa mimi nakushangaa unapo…

KUHUSU UTARATIBU .....

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ulichosema ni sahihi na namshangaa sana ndugu yangu hapa mimi nazungumzia issue katika general yake yeye anajaribu kwenda katika eneo dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya muda, kuna mzungumzaji pia mmoja amezungumzia kwamba uzalishaji wa umeme umepungua, nilitaka aende kwenye ukurasa wa 21 ataona mahitaji ya umeme ndiyo yaliyoongezeka kutoka megawats 1,026 kwenda megawats 1,051, lakini uzalishaji wetu ni megawats 1,450.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuishukuru sana Wizara hii. Geita tulikuwa tuna matatizo makubwa sana ya umeme, unakatika kila siku; hivi ninavyozungumza sasa hivi umeme wa Geita haukatiki, umeme wa Geita uko imara na ninachowaomba tu sasa hivi ni kuhakikisha sasa umeme huu kama ahadi ambavyo ilikuwa kwamba vijiji ambavyo vilikuwa havijapata umeme wa REA vinapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kusema hapa ni kwamba pamoja na umeme wa Geita kutokatika, lipo tatizo ambalo nilimwambia Mheshmiwa Naibu Waziri kwamba TANESCO hawana vifaa. Kwa hiyo watu wanapoomba umeme wanachukua muda mrefu sana kupata connection ya umeme; hivyo nadhani pamoja na juhudi za REA TANESCO wakae upya wafikirie namna ambavyo wanaweza kuongeza mtaji. Kama TANESCO wameshindwa kuwa na vifaa vya kutosha kwenye store, ni vizuri wakaruhusu vendors wengine wakawa na vitu hivi kwenye maduka na wao wa-control quality kuliko ilivyo sasa, mteja ameomba umeme leo anafungiwa mwezi wa 10 kwa sababu wewe huna meter, kwa sababu wewe huna waya wakati soko hili ni soko huria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ushauri wangu. Nakushukuru sana kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri yafuatayo; Serikali iongeze bajeti kwenye fungu la maendeleo na pesa hii ipo kwenye mafuta, umeme na maji yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya umwagiliaji inakumbana na pingamizi kwa kuwa ujenzi wa miundombinu umejielekeza kujenga mabwawa kukinga maji. Hapa wananchi wanaogopa kupoteza ardhi zao, kwa nini tusitumie mfumo wa visima virefu na wind wheels kuweka maji kwenye matanki na kusambaza kwa gravity kwa kuwa gharama ni nafuu na eneo linalopotea ni dogo. Mradi kama huu upo kata ya Kanyalla Ibada na umepingwa na wananchi kwa sababu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tatizo la maji Mjini Geita, hivi sasa Mradi wa Maji wa LV-Watsan unasuasua sana mpaka leo miezi minne imepita, mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi, nashauri mtu huyu afutwe kwenye orodha ya wakandarasi kwa kuwa hana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhaba wa maji katika Mji wa Kasamwe, naishauri Serikali kuunganisha mradi mpya wa maji wa fedha za India kwa Mji wa Geita ili maji yake yafike Kasamwa, kwa sababu kwa mujibu wa wataalamu hivi sasa kuna tanki kubwa la maji Buhalanda ambalo lipo kilometa 10 tu kutoka Kasamwa na ambapo maji yatafika kwa gravity na kwa kuanzia ziwekwe DP’s tu kwenye mitaa ili wananchi wapate maji, badala ya sasa kutumia bwawa ambalo gharama yake ni kubwa

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kunipa majibu maji katika Kata za Shiloleli, Bulela, Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Bung’wangoko yatafika kupitia mradi huu wa fedha za India? Kwa sababu hizi kata ni sehemu ya kata za Mji wa Geita Jimbo la Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuzungumzia uwanja wa ndege wa Chato. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini na ninashangaa sana watu wanaoona uwanja wa ndege unaojengwa Geita/ unaojengwa Chato kwamba ni matumizi mabaya ya fedha. Watu wana-define uwanja mkubwa kwa urefu wa runway, lakini nadhani wanapungukiwa exposure. Uwanja mkubwa ni facilities na uwanja ule ili uwe mkubwa ungekuta linajengwa jengo la abiria kubwa, kwa hivyo ndipo ungesema uwanja mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe tu, wamesema uwanja wa ndege uko pale strategically, wanasahau kwamba kutoka Chato kwenda Rubondo ni kilometa 30 na tunahamasisha utalii. Pia wanasahau kutoka Chato kwenda Biharamulo ambapo kuna mbuga za wanyama za Buligi pamoja na Biharamulo pale ni kilometa
50. Wanasahau kwamba tuko karibu kilometa 100 kwenda mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaposema ni strategic airport watu wengi hawaelewi tunazungumza nini, wanawaza tu kwamba ni uwanja wa Rais kwenda nyumbani. Mimi nasema ule uwanja umejengwa sehemu sahihi na uwanja ule sisi tunauhitaji ungejengwa katika eneo lolote lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine ambalo watu ni lazima walifahamu Rais alikuwa akitua Mwanza kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda Chato anatembea kilometa 270 anakwenda kupumzika. Akitua Bukoba anatembea kilometa 250 kwenda kupumzika. Sasa amejenga uwanja karibu anapokwenda kupumzika wanapiga kelele. Mimi nataka niwashauri, issue ya ukubwa si urefu wa uwanja, nenda kasome, issue ya ukubwa ni facilities za uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya TRA, jengo la TRA watu wanafikiri kurudi nyuma unakwenda mbele unaenda wapi? Badala ya kusema tunajenga jengo likae miaka 50 mbele wewe unawaza kujenga slope.

Mimi nasema hata ofisi za Serikali tuache sasa, tuanze kujenga majengo ya ghorofa. Habari ya taa ni habari ya Halmashauri yenyewe hata kama wangepita punda tunaangalia usalama wa raia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la madini. Serikali ilipoanza kusimamia vizuri madini sisi watu wa Geita Mjini tumeona manufaa yake na nataka nitoe takwimu hapa. Kabla ya Serikali kuweka mikono yake kwenye madini, mapato ya Halmashauri yangu Januari-Machi ilikuwa shilingi milioni 514; Aprili-Juni shilingi milioni 750; yakaongezeka kidogo hapo. Ilipofika Julai-Septemba tumepata bilioni moja kasoro, maana yake ni nini? Kulikuwa kuna wizi mkubwa sana unafanyika hapa kwenye madini. Wito wangu hapa kwa Mheshimiwa Waziri ninashauri ufanyike uchunguzi kurudi nyuma kuona kwa nini baada ya Serikali kutuma wawakilishi kwenye hizi kampuni za madini mapato ya Halmashauri yangu yameongezeka kutoka shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni moja wakati kazi ni ile ile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tulipitisha Sheria hapa ya Local Content, bado watu wa mgodi wanapiga. Bado wana walinzi kutoka nje, bado wana kampuni nyingi kutoka nje ambazo zinaweza kufanya kazi na Watanzania. Wakati wa Mpango wa mwaka uliopita nilishauri hapa kwamba tuna kampuni nyingi sana ambazo zinafanya kazi kwa remote, kampuni iko South Africa, iko Australia, inafanya services katika Mgodi wa Geita, hawalipi kodi! Bado halijafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuwaomba hawa watu watulipe service levy wanakwambia hii kampuni haipo Tanzania. Naomba kushauri, sheria hii tuliyoipitisha hapa Bungeni, yaelekezwe haya makampuni ya madini yaweze kuisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tunajenga reli kuja Dodoma, mimi nasema fine, tunakopa, tunafanya nini, mimi nasema fine, lakini wasiwasi wangu ni mmoja tu, hii reli itakapofika Dodoma kabla haijafika Mwanza itakuwa haina msaada mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania. Nataka kushauri, badala ya kufanya vipande vipande kwa muda mrefu ufanyike uamuzi wa mara moja wa kuwekeza reli hii moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ili itakapokamilika manufaa yake yaanze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mimi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tulipata bahati ya kwenda China na tukaenda katika jimbo moja la Guangdong. Tulipotembelea pale, Meya wa mji ule anatuambia jimbo lile limejengwa na private sector, anasema Serikali haijajenga miundombinu katika jimbo lile. Airport, barabara, madaraja wamejenga private sector. Tuache kukopa kujenga miundombinu, tukaribishe… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu hii ukiitazama ina matatizo makubwa mawili; la kwanza ni tatizo la fedha ambalo limesemwa na kila Mbunge; lakini la pili kama walivyosema baadhi ya Wabunge ni tatizo la uwezo wa matumizi ya pesa zenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Waziri alifanya ziara na alikuja Geita na yeye mwenyewe akawa anashangaa kuona maji hakuna, anashangaa kuona malalamiko ya maji yako nchi nzima lakini anasema ana takriban shilingi bilioni 50 kwenye akaunti na tatizo ni kwamba hakuna mtu analeta certificate kuonesha kwamba kuna kazi zinaendelea.

