Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Doto Mashaka Biteko (34 total)

MHE. SUSANNE P. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, baada ya taratibu kukamilika, je, Serikali itachukua muda gani kuwapatia leseni wachimbaji hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, yamejitokeza madai kuwa zuio la mchanga pale bandarini makinikia halikuwagusa wachimbaji wakubwa tu hata wadogo pia.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanasafisha mchanga wao hapa nchini ili kuendeleza uwekezaji na kutengeneza ajira zaidi kwa wachimbaji hawa wadogo? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itachukua muda gani, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taratibu za kuunda Tume ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya leseni ya uchimbaji madini, iko katika hatua za mwisho za kuundwa. Mara itakapokamilika kazi hiyo itaanza mara moja, kwa hiyo, haitachukua muda mrefu sana baada ya Tume hiyo kuwa imeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la zuio la mchanga, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Watanzania, kwamba Sheria ya Madini haijazuia usafirishaji wa michanga nje ya nchi isipokuwa zipo taratibu na sheria ambazo yule mtu anayetaka kusafirisha mchanga kama madini lazima azifuate kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tumezuia yale makontena kwa sababu yalikuwa na mgogoro ambao Serikali tuliona kuna haja ya kujiridhisha kabla ya kuruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekti, kama kuna wananchi ambao wana madini ya mchanga ambao wanataka kuyasafirisha kwenda nje ya nchi kama wengine ambavyo wanapata vibali na wao wafuate taratibu watapewa vibali. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali iliahidi kutenga maeneo ya Ibindi, Dirifu, Society na Kapanda kwa wachimbaji wadogo wa huko Mpanda, je, ni lini wachimbaji hawa watapatiwa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Kapufi kwa ufuatiliaji wake kwenye jambo hili. Kwa muda mfupi ambao nimeingia ofisini amekuwa mara nyingi akiniambia jambo hili juu ya wachimbaji wake wadogo wadogo. Naomba nitumie fursa hii kuwaambia Watanzania wote wakiwepo na wananchi wa Kibindi kwamba wale wote ambao wamejiunga kwenye vikundi wakaomba maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchimbaji madini Wizara ya Madini iko tayari kuwasaidia mara tu, Tume ya Madini itakapoanza kazi baada ya kuwa imekwishakuundwa.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nimpongeze Mheshimiwa Dotto kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo naomba niombe kuuliza au kupata kauli ya Serikali juu ya lini Serikali itaruhusu mwekezaji wetu Gulf Concrete awalipe fidia wananchi wapatao 80 wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Lugoba ili waweze kuendeleza eneo lile na wao waweze kuondoka na kulinda afya zao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji wa Gulf Concrete and Cement Product ambaye yuko Chalinze kwenye Kijjiji cha Nguza amekuwa akichimba kwa muda mrefu kwenye eneo hilo; na kwa kweli anachimba kwenye eneo hilo ametengeneza ajira zaidi ya 170 kwa watu wa Chalinze ambako Mheshimiwa Mbunge anafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetoa mgogoro mdogo ambao sisi kama Wizara ya Madini tunaushughulikia. Mwekezaji huyu amechimba na akaingia kwenye eneo la mwekezaji mwingine ambaye ana leseni anaitwa Global Mining; ameingia kwenye eneo ambalo lina ukubwa kama hekta 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya kwa sasa, tunataka tuumalize kwanza mgogoro huu ambao yeye Gulf Concrete ameingia kwenye eneo la mtu mwingine. Tukishamaliza twende kwenye hatua ya pili sasa ya kumsaidia Mwekezaji huyo ambaye kwa kweli ana tija kwa watu wa Chalinze na watu wa Mkoa wa Pwani aweze kulipa fidia ili aendeleze mradi wake.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na utaratibu wa Serikali pindi tu mawe yanapotoka kulazimisha wamiliki kupitisha mawe hayo kwenye chumba maalum (strong room) kabla ya kuuzwa mnadani, jambo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa wamiliki wa vitalu kutokuwalipa wafanyakazi hao kwa wakati.
Je, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuondoa usumbufu huu kwa wamiliki wa mgodi huu wa Tanzanite?
Swali la pili pamoja na wamiliki wa migodi wa Tanzanite kuwa na vibali halali kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuuza mawe hayo kwenye mnada kwa bei ya kutupa; je, Serikali haioni kama wamiliki hawa wa migodi wanapata hasara kubwa pamoja na kuwa wanalipa kodi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka nieleze tu kwamba tunawalazimisha watu kupitisha mawe kwenye strong room kabla ya kuuzwa, lengo letu ni moja tu kutaka kujua uhakika wa kiasi gani cha mawe yamezalishwa ili Serikali iweze kupata kodi zake na tozo zake mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili hatuwezi kurudi nyuma madini haya ya Tanzanite yamekuwa yametoroshwa na nchi hii imepata aibu kubwa. Asilimia 20 tu ya madini yote ya Tanzanite yanayochimbwa ndiyo tunaweza kuyaona yameingia kwenye mfumo wa Serikali. Kwa hiyo, tumeweka nguvu kubwa ya udhibiti na usimamizi na hili Mheshimiwa Anna ninamwomba aunge mkono juhudi za Serikali kwenye jambo hili tusirudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili utaratibu wa kuuza mawe haya kwenye mnada ni utaratibu ule ule na umekuwepo kwa muda mrefu, bei iliyopo pale sio bei ya kutupwa ni bei ya ushindani wale wanaotaka kununua wote wanakwenda kwenye eneo la mnada wanatoa bei zao yule anayeshinda anapewa kwa bei nzuri. Hili tunataka kulifanya kwa uzuri zaidi na litakuwa katika Mkoa wa Manyara ili lisimamiwe vizuri zaidi Serikali iweze kupata kodi zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tulifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini na katika kudhibiti na kusimamia CSR tulielekeza Halmashauri husika kushirikishwa katika mipango. Inaonyesha kwamba huko nyuma taarifa ambazo zipo kwenye Halmashauri zetu ni miradi hii ilikuwa inakuwa inflated na mingi ilikomea njiani.
Ni nini maelekezo ya Serikali kwa sababu migodi itaendelea kusimamia yenyewe na kutangaza kazi yenyewe katika sheria ijayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze tu kwa kueleza kwamba Mheshimiwa Kanyasu kwa muda mrefu amekuwa mtu ambaye ana kilio kikubwa juu ya matumizi ya hizi fedha za CSR zinazotolewa na migodi hapa nchini, wananchi wa Geita wanajua hilo na amekuwa akilisema hata hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sheria mpya ya madini, marekebisho mapya kwenye Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2010 imetoa utaratibu maalum kwa watu wote wenye migodi kutengeneza plan ya matumizi ya CSR na kuipeleka kwenye Serikali ya Halmashauri ili iweze kupata approval.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto imejitokeza kwenye migodi mingi ambapo ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Kanyasu inflation ya bei ya vitu imekuwa kubwa mno na miradi mingi imekuwa miradi ambayo haifiki mwisho. Sasa kama Wizara tunaandaa utaratibu wa kukagua CSR ambazo zimekwishakutolewa ili tuone kama kweli fedha hizi zilizotolewa ziliwafikia wananchi na halikuwa jambo la kutegeshea tu. Ahsante. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakipata maafa makubwa sana kwenye migodi na ukaguzi mnasema unafanyika, ningependa kujua huu ukaguzi unafanyika kwa mfano kila mara baada ya miezi mingapi ili tujue kwamba kweli hawa watu wanasimamiwa ili kusudi kuepusha hizi ajali zinazotokea mara kwa mara.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi kwenye migodi ni utaratibu maalum wa Wizara yetu ya Madini kukagua mara kwa mara na hatuna muda maalum, wakati wowote kwenye migodi tunakwenda tunakagua kujiridhisha kama kuna compliance ya kufuata sheria yetu ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye migodi yote ziko Kamati ndogo ndogo za ndani kwenye hiyo migodi ambazo zinafanya kazi ya ukaguzi. Niwaombe wamiliki wote wa leseni kuzitumia Kamati hizi za ukaguzi ili tuweze kupunguza maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wachimbaji wadogo wenyewe waangalie usalama mahali pa kazi, kwa sababu mtu wa kwanza wa kuangalia usalama wake ni yeye mwenyewe mchimbaji kabla ya Serikali kuja. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kushika nafasi hiyo mpya na kwa kweli ameanza kuifanya vizuri Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza aendelee kuifanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza sisi sote tunafahamu wazi kwamba maeneo yaliyo na madini yanatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri kwa machimbo madogo madogo kwa kujipatia kipato na vilevile Serikali kukusanya kodi. Tunafahamu kwamba Serikali ilishafanya utafiti katika maeneo mengi, lakini utafiti huo uko ndani ya vitabu mpaka uende maktaba jambo ambalo sio rahisi wananchi wa kawaida vijijini kutambua wapi kuna madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa nini Serikali isiainishe maeneo yote yenye madini kwa uwazi ili wananchi waweze kuyatambua na kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo?
La pili umesema kwamba wananchi wanaweza kutumia ofisi za kanda za Magharibi zilizopo Mpanda na Dodoma, jambo ambalo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida hasa wa vijijini kuzitumia ofisi hizo kutokana na umbali uliopo. Kwa nini Serikali isiweke branch katika mikoa yote ili kurahisisha wananchi kuzishilikia ofisi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ijulikane tu kwamba matumizi ya ofisi zetu za Wakala wa Jiolojia ni matumizi ambayo yanawahusu Watanzania wote. Ni bahati mbaya tu kwamba wageni wanaotoka nje kuja kutafuta madini hapa nchini wao wanazitumia zaidi ofisi hizi kuliko sisi Watanzania.
Naomba nitoe wito sasa kwa Watanzania wote tuzitumie Ofisi zetu hizi za Wakala wa Jiolojia ili ziweze kutusaidia katika sekta hii ya madini.
Lakini la pili kwa nini Serikali sasa isiweke branch kwa kila Wilaya na kila maeneo. Naomba nimuombe Mheshimiwa Malocha, na kwasababu amekuwa mdau mkubwa sana wa kufuatilia jambo hili kwaajili ya wananchi wake; sisi ni watumishi wa wananchi, sisi hatukai ofisisni Mheshimiwa Malocha ukiwahitaji wataalamu wetu wa Jiolojia kuja kwenye eneo lako wakati wowote watakuja, na hata kama utamuhitaji Waziri mwenyewe atakuja kwasababu sisi ni watumishi wa wananchi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, naishukuru Serikali kwa kutenga eneo la Mbesa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha kimtaji na kuwajengea mtambo wa kuchenjulia madini ya shaba ili waweze kusafirisha yakiwa yamechenjuliwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Tunduru kama alivyojibu kwenye swali la msingi ina mabango mengi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mtaalam wa kufanya valuation ya madini haya ya sapphire ili Halmashauri ipate takwimu sahihi za usafirishaji wa madini? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji wengi wa madini wanahitaji kusaidiwa kimtaji kama alivyosema na hasa kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini (value addition). Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii Serikali inaifanya kwa umakini kwa sababu tuna historia mbaya hapo nyuma.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo walivyopatiwa mitaji kupitia ruzuku fedha nyingi sana hazikutumika kwa malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. Kwa hiyo tunaangalia utaratibu mzuri zaidi kupitia mradi wetu wa SMRP kuona kwamba tunawasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa Tunduru.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba tupeleke Mtaalam wa valuation Tunduru kwa ajili ya kufanya uthamini wa madini ya vito, tunalichukua jambo hili na tunalifanyia kazi. Vile vile tutaandaa watu baada ya Tume ikishakuwa imekamilisha kazi zake za kuchukua watalaam ili tuweze ku-station mtu mmoja kwa ajili ya kufanya valuation pale Tunduru.