Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. January Yusuf Makamba (19 total)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa kulikuwa na maelekezo Serikalini kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Wizara za Kisekta za SMT na zile za SMZ ambayo yalikuwa yanahimiza ushirikiano wa karibu wa kitaalamu na utafiti na pale Wizara ya Maji ilikuwa imepangwa, Waziri wa Sekta ya Maji Bara na Zanzibar tarehe 8 Juni, 2014; mkutano ule ukaahirishwa kusubiri Bunge la Katiba:-
Je, kwa sasa hivi maelewano hayo yanaendeleaje kuimarishwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kazi ya Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuratibu mahusiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mambo yasiyo ya Muungano. Mwezi wa kwanza tumetengeneza ratiba ya vile vikao ambavyo viliahirishwa na mambo ambayo yalibaki kufanyika katika kuhakikisha kwamba mahusiano hayo yanaimarishwa.
Kwa hiyo, moja ya kikao kilichopangwa kufanyika na ambacho tumeweka fedha kwenye bajeti ili kifanyike, ni pamoja na hicho unachoongelea Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kuwapa faraja na taarifa wenzetu wa Zanzibar kwamba tumedhamiria kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba Muungano wetu unaimarika katika mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano na kazi hiyo tutaifanya kwa nguvu ili kutimiza ahadi yetu kama tulivyowaahidi Watanzania. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nimuombe kumuuliza maswali madogo sana ya nyongeza.
Kwa masikitiko makubwa sana suala hili limeleta gumzo sana katika chombo cha Baraza la Wawakilishi, limeleta gumzo muda mrefu na hatimaye likatua katika chombo hiki muhimu kwa wananchi.
Mwaka 2014 Serikali mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliunda kamati ya wataalam na kamati hiyo ya wataalam iliongozwa na wanasheria wazito wa nchi hii akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio swali hili nakuja nalo; imeunda Kamati iliyokuwa inaongozwa na Wanasheria Wakuu wawili kutoka Zanzibar na Bara ili kutatua changamoto zilizokuwepo katika mafuta na gesi ikiwemo ya Kisiwa hiki cha Latham na ripoti hii wakaikabidhi kwenye Serikali zote mbili. Je, ni lini Serikali imetoa ripoti ya suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Zanzibar ina mipaka yake ninachokifahamu hapa kama ni Serikali moja ni majibu yaliyojibiwa hapa; Zanzibar mipaka yake na hili eneo Zanzibar na swali lao. Tukamate wapi ambapo pana ukweli?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tangu mwaka 1968 ambapo suala la gesi na mafuta liliingizwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano; baada ya hapo kwa muda mrefu kumekuwa na hoja na haja ya kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano; na zimefanyika jitihada mbalimbali ili kufikia azma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010 ilikubalika baina ya Serikali zote mbili kwamba suala hilo liondolewe. Kamati anayoizungumza Mheshimiwa Jaku ya wataalam iliundwa ili kutafuta namna kwa sababu suala hili lipo Kikatiba na lingeweza kuondolewa Kikatiba; lakini kamati hiyo iliundwa mahususi ili kuwezesha jambo hilo lifanyike wakati mchakato wa kubadilisha Katiba unafanyika na matokeo ya kamati hiyo ilipelekea sasa kuapata mwanya ambapo Sheria ya Mafuta tuliyopitisha Bungeni mwaka jana iliruhusu Zanzibar iweze kuchimba na kutafuta mafuta na sasa kuna sheria inatungwa katika Baraza la Wawakilishi ya kuruhusu Zanzibar ichimbe na kutafuta mafuta hata kabla Katiba haijabadilishwa rasmi na kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba katika Katiba Inayopendekezwa suala hilo limezingatiwa na litaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho napenda kusisitiza ni kwamba sisi Jamhuri yetu hii ya Muungano kama nlivyosema kwenye lile jibu la msingi ni watu wa ndugu na jamaa moja; hakuna mgogoro wowote unaohusiana na mipaka au umiliki wa eneo lolote katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Na sisi pia kama ndugu tumejenga utaratibu wa kiutamaduni na kitaasisi wa kushughulikia na changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachopenda kutoa rai ni kwamba kwa wenzetu ambao wanapenda kutumia masuala ya Muungano kukabiliana na matatizo yao ya kisiasa, aidha, upande wa Bara au Zanzibar waache hayo mambo na watoe nafasi kwetu sisi ambao tumepewa dhamana ya kushughulikia mambo ya Muungano na Serikali iweze kufanya shughuli zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ambayo sijaridhika nayo hata kidogo, naomba sasa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mmiliki wa shamba hili ndugu Joseph Meier alimiliki shamba hili