Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juma Othman Hija (10 total)

MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Katika Jimbo la Tumbatu kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa amani kwa wananchi wanaoishi katika kisiwa hicho na katika hali ya namna hiyo inaporipotiwa kwa Jeshi la Polisi inakuwa tabu kwenda kwa haraka kwenye eneo husika kwa sababu kadhaa ikiwemo ya ukosefu wa usafiri:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Kituo cha Polisi katika kisiwa hicho na kuwapatia usafiri wa uhakika kwa kuzingatia jiografia ya maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo matukio ya kihalifu yanayoripotiwa kutokea katika Kisiwa cha Tumbatu. Jeshi la Polisi linafanya jitihada za kukabiliana na uhalifu kwa kutoa huduma za ulinzi na usalama katika maeneo ya Kisiwa cha Tumbatu kwa kila siku kuwapeleka Askari wa doria ili kuimarisha ulinzi. Kwa sasa lipo boti lenye uwezo wa kubeba Askari 10, iwapo uwezo wa kifedha ukiongezeka hitaji letu ni kupata boti kubwa la mwendo kasi lenye uwezo wa kubeba Askari zaidi ya 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona haja ya kuwepo Kituo cha Polisi katika eneo hilo, ili kusogeza huduma za ulinzi na usalama na hali halisi ya kisiwa hicho kilichozungukwa na bahari na uwepo wa matukio ya uhalifu. Katika kutekeleza hilo tayari Serikali imepata kiwanja na makisio ya ujenzi wa kituo hicho yanaendelea. Aidha, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu inapenda kuhamasisha wadau werevu na wananchi, akiwemo Mheshimiwa Mbunge, kutoa msaada wa hali na mali katika ujenzi wa kituo hiki.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Vipo baadhi ya vyuo binafsi vinalipisha wanafunzi ada kwa kutumia pesa za kigeni badala ya pesa za Kitanzania. Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti usumbufu huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya nyuma yalikuwepo malalamiko kuhusu baadhi ya vyuo vya binafsi kutoza ada kwa fedha za kigeni. Kifungu cha 48(1) cha kanuni zinazosimamia utoaji wa elimu katika vyuo vikuu yaani The Universities General Regulations, 2013 kinakataza kuwatoza ada wanafunzi wa Kitanzania kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vinaruhusiwa kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wananfunzi wasio raia wa Tanzania kama inavyobainishwa katika kifungu cha 48(2) cha kanuni tajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo napenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wamiliki wa vyuo binafsi kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kupewa onyo, kuvifungia na kutoruhusiwa kudahili wanafunzi.
MHE. JUMA OTHMANI HIJA aliuliza:-
Kumekuwa na matukio yasiyo ya kawaida na kukaribia kuhatarisha amani katika Kisiwa cha Tumbatu:-
Je, Serikali haioni ipo haja ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kisiwa hicho ili kukabiliana na matukio ya kiuhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO NA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yako matukio ya kihalifu yanayoripotiwa kutoka katika Kisiwa cha Tumbatu na Jeshi la Polisi linafanya jitihada ya kukabiliana na wahalifu kwa kutoa huduma za ulinzi na usalama katika kisiwa hicho kwa kufanya doria kila siku. Pamoja na doria, kumeanzishwa utaratibu wa detach ambapo askari wanakwenda kulinda kisiwa hicho na kubadilishana kwa zamu ili kuimarisha ulinzi. Aidha, ipo boti yenye uwezo wa kubeba Askari kumi. Iwapo uwezo wa kifedha ukiongezeka tutajitahidi kupata boti kubwa ya mwendo kasi na yenye uwezo wa kubeba Askari zaidi ya kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona haja ya kuwepo Kituo cha Polisi katika Kisiwa cha Tumbatu ili kusogeza huduma za ulinzi na usalama kwa kuzingatia jiografia ya kisiwa hicho na matukio ya uhalifu. Katika kutekeleza hilo, tayari Serikali imepata kiwanja chenye ukubwa wa mita za mraba 600 na makisio ya ujenzi wa kituo hicho umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu naomba kutumia fursa hii kuhamasisha wadau na wananchi akiwemo Mheshimiwa Mbunge kushirikiana kuanza ujenzi wa kituo hiki wakati Serikali inakamilisha mipango yake ya kupata fedha.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa hotuba ya bajeti 2016/2017 Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilionesha kuwa Serikali ya India imesaidia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya uimarishaji wa huduma ya maji nchini.
Je, Serikali inaweza kutueleza juu ya utekelezaji wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Jimbo la Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara yangu ilitoa taarifa ya mchango mkubwa inaoupata kutoka Serikali ya India ili kuboresha huduma ya maji nchini. Kwa kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India, awamu ya kwanza Serikali ya Tanzania ilipata dola za Kimarekani millioni 178.125.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zilizotekelezwa katika awamu ya kwanza ni mradi mkubwa wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, ujenzi wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara, ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa mradi wa Chalinze-Wami awamu ya tatu. Utekekelezaji wa kazi ya upanuzi wa ruvu juu na ulazaji wa bomba kutoka Mlandizi hadi Kimara umekamilika na miradi ya ujenzi wa mfumo wa usambazji maji kwa Jiji la Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa mradi wa Chalinze-Wami awamu ya tatu inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya pili, Serikali ya India itatoa fedha dola za Marekani milioni 268.35 kwa ajili ya mradi mkubwa wa kutoa maji katika mradi wa KASHWASA kutoka kijiji cha Solwa kwenda katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Tinde na Uyui pamoja na vijiji 89 vinavyopitiwa na bomba kuu umbali wa kilometa 12 kila upande, wakandarasi wa kutekeleza mradi huo wamepatikana na wapo katika hatua ya maandalizi ya utekelezaji (mobilization).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya tatu Serikali ya India imeahidi kutoa fedha kiasi cha dola milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 16 ya Tanzania Bara pamoja na miradi ya maji upande wa Zanzibar. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kufanya manunuzi ya Mhandisi Mshauri atakayefanya mapitio ya usanifu wa miradi na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi, kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa, lakini katika baadhi ya maeneo, miundombinu inayotumika hasa nguzo hairidhishi.
