Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Doto Mashaka Biteko (14 total)

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, vilevile niwashukuru sana ndugu Thadei Mushi kwa naMheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza; kwa kuwa Serikali inafahamu baada ya kuwa imempandisha daraja Mwalimu na kumrekebishia mshahara inachukua muda mrefu sana. Utumishi hawaoni kuwa nao imefika wakati wachukue ile model wanayochukua watu wa Nishati na Madini ijulikane kabisa kwamba ukipandishwa daraja kwa kipindi fulani mshahara wako utakuwa umerekebishwa ili watumishi hawa wawe na uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa malimbikizo ya mshahara baada ya kurekebishwa mshahara yanachukua muda mrefu, Serikali inawaambia nini watumishi wa umma hususan Walimu kwamba watalipwa lini, kwa uharaka zaidi malimbikizo ya mshahara haya ambayo yanachukua miaka mingi sana kabla ya kulipa?mna wanavyotupa ushirikiano.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nimshukuru kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia sana masuala mazima ya ustawi na maslahi ya utumishi wa umma hususan Walimu. Natambua ametokana na Chama cha Waalimu Tanzania, nakupongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Biteko alitaka kufahamu endapo Serikali labda kwa nini isifikirie mtumishi anapopandishwa daraja moja kwa moja aweze kuwa amefanyiwa marekebisho yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza kinachofanyika kupitia Mfumo huu wa Taarifa za Kiutumishi na nashukuru kwamba ameweza kumpongeza Afisa Utumishi aliyeko katika Wilaya ya Bukombe kwa kazi nzuri anayoifanya, wanapokuwa Kamati ya Ajira imeshampatia barua ya kupandishwa cheo, kinachofanyika wana-post katika mfumo huu wa Lawson wa taarifa za kiutumishi na mishahara, lakini ni jukumu sasa la Utumishi kuhakikisha kwamba, mtumishi huyu aliyepandishwa cheo kwanza taarifa zake za tathmini kwa uwazi kwenye OPRAS zipo, kuhakikisha kwamba katika muundo wa utumishi kweli anastahili kupanda katika ngazi hiyo na kutokana na sifa na uzoefu ambao umeainishwa katika muundo wa maendeleo ya utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhakikisha kwamba ni kweli ana utendaji mzuri pamoja na uadilifu. Bado naendelea kuhimiza niwaombe sana waajiri pamoja na Maafisa Utumishi ambao wanasimamia suala zima la mfumo huu, kuhakikisha kwamba wanapandisha kwa wakati vilevile wanafanya marekebisho kwa wakati kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali ambayo tumewapatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa madeni ya Walimu napenda tu kusema kwamba kwa kiasi kikubwa madeni haya yamelipwa, zaidi ya Walimu 13,000 tayari malimbikizo yao wameshalipwa ya mishahara, vilevile kwa upande wa Hazina madeni mbalimbali yamekuwa yakilipwa. Bado naendelea kusisitiza tena kuhakikisha kwamba, waajiri wanalipa kwa wakati malipo haya na kuhakikisha kwamba wanayatengea bajeti katika mwaka husika, vile vile wapandishe watumishi kwa kuzingatia muundo na kwa kuzingatia kwamba wana Ikama hiyo na bajeti kwa sababu wasipofanya hivyo ndiyo maana wanasababisha malimbikizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile changamoto nyingine ambayo tumekuwa tikiipata, unakuta mfumo wetu wa Lawson una-calculate automatic arrears, wakati huo huo unakuta Mwajiri mwingine naye analeta manual arrears, kwa hiyo tusipokuwa makini kufanya uhakiki unaweza ukajikuta umemlipa mtumishi mmoja malipo ambayo hayastahiki. Bado naendelea kusisitiza kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa watumishi na itakuwa ikiendelea kulipa kila mara kwa kadri ambavyo uwezo umekuwa ukiruhusu.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Matatizo yaliyoko Kasulu na yale yaliyoko Bukombe yanafanana kwa kiasi kikubwa na kwa sehemu kubwa yanatokana na ucheleweshwaji wa upelekaji wa fedha za miradi ya maji. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Bukombe juu ya maombi ya fedha, shilingi milioni 96 ambazo zimeombwa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji iliyoanzishwa? Ahsante.
