Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khalifa Mohammed Issa (6 total)

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majawabu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Hoja ilikuwa ni kwa namna gani vyombo vya Kiserikali vinaweza kusaidia au kushirikiana na hawa watumiaji wa uraibu huu ili kuweza kuzifikia zile channel za waagizaji, wasambazaji na watumiaji. Je, kuna mlinganisho gani wa wale waliokamatwa pamoja na watumiaji wenyewe ambao wako mitaani? Serikali inaweza kutupa ulinganisho kwa sababu mitaani wako wengi lakini ambao wanakamatwa ni wachache?
(b) Ni kweli kuna baadhi ya watumiaji wako katika maeneo ambayo wanapatiwa huduma za kupata nafuu. Vijana hawa na watu wengine kwa jumla wanatumia dawa hizi na wakati mwingine kwa vishawishi lakini na wakati mwingine kwa kukata tamaa tu za maisha. Sasa mara baada ya kwisha kuwapa dawa hizi au nafuu hii wakitoka mitaani tumewaandalia mambo gani ambayo yanaweza kuwasaidia katika kujenga maisha yao huko mitaani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU - MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena.
(a) Serikali inatumia vyombo vyake na wakati mwingine nalazimika kupata taarifa kutoka kwa waraibu wa dawa hizi ili kuwakamata wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa hizi. Ndiyo maana tumefanikiwa sasa kukamata baadhi ya watu wenye majina makubwa katika biashara hii na ninavyozungumza wako vizuizini na kesi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, limeulizwa swali kuhusu mlishanganisho; kuna mlinganisho gani kati ya wale wanaokamatwa na wale wanaotumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niseme kweli, hakuna statistics lakini lazima tuweke wazi kwamba biashara hii tofauti na biashara ya nyanya au vitunguu ni biashara inayofanyika kwa kificho sana. Kwa hiyo, kusema kwamba utapata proper statistics itakuwa ni kudanganya watu. Wapo watu maofisini na katika maeneo mbalimbali wanatumia dawa hizo na huwezi ukajua moja kwa moja.
(b) Huduma za kupata nafuu. Kwanza naomba nirekebishe kitu kimoja ambacho kinaweza kikaonekana kama over generalization. Siyo kila mtumia dawa za kulevya anafanya hivyo kutokana na kukata tamaa ya maisha. Mifano ipo ndani na nje ya nchi. Akina Michael Jackson na wengine siyo kama walikuwa wamekata tamaa ya maisha. Vishawishi is fine!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba juhudi za Serikali zinazochukuliwa za kukuza uchumi na kadhalika zina lengo la kuondoa ugumu wa maisha unaowaingiza vijana katika kutumia dawa za kulevya, kwa sababu sote tunafahamu kwamba vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na nchi yeyote yenye nia thabiti ya kuendelea, ni lazima ichukue hatua madhubuti ya kuwalinda raia wake kutokana na kutumia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, niongezee tu kwamba juhudi za kuondoa watu kwenye vishawishi vya kutumia dawa za kulevya, siyo za Serikali peke yake, hili ni tatizo la kila mtu. Kwa hiyo, kila mtu awe ni kiongozi wa kisiasa, kiongozi wa familia na raia wote, wana jukumu la kuhakikisha kwamba wananchi wanaondokana na vishawishi vya kutumia dawa za kulevya mara baada ya kumaliza tiba inayohusika.
MHE KHALIFA MOHAMMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na jawabu refu sana la Mheshimiwa Naibu Waziri, bado nina maswali mafupi mawili ya nyongeza. Swali la msingi lilikuwa ni risk, kuweka rehani roho za abiria. Hii haijalishi ukubwa wa ndege, ubebaji wa abiria wachache au wengi. Jawabu ilikuwa rubani kabla ya kurusha ndege, au vipindi kwa vipindi wanafanyiwa check-up.
Mheshimiwa Naibu Waziri, haoni binadamu katika maumbile yake unaweza kumfanyia check up sasa hivi lakini akifika pale hali yake ikawa na mgogoro. Je, haoni kwamba bado suala ni kuweka rehani roho za abiria?
