Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Saada Salum Mkuya (5 total)

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA (K.n.y. MHE. SAADA MKUYA SALUM) aliuliza:-
Vituo vingi vya afya vya kijeshi vinahudumia maafisa wa jeshi na wananchi waliopo karibu na vituo hivyo. Hata hivyo vituo hivi vinakabiliwa na upungufu wa dawa, vifaa tiba na wataalam wenye ujuzi.
(a) Je, Serikali inafahamu idadi ya vituo vyake vilivyopo Zanzibar?
(b) Je, kuna mkakati gani unafanyika kuhakikisha kuwa vituo hivyo vinapatiwa dawa, vifaa tiba na wataalam wa kuhudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum Mbunge wa Weleza kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kulingana na vipimo vya Umoja wa Mataifa (United Nations – UN), Zanzibar ina kituo kimoja cha afya ngazi ya tatu na vituo viwili ngazi ya pili. Aidha kimuundo kila Kikosi cha Jeshi kina kituo kidogo cha tiba.
(b) Kwa ujumla vituo vya afya vina changamoto za dawa, vifaa tiba na wataalam. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, changamoto hizo kwa sehemu kubwa zinategemewa kutatuliwa baada ya kukamilika taratibu za kuanzishwa mfuko wa Bima ya Afya kwa jeshi letu.
Aidha, changamoto ya wataalamu wa afya inategemewa kupungua baada ya wataalam wa afya walioajiriwa hivi karibuni waliopo katika mafunzo ya vitendo vikosini (exposure) na kwenye Vyuo vya Kijeshi kuhitimu mafunzo yao. Pia, upo mpango wa kuandikisha wataalamu wa afya katika ngazi ya Paramedics baada ya kupata kibali cha ajira mpya. Pia upo mpango wa kuandikisha wataalam wa afya katika ngazi Paramedics mara tu baada ya ajira mpya kuruhusiwa.
MHE. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:-
Vituo vya Afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Wananchi vimekuwa vikitoa huduma za afya kwa wananchi wengi na kutokana na umadhubuti na umakini wa watendaji, wananchi wamejenga imani kubwa juu ya huduma zinazotolewa katika vituo hivyo; hata hivyo huduma hizo zimekuwa zikikabiliwa na vikwazo mbalimbali vikiwemo uhaba wa dawa, Madaktari na vitendea kazi:-
Je, Serikali imeweka mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kuwa vifaa tiba, dawa na Madaktari vinapatikana ili kutoa huduma bora?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa linaendelea na hatua ya kuboresha huduma za tiba Jeshini, kama ifuatavyo:-
(a) Kuendeleza kuwashawishi wataalam wa tiba wenye sifa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kulingana na nafasi za ajira zinazopatikana.
(b) JWTZ limeendelea na utaratibu wa kuwaendeleza Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma kupata elimu katika ngazi mbalimbali zikiwemo Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili kupitia vyuo vyetu vya kijeshi mfano “Military College of Medical Services” pamoja na vyuo vya kiraia nje ya Jeshi. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwadhamini wataalam wa tiba wanaosomea Shahada ya Uzamili na Uzamivu.
(c) Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiendelea kutoa ruzuku na kuongeza upatikanaji wa madawa na vifaa tiba.
(d) Kupitia wafadhili mbalimbali mfano Serikali ya Marekani na Serikali ya Jamhuri ya Ujerumani, huduma za tiba zimeendelea kuboreshwa hasa kwa kuongeza miundombinu na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu niliyotoa katika sehemu (a) mpaka (d), Wizara yangu iko katika mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Bima ya Afya kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Ni imani yetu kuwa Mfuko huo utakapoanzishwa utaweza kuongeza rasilimali fedha katika utoaji huduma za afya Jeshini. Fedha hizo za ziada zitatumika katika kuboresha miundombinu na upatikanaji wa dawa na vifaatiba hivyo kuboresha huduma za afya kwa Wanajeshi na wananchi wanaotumia vituo vya afya vya Jeshi kupata tiba. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y MHE. SAADA MKUYA SALUM) aliuliza:-
Serikali nyingi duniani zinaunganisha diaspora katika mikakati yao ya kukuza uchumi na huduma za kijamii.
(a) Je, Serikali imefanya mikakati gani ya kuunganisha diaspora katika shughuli za kukuza uchumi na huduma za kijamii?