kwa njia za ulaghai ikiwa ni pamoja na kuwapatia viatu Wenyeviti wa Vijiji wa kipindi hicho kwa tiketi ya CCM na akamilikishwa shamba hilo, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuchukua hatua za kinidhamu kwa mmiliki huyu ambaye ni mmiliki haramu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Serikali katika majibu yake imesema kwamba mmiliki wa hili shamba analihudumia kwa kiwango kidogo sana, kwa maana ya kwamba katika ekari 1,000 ekari zinazoendelezwa ni kama ekari 10 tu kati ya 1000; je, Serikali haioni kwa kigezo hiki tu ni muda muafaka sasa wa kumpora huyu bwana hili shamba lirejeshwe kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi ambao hawana maeneo ya kulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza la nyongeza anasema kuwa huyu mwekezaji alichukua shamba hili kwa njia ya ulaghai. Sisi tunasema kwamba kama mwekezaji yeyote na ndiyo maana Msajili wa Mashirika ya Umma (TR) anapitia mikataba yote ya wawekezaji wetu ambavyo wameweza kumilikishwa mashamba na wengine ambao waliingia kwenye ubia wa mikataba mbalimbali ili kuweza kujua kama kuna tatizo lolote lile katika umiliki. Kwa hiyo, pale tunapogundua kwamba mwekezaji au mbia wetu ambaye tumeingia naye kama Serikali, kuna ubadhirifu wa aina yoyote ulifanyika, hatua zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaguzi hizo zinaendelea kwenye Mashirika yetu ya Umma yote kuhakikisha kwamba kuna usahihi wa umiliki, lakini vilevile hakuna ulaghai wa aina yoyote na hivyo kama itabainika kwamba kuna ulaghai ulitumika katika kujipatia shamba hili hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; kwamba huyu mwekezaji amekuwa akiendeleza shamba hili kwa kiwango kidogo sana, ambapo according to yeye Mheshimiwa Mbunge ni kama asilimia moja au mbili ya shamba alilokuwa amekabidhiwa la hekta 830, lakini ameweza kuendeleza kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza hapa kwamba kinachotakiwa sasa Mheshimiwa Mbunge ajue jukumu hili liko kwenye halmashauri yake, yupo Afisa Mteule wa Ardhi pale ambaye ana jukumu la kufanya ukaguzi kwenye shamba hilo kuona maendelezo ambayo yamefanyika na akigundua kwamba hakuna maendelezo yoyote yaliyofanyika kwenye shamba hilo, basi amwandikie notice ya siku 28 ya kufanya marekebisho na baadaye amwandikie notice ya siku siku 90 ya kujieleza kwa nini asinyang‟anywe ardhi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kama yote haya yatafanyika, mwekezaji huyu atakuwa ameshindwa kukidhi matakwa yanayotakiwa, basi atashauriwa Waziri wa Ardhi ili aweze kulitwaa shamba hilo na Waziri wa Ardhi atamshauri Mheshimiwa Rais afute hati husika. Baada ya hapo taratibu zikikamilika, basi hati itafutwa, umiliki utafutwa na umiliki wa shamba hili utarejeshwa kwenye halmashauri ambapo halmashauri ndiyo watapanga matumizi ya namna gani shamba hili litumike baada ya kuwa limerudishwa na Serikali mikononi mwa halmashauri.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu ni migogoro ya ardhi na eneo ambalo inasemekana kumekuwa na migogoro ya ardhi ni pamoja na eneo la Kibada Kigamboni ambapo kuna viwanja vilipimwa na Serikali na wananchi wakapewa na Wizara husika. Sasa, nataka kujua nini status ya eneo hilo wakati Wizara imepima, imewapa wananchi lakini leo imetokea kwamba eneo ambalo amepewa mtu mmoja tayari amejitokeza mtu mwingine amesema hilo eneo ni la kwake wakati Wizara ndio wametoa hati; nini status ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka sote hapa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi akiwa hapa Bungeni alitamka kwamba migogoro yote ya ardhi ambayo Waheshimiwa Wabunge mliwasilisha humu Bungeni na migogoro mingine ambayo inahusisha taarifa mbalimbali ambazo zimeshafanyiwa uchunguzi, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliunda Tume ya kupitia taarifa hizi za uchunguzi zilizofanyika, lakini na migogoro ambayo Waheshimiwa Wabunge tayari waliiwasilisha kipindi cha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekit, nataka kuwaambia kwamba, timu hiyo ya wataalam iko kazini na Mheshimiwa Bulaya avumilie, asubiri, taarifa hiyo ya wataalam itakapokamilika tutawaletea hapa Bungeni ili kila mmoja ajue status ya kila eneo la mgogoro ambavyo limeshughulikiwa na Serikali.