Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jumaa Hamidu Aweso (17 total)

MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa ujenzi wa barabara ni kichocheo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi.
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Tanga - Pangani - Saadani utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, barabara hii ili tuweze kuitendea haki, tuwasiliane Wizarani ili wataalam nao watoe mchango wao ili tunapotoa tarehe ya lini itaanza iwe taarifa sahihi. (Makofi)
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Athari za mabadilko ya tabia nchi ni donda ndugu kwa Mji wa Pangani. Kwa kuwa Mji wa Pangani ni mji mkongwe ambao umejengwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi na Mto Pangani, je, ni lini Serikali itajenga ukuta wa Mto Pangani kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu na fedha zake tayari zipo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepania na penye nia pana njia. Tutaujenga ukuta huo na fedha tumekwishapata. Tunatarajia Aprili, 2016, tutaanza ujenzi wa ukuta Pangani ili kuwahakikishia wananchi wa Pangani kwamba maisha yanaendelea. Pamoja na matatizo makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi lakini vilevile maisha lazima yaendelee. Tutatumia fedha za wahisani kutekeleza jukumu hili lakini pia tutaendelea kutenga fedha zetu za ndani katika bajeti kuhakikisha wananchi wetu wanaishi salama pamoja na athari hizo kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zinajitokeza hapa nchini.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nipate fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia barabara ya Tanga –Pangani - Saadani ndipo tunapozungumzia uchumi na siasa ya Pangani. Kwa kuwa katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri imeeleza kwamba African Bank wameonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya barabara hii, je, Serikali imefikia wapi katika ufuatiliaji kuhakikisha kwamba African Bank wanatoa fedha hizi ili wananchi wa vijiji vya Choba, Pangani Mjini, Bweni, Mwela pamoja na Makorola na Sakura wanalipwa fidia ili wajue hatma ya maisha yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inakusanya mapato na Wilaya ya Pangani ni miongoni mwa Wilaya ambazo zimejaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na Mbunga ya Saadani ambayo ni pekee Afrika mbuga ambayo imepakana na bahari. Kwa nini sasa Serikali isitenge fedha zake za ndani kuhakikisha kwamba inajenga barabara hii kwa haraka ili kukusanya mapato kupitia Mbuga hii ya Saadani?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge wa Pangani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Aweso anafahamu kwamba katika maeneo ya kwanza niliyotembelea ni Pangani na ilikuwa ni ziara ya kuifuatilia barabara hii pamoja na ile gati. Anafahamu baada ya hapo Waziri wangu naye alikwenda kwa ajili ya kufuatilia barabara hii pamoja na gati. Kwa hiyo, kwa namna wananchi wa Pangani walivyotupokea tukiwa na yeye, nina uhakika wanafahamu nia yetu ya kuhakikisha barabara hii inajengwa ni ya dhati na tutahakikisha fedha hizi ambazo wenzetu wa African Development Bank wanataka kutoa tutazifuatilia. Hivi ninavyoongea, kuna kikao Zambia kuhusiana na miradi ya African Development Bank. Kwa hiyo, namhakikishia tunafuatilia na tuna uhakika hatimaye tutazipata fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu hatuwaachii African Development Bank peke yake na sisi kama Serikali tutatenga fedha, moja kwa ajili ya masuala ya fidia lakini vilevile na masuala ya ujenzi. Kuna kiwango ambacho sisi kama nchi ni lazima tutenge. Kwa hiyo, hata Tanzania kama Serikali inawajibika katika kuhakikisha barabara hii inajengwa. Namhakikishia kama ambavyo tumemwonesha na wananchi wake wameona tutalifuatilia hili mpaka lifikie mwisho.
pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na changamoto kubwa ya maji katika kata nilizoainisha lakini tumekuwa na tatizo sugu katika suala la maji katika Mji wetu Mkuu wa Pangani, na mpaka sasa nioneshe masikitiko yangu kutokana na changamoto hii ya maji, fedha zilizokuwa zimeidhinishwa katika bajeti iliyopita kiasi cha shilingi milioni 200 mpaka sasa nazungumza hazijafika.