(b) Je, ni kwa kiasi gani diaspora imechangia uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI (K.n.y MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa diaspora katika kuleta maendeleo hapa nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Kuelekea uchumi wa kati diaspora ni moja wa wadau. Ili kutekeleza jukumu hili Serikali imeweka mikakati ifuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa katika kila eneo lenye uwakilishi wetu Ubalozi unawatambua Watanzania wanaoishi katika maeneo hayo pamoja na Watanzania hao kuunda Jumuiya zao.
(ii) Kupitia ziara za viongozi pindi wanapokuwa nchi za nje Serikali imehakikisha kuwa, kunakuwa na utaratibu wa viongozi kukutana na diaspora wa Tanzania ili kuwaeleza masuala yanayotokea nyumbani, hasa fursa za kiuchumi na uwekezaji.
(iii) Serikali imekuwa ikiratibu zoezi la kuwakutanisha diaspora na wadau wa hapa nchini na nje kupitia makongamano, ambapo kumekuwa na jitihada, mijadala yenye tija katika maeneo ya uchumi na maendeleo kwa ujumla.
(iv) Wizara imeunda timu ya kufanikisha uandaaji wa Sera ya Taifa ya diaspora itakayoainisha mikakati na kutoa miongozo kuhusu ushiriki wa diaspora katika kuchangia maendeleo nchini.
(v) Wizara imeelekeza Balozi zetu kusajili Watanzania waliopo katika maeneo yote ya uwakilishi na kuainisha shughuli wanazozifanya, taaluma na ujuzi walionao, ili kusaidia kuwa na takwimu sahihi na kuhusu diaspora wetu na kuweka mazingira wezeshi ya kuchangia maendeleo nchini.
(b) Mheshimiwa Spika, diaspora wetu wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi yetu kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali kama biashara, afya na elimu, kama ifuatavyo:-
(i) Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, yaani 2013 hadi 2017, diaspora kwa ujumla wao walituma nchini kiasi kisichopungua dola za Kimarekani milioni 2282 ikiwa ni wastani wa dola milioni 455 kwa mwaka.
(ii) Jumla ya nyumba 108 za Shirika la Nyumba la Taifa zilinunuliwa na diaspora wetu.
(iii) Mnamo mwezi Julai, 2017 tulipokea Madaktari wa Kitanzania waliopo Marekani, Dakota ambao walikuja kutoa huduma bila malipo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar.
(iv) Katika kipindi cha mwaka 2015/2017 timu ya Madaktari wa Kitanzania waishio Marekani, kupitia Taasisi ya Afya ya Elimu na Maendeleo – Head Incorporated, walitoa huduma za afya na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar na kukabidhi dawa na vifaatiba vyenye thamani ya dola 459,075; msaada wa mashine ya kupimia saratani ya matiti katika Hospitali ya Lugalo Dar es Salaam yenye thamani ya dola 200,000; huduma za matibabu ya ushauri na ushauri katika Hospitali ya Mwananyamala Dar es Salaam na Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo Zanzibar, kukabidhi msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya dola 300,000.
(v) Jumuiya ya Watanzania nchini Marekani Dakota iliandaa jukwa la afya lililofanyika nchini humo mwezi Novemba, 2017 ambapo walialika taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya afya kutoka hapa nchini ili kupeana ujuzi na uzoefu walioupata Marekani katika kipindi wanachoishi na kufanya kazi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika masuala hayo.
(vi) Diaspora wa Kitanzania waliopo Bujumbura walitafuta soko la bidhaa za wajasiriamali wa Kitanzania walioshiriki katika maonesho ya Juakali yaliyofanyika mwezi Disemba, 2017. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:-
Kati ya mambo yaliyokubalika katika mkakati wa kutatua changamoto za Muungano ni pamoja na kugawana ajira zilizopo katika Taasisi za Muungano kwa asilimia 21 (Zanzibar) na asilimia 79 (Tanzania Bara):-
Je, ni kwa kiasi gani mkakati huo umetekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo wa ajira katika Taasisi za Muungano wa asilimia 21 kwa Zanzibar na asilimia 79 kwa Tanzania Bara unatekelezwa kwa mujibu wa waraka wa Serikali Kumb.Na.CDA279/350/01/D/95 wa tarehe 10 Mei, 2013. Tangu kutolewa kwa mwongozo huo, umetekelezwa kwa asilimia 82.7 kwa Tanzania Bara na asilimia 18 Tanzania Zanzibar.
Changamoto iliyopo katika kupata taarifa sahihi za Wazanzibari wanaopata ajira katika Taasisi za Muungano ni kutokana na anuani zao za Zanzibar badala ya wengi wanaotumia anuani za Mikoa ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi zote za Muungano zina mwongozo wa utekelezaji wa makubaliano hayo na zinaendelea kuzingatia utaratibu huo pindi wanapopata fursa ya kuajiri.
MHE. SAADA SALUM MKUYA aliuliza:-