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Matatizo ya ardhi ambayo haijapata kuendelezwa yaliyopo katika eneo la Mbozi yanafanana kabisa na matatizo ambayo tunayo kwenye Wilaya yetu ya Karatu. Katika Kijiji cha Mang‟ola Juu kuna mwekezaji, Tembotembo ambaye amemilikishwa eka zaidi ya 3,000 lakini ameweza kuendeleza chini ya asilimia 25. Katika kijiji hichohicho pia kuna mwekezaji anaitwa Acacia naye ameendeleza eneo alilopewa kwa chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo sasa yamebadilika kuwa hifadhi na mapori bubu ya kuhifadhia wanyama wa porini ambao ni hatarishi kwa wananchi wanaolizunguka. Je, ni lini Serikali itatoa mashamba hayo na kuwarudishia wananchi hao ili waweze kuyatumia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kutwaa mashamba kwa hekta zisizopungua 500 mmiliki wa shamba hilo anapewa miaka miwili tu anatakiwa awe ameliendeleza shamba hilo na asipofanya hivyo yuko halali kabisa kunyang‟anywa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Namba 4 ya Mwaka 1999, kifungu cha 45 na cha 47, anayo haki ya kunyang‟anywa ardhi ile. Wale ambao ardhi yao wamekabidhiwa zaidi ya hekta 500, kama hajaiendeleza kwa asilimia 80 ndani ya miaka mitano ardhi ile inaweza kutwaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kwa sababu mamlaka haya, nani anayeanzisha kazi hii, kazi hii inaanzishwa na Afisa Mteule wa Ardhi pale halmashauri, waanzishe tu halafu watuletee, tena wafanye mapema na mimi bado nakaimu huu Uwaziri wa Ardhi ili tuweze kuyashughulikia mapema matatizo haya.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tatizo la ardhi kwenye Wilaya ya Mbozi linafanana sana na tatizo lililopo kwenye Mji wetu wa Tunduma. Katika Mji wa Tunduma katika Kata ya Mpemba kuna ardhi karibu ekari 500 ambazo zinamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na mpaka sasa hivi eneo lile halijaendelezwa zaidi ya miaka minane. Je, Serikali inasema nini ili kuikabidhi halmashauri, ambayo haina hata eneo la kujenga makao makuu ili iweze kutumia ardhi ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na swali hili ambalo limekuwa kila Mheshimiwa Mbunge akiliulizia, naomba tu nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa wetu Wateule wa Ardhi popote nchini, katika maeneo na katika malalamiko ya namna hii, Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 imewapa nguvu. Kwa hiyo, walianzishe jambo hili watuletee na sisi kama Serikali hatutawaangusha.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye mikakati mizuri. Naomba nitumie muda wangu kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuzi Wilayani Meatu inasuasua kwa kuwa chanzo chake cha bwawa kimejaa matope na kuathirika na mabadiliko ya tabianchi sambamba na chanzo cha New Sola Zanzui kilichopo Wilaya ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira imefanikiwa kupata sh. 230,000,000,000 ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta Mkoa wa Simiyu na usanifu bado unaendelea. Je, Serikali haioni haja katika usanifu huo ikajumuisha kupeleka bomba kuu katika Makao Makuu yote ya Mkoa wa Simiyu ikiwemo Wilaya ya Meatu na Maswa kwa awamu ya kwanza kwa sababu Wilaya hizi zimeathirika kiasi kikubwa na ukame na ziko katika phase two na fedha ya phase two haijapatikana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kuuliza swali na kwa umakini anaouonesha katika kufuatilia shida za maji za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe habari njema kwamba baada ya kupatikana sh. 250,000,000,000 siyo 230,000,000,000 za awamu ya kwanza sasa tunaanza utaratibu wa kupata fedha nyingine zaidi za awamu ya pili ambazo zitapeleka maji sasa katika maeneo yote aliyoyataja pamoja na mkoa mzima na mikoa mingine ambayo inakabiliwa na ukame mkubwa unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, Serikali inatamka rasmi kwamba, inatambua changamoto ya maji na ina mipango ya kuyapeleka kwa wananchi wote wanaokabiliwa na ukame katika eneo hilo kwa kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jibu zuri la kuridhisha la Serikali nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mto Lukuga kupoteza maji katika Ziwa Tanganyika, je, Serikali iko tayari kuwahamasisha wananchi wanaokata miti katika milima yote inayozunguka Ziwa Tanganyika, ili wakati wa masika maporomoko yote yanayoleta tope, mchanga, kupunguza kina cha maji ya Ziwa Tanganyika, kuacha shughuli hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, je, Serikali iko tayari kuwaelimisha wananchi waache kukata miti hovyo na kuwachukulia hatua wote wanaofanya kandokando ya Ziwa Tanganyika kufanya shughuli ambazo Serikali hairidhishwi, kama kujenga karibu na ziwa na kuharibu vyanzo vya maji vinavyoporomosha maji katika Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba, nilipata fursa ya kwenda Kinshasa kwa ajili kukutana na Mawaziri wenzangu wa Mazingira kuhusu suala la kupungua kwa kina cha maji cha Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikutana na Waziri wa Burundi, Zambia na Congo; na mpaka sasa hivi, nimpe tu taarifa