Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salum Mwinyi Rehani (6 total)

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na bei ya umeme bado Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) halijapunguza bei ya umeme kitu ambacho kinawanyima fursa wananchi wa Zanzibar kuweza kutumia nishati hii au rasilimali hii kwa ukubwa zaidi kuliko hali inavyokuweko sasa hivi. Kwa sababu wengine wanashindwa kuunga umeme kutokana na hali ya bei. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kukaa na ZECO ili kuona na kwamba na wao viwango vile vinaweza kupungua na kuwanufaisha wananchi wote kwa bei ya chini zaidi kama ilivyokuwa huku Tanzania Bara.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kule ZECO kama ambavyo mnajua, wanajua umeme wa jumla na kwa vile wananunua umeme wa jumla, siyo rahisi sana wakaona punguzo la bei ya umeme. Hata hivyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari kukaa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ZECO, TANESCO na EWURA ili kuona ni jinsi gani sasa gharama za umeme zinaweza kupitiwa upya. Nitoe tu angalizo, gharama za umeme zinazingatia sasa vyanzo vyetu pamoja na gharama nyingine za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, tutakaa pamoja na wewe pamoja na EWURA ili pia kuangalia upya bei za umeme huko Zanzibar.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize swali moja la nyongeza.
Kwa Zanzibar suala hili limekuwa na manung‟uniko sana na hasa kwa kutokuweko watendaji katika hizi taasisi na hili limetokana kwamba wanafunzi wengi wanaopata huduma kupitia TCU, NACTE na NECTA wamekuwa wanahisi hakuna uwiano na hakuna haki inayotendeka kwa vile hakuna watu ambao wanaohusiana wanaotoka upande ule kule. Je, Waziri au Wizara ina mpango gani wa kuweza kupata angalau maana yake watu wawili, watatu kuweza kuingia katika taasisi hizi ili kuepusha manung‟uniko ya kila siku hasa yanayohusiana na masuala ya vyeti na mengineyo ambao wanataka kujiunga katika vyuo mbalimbali vya huku Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaombe Watanzania tusifanye mambo kwa masuala ya hisia. Lazima twende katika misingi na misingi iliyopo ni hiyo ya kufuata sifa stahiki kwa nafasi zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba pamoja na kwamba hakuna hivi vigezo vilivyowekwa, kimsingi ukiangalia katika hizo taasisi zote wapo Wazanzibari ambao wanafanya hizo kazi na isitoshe kwa mfano kwa Baraza la Mitihani nafahamu hata Mkuu wa Kitengo kile kule Zanzibar anatoka Zanzibar. Lakini ukiacha hiyo nataka tu niseme kwamba sisi tumekuwa na mahusiano ya karibu sana na Serikali ambayo iko kwa upande wa Zanzibar na tunawasiliana katika masuala yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tarehe 11 Agosti, huu tulitembelewa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu na tuliweza kujadili mambo mablimbali ikiwemo ya kushirikiana na kusaidiana pale tunapoona upande mmoja haujakaa vizuri na kila jambo linalofanyika huwa tunashirikishana. Kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba Mheshimiwa Mbunge tusiende kwa hisia. Kama nafasi zitaonekana kwamba Watu walioomba wenye uwezo wengi wanatoka Zanzibar basi itabidi wapewe kwa sababu tunachohitaji ni uwezo na siyo tu kuangalia upande wanakotoka.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa mwenyekiti, napenda kuongezea katika majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa taaisis za Muungano kuwakilishwa kwa uwiano sahihi na muafaka kwa watu wa pande zote mbili, Serikali iliamua kwamba kuwe na quota kwa watumishi kwenye taasisi za Muungano na quota iliyokubalika ni asilimia 79 kwa asilimia 21 na sisi ofisi yetu tuliwaandikia taasisi na viongozi wote ambao wanahusika na masuala ya Muungano kwanza watuletee idadi ya watumishi waliopo, lakini pili watuletee mpango kazi wa kufikia quota iliyokubalika ya taasisi za Muungano ziwe na uwiano sahihi wa kimuungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu na mwisho ni kwamba Serikali ilishafanya uamuzi wa kufungua Ofisi ya Tume ya Ajira Zanzibar kwa sababu moja ya changamoto ilikuwa ni kwamba Tume ya Ajira ambayo inaajiri hawa watendaji na watumishi wengineo ipo Bara peke yaake na hizi nafasi wakati mwingine hazifahamiki au hazifikiwi na watu wa upande wa Zanzibar, kwa hiyo, ofisi hii sasa imefungua ofisi yake Zanzibar na nafasi zitatangazwa kwa upana wake kwa watu wa Zanzibar na wenyewe wataziomba ili waweze kupata fursa za kushiriki katika taasisi za Muungano.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Waziri; kwa vile utalii ni moja kati ya tegemeo kubwa la uchumi wa nchi yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo Mabalozi hasa walioko nchi mbalimbali za Latin America na America kuwa na uwezo wa kuweza kufanya ushawishi na kuweza kuunganisha Mashirika ya Kitalii yaliyoko katika nchi hasa za Ujerumani na Ufaransa kuweza kuja katika nchi zetu hizi na kuwa na mfano wa nchi ambazo wameweza kufanikiwa sana tukilinganisha nchi za Mauritius na nchi nyinginezo za Mashariki ya mbali ambazo zimefanikiwa sana katika suala hili la utalii?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kuniona, lakini napenda nianze kwa kweli kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sera ya Serikali ya economic diplomacy, hii ni moja ya nguzo ya kujenga mapato ya Serikali kwa kuzitumia Balozi zetu kutusaidia katika kutangaza utalii katika maeneo yao na tayari tumeanza kuandaa vitini ambavyo tutawapelekea Mabalozi ili hata mgeni akiingia kwenye Ubalozi wetu, ajue tayari ni vitu gani viko Tanzania. Kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane katika jambo hili ili kuweza kufanikisha sera hii.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini tulikuwa tunataka kujua mkakati gani Wizara inayo wa kuwafanya Wachina hawa kuhamisha teknolojia na viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali kutoka kwao kule kuanzishwa katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo katika Wizara yetu na nchi ya China ni kufanya makubaliano na kusaini makubaliano hayo ya kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi Tanzania na China.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado wamiliki wa vyombo hivi hawajawapa mikataba waendesha bajaji na bodaboda, matokeo yake wanakubaliana kwa maneno kwamba baada ya mwaka mmoja chombo hiki kitakuwa chako kwa kiasi fulani cha fedha lakini ikifika miezi saba au nane anamnyang’anya kile chombo na kumpa mtu mwingine.