MHE. NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dotto Biteko, umeomba shilingi milioni 96 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Vijiji vya Ibambilo, Bukombe na Ikuzi. Katika bajeti ambayo tumeitenga kwenye Halmashauri, naomba sana Mheshimiwa Biteko kwamba tufanye ushirikiano na Halmashauri kuhakikisha kwamba tunatekeleza kwanza ile miradi iliyokuwa inaendelea, tukikamilisha ndiyo tunakwenda kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama fedha haitatosha kama tulivyotoa ahadi katika Bunge hili, basi usisite, tufanye mawasiliano ili kuhakikisha kwamba mwaka wa fedha utaofuata tunaendelea kutenga fedha tena kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika. Nitoe taarifa kama ilivyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kweli tunashukuru kwamba fedha inatolewa na juzi tena Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametupatia shilingi bilioni 15. Kwa hiyo, maeneo yote yale ambayo yalikuwa hayajakamilika, tunaendelea kuyakamilisha.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru. Kiu ya wananchi wa Maswa ya kupandishiwa hadhi hospitali yao, kiu hiyo hiyo iko kwa wananchi wa Bukombe hasa wa Kata ya Uyovu, ambao kituo chao cha afya ni kikubwa sana na kinahudumia watu kutoka Wilaya za Chato, Biharamulo pamoja na Bukombe. Kinahudumia watu wengi zaidi kuliko hata Hospitali ya wilaya, kwa sababu chenyewe kinahudumia watu zaidi ya 82,000 wakati hospitali ya wilaya inahudumia watu 68,000 tu. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri atusaidie wananchi wa Bukombe, atuambie tuna uwezo wa kupandisha Kituo cha Afya cha Uyovu ili kiwe hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Biteko anafahamu, tulikuwa pamoja pale Geita katika uzinduzi wa hospitali na kuweka vifaa katika Hospitali ya Geita pale. Bahati nzuri nilipita katika eneo lake, jiografia yake kweli ina changamoto kubwa na wananchi lazima wapate huduma na kituo hiki cha afya anachokizungumzia amesema kinahudumia watu wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge sasa kwa uhodari wake uleule wa kutetea wananchi wake katika suala zima la maliasili ambapo namsikia mara nyingi zaidi na uhodari wake wa kutetea wananchi katika sekta ya afya na nakumbuka kwamba alileta malalamiko mpaka wataalam wake walihamishwa katika eneo la Jimbo lako na akasema Madaktari wamehama.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe kupitia vile vikao husika vya mchakato wa upandishaji vituo vya afya kuwa hospitali ya Wilaya kuanzia katika Ward C, Baraza la Madiwani, halafu mwisho wa siku naamini ikienda katika Wizara ya Afya ambao wao kazi yao ni kuangalai, kama vigezo vikikidhi, hospitali hiyo inapandishwa. Nadhani hawatosita, namwamini Mheshimiwa Dkt. Kigwangala na dada yangu Ummy Mwalimu watakuwa tayari kuhakikisha kwamba, watu wa Bukombe wanapata hospitali yao kwa mujibu wa vigezo vitakavyokuwa vimefikiwa.
MHE. DOTO M. BITEKO:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema mpango wa kujenga ile barabara ya Butengo Lumasa kwenda Masumbwe haupo kwa sasa na kwa sababu Mkoa wa Geita barabara ya Katoro - Ushirimbo ambayo inaunganisha Wilaya tatu za Mkoa wa Geita iko kwenye ngazi ya TANROADS.