njema Mheshimiwa Keissy, kwamba tumefika mahali pazuri kati ya Serikali hizi na Benki ya Dunia kuhusu upatikanaji wa zile fedha za kujenga banio ili kuzuia maji kutoka kwa kasi kwenye Ziwa Tanganyika kwa upande wa Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala la pili, ni kweli changamoto ipo kubwa. Nilipata bahati ya kutembea mikoa yote iliyo katika Mwambao wa Ziwa Tanganyika na kuna tatizo kubwa sana la shughuli za kibinadamu zinazosababisha ziwa kujaa tope na hata Bandari ya Kigoma pamoja na Kasanga na miji yote iliyoko kando ya mwambao kupata changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na viongozi wa halmashauri katika maeneo yote kuhakikisha kwamba, Sheria ya Mazingira inazingatiwa na shughuli za kibinadamu katika mita 60 kutoka kwenye mwambao wa Ziwa zinasitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu changamoto iliyopo kwa sababu watu wengi wanategemea uvuvi na shughuli nyingine na maji yaliyopo pale kufanya hiyo. Kwa hiyo, tunategemea ushirikiano wa Mheshimiwa Mbunge ambaye yeye ni mwanamazingira mzuri sana, Mheshimiwa Keissy, pamoja na viongozi wote tuweze kufanikiwa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kwamba, Wakuu wa Mikoa ya mwambao wa Ziwa Tanganyika wanaweza kufanya mkutano na forum pamoja na Wabunge, ili kujadili ustawi wa Ziwa Tanganyika kwa ujumla na sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tutakuwa tayari kuunga mkono huo mkutano (forum) wa wadau wote wa Ziwa Tanganyika, ili kuangalia suala hilo na masuala mengine yanayohusiana na ustawi wa ziwa hilo.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyekuwa Waziri katika Wizara ambayo ilikuwa ikishughulikia mambo ya Muungano, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye sasa hivi ni Makamu wa Rais, aliwahi kutuambia kwamba kuna kikao ambacho kilikaa kati ya pande hizi mbili, Wajumbe kutoka Zanzibar na Wajumbe kutoka Tanzania Bara waliokuwa wakizungumzia kuhusu kero ambazo zinahusu mambo ya Muungano. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni Wajumbe gani hao ambao walikuwa wakikutana kuzungumzia kero hizi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kumekuwa na taratibu mbalimbali za kushughulikia changamoto za Muungano hatuziiti kero ni changamoto za Muungano. Mwaka 2006 ukaanzishwa utaratibu mpya wa kikao cha Kamati ya Pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kikao kile cha Kamati ya pamoja kilikuwa kinaongozwa na Makamu wa Rais pamoja na Watendaji Wakuu wa Serikali za pande mbili. Maana ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar au Waziri Kiongozi kabla ya mabadiliko ya Katiba ya 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao kile kinajumuisha Mawaziri wote ni Mabaraza ya Mawaziri ya pande zote mbili za Muungano wetu. Kwa taarifa tu kikao cha mwisho kilikutana tarehe 13 Januari, 2017 kule Zanzibar ambapo kilijumuisha Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao hicho kinatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makatibu Wakuu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla ya hapo kinatanguliwa na kikao cha wataalam wa masuala husika yatakayozungumzwa katika kikao hicho kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kikao hiki na utaratibu huu ni mkubwa, ni mzuri na umetusaidia sana kupunguza changamoto za Muungano. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, tatizo lililoko Mikindani ni kubwa na halmashauri haina uwezo wa kumudu tatizo hilo. Wale waliotembelea Mikindani na wanaopita pale watakubaliana na mimi kabisa. Je, Serikali haioni sasa jukumu hili likabebwa na Serikali Kuu kuisaidia Halmashauri ya Mikindani kwa sababu matuta haya yalijengwa miaka 50 iliyopita na sasa ukarabati wake unahitaji fedha nyingi? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, tatizo lililopo Mikindani linafafana na tatizo lililopo Masasi. Mji wa Masasi umezungukwa na milima na hivyo kuleta athari kubwa sana ya maji kutoka milimani kuingia pale mji. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea Masasi na Mikindani kwenda kujionea hali halisi ili Serikali iingilie kati? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, kwanza nitatembelea Mikindani na Masasi baada ya Bunge hili ili kwenda kujionea hali halisi ya anayozungumza Mheshimiwa Mbunge. Kabla sijatembelea, nitatuma wataalam wa Ofisi ya Makamu wa Rais waende Miji wa Mikindani mapema wakatazame haya aliyouliza Mheshimiwa Ghasia na aliyozungumza Mheshimiwa Bwanausi na baada ya hapo tutafanya tathmini tuone nini kinahitajika kufanyika. (Makofi)