Je, ni nini commitment ya Waziri kuhakikisha kwamba fedha zile zilizoainishwa kwa ajili ya kwenda kutatua tatizo la maji mjini, na ni lini zinapelekwa na wakati bajeti inafikia ukingoni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; Wilaya yetu ya Pangani imejaliwa kuwa na Mto Pangani ambao unatiririsha maji baharini. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inautumia mto huu kwa kuanzisha mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kutatua suala zima la maji kwa Wilaya yetu ya Pangani na Wilaya za jirani kwa maana ya Muheza na Tanga Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kilio cha Mheshimiwa Mbunge ni kweli kilio sahihi, kwa reference ni kwamba miaka miwili iliyopita nilienda na nililala mpaka katika ule Mji wa Mwera pale. Nimeweza kubaini tatizo la maji katika Mji wa Pangani, lakini kama hiyo haitoshi nikaenda mpaka Redio Pangani nikawa nina kipindi cha moja kwa moja cha kuongea na maswali ya wananchi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru wananchi wa Pangani wengi walipiga simu kusikia Mbunge wa Pangani yuko eneo lile na miongoni mwa shida ambayo waliizungumza ilikuwa ni shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ni kweli, ule Mradi wa Pangani nadhani ulianzishwa takribani pale Pangani Mjini kati ya mwaka 1963 au 1973, miundombinu yake kweli kwa idadi ya watu waliokuwa wanahudumiwa kipindi hicho kwanza imechakaa, lakini population kipindi hicho ilikuwa ni ndogo. Ndio maana katika Ofisi ya Mheshimiwa Mbunge harakati zilizofanyika ni kwamba Ofisi ya Mkurugenzi walipeleka maombi maalum katika Wizara ya Maji, walitaka shilingi milioni 400 ikiwezekana kwamba waweze kupata bajeti ya kukarabati miundombinu ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, walipata awamu ya kwanza shilingi milioni 200 kutoka Wizara ya Maji, lakini hata hivyo wanasubiria kwamba kwa sababu ule mradi wa milioni 200 umepelekwa pale Pangani Mashariki, lakini kuna maeneo mengine bado ukarabati haujafanyika ikiwemo sambamba na ukarabati wa tenki. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali imesikia hiki kilio na inalifanyia kazi ndio maana nimezungumza haya yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ni program kubwa ni kweli, haiwezekani hata kidogo eneo la Pangani ambalo Mto Pangani ni mkubwa unapoteza maji baharini, halafu wananchi wa Pangani hawapati maji! Na hili ndio maana leo hii niliongea na Mkurugenzi wa Pangani pale na ameniambia sasahivi yuko Mahakamani kuna kesi za uchaguzi zinazoendelea; nikamwambia, nini programu yake anayotaka kuhakikisha Mto Pangani unatumika?