Kwa hiyo, ina maana tuna matatizo mawili, la kwanza inawezekana tuna tatizo la pesa ambalo ni dogo lakini tuna tatizo la uwezo wa kutumia pesa kutoka kwenye Wizara yenyewe na pengine inawezekana ni uwezo wa watu walioko chini kwenye Wizara wanaoweza kusababisha pesa zitumike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kuimarisha sana uwezo wa watu wake huku chini. Kuna lugha mbili zinazungumzwa hapa, Mheshimiwa Waziri anasema msiangalie sana ring fence ya bajeti yenu kwenye Halmashauri, anzisheni miradi, tengenezeni certificate mlete tulipe, lakini walioko kule chini wanaangalia kile ambacho wamepewa na Serikali ndiyo wanatangaza na pengine hawatangazi mpaka waambiwe pesa zipo. Kwa hiyo, inawezekana kuna tatizo la mawasiliano kati ya ofisi ya Mheshimiwa Waziri na watu wake ndiyo maana malalamiko ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali, kwa miaka yote miwili mfululizo tumekuwa na tatizo kubwa sana la maji katika Mji wa Geita. Katika taarifa yake ukurasa wa 53 amekadiria kwamba hivi sasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Geita ni kama takribani asilimia 37. Inawezekana takwimu hizi Waziri ameletewa lakini siyo kweli, Geita takwimu hizi ambazo nazipinga upatikanaji wa maji uko chini ya asilimia 15 na sababu ni kwamba maji yaliyoko Geita ambayo yanasukumwa na mgodi wa GGM, makubaliano ya uanzishwaji wa mradi ule ilikuwa Serikali ichangie asilimia 50 na mgodi asilimia 50, mgodi ukatumia shilingi bilioni 12; lakini Serikali ikatoa shilingi 400,000 peke yake. Kwa hiyo, matokeo yake ule mradi umekamilika lakini uwezo wake wa kufanya kazi unafikia kaya 1,700 peke yake. Mara nyingi Mji wa Geita hauna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hivi karibuni GGM wamesema wanajiondoa kwenye uendeshaji wa mradi ule na sasa hivi GEUWASA walikuwa wanakusanya mapato bila kuingia gharama ya kupeleka umeme wala kusukuma umeme kutoka kwenye chanzo cha maji. Maana yake ni kwamba muda mfupi ujao GGM wakijiondoa, GEUWASA wanatakiwa waanze kujilipia mwenyewe gharama ya uendeshaji na mradi ule uko category C.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya namna gani tunamaliza tatizo la maji katika Mji wa Geita. GGM watakapoacha kusukuma maji kwa sababu wanasema gharama ni kubwa na walikuwa wanatumia pesa za CSR ambazo Serikali kupitia sheria tuliyorekebisha hapa Bungeni tumewanyang’anya sasa tumezipeleka halmashauri, kwa hiyo, hawana tena uwezo wa kutumia zile pesa na wao hawana fungu lingine kwa maelezo yao na kwa mwezi mmoja wanatumia milioni 70 maana yake ni kwamba GEUWASA hawana uwezo tena wa kusukuma maji, hata hii asilimia 15 tunayoipata sasa hivi haitakuwepo. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje na majibu ni namna gani ataondoa tatizo hili kwa sababu tumesubiri pesa za India leo mwaka wa tatu hazionekani na muda unakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi pale wa LV- WATSAN na kwa nini nimesema tunalo tatizo la matumizi ya pesa na usimamizi, huu mradi una pesa tayari shilingi bilioni sita, Waziri ametaja kwenye taarifa yake lakini mradi ambao ungekabidhiwa mwezi Novemba, 2016; leo Mei, 2018 mradi huu haujakamilika na mkandarasi hayuko site, maana yake ni nini? Amesema mradi huu utakabidhiwa Mei, namhakikishia Mheshimiwa Waziri sio kweli kwa sababu sisi tunatoka kule site tangu alivyoondoka matenki na mabomba yako vilevile na mkandarasi haonekani na kama anaonekana atakuwa anafanya kazi nje ya mkataba kwa sababu alishasimamishwa na Wizara na watu wanaomsimamia. Sasa kama pesa zilikuwepo shilingi bilioni sita na hakuna tatizo la pesa hapa lakini mradi hauendi leo mwaka wa tatu maana yake ni kwamba liko tatizo pia la uwezo wa kumsimamia huyu mkandarasi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri pengine leo atakuja na majibu sahihi kwamba huu mradi wa LV-WATSAN utakamilika lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunashangaa kuona tunapokuja na bajeti ya visima, sisi tuko kilometa nane tu kutoka ziwani. Watu wa Shinyanga, Tabora na sehemu nyingine wangezungumzia visima nisingeshangaa, sisi tunataka maji ya ziwa. Pale kama Serikali itawekeza maji kutoka ziwani ukapandisha kwenye ule mlima ulioko pale Geita, maji yatashuka yenyewe kwa gravity kwenda mpaka Kahama, kwa nini tunahangaika na visima katikati ya Mji wa Geita ambavyo kiangazi vyote vinakauka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini moja ya miji inayokuwa haraka sana kutokana na shughuli za madini na mwingiliano wa watu ni Mji wa Geita. Nimeona humu kwenye ripoti ya Waziri wamekadiria wanapeleka maji kwa watu 130,000, sisi Geita pale tunaamini kuna zaidi ya watu 300,000 sasa hivi na tunahitaji maji mengi sana ili tuweze kuendelea na shughuli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii ametupatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji. Mwaka jana walitupatia tena shilingi bilioni mbili ambazo zilitupa kama kilometa 80 za mtandao wa maji. Tatizo kubwa tulilonalo ni maji machache ambayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampeni ya kuchoma kambi, kuvunjwa mitumbwi na kuchoma nyasi, haiwezi kuandoa uvuvi haramu kwa sababu mwisho wa siku itatengeneza maskini wengi ambao maisha yao yote ni uvuvi na watavua kwa sumu au njia mbaya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampeni ya kukata nyavu kutoka double triple kuwa single, haijafanyiwa utafiti, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika vina vyake haviko sawa. Ukiwafanya wavuvi wote kutega single watavua kwenye mazalia ya samaki na iwapo itakuwa hivyo zoezi lote hili ni kupoteza muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyavu ya single; iwapo itatumika maji marefu ile ya nchi 7", 8", 10" inaweza kukamata samaki wa robo kilo, kilo moja mpaka kilo 100. Utaratibu wa kupiga watu faini ovyo ni sawa na kuwaagiza wavuvi kutupa samaki kwenye maji kwa sababu samaki akinasa hufa pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyavu ya single; haiwezi kuvua maji marefu kwa sababu nyavu ina kina cha mita nne wakati ziwa lina kina cha mita 84.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu faini, zitumike sheria za uvuvi siyo sheria za mazingira kupambana na wavuvi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika. Nashukuru kwa mgao wa magari ya ambulance, mgao wa Madaktari Bingwa na watumishi. Pamoja na pongezi hizi, naomba kutoa ushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu ya cancer - Bugando; zipo taarifa kwamba zaidi ya asilimia 30 ya wagonjwa wa cancer - Ocean Road wanatoka Kanda ya Ziwa. Kutokana na takwimu hizo ni vyema Serikali ikaongeza bajeti ya vifaatiba kwa hospitali hii ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaotoka Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam jambo ambalo litapunguza gharama na usumbufu lakini pia litasaidia kupunguza gharama kubwa kwa mgonjwa inayotolewa hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Geita; kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita. Hivi sasa wananchi wa Mji wa Geita wanapata taabu sana kwa kukosa hospitali ya level ya Halmashauri ya Wilaya kwa kuwa hospitali yetu ya Wilaya/Mji ndiyo Hospitali ya Mkoa kwa sasa.

Naiomba Serikali kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Mkoa ambayo ipo Mjini Geita na inasuasua kutokana na uhaba wa fedha. Naitaka Wizara kutofautisha inapozungumza kuhusu Hospitali ya Mkoa inamaanisha hospitali ipi kati ya Hospitali ya Geita Mjini na Hospitali ya Chato. Ni vizuri kutofautisha ili kutoa uelewa mpana wa wananchi kufahamu ni kipi kipaumbele cha Wizara kati ya hizi hospitali mbili za Mkoa ndani ya Mkoa mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa watumishi; kwa muda mrefu Hospitali ya Mkoa wa Geita inaendelea kutokuwa na Madaktari Bingwa, hadi leo kuna Daktari Bingwa mmoja tu ambae ni surgeon, wale ambao Wizara iliwapeleka wote hawajafika. Pia kuna upungufu mkubwa wa manesi, wataalam wa kada za maabara, usingizi na madaktari wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana TFDA kwa kuendelea kusimamia viwango vya chakula kwa Watanzania. TFDA wanatoza ada kwenye kila leseni ya bar, grocery na migahawa ya shilingi 100,000 kwa mwaka. Ada hii ambayo ambayo ni sharti ya mfanyabiashara kupata leseni katika Halmashauri zetu, kwa ujumla hakuna kazi ambayo TFDA wanafanya kwenye bar kwa kuwa vinywaji vyote vinavyouzwa bar au grocery ni vya kununua na havitengenezwi na muuzaji. Hata kama lengo ni mamlaka hii kukusanya fedha ili iweze kujiendesha, busara ingetumika angalau shilingi 20,000 kwa hoteli kubwa zenye bar na shilingi 10,000 kwa grocery au bar za mitaani kwa kuwa ada hizi zinaongeza gharama kwa wananchi bila sababu yoyote.

Naiomba Serikali ifahamu pamoja na ada ya TFDA kuna ada ya leseni, ushuru, TRA, michango ya mwenge, majengo, ukaguzi wa watu wa afya, usafi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fedha za madeni ya watumishi; Jimbo langu kuna watumishi wengi Hospitali ya Mkoa ambao zamani walikuwa DC wana madeni makubwa na ya muda mrefu. Naiomba Wizara kulipa madeni yote kwa kuwa yameleta usumbufu mkubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kutoka Geita (Nyankungu) kwenda Kahama, barabara hii ambayo inapita Nyang’hwale kwenda Kahama ni kiungo kikubwa kwa Mkoa wa Geita na Shinyanga, na hii sasa inatumika sana kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika mgodini. Tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami kama ahadi ya Mheshimiwa Rais ilivyokuwa mwaka 2015. Hivi sasa barabara hii ni mbovu sana kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Uwanja wa Ndege Geita Mjini, Mheshimiwa Waziri kumekuwepo maneno mengi kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato. Sisi wananchi wa Geita hatuoni tatizo la ujenzi wa uwanja wa Chato. Tatizo tulilonalo ni umbali wa huduma hiyo kutoka Geita Mjini kwenda Chato, ndio utakuwa uwanja wa watu wa Geita Mjini; maana yake mtu atatakwa kusafiri kilometa 184 kutoka Geita kwenda Chato au kusafiri kilometa 120 kutoka Geita kwenda Mwanza Mjini na kwa sababu hiyo tatizo na uhitaji wa Uwanja wa Ndege Geita Mjini lipo pale pale. Ushauri wangu ni kwamba uwanja wa CCM uliopo hivi sasa ukarabatiwe na kuwa na uwezo wa kutumika kwa shughuli zote abiria wa Geita na CCM na kinachoweza kufanyika ni kutofautisha jengo la abiria peke yake hakuna sababu ya kuanza ujenzi wa eneo jipya.