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakubaliana sana na Mheshimiwa Naibu Waziri alipozungumza hasa hapo alipomalizia kwamba baadhi yetu tunatumia tu huu mwanya wa kuwepo kwa changamoto za Muungano kupitisha masuala ambayo kweli siyo changamoto za Muungano. Hili linatokea kwa sababu ya uelewa mdogo wa Muungano wetu na historia za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini hasa Serikali itaona umuhimu wa kuingiza mtaala maalum wa Muungano kama vile iipoona umuhimu wa kuingiza masuala ya mazingira, reproductive health na kadhalika ili kuepuka hizi dhana za kutokuelewa hasa kiini na msingi wa Muungano wetu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa maswali yaliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mtaala wetu wa sasa kuna somo la Uraia ambalo linagusa historia ya nchi yetu na masuala ya siasa ya nchi yetu. kwa hiyo, wazo la Mheshimiwa Mbunge la kuongeza na kupandisha hadhi na kuupa umuhimu Muungano wetu katika somo la Uraia tumelichukua na tutaongea na wenzetu wa Wizara ya Elimu tuone ni kwa namna gani tunapandisha na tunaongeza uzito wa masuala ya Muungano katika somo la Uraia. (Makofi)
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ziwa Tanganyika linamilikiwa na nchi nne: Burundi; Zambia; DRC Congo; na Tanzania. Hivi karibuni Ziwa Tanganyika upande wa Uvira DRC Congo ghafla limebadilika rangi na kuwa rangi ya kijani ingawa maji hayana rangi. Je, Wizara ya Muungano na Mazingira inayo taarifa hii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ziwa hili linamilikiwa na nchi tatu na kuna Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika Authority) na juzi tulikuwa na mkutano hapa na viongozi wa Mamlaka hiyo kuzungumzia uhifadhi mzima wa Ziwa Tanganyika ikiwemo hili suala lakini pia suala kubwa zaidi la kukatika kwa ukingo kwenye Mto Lukuga ambao unatoa maji mengi kwenye Ziwa Tanganyika na kuyapeleka Mto Congo. Kwa hiyo, haya masuala mawili tunayafuatilia na tutampa mrejesho Mheshimiwa Mbunge kuhusu matokeo yake.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nasikitika kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri hajajibu hili swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuathirika kwa kilimo ni matokeo ya athari za tabianchi. Tuambie Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na athari hizi? Maziwa yanakauka, mito inakauka, misitu inapotea. Mna mkakati gani mliouchukua au ndiyo mko kwenye mipango tu? Ndiyo jibu tunalolitaka kutoka kwako. Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ambalo Mheshimiwa Mwantum Dau Haji alitaka kujua Serikali tuna mipango na mikakati gani; nimeeleza kwamba mkakati wa kwanza tulionao tuliuandaa mwaka 2007 ambao unahusu uhimilivu katika mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimejibu hapa kwamba mwaka 2012 tuliandaa mpango mwingine wa mabadiliko ya tabianchi tofauti na ule wa mwanzo. Vilevile nimejibu hapa kwamba mpaka sasa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na kupitia wataalam tunaandaa na tunakaribia kumaliza kupata sasa mpango mkakati endelevu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye suala la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba mikakati haipo, nimeieleza hapa. Pia nimeelezea hapa kwamba hata juzi Mheshimiwa Rais amezindua ASDP Awamu ya Pili ambamo ndani mwake pia kuna mikakati mingi sana imezungumziwa. Pia mikakati na mwongozo niliousema ambao tumepeleka kwenye Halmashauri ambapo Maafisa Mipango wanatakiwa kuweka kwenye bajeti zao, tumeelezea kuhusu utafiti wa mbegu ambayo inahimili kwenye ukame pamoja na kilimo cha umwagiliaji na umwagiliaji wa matone.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mikakati hii ipo, Mheshimiwa Yussuf mtani wangu wa kisiasa, naomba uelewe Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni Serikali makini, ni Serikali ambayo inaongoza kwa kuwa na mikakati, tena mikakati ambayo inatekelezeka. Ahsante sana.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikipokea fedha mbalimbali kutoka kwa wafadhili ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kila mwaka. Miaka miwili iliyopita walikabidhiwa takribani shilingi bilioni 224 kwa ajili ya shughuli hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anaongelea kuhusu mikakati; je, kuna utekelezeji wowote wa mikakati hii ya kuhusisha mabadiliko ya tabianchi na kuboresha kilimo chetu kwa kutumia hizi fedha za wafadhili ambazo zinagusa hususan mabadiliko ya tabianchi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Sware ni mwanamazingira na ni kweli anafahamu kabisa kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais tumekuwa tukipata fedha ambazo zinasaidia miradi mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Amesema sasa mbali na mikakati, fedha hizi namna gani tunazi-link.