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka 2016, Serikali ilitoa Kauli kupitia Naibu Waziri wa Madini kipindi hicho Mheshimiwa Dkt. Merdad Kalemani, kuwa Serikali inafanya mazungumzo na Geita Gold Mine ili uweze kupunguza baadhi ya maeneo ambayo yako katika leseni yake. Swali la kwanza, napenda kujua kwamba, hayo mazungumzo yamefikia wapi ili wananchi walau waweze kupata maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wachimbaji wadogo wadogo Geita kati ya malalamiko ambayo wamekuwa nayo ni pamoja na maeneo yanayotengwa dhahabu kuwa mbali sana na kutokana na vifaa vyao duni wanashindwa kuweza kuzifikia. Serikali kupitia corporate social responsibility kwa maana ya huduma za jamii ambayo mgodi umekuwa ukitoa kama vitu vya afya na vinginevyo, haioni kwamba ni muhimu sasa ikatoa mwongozo kwa Geita Gold Mine na maeneo mengine ili katika upande wa corporate social responsibility kuwajibika kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao hata katika ule msimu wa kupasua miamba ili walau waweze kuzifikia dhahabu katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Upendo Peneza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lile alilolizungumza la mazungumzo kati ya Serikali na Mgodi wa GGM kuwapatia maeneo ya kuchimba wachimbaji wadogo, ni kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo hayo kwa maeneo mbalimbali ambayo migodi inaona kwamba inaweza kuyaachia kuwapatia wachimbaji wadogo. Hii siyo kwa GGM peke yake tu, wachimbaji na wenye leseni wengi kuna mahali tunazungumza nao ili waweze kuachia maeneo ya wachimbaji wadogo. Hii itawasaidia wale wanaochimba wenye leseni kuwa na mahusiano mazuri na jamii. Kwa sababu haina maana yoyote kama anachimba halafu kuna uvamizi unaendelea. Kwa hiyo, ili kudhibiti hilo, ni vizuri wakaangalia eneo fulani wawagawie wachimbaji wadogo ili kuwe na amani kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili juu ya matumizi ya CSR kwa ajili ya kuasaidia wachimbaji wadogo. Sheria na Kanuni mpya ya Madini CSR kwa sasa mpango unaandaliwa na mwenye leseni lakini mpango huo unapelekwa kwenye halmashauri, halmashauri yenyewe wajibu wake ni ku- approve kuona kwamba hicho wanachotaka kukifanya wanakihitaji. Kwa hiyo, naomba halmashauri pamoja na wenye migodi wakae chini wazungumze waone kama kipaumbele chao ni kutumia CSR kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wanaweza kufanya hivyo. Hata hivyo, Mgodi wa GGM umefanya kazi kubwa sana, tunajenga kituo cha mfano kule Rwamgasa cha uchenjuaji, Mgodi wa GGM umetoa fedha kwa ajili ya kusaidia kazi hiyo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Niipongeze sana Wizara ya Madini kwa kipindi cha mpito toka Mheshimiwa Rais aliposema leseni ambazo hazifanyiwi kazi na watu wanaomiliki leseni nyingi na zinazoisha waruhusiwe wachimbaji wadogo waweze kuchimba. Mkoa wa Geita una raha kwa kuachiwa maeneo ya Rwamgasa, Nyakafulu, Stamico, Tembo-Mine na Bingwa. Je, Wizara ni lini mtawamilikisha wachimbaji wadogo ambao tayari wako kwenye maeneo ambayo yalikuwa leseni zake zimeisha na nyingine hazitumiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anawapenda wachimbaji wadogo. Kwa kweli ametuelekeza tuwalee wachimbaji wadogo, tuwasimamie na tuwasaidie waweze kuchimba kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ambayo wameweza kupatiwa kwa ajili ya uchimbaji, ili tuweze kuwahalalisha ni lazima tuwapatie leseni. Naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba ndani ya wiki hii tunayo maombi zaidi ya 8,000 ya uchimbaji mdogo tunaanza kutoa leseni. Ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi, ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa miongoni mwa Retention License zilizofutwa ni pamoja na Retention License No. 0001/2009 ambayo ilikuwa inamilikiwa na Kabanga Nikel Company Limited. Kwa kuwa sababu zilizokuwa zimesababisha Kabanga Nikel wasiweze kuanza kuchimba ni kutokana na bei ya nikel kushuka lakini pia miundombinu ya usafirishaji kwa maana ya reli na Ngara kutokuwa na umeme wa uhakika. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Tanzania na hususan wananchi wa Jimbo la Ngara, ambao walikuwa wanategemea mgodi huu kama ungeanza wangeweza kupata ajira na kuinua kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Alex Gashaza, Mbunge wa Ngara. Kabla sijajibu, niseme tu kwamba, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Alex Gashaza kwa ufuatiliaji wake kwenye mradi huu wa Kabanga Nikel, kwa kweli, amekuwa mtu ambaye kila mara anataka kujua nini kinchoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo jana Naibu Waziri wa Madini, Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Waziri walivyojibu, walieleza juu ya ufutwaji wa leseni zote za retention. Nataka niendelee kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba leseni hizi zote za retention zimefutwa kwa mujibu wa sheria na Serikali sasa inaangalia namna bora ya kuzisimamia leseni hizo ambazo zimerudishwa Serikalini.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa eneo hili la Nyakafuru limekuwa chini ya utafiti kwa muda mrefu na tayari wachimbaji wadogo wameshalivamia. Je, Serikali iko tayari sasa kuwamilikisha wachimbaji hao wadogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, eneo pia la Nakanegere Mlimani nalo limekuwa chini ya utafiti kwa muda mrefu. Serikali inasemaje juu ya uwezekano wa kuwapatia wananchi kuchimba kwa leseni za wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwamilikisha wananchi kwenye eneo hilo, nieleze tu kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu wananchi wa Nyakafuru ndiyo wao wako pale wanaendelea na shughuli. Kwa kuwa wanaendelea na shughuli pale na kwa maelekezo tuliyopewa kazi yetu ni kuwasaidia wachimbaji wadogo, wale ambao hawako rasmi tuwarasimishe ili waweze kupata vibali halisi waweze kuchimba kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Nakanegere, eneo hili lote linamilikiwa na kampuni moja na lenyewe utaratibu wake utakuwa kama ule wa Nyakafuru.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kama lilivyo suala la madini katika Jimbo la Mbogwe, Mkoa wetu wa Manyara maeneo mengi yana madini kulingana na utafiti uliofanyika. Hivi sasa uchimbaji huo unafanywa kiholela na sina hakika kama Serikali ina mkakati wowote ama ina taarifa na suala hilo. Je, Serikali sasa iko tayari kutupa takwimu ama hali halisi ya madini yaliyoko katika Mkoa wetu, Wilaya za Mbulu, Simanjiro na Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bura atakumbuka kwamba wakati tunawasilisha bajeti yetu pamoja mambo mengine tulitoa machapisho na majarida mbalimbali ambayo ndani yake yalikuwa yanatoa takwimu kwa ujumla kwenye sekta ya madini kwa kila Mkoa, Wilaya na maeneo mbalimbali. Naamini Mheshimiwa Bura akienda kukapitia kale kakijitabu atapata taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili jambo lingine ambalo ameeleza juu ya wananchi kuchimba kwenye maeneo mbalimbali kwenye Mkoa Manyara. Niseme kwamba Serikali inazo taarifa za wachimbaji wadogo kuvumbua. Mara ugunduzi unapotokea, kazi yetu ya kwanza ni kupeleka usimamizi ili kudhibiti usalama lakini vilevile kudhibiti mapato ya Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Bura ugunduzi wowote unaotokea katika Mkoa wa Manyara tunafahamu na tayari kuna usimamizi ambao unafanywa na Ofisi zetu za Madini kwenye Kanda pamoja na Mikoa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuweka kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Jimbo la Busokelo na si Rungwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa sana wa madini aina ya marble pamoja na carbondioxide gas. Serikali imekiri hapa kwamba madini ya marble yanapatikana katika Kijiji cha Kipangamansi, Kata ya Lufilyo. Je, ni lini Serikali itakuja kufanya tafiti katika milima ya safu za Livingstone kwani inasadikika pia kuwa kuna madini aina ya dhahabu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiongea mara nyingi kwamba atutembelee Halmashauri ya Jimbo la Busokelo ili apate kushuhudia wananchi wangu wanaojishughulisha na hizo shughuli za marble. Ni lini Waziri atakuja kuwatembelea wananchi wa Jimbo langu na kuona shughuli hizo za madini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu namuomba radhi kidogo Mheshimiwa Mbunge kwa kukosea kutaja jina lake. Nieleze tu kwamba Mheshimiwa Mwakibete ni miongoni mwa Wabunge ambao kwa kweli katika kufuatilia masuala ya madini kwenye Jimbo lake amekuwa mstari wa mbele. Kama alivyoeleza hapa, mara nyingi amekuwa akitualika Wizara twende kwenye Jimbo lake na mara ya mwisho tulizungumza tukakubaliana tutakwenda. Nataka nimuhakikishie kwamba tutakwenda mara baada ya kukamilisha Bunge la Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini tutafanya utafiti kwenye Milima ya Livingstone, naomba nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Taasisi yetu ya GST inaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ili kubaini maeneo yenye madini ikiwemo eneo la Busokelo na Lufilyo kama alivyoomba.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika nchi yetu kuna madini ya aina mbalimbali kama vile ruby, sapphire blue, ulanga na tin katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Karagwe. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza madini haya katika soko la dunia kama inavyotangaza tanzanite, dhahabu na almasi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kahigi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini yote ambayo tunayachimba hapa nchini ni wajibu wetu kama Serikali kuyatangaza kwamba yapo ndani ya nchi na kuwavutia wawekezaji waje kuwekeza katika madini hayo. Madini ya tin na madini mengine aliyoyataja tunaendelea na mkakati huo wa kuyatangaza duniani kote na ndiyo maana ataona hata leo akienda hapo nje atakuta tuna maonyesho mbalimbali. Baada ya bajeti hii tutakuwa na vipindi mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti na machapisho mbalimbali kwa ajili ya kutangaza utajiri tulionao ndani ya nchi yetu yakiwemo madini ya tin na haya mengine ya vito aliyoyataja. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Longido ambao pia nina furaha kwamba Madiwani wao karibu wote leo wapo hapa kama wageni wa Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido sawa na Busokelo, kwamba tuna utajiri mkubwa wa madini ya rubi. Kwa kuwa madini ya rubi ukiyakata ili kuyaongezea thamani kulingana na utaratibu uliotolewa na Serikali yanasagika. Kwa kuwa Mawaziri walishatembelea na wakajua changamoto hiyo, wanatuambia ni lini utaratibu huo utakamilika ili wananchi waweze kuyauza mawe haya waendelee kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mimi pamoja na Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Nyongo tulikwenda Longido na hasa kwenye eneo la Mundarara anbako kuna machimbo ya rubi. Wananchi wa kule wanajihusisha na shughuli hiyo na changamoto aliyoizungumza Mheshimiwa Mbunge walitueleza kwenye mazungumzo yetu na wao. Jambo ambalo linapaswa lieleweke hapa ni kwamba Sheria yetu mpya ya Madini imezuia kabisa usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi. Lengo ni kwamba tunataka teknolojia na ajira zibaki ndani ya nchi kuliko kuzisafirisha kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madini ambayo yana upekee wa aina yake katika ukataji. Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini tunaandaa mwongozo wa namna bora zaidi ya kuwasaidia wananchi ili waweze kupata fursa ya kuuza madini haya.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe kuna wananchi wengi sana wameomba leseni kwa ajili ya utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe. Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini wananchi hawa mtawapa leseni hizo ili tuweze kuinua uchumi wa Mkoa wetu wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Neema William Mgaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Neema Mgaya yuko mstari wa mbele kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Njombe na hususan wanawake. Naomba nichukue nafasi hii nimpongeze kwamba juhudi zake si bure, wananchi na wanawake wa Mkoa wa Njombe wanaziona na sisi kama Serikali tutamuunga mkono kwa hatua alizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la lini tutaanza kuwapa leseni, naomba nimpe taarifa njema Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali kupitia Tume yetu ya Madini ambayo imeteuliwa hivi karibuni, tumeanza kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo zote ambazo zilikuwa zimeombwa na tunapitia maombi mengi ambayo yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kwamba mpaka sasa kuna jumla ya zaidi ya leseni 5,000 tunazitoa nchini kote. Wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wapo kwenye maombi hayo na wao watahudumiwa kama wengine. Nashukuru.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kusaidia wachimbaji wadogo wadogo. Jimboni kwangu wapo wachimbaji wadogo wadogo wa Kata ya Katuma ambao wanajishughulisha na uchimbaji wa dhahabu. Je, Serikali inachukua hatua ipi ya kusaidia wachimbaji wadogo waweze kufanya shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Moshi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuwainua ili watoke kwenye uchimbaji mdogo waje kwenye uchimbaji wa kati, na walio kwenye uchimbaji wa kati waende kwenye uchimbaji mkubwa. Kazi ya Serikali, hatua ya kwanza ya kuwasaidia wachimbaji wadogo ni kuwarasimisha. Kila mahali ambapo tunakuta kuna wachimbaji wadogo ambao hawapo rasmi tunawarasimisha kwa kuwaweka kwenye vikundi na baadaye kuwapatia leseni wawe na uhalali wa kuweza kuchimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kuwapatia mafunzo ya namna bora ya uchimbaji kwa kuzingatia sheria lakini vile vile utunzaji wa mazingira. Kazi hizi zote Mheshimiwa Mbunge ataziona baada ya bajeti hii kwa sababu hii ni Wizara mpya, tutakuwa na progamu maalum ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wake wa Kata ya Katama.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, anakiri kabisa kwamba madini haya ni muhimu katika kujenga uchumi wa taifa. Mheshimiwa Waziri, ningependa kukuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; tumeshuhudia bei ya tanzanite ikiendelea kushuka kila siku. Ningependa kujua mkakati wa Serikali; mna mkakati gani wa ziada wa kuendelea kulinda thamani ya tanzanite?