Mheshimiwa Naibu Spika, amekiri kwamba, sasahivi wanafanya utafiti na inaonekena gharama ya shilingi bilioni 10 nadhani itahitajika kwenye mradi ule, lakini bado iko katika suala zima la tathmini, lakini hili niseme ni nini! Ni kwamba Wizara ya Maji nayo ilisema kwamba sasa wataenda kutumia kama Serikali tutaenda kutumia vyanzo vyote vinavyowezesha kutumia maji. Imani yangu ni kwamba Mto Pangani tunaweza kuutumia katika sekta ya maji hasa Programu ya Awamu ya Pili ya Maji ambayo tunaenda kuibua suala zima la kutatua tatizo la maji kwa wananchi wetu wa Tanzania.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Wilaya ya Pangani imepakana na Mji wa Zanzibar na wakazi wa Pangani wamekuwa wakijishugulisha na Mji wa Zanzibar kutokana shuguli za kijamii na kiuchumi. Je, ni lini Serikali itatupatia usafiri wa uhakika ili wakazi wa Pangani na wananchi wa jirani Muheza na maeneo ya Kilimanjaro na Arusha ili waweze kunufaika na usafirishaji huu kwa unafuu ili kuweza kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumewahi kutamka ndani ya Bunge lako Tukufu kwamba, iliyokuwa TACOSHIL tuliipaki kwa sababu tulikuwa tunatarajia sekta binasi ndiyo ijihusishe zaidi katika kutoa huduma za usafiri wa majini katika Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana bado kuna kilio cha wengi na vile vile, hata jana nilikuwa na wateja wengine Dar es Salaam nao wanasisitiza kwamba, pengine tuangalie upya suala la TACOSHIL au tuseme huduma za meli kwenye upende wa Bahari kwamba na Serikali nayo ijihusishe kwa sababu kuna baadhi ya maeneo hayawezi kuendeshwa na sekta binafsi kwa faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaliangalia ndani ya Serikali, tuangalie kama kuna umuhimu wa kubadilisha sera hiyo na kama tutaona kwamba, hakuna umuhimu badala yake tuendelee kuhamasisha wawekezaji binafsi tutafanya hivyo. Kama tutaona kuna umuhimu tutaleta hapa tufanye maamuzi kwamba, labda turudishe ule uamuzi au yale masuala ambayo tulikuwa tunayafanya miaka ya nyuma chini ya TACOSHIL.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, kwa kuwa tatizo la Mazingira magumu kwa Jeshi la Polisi linafanana kabisa na Jimbo la Igalula, je, ni lini Naibu Waziri atafika katika Jimbo la Pangani kuhakikisha kwamba tunaenda kuangalia manyanyaso askari wanayopata katika Jimbo langu la Pangani hususan katika suala zima la makazi, pamoja na kituo kibovu cha Jeshi la Polisi?
Kwa hiyo, nilikuwa nataka commitment ya Naibu Waziri yupo tayari kushirikiana na mimi kwenda Pangani kuhakikisha kwamba akaone hali halisi ya Manyanyaso wanayoyapata Jeshi la Polisi wa Pangani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari, kwa hiyo, baada ya kikao hiki tupange ratiba.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Rufiji yanafanana kabisa na Jimbo langu la Pangani katika sekta ya kilimo na uvuvi. Nataka nijue ni lini Serikali itakuwa tayari kuwakumbuka wavuvi pamoja na wakulima wa zao la korosho katika Jimbo langu la Pangani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa changamoto za Pangani zimefanana kwa kiasi kikubwa na Rufiji na nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama alivyosikia kwenye wasilisho la Wizara ya Fedha kuhusu bajeti ya Serikali, korosho ni moja kati ya mazao ambayo tayari tuna mkakati mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata ahueni. Mmesikia tunaondoa tozo tano ambazo zimekuwa za usumbufu mkubwa kwa wananchi wetu. Tunategemea kwamba bei ya korosho itaendelea kuimarika na kuwa nzuri kwa sababu tayari tozo ambazo zilikuwa ni kero ziko mbioni kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie kwamba hata kuhusu uvuvi, nina hakika alifuatilia tulipowasilisha bajeti yetu, tumeweka mikakati mizuri sana ya kuhakikisha wavuvi wetu wananufaika na mipango mbalimbali ya Serikali ukiwepo mpango wa kutoa mikopo kwa ajili ya vikundi vya wavuvi, kutoa elimu kuhusu uvuvi mzuri lakini kuwasaidia wavuvi wetu kuweza kupata nyenzo za uvuvi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba wananchi wa Pangani katika uvuvi lakini vilevile katika kilimo hawajasahauliwa na Serikali. Hata hivyo, kwa sababu ni Mbunge makini na mara nyingi sana tumeongea naye, nimhakikishie tu kwamba kwa yale ambayo anafikiri tunahitaji kuelekeza nguvu zetu zaidi, naomba tukutane naye na ikibidi niko tayari kuandamana naye kwenda Pangani tukaangalie changamoto zilizopo.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa umeme ni kichocheo muhimu katika shughuli za kiuchumi. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Langoni, Kikokwe pamoja na Kigulusimba Misufini ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Pangani wanaenda kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kujiletea maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa hata sasa hivi bado Serikali inapeleka umeme kwenye vijiji vingi chini ya mradi wa REA awamu ya pili. Hata hivyo, kuna vijiji vingi havijapata umeme. Jimbo la Mheshimiwa la Pangani tunalifahamu, ni vijiji vichache sana vimepata umeme. Nimeshazungumza naye na nikamwambia alete orodha yake ya vijiji ambavyo havijapata umeme na ameshaniletea. Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge wa Pangani vijiji vyake vyote alivyovitaja vitapata umeme kwenye REA awamu ya tatu.