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie kwamba mojawapo ya miradi ambayo tumeihusianisha na hiki kilimo kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ukienda kule Rufiji tayari katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji tulikuwa tunatekeleza mradi ukiwa ni pamoja na kupanda mikoko na kuwawezesha wananchi wahimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga pamoja na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ukienda kule Pemba Kisiwa Panza mbali na kujenga ukuta, vilevile tulikuwa tunawasaidia wananchi waweze kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo cha mboga na matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo sasa hivi tuna Mikoa kama Tabora, Singida, Kagera, Morogoro, Tanga ambako tayari tunatekeleza miradi mbalimbali ya kutumia fedha hizi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wakulima wa namna wanavyoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatumia zile fedha katika kilimo cha mboga pamoja na matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni pamoja pia na Bonde la Kihansi kule Kilombero, vilevile tumeweza kutoa fedha ili wananchi wahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kilimo katika lile mbonde.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Sware kwamba siyo mikakati tu ambayo Serikali inaishia, ni pamoja na fedha hizi. Tumetoa fedha nyingine shilingi milioni 200 sasa ambazo zinapeleka maji kule Shinyanga na yale maji yatatumika pia katika kusaidia umwagiliaji kwenye kilimo. Hiyo ni katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YUSSUF S. HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Hii mito ambayo inatoka baharini na kuingia nchi kavu inakuwa na kasi sana wakati yale maji yapoingia ama yanapotoka, kwa sababu tabia ya bahari, maji yanapojaa yanakuwa yana nguvu sana na yanapotoka vilevile yanakuwa na nguvu. Maana yake ni kwamba ongezeko la soil erosion linakuwa kubwa kuliko linavyotarajiwa. Ni upi sasa mkakati wa Kitaifa wa Serikali kwa sababu ardhi yetu inapungua kwa kasi? Msimbati itakuwa ni moja kati mfano mzuri wa kasi wa maji haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni upi mkakati hasa wa Kitaifa wa Serikali kudhibiti suala hili la erosion katika kingo za bahari zetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ulishaanza na nitoe mifano, ukiangalia kingo za bahari pale Ocean Road tumejenga. Pia ukienda Pangani tumejenga na maeneo mengine tutaendelea kadri ambavyo tutakapokuwa tunapata fedha za kuhakikisha tunakabiliana na haya mabadiliko ya tabia nchi. (Makofi)
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wabunge hawa wanapouliza kuhusu kero za Muungano na vipi zinatatuliwa, ni kwamba tunaporudi kwa wapiga kura wetu tunazikuta. Kwa hiyo, inaonesha kwamba kero za Muungano zinatatuliwa kwenye meza, lakini kwenye vitendo hakuna. Kwa mfano, msafirishaji wa ng’ombe kutoka Zanzibar akija akichukua ng’ombe Bara kupeleka Zanzibar analipishwa ushuru sawasawa na anayesafirisha kupeleka Kenya kwa Sh.37,500 badala ya Sh.7,500. Sasa ni ipi faidi ya Wazanzibari kuwa ndani ya Muungano? Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli haikutazamiwa kwamba Mheshimiwa Mbunge atauliza ni zipi faida za kuwepo Muungano, kwa sababu hata yeye kuwepo kwake hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano. Muungano huu kwa pale tulipofikia hata haihitajiki kueleza faida zake kwa sababu zinaonekana dhahiri. Ukweli upo kwamba, zipo changamoto katika shughuli za kila siku za maingiliano na mahusiano hiyo haikataliwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko changamoto kubwa za kisera ambazo ndiyo zinashughulikiwa katika vikao vya viongozi, lakini kuna yale mambo ya kila siku kwamba Afisa Forodha pale ameamua mwenyewe kwa anavyoona afanye jambo. Tunachosema sisi kwa wananchi wa pande zote mbili ni kwamba yanapojitokeza mambo kama haya, kama hili alilosema Mheshimiwa Mbunge, yaletwe kwetu haraka kwa sababu ni masuala ya kiutendaji ambayo yanashughulikiwa haraka. Yako mambo mengi ya namna hii ambayo yametatuliwa kwa taarifa tu kwamba, kuna jambo hili sisi tunadhani haliendi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunasema kwamba, changamoto hizi ndogondogo zisitumike kuupa jina baya Muungano, kwa sababu wakati mwingine ndipo makosa yanapofanyika, kwamba inatokea tatizo ambalo lipo tu, ni la kiutendaji, la kibinadamu, lakini linatumika kwamba Muungano wetu haufai kwa sababu kuna kitu hiki. Muungano huu ni mpana zaidi na ni mkubwa zaidi na una maana kubwa zaidi kuliko changamoto zinazojitokeza kila siku.