Je, Serikali haioni muda umefika sasa barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Katoro - Lulemba - Ushirombo yenye kilometa 56 ni barabara muhimu ambayo inaunganisha Wilaya tatu za Mkoa wa Geita. Sisi kama Serikali tumeitengea pesa barabara hii kila mwaka; kwa mfano mwaka huu wa fedha 2016/2017 tumeitengea takribani shilingi bilioni 1.25 kwa matengenezo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge hapo baadaye tutakapopata fedha ya kutosha tutaifanyia feasibility study na detail engineering design barabara hii na hatimaye tuijenge kwa kiwango cha lami.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Jambo lililotokea Segerea linafanana sana na lile linalotokea barabara ya Bwanga Ruzewe ambapo wananchi walivunjiwa nyumba kupisha ujenzi wa barabara hiyo miaka minne sasa na waliahidiwa kwamba watalipwa fidia na wameambiwa mara nyingi kuandika barua, wamekuwa wakifuatilia lakini hakuna jambo lolote linalofanyika. Naomba commitment ya Serikali, ni lini wananchi hawa watapewa malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nafurahi sana Mheshimiwa Doto Biteko amechukua nafasi ya kuwa Mbunge wa Bukombe kwa sababu Mbunge aliyemtangulia alileta kwetu pendekezo kwamba tutangulie kukamilisha ujenzi wa lami wa ile barabara baada ya hapo tushughulikie fidia. Mheshimiwa Doto Biteko anafuatilia sana ulipaji wa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia yote mawili tutayafanya lakini naomba sana tena sana tuanze kwanza kukamilisha ile lami. Kwa hiyo, kadiri tutakavyopata fedha kwanza tumalizie lami ambayo tumekusudia kuimaliza hivi karibuni, baada ya hapo, tutaendelea na hilo la fidia kama ambavyo Mbunge aliyemtangulia alikuwa anasisitiza sana na sisi tunapenda kufuata ile continuity.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba nimshukuru sana Naibu Waziri kwa ushirikiano anaonipa kila wakati napoenda kumuona kwa mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa kidogo Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba lile zoezi la kuondoa wananchi kwenye msitu ule kama anavyosema kwamba walishirikisha Halmashauri si kweli nadhani kuna mahali fulani aliyempa taarifa hakusema ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Bukombe eneo lake kubwa ni hifadhi na wananchi wanafuata huduma za maliasili Wilayani Kahama umbali wa kilometa zaidi ya 96. Je, Serikali haioni kuwa sasa muda umefika ifungue Ofisi ya Maliasili Wilayani Bukombe ili wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali kama za kurina asali vibali vyao sasa wasihangaike kufuata Kahama ambako ni mbali sana?
Swali la pili, jambo lililotokea au tukio lililotokea Idosero linatishia vilevile vijiji mbalimbali ambavyo viko jirani, vijiji kama vile Nyakayondwa, Pembe la Ng’ombe, Kichangani, Matabe, Mwabasabi, Ilyamchele ambavyo viko Wilayani Chato vinatishiwa na jambo hili. Lakini vilevile kijiji kama vile Nyamagana, Ilyamchele vilivyoko kata ya Namonge, Wilaya Bukombe na vyenyewe wananchi wake hawajakaa kwa utulivu kwa sababu ya matishio haya haya. Serikali inawaambia nini wananchi hawa ili waweze kuishi kwa amani? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la umbali kutoka Kahama mahali ambapo wananchi hawa wa Bukombe wanakwenda kupata huduma zinazohusiana na masuala ya maliasili na ombi lake la kuletwa kwa kituo mahususi kwenye eneo la Bukombe au kwenye Wilaya ya Bukombe ili kuweza kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maliasili, napenda tu kwanza nimhakikishie kwamba nia njema inaonyesha wazi kwamba si kuleta huduma tu peke yake bali pia hata kuiwezesha Wizara ya Maliasili na Utalii kuweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa sheria inayohusiana na suala la uhifadhi. Kwa hiyo, hilo ni jambo jema na ninalichukua na tunalipokea na tutalifanyia kazi ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza kupata kituo kwenye eneo ambalo liko karibu na litakalowezesha wananchi kuweza kufika kwa karibu kutoka kwenye Wilaya ya Bukombe.