Je, Serikali inaweza kutuambia ni viwango gani (standards) vinavyotumika katika utafutaji wa nguzo hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini, Serikali imekuwa ikihimiza na kuzingatia ubora wa vifaa vinavyotumika hasa nguzo. Nguzo zinazotumika kwenye miradi hiyo hununuliwa kutoka viwanda mbalimbali vya hapa nchini na awali baadhi zilikuwa zinatoka nje ya nchi.
Wakati wa ununuzi Shirika la Umeme nchini TANESCO hutoa viwango vya ubora wa nguzo kwa viwanda vinavyohitajika na vinavyozingatia viwango vya kimataifa. Kwa kuzingatia viwango hivyo, nguzo kwa ajili ya usambazaji na usafirishaji wa umeme zinatakiwa kuwa na urefu kati ya mita tisa hadi 18 na kipenyo kati ya milimita 130 hadi 308.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazalishaji hutumia dawa bora kuzalisha nguzo hizo na TANESCO hufanya ukaguzi kabla ya kuanza kutumika ili kujiridhisha katika ubora wake.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Wataalam wa Afya wanaeleza kuwa mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini hana ugonjwa wa UKIMWI:-
Je, nini maana ya maelezo haya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Jimbo la Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini hana ugonjwa wa UKIMWI. Maana yake ni kuwa, mtu atakuwa na ugonjwa wa UKIMWI pale ambapo kinga zake zinapokuwa zimeshuka sana na hivyo kuanza kupata magonjwa nyemelezi ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha kuwa na virusi vya UKIMWI bila kuonyesha dalili za ugonjwa wa UKIMWI kawaida kinaweza kuchukua muda mrefu kuanzia miaka mitano hadi kumi zaidi tangu mtu apate maambukizi ya virusi vya UKIMWI. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Mradi wa kupeleka Umeme Vijijini (REA) ni mradi ambao unaendelea kwa kasi kubwa nchi nzima.
Je, Serikali inaweza kutuambia ni kwa kiasi gani umeme huu umesambazwa nchi nzima (coverage) tangu mradi huu ulipoanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imekamilisha utekelezaji wa Mradi wa REA I ambapo utekelezaji wake ulijumuisha ujenzi wa miundombinu ya umeme wa msongo wa kilovoti 11/33 wenye urefu wa kilometa 1,700; umeme wa msongo wa kilovoti 0.4/0.23 wenye urefu wa kilometa 800 na ufungaji wa transfoma 386. Jumla ya vijiji 231 vilipatiwa umeme na jumla ya wateja 22,100 waliungan`ishiwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mradi wa REA II ulijumuisha ujenzi wa miundombinu ya umeme wa msongo wa kilovoti 11/33 wenye urefu wa kilometa 17,740; ujenzi wa umeme wa msongo wa kilovoti 0.4/0.23 wenye urefu wa kilometa 10,970; ufungaji wa transfoma 4,100 za ukubwa tofauti na kuvipatia umeme vijiji 2,500 na kuunganishia umeme kwa jumla ya wateja 178,641 ambao ni sawa na asilimia 71.46 ya matarajio ya wateja 250,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa azma ya Serikali ni kupeleka umeme katika vijiji vyote kufika mwaka 2020/2021, Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) mwezi Julai 2017 ilianza kutekeleza mradi wa REA III kupitia grid extension na Densification itayopeleka umeme maeneo ambayo yaliyorukwa katika utekelezaji wa REA I na II.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuunganisha umeme maeneo ya pembezoni mwa miji (Peri-urban, electrification program), kusambaza umeme katika vijiji vyote ikiwa ni pamoja vilivyo pembezoni mwa mkuza wa njia ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga na utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu. Utekelezaji wa miradi ya REA III kwa mzunguko wa kwanza unajumuisha ufunguji wa miundombinu ya umeme ya msongo wa kilovoti 11/ 33 yenye urefu wa kilometa 16,420; njia za umeme wa msongo wa kilo vote 0.4 lenye urefu wa kilometa 15,600; ufungaji wa transforma 6,700 na kuvipatia umeme vijiji zaidi 3,559 na kuwaunganisha wateja 300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Machi utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme vijijini nchini umechangia kufikia matumizi jumla ya umeme nchini (overall access) kufikia asilimia 67.5 kwa vijijini ambapo vijijini ni asilimia 49.5 kutoka asilimia mbili iliyokuwepo wakati wakala unaanza kutekeleza majukumu yake mwaka 2007 na mijini ni asilimia 97.3.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuandaa rasilimali watu ili kufanikisha azma nzuri ya uchumi wa viwanda kwa nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutoa fursa sawa ya elimu kwa wote Serikali mpaka sasa inatumia takribani shilingi bilioni 23.85 kwa mwezi sawa na shilingi trilioni 1.14 kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne yaani elimu bure. Pia kutoa ruzuku pamoja na mikopo ya takribani trilioni 1.81 kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 kwa wanafunzi wa taasisi ya elimu ya juu ili kuwandaa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Sekta za Vipaumbele kwa Vijana ambapo kwa sehemu kubwa mafunzo hutolewa kwa vitendo mahali pa kazi. Programu hii hutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utatu yaani Serikali, vyama vya waajiri na sekta binafsi na vyama vya wafanyakazi. Utekelezaji wa programu hiyo ulianza mwaka wa fedha 2015/2016 kwa kutumia mifumo ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo kwa vitendo mahali pa kazi kwa njia ya mafunzo ya kukuza ujuzi kupitia wanangezi (apprenticeship), kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio rasmi wa mafunzo (recognition of prior learning skills), mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu (internship) na mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar pia kupitia Kituo cha Kulelea Wajasiriamali (Entrepreneurship Incubation Centre) kilichopo chini ya Wizara ya Kazi baadhi ya vijana, makundi ya walemavu na watu wenye uhitaji maalum, hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali, ambapo Taasisi ya COSTECH iliwawezesha jumla ya shilingi milioni 206 ili kuanzisha kituo hicho na mpaka sasa jumla kimewanufaisha wajasiriamali 875 wengi wao wakiwa ni vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kulingana na mahitaji ukiwepo ujuzi wa uzalishaji viwandani kuhakikisha nchi yetu inajitosheleza hatua kwa hatua katika eneo hili. Napenda kutoa wito kwa vijana kujitokeza na kushiriki katika fursa hizo za mafunzo.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-