Je, Serikali iko tayari kusimamia zoezi la kukabidhiwa mikataba waendesha pikipiki na wakamatwe waendesha pikipiki waulizwe mkataba aliokupa mwajiri wako uko wapi ili kuwashinikiza wamiliki hawa kutekeleza hii sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili aliloliulizia Mheshimiwa Mbunge la mikataba hapa lazima tuweke vizuri na ieleweke. Mikataba aliyokuwa anazungumzia Mheshimiwa Mbunge ni mkataba wa umiliki wa pikipiki hasa baada ya kuwa kuna makubaliano kati ya mwenye chombo na yule dereva ambaye amepewa chombo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali, mkataba ambao tuna uwezo wa kuusimamia wa kwanza kabisa ni mkataba wa ajira ambao upo kwa mujibu wa sheria, kifungu cha 14 cha Sheria Na. 6 ya mwaka 2004 ambacho kimeelezea vyema namna ambavyo kila mwajiriwa anapaswa kupewa mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo kalizungumzia Mheshimiwa Mbunge, ni makubaliano ambayo yamekuwa yakifanyika kati ya waendesha vyombo na wamiliki wa vyombo ambapo utaratibu katika maeneo mengi ni kwamba yule mmiliki anampatia muda muendesha chombo akisharejesha fedha yake basi baadaye chombo kile kinabaki kuwa cha yule dereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, nitoe tu wito wa kwamba makubaliano hayo yanaingiwa na pande mbili; mmiliki na mwendesha chombo, ikitokea namna yoyote ambayo haki ya mwendesha chombo huyu inadhulumiwa basi vyombo vya sheria vipo na tuwaombe watu hawa ambao wananyanyasika katika eneo hilo waende kulalamika na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya hao ambao wanakiuka utaratibu na makubaliano ambayo wameshaingia hapo awali.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kumuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza, tunataka tupate ripoti na siyo cheti kwa sababu cheti kinakuwa ni uthibitisho tu, lakini ripoti ndiyo kitu ambacho tunaweza kuona athari iliyopo au hakuna athari.
Pili, nilitaka kuelewa kwamba bwawa lile liko maeneo ya upande wa Morogoro, lakini wananchi wa pale wanategemea sana kuzalisha pamoja na mazao ya miwa na mpunga lakini na mazao mengine mbalimbali ambayo yako katika eneo lile.
Je, wasiwasi wangu uliokuweko maporomoko ya maji na mwelekeo wa maji ambayo yanashuka katika lile bwawa hayatoweza kuathiri mmomonyoko na uharibu wa lile bwawa pengine labda ikasaidia kuingia na kufanya contamination ya maji ambayo yatakuwa yanaingia katika maeneo yale.
Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu mzuri wa kilimo ambacho kitakuwa hakitumii kemikali ili kuepukana na athari za kikemikali katika maji yale ambayo wanatumia binadamu na kilimo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameomba kwamba kile cheti cha NEMC kiwasilishwe Bungeni, lakini kwa mujibu wa swali lake aliuliza, je, Serikali inaweza kuleta Bungeni ripoti ya tathmini pamoja na Environmental Impact Assessment juu ya mradi huo. Tumesema ndiyo tunaweza, sasa kama swali la pili unataka tulete basi utuagize tulete tutaleta, lakini kwa mujibu wa swali lako tumeshajibu kwamba tunaweza tukaleta.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kama ilivyojibiwa kwenye swali la msingi na Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba ripoti ya NEMC ipo na imeweka tayari na Environmental Management Plan. Kwa hiyo, hakutakuwa na athari ya aina yoyote pale ambapo kutakuwa na athari basi ripoti ile itafuatwa wataweka utaratibu kuhakikisha kwamba madhara ya aina yoyote kuhusu kemikali hayatajitokeza, madhara kuhusu mmomonyoko pia hayatajitokeza. Kwa sababu utokaji wa maji kwenye bwawa utakuwa controlled kulingana na matumizi ya kupeleka maji kwenye mashamba pamoja na kupeleka maji Mto Ruvu.