Swali la pili; katika aina ya tano ya madini umezungumzia madini ya nishati ambayo ni makaa ya mawe pamoja na gesi. Mkoa wetu wa Rukwa tuna aina ya madini ambayo ni helium, tangu imegundulika ni muda mrefu sasa. Kama ulivyosema dhana ni kujenga uchumi, ningependa kujua na Wanarukwa wafahamu; ni lini madini haya yataanza kuchimbwa ili yawasaidia Wanarukwa na uchumi wa taifa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni lile analoulizia madini ya gesi ya helium yataanza kuchimbwa lini. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tulishatoa leseni ya kuchimba madini ya helium katika Ziwa Rukwa. Tatizo tulilonalo pale ni kwamba katika eneo hilo ambalo tumetoa mashapo ya kuchimba helium ipo pia leseni ya kampuni nyingine ya Heritage ambayo inachimba madini ya gesi ambayo ipo inasimamiwa na Sheria ya Mafuta na Gesi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali tunachofanya ni ku-harmonize hawa watu wa Heritage pamoja na helium ili waweze kukubaliana tuweze kuanza kuchimba. Hata hivyo, tumeshawapa maelekeo watu wa Helium One waanze kuchimba kwenye eneo ambalo halina mgogoro na watu wa Heritage na mashauriano yanaendelea ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, la pili ni hili alilozungumzia, kuhusu madini ya nishati. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali tunaendelea kuwasimamia watu waweze kuchimba haya madini ili yaweze kuongeza uchumi wa nchi yetu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka 2002, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, kanuni ililitangaza eneo lile kuwa eneo maalum lakini pia iliamua kujengwe ukuta na mwisho tanzanite itangazwe kuwa nyara. Naishukuru sana Serikali kwa kutekeleza hasa ujenzi wa ukuta, Serikali inayoongozwa na jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wanafanya vizuri sana kuiendeleza sekta hii ya madini.