Kuhusu suala la vijiji jirani ambavyo vinaonekana kuwa na changamoto zinazofanana na zile tulizokutana nazo Idosero kwanza kwa kutamka tu kwamba ni vijiji maana yake ni kwamba ni vijiji vinavyotambuliwa kisheria na Serikali. Ukisema vijiji maana yake ni vijiji vya mujibu wa sheria na vimesajiliwa kwa hiyo, sasa kama nilivyotangulia kusema kwa upande wa Idosero. Kwamba kwa kuwa Idosero kama kitongoji ilipata GN chini ya Sheria ya Serikali na vilevile vijiji vilivyotajwa vilevile kwa kuwa ni vijiji uwepo ni kwa mujibu wa sheria basi nimesema sasa umefika wakati wa kwenda kuangalia sheria zote; hii ya maliasili na utalii na ile iliyoanzisha hivyo vijiji twende kuona namna gani tunaweza tuka-harmonize tuweze kupata suruhisho la kudumu, badala ya hizi operations ambazo zinazofanyika mara kwa mara na hazina majibu ya kudumu.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hali iliyopo Lwafi inafanana sana na hali iliyopo na mpango wa Wilaya ya Bukombe ambapo skimu ya umwagiliaji ilijengwa, iliyokuwa inagharimu shilingi milioni 606, lakini fedha ambazo zimeshatoka ni asilimia 58 peke yake. Skimu hiyo ilikuwa inakusudiwa kuhudumia Vijiji vya Kasozi, Nampangwe pamoja na Kijiji cha Msonga na hekta 100 zingeweza kuhudumiwa na skimu hii. Mpaka tunavyozungumza hapa, mradi huo umesimama: Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Nampangwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba skimu hiyo haijakamilika na kwamba fedha iliyolipwa ni asilimia 58 tu. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tumeamua kwanza kukamilisha miradi iliyokuwa inaendelea; na kwa sasa tupo vizuri. Tume ya Umwagiliaji imeshaundwa na ipo sasa hivi inajipanga, kwa hiyo, sasa hivi tutakuwa na mfumo mzuri wa kuhakikisha miradi hii inakamilika.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwa kuwa, matatizo yaliyoko Itilima yako vilevile Bukombe na Kituo cha Polisi cha Uyovu ambacho kinahudumia Wilaya za Bukombe, Biharamulo na Chato kiko kwenye hatari ya kuanguka wakati wowote kwa sababu jengo lile limechakaa. Je, Waziri anatuambia nini wananchi wa Bukombe juu ya Kituo hicho ambacho kina hali mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba, tuna changamoto kubwa sana ya vituo nchi nzima. Tuna vituo vibovu vingi tu na tuna sehemu nyingi ambazo hata vituo hamna. Takribani tunahitaji ujenzi wa vituo vipya kama 4,119 hivi kwa hesabu za haraka haraka, kwa hiyo tuna changamoto kubwa na tunafahamu kwamba kwa kutekeleza ujenzi wa vituo vyote na kukarabati vituo vyote nchi nzima kwa wakati mmoja si jambo jepesi, tutakuwa tukifanya hivyo hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimezungumza katika maswali mbalimbali niliyokuwa nikijibu, kwamba tuna mpango wa kuweza kurekebisha vituo hivyo awamu kwa awamu. Kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa kuwa amesimama hapa na ame-raise hii hoja ya kituo chake, basi tutajitahidi kadri ambapo uwezo utaruhusu ili tuweze kukikarabati kituo hiki.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwa kuwa tatizo la kutokupelekewa fedha kwenye Halmashauri linajitokeza sana hasa Wilaya ya Bukombe na hasa fedha za barabara. Mji wa Bukombe, barabara zake nyingi zimekatika na tunaelekea kwenye msimu wa mvua.
Je, Waziri anawaambia nini wananchi wa Bukombe juu ya barabara hizi ambazo wakati wa msimu wa mvua tuna uhakika hazitapitika kama fedha hazitapelekwa kwa dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli na naomba nikiri wazi kwanza siku zipatazo kama mbili Mheshimiwa Doto Biteko aliniletea request katika Halmashauri yake ikionesha miundombinu ya barabara hivi sasa ilivyoharibika kule katika eneo lake.