MHE. JUMA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya kumuuliza. Mimi kama Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Pangani sikubaliani na majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kusema kwamba mazungumzo yanaendelea, ilhali wananchi wangu wakitaabika. Tunapozungumzia suala la X-Ray, tunazungumzia uhai wa wananchi wa Jimbo langu la Pangani. Leo wananchi wanatoka Muhungulu, Mkalamo wanafuata huduma ya X-Ray Tanga Mjini.
Sasa nataka nijue ni nini nguvu ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inatupatia fedha za dharura ili X-Ray hii ipatikane kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pamoja na changamoto ya ukosefu wa X-Ray bado Hospitali yetu ya Wilaya imekuwa na changamoto lukuki za ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi baada ya Bunge kuhakikisha kwamba, tunaenda kukabiliana na changamoto ambazo Hospitali yetu ya Wilaya inakabiliana nazo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lolote haliwezi kukamilika bila ya mazungumzo, ndiyo maana halmashauri pale imefanya utaratibu wa kupata hii milioni 70 kutoka NHIF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba, utaratibu uliowekwa na halmashauri yake na yeye mwenyewe akiwa mjumbe wa Baraza la Madiwani; na nikijua kwamba yeye ni kijana mahiri anapambana sana juu ya suala la afya katika eneo lake; sisi tuta-fast track hiyo process ya kupata X-Ray haraka ili wananchi wa Pangani ambao kwa muda mrefu anawapigania waweze kupata huduma ya afya, lakini nimpongeze sana katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongozana na Mheshimiwa Mbunge, naomba nimwambie kwamba, niko tayari. Baada ya Bunge, mpango wangu ni kutembelea Mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani na Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, tutafika Pangani na tutakagua eneo hilo. Hali kadhalika tutakagua kituo cha afya ambacho wanaendelea kukijenga ili tuone namna ya kukusanya nguvu za pamoja za kuhakikisha kwamba, wananchi wa Wilaya ya Pangani wanapata huduma ya afya.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, tatizo la ukosefu wa Chuo cha Ufundi katika Wilaya ya Geita inafanana kabisa na Wilaya yangu ya Pangani. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba inatujengea Chuo cha Ufundi kwa sababu vijana wa Pangani wanashindwa kunufaika na rasilimali zilizopo katika Wilaya yangu ya Pangani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa Wilaya nyingi, ambazo zina uhitaji mkubwa wa kuhitaji kupata vyuo hivi vya VETA, niseme tu kwamba, tayari bajeti ya mwaka huu Waheshimiwa Wabunge wote mnayo na vyuo vitakavyotekelezwa vimo. Kwa hiyo, kama Wilaya yoyote ile imo katika orodha ya vyuo vinavyoanza kutekelezwa, basi ajue kwamba tupo katika kutekeleza mpango huo na kama haipo basi tunaendelea na michakato ya kupata ardhi ili na vyenyewe viweze kuwa katika mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumegundua kwamba kwa muda mrefu fedha ambazo zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya vyuo imekuwa ni kidogo, mwaka huu baada ya kutembelea na kuona huu uhitaji mkubwa tulichojifunza ni kuongeza maeneo hayo ya bajeti katika vyuo vyetu hasa hivi vyuo vya ufundi vya Wilaya.