Mheshimiwa Spika, naomba basi niulize swali dogo la nyongeza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali ushauri wangu, ni lini basi ushauri huu atautekeleza? Ahsante sana.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, mjiolojia mbobezi hapa nchini wa madini; nataka tu nimtoe wasiwasi kwamba jambo hili ndani ya Serikali tumeanza kulijadili kwa muda mrefu na katika hatua mbalimbali tulizowahi kufikia ni pamoja na mashauriano ya kuona namna gani ili tuweze kuyafanya madini haya ya tanzanite kuwa nyara ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie kwamba tunalichukua kwa uzito wake, lakini ilikuwa lazima tuanze kwa hatua ya kwanza ya udhibiti, na hatua ya kwanza ya udhibiti ilikuwa kujenga ukuta na kuweka mifumo ya usimamizi wa madini ya tanzanite.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo unakumbuka, katika madini ambayo yalikuwa hayajawahi kusimamiwa vizuri hapa nchini ni madini ya tanzanite yaliyopelekea kiasi cha madini ya tanzanite ambayo tulikuwa tunayaona kwenye mfumo rasmi wa Kiserikali ilikuwa ni asilimia tan tu ya madini yaayochimbwa.

Mheshimiwa Spika, sasa nafurahi kusema kwamba hatua ya mwanzo ya kuweka mifumo imeshakamilika, hatua ya pili ilikuwa kujenga masoko ili tuwe na uhakika wa mahali pa kuyauza, hatua ya tatu ni kuweka mitambo au viwanda kwa ajili ya kukata madini ili uongezaji wa thamani uweze kufanyika ndani ya ukuta.

Sasa hatua ya mwisho ni hiyo sasa ya kutangaza haya madini kuwa nyara ya Serikali, hili na lenyewe Serikali inalitafakari, baada ya muda wakati wa mashauriano Mheshimiwa Dkt. Kafumu na yeye tutazingatia kuchukua ushauri wake.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu alifika eneo la Sakale na akazungumza na wananchi wa Sakale, na pili haikuchukua muda mrefu akawatuma hao wataalam mbalimbali ambao walikwenda wakaangalia hiyo sehemu.

Mheshimiwa Spika, tulishakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba sehemu hiyo hatutaingilia eneo la Bonde la Mto Zigi ili kuepuka chanzo cha maji, na tulikubaliana kwamba tutafute wawekezaji wakubwa ambao wanaweza kuchimba eneo lile.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni, taarifa nzuri ni wawekezaji wameanza kupatikana lakini kuna tatizo la wawekezaji kuruhusiwa kuanza kuchukua sample pale na kuweza kujua kuna madini ya kiasi gani. Je, Wizara iko tayari kurahisisha utaratibu huo ili wawekezaji wale waweze kuangalia kuna madini ya kiasi gani pale Sakale?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni la ujumla tu la kutaka kujua. kwamba mpaka sasa hivi Wizara ina utaalam gani ambao unaweza kujua mgodi fulani kuna madini ya kiasi gani pale, kama ni dhahabu au almasi; je, utaalam huo tunao au bado hatuna?