Kumekuwa na changamoto mbalimbali katika Muungano ambazo zinaendelea kutatuliwa mojawapo ikiwa ni ajira za Muungano ziwe asilimia 21 kwa upande wa Zanzibar.

(a) Je, ni kwa kiasi gani makubaliano hayo yametekelezwa hadi sasa?

(b) Je, ni ajira ngapi zimepatikana kwa utaratibu huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba nichukue fursa hii sasa kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Utaratibu uliokubalika ni kwamba ajira katika taasisi za Muungano zinatakiwa kuwa kwenye uwiano wa asilimia 79 kwa watumishi wa Tanzania Bara na asilimia 21 kwa watumishi wa Zanzibar kwa utumishi wa ngazi ya utaalamu. Katika kutekeleza utaratibu wa muda wa mgao wa nafasi za ajira (quota) katika taasisi za Muungano kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Rais ilipewa kibali cha nafasi tatu, mtumishi mmoja alipangwa Zanzibar ikiwa ni asilimia 33 na watumishi wawili walipangiwa Tanzania Bara sawa na asilimia 67.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilipewa kibali cha nafasi 28 za Maafisa Mambo ya Nje na kati ya nafasi hizo saba zilijazwa na Watumishi kutoka Zanzibar ikiwa ni asilimia 25 na nafasi 21 zilijazwa na watumishi kutoka Tanzania Bara ikiwa ni asilimia 75.

(b) Tangu kufikiwa kwa makubaliano ya uratatibu wa muda wa mgao wa ajira katika Taasisi za Muungano mwaka 2013/2014 na kuanza kwa utekelezaji wa utaratibu huo mpaka sasa jumla ya wazanzibari 8 kati ya 31 wameajiriwa katika taasisi za Muungano ambao ni sawa na asilimia 25 ya waajiriwa hao. Taasisi za Muungano zina mwongozo wa utekelezaji wa makubaliano hayo na zinaendelea kuzingatia utaratibu huo wanaopata fursa ya kuajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo huu ulianza kutekelezwa mwaka 2013/2014 lakini utekelezaji wake umekumbwa na changamoto ikiwa ni kusitishwa kwa ajira Serikalini kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 kutokana na kupisha zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa na watumishi wenye vyeti feki. Hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa taasisi zote za Muungano zilipewa utaratibu huo na zitaajiri watumishi kama ilivyoelekezwa.