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la minazi ndiyo uchumi na ndiyo maisha ya wananchi wa Pangani. Ukisoma majibu ya sasa wamefanya tafiti lakini hawajajua mdudu ambaye anaeneza ugonjwa huo na wala hakuna tiba kama UKIMWI. Kwa kuwa, mnazi ndiyo uchumi, je, Serikali haioni haja sasa ya kuangalia nchi ambazo zinalima zao hili la mnazi kwa wingi ili kupata ushauri kujua namna gani tunaweza kuokoa zao hili la mnazi. (Makofi) Swali la pili; naomba sasa nipate commitment ya Waziri kwa kuwa tunaona jitihada zinazofanyika mpaka sasa hakuna majibu sahihi yaliyoweza kupatikana. Je, ili kuweza kuwaokoa wananchi wa Pangani kuondokana na umaskini kwa nini wasitupe zao mbadala ili kuhakikisha kwamba badala la mnazi tuwe na zao ambalo linakimu maisha ya wananchi wa Pangani? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba imechukua muda mrefu sasa mdudu anayeambukiza ugonjwa huo kuweza
kufahamika, lakini zaidi tiba kuweza kupatikana. Wizara na Serikali inaendelea kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na
Kimataifa ili kuangalia namna ya kutafuta tiba ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, tunashirikiana na Taasisi za nchi zinazoongoza kwa kuzalisha minazi kama nchi za Indonesia,
Ufilipino, India na Brazil ili kuangalia namna gani ya kuhakikisha kwamba ugonjwa huu tunautokomeza kama nilivyosema. Kwa sasa tunaangalia namna ya kudhibiti ili usiweze kuleta madhara makubwa zaidi wakati tunaendelea kutafuta tiba.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Serikali kutafuta zao mbadala; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali na Wizara inafahamu jitihada ambayo yeye pamoja na Mheshimiwa DC Zainab Abdallah wa Pangani wanafanya katika kuleta zao la korosho Pangani. Nilipotembelea Pangani miezi michache iliyopita niliona
jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na DC na Halmashauri ili kujaribu kuwashawishi na
kuwahimiza wananchi wapande mikorosho kama zao mbadala wakati Serikali inaendelea kutafuta tiba ya ugonjwa
wa minazi.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea kuangalia namna gani tunaweza tukahimiza matumizi ya mazao mbalimbali yanayozalishwa na mnazi. Kwa sababu mnazi ndiyo zao la pekee duniani ambalo hakuna chochote
ambacho hakitumiki, kuanzia mizizi mpaka matunda yote inatumika. Kwa hiyo, tunajaribu kuhimiza kwa mfano
uchakataji wa mbata ili kuweza kutengeneza mafuta ya kupikia na kujipaka. Waheshimiwa Wabunge mnafahamu kwamba mafuta ya nazi hayana lehemu katika maana ya cholesterol wala hayana mzio katika maana ya allergy. Kwa hiyo, tunaangalia uwezekano wa kuendelea kutumia products za mnazi kama njia mojawapo ya kuwasaidia wakulima wa minazi.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Aweso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi athari zake zimeonekana wazi wazi katika Mji wa Pangani. Serikali pamoja na jitihada kubwa wanazozifanya kukarabati ukuta wa Pangani, lakini bahari imekula kwa kiasi kikubwa kwa eneo la Pangadeco; je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya haraka kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa ukuta kwa eneo la Pangadeco?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini katika eneo lililobaki la Pangani ambalo kwa jina maarufu Pangadeco katika mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018. Serikali itafanya tathmini ya eneo hilo na kutafuta namna bora tutakayoitumia, aidha kujenga ukuta au njia nyingine.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa Mikoa ambayo imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Je, Serikali ina mkakati gani ya kufufua na kuwekeza viwanda vipya? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuwa na uwezo hili swali nisingelijibu, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ananilazimisha nisome hotuba ya bajeti yangu kabla ya muda na shughuli ni kesho kutwa. Nimejipanga kwa ajili ya Tanga na Jumatano nitawaonesha. (Makofi)