MHE. MAGDALENA HAMIS SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa Bungeni leo, hayaoneshi dhamira ya dhati kupiga marufuku mifuko ya plastiki hapa nchini. Ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, inadhamiria siku zijazo, siyo kesho wala mwakani, hatujui. Hivi tunavyoongea, kwenye masoko yetu wajasiriamali wengi wanauza mifuko mizuri, mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira, mifuko ambayo ni vikapu vya ukili na mifuko mingine ambayo inaweza kutumika isiharibu mazingira. Mifuko hiyo haina masoko, hainunuliwi kwa sababu mifuko ya plastiki inatolewa bure masokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kwamba tatizo siyo kukosekana kwa mfuko mbadala, tatizo ni Serikali kuendelea kulinda viwanda vinavyotengeneza mifuko hii inayoharibu mazingira?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hakuna Mtanzania yeyote au mdau yeyote asiyejua madhara ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Serikali hioni kuendelea na makongamano, sijui na vikao vya wadau ni kupoteza muda na gharama na Serikali sasa ichukue hatua za haraka kupiga marufuku mifuko hii hapa nchini kama ambavyo wenzetu wamefanya, Zanzibar wameweza, Rwanda wameweza, Kenya wameweza, maeneo mengine yote wameweza. Sisi tatizo nini? Naomba majibu ya uhakika.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana sana Mheshimiwa Sakaya kwa kuongea kwa uchungu kabisa na kuonesha ni mwanamazingira kabisa fasaha. Naomba nimhakikishie kwamba, katika hotuba yetu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo itakuja tarehe 16 kwa mujibu wa ratiba ya mwezi huu, tunaweza kutangaza hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wiki hii mimi nimeelekezwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa Majaliwa, nikutane na Taasisi za Serikali zinazohusika na jambo hili, NEMC, TBS, TRA, Uhamiaji, Polisi na Customs ili kuweka utaratibu wa namna tunavyoweza kupiga marufuku. Hapa nilipo, tayari ninazo kanuni nimeshazitengeneza ambazo zinangoja kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali. Kwa hiyo, kama tutakubaliana katika vikao vya wiki hii na vinayokuja, basi tarehe Mosi, Julai, inawezekana kabisa ikawa ndiyo mwisho wa matumizi ya plastiki hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali inalichukulia kwa uzito na tunalifanyia kazi. Ni kweli kabisa tumeongea na wadau wote, hakuna sababu yoyote ya kuendelea kutumia plastiki hapa nchini. Mimi kama Waziri wa Mazingira nakubali hilo. Mbadala upo na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukubaliane kwamba tutakapopiga marufuku, basi tuwe tumejiandaa kufanikiwa. Kwa sababu zipo nchi ambazo zimeamua kuchukua hatua hii, lakini hazikujipanga kwenye kufanya lile zoezi; mkajikuta kwamba mmetoa tangazo tu, lakini kitaasisi hamjajipanga, kiuratibu hamjajipanga, kwa hiyo, inakuwa ni bure tu. Kwa hiyo, tunataka tukitangaza tulifanye zoezi hili kwa namna ambayo tutafanikiwa. Tunaamini kabisa kwamba hatua hii itaibua ajira nyingine nyingi zaidi kuliko hata zile zilizopo kwenye mifuko ya plastiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuko pamoja kwenye hili.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri mahiri katika Wizara hii ya Muungano, lakini pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; bandari hiyo ambayo inatakiwa ijengwe Zanzibar pale Mpigaduru ina thamani au itagharimu dola za Kimarekani milioni 430, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshapata mdhamini au mkopo kutoka Exam Bank wa dola milioni 200, ni miaka nane sasa tokea mradi huu upite, Serikali ya Muungano imeisaidiaje Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata mikopo au msahada wa kumalizia hapo palipobaki ikajengwa gati hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu Serikali ya Muungano imeingia mkataba wa kujenga gati ya Bagamoyo na Oman ndiyo wafadhili wa gati hii, lakini mkataba ule unaizuia Oman kusaidia tena nchi yoyote ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa kilometa zilizowekwa kujengwa gati kama ile.

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba mkataba huu ndiyo ulioifanya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikose msaada kutoka Oman kwa ajili ya kujenga gati ile?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa katika mazungumzo na mazungumzo hayo yanaelekea ukingoni kuhusu kukamilisha kipande cha rasilimali zinazotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Mpigaduru. Tunafahamu kwamba ni moja ya ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ni bandari muhimu sana kwa uchumi wa Zanzibar na wote tunajua hivyo na tunafahamu hali ya bandari ya Zanzibar, sasa hivi ilivyo na msongamano. Kwa hiyo tunazungumza na wenzetu kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika hilo.