Swali la pili, pamoja na treaties nyingi za Kimataifa na kuridhiwa na Bunge, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kulisimamia hili na kukawa na ulazima maalum wa ndege yoyote ya abiria kuweza kuongozwa na rubani zaidi ya mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, risk inapimwa. Katika eneo hili sheria tulizo nazo za kimataifa ambazo nchi yetu imeziingiza katika sheria zetu na Bunge hili limeidhinisha, hiyo risk imepimwa kwa uzito wake na ndiyo maana ni aina fulani tu za ndege zinazobeba abiria kiwango fulani zinazoruhusiwa kuendeshwa na rubani mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuna marubani maalum wanaoruhusiwa kuendesha ndege usiku na wakati ambapo huwezi ukaona uwanja ulivyo, ni aina fulani tu ya marubani ambao wamepitia kozi maalum zinazozingatia leseni za IFR (Instruments Flights Rules). Ndege zile ambazo zinatumia CFR ambazo ni kwa marubani ambao hawaja-qualify sana hazihitaji masharti hayo na kwa kawaida hawaruhusiwi kuendesha usiku au kwenye kipindi ambacho mawingu ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala la afya, ambalo ndilo swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge, nadhani ukiweka hata marubani watatu, wanne, Mwenyezi Mungu kama afya hiyo hakubali nadhani siyo solution na ndiyo maana upimaji wa kila mwaka na kwa wale ambao wanarusha ndege za kimataifa za kibiashara upimaji wa kila baada ya miezi sita ni wa lazima. Ndugu zangu niwaambie, na niwaombe Wabunge wote tupime afya zatu. Tukiwa tunapima afya zetu kila wakati risk ya kupata labda pressure au nini ni ndogo sana. Wataalam wetu wanaotupima tuwaamini.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza mimi na-declare my interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati yako ya Kudumu ya Utawala na TAMISEMI. Kwa hivyo,
katika ziara zetu mbalimbali tumepata ushuhuda wa wanufaika wa kaya maskini na kiwango fulani wamenufaika kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kunufaika kwao bado haijaondoa umuhimu wa kuweza kuongezewa hii ruzuku kwa sababu kama nilivyosema katika swali langu la msingi kila siku maisha yanapanda, shilingi yetu inaporomoka
na bei ya bidhaa inaongezeka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anaonaje basi wakaweza kupewa viwango hivi wanavyopewa kwa mkupuo walau wa miezi sita ili ile tija ya kuweza kuendesha biashara zao, kujenga makazi yao ikapatikana?
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili dogo, mimi
nashukuru katika Jimbo langu pia mradi huu katika baadhi ya shehia unaendelea lakini kuna usumbufu wale walengwa kutoka katika vijiji vingi wanakusanyika katika center moja.
Waziri anaonaje akaongeza vituo vya kulipia ili wale watu ambao wamekusudiwa kupewa ruzuku hii wasipate matatizo hasa ukizingatia wengine ni wanyonge sana, wengine ni watu wazima mno…
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza katika majibu ya swali langu la msingi. Kwanza kabisa, ukiangalia mradi huu, kabla hatujaanza uhawilishaji mwaka 2013 tulianza mpango wa majaribio mwaka 2008 kwa miaka mitano katika Halmashauri tatu za Chamwino, Bagamoyo pamoja na Kibaha. Katika mpango huo wa majaribio, kaya 26,000 zilishiriki katika mpango huu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mwanzoni wakati
programu inaanza, wakati huo wa majaribio, kiwango cha juu kabisa kilikuwa ni Sh.17,500/=. Hata hivyo, tulipoanza mpango tulipandisha mpaka Sh.34,000/= na ilikuwa haiangalii watoto walioko katika kaya, haingalii watoto wanaopata huduma za kiafya na zinginezo. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeongeza, kwa sasa hivi kiwango cha juu kabisa ni Sh.76,000/= vilevile wanapata fursa pia ya kupata ujira, kwa siku 60 kila mwaka wanapata takribani Sh.138,000 kwa Sh.2,300 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema
kwamba katika majaribio ilionekana ukiwapa kiwango kikubwa sana inawezekana wakabweteka na wasiweze kufanya shughuli zingine za ujasiriamali na wakajitegemea tu kupitia ruzuku hii. Kwa hiyo, ilionekana kwa kweli kiwango hiki kinafaa na tumefanya majaribio na wako wengi ambao wameweza kunufaika na kupata maendeleo katika maishayao.