Thamani ya Shilingi ya Tanzania inaendelea kuporomoka kila siku, kuporomoka huko kunachangia kwa kiasi fulani ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida katika kupanga mipango yao ya kimaisha:-

Je, Serikali ina mkakati gani ya kudhibiti mporomoko huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine hutegemea nguvu za soko, yaani ugavi na mahitaji. Sababu za kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni ni pamoja na tofauti ya mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi wabia katika biashara, mauzo kidogo nje ya nchi, mahitaji makubwa ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje; kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje; kuimarika kwa fedha za kigeni kutokana na kuimarika kwa uchumi wa nchi wabia katika biashara na kuzuka kwa biashara ya kuhisia na kuotea ya sarafu za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sababu zote hizi hazikuwepo na hivyo thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Marekani ilikuwa tulivu ikilinganishwa na sarafu nyingine dhidi ya Dola ya Marekani. Kwa mfano, thamani ya shilingi ilipungua kwa wastani wa 2% kwa mwaka 2017/2018 na 2016/2017 ikilinganishwa na wastani wa 22% mwaka 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiujumla shilingi ilikuwa imara ikilinganishwa na sarafu nyingine kama vile Franc ya Rwanda iliyopungua kwa wastani wa 5% na shilingi ya Uganda iliyoshuka kwa 3.8% katika kipindi kama hicho. Utulivu wa thamani ya shilingi ulitokana na utekelezaji thabiti wa sera za fedha na bajeti pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni, Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:-