Mheshimiwa Spika, ni hayo tu, ahsante sana.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa moyo wa dhati kabisa ninaomba nikiri kwamba Mheshimiwa Balozi Adadi kwa watu wa Muheza na kwenye hilo eneo alilolitaja la uchimbaji, yeye amekuwa champion mkubwa wa kuhakikisha kwamba uchimbaji unaanza kwenye kazi hiyo kwa sababu wananchi wa pale kwa kweli ukienda wanategemea sana hilo eneo ili waweze kuchimba na kujipatia mapato na kubadilisha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyokuepo ni kwamba eneo hilo haliwezi kuchimbwa kwa uchimbaji mdogo kwa maana ya matumizi ya mercury ambayo yanaweza kingie kwenye Mto Zigi na kuathiri chanzo cha maji ambacho kwa kweli katika Bwawa la Mbayani ambalo linapeleka maji kule Tanga Mjini, Korogwe pamoja na Muheza, ukiruhusu hiyo watu wote wale maji yale yataweza kuchafuliwa na mazingira. Uchimbaji ambao unaweza kuruhusiwa pale ni ule tu uchimbaji wa kati ambao unakuwa na EIA ambayo NEMC wataitoa.

Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna wataalam ama kuna watu wanaotaka kuchukua sampuli, hakuna mahali popote wanazuia, kwa mujibu wa sheria wanaweza kuchukua sampuli na kupima na kuweza kujua kuna madini kiasi gani. Kwanza ni jambo la faida kwetu kwa sababu wanafanya utafiti kwa niaba ya Serikali na hivyo wanaweza kuchukua wakati wowote. Kama kuna mtu yeyote anawazuia kuchukua sampuli naomba nitoe wito wafuate taratibu zote zilizowekwa wachukue sampuli waweze kwenda kupima na hatimaye wapate taarifa wanazozihitaji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni je, Wizara tuna utaalam wa kujua kuna kiasi gani cha madini mahali fulani? Naomba nijibu tu kwa kifupi kwamba Serikali inayo huo uwezo kupitia Shirika letu la Serikali la GST, tuna uwezo wa kutambua kuna kiasi gani cha mashapo na kuna kiasi gani cha madini kinachoweza kuchimbwa. Kama kuna eneo ambalo analo, kwa kutumia Shirika letu la STAMICO, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awasiliane na STAMICO waweze kujua ni kitu gani kinaweza kufanyika.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza lenye vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, kutokana na shilingi na vifaa vya ujenzi kupanda thamani kila mwaka, deni la wananchi wa Nyamongo wanaodai fidia ni miaka sasa. Je, watakapolipa hizo fedha watawalipa pamoja na riba kwa sababu sasa vifaa vya ujenzi vimepanda?

Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na uthamini kila siku kufanyika kwa haohao wakazi wa Nyamongo lakini hawalipwi ukizingatia hali halisi kwamba na wao wana familia zao, wana watoto wanawasomesha na biashara zao na mahitaji yao ambayo yamesimama kusubiria kuondolewa katika maeneo yale. Je, Serikali ina mpango gani wa kulimaliza hili suala sasa ili wale waliobaki walipwe fedha zao?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agness Marwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nieleze kwamba tumekuwa karibu sana Mheshimiwa Agness Marwa kushughulikia masuala ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo. Kwa kweli, amekuwa mstari wa mbele kuwapigania kila wakati na kutualika mara kwa mara kwenda Nyamongo kwa ajili ya kukutana na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ziko fidia ambazo fedha zilishatolewa muda mrefu lakini bahati mbaya hazijalipwa kwa wananchi. Hii ni kwa sababu tu wako wananchi ambao walikataa zile fedha, kwa hiyo, zikawekwa Halmashauri. Kwa hiyo, nadhani si sahihi sana kuupa tena mzigo mgodi kwamba wao walipe na fidia ya interest kwa sababu fedha hazijachukuliwa. Wale wananchi waliokataa mwanzo walikuwa 138, wale wananchi wengine 70 wakachukua cheque zao wakabaki 64, niwaombe wakachukue cheque zao kwa sababu tayari uthamini ule ulikwishafanyika muda mrefu na fedha zao shilingi 1,900,000,000 ziko pale kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili ambalo ameuliza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba jambo hili la fidia sasa lifike mwisho. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Mgodi wa Barrick kuingia pamoja na Serikali kama mbia, tunachukua kila hatua kufuta yale makosa ambayo yalikuwa yanafanyika ACACIA. ACACIA walikuwa na utaratibu, mnaweza mkafanya uthamini leo kesho wakakataa kulipa tu kwa vigezo vingine. Nataka nimhakikishie kwamba tumeshazungumza na mbia mwenzetu Barrick anayekuja, jambo hili sasa litafika mwisho na Mthamini Mkuu ameshawasilisha vitabu vya uthamini ambavyo nimetaja wananchi zaidi ya 1,838 wamekwisha kufanyiwa uthamini. Kwa hiyo, tutalipa kwa wakati baada ya taratibu hizo kukamilika. Ahsante.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri ameeleza sababu ya kufungwa kwa eneo hili la madini, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, ni utaratibu gani ambao wameuandaa baada ya manyanyaso makubwa kwa wananchi, baada ya unyanyasaji mkubwa kunyang’anywa mali kuumizwa, ambao ulitokea kwenye eneo hili la madini. Wao kama Wizara wamechukua hatua gani kwa wananchi wa eneo lile, ambao walipata manyanyaso makubwa baada ya kugundua madini kwenye eneo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri atuambie huyo mwekezaji mkubwa au mwekezaji mzawa, wao kama Wizara wameshamtafuta au wameshampata au wameshatangaza au ni lini atapatikana ili aanze uchimbaji ili wananchi wanaozunguka eneo lile waweze kunufaika nalo? Ahsante.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yosepher kama ifuatavyo; kwanza hili la manyanyaso kama lipo na lilifanyika na watu walinyang’anywa mali zao ni muhimu tu tukatumia vyombo vyetu tulivyonavyo vya usalama kupitia Jeshi la Polisi malalamiko haya yaweze kuwasilishwa ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili je, tumetafuta muwekezaji naomba tu nimpe taarifa kwamba watanzania wengi sana ambao wameomba kuchimba kwenye maeneo hayo na nieleze tu kwamba Mheshimiwa Adadi tulienda pale SAkale tukafanya mkutano kwa wananchi na kwa watu ambao walionesha nia ya kuwekeza tumewapa taratibu za kufuata kwa sababu kwa kweli kuchimba pale ni kwenye mto ni lazima tuzingatie sheria ili tusije tukaharibu chanzo cha maji, kwa hiyo wako wengi tumewapa taratibu za kufuata ili waweze kuchimba kwa mujibu wa sheria.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia niipongeze Serikali kwa hatua mbili hizi ya kwanza ya kutufungulia soko la madini Tunduru Mjini hali ambayo imeweza kuboresha shughuli na biashara ya madini kwa ujumla kiasi cha kuwaongezea kipato wachimbaji wadogo Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lakini na Serikali kwa ujumla. Pia pongezi kwa kututengea maeneo katika eneo la Mbesa lakini pia kwenye eneo la Ngapa Mtoni. Nina maswali mawili madogo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uboreshaji uliokwishafanyika ambao ni mzuri na umetuletea mafanikio makubwa bado ziko changamoto kwenye maeneo ya afya, usalama na mazingira na changamoto nyingine zinazohusiana na ugawanaji wa maeneo kwenye maeneo makubwa yaliyotengwa na Serikali. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kwa wananchi hawa kuwasikiliza kwa karibu sana na kuratibu changamoto zao na kuzipatia majawabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili wanawake ni mahodari sana wa kuunda vikundi na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za ujasiriamali ni mahodari sana kwenye ujasiriamali na kuunda vikundi na kujishughulisha katika mambo ya ushirika.

