Answers to Primary Questions by Hon. January Yusuf Makamba (6 total)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Serikali Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliyotolewa mwaka 2014 Kisiwa cha Latham (Fungu Mbaraka) ni mali ya Zanzibar tangu kilipotangazwa rasmi mwaka 1898. Hata hivyo, zipo taarifa zilizothibitishwa kuwa Serikali ya Muungano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliiandikia SMZ kuwataarifu kwamba kisiwa hicho ni cha Tanzania Bara.
(a) Je, Serikali haioni mgogoro huo wa umiliki wa kisiwa hicho ni aibu kutokea kwa nchi moja na kuonesha kwamba bado kero za Muungano hazijapatiwa ufumbuzi?
(b) Kisiwa cha Latham kimepakana na vitalu namba 7 na 8 ambavyo tayari TPDC imeshavigawa bila ridhaa ya SMZ; je, Serikali haioni kuwa mgogoro huo sio wa mpaka bali ni wa mafuta na gesi?
(c) Je, Serikali inachukua hatua gani kumaliza mgogoro huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa swali ni kwamba kuna barua kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu hili suala, barua hiyo tumeitafuta kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hatujaiona. Kwa hiyo, Mheshimiwa atusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye swali; kwanza (a) hakuna mgogoro wowote kuhusu umiliki wa eneo lolote baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa tafsiri na suala zima la mipaka la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar limewekwa wazi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar kabla na baada ya Muungano.
Vilevile katika orodha ya changamoto 14 za Muungano zilizokwishashughulikiwa na zinazoshughulikiwa hakuna suala lolote linalohusu umiliki wa eneo lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mgogoro wowote wa mafuta na gesi baina ya Serikali zote mbili, huko nyuma ni kweli kwamba leseni za utafutaji mafuta zilitolewa na TPDC katika eneo husika kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 1980 kwa sababu suala la mafuta lilikuwa ni suala la Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya Serikali hizi mbili kuhusu suala hili, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Serikali. Hata hivyo, Serikali zote mbili zilikubaliana kwamba suala la mafuta na gesi liondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano na kuwezesha Zanzibar kuanza harakati za kutafuta gesi na mafuta na kwamba mpaka sasa Sheria mpya ya Mafuta ya mwaka 2015 imetoa fursa kwa Zanzibar kusimamia shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo ya Zanzibar na ndio maana Zanzibar sasa pia ipo katika mchakato wa kutunga Sheria yake ya Mafuta na Gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata pale ambapo mgogoro unaweza kuibuka tunao utaratibu mzuri wa kukabiliana na changamoto hiyo na watu wa pande zote mbili za Muungano ni ndugu na jamaa na hawawezi kufarakana hata siku moja kuhusu umiliki wa eneo lolote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE.ALLY K. MOHAMED aliuliza:-
Katika miaka ya 1960 kulikuwa na Kingo katika Mto Lukuga huko DRC- Congo; kingo hizo zilisaidia sana kuzuia kupungua maji katika Ziwa Tanganyika:-
Je, nchi za Burundi, Zambia, DRC-Congo na Tanzania zimefikia wapi katika mpango wa kuweka kingo katika Mto Lukuga ili Ziwa Tanganyika lisiathirike sana kwa kupungua maji na kutishia uhai wa viumbe katika ziwa hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Keissy Mohamed, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana kwa kufuatilia hili jambo kwa muda mrefu. Tatizo la kushuka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika ambalo kwa kiasi kikubwa limesababishwa na kubomoka kwa banio la maji kwenye Mto Lukuga (DRC) linafuatiliwa kwa karibu na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mto Lukuga ndio mto pekee unaotoa maji kwenye Ziwa Tanganyika upande wa DRC kupeleka Mto Congo na hatimaye kwenye bahari ya Atlantiki. Aidha, Serikali za DRC na Tanzania kwa pamoja zinamiliki asilimia 86 ya Ziwa lote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka huko kwa kina cha maji ya Ziwa kumeathiri shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo, meli kubwa kushindwa kutia nanga ili kupakia na kupakua mizigo na abiria kwenye bandari za ziwa hilo. Bandari hizo ni pamoja na bandari za Kigoma na Kasanga kwa upande wa Tanzania, Bujumbura Burundi, Kalemia, Uvira na Moba kwa upande wa Congo. Aidha kwa upande wa Tanzania chanzo cha maji kwa Mji wa Kigoma Ujiji pia kinaathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na mwezi Machi, 2014 Wakuu wa Nchi za Tanzania na DRC waliagiza Mawaziri wa nchi hizi mbili wanaoshughulikia masuala ya maji wakutane ili kujadili namna ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa banio