Mheshimiwa Spika, la pili, mkakataba wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo bado haujaingiwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kampuni ya China kwa kushirikiana na Oman. Kwa hiyo yale masharti yaliyopo yanayozungumzwa hayatumiki sasa kwa sababu bado utekelezaji rasmi haujaanza. Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wazanzibari wote kwamba Serikali haitaingia katika maamuzi ambayo yataathiri ustawi na uchumi wa Zanzibar.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo shida ya vitongoji vya Mbulu, katika Wilaya ya Rungwe Kitongoji cha Ngana kina wakazi wapatao 600, lakini waliounganishiwa umeme wa REA ni familia 36 tu peke yake; ni nini Serikali inajipanga kwenda kuhakikisha vitongoji vile na familia zingine zinapata umeme kama wanavyopata wananchi wengine?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Nishati, kwa majibu mazuri ambayo aliyatoa awali katika maswali yaliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie hili suala la vitongoji kwa sababu hii changamoto ipo karibu katika kila jimbo, kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kupeleka umeme katika vijiji karibu vyote, na tunavyo vijiji 12,345 hapa nchini na takribani vijiji vyote tutavimaliza itakapofika Desemba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika vijiji hivyo tuna vitongoji 64,760, na katika vitongoji 64,000 vitongoji 37,610 havina umeme. Kwa hiyo, vitongoji zaidi ya asilimia 58 havijafikiwa na umeme wakati vijiji zaidi ya asilimia 80 vimepata umeme. Na tunafahamu kwamba manufaa ya umeme siyo unapofika kijijini, ni pale unapowafikia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetazama mahitaji ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote, ni karibu shilingi trilioni 7.4, na tumeangalia mahitaji ya urefu wa nyaya, idadi ya transfoma na kila kitu ili tuweze kufanya kazi hii ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote kwa muda mfupi. Ndiyo kazi ambayo nilikuwa nimefanya tangu niingie katika nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa ni fedha. Kwa utaratibu wa tunavyopata fedha za REA sasa hivi itachukua miaka 23 kumaliza vitongoji vyote. Sasa ndani ya Serikali tumetafakari na tumekuja na options tatu na hapo mbele tutaamua ni ipi twende nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, option ya kwanza ni hii ya sasa hivi tunayoendelea nayo ambayo itachukua muda mrefu, kama miaka 23. Option ya pili ili tufanye ndani ya miaka minne lazima tutenge bajeti karibu shilingi trilioni 1.8 kila mwaka kwa kazi hiyo. Option ya tatu ni kutoa hati fungani ya nishati vijijini (energy bond) ambayo mapato ya mafuta, ile petroleum levy ya shilingi 100, tunai-ringfence kwa miaka 20 ambayo itatupa karibu dola bilioni 3.1 na hiyo bond tunaipeleka sokoni, hizi fedha zote tunazipata sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima tukubaliane kwamba charge ya mafuta tutai-peg kwenye dola, hiyo shilingi 100 kwa miaka 20. Na matumizi ya sasa hivi ya mafuta ni lita milioni 10 kwa siku, kwa hiyo kwa miaka 20 – na tunaamini matumizi yataongezeka – kwa miaka 20 kwa hakika kabisa tutapata pesa za kulipa hiyo hati fungani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, option ya tatu ni kitu wanaita EPC plus F, Engineering, Procurement, Construction plus Financing, kwamba kampuni kubwa zinazoweza kupeleka umeme vijijini kwa mkupuo kwenye vitongoji zinakuja na proposal lakini na financing ambayo ni concessional; asilimia moja kwa miaka 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba katika kutafakari hizo options tunaweza tukapata ambayo itakuwa ni nafuu kwa maana ya interest, lakini itatuwezesha kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote kwa kipindi cha miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapokamilisha kufanyia kazi hilo jambo tutakuja Bungeni na kuwaeleza ni option ipi ambayo tumekwenda nayo. Na tutakapoamua kwa hakika kabisa dhamira yetu sisi ni kwamba Wabunge hapa watakapokuwa wanaelekea kwenye uchaguzi basi umeme lisiwe jambo ambalo litawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na maelekezo hayo tumepewa na Mheshimiwa Rais, na katika kipindi hiki kifupi tutakuja na plan ya financing ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 37,000 katika kipindi cha miaka minne ili tusisubiri miaka 20. Kwa hiyo, naamini kabisa maswali yote ya umeme vitongojini yatakuwa yameisha mara tutakapokuja na hiyo plan. Ahsante sana. (Makofi)