Kuhusu barabara za Mjini Geita, Mheshimiwa Waziri tulipewa ahadi ya kilometa 10, ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni yake mwaka 2015. Kwa kuwa muda uliobaki, sasa ni miaka miwili tu naiomba Serikali kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuwa hali ya barabara za Mji wa Geita ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Geita ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubovu wa vivuko vya Kigongo Busisi, Mheshimiwa Waziri vivuko hivi vimechoka sana na vimekuwa vikisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa kivuko, zipo nyakati feri inabaki moja tu magari na abiria wanakaa hapo zaidi ya masaa 10 kusubilia feri. Naiomba Serikali kuja na suluhisho lingine la mahali hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya michezo. Serikali ije na mkakati kabambe wa kupatikana viwanja vya Serikali vya michezo. Mfano katika Mkoa mpya wa Geita, Mkoa mzima hakuna viwanja vya football, basketball, netball na hata riadha. Pia nataka kufahamu mkakati wa Wizara kuhusu bima ya wanamichezo wote kwa kuwa hivi sasa mchezaji anapopata tatizo dogo la kiafya maisha yake yanakuwa ya kuombaomba. Kwa nini Wizara isipitie upya sera yake ili kuwafanya wanamichezo wote kuwa na hifadhi maalum ya fedha na bima kwa afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina mbalimbali za michezo. Limekuwepo tatizo la Watanzania kuwekeza zaidi katika mpira wa miguu na kidogo ngumi ili kuongeza wigo au chaguo la aina ya michezo. Mfano shule ziache kuweka sharti la uwanja wa mpira wa miguu kama ishara ya kuwepo kwa michezo, ikiwezekana michezo kama kuogelea, ngumi, basketball, volleyball, table tennis na squash na mingine mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tushirikiane na Wizara ya Elimu kuratibu wamiliki wa shule kutoa proposal ya aina ya michezo ambayo shule itau-promote kwa nguvu zake zote kwa kuweka miundombinu yake badala ya kuweka mkazo kwenye masharti ambayo yamebaki kuwa mapambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vazi la Taifa, naishauri Serikali badala ya kulifanya vazi la Taifa kuwa moja kwa nchi nzima, vazi hili lianzie kwenye Wilaya, Mikoa na baadaye Taifa. Iwapo Wilaya kutakuwa na vazi lake na baadaye Mkoa mwisho wa siku Taifa litakuwa na vazi lenye kujumuisha Mikoa yote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nchi yetu bado inawahitaji wamiliki wa shule binafsi kama wadau wa elimu, ni vyema yafuatayo yakazamwa upya. Kodi nyingi zinazomwelemea mmiliki wa shule ambazo hatima yake ni kuwazidishia mzigo wazazi katika ada, ni vyema kodi nyingi hizi zikaondolewa kama ilivyo katika sekta ya afya. Serikali iendelee kudhibiti ubora wa elimu. Hoja ya shule binafsi kujitengenezea udhibiti isikubaliwe kwa kuwa imekuwa ikitumika vibaya kwa baadhi ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu wa walimu wa sayansi. Naiomba Serikali iendelee kutafuta suluhu ya upungufu wa walimu wa sayansi na naomba kuishauri Serikali kuruhusu wahitimu wa kada za sayansi za vyuo mfano, engineering na kadhalika ambao wapo mtaani kuajiriwa kama walimu kwa kuwa masomo yanafanana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Maji Kasamwa ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kasamwa kwa kuwa visima vyote huwa vinakauka wakati wa kiangazi. Hivi sasa Bwawa la Kasamwa limepasuka kutokana na mvua kubwa. Naomba Wizara
ifanye ukarabati mkubwa katika bwawa hili ambalo hivi sasa limepasuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hali ya maji Kasamwa, Mji wa Kasamwa una watu wanaokadiriwa kuwa 25,000 ambao wanategemea visima. Naiomba Serikali kupeleka maji ya bomba kutoka Geita Mjini kwa kuwa umbali uliopo kutoka Geita Buhalahala kwenda Kasamwa ni kama kilometa 10 umbali ambao ni mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya maji Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Bulela. Hizi ni kata ambazo ni sehemu ya Geita Mjini lakini hazimo katika hotuba ya Waziri na hali ya maji katika kata hizi ni mbaya sana. Naomba Serikali badala ya kufikiria kuchimba visima ni vyema kuweka mkakati wa kupeleka maji ya ziwa ya bomba ambayo yapo ndani ya kilometa 30 tu kutoka makao makuu ya mji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukaguzi wa TBS, NEMC, TFDA; Serikali kupitia mamlaka mbalimbali imekuwa ikifanya ukaguzi wa maeneo ya viwanda, bidhaa za viwanda na kutoa vibali au kuteketeza mali za wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la mamlaka hizi ni rushwa, urasimu na kutumia standards za Ulaya kwa kuwafanya Watanzania wengi kukwama kuanza biashara, kuchelewa kuanza biashara na kufilisika kutokana na matumizi mabaya ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kama tunataka viwanda viongezeke, nchi yetu lazima iondoe rushwa, urasimu na Europe Standards kwenye vigezo vya kufanya biashara au ubora wa bidhaa za Watanzania. Kwa sababu duniani kote kuna export quality na kuna internal consumption quality, lazima tuondoe masharti yanayokwamisha kuanza biashara na kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutumia TIC imekuwa ikihamasisha wawekezaji kutoka nje kuwekeza Tanzania. Wawekezaji wengi wanaokuja na mitaji yao na kununua ardhi na kumiliki kwa asilimia mia moja; nchi kabla ya kuingia kwenye mkakati huu wa viwanda haikuandaa sera itakayolinda wazawa na kuzuia utoroshaji wa faida zote kwenda nje. Mfano, viwanda vyote vikimilikiwa na wageni, maana yake faida yote ya uwekezaji mkubwa itakwenda kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kwamba tulitakiwa kuwa na sera ya kulinda maslahi ya nchi ili kuepuka matatizo tunayopata sasa kwenye uwekezaji mkubwa wa madini kumilikiwa na wageni watupu na kuruhusu wizi mkubwa, udanganyifu mkubwa kupitia transfer pricing na cheating kwenye contracts?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kutazama upya Sera ya Uwekezaji kwenye viwanda ili kuruhusu mgeni kuuza sehemu ya haki zake kwa wazawa, suala ambalo litasaidia kupunguza profit export kurudi kwao na kuiacha Tanzania maskini.
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia. Naomba niwashukuru wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia, lakini pia niwashukuru kwa sababu asilimia kubwa ya wachangiaji wameunga mkono hoja na sisi ambao tumeleta hoja hii tumefarijika kuona kumbe ulikuwa ni mtazamo wa kila mtu kuona umuhimu wa hifadhi hii kuwa National Park.

Mheshimiwa Spika, kama alivyomalizia kusema Mheshimiwa Angelina Mabula, watu wengi ambao hawajawahi kufika BBK hawaifahamu vizuri. Ukiwa BBK upande ambao tunapakana na nchi jirani kuna vijiji vinakwenda mpaka kwenye mto, mpaka wetu ni mto, lakini ukivuka mto peke yake unaingia kwenye BBK hizi ambazo tunazungumzia hii Kimisi, Burigi pamoja na Biharamulo. Maana yake ni kwamba, upande wa pili palikuwa na watu ambao wana access ya moja kwa moja na game reserve, lakini upande wetu huu kwa sababu, mpaka ni mrefu na kwa sababu ya uwezo ambao TAWA walikuwa nao tulikuwa tunshindwa kwa kweli kimsingi kusimamia ulinzi vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa tunafarijika kuona kwamba, baada ya kuwapatia TANAPA na kama walivyosema Wajumbe wengi ni kwamba, TANAPA kimsingi wanazo financial muscles ambazo zitatusaidia sana kwenye kuimarisha ulinzi. Katika kuhakikisha kwamba, hili linaungwa mkono na kauli hii, baada tu ya sisi kuonesha kwamba, tunataka kuichukua hii kuwa TANAPA, tayari TANAPA wamekwishatengeneza kilometa 121 za barabara, wamekwishapeleka magari matano kwa ajili ya kuimarisha doria, wamenunua maboti mawili kwa ajili ya usimamizi kwenye Ziwa Burigi na Ziwa Ngoma. Pia lakini tayari wametambua maeneo nyeti ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na wameongeza idadi ya wafanyakazi katika eneo hili na kupeleka wafanyakazi 70. Kwa hiyo, utaona utayari wa TANAPA katika kuhudumia eneo hili ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ushirikishwaji; tangu tulipokuja na wazo hili tumezitumia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya, lakini Viongozi wa Vijiji wa maeneo husika. Wote hawa wametumika katika kutoa elimu na kuwaeleza faida ambazo zitapatikana kutokana na eneo hili kuwa hifadhi ya Taifa. Hata hivyo, elimu itaendelea kutolewa kwa sababu, elimu ni suala la kudumu. Naamini kwamba, wananchi wa maeneo haya wamejiandaa vizuri zaidi kupokea eneo hili kuchukuliwa na TANAPA kwa sababu za historia ya TANAPA yenyewe namna inavyofanya kazi, lakini faida ambayo wanaipata.

Mheshimiwa Spika, tunategemea watapata faida gani; la kwanza, tunaamini kwamba, eneo lile likishafanyika uwekezaji wa kutosha, ukiacha suala la usalama lipo suala la biashara. Maeneo yale yatachangamka sana kibiashara, kutajengwa hoteli za ndani na nje ya eneo hilo ambazo zitafanya mzunguko wa pesa katika eneo hilo kuwa mkubwa, lakini tutaimarisha zaidi cultural tourism. Maeneo mengi sana ukiwa unatoea Arusha ukija kufika Serengeti wananchi wa maeneo yale wanaona umuhimu wa uwepo wa Ngorongoro na Serengeti kwa sababu, wakati watalii wanaelekea kwenye kutalii Serengeti na Ngorongoro wanapita kwenye maeneo ya wananchi na kuona namna ambavyo wananchi wanashiriki kwenye utalii. Vile vile, tunaamini kwamba, usimamizi mzuri wa mazingira utaimarika ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Msigwa ameonesha dalili ya kwamba, nikitafsiri vizuri lugha yake ni kama anaona kunafanyika upendeleo kupeleka TANAPA sasa hivi BBK na kuacha REGROW, Mheshimiwa Waziri wangu atazungumzia vizuri kuhusu REGROW, Lakini nataka nimtoe wasiwasi kwamba, nchi hii ni moja, mtazamo ambao Serikali inao kuhusu Kusini ni mtazamo uleule ambao inao kuhusu Kaskazini,
kuhusu Magharibi na sehemu nyingine zote na kwamba, haya hayafanyiki ili kuondoa umuhimu wa eneo la Southern Circuit.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya nishati ya mkaa na kuni kwa taasisi, nimesoma ushauri wa Waziri kwa taasisi kutumia nishati mbadala. Ushauri huu hauonekani kuwa ni msisitizo wa kuokoa misitu. Naishauri Serikali kuleta sheria ambayo itazilazimisha taasisi kuweka mkakati wa matumizi ya gesi badala ya kuni au mkaa. Pamoja na sheria hiyo Serikali itoe punguzo la kodi maalum kwa vifaa vya gesi yenyewe kwa taasisi zilizo tayari ambazo zitatambuliwa. Jambo hili iwapo litafanyika litasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Spika, suala la mipaka mipya ya hifadhi, naunga mkono maoni ya Kamati juu ya kuondoa kabisa mipaka mipya ya mbuga na hifadhi kwenye vijiji na nchi nzima kwa ujumla. Mipaka hii imeleta tafrani kubwa na imekiuka kabisa mipaka ya asili iliyowekwa kwa mujibu wa GN na sheria za nchi hii. Mipaka mipya isimame mpaka ushirikishwaji utakapofanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kesi za mifugo inayokamatwa, baadhi ya mifugo imekuwa ikikamatwa ndani ya hifadhi au mbuga za wanyama na Serikali kuzishikilia kwa muda mrefu. Kwa kuwa askari wa wanyamapori hawana utaalam wa mifugo, mifugo mingi huwa inakufa na Serikali na wananchi kupata hasara kubwa. Kwa mfano mwaka 2014/2015 huko Ngara Tanzania mifugo (ng’ombe) 887 ilikamatwa ndani ya hifadhi, mifugo 700 ilikufa kabla ya maamuzi ya Mahakama na hata waliobaki walikosa bei ya soko kwani walikuwa wamekonda sana.