Je, wakinamama wa Tunduru watasaidiwaje na Serikali kuweza kuboresha shughuli za uchimbaji mdogo na kwa kupitia vikundi na njia mbalimbali za ushirika ili kuweza kujiboreshea vipato wao wenyewe na kuboresha kipato cha Halmashauri ya Tunduru?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunazipokea pongezi hizo alizozitoa na nieleze tu kwamba katika pongezi hizo na yeye anastahili pongezi kwa sababu na yeye ni sehemu ya mchakato huo na nieleze tu kwamba sisi kama Wizara ya Madini na mimi binafsi niko tayari kurudi tena Ngapa kule kukutana na wananchi wa Tunduru kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu kuwasaidia wakina mama nieleze kwamba wakinamama kupitia Chama chao cha Wachimbaji Wanawake - TAHOMA wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuweza kutafuta maeneo kwa ajili ya kuchimba na kutafuta usaidizi wa aina mbalimbali, Wizara tunaendelea kushirikiana nao kwa karibu lakini katika eneo la Tunduru wapo wanawake wanaofanya vizuri sana pengine kuliko hata wanaume, kuna mama mmoja pale anaitwa Mwajuma ameajiri wanaume zaidi ya 40 wanachimba kwenye leseni yake, kuna mama mwingine pale anaitwa Debora Mwikani naye ameajiri wakina baba wengi wanafanya kazi pale, nieleze tu kwamba uchimbaji kwa kweli kinachohitaji ni nidhamu ya matumizi na wakinamama wameonesha nidhamu ya matumizi kwa kiwango kikubwa na kwa kweli nitumie nafasi hii kuwapongeza wanawake kwa kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji madini na tunaamini kupitia wanawake uchumi wa madini utatutoa nakushukuru. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nashukuru pia majibu ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mji na Geita Vijijini, tulikuwa tunaudai Mgodi wa Geita kiasi cha dola 12,830,000 na anafahamu vizuri kwamba ilifikia mahali mpaka tukaandamana tukawekwa ndani mimi nikiwa mmoja wao. Baada ya kutolewa pale tulikaa kwenye kikao cha pamoja pamoja na Wizara ya Madini na TAMISEMI, Waziri akaamua kwamba wakatulipe kwanza dola 800,000 halafu tufanye mazungumzo ya haraka ili waweze kulipa dola milioni 12,830,000.

Mheshimiwa Mwenyekit, lakini baada ya kutoka hapa documents zote tulizokuwa tunafuatilia sisi kama Halmashauri mbili, ziliporwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Toka walipochukua nyaraka zile Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mpaka leo miaka mitatu hakuna kinachoendelea. Swali la kwanza, ni nini kauli yako kwa Mkuu wa Mkoa kurudisha nyaraka kwenye Halmashauri zetu kwa kuwa tuna wanasheria wazuri ili tuendelee na mchakato wa kudai fedha zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, toka tumezaliwa tunaijua Bacliff haifanyi kazi ni utafiti usiokamilika. Miaka karibia hamsini na kitu ni utafiti usiokamilika; na kwa sasa leseni ile imeisha na kauli ya Rais ni kuzifuta leseni ambazo hazifanyi kazi ili wapewe wachimbaji wadogo na wewe mwenyewe Waziri unajisifu hapa na unaona tunavyofanya vizuri wachimbaji wadogo, tunafukuzana sasa na migodi mikubwa katika kukusanya dhahabu. Ni lini leseni hii itafutwa ili eneo lile warudishiwe wachimbaji wadogo?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Msukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kulikuwa na mgogoro wa ulipaji wa service levy kwa Mgodi wa GGM pamoja na Halmashauri hizo mbili nilizozitaja za Geita Mji pamoja na Halmashauri ya Geita Vijijini. Ukweli pia ni kwamba kulikuwa na tofauti ya namna ya kukokotoa hiyo service levy, maana wao GGM mwanzo walikuwa wanalipa kwa mujibu wa MDA yao, kwa maana ya kulipa dola 200,000 kwa mwaka lakini baadaye marekebisho yalivyofanywa ya kuweka addendum kwenye MDA mwaka 2004, ikaonekana sasa malipo yaanze kulipwa kwa mujibu wa sheria yaani 0.3% ya mapato yote ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti hiyo imechukua muda mrefu na Serikali imekuwa ikishirikiana na Halmashauri ya Geita pamoja na Mheshimiwa Mbunge anafahamu sisi Wizara tumesukuma sana jambo hili. Hata hivyo, hapo katikati Waheshimiwa Madiwani wa Geita waliamua kupeleka jambo hili mahakamani na Mheshimiwa Mbunge anafahamu jambo hili lilishapelekwa mahakamani. Kuhusu nyaraka zile kupotezwa na nini, nadhani tuwaachie mahakama nao wao kama wanazo nadhani watazipeleka mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni lile linalohusiana na Mgodi wa Bacliff. Ni kweli kwamba Mgodi wa Bacliff umechukua muda mrefu sana na kumekuwa na matatizo mengi sana, kwanza ya kileseni lakini pili ya kiubia. Yote hayo tunayafanyia kazi na hivi navyozungumza hapa nawasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia namna gani ule ubia utaweza kusimamiwa, ama pengine kama kuna haja ya kuuvunja uweze kuvunjwa. Ile leseni anayoizungumzia, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini hatujatoa leseni hiyo ambayo inahitaji kuhuishwa kwa sasa, kwa sababu bado kuna mambo ambayo tunahitaji kuyakamilisha kabla ya kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, moja ya kero kubwa ya wachimbaji wadogo ilikuwa ni ile sheria ambayo tulipitisha hapa Bungeni, ya kodi ya zuio ya asilimia tano kwa bei ya kuuzia madini kwa wachimbaji wadogo, lakini Bunge lako tukufu mwaka huu mwezi wa pili tulibadilisha hiyo sheria na kuondoa hilo zuio.

Sasa nataka kujua utekelezaji baada ya kuondoa hiyo sheria umefikia wapi kwa sababu ile sheria ilikuwa inapelekea madini mengi kutoroshwa nje ya nchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Silinde la nyongeza. Ni kweli kama alivyosema tumekuwa tukipata malalamiko ya baadhi ya watu, hasa maeneo ya Arusha na mikoa mingine kwamba, pamoja na kwamba withholding tax na VAT zimefutwa kwa mujibu wa sheria, wako watu wanaendelea kuzitoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomab kutoa wito na kutoa maelekezo rasmi kwa watu wote wanaohusika kwenye utozaji wa kodi na tozo mbalimbali kwenye sekta ya madini. Kodi ambazo zimefutwa na Bunge hili hakuna mtu mwingine yeyote wa aina yoyote anaruhusiwa kutoza hizo kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninasema hili na iwe marufuku kwa mtu yeyote na tutakapopata taarifa tena, kwa mtu ambaye anaendelea kutoza hizo kodi, hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge na awaambie Watanzania kwa mujibu wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 kampuni inatakiwa kulipa fidia ifanye relocation na ifanye resettlement kama inahamisha watu. Lakini hawajawahi kuhamisha mtu wala kumfanyia relocation na licha ya hivyo mpaka sasa kwa mfano wananchi wa Tarime waliofanyiwa uthamini maeneo ya Nyamongo kuanzia mwaka 2009 mpaka leo tunavyozungumza hawajawahi kulipwa. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Madini alikuwa pale ametoa kauli lakini mgodi unakiuka hausikilizi, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri ni lini hasa watu hawa wanaoendelea kuteseka kwa zaidi ya miaka 10 au 15 watalipwa sasa ahsante? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Heche Mbunge wa Tarime kwa kifupi tu na kwa sababu leo ni bajeti yetu tutaeleza kwa kina hayo yote.