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Ili kuboresha sekta hii ya utalii ni pamoja na kuboresha miundombinu yake. Ukiangalia hii mbuga ya Saadani barabara ambayo inaifikia mbuga ile ni mbovu na haipitiki kwa muda wote. Je, Wizara hii haioni haja sasa ya kukaa na Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba inaijenga barabara hii ya Tanga - Pangani - Saadani ili watalii waweze kufika kwa urahisi?Ahsante sana.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli ili utalii uweze kwenda sawasawa, ili tuweze kupata idadi kubwa ya watalii, ili watalii wakija waweze kufurahia kuwepo kwenye hifadhi zetu na kwenye maeneo yetu ya vivutio, wakae muda mrefu zaidi ili waweze kutumia fedha zaidi na kuweza kuboresha pato zaidi ni lazima mazingira hapo ambapo tumeweka vivutio yawe bora zaidi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya usafiri lakini pia hata malazi. Upande wa malazi kwa kiwango kikubwa hili ni eneo ambalo linafanywa au linatekelezwa na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu kama barabara ukweli ni kwamba eneo hili linatekelezwa na Serikali, lakini pia hata ndani ya Serikali, barabara zile ambazo zinaelekea kwenye hifadhi kutoka kwenye maeneo mengine ya miji jirani, hizi ni barabara ambazo zinatekelezwa kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwa upande wa barabara ambazo ziko ndani ya hifadhi, kwa mfano barabara zilizoko ndani ya Hifadhi ya Saadani, hili ni jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara pamoja na matengenezo yake ya kuweza kuzifanya zipitike hili ni jukumu ambalo linafanyika na Wizara kwa kupitia Shirika la TANAPA ambalo ni Shirika la Hifadhi za Taifa. Katika bajeti ya mwaka huu TANAPA wametenga fedha kama ambavyo tunatenga kila mwaka kazi yake ni kuboresha miundombinu kwa maana ya kuboresha iweze kupitika mwaka mzima hata msimu wa mvua, lakini pale ambapo inawezekana kupasua barabara mpya kutegemeana na bajeti na uwezo wa kifedha, basi utekelezaji wa mradi huo utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara aliyoitaja ya Tanga – Pangani – Saadani, hii ni barabara ambayo tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na hasa pale ambapo bajeti itakuwa imeweza kuruhusu.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Napozungumzia ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani, nazungumzia uchumi na maisha ya wananchi wangu wa Jimbo la Pangani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii ni ahadi ya muda mrefu na ujenzi wake umekuwa wa kusuasua yaani ahadi hii tangu mimi sijazaliwa mpaka sasa hivi nimekuwa Mbunge. Kwa kuwa Serikali imesahatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya Tanga – Pangani – Saadani, nini kinachokwamisha kuanza kwa ujenzi wa barabara hii na wananchi wangu kulipwa fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba inajenga barabara ya Tanga – Pangani – Saadani, yapo maeneo korofi ambayo yanasababisha matatizo na usumbufu kwa wananchi wangu, mfano ni eneo la kutoka Mkwaja kwenda Mkaramo, Tundaua kwenda Kirare.