Naishauri Serikali kubadilisha utaratibu wa kushikilia mifugo, badala yake iachwe kwa mtuhumiwa kwa uangalizi maalum mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja na niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa maoni na ushauri kwa hoja ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye wasilisho lake mapori yetu yote Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba kinachotofautiana ni matumizi ya maeneo lakini yote yanasimamiwa na yanalindwa na yana ulinzi wa kutosha. Tunapopandisha hadhi pori la akiba la Selous na kuliita Nyerere National Park kinachobadilika pale ni matumizi tu ya eneo hilo, kwamba sasa tunakwenda kufanya zaidi utalii wa picha badala ya utalii wa awali ambao ulikuwa unaruhusu utalii wa picha na uwindaji, lakini matumizi mengine yote na namna ambavyo yanasimamiwa na ulinzi yanafanana. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge ambao wameonesha kana kwamba kubadilika kwa hadhi sasa Wizara iende kuanza upya kufikiri namna ya kuhifadhi eneo hilo lakini na kuondoa wafugaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wote ambao tumewaona kwenye maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba ni wavamizi na wamekuwa katika maeneo hayo kinyume cha sheria, kwa hiyo wawe ndani ya National Park au wawe ndani ya Game Reserve hawa wako kinyume cha sheria na wanashughulikiwa na sheria ile ya Uhifadhi ambao hawatakiwi kuwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, nijibu tu maeneo mawili matatu ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema na Kamati, moja ni la kushirikisha wadau, wadau wameshirikishwa na mchakato huu tangu Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo pale wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bwawa la umeme wadau mbalimbali wameshirikishwa wakiwemo hao wenye mahoteli lakini pia wakiwemo wadau wanaofanya biashara za utalii na wananchi wa Mikoa ya jirani ya maeneo hayo. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi kwamba suala hili halijakimbizwa kwa haraka, hakuna mdau ambaye hakusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, katika wadau wakubwa ambao walikuwa katika maeneo yale, hasa ambao wanaathirika na ujenzi wa bwawa, Wizara kupitia Serikali wapo ambao wameguswa na wamepata fidia na wamepewa maeneo mengine ya kwenda kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo limeonekana lina shida kidogo ni kwamba eneo la hifadhi hii ni kubwa sana na kwa sababu hiyo yako maeneo ambayo hayatatumika kwa leo kwa faida, ni kweli kilometa za mraba elfu 30 ni nyingi na huwezi kuziendeleza na kuzitumia kwa mara moja. Kama mnavyofahamu tumekuwa na traditional product mbili sana Tanzania ni mbili tu ya kwanza ni Safari ambayo ni ya kupiga picha, na nyingine ni ya kupanda Mlima Kilimanjaro sasa maeneo haya ambayo yalikuwa yanatumika zaidi kwa uwindaji ni maeneo ambayo terrain yake hairuhusu utalii wa picha na wakati mwingine utalii wa safari tuliouzoea, lakini huu ni muda muafaka wa ku-develop aina nyingine ya product kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tu nitoe mfano, ukienda leo Serengeti utakutana na balloons nyingi zipo mle ndani ambapo wawekezaji kadhaa wameingiza balloons ambazo zinaweza kutoa watu sehemu moja kwenda sehemu nyingine lakini pia tunafikiria hii milima mingi iliyomo katika pori la akiba la Selous tunaweza ku-introduce cable cars pamoja na maboti yanayopita kwenye maeneo ambayo sisi tunaona kwamba hayapitiki lakini kuna hiking na michezo mingi ambayo inatumika kwenye maeneo ambayo hayatumiki kwa utalii wa picha. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tutakapolichukua litabaki bila matumizi.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, imezungumzwa hapa kuhusu vivutio vingi vya utalii vilivyopo mikoa ya kusini. Ni kweli kwamba mchakato huu unakwenda kufungua Mikoa ya Lindi na Mtwara na tunakwenda kufungua ukanda wote wa mashariki (ukanda wa bahari) na kwa sasa hivi baada ya mchakato huu kukamilika, kwanza nilitaka nitoe taarifa kwamba maeneo yale ya Mikindani na Kilwa yote haya mwanzo yalikuwa hayajiendeshi vizuri kwenye shughuli za utalii lakini Wizara ilikaa na kufikiri na kuona kwamba ili yaweze kuwa sehemu ya package ya watalii wanaotembelea maeneo haya na kwa juhudi za sasa za kupandisha hadhi eneo hili kuwa hifadhi ya Taifa ambazo zitaongeza miundombinu na kufungua maeneo haya yote, tuliyaunganisha pamoja na taasisi zetu zote kama TAWA.

Mheshimiwa Spika, na juzi nilikwenda Mafia nimekuta TAWA wapo pale wanaimarisha miundombinu lakini Mikindani pale wapo na hata maeneo yote ambayo ameyasema Mheshimiwa Hawa Ghasia ni maeneo ambayo tayari tumeyaweka kwenye mpango kazi wa kuyafungua.

Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba hata huu mradi wa REGROW ambao sasa ulikuwa sehemu ya juu ya Selous, awamu hii ya kwanza ya mradi huu wakati inaendelea kutekelezwa, Wizara imo katika mchakato kabambe wa Awamu ya II ya REGROW ambao sasa utaenda kuunganisha mikoa hii miwili ya huku chini na kuifungua kabisa na kuifanya iwe ni mikoa muhimu kwa ajili ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunatambua vivutio vingi vipo maeneo hayo, tunaamini kwamba tutakapoimarisha miundombinu na utangazaji wa maeneo hayo na tutakapokamilisha sasa uwekezaji, tutahamasisha biashara ya utalii ambayo imekuwa ni kivutio na chanzo kikubwa cha mapato kwa mikoa ya kaskazini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nitumie nafasi hii ingawa Mheshimiwa Mwambe amesema tusipongeze lakini niipongeze sana Serikali yangu kwa kuendelea kutekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ili uvuke uende Geita lazima upite Busisi na juzi tumeona uzinduzi wa kivuko kipya ambacho kitakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuchukua abiria wengi na magari na ni njia hiyo pekee ambayo kwa kutokea Mwanza naweza kufika Jimboni. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kutimiza ahadi yake hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali walikuwa wanafanya feasibility study nadhani kwa ajili ya kujenga daraja kwenye eneo lile ambalo litapunguza sana vifo visivyo vya lazima ambavyo vinatokea wakati unasubiri ferry kwenda Bugando kwa sababu ndiyo hospitali pekee ya rufaa, kama upembuzi yakinifu ule umekamilika basi nimwombe sana Waziri wa Fedha kwamba wananchi wa Kanda ya Ziwa hasa wananchi wa Geita na Mikoa mingine wanasubiri kwa hamu kuona ujenzi wa daraja lile unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri juzi amesema ameondoa kodi ya VAT kwenye taulo za kike, nampongeza sana kwa sababu ilikuwa ni ombi la kwetu wenyewe Wabunge. Wasiwasi wangu tu nataka aje anisaidie punguzo hili la VAT wamefanya utafiti litapunguza bei kwa kiwango gani kwa watumiaji. Nafahamu kwamba hizi exemptions mara nyingi mwisho wa siku zinawafaidisha zaidi wafanyabiashara na siyo watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Kamati kwenye suala la maji, mwaka jana na mwaka juzi tulipendekeza kwamba iongezeke Sh.50 ili tutunishe Mfuko huu wa Maji na hatimaye tuongeze uwezo wa Serikali kwenye kuhudumia miradi ya maji. Kwa hiyo, nimwombe mwaka ule alikataa lakini mwaka huu na dalili ilivyo na kwa sababu tumemaliza mwaka mmoja na nusu kwenda kwenye uchaguzi nadhani sasa anafahamu kwamba bila kufanya hivyo suala hilo litakuwa gumu sana kutekeleza na kwa sababu ni Ilani yetu wenyewe ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala lenyewe la hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Hapa karibuni baadhi ya wachangiaji wameonesha sana wasiwasi wa kwamba bajeti yetu Tanzania ni ndogo kulingana na nchi ya jirani kwa mfano Kenya ambao bajeti yao ni dola bilioni 30 na nimeona Uganda wenyewe wana kama dola bilioni 8.5 lakini imeongezeka kwa asilimia 15, Tanzania imeongezeka kwa asilimia mbili. Nadhani sababu ya Waziri kutokuongeza bajeti kama alivyokuwa anafanya miaka ya nyuma ni kutokana na tax base yetu kuwa ndogo na tax base yetu imekuwa ndogo siyo kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba Waziri wa Biashara anahangaika sana kuvutia wawekezaji waje, lengo lake ni kuongeza tax base ili Waziri Mpango aweze kukusanya kodi. Waziri wa Madini anahangaika kutengeneza sheria ili kuwarasimisha wachimbaji wadogo wadogo lakini kuhakikisha kwamba migodi yote inaweza sasa kulipa kodi ili kuongeza tax base.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu sana kama Serikali inakwenda kwa kufikiri pamoja. Wakati Wizara hii inahangaika sana kuboresha tax base unashangaa kuona Wizara nyingine inatumia sheria na kanuni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ambao wapo wanaendelea kulipa kodi wanafilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mfano kwenye uvuvi, nimeangalia hapa kwenye taarifa ya Kamati, uvuvi umetengewa 0.06. Hivi ninavyozungumza tumepata taarifa hapa kutoka kwa Mheshimiwa anayeshughulika na uvuvi na mifugo kwamba amekusanya takribani bilioni nane kwenye faini na kodi mbalimbali kwa wavuvi haramu, lakini anasema amekuja kugundua asilimia 98 ya wavuvi wote Tanzania ni wavuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba ameondoa walipa kodi asilimia 98 kwenye mfumo wa kulipa kodi ambao Mheshimiwa Dkt. Mpango alikuwa anakusanya kodi wote ni wavuvi haramu, amewaondoa kwenye mfumo bila kuja na mpango wowote wa kuhakikisha kwamba hiyo tax base anairudishia. Madhara yake ni kwamba tunaotoka kwenye maeneo ya uvuvi kabla ya Watanzania wengi kuingia ziwani kuvua samaki, wavuvi pekee walikuwa ni wale wenye viwanda na wenye viwanda walipewa kazi na Serikali ya kuwawezesha Watanzania kununua nyavu hizi ambazo ziliruhusiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waletaji wa nyavu wakalipa kodi, wakawakopesha Watanzania na wale Watanzania wakanunua wakaweka dhamana nyumba zao, nyavu ambazo zote ni haramu, zimekamatwa zote zimechomwa moto. Hawa wenye viwanda ambao leo hawawezi kuwakopesha tena Watanzania waliokuwa wanavua samaki na wale wote waliokuwa wanavua samaki hawana mitaji, maana yake ni kwamba hatuwezi tena kukusanya kodi lakini tumeua hiyo industry ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sishangai ninapomwona Waziri anaposema samaki wamekuwa wengi ziwani, ni kwa sababu anasahau there is no more industrial fishing tena kwa sababu asilimia 98 ya wavuvi waliokuwa mle ziwani ni wavuvi haramu kwa tafsiri yake, kwa nyavu alizopokea na alizoziruhusu yeye kuingia ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, tunalalamika kwamba bajeti yetu ni ndogo lakini ukiangalia system nzima haifanyi kazi pamoja. Nilitarajia kwa kuwa kanuni hizi ni za Waziri na kanuni zinazomwongoza kufanya kazi hii amezitunga yeye, Sheria ya Uvuvi iko vizuri sana. Kwa kuwa nyavu hizi zililipiwa kodi na kwa kuwa tunahitaji industry ya uvuvi iendelee kuwepo ili tupate kodi, nimeangalia kwenye kwenye kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango makusanyo yote haya kwa miezi minne sasa ukienda Mwanza hayapo, angefanya mpango maalum wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na transition period kabla ya kuanza kuchukua hatua ambazo zinaondoa walipa kodi, karibu asilimia 30 ya walipa kodi wa Kanda ya Ziwa ni Wavuvi wote wanaondoka kwenye mfumo na wakirudi kukopa wataanza kulipa interest na interest ina gharama kwenye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tunapotengeneza tax base, ukiangalia sasa hivi mwaka huu tumeshindwa kuongeza kwenye projection yetu ni kwa sababu tax base yetu ni ndogo. Tulikurupuka miaka fulani tukawa tunaongeza kila mwaka matokeo yake hatujawahi kukusanya kwa asilimia 100. Sasa kama tunatengeneza tax base leo kesho tunaibomoa, unaitengeneza kesho, kesho unaibomoa maana yake ni kwamba tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona juzi kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi amegundua kwamba operesheni ili iweze kufanikiwa sasa ni lazima twende kwa walaji na walaji ni kwenye hoteli na anatumia regulations hizo ambazo ni za uvuvi. Tatizo kubwa ambalo naliona, mimi nadhani Watanzania wengi hawajui kwamba source ya samaki siyo Ziwa Victoria peke yake, regulation iliyopo inazungumzia samaki wa Ziwa Victoria, sato na sangara lakini kuna watu wanafuga samaki, ambao hawafugi kwa masharti kwamba ili awavune lazima wafikie sentimita ambazo yeye anazitaka. Cost yake ya ku-run lile bwawa huwezi kusubiri mpaka samaki akae miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wa Mtera na Nyumba ya Mungu hawafanani na sato walioko Ziwa Victoria. Kwa nini Waziri akili yake anafikiri tu kwamba lazima hawa watakuwa ni kutoka Ziwa Victoria halafu ukikutana na sato species 50, Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa ni kwamba unaweza ukaletewa sampuli ya sato 10 lakini wale sato 10 ni species tofauti, hawafanani na kadri wanavyotofautiana hawakui kwa kufanana. Kwa nini Waziri anakimbilia kwenda… kwa sababu kadri unavyochukua hatua una- demoralize watu wote wanaoshughulika na ile biashara una erode tax base. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kurudi tena kwenye Bunge lako Tukufu. Nakishukuru sana chama change, Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na baadaye kushinda uchanguzi Jimbo la Geita Mjini. Naomba kuwaahidi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini kwamba nitaendelea kuwa mwakilishi mwaminifu sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kufungua Bunge ukurasa wa 41 alizungumzia madini na alisema sekta ya madini imekua kutoka mchango wake katika malipo ya pato la Taifa wa shilingi bilioni 168 mpaka 527 lakini katika pato la Taifa kutoka asilimia 3.4 mpaka 5.2. Naungana na Mheshimiwa Rais kuwapongeza sana Wizara ya Madini wanafanya kazi vizuri. Mimi ambaye natoka jimbo ambalo uchumi wake kwa asilimia zaidi ya 80 unategemea sana pato la madini, naona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ambayo imeleta heshima katika matumizi ya fedha za CSR katika Halmashauri yangu ya Mji wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja tu hapa wachimbaji wadogo investment capital yao ni kubwa kuliko faida wanayoipata. Teknolojia wanayotumia na duni na bado mitaji ni midogo. Unakuta wachimbaji wadogo wanaendelea kubahatisha. Inaweza kutokea rush wataanza kuchimba mpaka wanafika mita 60 mpaka 100 hajaanza kufanya uzalishaji lakini tunazo teknolojia. Niiombe Wizara kama makampuni yanafanya CSR na yenyewe ifanye hivyo, ileta mitambo ya kutosha ili sehemu rush zinapotokea wawaambie wachimbaji kwamba eneo hili mnalochimba dhahabu zipo au madini yapo na yapo umbali gani na mlalo wa miamba. Namna tunavyokwenda sasa hivi utakuta ni kweli tunaongeza uzalishaji wa dhahabu lakini kimsingi gharama za uzalishaji wa dhahabu hizo ni kubwa kuliko faida ambayo wachambaji wadogo wanapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika eneo hilo, juzi Mheshimiwa Rais akiwa kule Mbogwe alisema kwamba siyo sahihi wachimbaji wakubwa wanapopata license kuamini kwamba sasa wamenunua haki ya wananchi ya ardhi na kukiuka sheria ambazo zipo. Wananchi wangu katika maeneo ya Nyakabale, Magema, Compound na Katoma wameendelea kuishi kwenye mgogoro wa takriban miaka
20. Ni kweli wako ndani ya leseni ya mgodi lakini mashamba yao ya asili sehemu ambayo mgodi haujataka kuanza kuchimba, hawaruhusiwi hata kwenda kukata kuni. Sasa hivi kuna ulinzi katika maeneo ya Magema hawaruhusiwi hata kupita nyumba moja kwenda nyumba nyingine kwa sababu ni ndani ya mgodi wa leseni. Nataka kushauri, Mheshimiwa Waziri alitolea maelekezo lakini Serikali ya Mkoa imeendelea kuweka askari pale, wananchi wameendelea kunyanyaswa tutoe mwongozo sahihi kama mgodi unataka eneo lile walipe fidia kama wananchi bado wanatakiwa kukaa pale wawaache wafanye kazi zao kwa uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo la pili kwenye ukurasa wa 27 sehemu ya kilimo. Ni kweli kwamba nchi hii inategemea ajira kwenye kilimo ambacho ni zaidi ya asilimia 80 na kimesaidia sana kudhibiti mfumuko wa bei na mimi nakubaliana na hilo. Nataka kutoa challenge kidogo hapa kwamba bado Watanzania wanalima very local na shida ya Watanzania siyo ukubwa wa mashamba. Mheshimiwa Rais anaweza kuendelea kuongeza mashamba, kubadilisha hifadhi, kubadilisha mapori ya akiba lakini shida hapa ni productivity kwenye maeneo waliyonayo wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado wakulima mtu analima heka kumi anapata gunia kumi za mahindi. Nataka kuwaambia Wizara ya Kilimo twenda sambamba na hotuba ya Mheshimiwa Rais, tulime kisasa na hili linaweza likaonekana kabisa kwa macho lakini tupate mbegu za kisasa na tupate huduma za ugani za kisasa. Utasikia tu kwenye magazeti na vitabu huduma zipo lakini kimsingi wakulima wetu bado wanalima kwa kizamani sana, productivity ya heka moja ni sawasawa na mtu aliyelima nyuma ya nyumba. Niiombe Wizara hii katika kipindi cha miaka mitano iweze kufanya jambo hili kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona kwamba kilimo cha kawaida hakitiliwi maanani sana wakati wa mavuno ya mazao ya biashara, maeneo yetu sisi tunalima pamba, store zote za pamba zimeoza, zimeanguka na zimegeuka kuwa nyumba za watu binafsi. Kwa hiyo, niombe Wizara iweze kujipanga vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tunalolipata kwenye kilimo liko pia kwenye mifugo. Utona kuna uboreshaji wa matumizi ya mashamba ya NARCO, lakini bado hata walio katika NARCO kinachowafanya waonekane wanafuga kisasa ni fensi, ukiingia kwenye shamba la NARCO utakuta hakuna mashamba ya nyasi, hakuna teknolojia unaotumika lakini bado ufugaji wa mle ni local, usambazaji wa mbegu za kisasa ni wa kizamani. Kwa hiyo, utakuta wafugaji hawa hata tunazungumza tuna ng’ombe milioni 33 hazijawasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana hasa katika kipindi hiki tunachokwenda nacho mabadiliko haya yaweze kutafsiriwa kwenye level ambayo wakulima na wafugaji wa kawaida wataondokana na kufuga ng’ombe 500 zenye kilo 250 waende wafuge ng’ombe 100 zenye tani moja ambazo zinaweza kuzalisha maziwa mengi lakini teknolojia iweze kusambazwa kwa njia ya urahisi. Tumeangalia maeneo mengi sana unakuta migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, kwa nini? Ni kwa sababu mkulima akipata eneo la kwenda kulima akinunua mifugo anahamia hapo na akihamia hapo anajenga, kesho yake anasogea mbele anapata eneo la kulima anahamia na anajenga kwa sababu anafuga ng’ombe nyingi ambazo anashindwa kuzimudu kulingana na eneo alilonalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara katika kipindi iweze kutumia muda wa kutosha kufanya mabadiliko ya kisayansi. Unayaona haya mabadiliko kwenye vitabu lakini wafugaji na wakulima tunaokaa nao sisi bado wanafuga kizamani na wanalima kizamani na hakuna mabadiliko yoyote ambayo yameendelea kuwepo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda la mwisho, nimeona juhudi kubwa za Wizara ya Nishati katika Mikoa ya Pwani, ikisambaza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Nilitamani kujua mkakati wa Serikali wa gesi hii kuifikisha kwenye mikoa ambayo iko nje ya Pwani, kwa mfano gesi hii itafika lini Mwanza au Geita ili tuweze kuachana na matumizi ya kuni na mkaa? Ziko taasisi zinatumia zaidi ya cubic mita 40 za kuni kwa mwezi, tunafanya nini kuzibadilisha taasisi hizi ziweze kutumia nishati ya gesi asilia tuliyonayo na kuweza kuzuia misitu yetu ambayo inaharibika kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kusema kwamba jana Mheshimiwa Gambo aliuliza swali ambalo lilikuwa linahusiana na tozo mbalimbali ambazo zimeongezwa kwenye Hifadhi zetu za Taifa. Nami nikataka kuongeza kidogo mawazo yangu hapo kwamba wakati COVID inaingia duniani, tuliwashauri watalii tukasema don’t cancel your trip to Tanzania, postpone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wako watu walikuwa wamelipa, fedha zao zilikuwa tayari kwenye account za wateja; na kwa kuwa wali-postpone wanatarajia siku watakapokuja watahudumiwa kwa gharama ile ile waliyolipia mwaka 2020. Sasa haya mabadiliko yaliyofanywa, nataka kuwaambia Wizara ya Maliasili na Utalii wafahamu kwamba mteja aliyelipia mwaka 2019 aka-postpone safari akitarajia kuja Tanzania kukamilisha safari yake anatarajia kuhudumiwa kwa gharama ile ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukumbusha hapa pia kwamba liko tatizo kubwa kwamba tunataka kufikia watalii milioni tano, jambo jema kabisa, lakini watalii hawa wanalipia muda na ukarimu. Ukarimu wanaolipia ni pamoja na consistency ya makubaliano mnayokubaliana tangu siku hiyo unam-convince kuja Tanzania mpaka siku anapopata huduma na kuondoka. Mabadiliko yoyote katikati baada ya kulipia yanafanya watalii wengi zaidi wasije kuliko waliokuja Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kuongeza jambo lingine moja. Sasa hivi requirement ya airline ni kwamba tunatakiwa tufanye COVID Test. Hii inafanyika nchi nzima lakini laboratory iko Dar es Salaam. Mtalii anahitaji siku tatu mpaka nne kwenda kufanya COVID Test Arusha kusubiri majibu na baadaye kupanda ndege kurudi kwao. Matumizi haya ya muda kwa watalii hayasaidii Tanzania kuongeza idadi ya watalii. Tufanye mabadiliko, tupeleke watumishi kule, tuchukue test tuwapelekee wataalam waweze ku-test. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, liko tatizo hapa linazungumzwa kuhusu tatizo la TRA. Nawapongeza sana kwa kukusanya fedha nyingi, lakini iko shida. Nimemsikiliza mtu mmoja wa TRA kwenye TV akiwa anahojiwa TBC, anasema sawa biashara zinafungwa, lakini zinafunguliwa nyingi zaidi. Tumesema kwa miaka mitano, kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hii kitu inaitwa Task Force. Tulifanya Mkutano na Mheshimiwa Kalemani pale Geita, tukaita wafanyabiashara wa Mkoa mzima wa Geita. Wanalalamikia TRA makadirio yao siyo rafiki. Kwa nini siyo rafiki? Inawezekana ni kwa sababu ya target kwamba ni kubwa kuliko survey ilivyofanyika ya uwezo wa walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna tatizo na Regional Manager wa TRA, wasaidizi wake huku chini, wanaweza kukukadiria shilingi milioni 400, mwisho mkaishia shilingi milioni 30. Maana yake ni nini? Kuna room hapa katikati ya negotiation na Serikali inapoteza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Task Force inafanya jambo moja. Wanakuja wanafanya special audit, wakishafanya wanakwambia unatakiwa kulipa shilingi bilioni tano. Wakati huyu mteja ana-appeal wanazuia account, wanachukua fedha zote kwenye account. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikuta kuna fedha kwenye account ya mfanyabiashara leo, kwa mfano, biashara ya utalii; fedha siyo zake, ni za wateja wanaosubiri huduma. Unapozizuia maana yake unamzuia asitoe huduma kwa huyo mtalii, unazuia asilipe mishahara, unazuia asiendelee kufanya kazi. Ushauri wangu kwenye jambo hili, unapofanya special audit, ukagundua huyu mtu anatakiwa kulipa shilingi bilioni tano, akakata rufaa, wewe kabla hujatoa majibu ya rufaa ya aliyekata rufaa, umeshazuia account, umemnyang’anya passport, umepeleka maaskari pale kuzuia biashara. Kodi haitafutwi hivyo. Huwezi kutafuta kodi wakati compliance tax payers duniani wanabembelezwa. Dunia nzima ukiwa na compliance tax payer unawapa stimuli wakati wa shida ili waweze ku-survive walipe kodi. Sisi tunachokifanya tunatumia nguvu nyingi ku-meet target, matokeo yake tunawafanya watu wengi wana-exit business, tunafikiri wanaongezeka, lakini watu wanapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri kwamba lazima tutafute namna bora ya kukusanya kodi, namna bora ya kuwalea wafanyabiashara tulionao. Leo na hapa getini wapo, wafanyabiashara walikuwa wanaingiza vitenge; analipa shilingi milioni 125, karudi ghafla anakuta container shilingi milioni 350, ameacha kulipa. Kesho yake atakachokifanya, akilipa anafunga duka, anatafuta machinga, anagawia watu barabarani. Akishindwa anahamia nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuisaidia Serikali kukusanya kodi, lazima Wizara ya Fedha watusikilize, tunazungumza na wananchi. Inawezekana hawana taarifa sahihi. Biashara zinakufa na watu wana…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga, lakini acha nikuruhusu. Unasemaje Mheshimiwa?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuongezee Mheshimiwa Kanyasu kuhusu wafanyabiashara wa Kariakoo. Kwa kweli hilo ni tatizo kubwa kwa sababu sasa hivi ma-container mengi sana ya vitenge yako bandarini inapata labda miezi minne au mitano wameshindwa kulipa kodi kutokana na hilo ongezeko kubwa sana la kodi. Kodi imefikia mpaka milioni 400 kwa container moja wakati siku za nyuma walikuwa wakilipa milioni 165 au 160. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanaweka zuio, wafanyabiashara tayari walikuwa wameshaweka order viwandani kule China. Mzigo unafika bandarini tayari kuna ongezeko la karibia shilingi milioni 200 na kidogo. Kwa hiyo, sasa mizigo hiyo iko bandarini mpaka sasa hivi hawajui wafanye nini. Kwa hiyo, mimi naiomba Serikali iangalie jinsi ya kuwapunguzia kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kabisa Taarifa hiyo. (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naomba kuzungumzia kuhusu bajeti ya own source asilimia 40 maendeleo badala ya asilimia 60 ya awali. Halmashauri ya Mji wa Geita ilitenga asilimia 60 ya mapato ya ndani (own source) kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hivi karibuni Wizara yako imetoa maelekezo kwa Halmashauri yangu ya Geita Mjini kubadilisha mipango kutoka asilimia 60 ya own source kwenye maendeleo kwenda asilimia 40 na hivyo kufanya matumizi ya kawaida kuwa makubwa kuliko miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri yangu haioni sababu ya kubadili mipango yote ya bajeti ya fedha ambazo sisi wenyewe tumekusanya kwenye vyanzo vyetu wenyewe na tumekaa, tumeona tuzielekeze kwenye miradi ya maendeleo ambayo ndiyo vipaumbele vyetu. Naomba kupata ufafanuzi kuhusu sababu ya Wizara hii kutoa mwongozo ambao unaondoa vipaumbele vya maendeleo kwa matumizi ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, lingine ni madeni ya wazabuni mbalimbali. Pamoja na jitihada kubwa ya Serikali kulipa madeni, bado Wizara ya Fedha imeshindwa kuwalipa wazabuni wanaoidai Serikali kama wazabuni wa shule, magereza na taasisi za umma. Wazabuni wa pembejeo wanadaiwa na benki. Naomba juhudi za Serikali kupitia upya madeni hayo zifanyike mapema na kuleta orodha ya wauzaji wenye tuhuma za kuwapeleka mahakamani na kuwashitaki ili vyombo vya haki viweze kuona ni nani anastahili na nani hastahili kulipwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu PRIDE kushindwa kulipa fedha za wateja na mishahara. Yapo malalamiko makubwa kuhusu PRIDE Tanzania. Ipo taarifa kwamba wafanyakazi wana miezi 18 bila kupata mishahara na wateja walioweka akiba ya fedha wamekosa huduma kwa kuwa fedha hakuna.