Mheshimiwa Spika, katika swali lingine kwamba
wapewe sasa kwa mkupuo wa miezi sita, hoja yake Mheshimiwa tunaiona, napenda tu kusema kwamba tunaendelea kuifanyia kazi ili kuona kama inawezekana miezi sita au miezi mitatu na nini kinaweza kikafanyika. Kwa sasa nisiseme kama tumekubali, lakini niseme tunaona hoja ni ya msingi tuichukue twende tukaifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuongeza vituo vya kulipia fedha na yenyewe pia niseme tunaichukua ili kuona ni kwa namna gani tunaweza tukawarahisishia na kuwasogezea huduma karibu zaidi walengwa wetu.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushirikiano mzuri wa ndugu zetu hawa wa Cuba katika mambo ya tiba Tanzania, kwa kule Zanzibar ndugu zetu hawa walikuwa na programu maalum ya kuwafunza vijana wetu Udaktari na kwa kweli tayari sasa hivi intake mbili zimeshatoka, moja madaktari wanaendelea na kazi zao na wengine wako katika internship sasa hivi. Kwa kweli inaonekana kwamba wana mafanikio makubwa.
Je, kwa hapa Tanzania Bara programu hii imeanzishwa au imeshafikiriwa kuanzishwa kwa kuwatumia hawa ndugu zetu wa Cuba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza Cuba ni marafiki wa kihistoria wa Tanzania. Comradeship iliyotengenezwa na Fidel Castro na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni ya muda mrefu na imezaa matunda mengi katika nchi zote mbili, zaidi sisi tukiwa wafaidika kuliko wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ushirikiano huo, Watanzania wengi, hususan kwenye fani hii ya afya wamepelekwa Cuba kwa ajili ya masomo na wamesoma masomo ya ubingwa lakini pia katika nyakati mbalimbali hata wanajeshi wetu ambao wanahusika na mambo ya tiba na uokoaji pia wamepelekwa Cuba kwa ajili ya kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1986 ikaonekana kwamba isitoshe tu kuwa na exchange ya Watanzania kwenda kufundishwa kule Cuba mambo ya afya, ikaonekana kwamba tusaini mkataba mwingine ili waje hapa hapa watujengee uwezo. Kwa hivyo, harakati za kujenga uwezo zimekuwa zikifanyika kila mahali ambako madaktari wa Cuba wamekuwepo, pia wamekuwa wakifundisha katika vyuo vyetu hapa nchini, hivyo hata kwa Tanzania Bara tunao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hapa, tuna Madaktari Bingwa kumi na moja wanaotokea Cuba ambao wapo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini msingi wa swali langu katika introduction nilikuwa nazungumzia wajasiriamali kuwa hawapati fursa hii ya kukopeshwa au kuweza kujua fursa kwa sababu hawana utaalamu na uzoefu wa kuandika andiko la miradi.
Sasa nataka kufahamu ni lini hasa Serikali itatoa maelekezo na utaalamu wa kuweza kuwafanya wale wenye nia na hamu ya kupata fursa hii kuweza kuitumia vilivyo na kwa kupata taaluma?