Je, Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi na wa haraka ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yanarekebishwa ili wananchi wangu wasipate tabu kwa muda huu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika swali la msingi, barabara hii imetengewa fedha shilingi milioni 4,435. Nimhakikishie tu hiyo ndiyo dalili njema, huo ndiyo ushahidi kwamba sasa Serikali imedhamiria kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara hii ni pamoja na kuwalipa fidia wale wote wanaostahili fidia namna barabara hii itakavyopita.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Pangani na wengine ambao wanaguswa na barabara hii, dhamira ya Serikali ya kuijenga barabara hii iko palepale na tumeshaanza na tunatarajia muda si mrefu washirika wa maendeleo pamoja na African Development Bank kwa namna mazungumzo yanavyoendelea tutakuja kuongezewa fedha ili tukamilishe kazi hiyo kwa umakini unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kipande cha Mkaramo hadi Mkwaja, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Meneja wetu wa TANROADS Mkoa wa Tanga ataliangalia hili alete taarifa yake, gharama ya kurekebisha hiki kipande kidogo ili mawasiliano yawepo katika muda wote wa mwaka.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa kuondoa kodi katika zana hizi za uvuvi. Kitu ambacho nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri pamoja na kuondoa kodi na kuleta tozo kwa asilimia 40 kwa wavuvi wa Pangani lakini Serikali haikuwa wazi ni namna gani au utaratibu gani ambao unatakiwa ufuatwe na vifaa hivi vinapatikana wapi ili wavuvi hawa hususani wa dagaa waweze kupata zana hizo kwa ukaribu na rahisi?.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri Serikali ina mkakati gani wa kujenga bandari ya uvuvi hususani katika ukanda huu wa Pwani ya Mkoa wa Tanga kwa mantiki ya meli kubwa zinazovua bahari kuu kwa maana ya kuhaulisha, kuuza na kutoa takwimu sahihi kuhusu suala zima la uvuvi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na utaratibu unaotakiwa kufuatwa ili wavuvi waweze kupata punguzo katika zana za uvuvi, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kimsingi wavuvi wake wanaotaka kupata ruzuku ya vyombo vya uvuvi wanatakiwa wajiunge katika vikundi, lakini vilevile wachangishane fedha, wakishakuwa na fedha ya kununua kwa mfano injini ya boti wanawasilisha maombi yao Halmashauri ambao watawaelekeza namna ya kupata zile zana halafu Serikali itachukua asilimia 40 ya gharama ya chombo ambacho wanataka kununua. Mheshimiwa Aweso kwa sababu ni Mbunge kijana ambaye amekuwa akihangaikia sana wananchi wake kwa muda mrefu sana, nimuahidi tu kwamba kama anataka kupata ufafanuzi mzuri zaidi hata leo mchana anaweza akaja ofisini kwangu tukaongea ili wananchi wake wasiendelee kuchelewa kupata huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari ya uvuvi, wakati tunawasilisha bajeti yetu tulitoa maelezo marefu sana kuhusiana na mikakati mbalimbali ambayo kama Serikali tumeweka ili kuendelea kuboresha namna ya nchi kunufaika na uvuvi katika bahari kuu. Moja ya mikakati hiyo ambayo tulisema ni pamoja na kuanza na mchakato wa kujenga bandari ya uvuvi. Katika bajeti ya mwaka unaokuja, Wizara imetenga fedha za kufanya upembezi yakinifu ili tuweze kujua ni mahali gani hasa ambapo panafaa kuweka bandari ya uvuvi. Bandari ya uvuvi yenyewe gharama za awali ambazo tumekadiria tunafikiri inaweza ikagharimu zaidi ya…
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la maji Pangani ni kubwa na kwa kuwa katika Wilaya yetu ya Pangani tumejaliwa kupitiwa na Mto Pangani katikati ya Mji wa Pangani. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuutumia Mto Pangani ili kuondoa tatizo la maji katika Mji wa Pangani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa unawahudumia sana wananchi wako kwa sababu juzi umekuja ofisini, tumezungumza na tukaelekeza hatua za haraka uwasiliane na watu wa DDCA na Mhandisi aliniahidi kwamba katika muda wa wiki mbili atanipa majibu ili tufanye kwanza hatua za dharura. Lakini pia tunaendelea kutumia Mto Pangani ili tuhakikishe kwamba tunawapatia maji watu wa Pangani bila wasiwasi wowote Mheshimiwa Mbunge.