Mheshimiwa Spika, zipo taarifa kwamba management ya juu ya PRIDE imekimbia na zaidi ya shilingi bilioni 40 za fedha hii, kuna sehemu ni mali ya umma. Naitaka Wizara kutoa tamko kuhusu ukweli wa hali ilivyo PRIDE Tanzania na hatua zinazochukuliwa kulipa madeni ya wafanyakazi na wananchi walioweka akiba zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishaji vyeo Jeshi la Zimamoto; Askari walipandishwa vyeo baada ya mafunzo mwaka 2016 na walipewa barua za kupanda vyeo, lakini hawajabadilishiwa mshahara mpaka leo na badala yake kuna barua ya kufuta vyeo vilivyopanda. Naomba kujua lini Askari hawa watarejeshewa vyeo na mabadiliko ya mishahara yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Kituo cha Polisi Kati Geita; katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi ujenzi wa kituo hiki. Naomba kufahamu lini ujenzi huu wa kituo cha Polisi Kati Geita Mjini utaanza, ikiwa ni pamoja na jengo la zimamoto na magari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa magari, lipo tatizo kubwa la usafiri kwa Jeshi la Polisi Mkoani Geita. Mfano OCD Geita anategemea gari la FFU Kasamwa inapotokea ugeni wa viongozi hali za doria zimepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mlundikano wa mahabusu na ubovu wa Magereza; hali katika Gereza la Geita ni mbaya sana, idadi ya mahabusu ni wengi na hii imetokana na utaratibu mbaya wa kesi za kawaida ambazo zingeweza kumalizwa na wahusika, kulazimu kupelekwa Polisi na Mahakamani ambapo matokeo yake mahabusu mwenye kesi ya kuku kutumia gharama kubwa bdala ya faida inakuwa hasara. Naishauri Serikali kuleta mfumo utakaoondoa watu kujazana mahabusu na magereza kwa sababu hili linasababisha mateso na rushwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kuleta mkakati wa kuboresha vituo vya afya. Naomba kujua awamu nyingine ya fedha hizi, Mji wa Geita utapewa? Hii inatokana na kutokuwemo katika awamu ya kwanza. Geita Mjini haina hospitali hivi sasa kwa kuwa hospitali yetu ya wilaya kwa miaka minne imebadilishwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kukubali kuwarejesha Watumishi wa darasa la saba kazini. Naomba sana suala hili liwe kwa watumishi wote waliokumbwa na kadhia hili ikiwa ni pamoja na Manesi, Dereva na Idara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kukabiliana na tatizo la upungufu wa Walimu, kwa kuwa hivi sasa tunapunguza Walimu wa sekondari kwenda msingi ni vyema taratibu za kuangalia kwa makini waliokusudiwa zifuatwe kwa kuwa hivi sasa kuna kukomoana. Pia ni muhimu sana wanaohamishwa wawe ni wale wenye Diploma kwanza kuepuka kutengeneza tatizo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubora wa elimu, naishauri Serikali hasa kwa elimu ya Sekondari kuacha kuchukua watoto holela wa darasa la saba. Kwa mfano, mwaka 2017 iwapo uwezo wa Serikali nchi nzima ni wanafunzi 200,000 wa mwaka wa kwanza basi mwaka unaofuata Serikali ichukue kwanza 200,000 na baadaye iongeze idadi iwapo tu inazo taarifa za uwepo wa nafasi zaidi kuliko hivi sasa kuchukua kama kokolo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira mpya; bado hakuna uwazi wa kutosha katika mfumo wa kuchuja watahiniwa kwa kuwa hivi sasa ni rahisi sana kwa Watendaji wa Idara ya Utumishi wanaokuja mikoani kuja na watu wao.
The Finance Bill, 2016
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naunga mkono sehemu kubwa ya mapendekezo ya sheria hii lakini naomba tu nitoe ushauri kwenye maeneo machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nilitaka Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija atuambie, benki na taasisi nyingi zina riba kubwa sana ya mikopo, ni kodi kiasi gani ambayo Serikali inaweza kukusanya kutoka kwenye riba kubwa hizi ambazo wanatozwa wananchi na zina mchango gani? Kwa sababu naona kama hawa watu wanatengeneza faida kubwa na hatupati mapato yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye Muswada huu wa Sheria kifungu cha 65E mpaka 65N, yapo mapendekezo kwamba hesabu za mtu anayetafiti na ambaye yupo kwenye full operations zinabebana, anapoanza operations akija kwenye uchimbaji gharama zile zinachukuliwa zinahamishiwa huku, matokeo yake huyu mtu halipi kodi. Hapa nina mfano mzuri na kama tukiruhusu suala hili makampuni yataendelea kutokulipa kodi katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano nilikuwa Ngara kule kuna kampuni moja inaitwa Kabanga Nickle, kwa miaka 45 wao wanafanya utafiti na kila mwaka kuna watu pale wako kwenye operations, matokeo yake hizi gharama zote siku moja akija mwekezaji zitaingizwa kwenye kampuni itakayokuja, hii kampuni haitalipa kodi milele. Kwa hiyo, nashauri gharama za utafutaji ziwe tofauti na gharama halisi wakati huu mgodi unaanza operations kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya nchi. Tunao watu katika maeneo kama Geita pale, wameshikilia maeneo wana miaka 20, hawachimbi, hawafanyi chochote kila mwaka wana-renew licence. Matokeo yake gharama hizi za kusimamia maeneo haya watakuja kuiwekea Serikali halafu hawatalipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo nataka kusema ni kwamba halmashauri zetu zina migogoro mingi sana kwa sababu ya wafugaji na maeneo mengi ambayo yalikuwa yanafaa kwa ajili ya kilimo ili halmashauri zikusanye kodi yanatumika kwa ajili ya mifugo lakini mifugo hii ilisamehewa kodi. Naomba kuishauri Serikali iziruhusu halmashauri zitoze kodi kwenye mifugo ili mifugo hii iwe na faida kwa halmashauri. Tunaendelea kuiona mifugo haina thamani, haina maana yoyote kwa sababu tuliisamehe kodi sisi wenyewe. Mtu ana ng‟ombe 5,000 anaonekana ni masikini lakini mtu mwenye nyumba moja anakwenda kulipa kodi. Kwa hiyo, mimi sioni kama hapa kuna proportionality. Naomba sana Serikali ifanye mabadiliko kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, napendekeza kwamba tumesamehe kodi kwenye taasisi za umma hasa hospitali na Mashirika ya Dini, tukasahau kidogo kwamba Waraka wa Elimu wa mwaka 1978 unasema elimu ni huduma. Nataka kushauri Serikali kwenye property tax hapa kwamba shule zingewekewa badala ya kuacha hiki kiwango kikawa kinayumbayumba, kuwaachia TRA na Halmashauri waamue wenyewe, tutafute flat rate kwa ajili ya shule kwa sababu hivi vyombo ambavyo vinatoa huduma, ni taasisi za huduma ili tuepuke watoto na wazazi kuja kulipia gharama hizi kwenye Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika siku ya leo, pia niwape pole wananchi wa Wilaya ya Biharamulo ambao Mheshimiwa Mbunge wao wa Bunge lililopita Mheshimiwa Anthony Mbassa jana tulipata taarifa kwamba amefariki na niwatakie moyo wa subira kwa familia, ni majirani zetu Geita kwa hiyo tunafahamiana vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya jana ya Wakuu wa Wilaya na kwa kweli naomba nimpongeze kwa sababu ameendelea kuimarisha safu yake ya uongozi. Ninawapongeza walioteuliwa na niwatakie kila la kheri, pia niwapongeze ambao uteuzi wao umetenguliwa au hawakuteuliwa na niwatakie kila la kheri huko uraiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu nitoe mapendekezo mawili kwenye sheria hii. Ukiangalia vizuri nia njema ya Mheshimiwa Rais ya kuwateua vijana kuwa Wakuu wa Wilaya ni kwa ajili ya kuwaingiza katika Mfumo wa Uongozi wa Nchi ni nia njema sana na wengine wanateuliwa wakitoka kazini. Nafahamu Serikali iliyopita wakati wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, wapo baadhi ya ma-DC wakiwa Maafisa Tarafa, Maafisa Mipango, wakiwa na miaka 20 mpaka 30, wamehudumia miaka mitano na uteuzi huu wameachwa, ukitazama vizuri sheria hii sasa hawa walipoteza ajira yao huko nyuma na sasa hivi siyo tena watumishi, unaona kabisa kwamba vijana hawa baada ya miaka miwili watakuwa ni watu ambao ni mzigo kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema sheria ukishateuliwa kuwa DC ajira yako ya kwanza inapotea, akija Rais mwingine baada ya miaka 10 akikuacha na ajira yako bado una miaka 38 unapoteza kila kitu. Kwa hiyo, ni sheria ambayo ninaiona kama siyo nzuri. Kwa sababu wapo waliotoka kwenye Utumishi wa Umma sasa zaidi ya 20 ambao wanakwenda kuwa Wakuu Wilaya, baada ya miaka 10 ya Mheshimiwa Rais Magufuli, anaweza akuja Rais mwingine akasema nao hawahitaji, hawawezi kurudi Serikalini umri wao ni miaka 35, ninadhani Sheria hii siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini niwatakie kila la kheri walioteuliwa na niwape pole vijana wenzangu ambao tulikuwa nao na wengi wako chini ya miaka 40 ambao wameachwa, wajipange upya huko uraiani. Nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda sasa kwenye marekebisho ya sheria nianze na Sheria ya Elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imependekeza adhabu kali ya miaka 30, kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kumpa ujauzito mwanafunzi. Nazungumzia wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali sheria ni nzuri, ingawa kwa mtazamo wangu kuna mambo mengi ya kufanya. Mimi niko katika Kamati ya UKIMWI; tumeangalia kwenye taarifa tulizoletewa, tumeona watoto wanaanza kufanya mapenzi wengine wakiwa na miaka kumi na kuendelea. Maana yake ni kwamba waanza kufanya mapenzi na wanapata maambukizi ya UKIMWI chini ya miaka 15; na hawa ni wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari. Upo uwezekano huyu ambaye ameanza kufanya mapenzi katika umri mdogo anaporudi shuleni huyu binti wa miaka 12, miaka 13 akam-convince kijana awa kiume wa miaka 15, miaka 16 na matokeo yake huyu wa miaka 13 hadi miaka 14 akipata mimba unaweza kufikiri ni ya mwanafunzi kumbe amepata uraiani huko. Kwa sababu taarifa zinaonesha kwamba hawa wanapoanza kufanya mapenzi wanafanya na watu wazima wala hawafanyi na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maana yake ni nini? Sheria hii upo uwezekano wa kumfunga mtu miaka 30 mwisho ukagundua kwamba mimba hii haikuwa ya yule aliyefungwa na unagudua haikuwa ya yule aliyefungwa tayari mtu huyu alishatumikia kifungo cha miaka 30, unatoka jela mtoto siyo wa kwako, mtoto ni wa mtu mwingine kwa sababu watoto wetu siku hizi wanaanza kujifunza mambo haya wakiwa na umri mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali iende mbali zaidi kwa kuleta vipimo vya DNA ikiwezekana kwenye level ya kila Wilaya, kwa sababu kwenye ushauri uliotolewa juzi kila Kata haiwezekani, kwenye level ya kila Wilaya, au kwenye level ambayo itakuwa ni rahisi kugundua kwamba ujauzito huu siyo wa mwanafunzi. Ninazungumzia hapa kwa sababu vijana wetu hawa kwenye maeneo mengi ya shule anaweza akatafuta mnyonge wa kumkimbilia, akafuata mwanafunzi mwenzake, lakini kwa sababu mambo haya wanaanza mapema, inawezekana ujauzito huu ameupata uraiani huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hii kwa mifano sahihi kabisa ambayo tumepata kutoka kwenye Kamati yetu na inaonesha kabisa wazi kwa mba vijana wetu wana wanaanza matendo haya mapema zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuangalie namna ya kutengeneza adhabu nyingine zaidi, unapomfunga mtu miaka 30 anakwenda jela, halafu baada ya mwaka mmoja anakuwa kama vile amezoea maisha ya jela, inakuwa tena siyo adhabu, ninafikiri pamoja na miaka 30, kila mwezi huyu mtu awe anapata viboko 12, kwa miaka yote 30 mpaka atakapotoka. Hii itamfanya mtu asizoee kile kifungo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekutana na watu wengi sana jela huko, akishafungwa miaka mitatu inakuwa kama vile ni nyumbani, ukienda mtaani unakutana nao, hata Askari Magereza hana tena muda wa kuwachunga wanawaacha tu wanatembea wenyewe kwa sababu walishazoea maisha ni mazuri, anakula vizuri, ameshakuwa mnyampara mle, anapata sabuni mafuta. Kwa hiyo, unamkuta mtu yule huku aliacha ameharibu mtoto wa mtu lakini kule anaendelea na maisha yake kama kawaida. Kwa hiyo, nafikiri kila mwezi akipata viboko 12 mpaka miaka yote 30 itakapoisha itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine huyu binti ambaye sasa amekwishajifungua tunamfanyaje? Kwa vile atajifungua Baba amefungwa, atafukuzwa shule na hatasoma tena. Ushauri wangu ni kwamba baada ya kujifungua binti huyu, uangaliwe uwezekanano wa kubadilisha sheria ili aendelee na masomo, kwa sababu baadaye mtoto huyu