la Mto Lukuga lililobomoka. Mawaziri hao walikutana mwezi Aprili, 2014 na Agosti, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vikao hivyo Serikali hizi mbili zilitiliana Hati ya Makubaliano tarehe 7 Mei, 2015 ambapo zaidi ya dola za Kimarekani milioni sitini na tano zinahitajika kujenga banio lililobomoka. Pia nchi za Burundi na Zambia ambazo ni wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika zimeshirikishwa katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 7 – 9 Machi, 2016 kuliandaliwa Mkutano wa Wadau wa Maendeleo uliofanyika Nchini DRC na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Benki ya Dunia ambapo walituma wataalam ili kufanya tathmini ya awali kuhusu tatizo la kupungua kwa kina cha maji. Aidha, jitihada nyingine za kutafuta fedha zinaendelea kwa kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama ya gesi ili kuepuka matumizi ya mkaa na kuni?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania hatuzalishi gesi iliyosindikwa kiwandani (LPG) ambayo pia hutumika kama nishati ya kupikia. Gesi ya LPG huagizwa kutoka nchi za nje. Kama ilivyo kwa bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta ya petroli, gharama za LPG pia hutegemea bei katika soko la dunia.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha na kushirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya kupokea na kuhifadhi LPG ili kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya tani 16,000 za sasa. Hii itatuwezesha kuanza kuagiza LPG kwa mfumo wa uagizaji wa pamoja na hivyo kupungua kwa gharama za uagizaji na kupata nafuu katika gharama ya gesi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TPDC imetenga fedha Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia ambayo ipo hapa nchini na kuwaunganisha wateja kwa maeneo yaliyopitiwa na mradi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia. Gesi hiyo inayotumika kwa kupikia ni nafuu kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na vyanzo vingine vyanzo vingine vya nishati ya kupikia. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafikisha umeme katika Kata mbili ambazo hazijawahi kupata umeme kabisa katika Jimbo la Ndanda?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Jimbo la Ndanda kuna Kata 16 ambapo Kata mbili (2) kati ya Kata hizo hazina umeme. Kata hizo ni Msikisi na Mpanyani. Aidha, Kata ya Msikisi inaundwa na vijiji vya Miwale, Namalembo na Msikisi yenyewe, wakati Kata ya Mpanyani inaundwa na vijiji vya Nambawala A, Nambawala B, Mhima, Muungano na Mpanyani yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji hivyo vyote vya Kata hizo vinapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa na Mkandarasi M/s Namis Corporate Engineers and Contractors mwezi Aprili, 2021 na unatarajia kukamilika Desemba, 2022.
MHE. AIDA J. KHENANI K.n.y. MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa REA III katika Wilaya za Busokelo na Rungwe?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mradi wa REA awamu ya tatu (REA III) awamu ya kwanza jumla ya Vijiji 47 vimepatiwa umeme katika Halmashauri ya Busokelo, na Vijiji 22 katika Halmashauri ya Rungwe. Aidha, katika utekelezaji wa Mradi wa REA III round two, Vijiji vyote 32 vilivyobaki bila umeme katika Halmashauri ya Rungwe na Kijiji kimoja kilichobaki bila umeme katika Halmashauri ya Busokelo vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi M/S Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Co. LTD aliyepewa kazi ya kutekeleza mradi katika Mkoa wa Mbeya anaendelea na kazi katika maeneo ya Vijiji vya Busokelo na Rungwe ambapo wateja wa awali 594 wataunganishwa kwa huduma ya umeme.
Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 5.133. Serikali itaendelea kuongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kufikisha umeme katika maeneo yote ya vitongoji vya Halmashauri za Busokelo na Rungwe kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali juu ya wateja waliolipia shilingi 27,000 ambao wanatakiwa kulipa fedha zaidi ili kuunganishiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uunganishaji umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kwa maeneo yote ya mjini na vijijini, wateja wengi sana walijitokeza na bei ziliporudi za awali, wateja takribani 80,000 walibaki bila kuunganishiwa umeme na walikwishalipia huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Serikali uliotekelezwa na TANESCO ulikuwa ni kuwaunganishia umeme wateja wote waliolipia shilingi 27,000 bila kuongeza malipo yoyote. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2023, wateja wote waliolipia shilingi 27,000 kabla ya Januari, 2022 walikwishaunganishiwa umeme bila kulipa gharama za ziada, ahsante sana.