Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Salum Mwinyi Rehani (4 total)

MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-
Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ni Taasisi za Muungano na zina Ofisi Zanzibar.
(a) Je, kuna Wazanzibari wangapi watendaji katika taasisi hizo?
(b)Kama hakuna, je, Serikali haioni kuwa hakuna uwiano kwa vile taasisi hizo ni za Muungano na kwa nini kusiwe na watendaji wa pande zote mbili za Muungano baina ya pande mbili?
(c) Je, kuna mipango gani ya kufanya taasisi hizi kuwa na watendaji wa pande zote mbili hasa Ofisi ya Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Rehani, Mbunge wa Uzini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) huajiriwa kwa mujibu wa kifungu 13, 14 na 15 cha Sheria ya Vyuo Vikuu Sura ya 346 na Sura 129 ya sheria ya Baraza la Elimu ya Ufundi Tanzania pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi yaani Staff Regulatiaons pamoja na muundo wa utumishi yaani Scheme of Service wa taasisi hizo, Watanzania wote wenye sifa stahiki wanayo fursa sawa ya kuajiriwa bila kujali upande anakotoka muajiriwa. Hivyo Wizara haijaweka utaratibu wa kuwabaini watumishi kwa misingi ya maeneo wanayotoka. Aidha kwa mujibu wa sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 iliyoanzisha Baraza la Mitihani, inabainisha kuwa muundo wa bodi ya baraza inajumuisha wajumbe watatu wanaotoka upande wa Zanzibar kati ya Wajumbe wote ambao ni kumi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia utaratibu huo na kwa kutambua kwamba TCU na NACTE ni miongoni mwa taasisi zinazoshughulikia elimu ya juu na ufundi ambayo ni kati ya masuala ya Muungano na kwa kuwa Watanzania wote wana fursa na haki sawa, Serikali itaendelea kuajiri watumishi kwa vigezo vya sifa za kitaalamu ili kukidhi malengo ya utoaji huduma bora kwa jamii kama inavyostahili bila ubaguzi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa taasisi hizi zinatoa ajira kwa Watanzania wa pande zote za Muungano bila upendeleo wowote kwa kuzingatia sifa na mahitaji ya nafasi za ajira husika.
MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawatambua rasmi dereva bodaboda au bajaji kuwaandikia mikataba, kuwekewa akiba na kulipiwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na waajiri wao kwani vijana hao wameshajiajiri kwa zaidi ya asilimia 15 - 25 kwenye kila Wilaya au Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikwishakuwatambua rasmi madereva wa pikipiki (bodaboda) au bajaji tangu mwezi Aprili, 2009 ambapo pikipiki na bajaji zilikubaliwa kufanya biashara ya kusafirisha abiria kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili madareva wa pikipiki (bodaboda) au bajaji waweze kutambuliwa kwa urahisi kwa lengo la kupatiwa hduma mbalimbali zikiwemo za Hifadhi ya Jamii kutoka Serikalini na wadau wengine, Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuwahamasisha waunde vyama vyao katika ngazi mbalimbali ambapo kwa kupitia vikundi hivyo, elimu juu ya masuala ya sheria za kazi na hifadhi ya jamii hutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia matakwa ya sheria yanayomtaka mwajiri kutoka mikataba kwa mwajiriwa wake hasa ikizingatiwa kwamba, mkataba unabeba haki za kimsingi na wajibu wa kila upande.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kutoa maagizo kwa waajiri wote nchini wanaotoa ajira kwa vijana waendesha pikipiki au bajaji kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na mikataba ya kuhakikisha kuwa wanapata huduma nyingine muhimu zinazowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kwa kuzingatia usalama wa uhai wao na vyombo vyao.
MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-
Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Kidunda ambapo pia kutakuwa na miradi ya kilimo na ufugaji samaki.
• Je, kuna tathmini ya kitaalamu iliyofanyika ya kudhtibiti kemikali zinazotokana na utumiaji mkubwa wa dawa za kudhibiti magugu kwenye mashamba ya miwa na mpunga na utumiaji wa mbolea za SA ambazo husababisha uharibifu wa ardhi?
• Je, Serikali inaweza kuleta Bungeni ripoti ya tathmini pamoja na Environmental Impact Assessment juu ya mradi huo?
• Je, mradi wa umwagiliaji utachukua ekari ngapi na imepanga kulima nini katika mashamba hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Jimbo Uzini, lenye sehemu (a), (b), (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kulinga na tathmini ya athari za mazingira iliyofanyika Bwawa la Kidunda halitakuwa na athari za kikemikali za kudhibiti magugu kwenye mashamba ya miwa na mpunga kwani mashamba hayo yatakuwa upande wa chini wa bwawa yaani downstream ambapo kemikali haziwezi kurudi nyuma kuingia kwenye bwawa. Ripoti ya mazingira imeainisha athari zote zinazotarajiwa na namna ya kukabiliana nazo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaweza kuleta Bungeni cheti cha mazingira kilichotolewa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhusu mradi wa Kidunda.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Kidunda ni mahsusi kwa ajili kuhifadhi maji kwa matumizi ya majumbani na viwandani. Hata hivyo, kiasi cha maji lita milioni 432 kwa siku sawa na mita tano za ujazo kwa sekunde, yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji na shamba namba 217 la Mkulazi lenye hekta 28,000 zinazofaa kwa kilimo cha miwa na mpunga.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. SALUM MWINYI REHANI) aliuliza:-
Kambi za Jeshi za Ubago na Dunga zinawanyanyasa wananchi wa Shehia ya Kidimi kwa kuwataka waondoke katika maeneo hayo ambayo ni ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Ushirika kwa zaidi ya miaka 40 wameanza kupima na kuweka bikoni:-
Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo na hatma ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Ubago na Dunga yalipimwa mwaka 1985, kwa unyeti wake Uongozi wa Mkoa na Wilaya husika zilishirikishwa. Aidha, taratibu zote za utwaaji ardhi kwa matumizi ya umma zilitumika na kuruhusu maeneo haya kupimwa yaani Ubago na Dunga. Maeneo yote mawili tayari yamejengwa miundombinu ya Kijeshi ambayo siyo rafiki kwa matumizi mengine ya kiraia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 12 ya mwaka 1992 ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilipoanza kutumika, ramani za upimaji wote uliofanyika kabla ya 1992 zilitakiwa kupitiwa upya. Hivyo, ramani za upimaji wa maeneo ya Ubago na Dunga zilikwama kupata Hatimiliki kutokana na sheria hiyo. Hali hii ilitoa mwanya kwa wananchi kuingilia sehemu ya maeneo ya Kambi kwa shughuli za kiraia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 19 Mei, 2018 kulifanyika kikao na ukaguzi wa pamoja kati ya Wizara yangu na Waheshimiwa Mawaziri wa SMZ pamoja na Mkurugenzi wa Mipango Miji na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Zanzibar kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu wa wananchi walioko katika maeneo haya. Ukweli ni kwamba eneo hili linatumiwa na JWTZ kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya watalaam kutoka Idara ya Ardhi ya SMZ ikishirikiana na Uongozi wa Mkoa na Wilaya husika wanaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya uvamizi wa maeneo haya ili hatimaye kusaidia kufikia uamuzi kuhusu hatma ya wananchi ndani ya maeneo haya nyeti ya JWTZ.