atajikuta ana mama hakusoma, ana baba ambaye alifungwa akiwa mwanafunzi naye hakusoma tutakuwa tumetengeneza mtoto ambaye atakosa msaada kwa baba na atakosa msaada kwa mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sheria itazame vizuri, kuna wakati mwingine unakuta kwenye darasa moja binti ni umri mkubwa kuliko kijana. Labda binti ana miaka 23 alichelewa kusoma. Kule usukumani watu wanaanza shule wakiwa na umri mkubwa, anaweza kuanza kusoma akiwa na miaka 15 ndiyo anakwenda darasa la kwanza, kwa hiyo anajikuta amefika sekondari ana miaka 24; halafu huyu binti anapewa mimba na kijana wa miaka 15; sasa hapa mwenye kosa ni nani, kwa sababu inaonekana kama vile binti atakuwa ndiye aliyemtongoza kijana, halafu unakwenda kumfunga huyu kijana ana miaka 15 unamwacha huyu binti wa miaka 24 uraiani, ni kama vile tunaleta uonezi hapa. Nafirikiri sheria itazame vizuri ili kuangalia namna ambavyo sheria hii inaweza kwenda ikafanya kazi sehemu zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono marekebisho ya sheria nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kifupi sana kwanza niseme naunga mkono muswada huu na labda tu nitoe mapendekezo yangu machache, nilikuwa nimetarajia ningeweza kuchangia kesho, lakini naweza kusema haya machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza naungana na ambao wangependa tutofautishe Ibara ya 18, kuna tatizo la tafsiri kwamba haki ya kupata taarifa na haki ya kupata habari, lakini haki ya kupata habari palepale inalazimishwa ionekane iko sawa na haki ya kupata taarifa. Katika mazingira ya kawaida, taarifa hii inaweza kutolewa katika muda wowote ule ili mradi mlengwa aliyekuwa anataka taarifa anatakiwa apate hii taarifa kadri alivyokuwa anaihitaji. Kwa hiyo, pamekuwa na tatizo la kuichanganya hii kuonekana kwamba mtu asipopata taarifa pale pale Katiba imekiukwa. Siyo kweli kwamba Katiba inakiukwa kwa mtu kutokupewa taarifa pale pale lakini inatakiwa mtu apewe taarifa sahihi wakati wowote baada ya tukio hilo kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi katika hili ni kama walivyosema wenzangu, ni vizuri sana sheria yetu ikatofautisha ni maeneo gani tunaamanisha taarifa za siri. Zipo taarifa za intelijensia ambazo zikiachwa wazi zinahatarisha usalama wa nchi yetu, lakini ziko zingine ni taarifa ambazo zimekuwa tu zikibanwa na walengwa kwa nia ya kuficha baadhi ya siri kwenye taasisi na wengi wamezitumia hizi vibaya. Watu wengi wanasema kwamba kwenye Halmashauri zetu ni rahisi sana kupata taarifa, lakini mimi ambaye ninaamini nimekuwa kwenye Halmashauri kwa muda mrefu kuna wakati hata Mheshimiwa Mbunge kama taarifa unayotaka ina madhara kwa walengwa walioko kwenye Halmashauri ile unaweza ukasubiri taarifa ile kwa muda mrefu na usiipate.
Kwa hiyo, sheria hii ni ya muhimu, ni sheria ambayo kimsingi inawalazimisha wahusika kutoa taarifa sahihi hata kama taarifa ile haitatolewa pale pale lakini taarifa hii itatolewa kwa mtu ambaye anaihitaji na itakwenda kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi hapa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja atusaidie tunatunga sheria hii kwa ajili ya Serikali peke yake au pia kwa ajili ya makampuni binafsi. Kwa mfano, kama ni Serikali peke yake ieleweke lakini tunayo makampuni ambayo yanatuzunguka kwenye maeneo yetu, makampuni yanayofanya biashara na makampuni yanayochimba madini ambayo ni wadau wakubwa wa Serikali. Kuna wakati makampuni haya yanaweza yakalipa service levy bila wadau kujua yanalipa kutokana na mauzo yapi, yanalipa kutokana na mapato gani na unapokwenda kufuata hizi taarifa inaonekana ni taarifa za siri za hizo kampuni.
Kwa hiyo, ni vizuri pia kueleweka kwamba sheria hii inakwenda kugusa kila eneo, kila idara, kila taasisi au ni sheria ambayo inalenga kugusa Serikali peke yake au ni sheria ambayo inalenga kugusa kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ndugu zetu wengi wana wasiwasi sana na baadhi ya matumizi ya sheria hii unapofanya makosa. Mimi sijawahi kuona mtu anaadhibiwa bila kufanya makosa na ametusaidia hapa Mheshimiwa Bashe kwamba wadau wa habari wameshirikishwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya kawaida tunaamini lengo la sheria ni kujenga nidhamu. Kama watu wanatumia vibaya haki yao ya msingi ya kutoa taarifa na kupotosha umma lazima watu waadhibiwe. Hili lisije likaonekana kama ni suala baya kwa sababu bila kufanya hivyo tutakuwa tunajenga nchi ya watu wanaofanya makusudi, wanaopotosha umma na matokeo yake mtu anapata sifa kwa sababu ya kuharibu sifa ya mtu mwingine. Tumeshuhudia huko nyuma mtu anasimama hapa anatengeneza uongo, huko nje wanamsifu, halafu kesho yake hana hata data moja inayoonyesha kwamba taarifa hiyo ni ya ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mheshimiwa mmoja hapa kwamba ni vizuri sana source ya information pia tujiridhishe nayo. Kwa mfano, kama mtu anayetoa taarifa hana uhakika na taarifa ile halafu aliyepewa taarifa ndiye anayekwenda kuadhibiwa nadhani sio sahihi. Ni vizuri sana yule anayetoa taarifa ajiridhishe na taarifa ile kabla ya kuitoa na iwapo taarifa hiyo itakuwa na mapungufu yule aliyepewa taarifa pia asije akaadhibiwa kwa makosa ya taarifa ambayo aliiipata kimakosa kutoka kwa mtu ambaye alikosea. Vinginevyo adhabu hizi ziwekwe kwa watu wote wawili au watu wote wawili wasamehe na adhabu ambayo itakuja kufuatia kwenye sheria yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba niwapongeze sana Kamati kwa namna ambavyo wameutendea haki muswada huu. Nilipousoma mwaka 2017 na nilipokuja kusikiliza marekebisho, nimeona Kamati wamefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri pamoja na Watendaji wote katika Wizara hii. Kama walivyosema wenzangu, kimsingi tunaiona nia ya Serikali ya kuunganisha mifuko hii na kuondoa gharama za uendeshaji kama ambavyo zimetajwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Kamati. Kwa hiyo, tunaiona hiyo nia na hilo lengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu hapa, nilidhani baada ya Serikali kuondoa gharama hizo ambazo tumeziona kwenye maelezo ya Mheshimiwa Waziri, basi zingekuja chini zikawa na faida kwa mwanachama wa mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyomalizia kusema Mheshimiwa Mama Mushashu, kwa kweli tulitarajia kuona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba mwisho wa siku sasa haya mafao yanakwenda kuongezeka kwa asilimia ngapi au yanakwenda kuimarika kwa asilimia ngapi? Sasa linabaki kuwa kwenye Pandora box kitu ambacho nadhani tutahitaji pia baadaye kuanza kuhangaika na Mheshimiwa Waziri. Kwa ujumla wake, napongeze sana, marekebisho yamezingatia sana maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika section 35 kama walivyosema wenzangu, ni vizuri sana kufikiria kuhusu medical insurance na fao la elimu. Hivi tunapozungumza, watumishi wengi ambao walikuwa wamesoma Diploma, hawapati mikopo tena kwenye Bodi ya Elimu na wengi walikuwa wanakimbilia kwenye mifuko hii kwenda kuomba mikopo na baadaye wanakwenda vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuwa tume-merge na tukaliondoa hili kama ambavyo iko sasa, maana yake ni kwamba liko kundi la watu hawatasoma tena kulingana na gharama za elimu zilivyo juu. Kwa hiyo, ni vizuri sana kwenye section 29 kurudisha fao hili la elimu, kwa sababu mifuko ilikuwa inatoa na wanachama walikuwa wakijiunga katika mifuko hii kwa sababu waliona kuna kitu wanakihitaji kwenye mfuko huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naipongeza sana Serikali kwenye section 43. Mafao ya wastaafu yalikuwa yanaweza kuchelewa mpaka mwaka mzima na hakuna mtu aliyekuwa anajali. Ninao mfano wa watu ambao nimewasaidia, walicheleweshewa mafao yao kwa zaidi ya miezi sita, miezi nane na wako wengine mpaka leo wanasubiri na hakuna interest, wala hakuna mtu aliyekuwa anajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuweka provision hii katika section 42 na 43 maana yake tunaweka commitment kwa mifuko hii kuhakikisha kwamba hii miezi sita ya maandalizi na hizi siku 60 zilizotajwa katika sheria wasipolipa wajue kwamba watalipa kwa interest. Interest haimasaidii sana mstaafu, kwa sababu mstaafu akili yake ikimpelekea kufikiri kustaafu, mara nyingi hufikiri aweze kupata malipo yake na kuendelea na maisha yake mengine. Naipongeza Serikali kwa kuweka commitment hii kwa sababu itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi natoka kwenye maneo ya wachimbaji na mgogoro wangu mkubwa siku zote umekuwa ni fao la kujitoa. Ninaishukuru Serikali, maelezo aliyoyasema Mwenyekiti wa Kamati na Mheshimiwa Waziri, yanaleta picha kwamba kuna namna inalishughulikia. Hivi tunavyozungumza, wako wafanyakazi wengi walioko kwenye madini ambao wana zaidi ya miaka mitano, ambao wanasubiri sheria hii ili iwafungue namna ya kuendelea mbele, kwa bahati mbaya sana haijawa clear bado. Bado imekuja ikiwa imefumbwa fumbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, wapiga kura wangu wanataka kufahamu sasa hasa wale ambao tayari wako nje wanasubiri utaratibu kwa ahadi ya Rais aliyoitoa kule Kilimanjaro, ni nini kinafuata baada ya hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimsikia Mwenyekiti wa Kamati anasema kutakuwa na hiyo asilimia 33 kwa miezi sita na baadaye kuangalia kama hakuna tena ajira nyingine, basi mtu analipwa pesa yake, anaondoka. Tulione hili kwenye utaratibu ili liwasaidie watu kuweza kujipanga na maisha yao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tufahamu kwamba tunapoiunganisha mifuko hii tunaondoa ushindani kwa kupunguza gharama, pia kuna madhara ya kuondoa ushindani. Mara nyingi sana huko nyuma kabla ya mifuko hii kuwa mingi, pia hata customer care ilikuwa very poor. Lazima tulitambue hili kwamba baada ya mifuko hii kuunganishwa, watu watakuwa hawana option; wa umma watakwenda huku na wa upande wa binafsi atakwenda huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa option kunaweza kukawafanya watendaji wakalala usingizi. Kwa hiyo, lazima tuweke mfumo ambao utaendelea kuifanya mifuko hii kuendelea kuhakikisha kwamba inajali huduma za members wake, lakini pia inatoa huduma kulingana na mikataba ambayo ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na wasaidizi wao wote kwa kutuletea muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama walivyosema wachangiaji wengine wengi, ni vigumu sana mwekezaji yeyote makini kwenda kuwekeza mabilioni ya shilingi kama hana uhakika na usalama wa pesa zake. Kwa hiyo, mabadiliko haya ya sheria yalikuwa ni ya lazima kwa sababu wawekezaji wetu wengi duniani ni wawekezaji ambao pesa siyo za kwao, wanazipata kwenye mabenki, wanakopa. Kwa hiyo, anapokuja hapa bila kuwa na uhakika na usalama wa pesa zake hawezi kuja kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nilitaka nianze kwa taarifa ya Kamati kwenye ukurasa wa tisa ambapo ukienda kwenye item namba 2.2 utagunduakwamba mwaka 2017 tulipitisha hapa sheria ambayo ilikuwa inaruhusu Halmashauri zetu kubuni miradi ya kimkakati na kuwasilisha Serikalini na kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibuni hapa tulipata taarifa kwamba ni Halmashauri chache sana ambazo zilifanikiwa na moja ya sababu kubwa ambayo ninaiona ni kukosekana kwa ujuzi kwenye Halmashauri zetu na siyo kwenye Halmashauri peke yake. Kwa sababu kama Halmashauri zetu na Wizara zingekuwa na wataalam wa kutosha wangeweza kutoa msaada huu kwenye Halmashauri zetu. Leo tungekuwa tunapata tathmini ya hatua kubwa mbele tuliyoipiga kwenye sheria ambayo tuliiweka, lakini matokeo yake tunaendelea kuwa Halmashauri mbili/tatu ambazo zimetekeleza hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naungana mkono kabisa na Kamati kwamba iwepo programu maalum ya kuwawezesha wataalam wetu ili wapate uwezo wa ku-plan hii miradi, kuisimamia, lakini pia kutengeneza maandiko ambayo yatatupeleka kwenye utekelezaji wa sheria hii bila kuwa na ubabaishaji. Kama tukiendelea bila kujenga uwezo, tatizo tulilokuwa nalo mwanzo la kuwa na watu kwenye ofisi ambao hawawezi kufanya upembuzi yakinifu na pia hawawezi kufanya maamuzi, litaendelea, kwa hiyo, naungana mkono na Kamati.