Mheshimiwa Spika, niseme wazi kwamba sasa hivi lengo letu kubwa ni Kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yamekuwa korofi kwa sababu makusanyo yanaendelea kukusanywa tutaenda kuyafanyia kazi. Mheshimiwa Doto Biteko, naomba niseme kwamba lengo la Serikali na bahati nzuri hivi sasa unaona jinsi gani Serikali inakusanya misuli yake kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato. Naamini katika bajeti ya mwaka huu tutaipa vipaumbele hasa katika suala zima la miundombinu ya barabara kwa sababu tunajua ndiyo itachochea uchumi wa wananchi wetu kuweza kusafirisha mazao yao kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kwa hiyo naamini kwamba katika jambo hili tutalipa kipaumbele katika Ofisi yetu ya Rais, TAMISEMI.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa wepesi wake katika kutatua changamoto tulizonazo kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, chumba cha upasuaji cha Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kilikuwa kimejengwa kwa ajili ya kutumika kwa muda baadaye ijengwe theatre. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alikuja pale akaona hali halisi ilivyokuwa. Nataka tu kujua commitment ya Serikali, ni lini wataisaidia Hospitali ya Wilaya ya Bukombe na yenyewe ipate chumba cha upasuaji cha kisasa kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi wa Bukombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri wazi kwamba nilifika Jimboni kwa Mheshimiwa Mbunge na ni kweli nimeenda kuitembelea hospitali yetu ya Wilaya angalau pale upasuaji unaendelea. Kwa kuwa eneo lile lina changamoto kubwa sana, ndiyo maana tuna mpango vile vile siyo kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ile peke yake, isipokuwa hata katika Kituo chako cha Afya cha Uyovu kama tulivyoongea.
Mheshimiwa Spika, tutaangalia jinsi gani tutafanya ili tupeleke huduma katika maeneo yale, tupate na back up strategy katika Kituo cha Afya cha Uyovu, tupunguze idadi kubwa ya wagonjwa ambao wataendelea katika Hospitali yetu ya Wilaya. (Makofi)
Kwa hiyo, amini Serikali yako kwa sababu tumekuja kule, tumefanya survey, tumetembelea, tumekutana na wananchi, tumebaini changamoto. Baada ya kubaini changamoto, Serikali tunapanga mkakati wa kuweza kuwasaidia wananchi wa Bukombe.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwa kuwa, Serikali imesema kwamba imeshaweka utaratibu wa namna gani itatekeleza ahadi za viongozi, ikiwemo ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya ujenzi wa kilometa tano za lami kwenye Mji wa Ushirombo; wananchi wa Bukombe wanataka kujua tu sasa kwamba ni lini? Kwa sababu amesema ndani ya miaka mitano, basi waambiwe ni lini itaanza kutekelezwa katika kipindi cha miaka hii mitano, maana huu ni mwaka wa pili tayari tumeingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ndicho wananchi wanataka kusikia. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Biteko kwa kazi kubwa anayoifanya kufuatilia masuala ya miundombinu katika maeneo yake. Namwomba tu, yale ambayo tuliongea ofisini na yale ambayo tuliongea mbele ya Mheshimiwa Waziri wangu ni kweli tutayatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu tuliopewa, kitu cha kwanza ni kuhakikisha tunatekeleza ahadi zote, lakini wakati huo huo zina Wakandarasi site ili kuondoa matatizo ya kulipa interest pamoja na idle time. Hicho ndicho kipaumbele cha kwanza ili tuweze kupata hela nyingi zaidi za kuwekeza kwenye miundombinu badala ya kuwalipa watu ambao wanakaa tu hawafanyi kazi. Kwa hiyo, hicho ni kipaumbele cha kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha pili ni kuhakikisha ahadi zote za Mheshimiwa Rais na zilizoandikwa katika Ilani ya Uchaguzi tunazipangia ratiba. Sasa tunakwenda miaka kwa miaka; mwaka wa kwanza tumemaliza, mwaka huu mmeona kwamba mambo mengi tumeyaingiza ambayo ni mapya siyo yale ambayo tulikuwa tunategemea wakati ule kwa sababu tumeshapunguza kwa kiwango kikubwa yale madeni ambayo tulikuwa nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ushirombo kwamba ahadi zote katika miaka hii mitatu iliyobakia tutatekeleza ahadi hii tuliyoitoa wakati wa uchaguzi.