Mheshimiwa Spika, nieleze kwamba ni kweli kulikuwa na changamoto ya muda mrefu toka mwaka 2012 kwenye fidia za maeneo ya mgodi wa North Mara huko Nyamongo. Lakini kama Serikali tumechukua hatua kubwa sana kwa sababu kuna maeneo mengine ambapo kwa kweli tungekimbilia tu wananchi walipwe fidia walikuwa wamepunjwa sana, kwa mfano awamu ya 47 wananchi 66 ambao walikuwa wanadai fedha walithaminiwa kiasi cha shilingi milioni 224 peke yake, tumekwenda kule tumeangalia tumekuta wale wananchi walikuwa wamepunjwa sana tumeagiza uthamini huo ufanyike upya ili wananchi walipwe stahiki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Heche anafahamu Awamu ya 24 na Awamu ya 34 wananchi hawa walikwenda mahakamani na kwa kuwa wamekwenda mahakamani tuliwashauri kwamba wamalize shauri lao mahakamani wakishakumaliza sisi kama Serikali huku tutasimamia utaratibu wao wa kulipwa. Lakini Awamu ya 30, 32 (a) na (b) ambazo mgodi hauhitaji hayo maeneo Chief Valuer ameelekeza mgodi uwalipe kifuta jasho wananchi hao.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Heche kwamba jambo hili tumelifanya pamoja na kwenye bajeti tutalieleza kwa kina awe na subira tusiharakishe shughuli za Bunge ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Kakonko na kuzungumza na wadau ambao wanataka kuchimba madini hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, Naibu Waziri alipokuja wadau walimwonesha nia ya kuchimba madini haya pamoja na madini ya chokaa, yanayopatikana kwa wingi katika Wilaya ya Kakonko na katika Mkoa wa Kigoma ambayo yanatumika sana kwa shughuli za ujenzi, shughuli za kulainisha ngozi na kazi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa kuwa sisi tumejiandaa katika Wilaya ya Kakonko, kujenga kiwanda cha kuchakata chokaa kuwasaidia vijana. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, sehemu ya tatu, Mheshimiwa Waziri ameshauri vijana wote wanaotaka kushughulika na uchimbaji wafike kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Kigoma. Kutoka Nyamwilonge mpaka Kigoma ni kilomita zaidi ya 300. Swali la kwanza, je, haoni kwamba ingekuwa busara sasa, badala ya vijana wote hawa kwenda Kigoma kilomita 300, amwagize Afisa Mkazi huyu wa Madini yeye ndiye awatembelee kuwapa ushauri kule waliko? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa madini ya chokaa yanapatikana kwa wingi katika Wilaya ya Kakono na katika Mkoa wa Kigoma, lakini katika Wilaya ya Kakonko, madini yote haya yapo katika Pori la Akiba la Moyowosi, ambalo Serikali inawazuia kuchimba au kufanya shughuli za uchimbaji katika pori la akiba. Je, Mheshimiwa Waziri, yuko tayari sasa kukaa na Wizara ya Maliasili ili kuangalia uwezekano wa Wizara hizi mbili kutoa kibali kwa wachimbaji hawa kufanya uchimbaji salama ili waweze kuchimba chokaa hii? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze tu kumpongeza sana Mheshimiwa Chiza kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele sana kushughulika na suala la madini kwenye Wilaya ya Kakonko na kama utakumbuka tarehe 5 mwezi wa Aprili, aliuliza swali hapa hapa kwa ajili ya madini ya chokaa na leo ameuliza kwa ajili ya madini ya dhahabu, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tu kwamba ni kweli, tumeweka Ofisi za Madini kila Mkoa ambazo kazi yake ni kutoa huduma kwa watu wanaotaka kujishughulisha na uchimbaji wa madini na sasa kutoka Kakonko kwenda Kigoma pana umbali mrefu sana. Nakubaliana naye, kwamba, Afisa Madini awatembelee aweze kutoa elimu hiyo. Pia nimwombe sana Mheshimiwa Mbunge, yeye pamoja na wale vijana wapange tarehe, tarehe fulani watakuwa tayari, Afisa Madini atakuja pale kuwapa elimu juu ya utaratibu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa madini haya yako kwenye hifadhi na kwamba wanataka wachimbe ndani ya hifadhi ya Kigosi. Naomba tu nimjulishe kwamba Mheshimiwa Mbunge, utaratibu uliopo ni kwamba, Wizara ya Madini wajibu wake ni kutoa leseni ya Madini (Mineral Right) na mwenye wajibu wa kutoa kibali kwa ajili ya mtu kupata access ya kuingia kwenye mapori hayo ni yule mwenye surface right ambaye kwa mujibu wa sheria ni Wizara ya Maliasili na Utalii. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge, yeye pamoja na wenzetu Wizara ya Maliasili na Utalii, wazungumze kuona namna gani bora wanaweza kupata kibali cha kuwea kufanya kazi kwenye maeneo hayo kama Sheria ya Maliasili itaruhusu. Nakushukuru sana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilielekeza wananchi waunde vikundi vya uchimbaji ili wasimamie rush wenyewe, je, ni kwa nini sasa Kamishna wa Madini Kahama anaweka wasimamizi ambao si wanavikundi na utaratibu gani unatumika kuwapata wasimamizi hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini eneo la Wisolele limetolewa leseni kwa watu binafsi akiwemo mtu mmoja ambaye anajinasibu kuwa karibu na viongozi wa tume (jina nalihifadhi) aliyepata leseni zaidi ya 17 peke yake badala ya vikundi vya wachimbaji wadogo kama Waziri alivyojibu kwenye jibu la msingi?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la swali la msingi kuwa, Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa Waraka wa Ndani Na.3 ulioanza kutumika tarehe 15 Oktoba, 2019, wenye dhumuni la kutoa mwongozo kwa Maafisa Madini Wakazi na watumishi wengine katika kusimamia, kudhibiti shughuli za madini na mapato ya Serikali katika maeneo yenye rush. Kwa mujibu wa Waraka huo Afisa Madini Mkazi ni Mwenyeketi wa Kamati ya Uongozi unaofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush. Kamati hiyo inajumuisha DSO (Katibu), TAKUKURU (Mjumbe), OCD (Mjumbe), REMA (Mjumbe) na Halmashauri (Mjumbe).

Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kuwapata wasimamizi wa rush ni kupitia Kamati ya Uongozi unaofuatilia na kuimarisha usimamizi katika eneo la rush kama ilivyotajwa hapo juu. Kamati hiyo huteua Wasimamizi wa rush, ambapo Mwenyekiti wa rush anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:-

Awe mchimbaji mzoefu hasa katika usimamizi wa maeneo ya aina hiyo; awe hana historia ya wizi wa fedha za Serikali na awe mwaminifu. Wajumbe wengine kwenye usimamizi wa rush ni pamoja na Katibu, Mweka Hazina, Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Mjumbe wa REMA, TAWOMA, mwakilishi wa eneo/shamba.

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika eneo la Wisolele zimetolewa leseni za uchimbaji mdogo 55 kwa watu binafsi na vikundi mbalimbali. Aidha, kuna jumla ya maombi ya leseni za uchimbaji mdogo 95. Kati ya maombi hayo, maombi sita ni ya vikundi vya Amani Gold Mine, Chapakazi, Domain Gold Group na Pamoja Mining Group.

Mheshimiwa Spika, utolewaji wa leseni hizo 55 ukijumuisha leseni 17 zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge zilitolewa kabla ya rush na vikundi kuundwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini, 2010 pamoja na Marekebisho yake ya 2017 mchimbaji mdogo hazuiwi kumiliki leseni zaidi ya moja.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante ukizingatia sisi ndio mama zako au bibi zako lazima uturuhusu ahsante sana. Kutokana na shughuli za uchimbaji madini Mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, tatizo na ongezeko kubwa la kansa kwa Mkoa mzima wa Mwanza kumekuwa na tatizo kubwa la kansa na tunaamini kabisa hii zebaki ndio inayosababisha ongezeko hili la kansa. Je. Serikali ina mpango gani sasa wa kudhibiti kabisa uingiaji wa kemikali hizi, ili kunusuru wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Kabula kwa swali lake ambapo ameulizia kuhusiana na udhibiti.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, hatua ya kwanza tuliyochukua mahali ambako dhahabu inachenjuliwa, inaitwa mialo, mwanzo mialo ilikuwa holela, kila mahali mtu anajenga; sasa tumeamua kuidhibiti ile mialo yote iwekwe kwenye eneo maalum na jumla ya mialo 5,025 imesajiliwa kote nchini.