Pili, ni kweli kwamba kuna vikundi vingi tu ambavyo vinasaidia ama kwa kujichanganya katika SACCOS hizi au VICOBA, lakini kuna wajasiriamali mmoja mmoja ambao wangependa kutumia fursa hii ya kupata michanganuo na kuweza kupata fursa ya kukopa, lakini pia hawajawezeshwa, wala ile fursa ambayo ipo kiuchumi hawajaweza kuitumia vizuri, kwa sababu ile taaluma bado haijawafikia. Kwa hiyo, ni lini Serikali italeta taaluma hii ili watu wenye hamu na ari ya kuweza kutaka kujikwamua kiuchumi katika maisha yao, waweze kuipata fursa hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la kwanza kwamba Serikali itatoa lini maelekezo ili wajasiriamali wengi waweze kupata elimu hii na wafahamu fursa zilizopo. Kwa taarifa tu ambayo napenda kumpatia Mheshimiwa Mbunge hapa ni kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ndani yake lipo Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao kazi yao kubwa kabisa ni kutoa elimu lakini vile vile kuwaandaa Watanzania kushiriki katika uchumi wa nchi yao kwa kuwatangazia fursa mbalimbali zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, tayari tuna ma-desk katika kila Halmashauri kwa nchi nzima ambapo kuna Kamati ya Uwezeshaji ambapo wao sasa wanasaidia katika kuwapa wananchi elimu, lakini vilevile wananchi wanapata fursa ya kufahamu fursa zilizopo za kiuchumi. Kwa hiyo, kupitia hiyo, ni rahisi wananchi wengi zaidi kuweza kupata elimu na kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea tu, bado tumeendelea kufanya semina, makongamano na warsha mbalimbali za kuwafanya wananchi wetu wa Tanzania waelewe fursa zilizopo na watumie rasilimali zilizopo kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu na tumefanya katika mikoa mingi na tumepata mafanikio makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza, ameuliza kuhusu namna ambavyo Serikali inaweza ikawawezesha mjasiriamali mmoja mmoja naye akapata fursa ya kushiriki katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nitoe taarifa katika Bunge lako Tukufu na ninyi Waheshimiwa Wabunge mnisikilize ili mwende mkawasaidie wananchi wenu, katika nchi yetu ya Tanzania tunayo mifuko 19 ya uwezeshaji ambayo inatoa ruzuku na mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mifuko hii ina ukwasi wa kiasi cha shilingi trilioni 1.3 ambayo ni fursa ya kipekee kwa sisi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuwaelimisha wananchi wetu kuzitumia fursa hizi badala ya kutegemea Mifuko ya Maendeleo ya Vijana au Mifuko ya Maendeleo ya Akina Mama na mifuko mingine, lakini bado ziko fursa nyingi sana. Kuna watu wanaitwa TFF (Tanzania Forest Fund) ambao wenyewe wanatoa ruzuku kuanzia shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 50 katika vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wengine wote, naomba tuichukue hii kama fursa ya kwenda kuwaelimisha wananchi wetu watumie fursa hii kujinufaisha. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini pia nishukuru kwa majibu ya kitaalam ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sababu za kimaumbile pamoja na mabo mengine kama alivyotaja katika jawabu lake la msingi Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bado kuna mila potofu za ukeketaji wa wasichana kwa kutumia zana za kienyeji, zana moja kwa watu wengi. Lakini pia kuna mila potofu ya kurithi wajane, kuna mila ambazo mjane anarithiwa baada ya mume kufa bila ya kupima au kujulikana amekufa kwa sababu zipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, bado Virusi vya UKIMWI au UKIMWI katika nchi yetu ni tatizo na maambuzi kila siku yanazidi kuliko kupungua, na ziko njia nyingi ambazo zinasababisha maambukizi kama vile ngono na Serikali inajua kuna vishawishi vingi na kuna biashara ya ngono hasa katika maeneo ya mjini.
Je, Serikali ina mpango gani hasa hasa maalum ambao watautumia katika kuzuia biashara hizi za madangulo, biashara hizi zinafanyika na hatuwezi kuwalaumu…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba kumekuwa na mila potofu za ukeketaji na kurithi wajane ambazo kwa njia moja au nyingine nazo zinachangia kwa kiasi katika maambukizi dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Serikali tunaendelea kuchukua jitihada za kuelimisha jamii kuhusiana na madhara haya ya masuala ya ukeketaji na ya kurithi wajane. Moja ya shughuli ambayo na mimi nitaifanya baada ya Bunge hili kukamilika ni kwenda katika Wilaya ya Kilindi katika Mkoa wa Tanga kwenda kushiriki pamoja na jamii wale wakeketaji ambao walikuwa wanafanya shughuli hizi za kuiacha shughuli hiyo na sasa kuanza sasa kuhakikisha kwamba taratibu za kawaida zinaweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea kuchukua juhudi ya kutoa elimu lakini vilevile kuamasisha jamii kuachana na mila potofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na suala la biashara ya ngono. Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwenye jamii kuhusiana na biashara hii ya ngono na kuchukua taratibu za kisheria pale tunapobaini kwamba kuna madangulo katika maeneo husika.