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini nimpe taarifa tu kwamba mahitaji ya walimu kwenye Wilaya ya Bukombe sasa yameshaongezeka mpaka mahitaji tuliyonayo sasa ni walimu 914 na siyo walimu 400 kama ambayo imeripotiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nijue, huu mpango wa kuhamisha walimu walipo sekondari wa masomo ya sanaa ambao ni wa ziada, kuwarudisha shule za msingi umesemwa kuwa muda mrefu sana na inakaribia sasa mwaka unapita; namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri aseme specifically baada ya muda gani? Kwa sababu hali ya mahitaji ya walimu kule siyo nzuri. Ukiwapata wale walimu wanaweza kusaidia kuziba hilo pengo. Nakushukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie kwamba walimu hawa wa shule ya msingi wapo na bahati nzuri tayari tumeshapitisha na kama nilivyoeleza awali, kibali kilishatoka. Sasa hivi tunaendelea tu na hatua ya awali ili wahusika waweze kutuletea majina yao wafanyiwe uhakiki na hatimaye TAMISEMI waweze kuwapangia vituo.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu pamoja na Halmashauri nyingine na Halmashauri ya Bukombe nayo itaweza kupatiwa walimu wa kutosha.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi mzuri wa mitihani ni pamoja na kuwalipa stahiki zao wasimamizi wa mitihani wakiwemo walimu pamoja na askari, lakini mwaka 2015 walimu walisimamia mtihani ya kidato cha nne wakakopwa fedha zao, fedha hizo mpaka sasa hawajalipwa. Ninaomba kujua ni lini walimu hao watalipwa fedha zao walizokopwa wakati wanasimamia mitihani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka 2015 tulikuwa na deni ambalo walimu walisimamia mitihani walikuwa hawajalipwa na deni lile baada ya uhakiki lilikuwa karibuni shilingi bilioni 6.4. Ninapenda kuzipongeza baadhi ya Halmashauri hasa kuna Halmashauri maalum zingine zilifanya initiative ya kulipa zile fedha karibu shilingi bilioni tatu ziliweza kulipwa, hivi sasa tuna deni ambalo ni outstanding karibuni shilingi bilioni 3.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba deni lile tulipeleka Hazina na liko katika hatua ya mwisho kwa wale watu ambao hawajalipwa watalipwa pesa zao.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza naomba nichukue nafasi hii, nilishukuru sana Jeshi la Polisi Wilayani Bukombe kwa kudhibiti uhalifu ambao umekuwa wa mara kwa mara na kwa kutumia kikosi cha Anti-Robbery cha Mkoa kwa kweli wametusaidia kudhibiti uhalifu huu ambao ulikuwa unasumbua sana wananchi.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza ukweli ni kwamba sisi wa Wilaya ya Bukombe tuna eneo tayari kwa ajili ya kuwapatia polisi waweze kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya askari wetu. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri anithibitishie sasa ni lini wataweza kujenga kwa kuwa eneo lipo?
Mheshimiwa Spika, la pili; kwenye Kata ya Namonge pamoja na Bulega wananchi wenyewe wameamua kujenga vituo vidogo vya polisi na wamefika mahali vinahitaji finishing kwa ajili ya kuweka askari. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri awaambie wananchi wa Bukombe, je yuko tayari kuwasaidia wananchi ambao wamejotolea kwa kiasi kikubwa sana, aweze kukamilisha vituo vidogo hivyo vya polisi? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Doto Biteko kwa jinsi anavyofanya vizuri kazi za kibunge. Amesemea sekta zote ambazo ziko jimboni kwake kwa ufanisi mkubwa sana, na nadhani wananchi wa Bukombe watakuwa wameiona tofauti kati ya Ubunge wa Doto pamoja na ule mwingine ambao ulikuwa ni wa mvua hadi mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimhakikishie Mheshimiwa Doto Biteko kwamba kwa kuwa kiwanja kimeshapatikana, basi mimi naelekeza wataalam wangu watengeneze ramani zinazoendana na viwango ambavyo tumevisema kama Wizara na kama Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ili baada ya fedha kuwa zimepatikana tuweze kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao Mheshimwia Mbunge ameuleta.
Mheshimiwa Spika, kuhusu la pili ambalo amelisemea, wadau pamoja na vijana wangu walishafanya kazi hiyo ya kujenga nyumba na zinahitaji ukamilishwaji, nielekeze watuletee makadirio yanayohitajika kwa ajili ya ukamilishwaji ili niweze kuwakabidhi wataalam wangu na watendaji wangu waweze kutafuta kwenye akiba ya bajeti yetu tuliyonayo ili tuweze kukamilisha ili vijana wangu waweze kuhamia. Na nikupongeze Mheshimiwa Doto kwa kuwasemea vijana wangu Jeshi la Polisi kwani polisi wanapofanya kazi vizuri na mimi nakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mzuri na naendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. (Makofi)