Mheshimiwa Spika, pili, Chama cha Wachimbaji Wadogo kinaitwa FEMATA pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali wanatengeneza umbrella moja ya namna ya kuagiza zebaki hapa nchini na Mkemia Mkuu wa Serikali ameshatoa hiyo go-ahead lakini changamoto tuliyonayo ni ndogo ndogo tu ya uratibu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya miezi hii miwili uagizaji wa zebaki tutakuwa tumeudhibiti na tutakuwa na source inayoeleka.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kukiambia Kiti chako kwamba Serikali mpaka muda huu walikuwa hawajanipa majibu mimi kama Mbunge kabla ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu niliyopewa na Mheshimiwa Waziri, haki ya mfanyakazi anaposimamishwa hasa kwenye mafao ya PSSSF anatakiwa apewe hata kama kuna mchakato mwingine unaendelea. Ni lini Serikali itasimamia wananchi hao na wafanyakazi hao wa Mgodi wa Kiwira waweze kupata mafao yao wakati michakato mingine inaendelea?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; namwuliza Mheshimiwa Waziri, Mgodi wa Kiwira ulikuwa unaisaidia kiuchumi Wilaya kubwa tatu; Wilaya ya Rungwe yenyewe, Wilaya ya Kyela na Wilaya ya Ileje; sasa hawaoni kuchelewa kuendelea ule mradi unarudisha nyuma maslahi na uchumi wa Wana-Rungwe, Wana-Ileje pamoja na Wana-Kyela? Kwa nini wasifanye haraka na mradi huu ukaanza haraka iwekezanavyo? Ahsante.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mafao ya wafanyakazi; ni kweli hakuna mtu hata mmoja anafurahia kuona wafanyakazi wale wanapata taabu. Ukweli ni kwamba madai yale yalikuwa ya mwaka 2007, yalifanyiwa uhakiki na Serikali; uhakiki ndiyo umekamilika. Madai yale yalikuwa kuanzia shilingi bilioni 46; yaliyohakikiwa na kuthibitishwa ilikuwa ni shilingi bilioni 1.24. Serikali imekamilisha uhakiki wa madai hayo na sasa yako kwenye utaratibu wa kulipwa pamoja na madai mengine.

Mheshimiwa Spika, tumepiga hatua kubwa sana kuuendeleza mradi huu. Nikiri kwamba Waheshimiwa Wabunge wa maeneo yanayozunguka mgodi huo wamekuwa na msukumo mkubwa sana akiwemo Mheshimiwa Mbunge. Kwa sasa mgodi huo tumeshafanya mabadiliko makubwa mno. Sasa hivi Shirika limeshaujenga na tunazalisha pale Kabulo, lakini kwenye underground mining tayari tuna update, ile underground rail na tayari kiberenge cha kusafirisha tumeshakitengeneza, kinafanya kazi. Tutaanza kuzalisha mwezi huu tani 5,000 kila mwezi na kule Kabulo tutakuwa tunazalisha tani 50,000 kwa mwezi. Nadhani wateja wengi wapo, wananunua makaa ya mawe kutoka kwenye mgodi huo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amefanya kazi kubwa sana, lakini ameendelea kutoa hadithi zile zile. Sasa naomba tujue, ni lini mgodi huu utaanza kuzalisha ile mass production? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Bahati njema yeye mwenyewe katika kipindi kilichopita alitupa hati ya mashaka. Sasa hivi nataka nimwambie hati ile aiondoe kwa sababu tayari uzalishaji umeshaanza.

Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa, itakapofika mwezi Machi mwaka huu 2022 uzalishaji wa mass production wa tani 50,000 kwa mwezi utaanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, vile vile underground mining kama nilivyokukwa nikijibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, tayari tumeshaijenga na kiberenge kinapita na uzalishaji unaanza. Ndani ya mwezi huu tunaanza kuzalisha kwenye mradi wa Kiwira tani 5,000.

Mheshimiwa Spika, Block E na yenyewe tumeanza kuanzisha open pit kwa ajili ya kuchimba. Mgodi huu ulisimama kwa muda mrefu toka mwaka 2008. Ni Awamu ya Sita ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa ili mgodi huu uanze na wateja wako wengi, tayari wanapita. Hata barabara ile Mheshimiwa Mbunge alikuwa analalamikia tayari tumeshaijenga. Sasa hivi tunakamilisha lile Daraja la Mwalisi watu waanze kupita pale; na wananchi wa maeneo yale wananufaika na uwepo wa mradi huu. Ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini ni kweli kwamba GST ina uwezo mdogo sana wa kiteknolojia kulingana na maendeleo makubwa teknolojia duniani. Sasa Serikali ina mkakati gani wa dharura kuiokoa GST kiteknolojia kwa sababu uwezo wake ni mdogo sana kiasi kwamba hata minerals zile certified mineral chemicals ambazo zinasaidia kuthibitisha ubora wa sampuli haina uwezo huo.

Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura kuokoa GST?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia swali la pili, mpaka sasa Serikali imetoa leseni ngapi ambazo ziko kazini sasa hivi za madini ya kimkakati ambayo tunategemea GST itusaidie kuyabaini?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, la uwezo mdogo wa GST wa kufanya utafiti, naomba nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba GST kama taasisi ya utafiti itashirikiana na sekta binafsi. Kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, tunazo kampuni mbalimbli ambazo ziko ndani na nje ya nchi ambazo zinafanya kazi ya utafiti kusaidia Taifa letu. Hivi sasa tumeshazungumza na kampuni mbalimbali kubwa duniani kwa akjili ya kufanya utafiti huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwamba tumetoa leseni ngapi; tumeshatoa leseni kadhaa, naweza nisijue kwa idadi, lakini madini yote ya mkakati anayoyafahami iwe nickel, iwe graphite iwe rare earth, iwe helium na kadhalika; yote haya kuna leseni na makampuni mbalimbali yanaendelea na utafiti hapa nchini. Kwa hiyo naomba nimuhakikishie, demand ya madini mkakati ambayo anahitaji sasa hivi ni jambo ambalo halikuwa la muda mrefu, na wawekezaji wengi walikuwa busy na madini mengine. Sasa hivi muelekeo mkubwa ni kufanya haya madini mkakati na kampuni nyingi zipo zinafanya hizi kazi. Baada ya muda ataona migodi mingi inajengwa kama ambavyo kabanga inajengwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Katika Jimbo la Sikonge wananchi wangu wanaendelea kuamini kwamba katika Mlima wa Kipanga, Milima ya Kisanga na Mapori ya Ipembampazi kuna madini; na hili suala limeulizwa tangu enzi za Mheshimiwa Said Nkumba akiwa madarakani.

Je, Serikali itakuja lini sasa kuja kufanya utafiti ili kuitikia wito wa wananchi kwamba kule kuna madini?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba yapo maeneo mbalimbali Mkoa wa Tabora ambayo yanaaminika kuwa na madini na bahati mbaya hayajafanyiwa utafiti wa kina. Taasisi yetu ya utafiti GST iko katika Mikoa ya Kusini. Nataka nimhakikishie, baada ya kumaliza mzunguko wa Kanda ya Kusini tutawapeleka na Mkoa wa Tabora, ikiwemo eneo la Sikonge ili waweze kufanya utafiti wa awali.