Naomba sana kwamba katika hatua hii Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kufanya investment ya kutosha ili kupata watu ambao wataweza kuisaidia Serikali kwa sababu tunaweza kupitisha sheria nzuri, lakini mwisho wa siku sheria ikaendelea kubaki kwenye Kamati na isiweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingi sana ambazo pamekuwa na sheria hii na hasa katika nchi ambazo zimetolewa mfano hapa, zipo sababu nyingi ambazo zimesababisha ikaonekana kwamba Sheria ya PPP nayo haifai. La kwanza, ni mazingira ambayo Serikali itaweka. Inawezekana kabisa Waziri wa Fedha akawa na nia njema ya kutaka wawekezaji waje na wabia waje, lakini hayuko peke yake, ana watu wengi ambao lazima wafanye kazi pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaenda kwa Waziri wa Fedha, yuko sawa, wakaenda watu wengine wa Mazingira wakakwamisha, wakaenda watu wa Ardhi wakakwamisha, wakaenda watu wa Mambo ya Ndani wakakwamisha. Kwa hiyo, ni lazima hizi timu zote zifanye kazi kwa pamoja ili wawekezaji wanaokuja wenye nia njema ya kufanya kazi na Serikali waweze kuona kwamba nia kweli tumedhamiria kutumia sheria hii kuleta mabadiliko makubwa katika uwekezaji na katika uchumi na faida ziko nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukitumia pesa nyingi sana za kwetu kufanya miradi mingine. Iwapo tutapata partners, maana yake ni kwamba tutaelekeza pesa zetu za ndani kwenye maeneo ambayo tunadhani wawekezaji hawaoni faida, kwa sababu hakuna mtu amekwenda kuwekeza sehemu ambapo hawezi kupata faida. Jambo hili ni muhimu sana, kwa hiyo, Serikali yenyewe ni muhimu kuwa imejiandaa lakini kuwaandaa wawekezaji waweze kufahamu kwamba ni maeneo gani wakikwama, wakimbilie wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ni kitu muhimu sana kwenye suala hili. Nataka kutoa ushauri kwamba pawepo na kanzidata (database) ambayo itaonesha kutokea kwenye Halmashauri zetu/kwenye Manispaa ambayo itatusaidia kufahamu mtu akiwa duniani popote pale katika nchi yoyote duniani aweze kujua nikienda Tanzania, maeneo ya priorities ni haya hapa ambayo unadhani naweza nikaenda kuwekeza. Isitokee mahali unakuta sehemu hii wanafahamu hiki, sehemu hii hakuna muunganiko wa mawasiliano, tutajikuta kila siku na tunaanza upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kisiasa ni muhimu sana katika suala hili. Naomba tu niseme vizuri kwamba tunategemea sana kwamba kauli na msukumo wa Mawaziri wetu tuweze kuwasaidia wawekezaji. Tunalo tatizo sana kwenye maeneo yetu huku chini kwamba inawezekana huku mna-push suala liende, lakini kwa sababu watendaji wetu huko chini hawaoni faida na kwa sababu watu wengi wamezoea kupata commission, wanaona kwamba suala hili halina faida sana kwao, wakalikwamisha bila sababu. Kwa hiyo, tunataka sana Mheshimiwa Waziri mkono wake huu na wasaidizi wake huko chini uweze kusukuma mambo haya yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la mikataba. Nchi nyingi ambazo zimepata shida kwenye mikataba, haikuja kwa bahati mbaya, ni kwa sababu hapakuwa na transparency. Watu wengi wanaopelekwa kuingia kwenye mikataba aidha uwezo wao ni mdogo au ni mkubwa sana, kwa hiyo, matokeo yake badala ya kuona maslahi makubwa ya nchi wanajikuta wanaweka zaidi maslahi yao binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linafanyikaje? Anaweza kuja mwekezaji hapa leo, anataka kuwekeza shilingi bilioni 100 na anataka kufanya payback ya mradi ule ule labda miaka 10, lakini anayekwenda kuweka mkataba akasema wewe fanya hiyo miaka 20 na uhakikishe mradi huu unagharimu shilingi bilioni 200. Matokeo yake mradi huu unaonekana tena hauna faida kwa wananchi au una gharama kubwa. Kumbe tatizo kubwa hakukuwa na transparency kwenye mkataba.