(i) Kuhakikisha kuwa ongezeko la ujazi wa fedha linaendana na ukuaji wa shughuli za uzalishaji;

(ii) Kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma ndani ya nchi;

(iii) Kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, na;

(iv) Kudhibiti hali ya wasiwasi katika soko la fedha za kigeni inayosababishwa na hisia pamoja na biashara ya kuotea ambapo Benki Kuu hununua na kuuza fedha za kigeni katika soko la jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba jukumu la kuimarisha thamani ya shilingi ni shirikishi na pia lina wadau wengi na hivyo kila mmoja anahitajika kushiriki kwa nafasi yake ili kuleta mafanikio kwa nchi. Aidha, wadau wakuu ni Serikali pamoja na wananchi. Serikali ina majukumu makuu mawili:-

(i) Serikali kupitia Benki Kuu ina jukumu la kutekeleza na kusimamia Sera ya Fedha ili kudhibiti mfumuko wa bei, viwango vya kubadilisha fedha na ujazi wa fedha katika soko; na

(ii) Kuandaa na kusimamia sera thabiti za kibajeti, kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu na kujenga miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuchochea uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wananchi ambao ndio wawekezaji, wana jukumu la kuzalisha kwa wingi bidhaa na huduma mbalimbali hususan zile zinazoipatia nchi fedha za kigeni na/au zinazoipunguzia nchi mzigo wa mahitaji ya fedha za kigeni.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA Aliuliza:-

Miongoni mwa malengo ya Benki ya TPB ni kupeleka huduma ya kibenki kwenye maeneo ya vijijini na pembezoni ambayo hayafikiwi na huduma hizo:-

Je, ni kwa kiasi gani lengo hilo limefikiwa mpaka kufikia mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa malengo ya Benki ya TPB ni kupeleka huduma za kibenki na pembezoni mwa miji, kuongeza wigo na mtadao wa biashara ya benki ya kutumia teknolojia ya kisasa.

Katika kutekeleza malengo haya, Benki ya TPB imefanikiwa kuboresha huduma za kibenki kupitia mtandao wa ofisi 200 za Shirika la Posta Tanzania zilizopo katika kila wilaya na baadhi ya tarafa na kutumia teknolojia ya habari na mifumo ya kisasa kutoa huduma za kibenki ikiwemo simu za kiganjani (TPB POPOTE), mawakala wa kampuni za simu, mashine za POS pamoja na ATM katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Benki ya TPB imefanikiwa pia kuongeza idadi ya matawi makubwa kutoka 30 kwa mwaka 2017 hadi 36 mwaka 2018 na matawi madogo
yaliyoongezeka kutoka 37 mwaka 2017 hadi kufikia 40 mwaka 2018. Idadi hii ya matawi inahusisha matawi ya iliyokuwa Benki ya Twiga na Benki ya Wanawake Tanzania. Matawi yote yameunganishwa kwenye mfumo wa TEHAMA unaowawezesha wateja kupata huduma za kibenki bila kutembelea matawi walipofungulia akaunti zao.

Mheshimiwa Spika, vituo vya huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta viliongezeka kutoa 40 mwaka 2017 hadi kufikia 45 mwaka 2018. Aidha mashine za ATM ziliongezeka kutoka 51 mwaka 2017 hadi kufikia 72 mwaka 2018. Vilevile, mawakala wa SELCOM POS waliongezeka kutoka 225 kwa mwaka 2017 na kufikia 670 Desemba, 2018. Vituo vyote vua huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta vimeunganishwa pia kwenye mtandao na mfumo wa TEHAMA wa benki na hivyo kutoa fursa kwa wateja wa vijijini na pembezoni mwa miji kupata huduma kwa wakati kama ilivyo kwa wateja wengine wanaohudumiwa na matawi makubwa na madogo.

Mheshimiwa Spika, jumla ya akaunti 227,052 zilifunguliwa na wananchi wa vijijini na pembezoni mwa miji kwa kutumia mfumo wa kutoa huduma za kibenki kwa njia ya simu za kiganjani, ujulikanao kama TPB POPOTE. Mfumo huu wa TPB POPOTE unasaidia wananchi kufanya malipo mbalimbali kama kuhamisha salio, kutuma fedha, kulipa ankala za maji, kununua umeme wa luku na kununua vocha za simu bila kulazimika kwenda katika matawi ya benki ya TPB. Wateja wanaweza pia kuhamisha salio kwenda katika akaunti nyingine, kuhamisha fedha kwenda katika akaunti zao za M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na Halopesa na hatimaye kuchukua fedha kupitia mawakala.